read

Hadithi Tukufu Za Mtume [s]

Hadithi zinazojulisha kuwa kutawassal kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu kunafaa ni nyingi mno, na zinapatikana katika vitabu vya Historia na hadithi.

Katika maelezo yafuatayo tunataja sehemu yake tu:

Hadithi Ya Kwanza

Imepokewa toka kwa Uthman bin Hunaif kwamba amesema: "Mtu mmoja kipofu alikuja kwa Mtume [s] akasema:
"Niombee kwa Mwenyezi Mungu aniponye (upofu)."

Mtume akamwambia, "Ukipenda nitaomba na ukipenda uvumilie na ndiyo bora."

Yule mtu akamwambia Mtume: "Muombe Mwenyezi Mungu (aniponye)."

Basi Mtume [s] akamuamuru kipofu yule atawadhe vizuri na aswali rakaa mbili na aombe kwa kutumia Dua hii.

"Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba na ninaelekea kwako kupitia kwa Mtume wako Mtume wa Rehma, Ewe Muhammad hakika mimi naelekea kwa Mola wangu kupitia kwako katika haja yangu ili ikubaliwe, ewe Mwenyezi Mungu mfanye Muhammad kuwa muombezi wangu."

Ibn Hunaif anasema:"Basi Wallahi, tulikuwa hatujatawanyika tukiendelea kuzungumza mpaka aliingia kwetu kama kwamba hakuwa na ugonjwa (upofu)".

Maelezo Juu Ya Sanad Ya Hadithi Hii

Hakuna ubishi katika kusihi kwa Sanad ya hadithi hii, kwani hata huyo Imam wa Mawahabi "Ibn Taimiyyah" ameihesabu kuwa ni hadithi sahihi na akasema kuwa, makusudio ya "Abu Jaafar" jina linalopatikana katika Sanad ya Hadithi hi ni 'Abu Jaafar Al-Khatmi" na huyu Bwana ni mpokezi anayetegemewa. Imekuja katika Musnad ya Imam Ahmad (Abu Jaafar Al-Khatmi). Amma ndani ya Sunan Ibn Majah imekuja (Abu Jaafar) tu.

Mwandishi wa Kiwahabi katika zama hizi aitwaye Ar-Rifai ambaye wakati wote anajaribu kuzifanya dhaifu hadithi zinazohusu Tawassul anasema kuhusu hadithi hii tuliyoitaja hapo kabla:

"Hapana shaka kwamba hadithi hii ni sahihi na ni mashuhuri na imethibiti bila wasiwasi wala mashaka (kwamba) macho ya kipofu yule yalirudi (akawa anaona) kwa sababu ya Dua ya Mtume [s]."1

Na anasema tena: "Hadithi hii wameileta An-Nasai na Al-Baihaqi, At-Tabran na At-Tirmidhi na Al-Hakim wao wametaja "Allahumma Shaf-fihu Fihi" badala ya "Allahumma Shaf-fihu Fiy-ya."2

Mufti wa Makka Zaini Dahlan anasema: "Bukhari na Ibn Majah na Al-Hakim (ndani ya Mustadrak yake) pamoja na Jalalud-Dinis-Suyuti (katika Jaami' yake) wameitaja hadithi hii na Sanad zake ni sahihi.

Na sisi tunaitaja hadithi hii kutoka katika rejea zifuatazo:

1. Sunan Ibn Majah, Juzuu ya kwanza, uk. 441 ikiwa ni hadithi na. 1385, kimehakikiwa na Muhammad Fuad Abdul-Baqii, toleo la Dar-Ihyail-Kutubil-Arabiyya.

Naye Ibn Majah anaeleza kutoka kwa Abu Is-Haqa kwamba yeye amesema: "Hadithi hii ni sahihi."

Kisha akasema:
"Na ameipokea Tirmidhi katika kitabu "Abuwa-bul-ad-iyya" akasema, Hadithi hii ni ya kweli na ni sahihi gharib.

