Table of Contents

Uchambuzi Wa Mwisho

Hapa zimebakia sehemu mbili muhimu za uchunguzi tutazionyesha katika sehemu hii ya mwisho, nazo ni kama ifuatavyo:

A). Kumlilia maiti kabla ya kuzika au baada ya kuzika.

B). Kudhifia tamko la "Abdi" kwa mja.

Basi huenda mtu asiyejua hukmu za sheria akadhani kuwa, sheria zimeyaharamisha mambo hayo, na sasa hivi tunabainisha hukmu zake kwa mujibu wa kitabu (Qur'an) na sunnah na tunasema:

Kwanza: Kumlilia maiti:

Jicho na moyo havilaumiwi pindi mtu anaposimama juu ya kaburi la Mtume wake na Maimamu wa nyumba ya Mtume [a] na Masahaba wema r.a. (Jicho halilaumiwi) kutoa machozi (na moyo) kuhuzunika, ili kuonyesha kilichomo ndani (ya nafsi) katika upendo, kutawalisha, mapenzi, huruma na shauku, na kwa hakika jambo hili linafuatana na maumbile ya kibinaadamu na wala sheria ya Mwenyezi Mungu hailipingi.

Amma maumbile (yalivyo) ni kwamba:
Huzuni na kuathirika hulazimiana na huruma ya kiutu pindi mtu anapojaribiwa kwa msiba wa mtu ampendaye miongoni mwa wapenzi wake au mtoto wake na ndugu zake, na yeyote asiyekuwa na hisia hii huhesabiwa kuwa ni wa pekee katika maumbile ya kiutu, na wala simuoni yeyote ulimwenguni anayekanusha ukweli huu kwa nguvu zake zote.

Ama Sheria: Inatosha (kulieleza) hilo kufuatia kilio cha Mtume Mtume [s] na Masahaba na watu waliowafuatia kwa wema kuwalilia maiti wao.

Basi huyu hapa mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] anamlilia mwanawe mpenzi "Ibrahim" na anasema: "Jicho linatoa machozi na moyo unahuzunika, na wala hatusemi (chochote) isipokuwa kile anachokiridhia Mola wetu, nasi kwako Ewe Ibrahim ni wenye kuhuzunika:1

Wanasira na wanahistoria wamepokea kwamba wakati Ibrahim mtoto wa Mtume alipokuwa katika 'Sakratul-maut' Mtume [s] alikuja akamkuta miguuni mwa mama yake, akamchukua na kumweka miguuni mwake akasema:

"Ewe Ibrahim hakika sisi hatuwezi kukutosheleza kitu kwa Mwenyezi Mungu." Kisha macho yake yakatiririka machozi na akasema: "Hakika sisi kwako wewe ni wenye kuhuzunika ewe Ibrahim, jicho linalia na moyo unahuzunika na wala hatusemi kitakachomchukiza Mola, na lau lisingekuwa ni jambo la haki na ahadi ya kweli basi tungelikuhuzunikia huzuni kubwa mno kuliko hii."

Na pindi Abdur-Rahman bin Auf alipomwambia Mtume kwamba; "Je, hukutukataza kulia?"

Mtume alijibu kwa kusema: "Hapana, lakini nilichokataza ni sauti mbili za ujinga na sauti mbili zingine: Sauti wakati wa msiba, na kilio cha kishetani na sauti ya ngoma, na kilio changu hiki ni huruma, na asiyekuwa na huruma hahurumiwi."2

Na kilio hiki cha Mtume [s] hakikuwa ni cha kwanza na cha mwisho wakati akijaribiwa kwa misiba ya wapenzi wake, bali alikuwa akamlilia mwanawe "Tahir" na husema:

"Jicho linatoa machozi, na machozi hayazuiliki, na moyo unahuzunika na wala hatumuasi Mwenyezi Mungu."3

