read

Sita: Tawassuli Kwa Mujibu Wa Kizazi Cha Mtume

Maimamu wa Ahlul-Baiti wamehimiza sana kutawasali kupitia Qur’ani tukufu, Mawalii wa Mwenyezi Mungu na mengineyo. Atakayerejea kwenye vitabu vya Shia Imamiya, vitabu vyao vya Hadithi na vitabu vyao vya dua atalikuta ni jambo la wazi kabisa kiasi kwamba haiwezekani kulishakia. Ifatayo ni baadhi ya mifano:

a) Al-Harith bin Al-Mughira amepokea, amesema: “Nilimsikia Abu Abdullah akisema:

“Iwapo mmoja wenu anataka kumwomba Mola Wake Mlezi kitu kati ya haja za kidunia, basi asianze mpaka aanze kumhimidi na kumsifu Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumtakia rehema Mtume (s.a.w.w.) kisha amwombe Mwenyezi Mungu haja zake.”1

b) Kutoka kwa Abu Jafar (a.s.) amesema: Jabir Al-Answari amesema: “Nilimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.): Unasemaje kuhusu Ali bin Abu Twalib? Akasema: “Yeye ni nafsi yangu.”

Nikasema: Unasemaje kuhusu Hasani na Huseini? Akasema: Wenyewe wawili ni roho yangu na Fatuma mama yao ni binti yangu, kinanichukiza kile kinachomchukiza na kinanifurahisha kile kinachomfurahisha. Nashuhudia kwa Mwenyezi Mungu kuwa hakika mimi ninapigana na wanaopigana nao na nina amani na wale wanaokaa nao kwa amani. Ewe Jabir, ukitaka kumwomba Mwenyezi Mungu na akujibu ombi lako mwombe kupitia majina yao, hakika yenyewe ni majina vipenzi kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.”

c) Kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.): “Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi naelekea kwako kupitia Muhammad na Kizazi cha Muhammad na naku- rubia kwako kupitia wao na ninawatanguliza huku nikiwa na haja.”2

d) Imam Ali Kiongozi wa waumini (a.s.) ndani ya dua yake alikuwa akisema: “……..kwa haki ya Muhammad na Kizazi cha Muhammad iliyo juu yako, na haki Yako tukufu juu yao wapelekee Rehema kama unavyostahiki na unipe kilicho bora mno kuliko vile ulivyowapa waombaji miongoni mwa waja wako waumini waliotangulia na kilicho bora mno kuliko vile utakavyowapa waja wako waliosalia miongoni mwa waumini.” 3

e) Imam Abu Abdullah Husein (a.s.) katika dua yake ya Arafa amesema: ‘Ewe Mwenyezi Mungu hakika sisi tunaelekea kwako - jioni hii ambayo umeifaradhisha na kuitukuzakupitia Muhammad Nabii wako na Mteule wako miongoni mwa viumbe vyako.4

f) Imam Zainul-Abidin amesema ndani ya dua yake ya munasaba wa kuingia Mfungo wa Ramadhani: …..Ewe Mwenyezi Mungu, hakika mimi nakuomba kupitia haki ya Mfungo huu na haki ya atakayejibidisha humu kwa Ibada, mwanzo wake hadi mwisho wake; kuanzia Malaika uliyemkurubisha au Nabii uliyemtuma au mja mwema uliyempenda…..” 5

  • 1. Biharul-Anwar: juzuu 93, kitabu cha utajo na dua, mlango wa 17, Hadithi ya 19 kutoka kwenye Iddatu Ad-Dai: 97.
  • 2. Biharul-Anwar, Juz 94, mlango wa 28, Hadithi ya 19. Kutoka kwenye Da’awatul-Qutubi Ar-Rawandiyu.
  • 3. As-Swahifatul-Alawiyya cha As-Samahijiyu: 51.
  • 4. Iqbalul-Amali cha Ibnu Twawusi 2: 85.
  • 5. As-Swahifatus-Sajadiyya: Dua namba 44.