2. Musnad Ahmad bin Hanbal, Juzuu ya nne uk. 138, "kutoka kwa Athuman bin Hunaif" chapa ya "Maktabul-islami, Muasasah dari-Saadir/Beirut, na ameipokea hadithi hii kwa njia tatu.

3. Mustad-ra-kus-sahihain ya Al-Hakim An-Nishapuri, Juzuu ya kwanza, uk. 313, chapa ya Haidar-abad/India.

Amesema baada ya kuitaja hadithi hii: "Hadithi hii ni sahihi kwa sharti ya Bukhari na Muslim lakini hawakuiandika."

4. Al-Jamius-Saghiru cha As-Suyuti, uk. 59, kutoka kwa Tirmidhi na Al-Hakim.
5. Tal-khisul-Mustad-rak cha Adh-dhahabi-aliyefariki mwaka 748 A.H., kilichochapishwa katika Hashiya ya Al-Mustad-rak.

6. At-Tajul-Jamii, Juzuu ya kwanza, uk. 286, nacho ni kitabu kilichokusanya hadithi zilizomo katika sihahi tano isipokuwa sahih ya Ibn Majah.

Baada ya haya hakuna haja ya majadiliano kuhusu Sanad ya Hadithi hii au kuitia dosari.

Ama maelekezo yake na mafunzo yaliyomo, lau utamuonyesha hadithi hii mtu anayefahamu vyema lugha ya Kiarabu tena mwenye akili safi na akajiepusha na chuki za Kiwahabi na kuchanganya kwao mambo kuhusu tawassuli kisha umuulize: "Ni kitu gani Mtume [s] alimuamuru kipofu yule akifanye wakati akiomba dua ile?"

Kwa haraka tu jibu lake litakuwa: "Mtume [s] alimfundisha namna atakayo tawassal kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume wake Mtume wa Rehma na namna Mwenyezi Mungu atakavyokubali maombi yake."

Maana hii ndiyo inayofahamika moja kwa moja kutokana na maneno yaliyomo katika hadithi iliyotajwa.

Ndani ya maelezo yafuatayo tunaigawa hadithi hii katika mafungu ili kuongeza ufafanuzi.

Fungu La Kwanza

"Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi ninakuomba na ninaelekea kwako kupitia kwa Mtume wako."
Neno "Mtume wako" lina uhusiano na maneno mawili yaliyokuja kabla ya neno hili.
Maneno hayo ni: "Ninakuomba na ninaelekea kwako."

Kwa maneno yaliyo wazi tutasema kama ifuatavyo:
Kipofu yule anamuomba Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume [s] kama ambavyo anaelekea kwa Mwenyezi Mungu kwa kupitia heshima na utukufu wa Mtume [s] na wasila wake.

Kinachokusudiwa kwa neno "Mtume" siyo dua yake bali ni ile dhati yake tukufu. Ama anayesema kwamba neno dua limekadiriwa kabla ya neno Mtume na maana ya (As-aluka Binabiyyika) ni ninakuomba kwa dua ya Mtume wako, basi kusema hivyo ni madai bila ya dalili na ni kinyume cha maana iliyo dhahiri.

Na sababu ya madai hayo yaliyo kinyume na dalili ni kuwa, yeye haitakidi kutawassal kwa dhati ya Mtume [s] ndiyo maana akalazimika na akakadiria kusema kwamba neno dua hapa limekadiriwa ili tu kwa njia hii apate kuitakasa itikadi yake ya kupinga kutawassal kwa Mtume mwenyewe.

Fungu La Pili

"Muhammad Nabii wa Rehma."
Ili iweze kufahamika vyema kwamba makusudio katika Dua hiyo, ni kumuomba Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume na dhati yake na heshima yake, basi imekuja jumla baada ya neno "Mtume wako" isemayo "Muhammad Nabii wa Rehma", ili ifafanue lengo wazi wazi.

