read

Taarifu Kamili Ya Maana Ya Ibada

Bila shaka maana na Maf-humu ya Ibada iko wazi katika lugha ya Kiarabu, na lau tutakwa hatuwezi kuiarifisha "Ibada" kwa Taarifu ya kimantik kwa kutumia neno moja, basi ni kama mbingu na ardhi ambazo zina maana mbili zilizowazi, wakati ambapo wengi katika sisi hawawezi kutoa taarifu kamili kwa kutumia neno moja lakini hali hii haizuwii kujengeka maana ya ardhi na mbingu katika akili zetu tunapoyasikia matamko hayo.

Bila shaka basi, maana ya Ibada ni kama maana ya ardhi na mbingu ambayo inafahamika kwetu sote, pamoja na kutokuweza kuziarifisha mbingu na ardhi kwa taarifu ya kimantiki:

Kwa hiyo basi "Ibada" na "Kutukuza" na "Kuheshimu" na "Kukirimu" ni matamko mbali mbali yenye matawi yanayofahamika, na kuyachambua ni jambo rahisi tena jepesi.

Kwa hakika mtu ambaye anampenda yeyote yule kwa mapenzi ya kweli kabisa, utamuona akibusu kuta za nyumba ya mpenzi wake na kunusa mavazi yake na kuyakumbatia kifuani, na atapokufa (mpenzi wake huyu) atalibusu kaburi lake na udongo wa kaburi hilo....

Pamoja na matendo yote haya, hapana yeyote atakayeona kuwa matendo yake huyu mwenye kupenda ni ibada amfanyiayo yule mpenzi wake.

Hali hii ni kama ile ya watu kukimbilia kwenda kuona miili ya viongozi iliyomo ndani ya majeneza, au kuona kumbukumbu zao na majumba walioyokuwa wakiishi na kusimama dakika chache kuonyesha huzuni kwa ajili ya roho zao; yote haya hayazingatiwi kuwa ni ibada katika Taifa lolote miongoni mwa mataifa ulimwenguni, japokuwa mapenzi yao na unyenyekevu wao kwa watu hao uko katika kiwango cha unyenyekevu wa waumini kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Hivyo basi, watu wenye maarifa na wachambuzi wa mambo ndiyo ambao wanaweza kupambanua baina ya kuheshimu na ibada.

Ewe msomaji mtukufu iwapo tutataka kutoa taarifu ya ibada kimantik, basi ibada itakuwa na taarifu za aina tatu na zote hizi zitalenga maana moja.

Ama Mawahabi wao wamechagua Taarifu mbili nyingine na wakazitegemea, lakini zinaupungufu hazikukamilika. Katika maelezo yafuatayo tunazileta hizo Taarifu zao ili tuzijadili.

Taarifu Mbili Pungufu Kuhusu Ibada

A: Ibada ni kunyenyekea na kudhalilika.
Ndani ya vitabu vya lugha, Taarifu ya ibada imekuja kwa maana ya kunyenyekea na kudhalilika. Na maana hii imekuja katika Qur'an tukufu lakini Taarifu hii ya Ibada haitoi maana ya ibada kwa undani, na hiyo ni kwa sababu zifuatazo:

Ikiwa ibada inakubaliana katika maana na kuwa ni kunyenyekea na kudhalilika, basi haitawezekana kwa mtu yeyote kumzingatia kuwa anampwekesha Mwenyezi Mungu, kwani mtu kwa maumbile yake humnyenyekea Mwalimu wake na mtoto naye huwanyenyekea wazazi wake wawili na kila mpenzi kwa ampendaye.

Bila shaka Qur'an Tukufu ina-amuru mtu adhalilike kwa wazazi wawili inasema:

"Na wainamishie Bawa la udhalili kwa kuwaonea huruma na useme, Mola wangu wahurumie (wazazi) wangu kama walivyonihurumia mimi nilipokuwa mdogo."
Qur'an, 17:24

Basi iwapo unyenyekevu na udhalili maana yake ni kumfanyia ibada uliyemdhalilikia, basi italazimu kumhukumu ukafiri yeyote anayelea wazazi wake wawili na kinyume chake itakuwa ni lazima kumhukumu kuwa ni mtu wa Tauhidi yule anayewatelekeza wazazi wake na kutowafanyia wema.

B: Ibada ni ukomo wa kunyenyekea.
Baadhi ya wafasiri walijaribu kuitengeneza na kuirekesbisha Taarifu ya ibada ya kilugha pale walipogundua kuwa inaupungufu wakasema:
"Ibada ni ukomo wa kunyenyekea kwa yule ambaye utukufu wake na ukamilifu wake unafahamika."

Taarifu hii inashirikiana na ile ya kwanza katika upungufu na utata.

Mwenyezi Mungu anawaamuru Malaika wamsujudie Adam anasema:

"Na kumbuka tulipowaambia Malaika, msujudieni Adam, wakasujudu wote isipokuwa Iblisi...." Qur'an, 2:34

Bila shaka kusujudu ndiyo ukomo wa kudhalilika na kunyenyekea kwa yule unayemsujudia, basi ikiwa maana ya ibada ni ukomo wa kunyenyekea italazimu kuwakufurisha Malaika waliotekeleza amri ya Mwenyezi Mungu, na Iblisi kwa kupinga kwake amri ya Mwenyezi Mungu atakuwa ndiyo mwenye imani.

Hakika ndugu wa Nabii Yusuf na wazazi wake Nabii Yusuf wote walimsujudia Yusuf kama asemavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Na waliporomoka wote kumsujudia, (Naye Yusuf) akasema: Ewe Baba yangu hii ndiyo Tafsiri ya ndoto yangu ya zamani bila shaka Mwenyezi Mungu ameithibitisha."
Qur'an, 12:100.

