Table of Contents

Malengo Ya Hijja Ya Kisiasa Na Kijamii Katika Kauli Za Wanachuoni

Kwa hakika wanachuoni na wanafikra wengi wa Kiislamu wameandika umuhimu wa Hijja kisiasa na kijamii na wakazingatia kuwa ni msimu bora na fursa nzuri kwa Waislamu kuonyesha nguvu yao, mshikamano wao, muamko wao na umoja wao kwa kauli na matendo na kwa dhahiri na hisia.

Basi huyu hapa Al-Allamah Muhammad Farid Waj-di anaiandika ndani ya Dairatul-Maarif yake Maddah ya Hijja anasema:

"Amma hekima ya kufaradhishwa Hijja kwa Waislamu, hakuna nafasi ya kueleza katika kitabu hiki, lakini kitu ambacho ni wazi kuhusu Hijja ni kwamba lau wenye mamlaka ndani ya Waislamu wangetaka kuitumia Hijja katika kuleta umoja wa Kiislamu basi wangefaulu. Kwani hukusanyika kwa mamilioni ya watu katika uwanja mmoja kutoka miji mbali mbali ya ulimwengu na kuzielekeza nyoyo zao na masikio yao mahala hapo penye kukhofisha kwa kila linalotolewa kwani huwajibisha kuwaathiri wote kwa roho moja na hasa watakapolinganiwa mambo ambayo ndani yake mna kheri zao;
basi pindi wataporudi kwenye nchi zao na wakatawanyika kwenye miji yao watayatangaza mambo waliyojifunza kwa ndugu zao, na watakuwa kwao ni kama wajumbe wa mkutano mkuu uliohusisha jinsi zote na zama zote, ambapo wajumbe wake hukutana kila mwaka mara moja, basi ni athari iliyoje unayoikadiria kwa tukio hilo tukufu katika maisha ya umma huu mkubwa, na ni matokeo gani bora unayoyatarajia kutokana nalo pindi umma huu utakapozindukana kutoka katika usingizi wake.

Basi Hijja itakuwa miongoni mwa nyenzo zake kubwa, na unafahamu ya kwamba mataifa ya nje yanayozikalia baadhi ya nchi za Kiislamu yanawazuia raia zake kufanya Hijja, kwani mabadiliko ya maisha lau yataenea (yataingia) ndani ya mataifa hayo. Hakuna chochote kitakachoweza kuyazuwia na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye amri siku zote.1

Na imekuja ndani ya kitabu kiitwacho: "Ad-Dinu Wal-Hajj Alal-Madhahibil-Arba'a" kama ifuatavyo:

"Hijja ni njia ya mafahamiano, mshikamano, usawa na kuimarisha mahusiano na ushirikiano na maungamano baina ya mataifa ya Kiislamu. Basi nyoyo zao hushikamana na tamko lao kuwa moja na kutenda kitu kitakachotengeneza hali yao na kurekebisha dosari katika mambo yao."

Na ameandika ustadhi mtukufu Muhammad Mubarak ambaye ni mshauri katika chuo kikuu ya Mfalme Abdul-Aziz, amesema (katika maandiko yake): "Madhumuni ya Ibada peke yake bila kuunganisha na kitu chote iko wazi katika Hajji lakini kaiunganisha pamoja na maana nzuri ya kijamii, kwani Hijja ni mkutano wa ulimwengu (ambao) hukusanyika washiriki katika uwanja mmoja kwa ajili ya ibada ya Mungu mmoja.

Pamoja na hayo ibada hii siyo kwamba imejitenga na maisha (ya kila siku) bali imeshikana nayo kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema ndani ya kitabu chake kitukufu, "Ili washuhudie manufaa yao na kutaja jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalum.." (Qur'an, 22:28), basi kushuhudia manufaa yao ni maana pana, inawezekana kukusanya maslahi mbali mbali ya Waislamu."

Kwa hiyo iwapo tendo la kisiasa linajuzu ndani ya Hijja, kama ulivyokwisha tambua kutokana na Qur'an na Sunna na sera ya Salaf na kauli za wanachuoni watukufu bali Hijja ni fursa inayofaa kuwakhofisha maadui na kuwatisha na kuzitokomeza njama zao, basi ni adui gani aliyedhidi yenu kuliko Amerika ambayo inafanya njama dhidi ya Uislamu na Waislamu siku zote na inapora mali zao na kuiba Petroli yao?

