read

Mambo Ya Al-Qudhai Al-Misri

Baada ya kuwa nimeyahariri (maelezo yaliyotangulia) na kubainisha ufafanuzi wa ibada niliyaangalia kwa makini maneno ya mmoja wa wachunguzi miongoni mwa wanachuoni wa chuo cha Az-har, yaani Ustadh Sheikh Salamah Al-Qudhai Al-Izami As-Shafii ambaye ndiye Mwandishi wa kitabu kiitwacho "Fur-Qanul Qur'an Baina Sifatil-Khaliq Wa Sifatil-Ak-Waan.1
Yeye amesema: Mwenyezi Mungu aing'arishe hoja yake:

(Sasa tutazame maana ya Ibada kisheria, na ninataraji mahala hapa patatoa uzinduzi uliyo bora, kwa hakika kosa lililomo ni kuteleza kukubwa na ni kosa kubwa ambalo zilimwagwa damu (za watu) zisizo idadi ya kudhibitiwa na heshima za watu zilizovunjwa hazina hesabu, na jamii zikatenganishwa mahala ambapo Mwenyezi Mungu ameamuru ziunganishwe Mwenyezi Mungu atulinde kutokana na makosa na fitna hasa hasa fitna za Shubuhati - basi fahamu kwamba wao yaani Mawahabi waliifasiri ibada kuwa ni "Kufanya unyenyekevu ulio katika daraja ya juu sana", na wakakusudia ndani ya tafsiri hiyo maana ya kilugha tu.
Ama maana ya kisheria inatoa maana iliyo finyu kuliko hii (ya kilugha) kama itakavyodhihiri kwa mchunguzi mwenye kuvumilia katika utafiti iwapo ataangalia kila mahali ambapo neno ibada limekuja katika sheria, kwani maana yake ni "kufanya unyenyekevu wa hali ya juu kwa moyo kwa kuitakidi Uungu wa anayenyenyekewa, au kwa mwili pamoja na itikadi hiyo.

Basi ikiwa itikadi hii itakuwa haipo, unyenyekevu wa dhahiri alioufanya (Mwenye kunyenyekea) hauwezi kuwa ni ibada kisheria, ikiwa kanyenyekea sana au kidogo na kwa namna yoyote hata kama ni kusujudu na hata kama hakuamini Rububiyah kwa yule anayemnyenyekea lakini akaamini kuwa anazo khususiyah fulani za Rububiyah, basi hii pia itakuwa ni ibada. Kwa mfano kama ataitakidi kwamba huyo mwenye kunyenyekewa anajitegemea katika kunufaisha au kudhuru na kama vile kupitisha matakwa yake japokuwa kwa njia ya Shafaa kumshufaia huyo mwenye kumuabudia mbele ya Mola ambaye ni mkuu kuliko huyu mwenye kuabudiwa.

Kwa hakika washirikana walikufuru kwa sababu ya kuyasujudia masanamu yao na kuyaomba na mambo mengineyo miongoni mwa aina za unyenyekevu kwa sababu ya sharti hii kwani washirikina waliitakidi umola wa hayo wanayoyanyenyekea au wakayahusisha na khususiyyat za Rububiyah kama utakavyokujia ufafanuzi wake.

Na haiwezekani kusema kwamba kumsujudia asiyekuwa Mwenyezi Mungu bila itikadi hii ni ibada kisheria ukiachilia mbali aina zingine za unyenyekevu ambazo ni duni kuliko Sijda. Na kama tutasema, Sijda hii ni Ibada itakuwa ni kufru, na chochote kilicho kufru hakitofautiani kutokana na tofauti ya sheria wala amri ya Mwenyezi Mungu kwa kitu hicho wala Mwenyezi haamrishi kitu kama hicho:
"Waambie Mwenyezi Mungu haamrishi mambo mabaya." Qur'an, 7:28.

"..Na wala haridhii kufru kwa waja wake." Qur'an, 39:7.

