Matokeo Ya Kutoziandika Hadith

Kulitokea matokeo mabaya kwa sababu ya kutokuwa na Hadith zilizoandikwa wakati wa kuzieneza. Hapa sisi tutajaribu kuzizungumzia baadhi yao.

1. Upoteaji Mkubwa Mno Wa Hadith

Haya yalikuwa ni matokeo ya kutoandikwa kwa Hadith. Kwa Sahaba, uhifadhi moyoni ulileta matokeo ya kuhifadhika kwa idadi kubwa ya Hadith, na pia tukubali kuwa kulisababisha katika kupotea Hadith chungu nzima kwani kuhifadhi moyoni ni njia isiyoaminika katika kuhifadhi. Kukiri na kukubali kwa Muhaddithun (waliohadithia) katika jambo hili ni ushahidi ulio bora kabisa kwa ajili ya hayo.

Ibn Qulabah anasema, "vitabu na maandiko ni bora kabisa kuliko kupotea kwa fahamu na hatimaye kusahau." 1 Yahya ibn Sa'id anaandika, "mimi niliwaona Wanazuoni katika hali ya kuchukia uandishi wa Hadith. Laiti tungalikuwa tukiziandika, basi sisi tungalikuwa tunayo elimu kubwa mno ya Sa'id ibn Musayyab na vile vile mashauri yake." 2 Yahya hapa anasikitikia upoteaji wa idadi kubwa ya Hadith zilizosimuliwa na Sa'id na vile vile mashauri yake yote kwa sababu ya kutoziandika.

Urwah ibn al-Zubayr anaandika, "mimi niliandika idadi kubwa ya Hadith na hapo baadaye niliziteketeza. Sasa ninaona kuwa laiti nisingeziteketeza badala yake ningelikuwa nimetoa mali na fidia ya watoto wangu kwa kuzibakiza. 3 Hisham bin Urwah anaelezea "Baba yangu alivichoma vitabu vyake vyote alivyo kuwanavyo katika tukio la Harrah (mnamo mwaka 63 A.H./ 283 A.D. ambapo jeshi la Syria liliposhambulia mji wa Madinah na kuuteketeza mji huo); baadaye aliniambia, 'Laiti ningalikuwa nimeviweka, kwa hakika ingalikuwa bora kabisa kwangu kubakia na Hadith kuliko mali na watoto nilionao kwa hivi sasa." 4 Pia Yahya ibn Sa'id alikuwa akisema kama hayo. 5 Taarifa hizo zinatuonyesha vile baadhi ya watu walivyokuwa wakisikitika kwa kuteketeza vitabu vyao kutokana na sababu moja au nyingine.

Mu'ammar asema, "mimi nilimsimulia baadhi ya Hadith Yahya ibn Kathir. Yeye aliniambia kumwandikia Hadith fulani fulani. Lakini mimi nilimwambia kuwa sisi tulichukia maandishi ya Ilm. Yeye aliniambia, "Andika, kwani usipoandika, utapoteza yote." 6

Al-Mansurr asema, Laiti ningalikuwa nimeziandika Ahadith..........Kwani nimekwisha zisahau kwa idadi sawa na zile nizikumbukazo. Laiti ningalikuwa nimeziandika! Sasa nipo ninazikumbuka nusu tu ya Hadith ya zile nilizokuwa nimezisikia." 7

Ibn Rushd anaandika, "iwapo Wanzuoni wasingalikuwa wamehifadhi elimu kwa kuandika na iwapo wasingalikuwa wameweza kutofautisha katika uhalisi na uzushi, basi elimu yote ingalikuwa imeshapotea na kusingalikuwapo na mwelekeo wowote ule wa Din. Mungu awajaze jazaa iliyo bora kabisa. 8 Mwanzo wa kuandikwa kwa Hadith, mbali na kucheleweshwa kwake, yalikuwa ni maendeleo yaliyokuwa yamekaribishwa, khususan ilifuatia baada ya kuhifadhi Hadith moyoni zikiwemo halisi na zile zilizozuliwa.

