read

Tatu: Ruhusa Ya Tawassuli Ndani Ya Qur’ani Tukufu

Manabii na waja wema wamethibitisha ukweli wa Tawassuli kama Ibada ya kisheria isiyo na vumbi lolote. Na Qur’ani imetunukulia maeneo mengi ambayo watu walitawasali kupitia Manabii na Mawalii kwa lengo la kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, na baada ya dua zao yalikuwa yanatimia na kujibiwa maombi yao.

Miongoni mwa maeneo yaliyoelezwa na Qur’ani tukufu ni:

a) Mwenyezi Mungu amesema:

وَأُبْرِئُ الْأَكْمَهَ وَالْأَبْرَصَ وَأُحْيِي الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِ اللَّهِ ۖ {49}

“Na niwapoze vipofu na wenye mbalanga, niwafufue wafu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.”
Al-Imrani: 49.

Hapa tunakuta watu wametawasali kupitia Isa (a.s.), lakini kutawasali huku hakukutokana na imani kuwa Isa (a.s.) ana uwezo usiyokuwa wa Mwenyezi Mungu, bali kulitokana na imani yao kuwa Isa (a.s.) ana uwezo unaomwezesha kuponya magonjwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kwa kuwa yeye (a.s.) ni mwenye jaha mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hili halihesabiwi shirki; kwani shirki ni kuamini Isa ana uwezo wa kujitegemea usiotokana na uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na hakuna mwislamu yeyote anayesema hilo.

b) Mwenyezi Mungu amesema:

قَالُوا يَا أَبَانَا اسْتَغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا إِنَّا كُنَّا خَاطِئِينَ {97}

Wakasema: Ewe baba yetu tuombee msamaha kwa dhambi zetu, hakika sisi tulikuwa ni wenye makosa.”Yusuf: 97.
Hakika wana wa Yakub hawajaomba msamaha kutoka kwa Yakub kwa kumweka kando na uwezo wa Mwenyezi Mungu, bali walimfanyaYakub (a.s.) kiungo katika kuomba maghufira kwa kuwa yeye (a.s.) ni mtu wa karibu na mwenye jaha kwa Mwenyezi Mungu. Hili liko wazi kupitia jibu la Yakub kwa wanawe:

قَالَ سَوْفَ أَسْتَغْفِرُ لَكُمْ رَبِّي ۖ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ {98}

“Akasema: Nitakuombeeni msamaha kwa Mola Wangu Mlezi, kwani yeye ndiye Mwingi wa kusamehe Mwenye kurehemu.”Yusuf: 98.

c) Mwenyezi Mungu amesema:

وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّهَ تَوَّابًا رَحِيمًا {64}

“Na lau wangelikujia walipojidhulumu nafsi zao wakaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na Mtume akawaombea msamaha, bila shaka wangemkuta Mwenyezi Mungu Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.” An-Nisa: 64.

Aya inaashiria kukubaliwa kwa maghufira anayowaombea Mtume waisla- mu wenye kutubu, kwa sababu ana jaha kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Na wakati huohuo inatilia mkazo umuhimu wa waislamu kuja kwa Mtukufu Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa lengo la Mtume kuwaombea maghufira.1

Ndiyo, hayo yote ni zama za uhai wake.

Aina Za Tawassuli Kama Zinavyoonyeshwa Na Quran Tukufu18

Mwenyezi Mungu ndani ya Qur’ani tukufu amewahimiza waja wake waumini kutawasali na akaruhusu Tawassuli za aina mbalimbali, na hapa kwa ufupi tunakuletea aina mbalimbali za Tawassuli zilizoruhusiwa kisheria ndani ya Qur’ani tukufu.

A) Kutawasali Kupitia Majina Ya Mwenyezi Mungu:

Amesema:

وَلِلَّهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {180}

“Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri basi mwombeni kwayo, na waacheni wale wanaoharibu utakatifu wa majina yake watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”Al-Aaraf: 180.

Aya inatoa wasifu wa majina ya Mwenyezi Mungu kuwa yote ni mazuri bila kubagua, kisha inaamuru maombi kupitia kwayo, hivyo mja anapotaja majina yake ambayo yamebeba kila heri na uzuri, rehema, maghufira na utukufu, kisha mja akaenda mbele ya Mwenyezi Mungu kuomba maghufira dhidi ya madhambi na akaomba kukidhiwa haja, basi Mwenyezi Mungu atajibu dua ya mwenye kutawasali kupitia majina yake.

