read

11. Uzani Wa Makosa

Mtenda madhambi haimpasi kulifikiria kosa lake kuwa dogo bali daima awe akifikiri kuwa amelitenda tendo au dhambi kubwa mno mbele ya Allah swt. Inambidi aelewe wazi wazi kuwa adhabu, ghadhabu za Allah swt ni kali mno kiasi kwamba hata dunia au mbingu haziwezi kustahimili.

Allah swt anatuambia katika sura Buruuj aya 12:

Hakika kutesa kwa Mola wako ni kukali sana. (85:12)

Vile vile katika sura Muzammil, Aya 12-13 twaambiwa:

Hakika tuna (namna namna) adhabu na moto uwakao (mkali kabisa). Na chakula kikwamacho (kisakamacho) kooni na adhabu iumizayo. (73:12-13)

Katika Aya hizi Allah swt anatuelezea ghadhabu na adhabu zake na shida zake, yaani kwa ufupi ni kwamba inambidi kila mtu awe akiyafikiria madhambi aliyoyatenda na awe daima akisikitika na kuhuzunika hadi mauti yake. Kilio na huzuni yake vitaweza kupooza miale ya moto ya Jahannam. Kilio chake kitaweza kuondoa giza lililotanda moyoni mwake.

Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) amesema:
"Mwenye kutubu madhambi yake huwa sawa na asiyetenda dhambi kabisa (bali huwa bora zaidi ya huyo)."
(Thawabul A'mal wa Iqabiha. Uk. 273:Tawba)

Allah swt amesema katika sura al-Baqarah, Aya 222:

"Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubu na huwapenda wanaojitakasa." (2:222)

Doa –I- Abu Hamza Thumali:
"Ewe Allah swt! Nijaalie TAWBA ile ambayo ni dalili ya mapenzi yako, na kwa kupitia TAWBA nikufikie hadi kwako!"