Table of Contents

Kumuapa Mwenyezi Mungu Kwa Haki Ya Mawalii

Miongoni mwa nukta wanazotofautiana Waislamu na Mawahabi ni kwamba, Mawahabi wanadai kuwa, ni haramu kumuapa Mwenyezi Mungu kwa haki ya Mawalii, na pia kuapia kisichokuwa Mwenyezi Mungu.

Wakati mwingine Mawahabi wanaona kuwa viapo hivi viwili ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu katika Ibada. Katika maelezo yafuatayo tutaisherehesha kwa urefu maudhui hii ili kupata hukmu sahihi ya kisheria.

Bila shaka Qur'an inawasifu baadhi ya waja wa Mwenyezi Munga inaposema:

"Wafanyao subira na wasemao kweli na watiifu na watoao sadaka na wale wanaoomba msamaha saa zilizo kabla ya alfajiri." Qur'an, 3:17.

Basi lau mtu atasimama katikati ya usiku akasali kwa ajili ya Mola wake rakaa nyingi, kisha akanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu huko akisema:

"Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba kwa haki ya wanaokutaka msamaha wakati wa karibu ya al-fajiri, unisamehe dhambi zangu". Itakuwaje basi kauli yake hii tuione kuwa ni shirki katika Ibada?

Bila shaka shirki katika Ibada maana yake ni "Kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, au ni kumzingatia asiyekuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni Mungu na ndiyo chanzo cha matendo ya Kiungu."

Ama mahala hapa (tunapopazungumzia) yule mtu anayeswali anamuelekea Mwenyezi Mungu na haombi chochote (kwa mwingine) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu. Basi iwapo tendo hili ni haramu, hapana budi kuwe kuna sababu nyingine isiyokuwa shirki.

Sisi hapa (nia yetu) tunataka kuwaelekeza Mawahabi wafahamu kwamba, Qur'an Tukufu imetaja kipimo na kanuni ili kufafanua na kupambanua baina ya mshirikina katika Ibada na yule mwenye Tauhidi, na kwa kipimo hiki imeweka kizuwizi mbele ya kila tafsiri itayofasiriwa kwa maoni (binafsi) juu ya maana ya "mshirikina."

Kipimo hiki ni kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

"Na anapotajwa Mwenyezi Mungu peke yake, nyoyo za wale wasioamini Akhera huchukia, na wanapotajwa wale wasiokuwa Mwenyezi Mungu basi wao hufurahi." Qur'an, 39:45.

Na katika aya nyingine Qur'an inawataja waovu ambao ni wale wafanyao shirki inasema:

"Bila shaka wao walipokuwa wakiambiwa "Hakuna aabudiwaye kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, walikuwa wakipinga na husema je, sisi tuiache Miungu yetu kwa ajili ya huyu mtunga mashairi mwendawazimu." Qur'an, 37:35-36.

Kwa hiyo basi kwa mujibu wa aya mbili hizi mushrik (mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu) ni yule ambaye huchukia moyo wake atajwapo Mwenyezi Mungu peke yake, na hufurahi watajwapo Miungu batili, au hupinga upweke wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Baada ya kipimo hiki cha Qur'an tunajiuliza, "Hivi yule mtu asimamaye katikati ya usiku na akamaliza saa nyingi akifanya Ibada na kuomba na akaswali mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ikhlasi na unyenyekevu na akamuapa Mwenyezi Mungu kwa haki ya Mawalii wake wema na akamuomba Mwenyezi Mungu kupitia kwa waja wake wema..... hivi kweli mtu huyu atakuwa mushrik kwa amali yake hii?!

Basi ni kwa namna gani amepinga utajo wa Mwenyezi Mungu na ni vipi amekataa kukiri upweke wa Mwenyezi Mungu Mtukufu (hata aitwe ni mushrik)?!!!

Ni kwa nini basi waandishi wa Kiwahabi wanategemea misingi ya kubuni na dalili dhaifu kuliko hata nyumba ya buibui, kisha wanawatuhumu Waislamu kuwa wanafanya shirki halafu wao wakajiona kuwa peke yao ndiyo taifa teule la Mwenyezi Mungu?!

Vipi itafaa wawazingatie asilima 99% ya Waislamu kuwa ni washirikina na wao wawaone Mawahabi toka Najdi kuwa ndiyo peke yao ni watu wa Tauhidi pamoja na kuyazingatia (maelezo) ya kipimo cha Qur'an?

Na je, Mwenyezi Mungu amewapa uwakala Mawahabi wa kuifasiri maana ya shirki kama wapendavyo na waamue kwamba kundi hili ni washirikina wa kundi hili ni la watu wa Tauhidi? Ukweli ulivyo ni kwamba, "Mwenyezi Mungu ameweka kifuniko kwenye nyoyo zao basi wao hawafahamu (kitu)."