Rashid Ridha anaandika, "sisi tuna uhakika kuwa sisi tumesha sahau na kupoteza idadi kubwa ya Hadith za Mtume s.a.w.w. kwa sababu Wanazuoni hawakuziandika Hadith walizokuwa wakizisikia. Lakini kile kilichopotea hakikuhusiana na Qur’an wala hakikuhusiana na maswala ya dini." 9 Baada ya kuukubali ukweli wa kupotea kwa Hadith, yeye anajaribu kutuonyesha kutokuwapo kwa umuhimu wake kwa kusema kuwa kila kilichopotea hakikuwa juu ya Qur’an wala hakikuhusiana na maswala ya Dini.

Mawazo kama hayo hayawezi kukubaliwa: Je, inawezekanaje kwa kitu kiwe ni Hadith ya Mtume s.a.w.w. na papo hapo kisiwe na uhusiano na maswala ya Dini? Vyovyote vile, yeye anatuthibitishia kuwa baadhi ya Madhehebu ya Kiislamu hawana mafunzo yote ya Mtume s.a.w.w. ambayo yalihifadhiwa na Ahl al-Bayt a.s. yake.

Ibn Abd al-Birr aandika, "leo hakuna yeyote achukiae kuandika Hadith. Iwapo Hadith hazitaandikwa basi idadi kubwa ya elimu itaweza kupotea bure." 10

Umar ibn Abd al-Aziz asema, "Wakati nilipotoka Madinah mimi ndiye niliye kuwa mwenye elimu zaidi kuliko wote, lakini kufikia Syria mimi nilikwisha sahau nilichokijua." 11

Yazid ibn Harun alisema, "Mimi nilihifadhi Hadith elfu sabini kutoka Yahya ibn Sa'id. Lakini nilisahau nusu ya Hadith hizo pale nilipougua ugonjwa." 12

Ibn Rahewayh anaandika:"Mimi nilikuwa nimehifadhi moyoni mwangu Hadith elfu sabini na niliweza kujikumbusha zaidi ya Hadith laki moja. Mimi nilikuwa sisikii chochote kile isipokuwa nilikiweka katika hifadhi yangu moyoni. Lakini baada ya muda mimi nilisahau yote." 13

Al-Sha'bi anasema, "Hadi sasa mimi sijaandika hata ukurasa mmoja, na hadi leo hakuna yeyote aliyenielezea Hadith hata moja ambayo ilikuwa imeandikwa bali aliisimulia kwa mdomo tu, na wala sikupenda kusimuliwa kwa mara ya pili. Pamoja na hayo nimekuja kusahau mimi kiasi kikubwa cha elimu (ilm), kiasi kwamba iwapo mtu yeyote atakuwa na elimu hiyo basi atakuwa mwanachuo mkubwa katika zama zake."14 Ishaq ibn Mansur anaandika,"Mimi nilimwuliza Ahmad ibn Hanbal kuhusu wale waliochukia kuandika 'ilm. Yeye alisema kuwa baadhi walichukia na baadhi waliipendelea. Mimi nilidokeza iwapo 'ilm isingaliandikwa basi ingalipotea kabisa. Yeye alikubaliana akisema, 'iwapo kusingaliandikwa kwa 'ilm,' je tungalikuwa na nini hivi leo." 15

Ahmad ibn Hanbal anasema, "Baadhi walitusimulia kutoka fahamu zao na wengineo kutokea vitabuni. Hadith zilizotakana na vitabu zilithaminiwa zaidi." 16 Ahmad mwenyewe kamwe hakusimulia Hadith ila kutokea vitabuni tu. 17

Ibn Salah anaandika, "Iwapo Hadith isingalikuja kuandikwa, basi 'ilm yote ingalikuja kupotea katika zama zilizoifuatia." 18

Taarifa hizo zinatosheleza kuelezea maelezo yetu.

