Table of Contents

Khitamuhu Misk

Ewe msomaji mpendwa, sasa hivi umefika wakati wakuhitimisha uchambuzi huu mpana kuhusu itikadi za Kiwahabi na misingi yake na malengo yake kwa neno fupi lenye manufaa kwa jamii ya Kiislamu kwa jumla, na kwa vijana wa Kiislamu wenye ghera kwa upande wao.

Bila shaka Uislamu umejengwa juu ya maneno mawili:

Kalimatul-Tauhid na Tauhid-ul-Kalimah, basi ni wajibu juu ya umma wa Kiislamu kuulinda umoja wa kalima na mshikamano wa udugu, kama ambavyo ni wajibu juu ya umma kuihifadhi Kalimatul-Tauhid kwani viwili hivyo ni matawi mawili yanayotokana na asili moja.

Basi kama ambavyo Qur'an na Sunna vimehimiza juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu kwa dhati na kwa vitendo na ibada, basi ndivyo hivyo hivyo vimehimiza kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu na vimekemea mafarakano: "Shikamaneni katika kamba ya Mwenyezi Mungu na wala musifarakane." Qur'an, 3:103.

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na atakayemuasi Mtume baada ya kumdhihirikia uongofu na akafuata njia ya wasiokuwa waumini, tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza ndani ya Jahannam na hayo ni marejeo mabaya." Qur'an, 4:115.

Na amesema Imam Ali [a] "Basi shikamaneni na Jamaa kubwa kwani mkono (msaada) wa Mwenyezi Mungu uko pamoja na wengi na Ole wenu na mafarakano kwani hakika wenye kukhalifu miongoni mwa watu ni (kundi la) shetani kama ambavyo wenye kujitenga miongoni mwa kondoo ni kwa ajili ya mbwa mwitu, basi fahamuni ya kwamba mwenye kulingania kwenye utengano huu muueni japokuwa atakuwa chini ya kilemba changu hiki." 1

Basi iwapo Tauhidul-Kalimah iko katika daraja hii ya juu, basi itakuwaje hali ya mtu anayevunja mshikamano wa Waislamu na kueneza ndani yao utengano na kubomoa umoja wao na kuyavuruga maafikiano yao kwa kupandikiza mbegu ya mashaka ndani ya mambo ambayo umma wa Kiislamu ulikuwa ukiafikiana kabla (hata) ya kuzaliwa (huyu) aliyepandikiza mashaka yaani Ibn Taymiyyah na aliyeimwagilia mbegu hiyo yaani Ibn Abdul-Wahab.

Ewe msomaji mpendwa: Kwa hakika yote tuliyokueleza ndani ya kurasa hizi ni kwa mujibu wa Qur'an Tukufu na Sunna ya Mtume Mtukufu [s] na ni matokeo ya kile ambacho umma wa Kiislamu umekubaliana kwa karne zote. Basi lina thamani gani neno au maneno yanayopinga kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake [s] na kile ambacho umma umekubaliana?

Ni jambo zito kwa umma wa Kiislamu ukiongozwa na Wanachuoni wake na wanafikia wake kupatikana ndani ya Makka na mahala paliposhuka wahyi watu wanaoukufurisha umma wote wa Kisunni na Kishia na wala hawamvui miongoni mwao isipokuwa watu wachache toka miji ya Najd.

Na kwa hakika wakubwa watukufu wa umma wa Kiislamu walikwisha hadharisha hatari ya msimamo huo na madhara ya fikra za kishetani ambazo alizipandikiza Sheikh Ibn Taymiyyah mpaka Al-Hafidh Ibn Hajar amesema ndani ya kitabu chake kiitwacho, "Al-Fatawa Al-Hadithiyyah" kumuhusu Ibn Taymiyyah kama ifuatavyo:

"Ibn Taymiyyah ni mja ambaye Mwenyezi Mungu amemdhalilisha na amemuacha apotee na akampofua na kumfanya kiziwi; na wameyabainisha mambo haya yakawa wazi Maimamu ambao walieleza ufisadi wa hali yake na uongo wa kauli zake;
na mwenye kutaka (kujua) ni juu yake kutalii (kusoma) maneno ya Imam Al-Muj-tahid Abul-Hasan As-Subaki ambaye Uimamu wake na utukufu wake na kufikia kwake daraja ya Ij-tihadi kumekubaliwa na wote na pia asome maneno ya mwanawe (aliyekuwa akiitwa) At-Taaj na Sheikh Al-Imam Al-Izz miongoni mwa jamaa na watu wa zama zao miongoni mwa Mashafii na Malik na Mahanafii; na huyu Ibn Taymiyyah hakuishia kuwapinga Masufi wa zama zake bali amewataaradhi watu kama vile Umar Ibn Khataab na Ali Ibn Abi Talib r.a.
Kilichopo ni kwamba maneno yake hayana maana na ni yakutupwa njiani.
Na inaitakidiwa kwamba yeye ni mzushi mpotovu mwenye kupotosha amevuka mpaka, Mwenyezi Mungu amlipe kwa mujibu wa uadilifu wake."2

Na tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie "Miongoni mwa wenye kusikiliza maneno na wakafuata mema yake."

Rehma na Amani Zimshukie Bwana wetu Muhammad Mwisho wa Mitume na Aali Zake wema waliotakasika na Sahaba Zake Wema Watukufu.

Na Maombi yetu ya mwisho ni kuwa kila sifa njema zinamstahaki Mwenyezi Mungu Mola wa Walimwengu.

Ja'afar Subhani
Qum Takatifu,
Siku ya Idi ya Ghadir,
18 Mfunguo Tatu 1406.

  • 1. Nahjul-Balagha Khutba Na. 123.
  • 2. Al-Fatawa Al-Hadithiyyah, uk. 86.