read

Nne: Tawassuli Ndani Ya Hadithi Za Mtukufu Mtume (S.A.W.W.)

Zimepokewa Hadithi mbalimbali zikionyesha ruhusa ya kutawasali kupitia Nabii au Mawalii Wema.

(I) Toka kwa Uthman bin Hunaif amesema: “Mtu mmoja kipofu alikwen- da kwa Mtume akasema: ‘Niombee kwa Mwenyezi Mungu aniponye.’ Mtume akamwambia: ‘Ukipenda nitaomba na ukipenda vumilia na ndiyo bora.’ Yule mtu akamwambia Mtume: ‘Muombe Mwenyezi Mungu.’ Basi Mtume akamwamuru atawadhe vizuri na aswali rakaa mbili na aombe kwa kutumia dua hii: “Ewe Mwenyezi Mungu, hakika mimi nakuomba na ninaelekea kwako kupitia kwa Mtume wako, Mtume wa Rehema. Ewe Muhammad, hakika mimi naelekea kwa Mola Wangu Mlezi kupitia kwako katika haja yangu ili ikubaliwe. Ewe Mwenyezi Mungu mfanye Muhammad kuwa mwombezi wangu.”1

Hadithi hii haina dosari katika usahihi wake mpaka Ibnu At-Taymiyya ameiona kuwa ni sahihi na akasema: “Abu Jafar anayekusudiwa aliyomo ndani ya njia ya upokezi wa Hadithi hii ni Abu Jafar Al-Khatwamiyu, na yeye ni mwaminifu.”

Ama Ar-Rifai yeye amesema: “Hamna shaka kwamba Hadithi hii ni sahihi na ni mashuhuri. Na imethibiti bila wasiwasi wala mashaka kuwa macho ya kipofu yule yalirudia kuona kwa sababu ya dua ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.).”2

Hadithi hii wameileta An-Nasaiy, Al-Bayhaqiy, At-Tabaraniy, At-Tirmidhiy na Al-Hakim ndani ya Al-Mustadrak yake.3

Kwa Hadithi hii inazidi kuthibiti Sheria ya Tawassuli, kiasi tunamkuta Mtume wa Mwenyezi Mungu amemfunza kipofu namna ya kutawasali kwa Mwenyezi Mungu kupitia Nabii Wake, Nabii wa Rehema, na kum- wombea ili kukidhi haja yake. Na makusudio ya Nabii ni Nabii mwenyewe si dua yake. Na kuelekea kwa Mwenyezi Mungu kupitia jaha ya Mtume na njia yake.

(II) Atwiyatu Al-Awfi amepokea kutoka kwa Abu Said Al-Khidri kwam- ba Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Yeyote atakayetoka nyumbani kwake kwenda kuswali akasema:

“Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba kwa haki ya wanaokuomba na ninakuomba kwa haki ya mwendo wangu huu, kwani mimi sikutoka kwa maringo na majivuno, wala kujionyesha wala kutaka kusifiwa, nimetoka kwa kuogopa ghadhabu zako na kutafuta radhi zako; basi ninakuomba uniepushe na moto na unisamehe madhambi yangu, kwani hakuna anayesamehe madhambi isipokuwa Wewe.”

Basi Mwenyezi Mungu atamwelekea mtu huyo kwa dhati yake na watam- takia msamaha Malaika
elfu sabini.”4

Hakika Hadithi hii inaonyesha ruhusa ya kutawasali kwa Mwenyezi Mungu kupitia heshima ya mawalii wema na daraja zao na cheo chao walichonacho mbele ya Mwenyezi Mungu, basi mtu huwafanya hao ndio viun- go na waombezi ili haja zao zikubaliwe na dua zao zipokelewe.

(III) Anas bin Malik amesema: “Alipofariki Fatima binti Asad, Mtume aliingia mahala alipofia akakaa upande wa kichwa chake akasema: “Mwenyezi Mungu akurehemu ewe mama yangu mpendwa baada ya mama yangu mpendwa.” Akataja sifa zake juu yake na kumvisha sanda kwa joho lake, kisha Mtume akamwita Usama bin Zaydi, Abu Ayubu Al-Ansari, Umar bin Al-Khattab na kijana fulani mweusi ili wakachimbe kaburi.

Wakalichimba kaburi lake na walipofikia kuchimba mwanandani Mtume akaichimba hiyo yeye mwenyewe kwa mkono wake na kuutoa mchanga kwa mkono wake. Alipomaliza akaingia kwenye mwanandani kisha akalala ndani yake na akasema:

“Mwenyezi Mungu ndiye anayehuisha na kufisha, na Yeye yu hai wala hatokufa. Ewe Mwenyezi Mungu, msamehe mama yangu mpendwa Fatima binti Asad na uyapanue makazi yake kwa haki ya Mtume Wako na Manabii ambao wamepita kabla yangu.”5

Imepokewa kuwa As-Sawadi bin Qaribi alimsomea Mtume utenzi wake ambao ndani yake alitawasali kupitia Mtume (s.a.w.w.), akasema:

Nashuhudia kwamba hapana Mola isipokuwa Allah.
Na kwamba wewe ndiye mwenye kuaminiwa kuhusu mambo ya kila asiyekuwepo.

Nawe ndiye uliye karibu mno kama njia kwa Mwenyezi Mungu kuliko Mitume wengine, ewe mwana wa watukufu walio wema.

Tuamrishe yale yanayokufikia ewe mbora wa Mitume, japo yatakuwa mazito.

Na uwe mwombezi wangu siku ambayo mwombezi yeyote hatomnufaisha As-Sawadi bin Qaribi japo kwa sehemu ndogo.6

  • 1. Sunanu Ibnu Majah 1: 441, Hadithi ya 1385. Musnad Ahmad 4: 138 Hadithi ya 16789. Mustadrak Asw-Swahahain cha Al-Hakim An-Naisaburi 1: 313. Al- Jamius-Swaghir cha As-Suyutwi: 59. Minihajul-Jamiu 1:286.
  • 2. At-Tawassuli cha Subhani: 69. Amenukuu kutoka kwenye At-Tawassulu ila Haqiqatu At-Tawassul cha Ar-Rifai: 158.
  • 3. Sunanut-Tirmidhi: 5/ 531 Hadithi ya 3578. As-Sunanu Al-Kubra cha An-Nasai: 6, 169, Hadithi ya 10495.
  • 4. Sunanu Ibnu Majah 1: 256 Hadithi ya 778, mlango wa kwenda kwenye Sala
  • 5. Kashful-Irtiyabi: 312, amenukuu toka kwenye Wafaul-Wafai na Ad-Duraru As-Saniyatu: 8..
  • 6. Ad-Duraru As-Saniyatu: 27. At-Tawassulu ila Haqiqatu At-Tawassuli: 300. Fat'hul-Bari 7: 137