2. Uenezaji Wa Uongo Na Masingizio

Uovu mwingine wa matokeo ya kutoandika Hadith ni kukua kwa Hadith zilizozuliwa na za uongo. Haikuwezekana kudhibiti hali halisi ya Hadith na muundo wake halisi. Hapo mwanzoni, kama inavyoeleweka, watu hawakuupa umuhimu wa sanad (mfululizo wa watu waliosimulia Hadith) kwani hali ya kuaminiana ilikuwapo zamani na ilikuwa imeenea kote. Siku hizi, Wanazuoni wa Hadith, ili kukwepa kukiri kuwa kulikuwapo jambo kama hili la ukweli wa kihistoria, wanasema kuwa hapakuwapo na Hadith zozote zilizozuliwa katika zama za Sahaba. Lakini katika uchunguzi na utafiti uliofanywa siku hizi, imethibitishwa kuwa baadhi ya watu kama Abu Hurayrah, walizua Hadith nyingi mno. 19 Ni kweli kuwa zilifanywa jitihada nyingi katika kuzitofautisha Hadith zilizo halisi na zile zilizo za uongo, lakini haya yalikuwa yametokea katika kipindi ambapo idadi kubwa ya makundi yalijitokeza katika jamii pamoja na mambo ya Imani na Siasa hadi kwamba utofautisho wa halisi (thiqah) pia ulikuwa ukitofautiana na watu walivyokuwa wakielewa. Ni dhahiri kuwa jitihada kama hizi zinaweza kuleta matokeo ya uthamini sahihi wa Hadith na mapotoshi ya aina gani yaliyokuwapo.

Juu ya kuandika somo hili, abu Riyyah anasema, "Wakati Ahadith za Mtume s.a.w.w. zilipoachwa kuandikwa na Sahaba hawakuchukua hatua kuzikusanya, milango ya masimulizi ya Hadith kwa midomo ilifunguliwa kwa ajili ya wacha Mungu na vile vile hali hiyo kwa ajili ya waongo, wapotofu na wazushi, ambao walisimulia chochote kile walichokitaka bila ya kuwa na woga wa yeyote." 20
Mwandishi mwingine anaandika, "Moja ya sababu ya kuchomoza kwa waliokuwa wakibuni Hadith ni kwa sababu ya kutoziandika Hadith na Sahaba waliridhika kwa kusimuliwa kimdomo tu bila ya maandiko yoyote." 21

Abu al-Abbas al-Hanbali (716 A.H./1316 A.D.) anaandika:

Moja ya sababu ya kutofautiana kimashauri miongoni mwa maulamaa ni Hadith na maelezo yanayotofautiana. Baadhi yao wanafikiria kuwa Khalifa Umar ibn Khattab ndiye aliyehusika, kwa sababu Sahaba walimwomba ruhusa ya kuandika Hadith, lakini, yeye aliwazuia, mbali na kutambua ukweli wa amri ya Mtume s.a.w.w. ya kuandika hotuba yake ya Hijja ya mwisho kwa ajili ya Abu Shat na vile vile Mtume s.a.w.w.alikuwa amesema: "Ikamateni elimu yenu kwa kuiandika.'Iwapo kila Sahaba angaliandika alichokisikia kutoka kwa Mtume s.a.w.w., basi Sunnah zingalinakiliwa bila ya kuwapo na msimulizi zaidi ya mmoja (mfululizo wa wanaosimulia) baina ya Mtume s.a.w.w. na (kizazi kilichofuatia) Ummah." 22

Ni jambo la kuvutia sana kwa kuangalia kuwa Abu al-Abbas alishutumiwa kuwa ni rafidh (aliyeasi) na tashayyu (kuwa Shiah) kwa sababu ya maelezo yake hayo!

