read

Kutaka Uombezi Toka Kwa Mawalii Wa Mwenyezi Mungu

Neno "Shafaa" ni maarufu miongoni mwetu sote, nalo tunalitamka mara nyingi katika ndimi zetu katika nyakati na muhala mnamo husika.

Kwa mfano: Yanapofanyika mazungumzo kumhusu mtu fulani aliyetenda kosa fulani na mahakama imemhukumu kifo au kufungwa au namna nyingine, kisha akatokea mtu akaingilia kati na kumuokoa tokana na hukumu aliyohukumiwa, basi huwa tunasema mtu fulani kamuombea (kamshufaia) fulani.

Maana Ya Shafaa (Kushufaia)

Neno Shafaa linatokana na shaf'a kwa maana ya jozi ambalo kinyume chake ni witiri na sababu zilizofanya neno "Shafaa" litumike kwa maana ya kile kitendo cha kuombea na "Shafii" kwa maana ya yule mwenye kuombea ni kwamba, juhudi na bidii zifanywazo na huyu mwenye kuombea zinaoana na juhudi na bidii nyingine za kutaka kujiokoa zinazofanywa na yule anayeombewa, na ndipo yule mwenye kutenda makosa au mwenye kutuhumiwa hupata kuokoka kutokana na kuangamia.

Uombezi wa Mawalii wa Mwenyezi Mungu kuwaombea watu wenye madhambi kunakuja kutokana na ukaribu wao hao Mawalii kwa Mwenyezi Mungu, pia daraja yao na heshima yao mbele yake Mwenyezi Mungu. Basi wao huombea watu wenye dhambi kwa idhini ya Mwenyezi Mungu ndani ya masharti maalum ili Mwenyezi Mungu apate kuwasamehe au kuwapokelea maombi yao.

Kwa maelezo mengine ni kwamba "Shafaa" ni msaada wa Mawalii wa Mwenyezi Mungu kwa idhini yake kuwasaidia watu ambao hawakukata maungamano yao ya kidini kwa Mwenyezi Mungu na Mawalii wake, pamoja na kwamba wao ni wenye dhambi.

Taarifu hii ya "Shafaa" imetoa maana ya kina ambayo inapasa kuizingatia muda wote, na kwa maelezo ya namna ya tatu ni kwamba, Shafaa ni msaada wa mtu mwenye daraja ya juu kwa ajili ya mtu wa daraja ya chini, kwa sharti ya kuwepo maandalizi kupokea Shafaa kwa ajili ya ukamilifu wa mafanikio yake na kupanda kwenye daraja ya juu, na kumbadili kuwa mtu mwema mtakatifu.

Baada ya taarifu hizi nyingi tunasema: "Historia inathibitisha kwamba, Waislamu tangu zama za Mtume [s] na baada yake, walikuwa wanaomba "Shafaa" toka kwa Mawalii wema wa Mwenyezi Mungu, sawa sawa Mawalii hao wawe hai au baada ya kufa kwao, na wala hakuna mwanachuoni yeyote wa Kiislamu aliyeifahamu "Shafaa" kuwa inapingana na misingi ya Uislamu, mpaka alipokuja Ibn Taimiyyah katika karne ya nane Hijiriya akiwa na mawazo potofu akayapinga mambo mengi miongoni mwa misingi ya Uislamu na mwenendo wa Waislamu.

Na baada ya kupita karne tatu tangu yeye Ibn Taimiyyah kuzusha fikra hizo alikuja Muhammad bin Abdul-Wahab kutoka Najdi, yeye aliinyanyua juu bendera ya upinzani dhidi ya Waislamu na akazusha fitna na utengano baina yao, pia akaupa uhai uzushi wa Ibn Taimiyyah kwa nguvu kuliko hata alivyokuwa Ibn Taimiyyah mwenyewe.

Mawahabi wanaitakidi kusihi kwa "Shafaa" katika misingi yake, lakini tofauti iliyo baina yao na Waislamu ni kwamba wao Mawahabi wanaharamisha kuomba "Shafaa" kutoka kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu hapa duniani, na wao wanaeleza itikadi yao hii kwa maelezo machafu yanayoonyesha dharau kwa Manabii na Mawalii kiasi ambacho inatia woga kuyataja hayo wayasemayo Mawahabi.

