read

Kujenga Msikiti Karibu Na Makaburi Matakatifu

Je, kujenga msikiti kwenye makaburi ya watu wema au karibu yake kunajuzu au hakujuzu?

Na kama inajuzu basi nini maana ya hadithi iliyopokewa kwamba "Mtume [s] amewalaani Wayahudi na Wakristo kwa kuwa wao waliyafanya makaburi ya Manabii kuwa mahala pa ibada."

Je, matokeo ya kujenga msikiti karibu ya makaburi ya Mawalii hakuwezi kuambatana na laana iliyokuja katika hadithi hii?
Jawabu: Kwa hakika kujenga msikiti karibu na makaburi ya watu wema hakuna kizuizi kabisa, kwani jambo hili limo ndani ya misingi ya Kiislamu ya jumla inayoruhusu mambo kama haya.

Hali hiyo ni kwa sababu lengo la kujenga misikiti katika sehemu hizo ni kumwabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu karibu na makazi ya mmoja wa vipenzi vyake na Mawalii wake wema ambao kwa kuzikwa kwao hapo wameifanya ardhi ya mahali hapo kupata baraka na utukufu.

Na kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, lengo la kujenga misikiti katika sehemu hizo ni kuhamasisha utekelezaji wa faradhi za kisheria na ibada mbali mbali kabla ya kuzuru kaburi lililopo hapo au baada ya kulizuru.

Kimsingi, kuzuru makaburi siyo haramu hata kwa hao Mawahabi, na hivyo hivyo kusimamisha sala kabla ya ziyara au baada yake. Basi kauli ya kuharamisha kujenga msikiti karibu ya makaburi ya watu wema, ili kumwabudu Mwenyezi Mungu na kutenda faradhi zake, haina maana yoyote.

Mazingatio yanayopatikana katika kisa cha As-habul-Kahfi yanatudhihirishia kwamba kujenga msikiti karibu ya makaburi ni Sunna iliyokuwa ikifuatwa na watu wa nyumati na sheria zilizopita.

Nayo Qur'an tukufu inaiashiria Sunna hiyo bila ya kuikosa wala kuipinga.

Hapo kabla yametangulia maelezo kuhusu As-habul-Kahfi, wakati habari zao zilipojulikana baada ya kupita miaka 309, na watu walihitilafiana ni heshima na takrima ya aina gani waliyostahiki kufanyiwa hao As-habul-Kahf. Basi watu wakagawanyika makundi mawili.

1 Kundi moja wakasema, "wajengeeni jengo" ili kudumisha utajo wao.

2. Na kundi la pili ambalo ndilo lililopata ushindi lilitaka ujengwe msikiti kwenye pango hilo ili mahala hapo pawe ni kituo kwa ajili ya ibada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, karibu na makaburi ya watu ambao walikataa kumwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu na wakatoka katika nchi yao wakikimbia ukafiri na kwenda kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtii.

Wameafikiana wafasiri wa Qur'an ya kuwa rai ya kwanza kuhusu hawa As-habul-Kahfi ilikuwa ni ya washirikina, wakati ile ya pili ilikuwa ni rai ya waumini.1

Na kwa rai hii ya pili Qur'an tukufu inasema: "Wakasema wale walioshinda kwenye jambo lao, tutawajengea msikiti juu yao."

Na yamekuja maelezo katika historia kwamba kutokeza na kujulikana habari zao kulikuwa ni katika wakati wa ushindi wa Tauhidi dhidi ya shirki, na viongozi wa ushirikina waliokuwa wakihimiza ibada ya masanamu katika zama hizo walikuwa wameshindwa, basi rai ya kujenga msikiti ilitokana na wanaomuamini Mwenyezi Mungu na kumpwekesha.

Basi kama itakuwa kujenga msikiti kwenye makaburi ya watu wema au karibu yake ni alama ya ushirikina, basi ni kwa nini rai hii ilitokana na waumini?

Na ni kwa nini Qur'an imetaja rai yao hii bila ya kuikosoa wala kuipinga? Je, hiyo siyo dalili kwamba jambo hilo linajuzu kufanywa?

Na haiwezekani kabisa kwa Mwenyezi Mungu kuyataja maneno ya washirikina kisha akapita tu bila kukemea na kukosoa kwa jumla au kwa ufafanuzi.