Na haya yako wazi (yanaeleweka) kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Na (sasa) hebu msikilize Mwenyezi Mungu Mtukufu alipowaambia Malaika:

"..Msujudieni Adam, wakasujudu wote isipokuwa Ibilisi alikataa na akapinga.."
Qur'an, 2:34.
Na alisema Iblisi: "Mimi ni bora kuliko yeye." Qur'an, 7:12.

"Na alisema tena: Je, Nimsujudie Uliyemuumba kwa Udongo?" Qur'an, 17:61.

Na kusema kwamba Adam alikuwa ndiyo Qibla (cha Malaika walipamuriwa kumsujudia) ni usemi ambao haukubaliwi na ukweli na pia uchunguzi (wa jambo hili) katika kuifahamu aya inavyopasa kuifahamu unapinga kauli hiyo.

Na kama fahamu zako zitashindwa kulifahamu jambo hili, basi huyu hapa Nabii Yaqub na mkewe na watoto wao kumi na mmoja ambao Mwenyezi Mungu amesema kuhusu wao, "Wakaporomoka kumsujudia." Qur'an, 12:100.
Hapa inamaana walimsujudia Yusuf [a].

Mwanachuoni Al-Hafidh Ibn Kathir amesema katika Tafsiri ya aya hii, "Walimsujudia (Yusuf) wazazi wake wawili na ndugu zake na walikuwa watu kumi na moja, na tendo lao hili lilikuwa ni desturi inayokubalika kufanywa katika sheria zao wanapomsalimia mkubwa humsujudia.

Na desturi hii ilikuwa imeruhusiwa tangu kwa Nabii Adam [a] hadi kwenye sheria ya Nabii Isa [a], kisha iliharamishwa katika mila hii ya Kiislamu na kuifanya Sijda ni makhsusi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na haya ndiyo madhumuni ya kauli ya Qatada (juu ya Qadhiya hii na wengineo). Na kuna mapokezi katika hadithi kwamba: "Muadhi alifika Shamu akawakuta watu wa huko wakiwasujudia Maaskofu wao, naye aliporudi (Madina) akamsujudia Mtume [s], Mtume akasema "Nini hiki (ukifanyacho) Ewe Muadhi?"

Muadhi akasema: "Mimi nimewaona (Huko Shamu) wanawasujudia Maaskofu wao, nawe unastahiki mno mimi nikusujudie." Mtume akasema: Lau ningekuwa mwenye kumuamrisha yeyote kumsujudia mwingine, basi ningemuamuru mke amsujudie mumewe kutokana na haki kubwa aliyonayo kwake."

Na katika hadithi nyingine inasemwa kwamba: "Salmaan alikutana na Mtume [s] katika baadhi ya njia za Madina, na huyu Salmaan alikuwa kasilimu hivi karibuni, basi akamsujudia Mtume [s], Mtume akasema, "Ewe Salmaan usinisujudie bali msujudie (Mwenyezi Mungu) aliye hai ambaye hatakufa."

Lengo katika maelezo haya ni kuonyesha kuwa (Desturi ya kusujudia wakubwa) ilikuwa ikiruhusiwa katika sheria zao, (mwisho wa kauli ya Ibn Kathir).
Naye Imam Abu Ja'afar (At-Tabari) katika tafsiri yake amesema mfano wa maelezo haya. Bila shaka umekwisha fahamu kwamba (Kitendo) kilicho cha kufru hakitofautiani kwa kutofautiani sheria, wala Mwenyezi Mungu hakiamrishi kuwa kitendwe wakati fulani miongoni mwa nyakati, basi kusujudu kwa Malaika kumsujudia Adam wala sijda aliyosujudiwa Yusuf [a] hazikuwa ni kufru kwa kuwa waliosujudu hawakuwa wameitakidi itikadi ya mambo ambayo yanamuhusu Mwenyezi Mungu peke yake wakati walipowasujudia hao waliosujudiwa, bali Malaika waliposujudu (kumsujudia Adam) kwao ilikuwa ni ibada kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaamuru kufanya hivyo waliomsujudia Yusuf kwao ilikuwa ni maamkizi yaliyoruhusiwa, na ruhusa hiyo ilifutwa katika sheria yetu (ya Kiislamu).

