read

Matokeo Mazuri Yanayopatikana Kutokana Na Kuwazuru Watu Muhimu Wa Kidini

Makaburi yanayopata hadhi ya kutunzwa na kuheshimiwa na watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu katika ulimwengu - hasa Waislamu ni yale ambayo mara nyingi yanakuwa ni makaburi ya watu ambao wamebeba ujumbe wa amani na kuufikisha kama ilivyotakiwa ufike.

Watu hawa wamegawanyika sehemu tatu:

1. Manabii: Ambao ndiyo viongozi wa dini, walibeba mabegani mwao ujumbe kutoka mbinguni, walizitoa nafsi zao na mali zao pamoja na wanavyovipenda kwa ajili ya kufikisha ujumbe huo, na wakavumilia aina mbali mbali za taabu na matatizo ili wapate kuwaongoa watu.

2. Wanachuoni na wanafikra: Ambao ni kama mshumaa unaowangazia wengine wakati wenyewe unateketea.

Watu hawa waliishi maisha ya kichamungu na kujinyima na wakaupatia ulimwengu maelezo yenye thamani na uchambuzi mzuri, katika nyanja za elimu, fikra, tabia na elimu za maumbile na ufunuo kutoka mbinguni na elimu za ulimwengu, viumbe na mengineyo.

3. Mujahidina (wapiganaji Jihadi): Hawa ni wale wenye kupigania mabadiliko ambao walihuzunishwa na hali ya maisha ya jamii kutokana na dhulma na ubaguzi wa rangi na kabila na hawakuivumilia hali hiyo, wakapigana dhidi ya dhulma na ukandamizaji na wakadai heshima na haki za binadamu zilindwe, na wakajenga ngome ya uadilifu kwa kutoa damu zao zenye thamani kubwa.

Mapinduzi yoyote au mabadiliko ya jamii hayalinganishwi na kitu chochote isipokuwa kwa kutoa kitu cha thamani ili mafaniko yapatikane. Na thamani ya mapinduzi inayoweza kubomoa tawala za madhalimu na kuwasonga koo, ni kutoa damu tukufu ambayo wapiganaji mashujaa hujitolea muhanga kwa damu hiyo ili kurejesha haki na uhuru kwenye nchi za Kiislamu.

Kwa hiyo watu huwa wanazuru makaburi ya watu wa aina hizi, na hutokwa machozi wawapo makaburini na huwa wanakumbuka ushujaa wao na kujitoa kwao muhanga, pia huziliwaza roho za mashujaa hao kwa kusoma Qur'an kisha kuwazawadia thawabu za visomo hivyo.

Kadhalika huimba Qasida ambazo hutaja sifa zao na utukufu wao na kiwango cha daraja zao tukufu. Hakika kuzuru makaburi ya watu hawa muhimu ni moja katika aina ya kuwashukuru na kuwatukuza kwa kujitolea kwao na pia kujulisha kizazi kilichopo kuwa, hayo ndiyo malipo ya wale ambao hupita njia ya haki na uongofu na ubora, na ndiyo malipo ya wale wanaopigana na kulinda misingi ya itikadi (Uislamu).

Malipo yao ni kudumu kwa utajo wao, utajo ambao ni mwema na sifa nzuri hata kama ni muda mrefu umepita toka kufariki kwao.

Mpaka hapa tumefahamu umuhimu wa kuhuyisha utajo wa watu hawa muhimu wa dini, na kwa msingi huu inapasa kufanya juhudi ili kuendelea kuzifanya kumbukumbu zao kuwa hai na kuzihifadhi na kusimamisha sherehe kubwa za kukumbuka siku za kuzaliwa kwao na kuvaa mavazi ya kuonyesha msiba na kufanya hafla za kuomboleza na kukumbuka kufa kwao, pia kufanya vikao na mikusanyiko mikubwa na kutoa hotuba za kuwatambulisha watu hao watukufu na itikadi zao zilizopelekea wao wajitoe muhanga.

Kadhalika kuyaheshimu malazi yao (makaburi) na kujiepusha na kila linalotia dosari heshima yao, kwani kuyaheshimu makaburi yao ndiko kuheshimu ujumbe wao na itikadi zao.

Kinyume cha hivyo ni kuyadharau na kuyapuuza makaburi yao, na itakuwa ndiyo kuudharau ujumbe wao na ni kuwadharau wao wenyewe.