Fungu La Tatu

Sentensi isemayo "Ewe Muhammad, hakika mimi naelekea kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwako", inajulisha kwamba kipofu yule alimfanya Mtume mwenyewe kuwa ndiyo wasila wa maombi yake, siyo dua ya Mtume [s] yaani yeye alitawassal kwa dhati ya Mtume siyo kwa dua ya Mtume.

Fungu La Nne

Na aliposema: "Mfanye Muhammad awe muombezi wangu", alikuwa na maana ya kusema kuwa:
"Ewe Mola mfanye Muhammad [s] awe ndiye muombezi wangu na ukubali uombezi wake kwangu, katika haki yangu."

Ewe msomaji mpenzi bila shaka imekudhihirikia kwamba nukta muhimu katika dua yote ni dhati ya Mtume [s] na shakhsiyya yake tukufu, na katika dua hii hakuna utajo wa dua ya Mtume asilan. Na kila atayedai kuwa kipofu yule alitawassal kwa dua ya Mtume na wala hakutawassal kwa dhati ya Mtume wala shakhsiyya yake, huyu atakuwa amejifanya kutoyaelewa maneno ya hadithi hii yaliyo wazi na amejifanya kutoifahamu hadithi hii.

Nawe msomaji lau utaifanyia mazingatio kauli ya muombaji aliposema:
"Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba na ninaelekea kwako kupitia kwa Mtume wako, Mtume wa Rehma" na aliposema tena muombaji huyo:

"Ewe Muhammad hakika mimi naelekea kwa Mola wangu kupitia kwako", itakudhihirikia wazi wazi kwamba, lengo linalokusudiwa ni nafsi ya Mtume awe ndiyo wasila kupitishia maombi ya muombaji.

Na lau lengo ingekuwa ni dua ya Mtume ndiyo wasila ingelazimika kusema: "Ewe Mwenyezi Mungu nakuomba kwa (kupitia) dua ya Mtume."

Baada ya haya tuliyoyaeleza hivi punde hakuna mush-keli unaobakia miongoni mwa mush-keli aliyoitaja yule mwandishi wa Kiwahabi katika Kitabu kiitwacho "At-Tawassul Ilaaz HaqiqatitTawassul". Mush-keli hiyo tumeitaja pamoja na majibu yake ndani ya kitabu chetu kiitwacho "At-Tawassul" kuanzia ukurasa wa 147 mpaka 153 na unaweza kurejea ukaona.

Hadithi Ya Pili

Kutawassal Kwa Haki Ya Waombaji

Amepokea Atiya Al-aufi kutoka kwa Abu Said Al-Khudri kwamba Mtume [s] amesema: "Yeyote atakayetoka nyumbani mwake kwenda kuswali akasema: Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba kwa haki ya wanaokuomba, na ninakuomba kwa haki ya mwendo wangu huu kwani mimi sikutoka kwa maringo na majivuno, wala kujionyesha wala kutaka sifa, nimetoka kwa kuogopa ghadhabu zako na kutafuta radhi zako, basi ninakuomba unilinde kutokana na moto na unisamehe madhambi yangu, kwani hapana anayesamehe madhambi isipokuwa wewe.3

(Atakayesema hivi) Mwenyezi Mungu atamuelekea mtu huyo kwa dhati yake na watamtakia msamaha malaika sabini elfu."

Hadithi hii iko wazi mno katika maana yake na inajulisha kwamba mtu anayo ruhusa ya kutawassal kwa heshima ya Mawalii na daraja walizonazo na cheo chao mbele ya Mwenyezi Mungu. Basi na awafanye Mawalii hawa kuwa ndiyo wenye kukaa kati na kuwa waombezi, ili haja zake zikubaliwe na dua zake zipokelewe.