Ndoto aliyoiashiria Nabii Yusuf katika Aya hii, ni ile iliyoko katika kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema:
"(Kumbuka) Yusuf aliopomwambia Baba yake, Ewe baba yangu hakika nimeona (ndotoni) nyota kumi na moja na jua na mwezi vinanisujudia." Qur'an, 12:4.

Ni hakika (isiyopingika) kwamba Waislamu wote kwa kufuata mwendo wa Mtume [s] huwa wanalibusu "Hajarul-Aswad". Jiwe jeusi lililoko kwenye kona ya Kaaba Tukufu na pia hutaka baraka kwenye jiwe hilo.

Kitendo kile kile hufanywa na waabuduo sanamu kwenye masanamu yao jambo ambalo moja kwa moja ni shirki, lakini tendo la Waislamu kwenye Hajarul-Aswad ni tendo la Tauhidi bila shaka yoyote.

Kwa hiyo, maana ya ibada siyo ukomo wa kunyenyekea na kudhalilika ingawaje (kunyenyekea na kudhalilika) hakika ni miongoni mwa nguzo za Ibada lakini siyo kwamba hizo ndiyo nguzo pekee za ibada. Hivyo basi, hapana budi pasemwe kuwa, Ibada maana yake ni kunyenyekea na kudhalilika kunakoambatanishwa na itikadi maalum, kitu ambacho kitaifanya ibada iwe imeundika katika misingi miwili.

1. Kunyenyekea na kudhalilika.
2. Itikadi maalum.

Na hii itikadi maalum ndiyo ambayo inaweka msimamo wa kufafanua Qadhiya ya ibada, kwani kunyenyekea japo si sana, ikiwa kutaambatanishwa na itikadi maalum, basi itakuwa ibada.

Kwa hakika "Itikadi Maalum" ndiyo inayokivalisha kitendo vazi la Ibada, na bila itikadi hiyo maalum ibada haithibitiki japo itadhihirika katika hali ya Ibada.

Na sasa baada ya kuwa tumethibitisha ubatili wa Taarifu mbili ambazo Mawahabi wamezitegemea, na umedhihiri upungufu wake na udhaifu wake, umefika wakati wa kuzungumzia zile Taarifu tatu.

Sasa suali ni je, ni nini hiyo "Itikadi maalum" ambayo inaitenganisha ibada na visivyokuwa ibada?

Jawabu lake: Kwa hakika ukweli na usahihi, hapa ndipo mahali pa uchambuzi na uhakiki, na jawabu lake litaonekana ndani ya Taarifu tatu zifuatazo:

Taarifu ya Kwanza: Ibada ni kunyenyekea kimatendo au kimatamko, ambako kunatoka ndani ya itikadi ya mtu kwa ajili ya Uluhiyyah (Uungu).

Nini maana ya Uluhiyyah?.. nukta hii ni muhimu sana kwa hiyo ni lazima kuieleza.

Jibu: "Uluhiyyah" ni tamko litokanalo na neno "Al-Ilahu" na hilo neno "Al-Ilahu" ndiyo Allah kwa tamko la nakira, (naye ndiyo muumba mtukufu).

Na ilivyokuwa neno "Al-llahu" hupata likafasiriwa kwa maana ya mwenye kuabudiwa, basi tafsiri hiyo hiyo ni tafsiri ya kulazimiana, yaani Uluhiyyah unalazimu kuabudiwa siyo kwamba Ilahu maana yake ni mwenye kuabudiwa.

Bila shaka watu wanaoitakidi Ilahu vile vile wanaitakidi kuwepo ulazima wa kumuabudia, sawa sawa ikiwa ni Ilahu wa haki kama alivyo Mwenyezi Mungu au akawa siyo wa haki kama illvyo miungu isiyokuwa Mwenyezi Mungu.

Kwa hiyo neno Al-Ilahu hufasiriwa kwa maana ya chenye kuabudiwa kutokana na hali hii tu basi.

Dalili iliyowazi kuhusu taarifu hii ni Aya za Qur'an zilizokuja kuzungumzia nyanja hii.

Katika mazingatio ndani ya aya hizo inatudhihirikia kwamba "Ibada" na matendo na maneno yanayotokana na Itikadi za Uungu, na kwamba Itikadi hii inapokosekana, basi maana ya Ibada haithibitiki, na ndiyo maana utaiona Qur'an wakati inapoamuru ibada ya Mwenyezi Mungu, basi haraka sana hutoa maelekezo kwamba, hapana mungu asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Kwa mfano isema:
"Enyi watu wangu, muabuduni Mwenyezi Mungu ninyi hamna Mungu ila yeye."

Madhumuni ya aya hii yamekuja katika sehemu tisa ndani ya Qur'an au zaidi, nawe msomaji mpendwa unaweza kuzirjea aya hizi katika Surat A'araf aya ya 65, 73 na 58. Pia Surat Huud aya ya 5, 61 na 84, vile vile Surat Anbiyah aya ya 25, kadhalika Surat Mu’uminnuna aya ya 23 na 32 na Surat Taha aya ya 14.

Ibada zote hizi zinajulisha kwamba, ibada ni kule kunyenyekea na kudhalilika kunakotokana na itikadi ya kuitakidi Uluhiyyah na bila itikadi hii tendo hilo halitaitwa Ibada.

Hebu angalia aya zaidi zinazojulisha makusudio hayo.

Anasema Mwenyezi Mungu:
"Hakika wao walipokuwa wakiambiwa, hapana Mungu (Mwingine) ila Mwenyezi Mungu wao Hupinga." Qur'an, (As-Safaat) 37:35.

Ni kwa nini walikuwa wakipinga? Ni kwa sababu wanaitakidi waungu wasio Mwenyezi Mungu na wanawaabudu.