Katika siku zetu hizi, mtu anapoingia katika makaburi ya Baqii ili akazuru makaburi ya watu wa kizazi cha Mtume [s] na makaburi ya viongozi wa Kiislamu na watetezi wa dini na Masahaba, atayaona makaburi hayo yako katika hali inayohuzunisha kutokana na dharau yaliyofanyiwa, jambo ambalo linatetemesha nafsi na kuifanya ishangazwe na uovu wa kikundi cha Mawahabi ambao wanadai kuwa wao ndiyo watetezi wa Uislamu.

Ajabu ni kwamba, kwa upande mmoja Mawahabi huwataja masahaba kwa wema na kuwasifu katika majukwaa ya hotuba zao, lakini kwa upande wa pili wanayaacha makaburi ya Masahaba bila ya heshima yoyote, na katika hali ya kusikitisha katika kuyadharau na kuyapuuza makaburi hayo, Mawahabi hawayajali kabisa hata kama wanyama wataingia na kuharibu sehemu ya makaburi ya Masahaba.

Zawadi ya pekee ambayo Mawahabi huwapatia mahujaji na wanaozuru (makaburi ya Baqii) ni kuwaita kuwa ni washirikina na tendo lao la kuyazuru makaburi hayo ni tendo la shirki.

Mawahabi wanawaambia Waislamu maneno (haya machafu) kwa sababu tu Waislamu hao wanawaheshimu viongozi wa dini, na wanawatukuza Mawalii wa Mwenyezi Mungu.

Hali hii inaonyesha kwamba, Mawahabi wanaficha mioyoni mwao chuki na kero waliyonayo dhidi ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu na viongozi wa dini yake. Na sasa umefika wakati wa kuzungumzia ziyara ya kaburi la Mtume [s] kwa mujibu wa mtazamo wa dalili za Kiislamu.

Kuzuru Kaburi La Mtukufu Mtume

Katika maelezo yafuatayo tutatoa baadhi ya aya za Qur'an na hadithi tukufu za Mtume [s] ambazo zinahimiza kulizuru kaburi lake. Na tunataraji kuwa msomaji atapata maelekezo zaidi na kufahamu.

Ushahidi Wa Qur'an

Qur'an tukufu inawaamrisha wenye madhambi wafike mbele ya mjumbe wa Mwenyezi Mungu na wamuombe awaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu, kwani dua au maombi ya Mtume yatakubaliwa kwa ajili yao.

Mwenyezi Mungu anasema:
"Na lau wangelikuja kwako walipojidhulumu nafsi zao wakaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu, na Mtume pia akawaombea msamaha, bila shaka wangelimkuta Mwenyezi Mungu ni mwenye kupokea toba tena mwenye kurehemu." Qur'an, 4:64.

Lau aya hii ingekuwa ndiyo pekee katika mada hii, basi tungelisema kuwa inahusika tu katika zama za uhai wa Mtume [s] na ni kwa kipindi kile tu cha yeye kuwepo miongoni mwa watu. Lakini sisi tunachukua hukmu ya jumla inayoenea, ambayo haimuwekei Mtume mpaka wa mwisho kwa maisha yake ya dunia.

Hukmu hiyo iko katika maelezo yafuatayo:

Kwanza: Qur'an inabainisha kuwa, Manabii, Mawalii na baadhi ya watu wengine wako hai katika Bar-zakh (uhai baada ya kufa) na inawazingatia kuwa wanaona na wanasikia katika huo ulimwengu wa Barzakh.

Tutazionyesha hizo aya zinazobainisha jambo hili katika sehemu ya kuzungumzia kutawassal kwa roho tukufu.

Pili: Hadithi tukufu zinabainisha kwamba, Malaika humfikishia Mtume [s] salamu za yeyote anayemsalimia.

Imekuja hadithi katika Sihah:
"Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Hapana yeyote atakayenisalimia, isipokuwa Mwenyezi Mungu hunirudishia roho yangu mpaka nami nimrudishie salamu."1

Na amesema Mtume [s]:
"Niswaliyeni, kwani swala zenu zinanifikia (kutoka) popote mlipo."2

Tatu: Waislamu wamefahamu tangu siku hizo kwamba maana ya aya tuliyotangulia kuitaja inaendelea kutumika na wala haikomi kwa kufariki Mtume [s], kiasi kwamba kuna baadhi ya mabedui (kwa mujibu wa fikra zao nzuri) walikuwa wakilikusudia kaburi la Mtume na wanalizuru na wanaisoma aya hii kaburini kwa Mtume na kumuomba awatakie msamaha.