Hadithi Ya Tatu

Kutawassal Kwa Haki Ya Mtume Mtukufu [s]

Nabii Adam [a] yalipomtokea mambo ambayo ilivyokuwa ni bora yasimtokee, naye akarejea kwa Mwenyezi Mungu kutokana na hayo yaliyomtokea, alipokea maneno kutoka kwa Mola wake kama Qur'an Tukufu inavyoonyesha:

"Kisha Adam akapokea maneno kutoka kwa Mola wake, na Mola wake akakubali toba yake hakika yeye ni mwingi wa kupokea (toba) na ni mwingi wa huruma."4
Qur'an, 2:37

Wafasiri wa Qur'an na wataalam wa hadithi wamefafanua na kutoa rai zao na mtazamo wao kuhusu aya hii na maana yake, na wamefanya hivyo kutokana na kutegemea kwao baadhi ya hadithi ili kupata maana ya aya hii.

Yafuatayo ni maelezo ambayo ndani yake tutataja hadithi hizo ili tuone matokeo ambayo tunaweza kuyapata baada ya kuzitaja hizo hadithi.

At-Tabrani katika Al-muujamus-Saghir na Al-Hakim katika Mustadrak yake, na Abunuaim Al-Isfahani katika Hil-yatul Auliyai, Baidhawi naye katika Dalailun-nubuwwat, na Ibn Asakir Ad-Dimishqi katika Tarikh yake, As-Suyuti naye ndani ya Tafsirud-duril Manthur, Al-A'lusiy yeye katika Tafsiri Ruhul-maan wote hawa wametoa mapokezi kutoka kwa Umar bin Al-Khatab naye kutoka kwa Mtume [s] kwamba Mtume amesema:

"Wakati Adam alipokosea lile alilolikosea, alinyanyua kichwa chake juu akasema, Nakuomba (Ewe Mwenyezi Mungu) kwa haki ya Muhammad unisamehe, Mwenyezi Mungu akampelekea wahi Adam (akamwambia) huyu Muhammad ni nani? Adam akasema:

Limetukuka Jina Lako (Ewe Mwenyezi Mungu), wakati nilipokuwa nimeumbwa nilinyanyua kichwa changu, kuiangalia arshi yako, basi niliona maandishi (yasemayo) hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na Muhammad ni mjumbe wa Allah nikasema, bila shaka hapana kiumbe Mtukufu mbele yako kuliko yule ambaye umeliweka jina lake pamoja na jina lako, Mwenyezi Mungu akampelekea Adam wahi (akamwambia) huyo ndiyo Nabii wa mwisho katika kizazi chako, na lau si yeye nisingekuumba wewe."5

Akinakili toka kwa At-Tabrani na Abunuaim na Al-Bayhaqi na matni ya hadithi imenakiliwa kutoka kwa Ad-durul-Manthoor.

Maoni Yetu Juu Ya Hadithi Hii

Kinyume cha mazowea tuliyonayo kuwatambulisha watu hao au nafsi hizo. Qur'an inazungumzia nafsi au watu kwa kutumia neno "Al-Kalimah" kinyume cha matumizi yetu ya kawaida kuhusu neno hili.
Kwa mfano Mwenyezi Mungu anasema:

(a) "Mwenyezi Mungu anakupa bishara njema ya Yahya mwenye kumsadikisha neno atokaye kwa Mwenyezi Mungu.” Qur'an, 3:39.

(b) Kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Ewe Mariam, Mwenyezi Mungu anakupa bishara njema ya neno atokaye kwake jina lake ni Masih Isa mwana wa Mariam." Qur'an, 3:45.

(c) "Hakika Masih Isa mwana wa Mariam ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu na ni neno lake." Qur'an, 4:171.

(d) Kauli ya Mwenyezi Mungu:

"Waambie lau kama bahari ingekuwa ndiyo wino kwa (kuandikia) maneno ya Mola wangu, basi bahari ingekwisha." Qur'an, 18:109.

(e) Kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

"Na bahari hii (ikafanywa wino) na bahari nyingine saba (zikaongezwa), maneno ya Mwenyezi Mungu yasingelikwisha." Qur'an, 31:27.