Na anasema Mwenyezi Mungu:

"Au wanaye Mungu mwingine asiye Mwenyezi Mungu, ametakasika Mwenyezi Mungu kutokana na hao washirikina hao wanaowashirikisha." Qur'an, 52:43.

Qur'an inawazingatia watu hawa kuwa ni washirikina kwa kuwa wanaitakidi uungu kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Anasema tena Mwenyezi Mungu: "Wale ambao wanafanya pamoja na Mwenyezi Mungu; Mungu Mwingine basi hivi karibuni watajua." Qur'an,15:96.

"Na wale ambao hawamuombi mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu .. " Qur'an, 25:68.

Na miongoni mwa aya zinazojulisha kwamba maombi ya Washirikina yalikuwa yakiambatana na itikadi ya uungu kwa masanamu yao ni hizi zifuatazo:

"Waliwafanya waungu wengine badala ya Mwenyezi Mungu ili wawe wenye nguvu."
Qur'an, 19:81.

"Je, ninyi mnashuhudia kwamba kuna waungu wengine pamoja na Mwenyezi Mungu."
Qur'an, 6:19.

"Na (kumbukeni) Ibrahimu alipomwambia Baba yake Azar. 'Unawafanya Masanamu kuwa ni waungu." Qur'an, 6:74.

Mazingatio katika aya zinazozungumzia shirki yawatu wanaoabudu sanamu yatatudhihirishia ukweli huu, nao ni kuwa ushirikina wa watu hawa umekuja kwa sababu ya kuitakidi kwao uungu wa masanamu yao waliyokuwa wakiyaabudu, na kwamba masanamu hayo ni miungu wadogo ambao Mungu mkubwa amewapa baadhi ya mambo yanayomstahiki, basi (masanamu hayo) yameumbwa na wakati huo huo yanaabudiwa. Na kwa ajili hii basi walikuwa wakiikataa Tauhidi.

Qur'an inasema: "Hii ni kwa sababu mlikuwa akitajwa Mwenyezi Mungu peke yake mnakanusha, na akishirikishwa mnaamini, basi (leo) hukumu ni yake Mwenyezi Mungu Mtukufu aliye mkuu." Qur'an, 40:12.

Na kwa ajili hii mfasiri mkubwa mar-hum Ayatullah Sheikh Muhammad Jawad Al-Balaghi ametoa Taarifu nzuri ya "Ibada" katika tafsiri yake madhubuti iitwayo Aalaur-Rahman anasema:

"Ibada: Ni hisia ya unyenyekevu wanayoifanya kwa ajili ya yule wanayemfikiria kuwa ni Mungu wake ili atimize haki yake makususi ya uungu.1

Bila shaka marehemu Al-Balaghi ametoa mtazamo wake wa kielimu kutokana na ufahamu wa kimaumbile juu ya neno "Ibada" katika msingi wa tamko, ndipo ilipokuja Taarifu hii inayokubaliana na aya za Qur'an.

Taarifu ya Pili ya Ibada: Hakika Ibada ni kunyenyekea mbele ya yule ambaye (Mwenye kunyenyekea) humzingatia kuwa ndiyo Rabbi (Mola).

Na tunaweza kuiarifisha ibada kama ifuatavyo; Ibada ni kunyenyekea kimatendo au kimaneno kwa yule anayeitakidiwa kuwa Mola basi kuabudiwa kunalazimiana na kuwa Mola na ikiwa mtu atajiona yeye mwenyewe kuwa ni mja kwa yule anayemuitakidi kuwa ni Mola wake kwa kuumba; sawa sawa Mola huyo akiwa ni kwa hakika au hapana, na akamnyenyekea pamoja na itikadi hii basi atakuwa amemuabudia.

Na katika Qur'an Tukufu kuna aya zinazofahamisha kuwa ibada ni miongoni mwa mambo ya umola yaani "Ar-rububiyyah".

Hebu ziangalie baadhi ya hizo aya:

"Naye Masihi alisema, Enyi wana wa Israeli, mwabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu na Mola wenu." Qur'an, 5:72.

"Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mola wangu na ni Mola wenu. Basi muabuduni hii ndiyo njia iliyonyooka." Qur'an 3.51.

Na aya nyinginezo zaidi ya hizi. Na kuna aya nyingine zinazoizingatia Ibada kuwa ni miongoni mwa mambo ya muumba kama ilivyo katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema:

"Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu, hakuna anayeabudiwa kwa haki ila yeye muumba wa kila kitu, basi muabuduni." Qur'an 6:102.

Nini maana ya neno (Ar-Rabbu)? Neno Rabbu hutumika katika lugha ya Kiarabu kwa yule aliyetegemezewa uangalizi wa kitu fulani na yakaachwa mikononi mwake matokeo au ukomo wa kitu hicho.

Basi iwapo neno hili litatumika kwa mtu anayemiliki nyumba na au anayemiliki ngamia au mlezi wa mtoto na mkulima na wengineo, basi hiyo ni kwa sababu wanamiliki kuendesha kitu hicho na kusimamia majukumu yake.

Nasi tunapomzingatia Mwenyezi Mungu kuwa ni "Ar- Rabbu" ni kwa sababu mambo yetu na mwisho wetu kama vile mauti, uhai, rizki, afya na uwekaji wa sheria pia msamaha na mambo mengineyo, yote yako mikononi mwake Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Sasa basi lau kuna mtu ataitakidi kwamba, moja katika mambo haya au yote, Mwenyezi Mungu amempa mtu fulani (ayasimamie), basi maana ya itikadi hii ni kwamba kumzingatia huyo mtu kuwa ni "Rabbu" na kumuamini Rabbi huyu na kumnyenyekea itakuwa ni kumuabudia.

