read

Kwanza: Maana Ya Tawassuli Kilugha Na Kiistilahi

Ndani ya kamusi ya Lisanul-Arabi imeelezwa kuwa: Al-Wasilatu Indal- Malaki: Al-Wasilatu ni: Ngazi na ukuruba. (Husemwa): fulani ametumia Wasila kwa Mwenyezi Mungu: Pindi anapotenda amali itakayomkurubisha Kwake.

Al-wasilu: Mwenye raghba na Mwenyezi Mungu. Labidu amesema: “Nawaona watu hawajui thamani ya jambo lao. Ndio; kila mwenye rai ana raghba ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu.”

Ametawasali Kwake kwa Wasila: Pindi anapojikurubisha Kwake kwa amali fulani.

Na ametawasali Kwake kwa kadha: Amejikurubisha Kwake kwa utukufu wenye huruma utakaomhurumia.

Na Al-Wasilatu ni: Fungamano na ukuruba, na wingi wake ni Al-Wasailu. Mwenyezi Mungu amesema: “Hao wanaowaomba, wao wenyewe wanatafuta njia (Al-Wasilatu) iliyo karibu sana miongoni mwao ya kwenda kwa Mola Wao Mlezi(17: 57) 1

Na kamusi nyingine za lugha ya kiarabu zimetoa baadhi ya mifano halisi ya neno Al-Wasilatu, kwa sababu maana yake ni miongoni mwa ufahamu wa wazi na uhalisi wake si zaidi ya kukifanya kitu njia ya kufikia jambo jingine ambalo ndilo makusudio na shabaha. Na njia hiyo hutofautiana kulingana na tofauti za makusudio.

Yule anayetafuta radhi za Mwenyezi Mungu njia yake ya kupitia huwa ni matendo mema ambayo kwayo hupata ridhaa zake, na anayetaka kuizuru Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu hutumia kile kitakachomfikisha huko.2

Ibnu Kathir amesema kuhusu Tawassuli kuwa: “Ni mwanadamu afanye kiungo kati yake na Mwenyezi Mungu ili akidhiwe haja yake kwa sababu ya kiungo hicho.”3

  • 1. Lisanul-Arabi cha Ibnu Mandhuri, Juzuu ya 11, kitomeo: Wasala.
  • 2. At-Tawassul fi Ash-Shariati Al-Islamiya, Jafar Subhani: 17.
  • 3. Tafsir ya Ibnu Kathir 1: 532.