Na Al-Allama Al-Amini ndani ya kitabu chake kikubwa kiitwacho 'Al-Ghadir,' amekusanya mahali pengi ambapo Mtume [s] na Masahaba na Tabi'ina waliwalilia maiti wao na wapenzi wao pindi walipofariki na hapa tunanakili ibara ya mwanachuoni huyu mtafiti:

Huyu hapa Mtume [s] wakati Hamza r.a. alipouawa, kisha Safiyah binti Abdil-Muttalib r.a. akaja akimtafuta Hamza, Maansari wakamzuia, basi Mtume [s] akasema "mwacheni". Akakaa mbele yake, ikawa Safiyah anapolia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu naye hulia, na anapozidisha kulia kwa uchungu, Mtume [s] naye hulia kwa uchungu. Naye Bibi Fatimah alipokuwa akilia Mtume [s] naye hulia na kusema: "Sintapata msiba kama wako kamwe."4

Na pindi Mjumbe wa Mwenyezi Mungu aliporudi toka Uhdi, wanawake wa Kiansari waliwalilia mashahidi wao, basi sauti zao zikamfikia Mtume [s] akasema:

"Lakini Hamza hana wakumlilia". Basi Maansari wakarudi na wakawaambia wanawake wao "Msimlilie yeyote mpaka muanze kumlilia Hamza", basi desturi hiyo kwa Maansari imebakia mpaka leo hawamlili mtu ila kwanza humlilia Hamza.5

Na huyu (tena) ni Mtume [s] anawapa watu wa Madina habari ya shahada ya Ja’afar na Zaid bin Harith na Abdallah bin Ruwah na hali macho yake yanatiririka machozi.6

Na hapa Mtume [s] alilizuru kaburi la mama yake na akalia na akawaliza waliokuwa pamoja naye.

Pia Mtume [s] anambusu Uthman bin Madh-un akiwa ni maiti na machozi yake (Mtume) yanatiririka usoni.7

Vile vile Mtume [s] anamlilia mtoto wa mmoja wa mabinti zake na Ubbadah Ibn Samit akamwambia "Nini hiki ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu?"

Mtume Akasema:

"Ni huruma aliyoiweka Mwenyezi Mungu ndani ya wanaadamu, na kwa hakika Mwenyezi Mungu anawahurumia wenye huruma miongoni mwa waja wake."8

Naye Bibi mkweli aliyetakasika, (Fatimah binti Muhammad [s] anamlilia baba yake na anasema:

"Ewe baba yangu uko karibu mno na Mola wako, Ewe baba yangu umemwitika Mola aliyekuita, Ewe baba yangu tunakuomboleza kwa Jibril, Ewe baba yangu makazi yako ni pepo ya Firdaus."9

Na vile vile Bibi Fatimah [a] alisimama kwenye kaburi tukufu la Baba yake na akachukua gao la udongo wa kaburi akauweka (karibu na macho) na akalia na kusoma shairi akasema:

"Ana lawama gani mtu atakayenusa udongo wa kaburi la Ahmad [s] iwapo hatanusa ghaliya 10 milele. Nimefikwa na msiba ambayo lau ungeufika mchana ungegeuka na kuwa usiku.

Na huyu hapa Abu Bakr Ibn Abi Qahafah anamlilia mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] na kumuomboleza kwa kusema: "Ewe Jicho lia usichoke, ni haki kumlilia Bwana."

Na amesema tena: "Wanamlilia yule ambaye mbingu inamlilia na ni yule ambaye ardhi imemlilia na watu wamehuzunika mno."
Na anasema: "Ewe Jicho lia kwa machozi mengi yanayotiririka, na usichoke kutoa machozi kila wakati na kulia."

Naye Ar-wi binti Abdul-Muttalib anamlilia Mtume [s] na kumuomboleza kwa kusema:
"Fahamu Ewe Jicho! Ole wako nipoze kwa machozi yako muda wote nitaobakia, na unipe ushujaa. Fahamu Ewe jicho, Ole wako jitokeze kwenye nuru ya miji na unipoze."