Na wanachuoni wamehukumu kuwa, ni kufuru kwa yeyote mwenye kusujudia jua, au mwezi au sanamu, kwa kuwa kufanya hivyo ni alama za kufru ambayo ni kupinga mafunzo ya msingi katika dini kama ambavyo wamehukumu kuwa, mwenye kutamka shahada mbili ni mu'umini kwa hivyo ndizo dalili za imani, na imani ni kitu cha moyoni. Wamehukumu hivi sio kwa kuwa eti kile kitendo cha kwanza yaani kusujudia mwezi na jua kwa dhati yake ndiyo kufru na kile cha pili (kutamka shahada mbili) ndiyo imani.

Ikiwa kuna uzito wa kufahamu maelezo haya ambayo siyo mazito kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, hebu iangalie nafsi yako mwenyewe, huenda heshima na adabu uliyonayo kwa baba yako ikakuzuwia kukaa au kulala mbele yake, hivyo ukawa umesimama au kuketi kiasi saa moja au zaidi, na (kufanya hivi) haitakuwa ni ibada uliyomfanyia. Kwa nini basi?
Hii ni kwa sababu tendo lako hili halikuambatana na itikadi ya mambo ambayo ni maalum kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na utaposimama kiasi cha kusoma Sura Al-Fatihah, na ukakaa kiasi cha kusoma Tashahudi kwa kiasi cha dakika moja au mbili hivi na ikahesabiwa kuwa umefanya ibada kwa huyo uliyemsalia. Siri ya kuwa matendo haya ni ibada, ni kule kunyenyekea kwako kulikofanyika ndani ya kisimamo chako na kukaa kwako kuliko ambatana na itikadi ya Uungu wa yule uliyemnyenyekea ambaye ni Mwenyezi Mungu.

Na (kwa mfano) unamwita kiongozi wako katika kazi au amiri wako ili akusaidie dhidi ya mtu aliyekudhulumu, au akusaidie kutokana na shida iliyokufika na hali wewe hukuitakidi kuwa huyo umwitaye ana uwezo wake wa kujitegemea kuleta manufaa au kuondosha madhara lakini tu Mwenyezi Mungu amemfanya awe ndiyo sababu ya kupitishia mambo ya kawaida mikononi mwake kwa yale ayapendayo yeye Mwenyezi Mungu.

(Basi kuomba kwako msaada kwa kiongozi wako au amiri wako) haiwezi kuwa ni ibada kwa yule uliyemuomba kama tulivyokwisha eleza.

Lakini iwapo utamwita (akusaidie) hali ya kuwa unaitakidi kwamba yeye ndiye anayenufaisha kwa dhati yake au kudhuru au kupitisha maamuzi bila kupingwa kwa ombi hilo, itakuwa wewe ni mwenye kumuabudia yeye, na kwa ibada hii umemshirikisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kuwa umeitakidi ndani ya tendo hilo mambo yanayomuhusu Mwenyezi Mungu, kwani bila shaka kujitegemea kwa dhati, kuleta manufaa au kuondoa madhara na kupitisha maamuzi bila kipingamizi ni katika matendo makhususi ya Mwenyezi Mungu.

Na washirkina walikufuru kwa kuyasujudia masanamu na mfano wake kwa sababu ya kuyaitakidi masanamu hayo kuwa na uwezo wa dhati wa kujitegemea kunufaisha au kudhuru na kupitisha maamuzi bila kuyatenganisha na Mwenyezi Mungu japo kwa njia ya uombezi mbele yake kwani wao wanamuitakidi Mwenyezi Mungu kuwa ndiyo Mungu mkubwa na vile wanavyoviabudia ni waungu chini ya Uungu wa Mwenyezi Mungu, na kwa sababu ya uungu walionao imebidi wapitishe maamuzi wao na Mwenyezi Mungu bila kipingamizi.

Aya nyingi za Qur'an zinajulisha kama tulivyoeleza na kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

"Ni nani huyu ambaye ni mlinzi wenu atakayekusaidieni pasipo (Mwenyezi Mungu) mwingi wa Rehma, hawako makafiri ila katika kudanganyika." Qur'an, 67:20.

