read

Pili: Rai Mbalimbali Kuhusu Hukmu Ya Tawassuli.

Kabla hatujaingia kwenye dalili za Tawassuli na uhalisi wake kisheria na kisha kuzijadili, hatuna budi kwanza tunukuu muhtasari wa rai mbalimbali ambazo zimepatikana kuhusu kuruhusiwa na kukatazwa kwa Tawassuli.

Rai Ya Kwanza: Kukatazwa Tawassuli:

Al-Baniyu ndani ya kitabu chake ametoa rai hiyo na kuona kuwa ni upotovu. Na katika utangulizi wa Kitabu Sharhu At-Twahawiyatti1 amesema: “Hakika suala la Tawassuli si miongoni mwa maswala ya kiimani.”

Na miongoni mwa wanaokataza Tawassuli ni Muhammad bin Abdul- Wahabi, anasema: “Iwapo baadhi ya Mushirikina (Yaani Waisilamu wasiyokuwa Mawahabi) wakikwambia: Sikilizeni; “Hakika vipenzi vya Mwenyezi Mungu havina khofu wala havihuzuniki.”2

Au shufaa ni haki au Manabii wana jaha kwa Mwenyezi Mungu au akatoa maneno ya Nabii ambayo kwayo anafanya ni dalili juu ya batili yake, na ikawa wewe hufahamu (Yaani huna uwezo wa kumjibu), basi jibu lake ni kumwambia: Hakika Mwenyezi Mungu ndani ya Kitabu chake ametaja kuwa ambao ndani ya nyoyo zao mna upotovu huacha Aya zilizo waziwazi na hufuata yaliyofichikana.”3

Na miongoni mwa wanaozuia ni Abdul-Aziz bin Bazi, kwani anasema: “Atakayemwomba Nabii na kumwomba shufaa, basi ametengua Uislamu wake.”4

Rai Ya Pili: Kauli Ya Kuruhusu:

As-Shawkani Az-Zaydiyu ameona hivyo ndani ya kitabu chake (Tuhfatudh-Dhakirina) kwa kusema: “Na anatawasali kwa Mwenyezi Mungu kupitia Manabii wake na watu wema.”5

As-Samuhudiyu Ash-Shafiiyyu ameruhusu kwa kusema: “Kutawasali kupitia Mtume inawezekana kukawa kwa kuomba jambo hilo kutoka kwake, ikimaanisha kuwa (s.a.w.w.) ana uwezo wa kusababisha jambo hilo kwa yeye (s.a.w.w.) kuomba na kukuombea kwa Mola wake Mlezi, hivyo inarudi kwenye kumwomba dua yake; japokuwa ibara zinatofautiana.

Na miongoni mwa Tawassuli ni mtu kumwambia: Nakuomba kuingia pamoja na wewe Peponi Hakuna kinachokusudiwa hapa ila ni Mtume (s.a.w.w.) kuwa sababu na mwombezi”6

Ibnu At-Taymiyya ndani ya kitabu (Mansakul-Marawiziyu) amenukuu kutoka kwa Ahmad bin Hanbali kuwa Mtume (s.a.w.w.) ana Tawassuli na Dua. Pia amenukuu hilo kutoka kwa Ibnu Abid-Duniya na Al-Bayhaqi na At-Tabarani kwa njia mbalimbali akithibitisha usahihi wake.7

Na miongoni mwa wanaosema kuwa inaruhusiwa ni Imam Shafi, amesema: “Mimi hutafuta baraka kupitia Abu Hanifa na huja kwenye kaburi lake kila siku, na ninapopatwa na haja huswali rakaa mbili kisha huja kwenye kaburi lake na kumwomba Mwenyezi Mungu haja kwake na huwa haichelewi kukidhiwa.”8

Na miongoni mwa wanaosema kuwa inaruhusiwa ni Abu Ali Al-Khalali Sheikh wa kihambali kwani anasema:
“Sikuhuzunishwa na jambo lolote kisha nikaja kwenye kaburi la Musa bin Jafar na kutawasali kupitia kwake ila Mwenyezi Mungu alinirahisishia lile nilipendalo.”9

Ama Shia Imamiya wao wamesema: “Katika kukidhiwa haja na kuondolewa matatizo inaruhusiwa kutawasali kupitia Nabii na Maimamu baada ya kifo chao, kama inavyoruhusiwa katika hali ya uhai wao, kwakuwa kufanya hivyo; kwanza si kumsemeza asiyekuwepo, na pili si shirki.”10

Rai Ya Tatu: Kutenganisha Kati Ya Aina Za Tawassuli:

Rai hii ni ya Ibnu At-Taymiyya, lakini tunamkuta katika suala la Tawassuli anatapatapa kirai, mara anakanusha na mara nyingine anaruhusu, na tatu anatenganisha. Na alipoonyesha vigawanyo vyake vya sura za Tawassuli, aliruhusu viwili na kuharamisha cha tatu, amesema: “Neno Tawassuli, linakusudiwa maana tatu: Mojawapo ni: Kutawasali kwa kumtii Mtume na kumwamini, na hili ndio asili ya Imani na Uislamu, na atakayelikanusha basi ukafiri wake ni dhahiri kwa watu maalumu na wa kawaida.

Pili: Kutawasali kwa dua yake na shufaa yake - Yaani Mtume hapa ndiye anayeomba na kumwombea moja kwa moja - hili lilifanyika zama za uhai wake na litafanyika siku ya Kiyama, watatawasali kupitia shufaa yake. Na atakayekanusha hili basi yeye ni kafiri murtadi anayetakiwa kutubu, basi akitubu sawa na kama sivyo huuwawa akiwa murtadi.

Tatu: Kutawasali kupitia shufaa yake baada ya kifo chake na kuapa kwa Mwenyezi Mungu kupitia dhati yake, hili ni miongoni mwa Bidaa iliyozushwa.”11

 • 1. Al-Bisharatu Wal-Ittihafi cha As-Saqafi: 52. Amenukuu toka kwenye Sharhu At-Twahawiya: 60.
 • 2. Yunus: 62.
 • 3. Kashfu -Shubuhati cha Muhammad bin Abdul-Wahabi: 60.12 Mukhalafatul-Wahabiyati Lil-Qur’ani Was-Sunnati cha Umar Abdus-Salami:
 • 4. Amenukuu toka kwenye Al-Aqidatus-Swahihatu Wanawakidhul-Islami cha Abdul-Aziz bin Abdullah bin Bazi.
 • 5. Tuhfatudh-Dhakirina cha Ash-Shawkani: 37.
 • 6. Wafaul-Wafa Biakhbari Daril-Mustwafa cha As-Samuhudiyu 2: 1374.
 • 7. At-Tawassulu Wal-Wasilatu cha Ibnu At-Taymiyya: 144-145, chapa ya Darul- Afaki mwaka 1399 A.H. Na itakujia rai yake yeye mwenyewe.
 • 8. Tarikhu Baghdadi 1: 123, mlango wa yaliyoelezwa kuhusu makaburi ya Baghdadi.
 • 9. Tarikhu Baghdadi 1: 120, mlango wa yaliyoelezwa kuhusu makaburi ya Baghdadi.
 • 10. Al-Barahinu Al-Jaliyatu fi Daf ’i Tashikikatil-Wahabiyya, cha As-Sayyidu Muhammad Hasani Al-Kazawiniyu Al-Hairiyu: 30.
 • 11. Tazama: At-Tawassulu Wal-Wasila: 13, 20, 50.