Ametaja Taqiyyud-din As-Subaki katika kitabu kiitwacho "Shifaus-siqami" na pia As-Samhudi katika kitabu kiitwacho "Wafa-ul Wafa" mifano mbali mbali ya Waislamu kuzuru kaburi la Mtume [s] na kusoma kwao aya hii mbele ya kaburi lake tukufu.

Tunataja baadhi ya mifano kama ifuatavyo:

Amepokea Sufyan bin Anbar kutoka kwa Al-Utbi, na wawili hawa ni Masheikh wa Imamu Shafii na ni waalimu wake, kwamba yeye amesema, "Nilikuwa nimekaa kwenye kaburi la mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s], mara akaja bedui mmoja akasema:

"As-Salaamu Alaika ya Rasulallah, nimemsikia Mwenyezi Mungu akisema: "Na lau wangelikuja kwako walipojidhulumu nafsi zao wakaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na Mtume pia akawaombea msamaha, bila shaka wangelimkuta Mwenyezi Mungu ni mwenye kupokea toba tena mwenye kurehemu." Nami nimekujia mwenye kutaka msamaha kutokana na dhambi zangu mwenye kutaka Shafaa kwako (uniombee) kwa Mola wangu."
Kisha bedui yule akalia, na akawa anasema:

"Ewe mbora wa waliozikwa ardhini, kwa uzuri wako ardhi na mimea (iliyopo hapa) vimependeza, nafsi yangu iwe fidia ya kaburi ulilomo, ndani yake kuna utakatifu na kuna kila ukarimu na ubora". Kisha bedui yule akaomba msamaha na akaenda zake.3 [91]

Naye Abu Said As-Sam-ani anapokea kutoka kwa Imam Ali bin Abi Talib [a] kwamba, bedui mmoja alikuja Madina baada ya siku tatu tangu Mtume [s] azikwe, akajitupa kwenye kaburi tukufu la Mtume akajipaka udongo wa kaburi kichwani mwake na akasema: "Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu, ulisema nasi tukaisikia kauli yako, umepokea kwa Mwenyezi Mungu mambo ambayo tumeyapokea kwako na katika aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu ni "Na lau wangelikuja kwako walipojidhulumu nafsi zao.... nami nimedhulumu nafsi yangu na nimekuja ili unitakie msamaha kwa Mola wangu."4

Yote haya yanajulisha cheo kikubwa alichokitoa Mwenyezi Mungu kwa Mtume [s] kama ilivyobainisha aya hii kwamba cheo hicho siyo makhsusi katika uhai wake tu, bali inatia mkazo kuwa kinathibiti hata baada ya kufa vile vile.

Kwa ujumla Waislamu wanazizingatia aya zote zilizoshuka kwa ajili ya kumtukuza Mtume [s] kwamba, zinakusanya kipindi cha uhai wake na baada ya kufa, na hapana yeyote anayezihusisha katika wakati wa uhai wake tu.

Na katika historia imekuja kwamba: Alipouawa Imam Hasan bin Ali [a] na mwili wake Mtukufu ukaletwa ndani ya msikiti wa Mtume [s], Banu Ummayya walidhani kwamba Banu Hashim wanataka kumzika karibu na kaburi la Babu yake, wakaeneza fitna na makelele ili asizikwe karibu na Babu yake.

Imam Husein [a] akasoma kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:
"Enyi mulioamini, musipaze sauti zenu kuliko sauti ya Mtume." Qur'an, 49:2.

Hakuna mtu yeyote aliyempinga Imam Husein [a] eti kuwa aya hii inahusu zama za uhai wa Mtume [s], hata hao Banu Ummayya hawakuthubutu. Na leo hii utawaona Mawahabi wameiandika aya hii na kuiweka kwenye ukuta unaokabiliana na kaburi la Mtume [s] hali ya kuwa wanakusudia kuzuwiya watu wasipaze sauti zao mahala hapo.

Na kwa mtiririko huu tunaweza kutoa maana pana zaidi ya aya hii, nayo ni kwamba, ni juu ya Waislamu wa leo kusimama mbele ya kaburi la Mtume [s] na wamuombe Mtume awatakie msamaha kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa hiyo kumzuru Mtume [s] hakuna maana isipokuwa kufanya yale ambayo yamo katika aya hii na zinginezo.