Abu Riyyah katika maelezo yake mengineyo, yeye anajitokeza katika kukana imani kuwa Mtume s.a.w.w. ndiye alitoa amri ya kutoandikwa kwa Hadith, anasema:

"Je ni sahihi kuwa Mtume s.a.w.w. atakuwa amepuuzia nusu ya kila alichofunuliwa, akiiacha bila kuhifadhiwa katika mioyo ya watu, ambamo mmoja wao anakumbuka, na mwingine, anasahau wakati huo huo na mwingine anaongezea atakacho kwa yale yasiyoandikwa......? Je, uangalifu wa Sahaba upo wapi vile walivyoijali Qur’an? Hakuna kingine chochote kile kwa sababu ya dharau isipokuwa ni matokeo ya kutoandikwa huku kwa nusu ya ufunuo na wao wote ni wenye madhambi katika swala hili." 23

Ibrahim ibn Sa'id ameelezea zaidi kuwa uandishi wa Hadith ulianza pale ambapo palipogunduliwa kuandikwa kwa Hadith za uongo na uzushi. Yeye anasema, "Kama isingalikuwa kutokezea kwa Hadith kutokea Mashariki, sisi tusingalikuwa tumeandika Hadith hata moja, wala kusingaliruhusiwa kuandikwa kwake." 24

Habari kama hiyo pia imeelezwa na Ibn Shihab al-Zuhri. Hata hivyo, Hadith ziliandikwa kwa kuchelewa mno. Uchelewesho huo unaweza kuonekana kutokana na ukweli kuwa Sahih ya al-Bukhari ilichaguliwa miongoni mwa Hadith laki saba na Abu Hanifa alizikubali Hadith 150 tu kati ya Hadith milioni moja!

3. Kusimulia Hadith Kwa Kutoa Maana Tu Na Wala Si Kwa Maneno Yake

Mojawapo ya athari za kutoandika kwa Hadith ni kule kusahauliwa kwa maneno halisi ya Hadith na lilikuwa ni jambo la kawaida kutokea masimulizi yaliyokuwa juu ya maana tu. Ni jambo la kawaida pia kwa mtu aliyesikia Hadith miaka ishirini iliyopita kuielezea kwa maana yake tu wakati aisimuliapo. Kuongezwa na kupunguzwa ni mambo ya kawaida katika hali kama hizo. Hata hivyo, iwapo Hadith zingalikuwa zimeanza kuandikwa kuanzia hapo mwanzoni, uwezekano wa janga kama hilo lingalikuwa dogo.

Imran ibn al-Husayn anasema:

"Kwa kiapo cha Mungu, nilitaka kusimulia Hadith za Mtume s.a.w.w. kwa mfululizo wa siku mbili, lakini kile kilichonizuia kilikuwa ni kuwaona kwangu wale waliosikia Hadith kama mimi, lakini wao walisimulia Hadith katika sura isiyokuwa ya halisi. (Kusimulia kwa kuelezea maana tu). Nami nilikuwa nikiogopa nisije nikasimulia Hadith kama wao. Lakini nakuambia, wao wanafanya makosa mengi katika kusimulia Hadith, ingawaje ni bila ya kunuia." 25

Sufyan anasema:

"Mimi nilisikia kupitia wasimulizi wa Hadith kutokea Bara' ibn Azib kutokea Mtume s.a.w.w. kuwa: "Nilimwona Mtume s.a.w.w. akiinua mikono yake alipokuwa akiianza sala." Na pale nilipokwenda Kufah, nilimwona msimulizi Ibn Abi Layla, akiongezea maneno "Hapo baadaye hakurudia hivyo' katika hayo. Inaonekana kuwa fahamu zake zilikuwa nzuri pale alipokuwa Makkah. Mimi niliambiwa kuwa fahamu zake zimepata mabadiliko kidogo." 26

Ibn al-Jawzi, katika kuelezea habari za wasimulizi wa Ahadith zenye uzushi, anaandika:

Aina ya kwanza ni wale, ambao chini ya ushawishi wa utawa, polepole walipuuzia kuhifadhi Hadith pia kuzitambulisha Hadith na wale, katika hali ya makosa walisimulia Hadith kutokana na hifadhi zao baada ya vitabu vyao kupotea au kuungua au kuzikwa. Aina hii ya watu mara nyingi walisimulia Hadith mursal kama marfu', mawqul kama musnad na mara nyingi waliziingiza Hadith za hapa kuingia pale na za pale kuingizwa hapa. 27

4. Ufarakano Miongoni Mwa Waislamu

Matokeo mengineyo ya kutoandika Hadith ni kugawanyika na kufarakana kwa mashauri ya Waislamu katika mambo ya halali (Shariah), hadi kufikia ufarakano wao katika fatawa na imani. Na haya yalitokana na Hadith zilizotofautiana, ndivyo ilivyokuwa hali ya Waislamu katika nyakati hizo. Kufuatia ushindi wa awali, Islam ilienea katika maeneo mapya. Sahaba na Tabi'un ambao walielekea sehemu mbali mbali zilizokuwa mpya, kila mmoja wao alichukua sehemu ile tu ya Hadith ambayo alisikia kutokea kwa Mtume s.a.w.w. au Sahaba. Kutoka Madinah, baadhi yao walikwenda Makkah na Yemen, baadhi yao walikwenda Syria na Palestina, na baadhi yao waliishi katika miji ya Iraq kama vile Kufah na Basrah.

Matokeo ya hayo, ni kwamba kila mmoja wao alichukuliwa msimamo wake kwa mujibu wa Ahadith alizokuwa nazo. Bila ya kujua Ahadith walizonazo wengineo, kila mmoja wao alifuata fatawa tofauti. Ufarakano huu ulipotambuliwa katika kipindi cha Tabi'un, wao walianza kusafiri ili kuzuru miji tofauti, na hivyo ndivyo 'Safari ya kutafuta Hadith' (al-rihlah talab al-Hadith) ilivyokuja kubuniwa.

Wingi wa safari hizi zilitokea katika karne ya 2 A.H./8 A.D. na 3 A.H./9 A.D. , na hata baada ya hapo sababu ya uhakika nyuma yao ilikuwa kutawanyika kwa Hadith kwa kupitia miji tofauti na Wanazuoni waliotembea huko na huko katika kutafuta na kuleta namna moja ya Hadith baina ya Hadith za sehemu moja na nyingine; lakini wakati mwingine ilitokea kwamba Hadith moja iliweza kusimuliwa tofauti katika sehemu zinginezo - jambo ambalo mfano wake tumeulezea hapo awali.

Sisi twaambiwa kuwa Abdallah ibn Mubarak alisafiri hadi Yemen, Misri, Syria na Kufah kwa madhumuni ya kukusanya Hadith. 28

Abu Hatim al-Razi anaandika:

"Safari zangu za awali zilinipeleka katika kutafuta Hadith, zilinichukua miaka saba. Mimi nilipiga hisabu ya umbali niliosafiri kwa miguu nikapata jumla ya 'Parasang' (parasang moja ni sawa na takriban maili nne hivi) elfu moja. Basi mimi nilikuwa nikiendelea kuongezea hivyo hivyo hadi zilipokuwa zikifikia parasang elfu moja......Mara nyingi nilisafiri kutoka Makkah kwenda Madinah na kutoka Misri hadi Ramlah, kutoka hapo hadi Asqalan, Tabariyyah, Damascus, Homs......29

Ibn Musayyat anasema: "Mimi nilikuwa nikisafiri usiku na mchana katika kutafuta Hadith moja."30 Safari hizi zilikuwa zimeenea sana hadi al-Khatib alikusanya maandiko juu ya somo hilo kwa kukipatia jina la al-rihla fi talab al-Hadith na vile vile al-Ramhurmuzi aliandika sura juu ya somo hilo katika kitabu chake al-Muhaddith al-fadhil.