Kwa maneno mengine tunasema, "Bila shaka ibada inatokana na hisiya za mtu kujiona kuwa yeye ni mja (mtumwa) na hii ndiyo hakika ya ubudiyah na ni mtu kuizingatia nafsi yake kuwa amemilikiwa na yuko juu yake aliyemmiliki, kuwepo kwake na kifo chake na uhai na rizki yake na mengineyo.

Au kwa uchache akamfanya huyo aliye juu yake kuwa ni mwenye kumiliki uwezo wa kusamehe:

(1) Mwenyezi Mungu Anasema: "Nani anayesamehe madhambi isipokuwa ni Mwenyezi Mungu." Qur'an 3:135.

(2) Mwenyezi Mungu Anasema: "Waambie Shafaa ni ya Mwenyezi Mungu." Qur'an 39:44.

(3) Mwenyezi Mungu Anasema: "Waliwafanya Makasisi wao na watawa wao kuwa ni Mola badala ya Mwenyezi Mungu.. " Qur'an 9:31.

Na Shafaa, na kumuwekea Kanuni (za maisha yake) na wajibu mwingineo, basi kwa ajili hiyo atakuwa amemfanya kuwa ni "RABBU" mlezi wake.

Kwa hiyo yeyote ambaye atakayeamini na kuitakidi katika nafsi yake (kama tulivyoeleza hapo kabla) na akaifasiri itikadi hiyo kwa maneno na matendo, basi hapana shaka kwamba anamuabudu huyo aliyemzingatia kuwa ni "Rabbu".

Taarifu Ya Tatu Ya Ibada

Hapa tunaweza kutoa Taarifu hii ya tatu ya ibada inayopatikana kutokana na maumbile na nguvu ya nafsi.

Tunasema: "Ibada ni kumnyenyekea yule ambaye tunamzingatia kuwa Mungu na ndiyo asili ya matendo ya kiungu."

Hapana shaka kwamba matendo ambayo yanahusiana na ulimwengu, kama vile kusimamia uendeshaji wa ulimwengu na kuhuisha na kufisha na kugawa rizki baina ya viumbe na kusamehe madhambi yote haya yanamuhusu Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Nawe (msomaji) lau utazizingatia vyema aya za Qur'an zinazozungumzia maelezo tuliyotangulia kuyataja, katika Aya ya 35 Surat Al- Qasas, Aya ya 60 mpaka Aya ya 64 Surat An-Namli, Aya ya 5 na ya 6 Sura Az-Zummar. Utaona kwamba Qur'an inasisitiza kwa nguvu sana kuwa matendo haya yanamuhusu Mwenyezi Mungu tu na wala hayamuhusu mwingine asiyekuwa yeye.

Hii ni kwa upande mmoja, ama kwa upande wa pili:

Sote tunafahamu kwamba ulimwengu wa viumbe ni ulimwengu uliopangwa vyema kabisa, na hakiwezi kutokea kitu isipokuwa sababu ya kutokea kwake itarejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Qur'an Tukufu inaonyesha (ukweli) wa jambo hili.

Mwenyezi Mungu anasema: "Na ni yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye anayehuisha na kufisha, na mabadiliko ya usiku na mchana yamo katika milki yake." Qur'an, 23:80.

Katika mahala pengine Mwenyezi Mungu anasema kwamba miongoni mwa Malaika wapo wanaosimamia utoaji wa Roho.

Nayo ni kauli yake isemayo: "Hata pale mmoja wenu anapofikiwa na mauti wajumbe wetu humfisha." Qur'an, 6:61.

Kwa kuijengea hali hii, inawezekana kuzikusanya aya hizi mbili na tukasema kama ifuatavyo:
"Bila shaka hizi sababu zinazosababisha pia matendo ya ulimwenguni, kama yatakuwa ni ya kimaumbile ya kawaida au kimaana kama vile Malaika, basi iwe iwavyo yanathibitika kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu naye ndiye mtendaji halisi."

Kwa maneno mengine ni kwamba, kitendo cha watendaji hawa wawili (Mwenyezi Mungu na Malaika) ni kitendo kimoja tu na si vitendo viwili lakini mtendaji wa kwanza anafanya kwa uwe wake na yule wa pili anamfuatia yule wa kwanza (kutekeleza maamrisho yake).

Maana hii ni miongoni mwa maarifa ya juu katika Qur'an ambayo hufahamika kwa kuzirejea aya za Qur'an zinazozungumzia matendo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Sasa basi ikiwa mtu ataitakidi kwamba Mwenyezi Mungu amewapa baadhi ya viumbe wake kama vile, Malaika na Mawalii matendo yake ya kuruzuku, na kuhuisha na yasiyokuwa hayo, na akaamini pia kuwa viumbe hao ndiyo wanaoendesha mambo ya ulimwengu na kuyasimamia mambo yake na akaona kuwa Mwenyezi Mungu hahusiki tena kwenye matendo hayo kiasi kwamba itikadi hiyo ikampelekea kuwanyenyekea viumbe hawa, basi hapana shaka yoyote kwamba unyenyekevu wake huu ni ibada na tendo hili ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kwa maneno mengine tunasema:

"Lau mtu ataitakidi kwamba Mwenyezi Mungu ameukabidhi ustahiki wa kutekeleza matendo kwa Malaika na Mawalii, na Mwenyezi Mungu akawa amebaki hana ustahiki wowote (katika matendo hayo) na hao Malaika na Mawalii wanayafanya matendo hayo bila kumtegemea Mwenyezi Mungu na bila idhini yake, basi mtu huyu aliyeitakidi itikadi hii, hakika amemfanyia Mwenyezi Mungu mshirika na amemfananisha (Na viumbe vyake).

Hapana shaka kwamba itikadi kama hii ndiyo kuishirikisha dhati ya Mwenyezi Mungu na kutawassal na kunyenyekea kunakotokana na itikadi hii ni ibada kama ilivyokuja katika Qur'an Tukufu.