Na je, ni adui gani aliye dhidi yetu kuliko Israel ambayo imepora ardhi yetu na kuwafukuza wananchi wetu na ikawaua na inaendelea kuwaua watoto wa Kipalestina na kuhalalisha mauaji yao na kuvunja utu wao?

Na ni adui yupi aliye dhidi yetu kuliko Urusi ambayo inayoufanyia uadui Uislamu na Waislamu katika itikadi na katika kila kitu na inaikalia ardhi yetu ndani ya Afghanistan na kuwaua vijana wake na kuibomoa miji yake na inaendelea (kufanya hayo)?

Na je, ni adui gani aliye dhidi yetu kuliko Uingereza ambayo imeunda dola ya Israel na ikafanya njama na inaendelea kufanya njama dhidi yetu kwa mujibu wa chuki za jadi za vita ya msalaba.

Na ni adui gani aliye dhidi yetu kuliko Ufaransa ambayo imeua malaki ya wanachi wetu Waislamu katika Algeria, na bado inaendeleza mauaji na njama huku na huko katika miji ya Waislamu?

Na ni kwa nini tunatofautisha baina ya Marekani na Urusi na wote hao mila yao ni moja katika kuipinga dini yetu na kufanya njama mbaya dhidi yetu na kuyaua mataifa yetu na kupora utajiri wake?

Na ni kwa nini tunaiacha fursa ya Hijja Tukufu na mkusanyiko wa pekee wa mamilioni (ya Waislamu), mkusanyiko ambao unakusanya nchi 40 za Kiislamu upotee bure bila ya kuutumia kuwa-amsha Waislamu na kuwafanya wajitolee kupinga maovu ya (watu wa) magharibi na mashariki dhidi yetu. Na je, hivi sisi tunazijua hukmu za Hijja zaidi kuliko Mtume [s] na Salaf wema waliokuja baada yake ambao katika Hijja walikuwa wakichanganya baina ya ibada na matendo ya kisiasa?

Na ni kwa nini hatutoi nafasi katika Makka, Madina, Arafat, na Mina kwa Wapalestina, Philipine, Iraq, Iran, Afghanistan, Africa, Lebanon na Eritrea na kwingineko wanakodhulumiwa wabainishe dhuluma (wanazotendewa) na wawaamshe Waislamu juu ya yale wanayokabiliana nayo miongoni mwa dhulma na ukandamizaji na mauaji na jinai za kikoloni na wafuasi wao na watumishi wao?

Na ni kwa nini hatutoi fursa katika Hijja ili wanafikra wa Kiislamu kutoka kila nchi na sehemu zote wajadili matatizo ya Waislamu na watafiti ufumbuzi wa pamoja wa taabu wanazozipata toka kwa mabeberu?

Kwa nini watawala wa Makka na Madina hawatoi nafasi kufanyika mikutano ya Jumuiya ili kuwajulisha Waislamu undani wa ukoloni wa Kimarekani, Kirusi, Kiingereza, na Kifaransa na malengo yao ya kishetani na wafahamishe matendo wanayotenda wavamizi hawa kutoka nje, ikiwa ni pamoja na kupora na kuiba na kuua na ukandamizaji.

Mpaka lini Hijja itatengwa na athari zake za kijamii na kisiasa chini ya mapendekezo ya watu kutoka nje?

Na ni mpaka lini idadi hii kubwa ya Waislamu kutoka kila sehemu ya ulimwengu (itaendelea) kukusanyika kisha kutawanyika bila ya ndugu huyu kumtambua nduguye na bila ya ndugu huyu kuyajua matatizo na matarajio ya nduguye? Na ni hadi lini (tutaendelea) kuipoteza fursa hii kubwa ambayo Uislamu umeiandaa kwa ajili ya umma huu?

Na iwapo Hijja itatupita (tukakosa kuitumia) basi ni wapi pengine itakapowezekana kuupata mkusanyiko huu mkubwa na idadi kubwa, na kongamano hili la waumini lililojiandaa kutenda na kuitika wito wowote wa Kiislamu unaowataka kupigana jihadi na kuwahimiza kuwa na muamko?

Na ni vipi watawala wa Hijazi wanakubali waipoteze fursa hii kubwa na wanawazuia Waislamu kunufaika nayo kama alivyoamrisha Mwenyezi Mungu (Na washuhudie manufaa yao)?

Bali ni vipi Waislamu wenyewe wanaruhusu kuiacha fursa ya Hijja ipotee bure bila ya kuitumikisha katika njia ya mambo yao yanayowahusu na kutatua matatizo yao?

  • 1. Dairatul-Marif, Juz. 3, uk. 350.