read

C. Hadithi Ya Abul-Hayyaj

Hivi sasa umefika wakati wa kuichunguza hadithi wanayoitegemea Mawahabi kuharamisha kujenga juu ya makaburi. Kabla ya yote tunaitaja hadithi yenyewe kwa sanadi aliyoipokea Muslim katika kitabu chake.

"Ametusimulia Yahya ibn Yahya, na Abubakar ibn Abi Shaiba na Zuhayr ibn Harb, Yahya ametusimulia; (na watu wawili wa mwisho wamesema): Ametusimulia Waki'i, amepokea kutoka kwa Sufyan, toka kwa Habib bin Abi Thabiti, naye kapokea kwa Abi Wa'il ambaye kapokea toka kwa Abil Hayyaj Al Asadi' amesema: "Ali ibn Abi Talib alimwambia: Je, nikutume kwa jambo ambalo Mtume wa Mwenyezi Mungu alinituma kwamba, usiache sanamu yoyote ila uiondoshe wala kaburi lolote lile lililonyanyuka isipokuwa ulisawazishe."1

Hadithi hii Mawahabi wameifanya kuwa ndiyo dalili ya kuharamisha kujenga juu ya makaburi bila hata ya kufanya uchunguzi wowote kwa watu walioipokea na Sanadi yake.

Kuijadili Hadithi

Kwa ujumla tunapotaka kutoa ushahidi kwa kutumia hadithi ili tutoe hukmu miongoni mwa hukmu za Mwenyezi Mungu, hapana budi hadithi hiyo itimize masharti haya mawili:

1) Kusihi kwa Sanadi: Hii ikiwa na maana kwamba, wapokezi na watu wahusikao kwenye hadithi yenyewe katika kila ngazi wawe ni waaminifu kiasi ambacho iwezekane kuwategemea katika maneno yao.

2) Ushahidi wa hadithi: Maana yake ni kwamba, matamko na sentensi zilizomo katika hadithi hiyo ziwe zimetimia katika kuelekeza makusudio yetu kwenye hadithi hiyo, kiasi waweze kuifahamu na wengine wanaofahamu vizuri lugha iliyomo katika hadithi hiyo, na wazifahamu pia kanuni zake kama tunavyozifahamu sisi na waweze kutoa matokeo tunayoweza kuyatoa.

Na kwa bahati nzuri, hadithi ya Abul-Hayyaj imekosa sharti zote mbili na hasa ile ya pili, kwani hakuna mahusiano yoyote kabisa ya kujenga juu ya makaburi katika hadithi hiyo.

Ufafanuzi Wa Mambo Haya

(A) Ama upande wa Sanad, ndani ya hadithi hii wamo wapokezi ambao wanachuoni wa hadithi hawakuafikiana juu ya uaminifu wa wapokezi hao, pia hapa chini tunataja majina ya wapokezi waliomo katika hadithi hii ambao wanachuoni wa hadithi wamezikataa hadithi zao:

1) Waki'
2) Sufyan Ath-Thauri

3) Habib ibn Abi Thabit
4) Abu Wai'l Al-Asadi.

Wapokezi hawa wanne amewatia kasoro Al-Hafiz ibn Hajar Al-'Asqalani katika kitabu chake kiitwacho "Tahdhibut-Tahdhib, na amewataja kwa sifa ambazo zinaondoa uaminifu katika hadithi yao hii tuliyotaja hapo kabla na pia kwenye hadithi zao nyingine.

Kwa upande wa huyu Waki' anapokea Al-Hafiz Al- 'Asqalani kutoka kwa Ahmad bin Hanbal (Imam wa Madh-hebu ya Kihanbal) amesema: "Hakika Waki' amefanya makosa katika hadithi mia tano".2

Anasema tena Al-'Asqalani akimnakili Muhammad bin Nasr Al-Marwazi "Waki' alikuwa akisimulia hadithi kwa mujibu wa maa'na yake' isitoshe hakuwa mtaalam wa lugha". 3