Tukiziangalia aya hizi inawezekana kabisa kusema kwamba:

Makusudio ya "Kalimaat" yaani katika ile aya isemayo "Akapokea Adam kutoka kwa Mola wake maneno" makusudio yake ni dhati tukufu yenye heshima ambayo kwayo Nabii Adam alitawassal kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Na katika hadithi iliyotangulia utaliona jina la Muhammad [s] tu ndiyo lililotajwa.

Ama katika hadithi zilizoko katika madheheb ya haki (Shia) utaona hadithi hii imepokewa kwa sura inayokubaliana na aya tukufu ya Qur'an, pia utaikuta imepokewa kwa namna mbili.

Wakati mwingine neno "Kalimaat" limefasiriwa kwa maana ya majina ya watukufu watano [a], na wakati mwingine limefasiriwa kwa sura zao zenye nuru.

Hebu itazame hadithi ifuatayo: "Hakika Adam aliona kwenye arshi pameandikwa majina matukufu yenye heshima akauliza, majina hayo (ni ya kina nani)? Akaambiwa, haya ni majina ya viumbe watukufu mno kwa daraja mbele ya Mwenyezi Mungu, kuliko viumbe wote na majina hayo ni, Muhammad, Ali, Fatma, Hasan na Husein. Basi Adam [a] akatawas-sal kwa Mola wake kupitia kwao ili kukubaliwa toba yake na kunyanyuliwa daraja yake.6 Na baadhi ya hadithi zinajulisha kwamba Adam [a] aliona Sura za nuru za watukufu watano, basi akatawassal kwazo baada ya kuziona. (Kwa ufafanuzi zaidi tazama Tafsir AI-Burhan, juz. 1, uk. 87, Hadith na 13, 15, na 16.)

2. Na tunaporejea vitabu vya historia na hadithi inatudhihirikia kwamba, Qadhiya ya Adam kutawassal kwa Mtume Muhammad [s] lilikuwa ni jambo mashuhuri miongoni mwa watu, ndiyo maana utamkuta Imam Malik bin Anas (Imam wa Madhehebu ya Malik) anasema kumwambia Mansur Ad-Dawaniq katika Msikiti wa Mtume [s] : "Mtume ni wasila wako na ni wasila wa Baba yako Adam."

Nao washairi wa Kiislamu wameuonyesha ukweli huu katika mashairi yao.
Mmoja wa washairi hao anasema: "Kwa Mtume [s] Mwenyezi Mungu alikubali maombi ya Adam na aliokolewa Nuhu ndani ya Safina."7

Mwingine naye anasema: Ni watu ambao kwao lilisameheka kosa la Adam, nao ndiyo wasila na nyota zing'aazo.8

Hadithi Ya Nne

Mtume Kutawassal Kwa Haki Yake Na Haki Ya Manabii Waliomtangulia

"Alipofariki Bibi Fatma binti Asad, Mtume aliingia mahala alipofia Mama huyo, akakaa upande wa kichwa chake akasema:

"Mwenyezi Mungu akurehemu ewe mama yangu baada ya mama yangu. Kisha Mtume akamwita Usama bin Zaid, na Abu Ayyubul-Ansari na Omar bin Al-Khattab na kijana fulani mweusi ili wakachimbe kaburi.

Wakachimba kaburi hilo, na walipofikia kuchimba mwanandani, Mtume [s] akaichimba mwanandani hiyo yeye mwenyewe kwa mkono wake na kuutoa mchanga. Alipomaliza, akaingia kwenye mwanadani kisha akalala ndani yake na akasema:
"Mwenyezi Mungu ndiye anayehuisha na kufisha, na yeye yu hai wala hatokufa. Ewe Mwenyezi Mungu msamehe mama yangu Fatma binti Asad na uyapanue makazi yake kwa haki ya Mtume wako na Manabii ambao wamepita kabla yangu." Mtungaji wa kitabu kiitwacho "Khulasatul-kalam" amesema:

Hadithi hii imepokewa na, Tabrani katika kitabu kiitwacho, Almuujamul-Kabir na Almuujamul-Ausat, na ameipokea Ibn Hiban na Al-Hakim na wamesema kuwa ni hadithi sahihi.9