B) Kutawasali Kupitia Matendo Mema:

Kwa hakika matendo mema huhesabiwa kuwa ni njia za kisheria ambazo kupitia kwazo mja hujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Tawassuli maana yake ni kutanguliza kitu fulani kwenye uwanja wa Mola Mlezi kwa lengo la kupata ridhaa yake, basi hamna shaka kuwa matendo mema ni miongoni mwa njia bora ambazo anashikamana nazo mja kwa lengo la kutimiza haja zake. Mwenyezi Mungu amesema:

وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا ۖ إِنَّكَ أَنْتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ {127}

رَبَّنَا وَاجْعَلْنَا مُسْلِمَيْنِ لَكَ وَمِنْ ذُرِّيَّتِنَا أُمَّةً مُسْلِمَةً لَكَ وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا وَتُبْ عَلَيْنَا ۖ إِنَّكَ أَنْتَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ {128}

“Na Ibrahim na Ismail walipoinua misingi ya Nyumba. Eee Mola wetu Mlezi utukubalie, hakika Wewe ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua. Eee Mola Wetu Mlezi, utufanye tuwe wenye kunyenyekea Kwako na utuonyeshe ibada zetu na utupokelee, bila shaka Wewe ndiye Mwenye kupokea, Mwenye kurehemu.” Baqara: 127-128.

Hapa Aya inahimiza mafungamano ya matendo mema, nayo ni kujenga Nyumba na dua ambayo Nabii Ibrahim alikuwa akitamani itimie, nayo ni kukubaliwa kwa matendo mema. Na kutokana na kizazi chake upatikane umma wenye kunyenyekea kama inavyosisitiza kauli ya Mwenyezi Mungu:

الَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا إِنَّنَا آمَنَّا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ {16}

“Ambao husema: Mola wetu Mlezi, hakika sisi tumeamini basi tusamehe madhambi yetu, na utuepushe na adhabu ya moto.”Al- Imrani: 16

Utaona kaunga kitendo cha kuomba maghufira kwenye kauli yake: “Eee Mola wetu Mlezi, hakika sisi tumeamini.” Hivyo Al-Fau hapo inaonyesha fungamano kati ya imani na kuomba maghufira.

C) Kutawasali Kupitia Dua Ya Mtukufu Mtume:

Qur’ani tukufu imeashiria nafasi ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), utukufu wake na hadhi yake mbele ya Mwenyezi Mungu na tofauti kati yake na watu wengine, akasema:

لَا تَجْعَلُوا دُعَاءَ الرَّسُولِ بَيْنَكُمْ كَدُعَاءِ بَعْضِكُمْ بَعْضًا ۚ {63}

“Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi.” An-Nur: 63.

Pia Qur’ani tukufu ikaashiria kuwa Mtukufu Mtume ndiye mmoja wa amani mbili ardhini, akasema:

وَمَا كَانَ اللَّهُ لِيُعَذِّبَهُمْ وَأَنْتَ فِيهِمْ ۚ وَمَا كَانَ اللَّهُ مُعَذِّبَهُمْ وَهُمْ يَسْتَغْفِرُونَ {33}

“Na Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaadhibu maadamu wewe umo pamoja nao, wala Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaadhibu hali wanaomba msamaha.”Al-Anfal: 33.

Kisha tunaikuta Qur’ani tukufu sehemu zaidi ya moja inakutanisha Jina la Mwenyezi Mungu na Jina la Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na kuyanasibisha na kitendo kimoja, anasema:

وَسَيَرَى اللَّهُ عَمَلَكُمْ وَرَسُولُهُ ثُمَّ تُرَدُّونَ إِلَىٰ عَالِمِ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ {94}

“Na Mwenyezi Mungu ataviona vitendo vyenu na Mtume wake, kisha mtarudishwa kwa Mjuzi wa siri na dhahiri.”At-Tawbah: 94.

Na anasema:

وَمَا نَقَمُوا إِلَّا أَنْ أَغْنَاهُمُ اللَّهُ وَرَسُولُهُ مِنْ فَضْلِهِ ۚ {74}

“Na hawakuona kosa ila ya kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake amewatajirisha kwa fadhila Zake.”At-Tawbah: 74.

Na Aya nyingine ambazo ndani yake kuna jina la Mtukufu Mtume limekutanishwa na jina la Mwenyezi Mungu, hivyo ikawa hii ndio nafasi ya Mtume kwa Mwenyezi Mungu, basi dua yake haikataliwi na hujibiwa ombi lake, na anayeshikamana na dua yake anakuwa kashikamana na nguzo imara.