Miongoni mwa maneno wayasemayo ni kwamba "Mtume wa Uislamu yeye na Manabii wengine na Mawalii na Malaika, wanayo haki ya kushufaia huko Akhera tu, lakini kuomba Shafaa ni lazima iwe kwa Mwenyezi Mungu na sio kwao na isemwe kama ifuatavyo:

"Ewe Mwenyezi Mungu mfanye Mtume wetu Muhammad [s] awe muombezi siku ya Qiyama, au Ewe Mwenyezi Mungu wafanye waja wako wema wawe waombezi wetu au Malaika wako au mfano kama huu miongoni mwa mambo ambayo huombwa kwa Mwenyezi Mungu na siyo kwao Mitume na Mawalii na Malaika hapo haiwezi kusemwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu au Ewe Walii wa Mwenyezi Mungu nakuomba "Shafaa" au kitu kingine miongoni mwa mambo ambayo hakuna ayawezaye isipokuwa Mwenyezi Mungu, basi iwapo utaomba "Shafaa" katika siku zao za kuwa katika Bar-zakh basi tendo hilo litakuwa ni miongoni mwa shirki."1

Kwa hali hii unawaona Mawahabi wanavyowatuhumu Waislamu eti kuwa wanafanya shirki kwa kuomba "Shafaa" toka kwa Mtume [s] na Mawalii wa Mwenyezi Mungu hapa duniani na huko Akhera. Sisi kabla ya kuingia katika majadiliano dhidi ya hoja na dalili za Mawahabi kwanza tunaanza kuyachunguza mas-ala hayo ya "Shafaa" kwa mujibu wa Qur'an Tukufu na Sunna, pia sera ya Waislamu kisha tuzilete hizo dalili za Mawahabi na tuzichunguze na kuzijadili.

Dalili Zinazoruhusu Kuomba Shafaa Hapa Duniani

Dalili yetu inayoruhusu kuomba Shafaa hapa duniani imefungamana na mambo mawili, na yatakapothibiti mambo hayo, maudhui ya Shafaa itakuwa imekaa wazi kikamilifu.

Mambo hayo mawili ni haya yafuatayo:

1. Kuomba Shafaa ni kuomba dua.

2. Kuomba dua toka kwa watu wachamungu ni jambo Mustahabbu katika Uislamu.

Sasa hebu angalia uchambuzi wa mambo haya mawili kama ifuatavyo:

1) Kuomba Shafaa Ni Kuomba Dua

Uombezi wa Mtume [s] na waombezi wengine miongoni mwa watu wema si kitu kingine, bali ni maombi yao kwa Mwenyezi Mungu, kwani wao daraja yao na heshima yao ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kwa sababu ya daraja yao huwa wananyenyekea mbele ya Mwenyezi Mungu kwa dua na kuwatakia maghfira (msamaha) watu wenye dhambi, naye Mwenyezi Mungu huyakubali maombi yao na kuieneza huruma yake kwa waja wake hao wenye kufanya maasi na kuwasamehe na kuyakosha madhambi yao.

Kuomba dua kutoka kwa ndugu muumini Muislamu yeyote ni jambo zuri linalopendekezwa (katika Uislamu) na hapana mtu mwenye shaka juu ya ubora wa jambo hili miongoni mwa wanachuoni wa Kiislamu na Madhehebu mbali mbali hata hao Mawahabi wenyewe, basi itakuwaje hali ya dua ya Mtume na Mawalii wema?

Bila shaka haiwezekani kusema kwamba Shafaa maana yake ni ile dua ya siku ya kisimamo cha Qiyama, lakini kinachowezekana kusemwa ni kwamba, katika maana zilizo wazi kuhusu Shafaa ni dua na pia kwamba yeyote anayemsemesha mmoja miongoni mwa Mawalii akasema, "Ewe mwenye cheo mbele ya Mwenyezi Mungu tuombee kwa Mwenyezi Mungu", huwa hakusudii ila maana ya dua.