Na kauli yake nyingine aliposema: "Je, wanao Miungu wanaowalinda badala yetu, hawawezi kujisaidia wenyewe na wala hawatahifadhiwa kutokana nasi." Qur'an, 21:43.

Na Istif-hami iliyoko katika aya hizi mbili ni ya makemeo kwanjia yakuwalaumu katokana na yale waliyoitakidi. Pia Mwenyezi Mungu amesimulia habari za watu wa Nabii Huud [a] walipomwambia:
"Hatusemi ila ni kuwa baadhi ya Miungu yetu imekwisha kukutia katika balaa."
Qur'an, 11:54

Naye Nabii Huud alipowaambia: "Basi nyote nifanyieni hila (kunidhuru) na musinicheleweshe." Qur'an, 11:55-56.

Nyingine ni kauli yake Mwenyezi Mungu atakayosema kuwalaumu washirikina siku ya Qiyama kutokana na itikadi walizoziitakidi kwa masanamu ikiwa ni pamoja na kuamini kuwa yana uwezo wa kunufaisha na kupitisha maamuzi kama yapendavyo:

"Wako wapi mliokuwa mkiwaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu, Je, wanaweza kukusaidieni au kujisaidia wenyewe?" Qur'an, 26:92-93.

Nao washirkina watasema hali wakiwa motoni wakizozana na kuwaambia hao waliowaitakidi kuwa ni Miungu na wanazo khususiya za kiungu:

"Wallahi bila shaka tulikuwa katika upotofu uliodhahiri, tulipokufanyeni sawa na Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote." Qur'an, 26:97-98

Hebu angalia kulinganisha walikokiri (washirikina) kiasi kwamba muongo anasema kweli na muovu naye anajuta wakati majuto yake hayamsaidii kitu.

Bila shaka kulinganisha kulikotajwa ikiwa ni kwa ajili ya kuthibitisha kitu katika sifa za Uungu, basi hilo ndilo lengo na kutokana na hali hii ndipo unapatikana ushirikina wao na kufru yao, kwani sifa za Mwenyezi Mungu zinawajibisha upweke kwa maana ya kutokuwa na mfano wake kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kama ilivyotangulia kuelezwa.

Na kama kulinganisha huko ni katika kustahiki kwake ibada, basi italazimu kuitakidi ushirika katika yale ambayo ndani yake kuna ustahiki wa ibada, na huo ustahiki ni sifa za Uungu au baadhi ya sifa hizo, na ikiwa (kulinganisha) ni katika nafsi ya ibada yenyewe basi kitendo hicho hakifanywi na mtu mwenye akili ila kwa yule anayeitakidi kustahiki huyo mwenye kuabudiwa kama vile anavyostahiki Mola wa ulimwengu.

Basi ni vipi itakanushwa itikadi yao ya Uungu kwa miungu yao hali ya kuwa waliifanya kuwa niwashirika wa Mwenyezi Mungu na wakaipenda kwa mapenzi anayostahiki kupendwa Mwenyezi Mungu kama alivyosema yeye Mwenyezi Munga akieleza habari zao:
"Na miongoni mwa watu kuna wanaowafanya miungu wasiokuwa Mwenyezi Mungu, wanawapenda kwa mapenzi anayostahiki kupendwa Mwenyezi Mungu." Qur'an, 2:165.

Na neno "Andaad" lililotumika kwenye Aya hiyo hapo juu ni uwingi wa "Nidd" na maana yake ni kama walivyosema wataalam wa tafsiri na lugha.

Ama kauli ya Mwenyezi Mungu akiwazungumzia washirikina akasema: "Na ukiwauliza ni nani aliyewaumba, bila shaka watasema, ni Mwenyezi Mungu." Qur'an, 43:87.

Kauli hii na nyinginezo mfano wa hii maana yake siyo kwamba wao (washirikina) hawauthibitishi uungu wa miungu yao na yale mambo maalum yanayohusu uungu, bali maana yake ni kwamba, wanapohojiwa hukiri kutokana na ukweli ambao Mwenyezi Mungu ameziumbia nafsi (kumtambua). Lakini ni kwa kiasi gani wao hurejea haraka katika itikadi zao za waungu wa uongo kwa miungu yao, hurudi na katumbukia humo kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika aya nyingine.