Hakika huku ni kukiri kwa Qur'an juu ya kusihi kwa rai ya waumini, na iwe iwavyo ni kwamba kukiri kwa Qur'an ni hoja ya kisheria kama ilivyothibiti katika elimu ya Usulul-fiqh (Misingi ya Sheria ya Dini).

Hali hii inatuonyesha kwamba mwendo wa waumini wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika ulimwengu wote ulikuwa ukitenda jambo hili na lilikuwa likizingatiwa kuwa ni moja ya namna ya kuheshimu mwenye kaburi na kutaka baraka kwake.

Ilikuwa ni bora kwa Mawahabi kuyalinganisha (kuyapima) mas'ala haya kwenye Qur'an kwanza, kisha watafiti huku na huko katika hadithi tukufu.

Katika maelezo yafuatayo tutataja mategemeo ya Mawahabi katika kukataza kwao jambo hili, ili tuonyeshe udhaifu wa mashiko hayo na ubatili wake:

Dalili Za Mawahabi Katika Kuharamisha Kujenga Misikiti Karibu Ya Makaburi Ya Watu Wema

Mawahabi wametegemea hadithi nyingi katika kuharamisha kujenga msikiti kwenye makaburi ya watu wema. Hapa tunataja hadithi hizo pamoja na kuzijadili na kuzitafiti:

Bukhari katika Sahihi yake ametaja hadithi mbili kwenye "Babu Karahatit-Tikhadhil-Masajid Alal-Qubuur".

1. Alipokufa Al-Hasan ibn Al-Hasan ibn Ali, mkewe aliweka Qubbah juu ya kaburi lake, likadumu kwa mwaka mmoja kisha likaondolewa, kisha walisikia sauti ikisema, "Je, wamekipata walichokuwa wamekikosa?" Mwingine akajibu, "Hapana, isipokuwa wamekata tamaa wakarudi."

2. "Mwenyezi Mungu amewalaani Mayahudi na Wakristo, waliyafanya makaburi ya Mitume yao kuwa ni misikiti." Bibi Aisha amesema: "Lau si hivyo, basi wangelidhihirisha kaburi lake (Mtume), lakini mimi ninahofu watalifanya kuwa msikiti."2

Muslim naye ameitaja hadithi hii pamoja na kuwa kuna tofauti ndogo, na ametaja vile vile ibara ifuatayo:

".......Fahamuni kwamba, waliopita kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Mitume yao na watu wema kuwa misikiti; basi msiyafanye makaburi kuwa ni misikiti, hakika mimi nakukatazeni jambo hilo."3

4. Hakika Ummu Habiba na Ummu Salama walilitaja Kanisa moja waliloliona huko Ethiopia ndani yake mna picha za Wajumbe wa Mwenyezi Mungu. Basi Mjumbe wa Mwenyezi Mungu akasema:
"Watu hao walikuwa kama kuna mtu mwema miongoni mwao akifa hujenga juu ya kaburi lake msikiti na wakachora humo picha hizo; basi hao ni viumbe waovu mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama."4

Naye An-Nasai anasimulia katika kitabu chake Sunan (Babut-Taghliz Fit-Tikhadhis-Surji Alal Qubur):

5. Imepokewa toka kwa Ibn Abbas: "Mtume amewalaani wanawake wanaozuru makaburi na wanaoyafanya kuwa misikiti na kuyawashia taa."5

Na utamuona Ibn Taimiyyah ambaye anaitakidiwa kuwa ndiyo mwanzilishi wa itikadi hii potofu, na Muhammad ibn Abdil-Wahhab ambaye anakula makombo ya Ibn Taimiyyah anazitegemea hadithi hizi kuharamisha kujenga msikiti juu ya makaburi ya watu wema au karibu yake.

Amesema Ibn Taimiyyah: "Wanachuoni wetu wanasema: Haijuzu kujenga msikiti juu ya makaburi."6

Kuzihakiki Maana Za Hadithi Hizi

Sasa hivi ni lazima kuzihakiki na kuzifanyia mazingatio hadithi hizi, ili tufahamu usahihi wa maana zinazozijulisha.

Kabla ya kufanya kitu chochote ni lazima tujue kama asili ya jumla kwamba, kama ilivyo aya ya Qur'an kufasiriwa na aya nyingine, basi ndivyo ilivyo katika hadithi moja kuifasiri nyingine, na kuiweka wazi kutokana na utatanishi.