Amepokea Nidhamud-dini An-Nishapuri, kuhusu tafsir ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat an-Nisa aya ya 85 isemayo: "Yeyote atakayeombea maombezi mabaya atakuwa na sehemu katika mabaya hayo."
Yeye Nidhamud-din amepokea toka kwa Muqatil amesema: "Shafaa kwa Mwenyezi Mungu maana yake ni kumuombea Muislamu."

Na pia imepokelewa kwa Mtume [s] kwamba, anayemuombea nduguye Muislamu hali ya kuwa hayupo, maombi yake hukubaliwa, nao Malaika husema (kumuambia aliyeomba) nawe upate mfano wa hayo uliyomuombea nduguyo.

Hakika huyu Ibn Taimiyyah yeye ni miongoni mwa wale ambao wanaofahamu wazi kwamba, kuomba dua kwa mtu aliye hai (akuombee) ni jambo sahihi, na kwa msingi huu basi kutaka Shafaa hakumhusu Mtume na Mawalii wa Mwenyezi Mungu peke yao, bali pia inafaa jambo hilo kwa kila muumini mwenye daraja tukufu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Al-Imam Fakhrudin Razi, ni miongoni mwa wale wanaoifasiri maana ya "Shafaa" kuwa ni dua na ni Kutawassal kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Amesema Fakhrudin Razi katika kufasiri kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

"..Na wanawaombea msamaha wale walioamini (kwa kusema), Ewe Mola wetu, umekienea kila kitu kwa Rehema…" Qur'an, 40:7 akasema kama ifuatavyo:

"Aya hii inajulisha kuwepo kwa Shafaa toka kwa Malaika kuwaombea waja wenye dhambi.... Na litakapothibiti jambo hili katika haki ya Malaika (kuwaombea wenye dhambi) basi hali itakuwa ni hiyo hiyo katika haki ya Manabii kuwaombea wenye (dhambi) kutokana na kukubaliana Ijmai kwamba hakuna tofauti yoyote kati ya Malaika na Manabii katika jambo hili.

Na amesema vile vile kwamba:

Kadhalika Mwenyezi Mungu amemwambia Mtume Muhammad [s] "Omba msamaha kwa makosa yako na uwatakie msamaha waumini wanaume na waumini wanawake," (Mwenyezi Mungu) akamuamuru Mtume kwanza aombe msamaha kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe kisha awaombee msamaha wengine."

Pia Mwenyezi Mungu anasimulia habari za Nuhu [a] kwamba, yeye Nuhu alisema: "Ewe Mola wangu nisamehe mimi na wazazi wangu na umsamehe yeyote atakayeingia nyumbani mwangu hali ya kuwa ameamini na uwasamehe waumini wanaume na waumini wanawake."2

Ufafanuzi huu wa Fakhrur-razi unashuhudia kwamba yeye anaona maana ya Shafaa kuwa ni maombi ya mwenye kumshufaiya mwenye dhambi na kuomba Shafaa ni kuomba dua kwa huyo mwenye kushufaia.

Pia imekuja katika hadithi nyingi za Mtume [s] kwamba, dua ya Mwislamu kumuombea nduguye Mwislamu ni kumshufaia.

Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas naye kapokea toka kwa Mtume [s] kwamba, Mtume amesema:

"Hapana mtu yeyote Muislamu atakayekufa kisha wakasimama kusalia Jeneza lake watu arobaini wasiomshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote isipokuwa Mwenyezi Mungu atakubali uombezi wao kwa mtu huyo."3

Kwa hakika imekuja katika hadithi hii matumizi ya maneno ‘Shafaa-humullahu fihi’ kwa ajili ya wale wanaomuombea ndugu yao mwislamu ili kuonyesha maana ya Shafaa kuwa ni dua.

Kwa mujibu wa hadithi, lau mtu atawausia (katika uhai wake) watu arobaini miongoni mwa marafiki zake, wasimame kusalia Jeneza lake atakapokufa na wamuombee, basi mtu huyo atakuwa amewaomba watu hao "Shafaa" na atakuwa ameandaa uombezi wa waja wa Mwenyezi Mungu kumuombea nafsi yake.

Naye Bukhari katika Sahih yake ametenga mlango maalum akauita "Watu watakapoomba Shafaa kwa Imam awaombee mvua basi asiwakatalie."