Na Atikah binti Abdul-Muttalib anamuomboleza Mtume [s] na anasema:

"Enyi macho yangu! lieni sana siku zote na mutoe machozi, mtiririshe machozi bila udhuru.

Ewe Jicho lia kwa machozi yasiyokatika. Ewe Jicho lia kwa machozi sana kwa ajili ya Mtume mwenye nuru aliyechaguliwa kuliko viumbe wengine wa Mwenyezi Mungu."

Naye Safiyah binti Abdul-Muttalib, anamlilia Mtume na kumuomboleza kwa kusema:

"Ewe Fatimah lia pamoja na wenzako wala usichoke mpaka nyota zichomoze, Mtume ni mwenye kuliliwa na anastahiki kuliliwa, Yeye ndiye Mtukufu na Bwana aliye mzuri". Na pia anasema: "Enyi macho yangu lieni kwa machozi mfululizo. Enyi macho yangu lieni na mtiririshe machozi kwa huzuni nyingi."

Na huyu hapa Hind bint Al-Harith Ibn Abdil-Muttalib anamlilia Mtume na anasema:

"Ewe Jicho lia kwa machozi na uyatirirshe kama yanavyoshuka maji ya mvua yakatiririka."

Na Hind binti Athatha anamuomboleza Mtume anasema:

"Ewe Jicho lia usichoke kwa hakika nimepata khabari ya mauti ya yule umpendaye (Mtume [s])."

Na huyu hapa Atika binti Zaid anamuomboleza Mtume na anasema:

"Na sasa vipando vyake vinatingisha moyo na kwa hakika alikuwa akivipanda yule ambaye ni pambo lake. Na vipando hivyo vimekuwa vinamlilia Bwana wake na macho yake yanatiririsha machozi."

Naye Ummu Ayman anamuomboleza Mtume kwa kusema:

"Ewe Jicho langu lia kwa sababu huzuni yangu itakuwa Shifaa, basi lia sana kwa machozi mengi mpaka ifike hukumu ya Mwenyezi Mungu ya kheri."

Na huyu hapa Shangazi ya Jabir bin Abdallah alikuja siku ya Uhdi akimlilia nduguye Abdallah Ibn Amr, na Jabir amesema:

"Nikawa nalia na watu wakawa wananikataza na mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] hanikatazi, basi mjumbe wa Mwenyezi Mungu akasema: "Lieni kwa ajili yake hata musipolia, Wallahi Malaika hawakuacha kumfunika kwa mbawa zao mpaka mumemzika."11
Naam, imepokewa toka kwa Umar lbn Khattab na Abdallah Ibn Umar kwamba Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] amesema:

"Hakika mauti huadhibiwa kwa kilio cha watu wake."

Mimi nasema: Dhahiri ya hadithi hii iko kinyume na matendo ya Khalifa (mwenyewe) aliyotenda mahala pengi palipothibitishwa na historia.

Miongoni mwake ni kwamba, yeye alimlilia Nuuman Ibn Muqrin Al-Muzani pindi ilipomfikia habari ya kifo chake, basi akatoka akawajulisha watu akiwa juu ya mimbar na akaweka mkono wake juu ya kichwa chake akalia.12

Na miongoni mwake ni kulia kwake yeye na Abu Bakr wakimlilia Saad Ibn Muan mpaka Aisha akasema:

"Naapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi mwake hakika mimi nilikuwa na tambua sauti ya kilio cha Abu Bakr na sauti ya kilio cha Umar, wakati mimi nikiwa chumbani mwangu."13

Na miongoni mwake ni kilio chake juu ya nduguye Zayd Ibn Khattab, na huyu (Zayd) alifuatana na mtu fulani katika Bani Adiy Ibn Kaab, basi yule mtu akarudi Madina na alipomuona macho yake yakatiririka machozi akasema: "Wewe umemuacha Zayd hali ya kuwa ni maiti nawe umekuja kwangu."14

Basi kulia kwa Khalifa ambako kumekaririka kunatuongoza kwamba, makusudio ya hadithi hata kama Sanadi yake itasihi yana maana nyingine, itakuwaje (hali hii)? Na dhahiri ya hadithi lau tutaiamini inakwenda kinyume cha Qur'an, na hapa nakusudia kauli yake Mwenyezi Mungu isemayo, "Wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine." Qur'an, 35:18.