Anasema Mwenyezi Mungu:

"Na miongoni mwa watu wako wanaofanya waungu badala ya Mwenyezi Mungu, na wanawapenda kama (anavyostahiki) kupendwa Mwenyezi Mungu." Qur'an, 2:165.

Kwa hakika chochote chenye kuwa na kuwepo hakiwezi kuwa mfano wa Mwenyezi Mungu au mshiriki isipokuwa kitakapokuwa na uwezo wa kuuendesha ulimwengu kwa matakwa yake binafsi bila ya matakwa ya Mwenyezi Mungu lakini hakuna yeyote mwenye uwezo huo. Bali kila kilichopo ni chenye kunyenyekea mbele ya matakwa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kitake au kisitake basi kwa hiyo hakiwezi kuwa mshirika wa Mwenyezi Mungu bali kitakuwa kitiifu kwake kutenda kama atakavyo yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Ukweli halisi in kuwa, washirikina walikuwa wakiitakidi kwamba, masanamu yao waliyokuwa wakiyaabudu yanajitegemea katika kuuendesha ulimwengu huu na pia katika mambo ya uungu.
Na katika zama za Jahiliya (kabla kuja Uislamu) kulikuwa na ushirikina wa namna mbali mbali na ushirikina wa daraja ya chini kabisa ilikuwa ni itikadi ya Mayahudi na Wakristo kwamba mapadri na Makasisi wao wanayo madaraka ya uwekaji wa kanuni na sheria kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

"Waliwafanya wanachuoni wao na watawa wao kuwa ni waungu wao kinyume cha Mwenyezi Mungu." Qur'an, 9:31.

Kadhalika washirikina walikuwa wakiitakidi kwamba, ustahiki wa Shafaa na Maghfira (mambo ambayo yanamstahiki Mwenyezi Mungu tu) vimekabidhiwa kwa Masanamu yao wanayoyaabudu, na masanamu hayo yanafanya mambo hayo yenyewe kikamilifu kwa kujitegemea katika ustahiki huo.

Na kwa ajili hii utaona aya nyingi za Qur'an zinazozungumzia Shafaa zinasisitiza kwamba Shafaa haithibitiki ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu asemavyo ndani ya Qur'an:

"Na ni nani huyo awezaye kushufaiya (kuombea) mbele ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa idhini yake." Qur'an, 2:255.

Na lau washirikina wangekuwa wanaitakidi kwamba, masanamu yao waliyokuwa wakiyaabudu yanauwezo wa kushufaiya kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, basi usingeona Qur'an inakanusha moja kwa moja Shafaa bila ya idhini ya Mwenyezi Mungu.

Baadhi ya wanafalsafa wa Kiyunani walikuwa wamejenga ndani ya fikra zao Miungu wengi kwa kila jambo miongoni mwa mambo ya ulimwenguni. (Kwa mfano) mvua ina Mungu wake, mimea ina mungu wake, mtu ana Mungu wake na mambo mengine (kila moja lina mungu wake).

Na walikuwa wakidai kwamba utendaji wa kuendesha mambo ya ulimwengu ambao unamuhusu Mwenyezi Mungu peke yake, umekabidhiwa kwa miungu hawa.

Na katika zama za Jahiliya, baadhi ya Waarabu walikuwa wakiabudu Malaika na nyota zitembeazo na zile zisizotembea hali ya kuwa wakidhani kwamba usimamizi wa mambo ya ulimwengu na watu umekabidhiwa kwa vitu hivyo, navyo ndivyo vinavyotenda kikamilifu kwa kujitegemea na hiyari kamili, na kuwa Mwenyezi Mungu amezuiliwa na hana uwezo wowote juu ya mambo haya kabisa (ametakasika Mwenyezi Mungu na fikra hizi sana sana).2

Na kwa hiyo basi kila aina ya unyenyekevu utaofanywa kwa Malaika na nyota utazingatiwa kuwa ni ibada kwa kuwa unatokana na itikadi hii yenye makosa.

Kuna baadhi ya Waarabu wengine wa zama za Jahiliyyah, hawakuyaitakidi masanamu yaliyochongwa kwa miti na madini kuwa ni Miungu na kwamba ndiyo yaliyowaumba wala kusimamia mambo ya ulimwengu na watu, bali wao walikuwa wakiyaamini kuwa yanao uwezo wa kuwaombea na walikuwa wakisema: "Masanamu haya ni waombezi wetu mbele ya Mwenyezi Mungu."3
Na kwa msingi wa mtazamo huu batili, walikuwa wakiyaabudu Masanamu haya kwa lengo la kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na walikuwa wakisema:

"Sisi hatuyaabudu (Masanamu) isipokuwa kwa ajili ya kutukurubisha kwa Mwenyezi Mungu." Qur'an, 39:3.

Kwa kifupi tunasema: "Bila shaka tendo lolote litokanalo na itikadi hii na likajulisha kufuata na kunyenyekea basi ni ibada, na kinyume chake ni kuwa tendo lolote ambalo halikutegemezewa itikadi kama hii haliwezi kuzingatiwa kuwa ni ibada wala shirki."

Lau mtu atanyenyekea mbele ya mtu na akamuheshimu na kumtukuza bila ya kuamini itikadi kama hii, basi tendo hili halitachukuliwa kuwa ni shirki wala ibada hata kama tendo hilo litakadiriwa kuwa ni haramu.