Na kwa upande wa "Sufyan At-Thauri" Al-'Asqalani anasema kwa kumnakili ibn Mubarak: "Sufyan alikuwa akisimulia hadithi, basi mimi nikafika kwake na yeye alikuwa anafanyia Tadlis hadithi hiyo (kufanya udanganyifu katika hadithi), basi aliponiona aliona haya (kwa tendo lake hilo).4

Kitendo cha kudanganya katika hadithi kwa namna yo yote ile, kinajulisha kwamba yule msimulizi alikuwa hana tabia ya uadilifu na ukweli, kwa hiyo alikuwa akikifanya kitu kisicho cha kweli kionekane kuwa ni kweli, kama ilivyo maana ya tadlis katika lugha ya Kiarabu.

Ama huyu "Habib ibn Abi Thabit", Al-Asqalani ameandika akimnakili Abu Habbani:

"Kwa hakika Habib: Alikuwa mdanganyifu."5

Na ameandika Al-'Asqalani akimnakili Qat-tan: "Hakika Habib siyo mtu wa kufuatwa."

Ama huyu Abu Wa'il, yeye alikuwa mpinzani wa Imam Ali [a] na ni miongoni mwa watu waliomfanyia uadui na kero Imam Ali [a].6
Basi vipi atategemewa mtu kama huyo, wakati Mtume [s] amesema; "Ewe Ali, hatakupenda wewe isipokuwa mtu mu'umini, na hatakubughudhi isipokuwa mtu mnafiki."7

Na inafaa kusema kwamba mpokeaji wa hadithi ya Abul-Hayyaj hana hadithi hata moja katika sihahi zote sita isipokuwa hadithi hii tu tunayoizungumzia. Basi utasema nini kuhusu mtu ambaye hakusimulia ila Riwaya moja? Jambo hili kwa hakika linajulisha kwamba mtu huyu hakuwa mpokeaji wa hadithi, na kwa msingi huu basi kumtegemea katika hadithi yake ni jambo lenye mushkili.

Ewe msomaji mpendwa, hii ndiyo Sanad ya hadithi ya Abul-Hayyaj; na umefahamu udhaifu wa wapokezi wake, na kwamba wanachuoni wa hadithi hawakuafiki ukweli wa wapokezi hao.

Basi iwapo hadithi itakuwa imezungukwa na matatizo kama haya mengi haitawezekana kwa faqihi yeyote kuitegemea hadithi hiyo kwa ajili ya kufahamu hukmu ya shari'ah au kutoa fatwa.

Ama utambulisho wa hadithi hii, hautaepukana na matatizo licha ya ile Sanad yenyewe, kwani ile nukta muhimu wanayoitolea ushahidi Mawahabi ni hii ifuatayo:

"Walaa qabran mush-rifan illa Sawwaitahu."

Hapa ni lazima kutulia na kufanya mazingatio na uchunguzi kwenye maneno mawili:

1) Mushrifan
2) Sawwaitahu.

1. Tamko Al-Mushrif maana yake ni kitu kuwa juu na chenye kunyanyuka.

Amesema katika Munjid: Al-Mushrif minal-amakin: Al-aali Wal-mutilu ala Ghairih.

Maana yake: Mahali Mush-rif, ni pale palipo juu na pamejitokeza kuliko mahali pengine.

Naye mwenye Al-Qamus ambaye ni mpangaji bora wa utaratibu wa maana za matamko amesema:
"Ash-Sharaf: Al-Uluwu, Waminal-Ibili Sanaamuhu."

Yaani Ash-Sharafu ni kuwa juu; na likitumika kwa ngamia maana yake ni nundu yake."

Kwa hiyo basi maana ya "Mushrif" ni kuwa kitu chenye muinuko (kutokeza); na hasa muinuko ulio katika umbile la nundu ya ngamia.

Basi hapa ni wajibu pamoja na kuzirejea dalili na Qarina, tufanye uchambuzi kuhusu nini lengo la neno "Al-Mushrif" lililoko katika hadithi tunaoizungumzia.