Basi kuna maana gani ya kumuadhibu maiti kutokana na watu wengine kumlilia!!

Shafii amesema: Na hadithi aliyoipokea Aisha toka kwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] (Itatajwa baadaye) inaaminika kwamba ni hadithi iliyosemwa na Mtume [s] (Kuliko hadithi zilizotajwa na Umar na Abdallah) na dalili yetu ni Qur'an na Sunnah. Na iwapo itasemwa iko wapi dalili ya Qur'an, patasemwa, ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo "Wala Hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine" na ile isemayo: "Na kwamba hatapata mtu isipokuwa yale aliyoyafanya." Qur'an, 53:39.

Na kauli yake isemayo: "Basi anayefanya wema (hata) wa kiasi cha mdudu chungu atauona na anayefanya uovu (hata) wa kiasi cha mdudu chungu atauona." Qur'an, 99: 7-8.

Na kauli yake isemayo: "Ili kila nafsi ilipwe kwa yale iliyoyafanya." Qur'an, 20:15.

Na iwapo itasemwa iko wapi dalili ya Sunnah? Patasemwa, "Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alimwambia mtu fulani "Huyu ni mwanao"? Akasema "Ndiyo" "Hakika yeye hatafanya makosa kwa ajili yako, wala hutafanya makosa kwa ajili yake." Basi Mtume akamjulisha kama alivyomjulisha Mwenyezi Mungu kwamba kila kosa la mtu ni lake mwenyewe kama ambavyo amali yake siyo ya mwingine wala dhidi yake.15

Ufahamisho wa hadithi: Yote tuliyonakili yanatujulisha kwamba makusudio ya hadithi inayosema kwamba, "Hakika maiti anaadhibiwa kwa kumlilia walio hai" (Kama Sanadi yake itasihi) sicho kinachofahamika kutokana na dhahir yake, na hadithi ilikuwa na qarina kujulisha maana yake lakini zilianguka wakati wa kunakili.

Na kwa ajili hiyo baadhi ya watu wamedhania kuwa ni haramu kumlilia maiti kwa kutegemea hadithi hii hali ya kuwa wameghafilika na lengo la hadithi na maana yake.

Amepokea Umrah, kwamba yeye alimsikia Aisha r.a. wakati alipoambiwa kwamba Abdallah Ibn Umar anasema: Maiti huadhibiwa kwa ajili ya kilio cha walio hai, basi Aisha r.a. akasema:

"Amma yeye hajasema uongo (kwa makusudi) lakini amekosea au amesahau, hakika mjumbe wa Mwenyezi Mungu alipita kwenye mazishi ya Myahudi ambaye jamaa zake walikuwa wanamlilia akasema: "Hakika wao wanamlilia naye anaadhibiwa kaburini mwake."16

Na imepokewa toka kwa Ur-wa naye toka kwa Abdallah bin Umar amesema: "Amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] hakika maiti huadhibiwa kwa ajili ya kilio cha watu wake juu yake basi Ur-wa akamtajia Aisha hadithi hii akasema hali akimkusudia Ibn Umari:

"Kwa hakika Mtume [s] alipita kwenye kaburi la Myahudi akasema, hakika mwenye kaburi hili anaadhibiwa na hali ya kuwa watu wake wanamlilia kisha akasoma, "Na wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine."17

Huu ndiyo ufahamisho wa hadithi na maana yake na hawezi kutia shaka katika kusihi maana hii mtu mwenye utambuzi na maarifa ya Qur'an na hadithi.