Naye Sayyid Ahmad Zaini Dah-lan ameandika katika kitabu kiitwacho "Ad-Durarus-Saniyya Fiir-radd Alal-Wahabiyya" kama ifuatavyo:

"Amepokea Ibn Abi Shaiba kutoka kwa Jabir (kama tulivyoitaja hadithi hii, na vile vile ameipokea hivyo hivyo Abdul-Bari kutoka kwa lbn Abbas, na ameipokea Abu Nuaim katika kitabu "Hil-yatul-Auliyai" kutoka kwa Anas, na yote haya ameyataja Alhafidh Jalalud-dinis-Suyuti katika kitabu "Al-jamiul-Kabir"10

Ama sisi tumetaja hadithi hii kutoka kwenye rejea mbili, moja inaambatana na maudhui haya tunayozungumzia ambayo yanahusu dua, na ya pili haihusiani na maudhui haya.

Rejea hizo ni:
(1) Hil-yatul-Auliyai ya Abu Nuaim Al-Isfahani, juzuu ya tatu, uk. 121.
(2) Wafaul Wafa ya As-Samhudi, juzuu ya tatu, uk. 899.

Haditihi Ya Tano

Kutawassal Kwa Mtume Mwenyewe

Wanachuoni wengi wa hadithi wamepokea kwamba, bedui mmoja aliingia kwa Mtume [s] akasema: Kwa hakika tumekujia hali ya kuwa wanyama na wanaadamu wote hawana hata sauti kwa ajili ya njaa."

Kisha akasema Ushairi huu:

"Tumekujia (Ewe Mtume) hali ya kuwa maziwa ya mwanamke kijana yanatoka damu (badala ya maziwa, kwa sababu ya njaa) na kwa hakika mama mwenye mtoto naye hamjali mwanawe na hatuna chochote kinacholiwa na watu isipokuwa hanzal (matunda machungu) na Il-hizi 11. Na wala hatuna pengine pa kukimbilia isipokuwa kwako. Basi watu wakimbilie wapi? Hakuna, isipokuwa waende kwa Mtume."

Basi Mtume [s] alisimama huku nguo zake zinakokota chini mpaka akapanda kwenye Mimbar na kunyanyua mikono yake akasema, ewe Mwenyezi Mungu tupe mvua nyingi kabla Mtume hajateremsha mikono yake, basi mbingu ilinyesha mvua, kisha Mtume akasema: "Mwenyezi Mungu amlishe Abu Talib huko peponi. Lau angekuwa hai angelifurahi sana basi nani atatusomea maneno yake?"

Akasimama Ali bin Abi Talib [a] akasema, ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu kama kwamba unakusudia maneno yake haya yafuatayo:

"Na mwenye nuru ambaye huombwa mvua kwa uso wake yeye ndiye tegemeo la mayatima na yeye ndiyo mlinzi wa wajane. Wanamzunguka wenye matatizo miongoni mwa kizazi cha Hashim, basi kwake yeye wao wanapata neema nyingi na raha."

Mtume [s] akasema "Naam".

Imam Ali [a] alisoma beti nyingi za Qasida ile na huku Mtume anamuombea Magh-fira Abu Talib hali yeye akiwa kasimama kwenye Mimbar.

Baadaye mtu mmoja miongoni mwa Bani Kinanah akawa anasoma Qasida akasema, "(Ewe Mwenyezi Mungu) unastahiki shukurani, na shukurani hizi zatoka kwa mwenye kushukuru. Kwa hakika tumepata mvua kupitia kwenye uso wa Mtume mwenyewe."

Mimi nasema, "Rejea zilizotaja Qadhiya hii ni nyingi mno, nasi tumeitaja Qadhiya hii kutokana na rejea zifuatazo:

(1) Umdatul-qarii fii shar-hil Bukhari, juzuu ya saba, uk. 31 utunzi wa Badru-din Mahmud bin Ahmad Al-ain aliyefariki mwaka 855 A.H, chapa ya Idaratut-Taba-atil-Muniriyya.

