read

Tauhidi Katika Ibada

Msingi wa wito wa Manabii [a] siku zote umekuwa ni kulingania kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake na siyo kumuabudu mwingine peke yake, au kumshirikisha na Mwenyezi Mungu. Na msingi wa hukmu za mbinguni tangu mwanzo wa kutumwa ujumbe wa Manabii ilikuwa ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kukata mizizi ya shirki.

Ukweli halisi ulivyo ni kwamba, lengo la kutumwa kwa Manabii ni kulingania (watu) kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake, na kupiga vita ushirikina wa aina zote na khususan kupinga shirki katika ibada.

Qur'an Tukufu inaashiria ukweli huu wazi wazi na inasema:

"Na bila shaka tulimpeleka Mjumbe kwa kila umma (akawambie umma wake) muabuduni Mwenyezi Mungu na muyaepuke masanamu." Qur'an, 16:36.

"Na hatukumtuma kabla yako Mjumbe yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hakuna apasiwaye kuabudiwa ila mimi, basi niabuduni." Qur'an, 21:25.

Qur'an imeizingatia ibada ya Mwenyezi Mungu kuwa ni jambo linalokusanya na kushirikisha sheria zote za mbinguni na inasema:

"Waambie, Enyi mliopewa Kitabu cha Mwenyezi Mungu njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu, ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu na wala tusimshirikishe na chochote." Qur 'an, 3:64.

Tauhidi katika ibada ni msingi imara kwa Waislamu wote, na hapana yeyote aipingaye Tauhidi au kuwa na tofauti ndani yake miongoni mwa vikundi vyote vya Kiislamu, ijapokuwa Mu’tazilah mtazamo wao juu ya Tauhid ya matendo ya Mwenyezi Mungu unatofauti, na vile vile Ash’aria nao wanayo tofauti juu ya Tauhid katika sifa za Mwenyezi Mungu, lakini madhehebu zote za Kiislamu zinaafikiana kuhusu Tauhid ndani ya ibada na hakuna nafasi ya kupinga hilo.

Kama kutakuwa na khitilafu, basi ikhtilafu hiyo haiko katika msingi wa Tauhidi ya ibada bali iko katika Misdaaq za Tauhidi ya Ibada.

Hii inamaanisha kwamba, baadhi ya Waislamu wanaona kuwa baadhi ya matendo ni ibada na Waislamu wengine wanaona kuwa (matendo hayo) ni Takrima na Taadhima tu na siyo ibada.

Na kwa mujibu wa Istilahi ya Elimu ya "Mantik" tofauti kama hii iko ndani ya 'As-Sughraa" ambayo ni je, kitendo hiki ni ibada au hapana? Wakati ambapo hakuna tofauti katika 'Al-Kubraa" ambayo ni je, inafaa kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu au hapana? Na hii wameafikiana (Waislamu wote) kwamba haijuzu kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Kwa maneno mengine (Tunaweza kusema) tofauti iliyopo inatokana na Mawahabi kuyazingatia matendo fulani kuwa ni ibada wakati ambapo wasiokuwa wao miongoni mwa Waislamu ulimwenguni kote hawayazingatii kamwe matendo hayo kuwa ni ibada.

Hapana budi tuifafanue maana ya "Ibada" kwa mujibu wa lugha na vile vile kwa mjibu wa Qur'an, na hapo ndipo yatakapofahamika matawi ambayo ndani yake imekuja tofauti kuyahusu mwenyewe kwa dhati yake, na ndipo utakapotudhihirikia uhakika na ukweli wa ibada.