2. Tamko "Sawwaitahu" maana yake ni, kukifanya kitu kuwa sawa (kukisawazisha) na kurekebisha kiwe sawa sawa.

Sawwas-shaia: Maana yake amekifanya kiwe sawasawa; husemwa: Nimesawazisha kitu kilichopinda kikasawazika, (Nimekitengeneza sawasawa).

Katika Qur'an tukufu kuna aya isemayo "Al-ladhii Khalaqa Fasawwaa" (Aliyeumba Akasawazisha).Surah Al-A’alaa, aya ya 2.

Baada ya kuangalia maana ya maneno mawili tofuati, tunawajibika kufahamu nini makusudio ya maneno haya katika hadithi.

Kwa hakika hadithi hii ina mielekeo miwili, na ni lazima kuchagua mmojawapo kwa mujibu wa maana zitumikazo kwenye maneno haya pamoja na dalili nyingine.

Mwelekeo Wa Kwanza

Ni kwamba Imam Ali [a] alimuamuru Abul-Hayyaj kuyabomoa makaburi yaliyoinuliwa na kuyasawazisha kabisa na ardhi.

Lakini mwelekeo huu ambao ndio wanaoushikilia Mawahabi haukubaliki kutokana na sababu nyingi.

Ya Kwanza: Neno "At-Taswiyya" katika lugha ya Kiarabu halikuja kwa maana ya kubomoa; na lau makusudio yake hapa ingekuwa ni kubomoa basi ilitakiwa hadithi hiyo isemwe hivi: "Wala Qabran Illa Sawwaitahu bil ardhi" Yaani "Wala (usiache) kaburi ila ulisawazishe na ardhi". Lakini hadithi haikuja namna hiyo.

Ya Pili: Lau kama makusudio katika hadithi yangekuwa ni kubomoa, basi ni kwa nini hakutoa fatwa mwanachuoni ye yote wa Kiislamu kuyabomoa? Zaidi ya hapo ni kwamba, kulisawazisha kaburi na ardhi ni kinyume cha sunna ya Kiislamu na mapendekezo ya kisheria; kwani inapendekezwa na sheria kaburi linyanyake kuliko ardhi, na hii ndiyo fatwa waliyoitowa mafaqihi wote wa Kiislamu kwamba kaburi liinuke kutoka katika ardhi kiasi cha shibri moja.

Katika kitabu cha Al-Fiqhu Alal-Madhaahibil-arba'ah (Fiqhi kwa mujibu wa madhehebu manne) kuna maelezo yafuatayo:

"Ni Sunna kuinua udongo juu ya kaburi kiasi cha shibri moja."8

Basi itapokuwa muelekeo huu wa kwanza haukubaliki itakuwa ni lazima kuifasiri hadithi hii kwa kutumia muelekeo wa pili ufuatao.

Mweleko Wa Pili

Makusudio ya neno "Tas-wiyatul-Qabri" itakuwa ni kulisawazisha kaburi likawa sawa kwa sawa kinyume na makaburi ambayo hujengwa kwa umbile la samaki au nundu ya ngamia.

Kwa msingi huu hadithi itakuwa inakusudia kwamba, sehemu ya juu ya kaburi iwe imetandazwa sawa sawa, na haifai kuwa kama mgongo wa samaki au nundu ya ngamia, kama wafanyavyo baadhi ya Waislamu wa Madhehebu ya Kisunni. Maimamu wa Madhehebu ya Kisunni (isipokuwa Imam Shafi'i) wametoa fatwa kwamba inapendekezwa kulifanya kaburi kama nundu.9

Na kwa ajili hii basi hadithi hii inathibitisha ukweli wa fatwa ya wanachuoni wa Kishia na Kishafi'i ambao wanasema kwamba, "Inapasa kulisawazisha kaburi na kuliinua kuliko ardhi".

Muslim katika sahihi yake ameileta hadithi hii ya Abul-Hayyaj pamoja na hadithi nyingine (ambayo tutaitaja) kwenye Babul-Amri Bitas-wiyatil-Qabri, na vile vile At-Tirmidhi na An-Nasai katika Sunan zao wameileta hadithi hii kwenye hiyo hiyo Babul-Amri Bi Tas-Wiyatil-Qabri.