Mawahabi wameshikilia dhahiri ya hadithi moja na wakatoa uharamu wa kujenga msikiti juu ya makaburi ya watu wema au karibu yake, wakati ambapo lau wangezikusanya (hadithi) mahala pamoja na kuzichambua wangefahamu alichokikusudia Mtume [s].

Mawahabi hawa, wamejifungia wenyewe mlango wa Ijtihadi, kitu ambacho kimewafanya wazifasiri hadithi nyingi kwa tafsiri ya makosa.

Mimi nasema:
Hadithi walizozishikilia Mawahabi kuharamisha kujenga Msikiti juu ya kaburi, zitakubalika tu iwapo Sanad zake zitakuwa sahihi na wapokezi wake watakapokuwa waaminifu. Kinyume cha hali hii, hadithi hizo hazitafaa kutolea ushahidi kabisa.

Kwa kuwa kuzungumzia Sanad ya kila hadithi itasababisha maneno kuwa marefu, basi tunafupisha mazungumzo kwa maelezo yaliyomo ndani ya hadithi hizo na tunasema:

Hadithi ya kwanza ni ile isemayo "Alipokufa Al-Hasan bin Al-Hasan mkewe aliweka Qubbah kwenye kaburi lake....."

Hadithi hii inapinga madhehebu ya Mawahabi, kwani ni dalili inayoruhusu kuweka vivuli na Qubbah juu ya kaburi, na Mawahabi wao wanaharamisha moja kwa moja kuweka kivuli sawa kikiwa cha Qubbah au jengo.

Basi hadithi hii inajulisha ruhusa ya kuweka kivuli na kujenga Qubbah juu ya kaburi, na lau jambo hilo lingekuwa haramu lisingefanywa na mke wa Hasan bin Hasan, kwani kitendo hicho kilifanyika mbele ya macho na masikio ya Tabiina na wanachuoni wa Madina.
Na huenda aliweka Qubbah hilo kwa ajili ya kusoma Qur'an kwenye kaburi ajikinge na joto, baridi na mengineyo.

Na ama kauli ya mpokeaji wa hadithi aliposema:

(Wakaisikia sauti inasema.....) Inafanana na kauli ya mtu asiyemcha Mungu, kwani kauli hiyo ni moja ya aina za kufurahia msiba wa mwingine, na kufurahia msiba wa mwingine siyo miongoni mwa tabia za wachamungu, na mfano ni huo huo kwa yule mwingine anayedaiwa kuwa alijibu.

Kwa mwanamke yule kuweka Qubbah juu ya kaburi la mumewe haikuwa lengo ni kumfanya mume huyo arudi mpaka aambiwe kuwa amekata tamaa, bali lengo lilikuwa ni kwa ajili ya kusomea Qur'an na ibada nyinginezo.

Kifupi, kauli ya huyo anayedaiwa kusema na yule mwingine aliyejibu siyo hoja ya kisheria, kwani kauli zao siyo Qur'an wala siyo Sunna tukufu ya Mtume wala maneno ya Ma'sum.

Ama kwa upande wa zile hadithi zinazowalaani Wayahudi na Wakristo na kuwahadharisha Waislamu kufanana na Wayahudi na Wakristo sisi tunajibu kwa kusema:

Kufahamu makusudio ya hadithi hizo kutategemea kufahamu waliyokuwa wakiyafanya Wayahudi na Wakristo kwenye makaburi ya Manabii wao na kwa ajili hiyo ndiyo maana Mtume [s] akakataza kufanya waliyokuwa wakiyafanya Wayahudi na Wakristo.

Tutakapofahamu hilo, ndipo tutakapofahamu uharamu uliokatazwa.

Katika hadithi zinapatikana dalili zinazoshuhudia kwamba Wayahudi na Wakristo walikuwa wakiyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni kibla chao, na wanaacha kuelekea kibla inayowapasa kuielekea.

Na zaidi ya hapo, walikuwa wakiwaabudu Manabii wao karibu na makaburi yao badala ya kumwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja, au walikuwa wakiwafanya Manabii wao kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika ibada.