Na ametenga mlango mwingine pia ambao ameuita "Pindi washirikina watakapoomba Shafaa kwa Waislamu wakati wa ukame."4

Na hadithi zote ambazo Bukhari amezitaja katika milango yote miwili zinajulisha kwamba kuomba "Shafaa" ni kuomba dua na wala haifai kuifasiri Shafaa kwa maana nyingine ila hiyo.
Mpaka hapa tumemaliza kutoa dalili ya Shafaa katika sehemu ya kwanza, na imethibiti kwamba, kuomba Shafaa ni kuomba dua wala siyo kinyume chake.

Na sasa hivi tunaanza uchunguzi wa maudhui ya pili ambayo ni kwamba, "kumuomba dua Mu’umini (akuombee) ni jambo mustahabu basi vipi kuomba dua kwa Mitume na Mawalii wa Mwenyezi Mungu?"

2) Qur'an Na Kuomba Dua Toka Kwa Watu Wema

Aya nyingi za Qur'an zinashuhudia kwamba Mtume [s] anapowaombea msamaha kwa Mwenyezi Mungu baadhi ya waja wake ni jambo lenye manufaa sana.

Mwenyezi Mungu anasema: "Omba msamaha kwa makosa yako na uwaombee waumini wa kiume na waumini wa kike." Qur'an, 47:19.

"Na uwaombee dua, hakika kuwaombea kwako dua kutawapa utulivu (wafanikiwe).. "
Qur'an, 9:103.

Iwapo dua ya Mtume [s] aombapo inaleta matokeo haya mazuri kwa yule anayeombewa, basi kuna kizuwizi gani kwa mtu kuomba kwa Mtume amuombee mtu huyo hali ya kuwa tunajua kwamba kuomba dua ni kuomba Shafaa kwa Mtume.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:
"Na lau wangelikujia walipojidhulumu nafsi zao wakaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na Mtume naye akawaombea msamaha, bila shaka wangemkuta Mwenyezi Mungu ni mwenye kupokea toba na mwenye kurehemu." Qur'an, 4:64.

Maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema, "Wangelikujia" ina maana ya kumjia Mtume [s] na kumtaka awaombee dua na msamaha, lau kama si maombezi ya Mtume kwao hao watu, basi kuja kwao kusingekuwa na maana ila upuuzi na mchezo tu. Kwa hakika kufika kwao mbele ya Mtume [s] na kuomba kwake dua awaombee msamaha ni dalili ya kuathirika nafsi zao na kupatikana mabadiliko yanayoandaa njia inayofaa ya kukubaliwa dua.

Qur'an inawanakili watoto wa Yaqub [a] ya kwamba, wao walimuomba baba yao awaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu, naye akaitikia maombi yao na akatekeleza ahadi yake.

Mwenyezi Mungu anasema: "Wakasema, Ee baba yetu tuombee msamaha kwa makosa yetu, hakika sisi tulikosea, akasema nitakuombeeni msamaha kwa Mola wangu..."
Qur 'an, 12:97-98.

Aya zote hizi zinajulisha kwamba kuomba dua kwa Manabii na watu wema jambo ambalo ndiyo kuomba Shafaa halipingani na hukumu za kisheria, kanuni na mizani ya Kiislamu. Ewe msomaji Mtukufu, ziko hadithi nyingi zinazohusu kuomba dua kwa waja wema na Mawalii, lakini tumeziacha ili kufupisha maelezo.

3) Hadithi Za Mtume Na Sera Ya Masahaba

Tirmidhi amepokea ndani ya Sahih yake kutoka kwa Anas kwamba amesema: "Nilimuomba Mtume [s] aniombee siku ya Qiyama akasema, mimi nitafanya, mimi nikasema, basi nitakuona wapi siku hiyo? Akasema: kwenye Sirat.5

Hadithi nyingine ni ile ambayo Sawad bin Qarib alipokuja kwa Mtume [s] akimtaka amshufaiye akasema katika beti za kishairi alizoziimba:

"Uwe wewe Mtume ndiyo muombezi wangu katika siku ile (ambayo) hakuna mwenye kuombea atakayemnufaisha Sawad bin Qarib japo kidogo."6