Na kuna Riwaya nyingine zinazojulisha kwamba Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] alimkemea Umar kutokana na kuwakataza kwake wanawake waliokuwa wakiwalilia maiti.

Imepokewa toka kwa Ibn Abbas amesema:

"Alipofariki Zainab binti ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] Mtume [s] alisema, mfuatishieni kwa Salaf wetu mwema (aliyetangulia) Uthman Ibn Madh-un, basi wanawake wakalia, Umar akawa anawapiga kwa fimbo yake, mjumbe wa Mwenyezi Mungu akaushika mkono wake akasema, tulia Ewe Umar, waache walie na Ole wenu! na maombolezo ya shetani". Hadi akasema. Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alikaa ukingoni mwa kaburi na Fatimah akiwa pembeni mwake analia, basi Mtume [s] akawa anayapangusa macho ya Fatimah kwa nguo yake kwa kumuonea huruma."18
Na Al-Bayhaqi ameandika ndani ya Sunan Al-Kubra hadithi kama hiyo kuhusu kufariki kwa Ruqaiyyah binti ya mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Na mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] alisema:
"Wacha Ewe Umar" Kisha akasema: "Ole wenu! na maombolezo ya shetani, kwani chochote kiwacho kutoka jichoni na moyoni ni miongoni mwa huruma na kiwacho kutoka ulimini na mkononi kinatokana na shetani."19

Na katika Riwaya nyingine:
Mjumbe wa Mwenyezi Mungu akasema: "Ewe Umar waache kwani jicho linalia na moyo unapata huzuni na ni hivi punde tu msiba umetufika."20

Hiki ndicho tulichokinakili kutoka katika riwaya nyingi, kitamjulisha msomaji Mtukufu hukmu ya Kiislamu katika Mas-ala ya kumlilia maiti sawa sawa maiti akiwa ni jamaa na ni kipenzi au akawa ni rafiki mpenzi, basi iwapo itajuzu kuwalilia hao basi kumlilia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] na watu wa nyumba yake waliotakasika na Masahaba wake wema ni awla kujuzu.

Kwa nini isiwe na hali yakuwa riwaya nyingi zimekuja kuhusu jambo hili kutoka kwa makundi mawili Shia na Sunni zinazohusu kumlilia Mtume [s] na misiba ya watu wa nyumba yake, hatukulenga kuzitaja kwa, kufupisha maelezo na atakae kufahamu arejee kitabu kiitwacho, "Siratuna Wa Sunnatuna Siratun-Nabiyyi Wa Sunnatuh" cha mwanachuoni mkubwa Sheikh Abdul-Husain Al-Amini r.a. Japokuwa tuliyoyataja katika kurasa hizi yanaambatana na yale aliyoyahakiki mwanachoni huyo katika mlango huu (Mwenyezi Mungu amrehemu).

Pili: Kudhifia tamko la "Abdi" (lenye maana ya mja au mtumwa) kwa kiumbe:

Kwa hakika imekuwa ni jambo mashuhuri kwa wapenzi wa Ahlul Bayt [a] kuwaita watoto wao (majina ya) "Abdur-Rasul" na "Abduali" na "Abdul-Husein".... na mfano kama huo, yaani kudhifia neno "Abdi" kwenye majina ya (Ahlul-Bayt) [a].

Na kuita majina (kwa namna hii) kumezusha wasi wasi ndani ya baadhi ya makundi na hasa Mawahabi, hali yakuwa wanadai kwamba kuita jina (namna) hii ni aina ya shirki na wala hakuafikiani na misingi ya Tauhidi.