Kwa mfano: Haitazingatiwa kuwa ni ibada sijda ya mpenzi kwa mpenzi wake, wala mwenye kuamriwa kumsujudia aliyemuamuru na mke kumsujudia mume pamoja na kwamba Sijda kumsujudia asiye Mwenyezi Mungu ni haramu kisheria, kwani Sijda ni Makhsusi kwa Mwenyezi Mungu peke yake wala hairuhisiwi kwa yeyote yule kafanyiwa japo itakuwa ni kwa sura ya dhahiri isiyokuwa na itikaadi isipokuwa kama Mwenyezi Mungu ataamuru kufanywa kwa sijida hiyo (kwa asiye Mwenyezi Mungu).

Natija Ya Utafiti

Mpaka hapa kwa namna fulani tunaweza kufafanua uhakika wa Ibada na sasa ni lazima tueleze kwa kifupi matokeo ya utafiti huu na tunasema:

Lau mtu atawanyenyekea watu wengine bila ya kumzingatia mmoja wapo kuwa ni Mungu au Rabbu au kuwa ni asili inayojitegemea kwa kutenda matendo ya Mwenyezi Mungu, bali amewaheshimu tu kwa kuwa wao ni: "Waja waliotukuzwa hawamtangulii Mwenyezi Mungu kwa neno (Lake asemalo) nao wanatenda amri zake." Qur'an, 21:27. Basi mtu huyo tendo lake hili la kunyenyekea haliwi ila kuwaheshimu na kuwatukuza, wala hakuna uhusiano wowote wa tendo hili na ibada kamwe.

Bila shaka Mwenyezi Mungu amewataja baadhi ya waja wake kwa utajo mwema na amewasifu kwa namna inayoamsha raghba (hamu) ya kila mtu awatukuze na kuwaheshimu.

Miongoni mwa utajo huo ni kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema:
"Bila shaka Mwenyezi Mungu alimchagua Adam na Nuh na kizazi cha Ibrahim na kizazi cha lmran juu ya walimwengu wote." Qur'an, 3:33.

Vile vile Qur'an inabainisha kwamba Mwenyezi Mungu alimchagua Nabii Ibrahim kwa ajili ya Uimamu anasema:
"(Mwenyezi Mungu) akasema bila shaka ninakufanya uwe lmamu kwa ajili ya watu."
Qur'an, 2:124.

Pia Mwenyezi Mungu katika Qur'an amewataja kwa utajo mwema Manabii Nuh, Ibrahim, Dawood, Suleiman, Musa, Isa na Muhammad, (Rehma za Mwenyezi Mungu ziwashukie wote).
Na amewasifu kwa sifa tukufu kiasi kwamba kila sifa moja peke yake inatosha kuuvuta moyo na kuleta mapenzi ndani ya nafsi za watu. Na utaiona Qur'an Tukufu inatangaza ubora wa kizazi cha Mtume Muhammad [s] katika aya nyingi.

Miongoni mwa aya hizo ni hizi zifuatazo:

"Bila shaka Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu Enyi watu wa nyumba (ya Mtume) na akutakaseni sana sana." Qur'an 33:33.

"Waambie sikutakeni malipo yoyote juu ya utume wangu isipokuwa muwapende Al-Qurbaa." Qur'an 42:23.

Na huwalisha chakula katika mahaba ya Mwenyezi Mungu, masikini, yatima na mateka hali ya kuwa wenyewe wanakipenda (chakula hicho) (nao husema moyoni mwao) tunakulisheni kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu (tu) hatutaki kwenu malipo wala shukurani, hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu hiyo siku yenye shida na taabu, basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo na kuwakutanisha na neema na furaha na atawalipa mabustani ya pepo na (nguo) za hariri kwa sababu ya kusubiri (kwao)... mpaka mwisho wa Surat hii ya 76.4
Basi lan watu wangesimama upande wa Mawalii hawa watukufu kwa matendo ambayo yanakubalika ikiwa ni pamoja na kuwatukuza na kuwaheshimu, sawa sawa katika zama za uhai wa Mawalii hao au baada ya kufa kwao, bila ya kuwaitakidi kuwa wao ni miungu na ni vyanzo vinavyojitegemea kwa matendo yanayomstahiki Mwenyezi Mungu, basi hapana mtu yeyote ambaye angeyaona matendo haya kuwa ni ibada wala anayeyasimamia asingeonekana kuwa ni mshirikina, bali kinyume chake angewaona kuwa ni watu wenyc mafanikio wanaoheshimu Mawalii wa Mwenyezi Mungu na kudumisha utajo wao na kuwafanya Mawalii hao kuwa ni kiigizo (chema) kwa watu hao.

Bila shaka kuwatukuza Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni kutukuza vitambulisho vya Mwenyezi Mungu kama ilivyokwisha onyeshwa hapo kabla, na kwamba Uislamu unavitukuza vitambulisho vya Mwenyezi Mungu.

Mtume [s] alikuwa akilishika na kulibusu "Hajarul-Aswad" pamoja na yeye kufahamu wazi kwamba hilo ni jiwe tu. Na sisi pia tunamfuata Mtume [s] kwa tendo lake hilo, tunalibusu Hajarul Aswad na tunatufu nyumba ya Mwenyezi Mungu ambayo si kitu ila mkusanyiko wa mawe na udongo, na tunakimbia baina ya Safa na Marwah na si kitu ila vilima viwili.

Hii ni (kana kwamba) tunatenda matendo yale yale yaliyokuwa yakitendwa na waabuduo sanamu kwa masamu yao, lakini hapana kabisa mtu yeyote ambaye imepata kumpitia katika fikra zake kwamba sisi tunaabudu udongo na mawe.

Basi je, ni kwa nini? Ni kwa sababu mawe hayo hayadhuru wala kunufaisha.

Ama tungetekeleza Ibada hizi hali ya kuwa tunaitakidi kuwa mawe haya na vilima hivi ni miungu na ndiyo chanzo cha athari za uungu, basi tungekuwa miongoni mwa wanaoabudu sanamu.