Aya hii inajulisha maudhui mbili nazo ni:
1. Mtu anawajibika kusimama kwenye kaburi la Mtume [s] baada ya kufa kwake na kumuomba Mtume amtakie msamaha kwa Mwenyezi Mungu.

Tutafafauna maudhui haya wakati wa uchambuzi kuhusu kutawassal kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, Insha-Allahu Taala.

2. Aya hii inashuhudia kuweko ruhusa ya kuzuru kaburi la Mtume [s] kwani ukweli wa ziyara huwa hauna maana isipokuwa mwenye kuzuru afike pale alipo anayemzuru.

Basi ikiwa kusimama mbele ya kaburi la Mtume [s] na kumuomba atutakie msamaha kwa Mwenyezi Mungu ni jambo linalojuzu, bila shaka yatathibiti mambo mawili:

1. Tutakuwa tumemuomba atuombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu.
2. Tumefika mbele yake na tumemsemesha.
Na maana ya ziyara hakuna isipokuwa mambo haya mawili.

Dalili Nyingine

lj-mai ya Waislamu juu ya hukmu fulani miongoni mwa hukmu za kisheria katika zama mbali mbali, huwa inazingatiwa kuwa ni dalili iliyo wazi kabisa ya kusihi kwa hukmu hiyo na kuthibiti kwake.

Na ziyara kwenye kaburi la Mtume [s] ni miongoni mwa mambo haya na unadhihiri ukweli wa mambo iwapo tutarejea vitabu vya hadithi, Fiqhi, Akhlaq na Historia na hasa sehemu zinazohusu ibada ya Hija katika vitabu hivyo.

Ameutaja ubora wa kuzuru kaburi la Mtume [s] Al-Marhum Al-Allama Al-Amini kutoka katika rejea arobaini na mbili zikiwa ni miongoni mwa rejea muhimu za elimu za Kiislamu.

Ndani ya kitabu chake kiitwacho Al-Ghadir kwenye juzuu ya tano ukurasa wa 106 mpaka ukurasa wa 129, amezitaja nassi na ibara zinazohusu maudhui hii kwa undani sana.

Miongoni mwa vitabu ambavyo tumevitegemea kutolea ushahidi kuhusu mada hii ni kama ifuatavyo:

1. Shifaus-siqami fi Ziyarati Khairil-Anami, kilichoandikwa na Taqiyyud-din As-Subaki as-Shafii, aliyefariki mwaka 706 A.H. Ndani ya Kitabu chake hiki ametaja mkusanyiko wa maneno ya wanachuoni walioboresha ziyara ya kuzuru makaburi na kuisisitiza sana.

2. Wafa-ul Wafa, kilichoandikwa na As-Samhudi aliyefariki mwaka 911 A.H., naye ametaja katika kitabu chake maneno ya wanachuoni katika kuboresha na kupendekeza ziyara.

3. Al-Fiqhu Alal-madhahibil-ar-baa, kilichotungwa na wanachuoni wanne wa Madhehebu manne, na wamekusanya ndani ya kitabu hicho Fatwa za Maimamu wa Madhehebu manne mashuhuri kwa Masunni.

Wanachuoni hawa wanasema:

"Kulizuru kaburi la Mtume [s] ni sunna iliyo bora kuliko Sunna zote kwani hadithi nyingi zimekuja juu ya jambo hili."5

Sasa umefika wakati wa kutaja baadhi ya hadithi zilizopokelewa na wanahadithi kuhusu kuzuru kaburi la Mtume [s].

  • 1. Sunan Abi Dawuud, juz. 1, Kitabul-Haj Babu Ziyaratil-Qubur, uk. 470-471.
  • 2. At-Tajul-Jamiu Lil-Usuli Fiahadithir-Rasuli, kilichoandikwa na Sheikh Mansur Ali Nasif, juz. 2, uk. 189.
  • 3. (1) Wafa-ul Wafa, juz. 4, uk. 1361. (2) Ad-durarus-Saniyyah cha Ahmad Dah-lan uk. 21.
  • 4. Al-Jauharul-munadham cha Ibn Hajar; Na ameitaja As-Samhudi katika Wafa-ul Wafa, juz. 2, uk. 612, na katika Ad-durarus-saniyya cha Dah-lan, uk. 21.
  • 5. Al-Fiqhu Alal-madhahibil-ar-baa, juz. 1, uk. 590