Na makusudio ya Babul-Amri Bitas-wiyatil-Qabri ni (kujulisha) kwamba kaburi linatakiwa liwe ni lenye kusawazishwa, na lau ingekuwa makusudio ni kulisawazisha na ardhi basi ingekuwa lazima kuuita mlango huu kuwa ni "Babul-Amri bi Takhiriibil Quburi Wahadmiha" yaani mlango wa kuharibu na kubomoa makaburi.

Manna tuliyoieleza juu ya neno Tas-wiyah lililo ndani ya hadithi ndiyo unayoweza kuikuta katika lugha ya Kiarabu, kwani neno Tas-wiyah linapotumika kwenye kitu kama kaburi, maana yake huwa ni kwamba, hilo kaburi lisawazishwe na siyo lilinganishwe na kitu kingine kama vile ardhi.

Hebu tuangalie hadithi nyingine aliyoitaja Imam Muslim katika Sahihi yake, hadithi ambayo inayo madhumuni yale yale tuliyoyateuwa:

"Kunnaa Maa Fadhaalah Ibn Ubaid Biardhir Ruum, Biraudasi, Fatuwufiyya Sahibun lana, Faamara Fadhaalah Ibn Ubaid Biqabrihi Fasuwwiya Thumma Qaala, Sami’tu Rasulallahi Ya'muru Bitas-wiyatiha."

Maana Yake: Tulikuwa pamoja na Fadhaalah ibn Ubaid huko Ruum (katika sehemu iitwayo) Raudas; basi mwenzetu (mmoja) akafishwa; na Fadhaalah ibn Ubaid akaamuru lichimbwe kaburi lake (kisha tulipokwisha mzika) akalisawazisha halafu akasema: Nilimsikia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu akiamuru kuyasawazisha makaburi.10

Kwa kifupi ufunguo wa kuifahamu hadithi hii umejificha katika tamko la "Sawwaitahu", na ndani yake mna uwezekano wa kupatikana maana tatu.

Pamoja na kuzifahamu dalili na Qarina hapana budi kuchagua maana moja tu. Maana hizo tatu ni hizi zifuatazo:

Ya Kwanza: Maana yake iwe ni kuyabomoa majengo yaliyojengwa juu ya kaburi.

Na maana hii ni batili kwa sababu makaburi yaliyokuwepo Madina zama hizo hayakuwa na maqubba au madharih.

Ya Pili: Iwe maana ya "Tas-wiyah" ni kulisawazisha kaburi na ardhi.

Maana hii pia haikubaliki kwa kuwa Sunna iliyothibiti ina amuru kuliinua kaburi kiasi cha shibri moja.

Ya Tatu: Maana yake iwe ni kulisawazisha kaburi na kurekebisha (likae sawa) na wala isiwe kuliinua kama ngongo wa samaki au nundu ya ngamia.

Na maana hii ndiyo maana inayokusudiwa. Kwa hiyo haina uhusiano na makusudio wanayoyatolea ushahidi Mawahabi.

Sasa hivi ndugu msomaji, hebu muangalie Al-Allamah An-nawawi ambaye ndiye aliyeandika Sharhi ya Sahihi Muslim na uone ni vipi alivyoisherehesha hadithi hiyo:

Anasema: "Innas-Sunnata Annal-Qabra la Yurfa'u Anil Ardhi Kathiran wala Yusannamu, bal Yurfau Nahwa Shibrin wayusattahu."11

Maana Yake: Iliyo sunna ni kwamba, kaburi lisiinuliwe (muinuko) mkubwa kutoka ardhini bali liinuliwe kiasi cha shibri lizawazishwe.

Katika ibara hii inadhihiri kwamba mshereheshaji wa Sahih Muslim amefahamu maana ile ile tuliyofahamu katika hadithi hii, kwamba Imam Ali [a] alimuusia Abul-Hayyaj kuyabadilisha makaburi yenye kunyanyaliwa mno au yale yenye maumbile kama mgongo wa samaki yasawazishwe na wala hakuamuru kuyasawazisha na ardhi.