Safari hizi za kutafuta Hadith zilikuwa muhimu mno hadi Yahya ibn Muin ilimbidi aseme: "Kuna aina nne ya watu ambao hawawezi kutegemea kukomaa kwao....mmoja wao ni yule ambaye atabakia mjini mwaka akiandika Hadith hapo, na hakusafiri hadi miji mingine katika kutafuta Hadith." 31

Matatizo kama hayo, ambayo ni matokeo yenyewe ya kutoandika Hadith, hayakutokea katika swala la Qur’an. Iwapo Hadith za Mtume s.a.w.w. zingalikuwa zimeshaanza kuandikwa kutokea mwanzoni, kwa ushirikiano wa Sahaba wote kwa pamoja, Vyuo vyote vya Kisheriah - na hata kiitikadi na kisiasa - zilizotokezea hapo baadaye basi zisingaliweza kuwapo. Vyuo vyote hivi vinategemea imani zao juu ya Ahadith. Je, kwa kiasi gani Hadith hizo zilikuwa Sahihi? Je, kwa kiasi gani zilikubaliwa na wengine? Kwa kiasi gani wengineo walikubalia maagizo yake iwapo masimulizi yalitegemea maana tu? Haya ni maswali ambayo hayakupatiwa majibu.

Abu Suhrah anaandika:

Wakati Umar alipofariki na Sahaba walipoondoka kwenda miji tofauti, kila mmoja wao alianzisha Chuo cha Sharia kwa ajili yake na hivyo kila mmoja wao aliifuata njia yake. Ulipofika wakati wa Tabi'un, kila mji ulikuwa na Chuo chake cha Sharia na mitazamo yao ilikuwa tofauti na mbali na zingine kama vile miji yenyewe ilivyokuwa mbali na nyingine. 32

Siku moja, al-Mansur alimwambia Malik ibn Anas, juu ya nia yake ya kutengeneza/kutoa kiwango maalum ya ‘kazi zake juu ya Hadith’ iitwayo Muwatta.

Alipendekeza kunakili kitabu kwa kila mji na kuwaagiza watu kufundisha maudhui yake tu (yaani kufundisha na kufuata yaliyokuwamo katika kitabu cha Muwatta) na kujiepusha na chochote kile kingine [zaidi ya Muwatta] kama ndiyo Shariah ya Dini. (au kama ndiyo mamlaka ya Shariah).

Malik alimwambia, "Ewe Amir al-Mu’miniin, usithubutu kufanya hivyo. Watu hawa wanazo itikadi zao, wakiwa wamesikia Ahadith na kuzisimulia, na kila mmoja wao anaamini katika kile alichokuwanacho. Waache peke yao watu wa kila mji pamoja na kila walichojichagulia wao wenyewe." 33

5. Kuenea Kwa Ra'y

Athari nyingine ya kushindwa kwa uandikaji wa Hadith ilikuwa ni kutokezea na kutumika zaidi mno kwa ra'y (hukumu zisizo halisi au hukumu za kibinafsi) miongoni mwa Mahakimu wa Kiislamu, kwa sababu kila mmoja wao alikuwa na kiasi kidogo tu cha Ahadith alizokuwa akiweza kuzifikia, kwani nyingi mno (za Ahadith) ama zilipotea au hazikuweza kufikiwa.

Watu waliwahimiza (mahakimu/wanazuoni) kutoa fatawa wakati ambapo wao walikuwa hawana kiasi cha kutosheleza cha Ahadith kuwasaidia katika hatua hiyo. Kwa hivyo wao iliwabidi kuchagua njia ya ra'y ili kuweza kuwajibu watu. Zaidi ya hayo, wengineo walikuwa ni mabingwa katika ra'y kwa sababu ya kutokuwa na imani katika Hadith, na hii ni wazi kwa kutokezea kwa sababu ya ukosefu wa Ahadith zilizoandikwa.