Na kuna kikao huko Syria kilichotukutanisha mimi na Sheikh Nasirudin Al-Abani ambaye ni msahihishaji na ni mhakiki na baadhi ya vitabu vya hadithi, basi niliiona kwake chuki kubwa kutamkwa jina la Abdul-Husein, na hali hiyo (Ilitokea) pale yalipokuja mazungumzo kumhusu Al-Allamah Al-Hujjah As-Sayyid Abdul-Husein Sharafud-din Al-Amili ambaye ndiye mwandishi wa Al-Muraja'at (Mwenyezi Mungu aitakase roho yake).

Na kwa ajili ya kuondoa utata mbele ya ukweli, sisi tunasimama kutatua Mas-ala haya kwa mtazamo wa Qur'an na Sunna, na tunasema: "Ubudiyyah, hutumika na kukusudiwa kutokana nayo (maana zifuatazo):

Kwanza: Maana inayokabili uungu, nalo kwa maana hii linajulisha kwamba mtu huyo au watu wote ni milki ya Mwenyezi Mungu katika asili ya kuumbwa, na mwenye kumiliki ni yeye Mwenyezi Mungu, nawe unafahamu kwamba mtu ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu na ndiye Bwana wake, na chanzo cha mambo haya mawili ni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyemuumba baada ya kuwa hakuwepo naye ndiye mwenye kumpa kila kitu kinachomuhusu.

Kwa hiyo basi Ubudiyyah kwa maana hii ni asili ya kila kilichopo, na ni asili ya kila kitu na kamwe hakiepukani na maana hiyo inayokusudiwa na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo:

"Hapana yeyote aliyeko mbinguni na ardhini isipokuwa atafika kwa (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa Rehma hali ya kuwa ni mtumwa "Abdi." Qur'an, 19:93.

Kama ambavyo kauli ya masihi (Isa bin Mariyam) [a] inavyoashiria akasema:

"Hakika mimi ni Abdullahi (Mtumwa wa Mwenyezi Mungu) amenipa kitabu na amenifanya kuwa ni Nabii." Qur'an, 19:30. Na aya nyinginezo.

Na Idhafa ya Abdi kwa maana hii haiwezekani ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

Pili: Ubudiyyah hutumika na kukusudiwa kutokana nayo utiifu au maana inayokaribiana na hiyo, na kwa hakika wameifafanua maana hii waandishi wa kamusi za lugha.

Amesema ndani ya "Lisaanul-Arabi": At-Taabudu (Maana yake ni) At-Tanaasuku (kufanya ibada.), Al-Ibada (maana yake) "At-Ta'a" (utiifu).

Na amesema ndani ya "Al- Qamusul-Muhit":

"Wal-Abdiyah, Wal-Ubudiyyah, Wal-Ubudah, Wal Ibadah, (Maana yake ni) At-Ta'a (yaani utiifu)."

Na kwa msingi huu basi, makusudio ya "Abdur-Rasuli", "AbduAli" na.... "Ni Mwenye kumtii Mtume na mwenye kumtii Ali. Na "Makusudio haya" yako wazi, basi kwa nini isiwe hivyo na Mwenyezi Mungu ametuamuru kuwatii wao akasema: "Mtiini Mwenyezi Mungu na mumtii Mtume na wenye mamlaka miongoni mwenu." Qur'an, 4:59.

Basi Qur'an imetambulisha kuwa Mtume ni mwenye kutiiwa na Waislamu ni wenye kutii, na halaumiwi mtu kuidhihirisha maana hii kwa kuwaita wanawe na awapendao (kwa majina hayo).

Naam, ndani ya hadithi ya Abu Hurairah (imesemwa) "Asiseme mmoja wenu kumwambia aliyemmiliki "Abdii" Wa "Amatii" Yaani mtumwa wangu na mjakazi wangu, na aseme kijana wangu" (Lakini) Ibnul-Athir ndani ya kitabu chake kiitwacho, "An Nihayah" ameitolea dosari hadithi hii kwa kauli yake aliposema:

"Hadithi hii ni kwa maana ya kupinga kuwafanyia ujeuri juu yao na kuwanasibishia utumwa kwa maana ile ya kwanza. Kwani mwenye kustahiki hilo ni Mwenyezi Mungu Mtukufu naye ndiyo mlezi wa waja wote,"21

