read

(9) Wanavyosema Wapinga Maulidi Na Majibu Yetu

Wiki iliyopita tuliyataja maneno ambayo Ahlu-Tawheed wameyatoa katika Barzanji na Burdah ambayo, kwa maoni yao, ni shirki. Tukaahidi kuyajadili maoni hayo leo, baada ya kuieleza shirki ni nini.

Kwa taarifa tuliyoitoa sisi (na tumeomba tuelezwe kama tumeacha kitu katika taarifa hiyo), kati ya madondoo sita yaliyonukuliwa na ndugu zetu hao, matano yametushinda kuelewa vipi yaweza yakawa ni shirki. Kwa hivyo hatutashughulika nayo kwa leo mpaka hapo tutakapofafanuliwa inshallah. Tutakaloshughulika nalo leo ni moja tu lililobaki ambalo, kwa hujja walizozitoa kulipingia, tumeweza kulifahamu lililowafikirisha wao kuwa ni shirki. Nalo ni lile la Buswiri kusema katika Burdah: "Haukupata kunipiga vita Ulimwengu nikataka nusra kwa Mtume ila huipata tu."

Kulikosoa hilo, Ahlu-Tawheed wameitaja Sura 3:126 ambayo wameifasiri hivi: "Na msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu na Mwenye hikima". Kwa kuitaja aya hii, kwa hivyo, tumeelewa kwamba ndugu zetu hao wameyaelewa maneno ya Buswiri hivi: "Kwa kuwa msaada (nasr) hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, kuuomba kwa mtu mwengine yoyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu, hata awe ni Mtume (s.a.w.w.), ni sawa na kumfanya mtu huyo ni Mwenyezi Mungu! Na kufanya hivyo ni shirki; kwa hivyo katika Burdah muna shirki!"

MAJIBU YETU : Kwanza; katika tafsiri yao ya hiyo Sura 3:126 wameongeza maneno katika pinde, tuliyoyachapa kwa italiki, ambayo hayamo katika aya hiyo, wala hayaipunguzii maana lau yasingeongezwa.

Pili; kama maana ya "msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu" ni kwamba haturuhusiwi kutafuta msaada kwa asiyekuwa Yeye, au asiyekuwa Yeye hana msaada wa kuutoa, basi ilikuwaje watu wa Madina wakaitwa answaar (wasaidizi)? Walimsaidia nani? Huyo aliyesaidiwa, aliukosa msaada wa Mwenyezi Mungu hata wakaingia kati wao? Na sisi Waislamu, pamoja na Mtume wetu (s.a.w.w.), tunamshirikisha Mwenyezi Mungu kwa kuwaita answaar watu wa Madina?

Tunaposoma Sura 3:81 tunaona jinsi Mwenyezi Mungu alivyochukua ahadi kwa Mitume Yake kwamba itamsaidia / itamnusuru (latansurunnahuu) Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Jee, kama "msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu," ilikuwaje hapo, Yeye Mwenyewe, akautaka kwa asiyekuwa Yeye? Jee, kwa kitendo hicho, Mwenyezi Mungu -- Mwenyezi Mungu apishe mbali! -- alikusudia kuifanya Mitume Yake ni miungu?

Katika Sura 7:157, kati ya sifa za waumini ambao "ndio wenye kufaulu", ni wale ambao wamemsaidia / wamemnusuru (wanaswaruuhu) Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Jee, kama "msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu", kwa nini akawaagiza waumini wamsaidie Mtume Wake? Kwa sifa hiyo hapo, ndio Mwenyezi Mungu amewafanya waumini kuwa ni miungu? Mwenyezi Mungu -- Mwenyezi Mungu apishe mbali -- hapo amefanya shirki?

Hali kadhaalika; tunaposoma Sura 28:15 tunaona jinsi jamaa yake Nabii Musa (a.s) "alivyomuomba msaada" (fastaghaathahuu) juu ya adui yake. Jee, Nabii Musa (a.s) alimrukia jamaa yake huyo, na kumwambia asilete shirki kwa kumuomba yeye msaada badali ya Mwenyezi Mungu? La! Alimsaidia; na siku ya pili (Sura 28:18) yule aliyeomba msaada jana (istanswarahuu) akamuomba tena! Jee, kama "msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu", kwa kutoa msaada wake huo, Nabii Musa (a.s) alikuwa Mwenyezi Mungu, au hakujua kuwa "msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu"?

Kwa kutaja mifano hiyo hapo juu, sisi tusomao maulidi hatukusudii kukanusha yaliyomo katika aya iliyotajwa na wapinga maulidi, kuwa "msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu"; hasha! Tunalokusudia ni kufahamisha kwamba: maneno yanapofanana, si lazima na maana yafanane (yawe mamoja). Kwa hivyo, msaada ambao Buswiri aliuomba kwa Bwana Mtume (s.a.w.w.), na sisi huukariri tunapoisoma hiyo Burdah, sio msaada ambao huombwa kwa Mwenyezi Mungu. Ni majina tu kufanana -- kama ulivyokuwa ule ambao Mwenyezi Mungu alimtakia Mtume Wake kwa Mitume mengine, na aliotutaka sisi waumini tumpatie Mtume Muhammad (s.a.w.w.), na ambao watu wa Madina walimpatia Bwana Mtume (s.a.w.w.) hata wakaitwa answaar (wasaidizi wake), na ule ambao Nabii Musa (a.s) alimpatia jamaa yake.

Msaada wa Mwenyezi Mungu unatokana na Yeye Mwenyewe; hakupawa na yoyote uweza huo wa kusaidia. Lakini wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, akiwamo Mtume Muhammad (s.a.w.w.), si wake mwenyewe; ni wa kupawa (kuwezeshwa na Mwenyezi Mungu). Na hapo ndipo palipo na tafauti baina ya shirki ni nini, na si nini.

Ukiamini kwamba Mtume (s.a.w.w.) -- yeye mwenyewe, bila ya kupawa uweza huo na Mwenyezi Mungu -- aweza kusaidia; hiyo ni shirki. Na hilo silo alilokuwa akiliamini Buswiri, wala silo tunaloliamini sisi tusomao maulidi. Lakini ukiamini kuwa msaada uwezao kupawa na Mtume (s.a.w.w.) ni ule aliowezeshwa yeye na Mwenyezi Mungu; hiyo si shirki. Na hilo ndilo alilokusudia Buswiri katika Burdah, na ndilo tunaloliamini sisi tunaosoma maulidi. Kwa hivyo kubwa ambalo wapinga maulidi waweza kutwambia sisi ni kuwa Mtume (s.a.w.w.) hakuwa / hana uweza huo; kwa hivyo ni kazi bure kumuomba hivyo -- jambo ambalo hatulikubali kwa sababu ya hujja tulizonazo. Lakini hawawezi kutwambia ni shirki, kwa mifano mingi tuwezayo kuwatolea katika Qur'ani Tukufu.

Inshallah wiki ijayo tutaeleza kwa urefu ni wapi ambapo wapinga maulidi hupotea na kukosea kuielewa shirki. Nataraji baada ya hapo wataweza kuyaelewa yaliyomo katika Barzanji na Burdah.

ABDILAHI NASSIR
P.O. BOX 84603
MOMBASA

15 Jamaadal Uulaa, 1423
26 Julai, 2002