Wakati fulani, katika mji mmoja hukumu ilitegemea Hadith iliyokuwapo, ambapo mahala pengine hukumu ilikuwa inategemea uamuzi wa (ra'y) kibinafsi. Kwa bahati mbaya, baada ya muda fulani, zile hukumu za ra'y zilijipatia nafasi za mamlaka halisi ya hukumu kwa ajili ya wengine ambao wao pia hawakuwa na ufikio wa kutosheleza katika Hadith, wao walipendelea kufuatilia ra'y za mababu zao badala ya wao kubuni maamuzi yao ya kibinafsi (vile walivyokuwa .wakipendelea wao wenyewe). Kutanda huku kwa tabia ya ra'y kwa kufikia kiasi hiki miongoni mwa Ahl al-Sunna kulitokana na kutokuwapo na kutosheleza kwa Hadith, ambavyo kwa upande wa pili ulitokana na kupotea kwa idadi kubwa mno ya Hadith za Mtume s.a.w.w. na Sunnah zake.

 • 1. Adab al-Mufrad, 69
 • 2. Ingawaje baadhi ya wakusanyaji walianza kazi zao za ukusanyaji katika karne ya 2/8, tarehe za kufariki kwao kwa ujumla zimo katika karne ya 3 / 9.
 • 3. Taqyid al-'ilm , 103
 • 4. Tabaqat al-Kubra , V, 141; Jami’ bayan al - ‘ilm ,I, 81
 • 5. Taqyid al-'ilm , 60; Jami’ bayan al - ‘ilm , I, 75
 • 6. Tabaqat al-Kubra , V,179; Al- Musannaf ‘Abd al-Razzaq, XI, 425; Jami’ bayan al - ‘ilm , I, 90
 • 7. Jami’ bayan al - ‘ilm , I, 89; Taqyid al-'ilm , 111
 • 8. Al- Musannaf ‘Abd al-Razzaq , XI, 259; al-Kifayah fi ‘ilm-al-riwayah, 106
 • 9. Taqyid al-'ilm , 60, al-Muhaddith al-fadhl kutoka al-Ramhurmuzi.
 • 10. Al- Taratib al-idariyyah , II, 249
 • 11. Tafsir al-manar, VI, 288
 • 12. Jami’ bayan al - ‘ilm , I, 84
 • 13. Tadhkirat al-huffadh , I 119.
 • 14. Tadhkirat al-huffadh ,I, 339
 • 15. Tabaqat al-Fuqaha’, 78
 • 16. Tadhkirat al-huffadh , I, 81
 • 17. Jami’ bayan al - ‘ilm , I, 91
 • 18. Taqyid al-'ilm , 115
 • 19. Al- ‘Imla’ wa al- ‘istimla’ , 47
 • 20. Tadrib al- rawi , II, 65
 • 21. Tazama Abu Hurayrah ya Sayyid Sharaf al-Din na Shaykh al- Mudirah ya Abu Riyyah
 • 22. Adwa’ ‘ala al-Sunnat al-Muhammadiyyah, 268
 • 23. Ta'rikh al-fiqh al-Islami, 68
 • 24. Al-Imam al-Sadiq wa al-madhahib al-‘arba’ah, I, 260
 • 25. Adwa’ ‘ala al-Sunnat al-Muhammadiyyah, 52, 53
 • 26. Al-Ma’arifah wa al-ta’rikh , II, 762
 • 27. Ta’wil mukhtalaf al-hadith, 40; al-Mawdu’at, I, 93; Tarikh al-madhahib al-fiqhiyyah, 20.
 • 28. Al-Jarh wa al-ta’dil, ya Abu Hatim al-Razi, I, 43 , 44.
 • 29. Al-Mawdu’at , I 35, 36; Tarikh Ibn ‘Asakir, II, 10
 • 30. Al-Jarh wa al-ta’dil , I, 263
 • 31. Al-Jarh wa al-ta’dil , I, 359, 360
 • 32. Tabaqat al-Kubra , V, 120; Tadhkirat al-huffadh , I, 56; al-Rihlah fi talab al-hadith, 127
 • 33. Al-Muhaddith al-Fadhl, 230