Na yapo maelezo yaliyokuja katika historia kwamba, kuna mtu mmoja aliyekuwa akiitwa "Tub-baa", na aliishi miaka zaidi ya Elfu moja kabla ya kudhihiri Mtume [s]., pia habari za kudhihiri kwa Nabii wa zama za mwisho kutoka Makka zilikwisha kumfikia, basi aliandika maandiko akayatoa kwa baadhi ya jamaa zake ili wamfikishie Mtume [s]., ndani ya maandishi hayo alieleza imani yake na Uislamu wake na kwamba yeye ni katika umati wa mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s]. Akasema katika maandiko hayo:

"Iwapo sitakuwahi (Ewe Muhammad) basi niombee siku ya Qiyama usinisahau." Bwana huyu alifariki, lakini maandiko yake yakawa yanapokewa toka kwa mtu hadi kwa mwingine mpaka alipodhihiri Mtume [s]. Na yalipomfikia maandishi haya mikononi mwake, Mtume [s] alisema, "Karibu ewe ndugu mwema" mara tatu."7

Basi iwapo kuomba Shafaa ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu, Mtume asingemwita yule "Tub-baa" kuwa ni 'Ndugu mwema" na wala asingesema mara tatu "karibu".

Hizi ni baadhi ya hadithi ambazo zinathibitisha kuruhusu kuomba dua na uponyo toka kwa Mtume [s] zama za uhai wake.

4) Kuomba Shafaa Baada Ya Kufa

Zipo riwaya nyingi zinazofahamisha kwamba Masahaba walikuwa wakiomba Shafaa kwa Mtume [s] baada ya kufa kwake.

Hebu tazama baadhi ya mifano ifuatayo:

1. Ibn Abbas amesema: "Pindi Amiril-Mu'minina Ali [a] alipomaliza kumkosha Mtume [s] alisema; "Baba na mama yangu wawe fidia kwako unapendeza ukiwa mzima au umekufa.... tukumbuke mbele ya Mola wako."8

2. Na imepokelewa kwamba, alipofariki Mtume [s], Abu Bakr alimfunua Mtume usoni kisha akaumbusu na akasema: "Baba na mama yangu wawe fidia kwako unapendeza ukiwa mzima au umekufa, tukumbuke mbele ya Mola wako."9

Riwaya mbili hizi na nyingine kama hizi zinajulisha kwamba, hakuna tofauti baina ya kuomba Shafaa kwa muombezi katika hai wake, na baada ya kufa kwake, na Masahaba walikuwa wakiomba dua kwa Mtume [s] baada ya kufariki kwake.

Ikiwa kuomba dua kwa Mtume [s] baada ya kufa kwake ni jambo sahihi basi kuomba Shafaa ambayo ni aina za dua itakuwa ni sahihi pia.

Kwa ufupi, kwa kutegemea aya na riwaya pamoja na sera ya Waislamu kwa karne nyingi zilizopita kuomba Shafaa ni jambo litakalozingatiwa kuwa ni sahihi moja kwa moja wala hakuna nafasi ya kufanyia shaka jambo hili kabisa.10

  • 1. Al-hadiyatus-saiyya Risala ya pili, uk. 42
  • 2. Tafsir Fakhrur-Razi, Juz. 7, uk 33-34
  • 3. Sahih Muslim, Juz. 3, uk. 53
  • 4. Sahih Bukhari, Juz.1
  • 5. Sunan Tirmidhi Juz. 4, uk. 42, Babu Maajaafi Shaan Sirat.
  • 6. Ad-durarus-Saniyyah cha Zaini dahlan Uk. 29.
  • 7. (1) Al-Maqib cha Ibn Shah-rashuu Juz. 1, uk. 16 (2) Biharul-anwar, juz.15, uk 224.
  • 8. Nah-jul-Balagha Khutba Na. 230.
  • 9. Kash-ful-ir-tiyab uk 65, akinakili kutoka Khulasatul-kalaam.
  • 10. Tumeandika kitabu maalum juu ya Shafaa na tumetaja ndani yake hadithi mia moja, arobaini na nne katika hizo zinatoka katika vitabu vya Kisunni, na zilizobaki zinatoka katika vitabu vya Kishia, ili kufahamu zaidi rejea kitabu hicho.