read

Tano: Sera Ya Waislamu Katika Tawassuli

Sera ya waislamu zama za uhai wa Mtume (s.a.w.w.) na baada ya kufa kwake ni kutawasali kupitia Mtume (s.a.w.w.) na Mawalii wa Mwenyezi Mungu na kuomba shufaa kupitia vyeo vyao na heshima zao mbele ya Mwenyezi Mungu. Ifatayo ni mifano ya sera hiyo ya waislamu:

a) Baada ya kufariki Mtume wa Mwenyezi Mungu Abu Bakr alisema: “Ewe Muhammad tutaje mbele ya Mola wako Mlezi na tuwe ndani ya kumbukumbu yako.”1

b) Al-Hafidh Abu Abdullah Muhammad bin Musa An-Nu’mani ndani ya kitabu chake Misbahu Adh-Dhulami amesema: “Hakika Al-Hafidh Abu Said As-Samuani ameeleza tuliyopokea kutoka kwake kutoka kwa Ali bin Abu Twalib kuwa (a.s.) alisema: “Baada ya siku tatu tangu tulipomzika Mtume wa Mwenyezi Mungu alitujia bedui akajitupa juu ya kaburi la Mtume (s.a.w.w.) na kumwagia sehemu ya udongo wake juu ya kichwa chake na kusema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ulisema tukasikia kauli yako. Ukatuelimisha kuhusu Mwenyezi Mungu na tukaelimika kuhusu wewe, na miongoni mwa yaliyoteremshwa ilikuwa ni: “Lau wangelikujia walipojidhulumu nafsi zao wakaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu...”
Na nimeshaidhulumu nafsi yangu na nimekujia uniombee msamaha.” Basi akaitwa toka kaburuni: Hakika Yeye (Mwenyezi Mungu) ameshakusamehe.”2

c) Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa keshamfunza mtu fulani namna ya kuomba awe anamwomba Mwenyezi Mungu, kisha awe anamse- meza Mtume na awe anatawasali kupitia yeye (s.a.w.w.), kisha amwombe Mwenyezi Mungu akubali shufaa yake, aseme:

“Hakika mimi nakuomba na natawasali kwako kupitia Nabii wako Nabii wa Rehma. Ewe Muhammad; ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu; hakika mimi ninatawasali kupitia wewe kwa Mola Wangu Mlezi katika haja yangu ili nikidhiwe. Ewe Mwenyezi Mungu mfanye awe mwombezi wangu.”3

d) Ndani ya Sahih Bukhari imekuja kuwa: Umar bin Al-Khattab alikuwa kila wanapopatwa na ukame huomba mvua kupitia Abbas bin Abdul-Mutwalibi (r.a.) na kusema: “Ewe Mwenyezi Mungu tulikuwa tuk- itawasali kwako kupitia Mtume wetu na ukitupa mvua, basi sasa tunatawasali kwako kupitia ami ya Mtume wetu basi tupe mvua.” Bukhari amesema: “Basi hupewa mvua.”4

e) Al-Mansur Al-Abasiyu alimuuliza Malik bin Anas –Imam wa madhehebu ya Maliki - kuhusu namna ya kumzuru Mtume (s.a.w.w.) na namna ya kutawasali kupitia yeye…. Akamwambia Malik: Ewe Abu Abdullah, nielekee Kibla niombe au nimwelekee Mjumbe wa Mwenyezi Mungu? Malik akajibu: Kwa nini unampa kisogo Mtume wakati yeye ndiyo njia yako na njia ya baba yako Adamu Siku ya Kiyama? Bali mwelekee na umwombe akuombee na Mwenyezi Mungu atakubali maombi yako, kwani Mwenyezi Mungu anasema: “Na lau walipozidhulumu nafsi zao….”5

f) Shafi’i amesoma beti hizi mbili za shairi lake akitawasali kupitia Kizazi cha Mtukufu
Mtume (s.a.w.w.):

“Kizazi cha Mtume, wao ni njia yangu na wao ni wasila wangu kwa Mwenyezi Mungu. Kwao wao kesho nataraji kupewa kitabu changu kwa mkono wa kulia.6

Baada ya maelezo yote yaliyotangulia miongoni mwa dalili, hoja na ushahidi wa kihistoria inawezekana kusema kwamba: Manabii na watu wema miongoni mwa waja Wake wanahesabiwa kuwa ndio njia za kishe- ria ambazo alizikusudia Mwenyezi Mungu kwenye kauli yake: “Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu na tafuteni njia ya kumfikia.”7

Na hapa njia inajumuisha mambo ya Sunna na wala haikomei kwenye kutekeleza mambo ya faradhi na kujiepusha na mambo ya haramu pekee.

  • 1. Ad-Durarus-Saniyatu fi Radi A'lal-Wahabiyya: 36.
  • 2. Wafaul-Wafai cha As-Samuhudiyu 2: 1361.
  • 3. Majumuatu Ar-Rasaili Wal-Masaili cha Ibnu At-Taymiyya 1: 18.
  • 4. Sahih Bukhari: Mlango was ala na kuomba mvua 2: 32, Hadithi ya 947.
  • 5. Kutoka kwenye Wafaul-Wafai cha As-Samuhudiyu 2: 1376.
  • 6. As-sawaaiqul-Muhriqa: 274.
  • 7. Al-Maida: 35.