"Wanazijua neema za Mwenyezi Mungu kisha wanazikanusha na wengi wao ni makafiri."
Qur'an, 16:83.

Na kauli nyingine ya Mwenyezi Mungu akizungumzia kikundi miongoni mwao:
"Kila wakirudishwa katika fitna, huangushwa humo." Qur'an, 4:91.
Kurudishwa katika fitna na kuangushwa humo siyo jambo la ajabu kutokea kwa wale walioyafanya matamanio yao kuwa miungu yao, nawe msomaji utawaona hao wenye matamanio hayo iwapo utamjadili katika Bid'a zake, atakusikiliza kwa makini na atakinaika (atatosheka) wakati wa majadiliano na atakiri kuwa amekwenda kinyume cha haki na ataonyesha dalili za uadilifu (katika majadiliano na matokeo yake). Kinapomalizika kikao cha mjadala hurudi kule kwenye mazoea ya matamanio na kurudia Bid'a yake kama kwamba hapakuwa na mjadala baina yako na yeye (isipokuwa waliorehemewa na Mwenyezi Mungu).

Na hali kama hii tumeiona mara nyingi kwa wale tuliokutana nao miongoni mwa wanaofuata matamanio. Tunamuomba Mwenyezi Mungu kwa fadhila zake atupe mafanikio.

Pamoja na yote haya, lau itakubalika kwamba (washirikina) hawakuitakidi kwa miungu yao kuwa na uwezo wa kuumba, kuruzuku wala kuendesha mambo, lakini wanaitakidi ndani ya miungu hiyo mambo yasiyokuwa hayo ambayo yanahusu mas-ala ya uungu nao ni wajibu wa kupitisha maamuzi wayatakayo.

Basi wao wanaona kuwa shafaa ya masanamu hayo inakubaliwa moja kwa moja hairudishwi na haitegemei idhini ya Mwenyezi Mungu. "Ametakasika sana Mwenyezi Mungu na yale wayasemayo wajinga."

Kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu amesema katika Qur'an akijibu madai yao haya:

"Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake (Mwenyezi Mungu) bila idhiniyake?"
Qur'an, 2:255.

Amesema Qadhi Nasirudin Al-Baidawi katika tafsiri ya aya hiyo, "Ni ubainifu wa utukufu wa mambo yake, na hiyo ni kwa sababu hakuna anayeungana naye au kumkurubia awezaye kutoa akitakacho iwe kwa shafaa au kunyenyekea, basi itakuwaje iwezekane kwa njia ya kumpinga": Hivyo basi iangalie kauli ya Baidawi aliposema; "Awezaye kutoa akitakacho ikiwa ni kwa Shafaa" utakuta ni dhahiri kuwa inahusu wajibu wa matakwa yake yakubalike kwanza kwa Mwenyezi Mungu na wajibu wa kupitisha maamuzi ni miongoni mwa mambo yanayohusu uungu kama inavyofahamika.

Na aina hii ya Shafaa ni Shafaa ya shirki ambayo Qur'an imeibatilisha, kwani kuiamini Shafaa ya aina hii ni kufru kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

"Au ndiyo wamejifanyia waombezi kinyume cha Mwenyezi Mungu?" Qur'an, 39:43.

Na kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
"Waambie, ni nani ambaye anaweza kukulindeni kutokana na Mwenyezi Mungu kama akikutakieni ubaya au (nani anayeweza kuzuwiya Rehma yake) kama akikutakieni Rehma?" Qur'an, 33:17.

Ama Shafaa ambayo wanaiitakidi watu wa Tauhidi na ndiyo iliyoletwa na Qur'an na Sunna, yenyewe iko mbali na itikadi ya Shafaa inayoitakidiwa na washirikina kama ulivyo umbali wa imani na kufru na umbali wa mwangaza na kiza.

Na Shafaa ya watu wa Tauhidi ni maombi ya mwenye kushufaiya kumuombea mwenye kushufaiwa, na Mwenyezi Mungu kwa fadhila zake humkubalia amtakaye na hiyo ndiyo maana ya Istith-nai katika kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema: "Isipokuwa kwa idhini yake."