Basi ikiwa maana iliyoko katika hadithi hizo ni: Msiyafanye makaburi ya watu wema kuwa ni kibla chenu, au msiwafanye watu wema kuwa washirika wa Mwenyezi Mungu katika ibada, basi haiwezekani kabisa kuzitolea ushahidi kwa namna yoyote ile kuharamisha kujenga kwenye makaburi yao, kwani wanaozuru hawayafanyi makaburi hayo kuwa ni kibla chao wala hawawaabudu wala kuwafanya washirika wa Mwenyezi Mungu katika ibada. Bali lililopo ni kwamba wote ni waumini wanaomwamini Mwenyezi Mungu na kumpwekesha na katika sala zao wanaelekea kwenye Al-Kaaba tukufu.

Na lengo la kujenga msikiti kwenye makaburi hayo ni kupata tu baraka iliyopo kwenye ardhi hiyo ambayo imehifadhi miili yao mitukufu.

Na muhimu sasa ni kuthibitisha kwamba lengo la hadithi hizo kukataza kuyafanya makaburi kuwa misikiti ni lile tulilolitaja.

Hebu angalia dalili zinazojulisha hilo:

1. Hadithi iliyotajwa katika Sahih Muslim ni hadithi namba 4 nayo itafafanua hadithi nyingine.

Wakati Mama Ummu Habiba na Ummu Salama, ambao wote ni wakeze Mtume [s], waliposema kwamba wameona picha za Nabii katika moja ya Kanisa la Ethiopia Mtume [s] alisema:
"Hakika watu hao, anapokuwepo miongoni mwao mtu mcha Mungu kisha akafa, hujenga kwenye kaburi lake msikiti na kuchora picha hizo."

Lengo la kuweka picha za wachamungu hao karibu na makaburi yao ilikuwa ni kwa ajili ya kuzisujudia na kusujudia makaburi, kiasi cha kuwa kaburi na picha inakuwa ndiyo kibla chao, au vikawa kama sanamu zinazoabudiwa na kusujudiwa.

Hakika maana hii tuliyoitaja katika hadithi hii inakubaliana na mwenendo walionao Wakristo katika kumwabudia Masihi Mwana wa Mariamu, na kuweka picha na sanamu zake na za Bibi Mariamu [a]. Kwa maana hii tuliyokwisha ieleza, haiwezekani kutolea ushahidi hadithi hizi kuharamisha kujenga misikiti kwenye makaburi ya wacha mungu au karibu yake kama kutakuwa hakuna kitu kinachopelekea kuabudiwa kama ilivyo kwa Wakristo.

2. Anasimulia Ahmad ibn Hanbal katika Musnad yake, na Malik ibn Anas naye katika "Muwataa" ukamilifu wa hadithi hii, nayo ni kwamba Mtume [s] amesema baada ya kukataza kuyafanya makaburi kuwa misikiti: "Ewe Mwenyezi Mungu usilifanye kaburi langu kuwa sanamu litaloabudiwa."7

Maneno haya yanajulisha kwamba watu hao walikuwa wakiyafanya makaburi na picha zilizokuwa kwenye makaburi hayo kuwa ni kibla cha kukielekea na wakiabudu masanamu kinyume cha Mwenyezi Mungu.

3. Mazingatio katika hadithi ya pili ya Bibi Aisha yanaongeza ufafanuzi wa ukweli huu, kwani yeye Bibi Aisha baada ya kupokea toka kwa Mtume [s] anasema: "Lau si hivyo wangelidhihirisha kaburi lake Mtume, lakini mimi nachelea kuwa litafanywa kuwa msikiti.

Tunajiuliza: Kusimamisha ukuta pembeni ya kaburi kunazuia kitu gani?

Ukweli ni kwamba ukuta unazuia kuswali juu ya kaburi lenyewe na kufanywa kuwa sanamu linaloabudiwa na kwa mukhtasari lisije kuwa kibla likaelekewa.

Ama kuswali karibu ya kaburi bila ya kuliabudia kaburi au kulifanya kibla kwa ajili ya ibada hakuna kizuizi, sawa sawa kuna kizuizi kinachozuia kuliona kaburi au hapana na vile vile kaburi liwe limetokeza kwenye ardhi au hapana.

Na hiyo ni kwa sababu Waislamu tangu karne kumi na nne zilizopita, wanaswali karibu na kaburi la Mtume [s] wakielekea kibla wakati huo wa kuswali na wanamwabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kwa hiyo kuwepo kizuizi hakuzuii yote haya.