Na sisi katika kutoa maana hii ndani ya hadithi hii hatuko peke yetu bali amesema pia Al-Hafiz Al-Asqalani katika kitabu chake Irshaad as-sraari fi sharhi Sahihil-Bukhari.

Baada ya yeye kutaja kwamba iliyo sunna katika kaburi ni kulisawazisha; na kwamba haifai kuiacha sunna hii eti tu kwa sababu kufanya hivyo imekuwa ni alama ya marafidhi (anakusudia Mashia) kwani hakuna upinzani baina ya kusawazisha kaburi na hadithi ya Abul-Hayaj. Al-Hafiz Al-Asqalani anasema kama ifuatavyo:

"....Ni kwamba (katika hadithi hiyo) hapakukusudiwa kusawazisha kaburi na ardhi bali alichokusudia ni kulisawazisha (yaani kuliweka sawa) na kwa hiyo tunakusanya maana za haadithi zote."

Baada ya yote haya lau ingekuwa maana ya wasia wa Imam Ali [a] kwa Abul-Hayyaaj ni kubomoa maqubba na majengo yaliyojengwa kwenye makaburi, basi ni kwa nini Imam [a] hakuamuru kuyabomoa maqubba ambayo yalikuwa kwenye makaburi ya Manabii katika zama zake?

Pamoja na kwamba inaeleweka kuwa yeye Imam Ali [a] alikuwa ndiyo mtawala wa nchi zote za Kiislamu na alikuwa akiyafahamu maqubba yaliyojengwa kwenye makaburi ya Manabii huko Palestina, Syria, Iraq, Misri, Iran na Yemen, (lakini hakuyabomoa).

Na tukiyafumbia macho maelezo yaliyotangulia hivi punde, na tukakadiria kwamba Imam Ali [a] alimuamuru Abul-Hayyaj kuyabomoa makaburi yaliyoinuliwa na ayasawazishe kabisa na ardhi, basi ndani ya hadithi hiyo hakuna kinachojulisha wajibu wa kubomoa majengo yaliyojengwa kwenye makaburi, kwa kuwa Imam Ali [a] alisema (iwapo tutakadiria kuwa hadithi hiyo imesihi):

"Wala Qabran illa Sawwaitahu" (wala kaburi ila ulisawazishe); na wala hakusema "wala Bina’an Wala Qubbatan Illa Sawwaitahuma" (yaani wala jengo wala quba isipokuwa uyabomoe). Kwa kuwa uchunguzi wetu katika maudhui haya hauhusu kaburi lenyewe, bali majengo yaliyojengwa juu ya kaburi, kwa kuwa majengo haya yaliyoko kwenye makaburi waumini huwa wanapata kivuli kwa ajili ya kusoma Qur'an, dua na kusali, basi je, katika sentensi hii (wala Qabran illa Sawwaitahu) kuna chochote kinachojulisha kuyabomoa majengo haya na kumbukumbu ambazo zinawasaidia wenye kuzuru makaburi hayo kufanya ibada na kuwakinga kutokana na joto au baridi?

Uwezekano Wa Maana Mbili Mwishoni

Mwisho wa uchunguzi kuna maana mbili nyingine hatuwezi kuepuka kuzitaja ili kukamilisha maudhui hayo.

Ya Kwanza: Ni kwamba hadithi hii (ya Abul-Hayyaj na nyinginezo zinazofanana) ni ishara ya yale yaliyokuwa yamezoweleka kwa baadhi ya nyumati zilizopita ikiwa ni pamoja na kuyafanya makaburi ya wachamungu kuwa ndiyo kibla chao wakayaelekea wakati wa ibada. Watu hao pia walikuwa wakiweka picha kwenye kaburi, kwa hiyo waliacha kuelekea kibla aliyowaamuru Mwenyezi Mungu wakati wa ibada na wakayaelekea makaburi hayo.