Na maana ya idhini hapa ni kuridhia kama alivyosema kwenye aya nyingine: "Wala hawamuombei yeyote ila yule aliyeridhiwa (na Mwenyezi Mungu).. " Qur'an, 21:28.

Na nyingine tena: "Na wako Malaika wangapi mbinguni ambao uombezi wao hautafaa chochote isipokuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia." Qur'an, 53:26.

Na kwa maelezo haya inakubainikia tofauti baina ya yale iliyoyathibitisha Qur'an katika Shafaa na yale iliyoyakanusha (ambayo hayana idhini yake na radhi yake.) Mwenyezi Mungu ni mkubwa, hakifanyiki kitu katika ufalme wake ila yeye atake.

Ama Shafaa kwa idhini yake na radhi yake inayotokana na waja wake wema walio wateule kuwaombea wenye kuasi katika watu wa Tauhidi inafaa, na limethibiti hilo kwa njia ya mutawatir wala hapana kizuizi ndani yake na kuitakidi hivyo ni katika mambo ya dini, kwani jambo hili liko katika mlango wa Dua, naye Mwenyezi Mungu huwakubalia waaminio na wakatenda mema na huwazidishia fadhila zake.

Tunataraji itakuwa imeeleweka kwako msomaji (Insha-Allah) nini maana ya ibada kisheria, na wakati huo huo utakuwa umefahamu kuwa siyo ibada ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu pale Mwislamu anapotaka wasila kwa Mwenyezi Mungu.2

Basi haya yalikuwa ndiyo maneno yaliyoandikwa na Al Allamah Al-Qudhai, nasi tumeyaleta kutokana na faida nyingi zilizomo, na bila shaka tumeifafanua hali yake, ni juu yako ewe msomaji muadilifu kufanya uchunguzi.

  • 1. Ni miongoni mwa vitabu bora kilichotungwa katika zama za hivi karibuni, na mtunzi huyu pamoja na mwenziwe aitwaye Al- Ustadhi Muhammad Zahid AI-Kauthari Al-Misri ambaye ni mwanachuoni wa hadithi na muhakiki, ni miongoni mwa Wanachouni ambao walisimama kupinga uzushi wa Kiyahudi unaomshabihisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumfanyia mwili na upande na mahali. Kwa hakika uzushi huu ulianza kupata nguvu mwanzoni mwa Qarne ya nane kutoka mkononi mwa Sheikh wa Bid'a na upotofu aliyekuwa akiitwa: "Ahmad Abdil-Halim Ibn Taimiyyah Al-Jarrani na baada yake kupitia mkononi mwa mwanafunzi wake lbn Al-Qayyim, na baada ya wawili hao, kupitia kwa yule aliyekunywa makombo yao yaani Sheikh Muhammad Ibn Abdil-Wahab.

    Basi huyo mwanachuoni wa mwanzo alisimama akatunga Kitabu chake kiitwacho, "Fur-Qanul-Qur'ani akapinga uzushi huu (wa Ibn Taimiyyah na wenzake) na mwingineo miongoni mwake ikiwa ni kuzuwia (watu) kutawassal na kuomba msaada na kutaka shafaa kwa yule ambaye Mwenyezi Mungu amemjaalia kuwa mwenye kusaidia kwa idhini yake na mwenye kushufaiya kwa amri yake Mwenyezi Mungu, kama ambavyo yule mwanachuoni wa pili alisimama kwa kusambaza kitabu kiitwacho "Al-Asmau Was-sifatu" cha Al-Hafidh Abubakr Al-Bayhaqi ikiwa ni pamoja na kukihakiki na kukiwekea ufafanuzi wa utangulizi wenye manufaa, na vitabu hivi viwili vilichapishwa Misri Mwaka 1358 A.H. katika mjaladi mmoja. Basi Mwenyezi Mungu awalipe juhudi zao na juhudi za msambazaji wa vitabu vya haki.

  • 2. Fur-qanul-Qur'an, uk. 111-115