Kifupi cha maelezo ni kwamba ukamilifu wa hadithi ya pili ambayo ina maneno ya Bibi Aisha unaiweka wazi maana ya hadithi, kwani Bibi Aisha anataja sababu ambayo iliyozuia kudhihiri kwa kaburi la Mtume [s] ili kuepusha kufanywa msikiti, na kwa ajili hiyo ulijengwa ukuta pembeni ya kaburi tukufu la Mtume [s].

Kizuizi hiki kinazuia mambo mawili:

1. Ni kuzuia lisije likageuzwa kaburi hilo na kuwa sanamu na watu wakasimama kuliabudia, hivyo basi ikiwa kuna kizuizi haitawezekana kuliona na halitafanywa sanamu kwa ajili ya ibada.

2. Ni kuzuia lisifanywe kuwa ndiyo kibla, kwani kulifanya kuwa ni kibla kutategemea kule kuonekana kwake.

Iwapo mtu atasema: "Mbona Al-Kaaba ni kibla cha Waislamu wakati Waislamu wengi hawaioni Al-Kaaba wakati wa ibada?

Jawabu lake ni kuwa: Haifai kulinganisha kaburi na Al-Kaaba kwa sababu Al-Kaaba ndiyo kibla cha Waislamu wote ulimwenguni. Na wala kibla hicho siyo kwa ajili ya ibada peke yake bali ni kwa ajili ya ibada na mengineyo kama vile kuchinja, kuzika na mfano wa hayo.

Kwa hiyo Al-Kaaba ni kibla katika kila hali wala haina uhusiano wa kuonwa au kutokuonwa.

Ama kule kulifanya kaburi la Mtume [s] kuwa ni kibla jambo hilo linawezekana kwa wale waliomo katika Msikiti wake na wanaswali humo, hivyo kudhihiri kwa kaburi lake kunaweza kupelekea urahisi wa kulifanya kuwa kibla kwa mujibu wa fikra ya Bibi Aisha katika hadithi, kama vile alivyoona kwamba kulisawazisha na ardhi hakuna hatari hii.

3. Katika dalili zinazojulisha kwamba katazo la Mtume [s] ni kule kuyaabudu makaburi, ni kwamba wafasiri wengi waliosherehesha Sahih Bukhari na Sahih Muslim, wamefasiri hadithi hiyo kama tulivyoifasiri, na waliielewa kama tulivyoielewa sisi.

Kwa mfano:
Anasema Al-Qastalani katika kitabu kiitwacho Irshaadus-Saari:

"Hakika mwanzoni watu walitengeneza picha za wachamungu na Mawalii na Mitume, ili wajiliwaze kwa picha hizo na wakumbuke matendo yao mema, wapate kujitahidi kama walivyojitahidi wale, na wakawa wanamwabudu Mwenyezi Mungu kwenye makaburi yao, kisha walifuatia baadaye watu ambao hawakujua lengo la wazazi wao, na shetani naye akawashawishi kuwa wazazi wao walikuwa wakiziabudu picha hizi, ndiyo maana Mtume [s] akatahadhari jambo hili."

Anaendelea kusema: -

"Baidhawi amesema: "Wayahudi na Wakristo walipokuwa wakisujudia makaburi ya Mitume wao ili kuwatukuza, na wakayafanya kuwa ndiyo kibla cha kuyaelekea wakati wa sala na wakayafanya kuwa masanamu, Waislamu wamekatazwa kufanya namna hiyo. Ama kule kujenga msikiti karibu ya kaburi la mtu mwema na kukusudia kupata baraka na siyo kumwabudu au kumwelekea kama kibla, jambo hili haliingii katika maonyo yaliyotajwa ndani ya hadithi."8

Naye Ibn Hajar katika Fat-hul-Bari Juz. 3 uk. 208 amesema:

"Makatazo yako kwenye mambo yanayopelekea matendo waliyokuwa wakiyafanya Ahlul-kitab; ama kinyume cha hivyo hakuna ubaya."

Na huyu AI-Qastalani siyo peke yake aliyesherehesha namna hii, bali pia As-Sindi aliyetoa Sherehe ya As-Sunan An-Nasai anasema:

"Waliyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa Misikiti" maana yake ni: Waliyafanya kuwa kibla wakati wa sala, au walijenga misikiti juu yake na wakawa wanasali humu, na inaonyesha kuwa huenda ukaraha huu unapelekea kule kuliabudu kaburi lenyewe."