Na kwa maana hii basi, haiwezekani kwa hadithi hii kuwa na uhusiano wowote na makaburi ya Waislamu, na wala haijapata kuonekana kwa Muislamu yeyote kuyaelekea makaburi katika swala au kuyasujudia; isipokuwa mwenendo wa Waislamu ni kuswali jirani ya makaburi bila ya kuwa yenyewe ndiyo kibla chao, bali nyuso zao zinaelekea upande iliko Al-Kaaba, nao husimamisha swala na kusoma kitabu cha Mwenyezi Mungu huku wakiwa karibu ya makaburi.

Na kama Waislamu wanakwenda kuzuru makaburi ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu, na wakatumia huko muda mrefu kufanya ibada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu karibu na malazi hayo matukufu, basi si kwa jingine ila ni kwa sababu ya utukufu uliyopatikana kwenye ardhi hizo kwa kuwepo watu watukufu waliozikwa mahali hapo.
Jambo hili ufafanuzi wake utakuja baadaye.

Maana ya Pili: Ni kwamba, makusudio ya kauli ya Imam Ali [a] kwa Abul-Hayyaj aliposema: "Anlaa Tada'a Timthaalan Illa Tamastahu, Wala Qabran Mushrifan Illa Sawwaitahu", makusudio yake kusema "At-Timthal" ni mapicha na masanamu, na "Al-Qabr" ni makaburi ya washirikina ambayo yalikuwa yakienziwa na kuheshimiwa na wahusika.

Kwa kifupi ni kwamba hadithi ya Abul-Hayyaj haina uhusiano wowote kabisa na kujenga juu ya makaburi, isipokuwa inahusu makaburi yaliyoinuliwa mno (kama ilivyoelezwa hapo kabla) au makaburi ya washirikina na masanamu.

Maelezo yafuatayo tunataja fatwa ya Maimamu wa Madhehebu manne ya Kisunni kuhusu kujenga juu ya makaburi.

"Yukrahu An-yubnal-qabru Bibaytin au Qubatin au Madrasatin au Masjidin."12

Maana Yake: Ni karaha kulijengea kaburi katika nyumba au Qubbah au chuo au msikiti.

Basi maadamu Maimamu wa Madh-hebu nne za Kisunni wameafikiana kuwa ni karaha tu kuyajengea makaburi basi ni vipi Qadhi wa Najdi anathubutu kutoa fatwa ya uharamu wa kuyajengea?

"Kwa hakika huu ni uzushi."

Tena tunajua kwamba fatwa ya ukaraha wa kujenga juu ya makaburi haitegemei dalili sahihi yo yote, na hasa itapokuwa jengo hilo linamsaidia mwenye kuzuru hapo aweze kusimamisha mambo ya faradhi ya dini na kusoma Qur'an kwenye jengo hilo.

 • 1. (1) Sahih Muslim, juz. 3, Kitabul-Janaiz, uk. 612 (2) Sunan Tirmidhi, juz. 2. uk. 256, Babu Majaa fii taswiyatil-qubur. (3) Sunan an-nasaiy, juz. 4. uk. 88, Babu Taswiyatil-qubur.
 • 2. Tah-dhibut-Tah-dhib. juz. 11, uk. 125
 • 3. Tah-dhibut-Tah-dhib. juz. 11, uk. 130
 • 4. Tah-dhibut-Tah-dhib. juz. 4, uk. 145
 • 5. Tah-dhibut-Tah-dhib. juz. 2, uk. 179
 • 6. Sharh Nahjul-Balagha ya Ibn Abil Hadid, juz. 9, uk. 99
 • 7. (1) Majma'uz-zawa'id, ya Al-Haithami, Juz. 9 uk 133. (2) At-Tirmidhi katika Sahihi yake, Juz. 2 uk 301. Muslim, katika Sahihi yake, (Mlango wa Imani)
 • 8. Al-Fiqhu Alal-Madhaahibil-arba'ah, juz. 1, uk.420
 • 9. Al-Fiqhu Alal-Madhaahibil-arba'ah, juz. 1, uk. 420
 • 10. Sahihi Muslim, juz. 3 Kitabul Janaiz, uk. 61
 • 11. Sharhu Sahihi Muslim Lin-Nawai.
 • 12. Al-Fiqhu Alal Madhahibi-l-arba'a, juz. 1, uk. 421