Na kwa msingi huu, bila shaka kuubusu mkono wa Nabii au Imam au Mwalimu au wazazi wawili na pia kuibusu Qur'an na vitabu vya dini kama vile "Nahjul-Balagha" na kubusu Zariha na kila kile chenyc kuhusiana na waja wema wa Mwenyezi Mungu, hakuna kinachokusudiwa ila ni heshima na kuwatukuza, na kawatukuza wao si kitu kingine ila kumtukuza Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Ndani ya Qur'an imekuja (Habari) ya Malaika kumsujudia Adam [a] na pia ndugu wa Nabii Yusuf kumsujudia Yusuf [a], lakini hapana yeyote iliyempitia katika akili (yake) kwamba kusujudu (kwao hawa) ilikuwa ni kumuabudia Adam au Yusuf na hiyo ni kwa sababu hao waliomsujudia Adam na Yusuf hawakuwaitakidi wawili hao kuwa ni miungu na hawakuwazingatia kuwa wao ndiyo asili ya matendo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, bali jambo hilo lilikuwa ni heshima na utukufu na siyo ibada kama inavyoonekana.

Bila shaka Mawahabi wakati wanapokutana na aya hizi, wanagongana nazo, kwani utawaona wanachunguza huku na huko ili kuzikwepa na kuzificha na husema; "hakika kusujudu kwa watu hao ilikuwa ni amri ya Mwenyezi Mungu kwa hiyo haiwezi kuzingatiwa kuwa ni ibada."

Ni sawa kwamba yote hayo na hata kusujudu kwa ndugu wa Yusuf [a] kulikuwa ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu au radhi yake, lakini kitu ambacho Mawahabi wanajisahaulisha na kujifanya hawakijuwi ni ule ukweli wa tendo lenyewe Ia Sajdah siyo ibada na ndiyo maana Mwenyezi Mungu akaliamrisha.

Na lau Sajdah ingekuwa ni ibada kwa anayesujudiwa, Mwenyezi Mungu asingeliamrisha kabisa, kwani amri haiwezi kuitoa ibada kwenye uhakika wake na wala haiwezi kuifanya shiriki kuwa Tauhidi.

Mwenyezi Mungu anasema: "Waambie, bila shaka Mwenyezi Mungu haamrishi maovu, Je, Mwasema juu ya Mwenyezi Mungu mambo msiyoyajua?" Qur'an, 7:28.

Kifupi ni kuwa, uhakika wa tendo lolote lazima uwe siyo wa kiibada kabla haijatolewa amwi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuliamrisha tendo hilo ili (itakapotoka amri) ipate kuihusisha ibada (kwenye tendo hilo) na wala hakuna namna yoyote ya amri itakayokuja kulitengua tendo hilo kutoka kwenye hukmu ya Ibada.

Bila shaka kujitakasa ambako Mawahabi wanategemea, kitu ambacho muda mrefu tumekuwa tukisikia toka kwa Masheikhe zao huko Maka na Madina, kunajulisha ukaidi walionao juu ya kufahamu maarifa ya Qur'an na kukosa kwao kuelewa kuwa "Ibada" inao uhakika wa pekee unaojitegemea na hupata ikatokeza amri kuamrisha ibada na wakati mwingine katazo kukataza.

Hii ina maana kwamba, kitu ambacho kwa dhati yake ni ibada, Mwenyezi Mungu hukiamrisha au kukikataza, kama vile Sala na Saumu ambazo Mwenyezi Mungu amewaamrisha watu "Mukalafu" kazitekeleza na amemkataza (kufanya ibada hizo) mwanamke mwenye hedhi, ati kama vile kufunga siku ya Idi al-Fitri na Adh-haa ambazo Mwenyezi Mungu amewakataza watu wote "Wasifunge".

Basi kama kusujudu kwa Malaika kumsujudia Adam [a] na ndugu wa Yusuf [a] na wazazi wake wawili kumsujudia Yusufu [a] ni kuwafanyia Ibada, basi ile amri ya kuamrishwa kwao kusujudu, hakuitoi sijda katika uhakika wa kuwa ni ibada bali hapana budi tuseme kuwa kuitakidi Uungu ndiko kutakakokiharamisha kitendo hicho na kukifanya kuwa ni ibada, au kuitakidi kuwa yule anayenyenyekewa ndiyo asili (chanzo) cha matendo ya Mwenyezi Mungu. Vipi tutapata msimamo?

Ewe msomaji mpendwa inapasa ufahamu kuwa, kuondosha tofauti iliyopo kati ya Waislamu na Mawahabi ndani ya mambo mengi (wanayohitalifiana) inategemea kupata ufumbuzi wa maana ya ibada. Ikiwa haikubainishwa maana ya ibada kwa taarifu ya kimantiki, na ikawa hakuna maelewano na uadilifu katika pande mbili, basi hakuna faida ya kutafiti na kujadiliana.

Kwa maelezo haya basi, hana budi mtu mwenye kutafuta ukweli afanye kila njia ya kuchunguza maudhui hii kwa undani na asihadaike na taarifu za kilugha zilizopungufu kuweza kutatua na kufafanua.

Rejea iliyo bora atakayoirejea ni aya za Qur'an, hiyo ndiyo dalili inayoongoza (kufahamu) maudhui hii na kila maudhui.

Na miongoni mwa mambo yanayohuzunisha ni kwamba, waandishi na watunzi wa Kiwahabi na walioandika kuwajibu Mawahabi, wamefanya utafiti na uchunguzi kwa urefu katika nukta zingine na wala hawakuitilia maanani nukta hii muhimu (ya Ibada) kwa kuisherehesha na kuithibitisha.

Basi Mawahabi wanasema, "Matendo mengi muyafanyayo Enyi Waislamu kumhusu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] na Maimamu wa nyumba yake ni kumuabudia, na hali hiyo inalazimu kumshirikisha Mwenyezi Mungu katika ibada."