(2) Shar-hu Nah-jul-Balaghah cha Ibn Abil-Hadid, juz. 14, uk. 80.

(3) As-siratul-Halabiyya, juz. ya 3, uk 263.

(4) Al-hujat Ala dhahib ila tak-fiiri Abi-Talib, utunzi wa Shamsuddin Abi Ali Fakhar bin Maad aliyefariki mwaka 630, chapa ya Najaf katika Maktaba ya Alawiyya, uk 79.

(5) Siratu Zaini Dah-lan, kilichochapishwa katika Hamish Sirat Al-halab-iyyah, juzuu 1, uk. 81.

Hadithi Ya Sita

Vile Vile Inahusu Kutawassal Kwa Mtume

Imepokewa kwamba, Sawad bin Qarib alimsomea Mtume [s] Qasida yake ambayo ndani yake alitawassal kwake Mtume [s] akasema: "Nashuhudia kwamba hapana Mola isipokuwa Allah, na kwamba wewe ndiwe mwenye kuaminiwa kuhusu mambo ya kila asiyekuwepo. Nawe ndiye uliye karibu mno kama wasila kwa Mwenyezi Mungu kuliko Mitume wengine ewe mwana wa watukufu walio wema. Tuamrishe (tutende) yale yanayokufikia ewe mbora wa Mitume, japo yatakuwa mazito, na uwe muombezi wangu siku ambayo maombezi yeyote hatamnufaisha Sawad bin Qarib japo kwa sehemu ndogo.12

Ewe msomaji mpenzi, mpaka sasa tumetaja kiasi cha kutosha cha hadithi zilizopokelewa kuhusu Tawassul, na tumetegemea vitabu vya hadithi na historia vya Kisunni.

Ama kutawassal kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa mapokezi ya watu wa nyumba ya Mtume [s] katika vitabu vya kishia jambo hili liko wazi mno na limethibiti barabara kiasi ambacho limekuja kwa njia ya dua vile vile.
Sote tunawajibika kujiuliza:
"Je tunalazimika kuchukua maarifa ya Kiislamu na hukumu za sheria kutoka kwa "Ibn Taimiyyah" na "Muhammad Ibn Abdul Wahab" na wengineo mfano wa watu kama hawa, au tuchukue maarifa ya Kiislamu na hukumu za sheria toka kwa watu wa kizazi cha Mtume [s] ambao Mtume amewataja katika hadithi "Thaqalain" (vizito viwili) kwamba wao ndio kile kizito kidogo cha pili na kwamba wao ni sawa na Qur'an?

Kwa hakika kila Muislamu mwenye akili safi ataamua na kuona ulazima wa kuchukua mafunzo hayo toka kwa watu wa kizazi cha Mtume [s] ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na kuwatakasa mno.

Mifano Ya Dua Za Tawassul

Ama dua ambazo zimekuja na ndani yake kuna kutawassal kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, na zimetapakaa katika Sahifatul-Alawiyyah13, na dua ya Arafah14, na Sahifatus-Sajjadiyyah15 na vitabu vinginevyo ni nyingi mno, tunataja mifano ya dua hizo kama ifuatavyo:

1. Imam Ali [a] katika dua yake anasema:
Kwa haki ya Muhammad na Aali Muhammad iliyo juu yako, (Ewe Mwenyezi Mungu) na kwa haki yako tukufu juu yao (nakuomba) uwape rehma kwa sababu wewe ndiwe unayestahiki na unipe mimi kilicho bora mno ya vile ulivyowapa waombaji miongoni mwa waja wako waliopita katika waumini na unipe kilicho bora mno ya vile utakavyowapa waja wako waliosalia miongoni mwa waumini.

2. Na anasema bwana wa mashahidi Al-Imam Husein bin Ali [a] katika dua yake ya Arafah:
"Ewe Mwenyezi Mungu tunaelekea kwako jioni hii ambayo umeifaradhisha na kuitukuza kwa haki ya Muhammad Mtume wako, mjumbe wako na mteule wako katika viumbe vyako."