Kwa ajili hiyo tunamkuta Mwenyezi Mungu anawaamuru wenye dhambi miongoni mwa waislamu washikamane na dua yake na wamwombe maghufira Mwenyezi Mungu kwenye kikao chake na wamwombe Mtume awaombee maghufira ili kitendo cha Mtume kuwaombea maghufira kiwe sababu ya kuteremka rehema zake na kukubaliwa toba yao. Mwenyezi Mungu amesema:

وَمَا أَرْسَلْنَا مِنْ رَسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّهِ ۚ وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّهَ تَوَّابًا رَحِيمًا {64}

“Na hatukumpeleka Mtume yeyote ila apate kutiiwa kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Na lau wangelikujia walipojidhulumu nafsi zao wakaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na Mtume akawaombea msamaha, bila shaka wangemkuta Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.”An-Nisa: 64.

Na kuhusu maana hii ni kauli ya Mwenyezi Mungu:

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا يَسْتَغْفِرْ لَكُمْ رَسُولُ اللَّهِ لَوَّوْا رُءُوسَهُمْ وَرَأَيْتَهُمْ يَصُدُّونَ وَهُمْ مُسْتَكْبِرُونَ {5}

“Na wanaambiwa: Njooni Mtume wa Mwenyezi Mungu atakuombeeni msamaha huvigeuza vichwa vyao, na unawaona wana- jizuia na wakijiona ni wakubwa.”Al-Munafiquna: 5.

D) Kutawasali Kupitia Dua Ya Ndugu Muumini:

Mwenyezi Mungu amesema:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِنْ بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَحِيمٌ {10}

“Na waliokuja baada yao wanasema: Mola wetu Mlezi tusamehe sisi na ndugu zetu waliotangulia katika imani, wala usiweke mfundo kwa walioamini, Mola wetu Mlezi, hakika wewe ni Mpole sana, Mwenye kurehemu.” Al-Hashr: 10.

Aya tukufu inaonyesha kuwa waumini waliofuatia wanawatakia maghufira ndugu zao waliotangulia, na hii inaonyesha kuwa dua ya ndugu kwa ndugu yake ni jambo la kupendeza na hujibiwa.

E) Kutawasali Kupitia Manabii Na Watu Wema Wao Wenyewe:

Fungu hili si fungu lililotangulia ambalo ni kutawasali kupitia dua ya Mtukufu Mtume, bali lenyewe ni kutawasali kupitia Manabii wenyewe na watu wema na kuwafanya njia ya kujibiwa dua na kuelezea kwa sauti ya juu cheo na hadhi waliyonayo mbele ya Mwenyezi Mungu.

Ikiwa tumetawasali kwa Mwenyezi Mungu kupitia dua ya Mtume kama njia ya kufika kwake, basi katika fungu hili tunamfanya Mtume mwenyewe na heshima yake njia ya kufika kwa Mtukufu Mola Mlezi. Inajulikana kuwa Al-Wasila ni dua itokanayo na ule utu ambao Mwenyezi Mungu ameutukuza na kuukuza na kunyanyua hadhi yake kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

وَرَفَعْنَا لَكَ ذِكْرَكَ {4}

“Na tukakutukuzia sifa zako.”Al-Inshirah: 4.

Na akawaamuru waumini kumheshimu na kumtukuza, akasema:

فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنْزِلَ مَعَهُ ۙ أُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ {157}

“Basi wale waliomwamini yeye na kumtukuza na kumsaidia na wakai- fuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye, hao ndio wenye kufaulu.” Al- Aaraf: 157.
Ikiwa nguzo ya kujibiwa dua ni utu wake wa pekee wa juu na nafasi yake kwa Mwenyezi Mungu basi ni bora mwanadamu atawasali kupitia utu huo kama anavyotawasali kupitia dua yake. Hivyo atakayekiri kuruhusiwa aina ya mwanzo na akakataza ya pili basi atakuwa ametenganisha kati ya mambo mawili yasiyoachana.

Aina hii ya Tawassuli inaungwa mkono na Sunna ya Mtukufu Mtume iliyopokewa kwa njia sahihi ambayo vigogo wote wa Hadithi wameikubali.2

F) Kutawasali Kupitia Haki Ya Waja Wema, Heshima Yao Na Vyeo Vyao:

Hakika anayefuatilia sera ya waislamu ataikuta imejaa aina hii ya Tawassuli, yaani wao wanatawasali kupitia vyeo vya waja wema na heshi- ma zao mbele ya Mwenyezi Mungu na haki yao juu Yake, na hili ndilo ambalo ufafanuzi wake unakuja kama ifuatavyo:

  • 1. Tazama: Mukhalafatul-Wahabiyati Lil-Qurani Was-Sunnati: 22.
  • 2. Rejea At-Tirmidhi, kitabu cha maombi, mlango wa 119, namba 3578, 5: 531. Na Sunanu Ibnu Majah 1: 441 namba 1385. Na Musnad ya Ahmad 4: 138, Hadithi ya 16789.