Anasema tena: "Mtume [s] anauonya umma wake wasije lifanya kaburi lake kama walivyofanya Wayahudi na Wakristo kwenye makaburi ya Mitume wao pale walipoyafanya kuwa ni misikiti, iwe ni kwa kusujudu au kuyafanya kuwa ni kibla cha kuelekea wakati wa sala."

Naye An-Nawawi anasema katika Sherehe ya Sahih Muslim:

"Wamesema wanachuoni: Mtume amekataza kulifanya kaburi lake na kaburi la mwingine yeyote kuwa ni msikiti kwa kuchelea kuvuka mpaka wa kumtukuza na kufanya watu wapotee, jambo ambalo huenda likapelekea watu kukufuru, kama ilivyotokea kwa nyumati zilizopita. Na Masahaba na Tabiina walipotaka kuuongeza Msikiti wa Mtume [s] kutokana na ongezeko la Waislamu, uliongezeka mpaka nyumba za wakeze Mtume zikaingia katika msikiti kikiwemo chumba cha Bibi Aisha ambacho ndimo alimozikwa Mtume [s] na Masahaba wake wawili, basi walilijengea kaburi ukuta mrefu kulizunguka lisiwe linaonekana katika msikiti na watu wa kawaida (wasio na ujuzi wa kutosha) wasije wakaliabudia na kwa ajili hii Bibi Aisha amesema katika ile hadithi "Lau si kuogopea hilo jambo wangelidhihirisha kaburi la Mtume, isipokuwa paliogopewa kuwa litafanywa msikiti."

Yuko mshereheshaji mwingine anasema:

"Hakika hadithi ya Aisha inafungamana na Msikiti wa Mtume kabla haujaongezwa; ama baada ya kuongezwa na chumba [cha Bibi Aisha] kuingizwa msikitini, chumba hicho kilijengwa kwa umbile la pembe tatu ili isiwezekane kwa yeyote kuswali juu ya kaburi.... Wayahudi na Wakristo walikuwa wakiwaabudu Mitume wao karibu na makaburi yao au wakiwashirikisha na Mwenyezi Mungu katika ibada."

Mimi nasema: Pamoja na qarina zote hizi na vile walivyofahamu washereheshaji wa hadithi ni lazima pawe na maelezo kuhusu hadithi hii, na haiwezekani kupata matokeo kinyume chake au fatwa isiyokuwa hiyo. Tukizifumbia macho qarina hizi, tunaweza kutatua tatizo kama ifuatavyo:

Kwanza: Hadithi yenyewe ilivyokuja inalenga kuwa: "Kama msikiti wenyewe utakuwa umejengwa juu ya kaburi". Kwa maana hiyo haina uhusiano wowote na maziyara matukufu, kwa kuwa misikiti yote iko karibu na makaburi hayo wala siyo juu yake, kwa namna ambayo kila kimoja kiko mbali na mwenziwe. Kwa hiyo yale maziyara yanakuwa ni kwa ajili ya kuzuru na kutawas-sal kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwa huyo Walii mwema, na ule msikiti uliyo karibu yake ni kwa ajili ya kuswali na ibada nyinginezo.

Baada ya haya, basi vipi itawezekana kusema kwamba ni haramu kujenga Msikiti karibu na kaburi au ni karaha? Wakati ambapo kwa macho yetu tunauona Msikiti wa Mtume [s] uko karibu na kaburi lake tukufu?

Iwapo Masahaba ni kama nyota na ni wajibu kuwafuata, basi ni kwa nini hawafuatwi katika jambo hili? Bila shaka wao (Masahaba) ndiyo walioongeza ndani ya msikiti wa Mtume nyongeza nyingi kiasi kaburi la Mtume [s] limekuwa katikati ya msikiti, baada ya kuwa msikiti ulikuwa upande wa mashariki mwa kaburi hilo tukufu, na kwa sababu ya hizo nyongeza nyingi, upande wa magharibi nao ukaingia ndani ya msikiti.

Basi ikiwa kujenga msikiti karibu na makaburi ya watu wema ni haramu, ni kwa nini Waislamu waliziweka nyongeza hizi katika kila upande wa msikiti?

Basi Je, ile maana ya kuwafuata Salafa na Salafiyyah wanayoilingania Mawahabi iko katika kuwafuata kwenye maudhui moja tu na kuziacha zingine?

Kwa hali hii tunafahamu kwamba maneno ya Ibnul-Qayyim anaposema kuwa "Kaburi na msikiti havikutani mahali pamoja" yanakhalifu mwenendo wa Waislamu waliopita hapo kabla; wala maneno yake hayana msingi wo wote wa kusihi.