Na anasema Al-Imam Zaynul-Abidiina katika dua yake inayohusu kuandama kwa Mwezi wa Ramadhan:

"Ewe Mwenyezi Mungu nakuomba kwa haki ya Mwezi huu na kwa haki ya wale wataofanya Ibada ndani yake tangu mwanzo hadi mwisho, miongoni mwa Malaika uliyemkurubisha au Nabii uliyemtuma, an mja mwema uliyempenda."16

 • 1. At-Tawassul Ilaa Haqiqatit-Tawassul, uk. 158
 • 2. At-Tawassul Ilaa Haqiqatit-Tawassul, uk. 158.
 • 3. Sunan Ibn Majah, juz. 1, uk. 256. Hadith namba 778
 • 4. 4. Maelezo: Imethibiti kwamba, lile katazo lililoko katika kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: 'Msiukurubie mti huu" ni katazo la kutoa muongozo na siyo katazo la kuharamisha litokalo kwa Mola. Na katazo la muongozo liko katika mahala pa nasaha na mawaidha, na kulikhalifu katazo hili hakuwajibishi adhabu, wala haliondoshi isma kwa namna yoyote ile. Basi huwajibisha Taathira kwenye dhati ya kitendo, k.m., Lau tabibu atamkataza mgonjwa wa mafua kutumia vitu vichachu, kisha mgonjwa akakhalifu, basi tendo lake la kukhalifu litaakisi athari ya kimaumbile ambayo ni kuzidi kwa mafua na ugonjwa.
  Na ndani ya Qur'an Tukufu ziko aya nyingi zinazojulisha kwamba, katazo alilokatazwa Adam kuukurubia mti ule lilikuwa ni katazo la kutoa muongozo na hapana athari kwa kukhalifu katazo hili isipokuwa ni matokeo ya kimaumbile kwa kukhalifu huko. Unaweza kurejea aya ya 118 na 119 katika Surah Taha.
 • 5. (1) Mustadrakus-Sahihain, juz. 2, uk. 615. (2) Ruhul-Maani, juz. 1, uk. 217. (3) Ad-durul-Manthoor, juz. 1, uk. 59.
 • 6. (1) Maj-maul-bayan Juz. 1 uk 89 Chapa ya Lebanon (2) Tafsirul-bur-han Juz. 1, uk 86-88 hadithi namba 2, 5, 11, 12, 14 na 27.
 • 7. Kashful-irtiyab, uk. 307. Ameinakili kutoka katika Mawahib, na shairi hili ni la Ibn Jabir.
 • 8. Kashful-irtiyab, uk. 308. Na Shairi hili ni la Al-wasiti.
 • 9. Kashful-irtijab, uk. 312 amenakili toka Khulasatul-kalaam.
 • 10. Ad-durarus-Saniyya,uk. 8
 • 11. Il-hizi ni kitu walichokuwa wakikitumia katika miaka ya njaa na kilikuwa kikitengenezwa kutokana na mchanganyiko wa damu na manyoya ya ngamia kisha hukikaanga kwa moto na kukila. Taz: Annihayah fi Gharibi-lhadith cha Ibn Athir al-Jazari chapa ya Beirut, juz. 3, uk 293.
 • 12. Ad-duraru Saiyyah, uk. 27 utunzi wa Zaini Dah-lan, At-tawassul Ilahaqiqati-tawassul, uk 300.
 • 13. Ni mkusanyiko unaokusanuya baadhi ya dua za Imam Ali, Amirul-Muuminina [a] alizikusanya Sheikh Abdulla As-Samahiji.
 • 14. Ni dua ya Imam Husein [a] katika Arafaat siku ya Arafah.
 • 15. Ni baadhi ya dua za Imam Zaynul Abidiina.
 • 16. Sahifatus-Sajjadiyah dua namba 44.