Kwa hiyo basi inabidi Waislamu walete ufafanuzi na maelezo ya kina kuhusu ibada ili kuiondoa dalili yao ya upuuzi. Kwa hakika Mawahabi wanayaona mambo mengi wayatendayo Waislamu kwa maiti kuwa ni kumuabudia.
Kwa mfano:

1) Kuomba Shafaa kwa Mtume [s] na watu wema.
2) Kuomba uponyo kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu.
3) Kuomba kutekelezewa haja toka kwa viongozi wa Dini.
4) Kumheshimu na kumtukuza mwenye kaburi.
5) Kutaka msaada kwa Mtume [s] na wengineo.

Basi wao (Mawahabi) wanasema, "Hakika Shafaa ni katika matendo ya Mwenyezi Mungu na vile vile kuponya ni kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuomba mojawapo ya mawili haya kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu kunapelekea kumuabudu huyo (aombwaye).

Ni Kipi Kitendo Cha Mwenyezi Mungu?

Katika kitabu hiki kidogo tunatanguliza uchunguzi juu ya matendo ya Mwenyezi Mungu na maana yake ili maudhui hii ipate kufahamika na tunasema: "Ikiwa ambaye anasimamaia Shafaa na kuponya kwa uwezo wake mwenyewe na kwa kutaka kwake hali ya kujitegemea bila ya kuipata haki ya Shafaa kutoka kwa yeyote yule na bila ya kutegemea uwezo wa aliye juu zaidi kuliko yeye kiuwezo) basi haya ni miongoni mwa matendo ya Mwenyezi Mungu yanayomuhusu peke yake.

Na kuomba Shafaa kwa yeyote yule hali ya kaitakidi (kama tulivyosema hivi punde) maana yake ni kuamini Urabbi na Uungu wa huyo anayeombwa.
Ama ikiwa kuomba Shafaa na uponyo kumesalimika kutokana na itikadi hii, na mtu akaomba Shafaa kwa mtu anayemuitakidi kuwa ni mja wa Mwenyezi Mungu, pia anatenda kwa msaada na uwezo wa Mwenyezi Mungu na idhini yake, basi Shafaa hii na uponyo huu havilazimiani na itikadi ya Uungu na siyo kuomba tendo la Mwenyezi Mungu kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu."

Qur'an Tukufu inasema ikimnukuu Nabi Isa [a]:

"Na ninaponya vipofu na wenye mbaranga, na ninafufua wafu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.." Qur'an, 3:49.

Na ufafanuzi kama huu unakuja pia ndani ya munasaba wa kuomba kukidhiwa haja toka kwa mmoja wa Mawalii wa Mwenyezi Mungu au kumuomba msaada.Basi kutaka kukidhiwa haja na Walii huyo kuna namna mbili:

1). Kumuomba mja pamoja na kuitakidi kuwa anao uwezo wa kujitegemea Mwenyewe, hii itakuwa ni Ibada.

2). Kumuomba mja hali ya kuitakidi kuwa yeye ni mja wa Mwenyezi Mungu na nguvu zake zinatoka kwa Mwenyezi Mungu, basi hali hii haihusiani kabisa na ibada.

Kwa Hakika ufafanuzi huu siyo tu ndiyo ukomo wa kutenganisha baina ya ibada na kisichokuwa ibada kwa munasaba wa matendo haya, bali ni kanuni ya ujumla inayotenganisha baina ya Shirki na Tauhidi katika kila vinavyo athiri na sababu.

Bila shaka kuitakidi athari (matokeo) ya 'Asprini' (kwa mfano) katika kutuliza maumivu, na kuitakidi kuwa ikiwa athari hiyo inatokana na uwezo wake wa kujitegemea na kwamba hakuna mafungamano na uwezo uliyo juu zaidi ambaye ni Mwenyezi Mungu, basi maana yake ni kuitakidi Uungu wa hiyo 'Asprini'.
Ama kuitakidi kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyeyaweka matokeo haya na athari hii ndani ya Asprini na pia dawa hii si lolote ila ni sababu ya kutuliza maumivu na vile vile haiwezi kutuliza maumivu isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, bila shaka itikadi ya namna hii inatokana na Tauhidi yenyewe khasa, kwani hapana mwenye kuathiri ila yeye Mwenyezi Mungu.

Na kwa sababu hii tumesema kwamba "Kuondosha tofauti mbali mbali kunaegemezewa kwenye ufafanuzi wa maana ya Ibada na kuitakasa Tauhidi kutokana na shirki na matendo ya Mwenyezi Mungu kutokana na mengineyo na kuutakasa uungu kutokana na Ubudiyyah.

Na hapo kabla imeonyeshwa kuwa Waarabu wa zama za Jahiliyya walikuwa wakiitakidi itikadi hii yenye makosa, kwamba Masanamu (hayo hayo) ndiyo yaliyokuwa yanaendesha baadhi ya mambo ulimwenguni kwa kujitegemea na yalikuwa yakimiliki Shafaa na mambo mengineyo.Itikadi hii ndiyo iliyowafanya wawe washirikina.

Kwa hiyo, iwapo utataka ufafanuzi wa kielimu juu ya maudhui hii rejea vitabu hivi viwili vifuatavyo vilivyoandikwa na Mwandishi wa kitabu hiki.

1). Maalimut-Tauhidi Fil-Qur-'anil-Karim.
2). At-Tauhidu Was-Shirku Fil-Qur-anil-Karim.

  • 1. Tafsiri Alaul-Qur'an, juz. 1, uk 57.
  • 2. Al-Milal Wanihal cha Shahirstani, juz. 2, chapa ya Misri uk. 244-247
  • 3. Qur'an, 10:18.
  • 4. Qur'an, 76:8-12