Pili: Tunaweza kufahamu kutoka katika hadithi hizi (iwapo tutazikadiria kuwa ni sahihi) na kwamba Mtume [s] amekataza kujenga msikiti juu ya makaburi ya wachamungu au karibu yake. Lakini haipatikani dalili ya yakini inayothibitisha kwamba katazo hili ni katazo la kuharamisha, bali inawezekana kuwa ni Nahyi Tanzihi (karaha), na ndiyo maana Bukhari amezitaja hadithi hizi kwenye kitabu chake chini ya anuani isemayo "Babu Ma-yukhrahu Minittikhadhil-Masajid Alal-Qubur," (Mlango wa, ni karaha kujenga misikiti juu ya makaburi).9

Na jambo hilo pia linashuhudia kwamba katazo limeambatanishwa na laana kwa wanawake wanaozuru makaburi."10

Kilichothibiti ni kwamba kuzuru makaburi kwa wanawake ni makruhu kutokana na baadhi ya mambo fulani na wala siyo haramu.

Iwapo Mtume [s] anawalaani wanawake wanaozuru makaburi basi laana hiyo haijulishi kuwa jambo hilo ni haramu, kwani kutokana na mambo mengi ya karaha imekuja laana kwa mwenye kuyatenda katika hadithi nyingi, na lengo la laana hiyo, ni kuonyesha ukaraha mkubwa wa jambo hilo na kwamba (kulitenda) hi kujiweka mbali na Rehma za Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kwa mfano, imekuja katika hadithi:

"Mwenyezi Mungu amewalaani watu watatu; Mwenye kula chakula chake cha safari peke yake, na mwenye kulala ndani ya nyumba peke yake, na mwenye kusafiri jangwani peke yake."

Na inafahamika kwamba mambo haya matatu siyo haramu.

Na hatimaye, tunasisitiza kwamba kujenga misikiti kwenye makaburi ilikuwa ni Sunna inayotendeka tangu mwanzo wa kuja Uislamu.

As-Samhudi anasema katika hadithi ambayo ametaja kifo cha Bibi Fatma binti Asad "Mama wa Imam Ali [a]."

"Alipofishwa (Bibi Fatma Binti Asad), Mtume [s] alitoka na akaamuru lichimbwe kaburi, likachimbwa mahala penye msikiti ambao leo unaitwa "Qabr Fatimah."11

Anachokusudia As-Samhudi hapa ni kwamba "Mahali lilipokuwa kaburi la Bibi Fatma bint Asad paligeuzwa na kuwa msikiti."

Anasema tena As-Samhudi:

"Hakika Mus'ab ibn Umair na Abdallah ibn Jahshi wamezikwa ndani ya msikiti ambao ulijengwa juu ya kaburi la Hamza."12

Msikiti huo ulikuwepo mpaka pale uvamizi wa Kiwahabi ulipoivamia ardhi hii tukufu na kuubomoa msikiti huu na misikiti mingine pamoja na kumbukumbu nyingi kwa sululu za wakoloni wa Kiingereza.

 • 1. Tafsir Al-Kash-Shaaf ya Az-Zamakhshari, na Ghara'ibul-Qur'an ya An-Nishapuri na nyinginezo.
 • 2. (1) Sahih Bukhari, kitabul-Janaiz Juz. 2 uk. 111. (2) Sunan An-Nasai Juz. 2 uk. 871 Kitabul Janaiz.
 • 3. Sahih Muslim, Juz. 2, uk. 68.
 • 4. Sahih Muslim kitabul-Masajid, Juz. 2 uk. 66.
 • 5. As-Suna cha An-Nasaiyy, juz. 3, uk. 7 Chapa ya Mustafa Al-Halabiy Misri.
 • 6. Ziyaratul-Qubur, uk. 106
 • 7. Musnad Ahmad, juz. 3 uk 248.
 • 8. Ir-Shadus-Sari, Fi Sharhi Sahih Al-Bukhari.
 • 9. Sahih Bukhari, juz. 2, uk. 111.
 • 10. Sunan An-Nasai, juz. 3, uk 77, chapa ya Misri.
 • 11. Wafaul-Wafa, juz. 3, uk 897
 • 12. Wafaul-Wafa, juz. 3, uk. 922-936.