Na hadithi hii kwa dhahiri yake inakwenda kinyume na Qur'an Tukufu, vipi itakuwa wakati yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliyewanasibishia "Ubudiyyah" kwa watu wanaowamiliki.
Akasema Mwenyezi Mungu: "Waozeni wajane miongoni mwenu na waliowema katika watumwa wenu (Ibadikum) na wajakazi wenu (Imaikum) na wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha katika fadhila zake na Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa mwenye kujua." Qur'an, 24:32.

Utaona kwamba Mwenyezi Mungu anaunasibisha Ubudiyah (utumwa) na Imaiyah (Ujakazi) kwa wale wanaowamiliki, na lau ndani ya Taabiri (Hii) kungekuwa na kitu fulani (kinachoonyesha) kiburi kwa mtumwa, basi Mwenyezi Mungu asingelitumia Taabiri hii.

Kisha ni kwamba msingi wa Shubha hii ni kuwa, wenye kuwa na mushkeli (wa jambo hili) hawatofautishi baina Ubudiyyah Tak-winiyyah Al-haqiqiyyah ambayo haiepukani na mtu tangu mwanzo wa kupatikana kwake mpaka kwenye siku zake za mwisho, na baina ya milki yenye kujitokeza (isiyokuwa ya asili) kwa mtu kufuatia hali na masharti (yanayohusika) basi hapo bwana huwa mtumwa na mtumwa huwa bwana na hakimu.
Hii ndiyo Fiqh ya Kiislamu inayojulisha kuwafanya mateka wa vita wanaume na wanawake kuwa watumwa. Amesema Ibn Quddamah ndani ya Kitabu chake kiitwacho, "Al-Mugni": "Pindi Imam anapowateka mateka, basi anahiyarishwa, akiona kuwa (inafaa) kuwaua (atawaua), na akiona awasamehe bila ya badali (ya kitu chochote atawasamehe), na akiona atawaachia kwa (badali ya) mali atakayoichukua toka kwao (atawaachia) na akiona (inafaa) atakubali fidia. Na akiona kuwa inafaa kuwafanya watumwa ni bora, (basi atafanya analoona kuwa linafaa kati ya hayo)".

Kwa hiyo ndani ya vitabu vya Fiqhi kuna mlango mpana unaohusu hukmu za watumwa na wajakazi, hivyo wanazo hukmu maalum anazifahamu yule aliye mtaalamu wa Fiqhi ya Kiislamu. Basi hulitumia tamko la "Maula" kwa yule Bwana anayewamiliki watumwa kwa kuwateka (vitani) au kwa kuwanunua, kama ambavyo hulitumia tamko la "Abdi" na "Amah" (mtumwa na mjakazi) juu ya mateka ambao hakimu ameona kuwa inafaa kuwafanya mateka, na hapana mwanachuoni yeyote miongoni mwa Mafaqihi aliyeona ubaya wa kutumia jina hili mtumwa au mjakazi.

Na miongoni mwa mambo yanayostaajabisha ni kauli ya Muhammad Abdul-Wahab isemayo kuwa: "Yeyote mwenye kumwambia mtu fulani, Maulana au Sayyidina basi mtu huyo ni kafiri".22 Wakati ambapo Qur'an Tukufu inalitumia tamko la Sayyid kwa mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Mwenyezi Mungu amesema: "....Mwenye kusadikisha kwa neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu na atakayaekuwa "Sayyid" (Bwana) na mtawa." Qur'an, 3:39.

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na akairarua kanzu yake kwa nyuma na akawakuta Sayyid wake mlangoni." Qur'an, 12:25.

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na watasema Mola wetu hakika tuliwatii Masayyid wetu na wakubwa zetu basi wao wametupoteza njia." Qur'an, 33:67.

Zaidi ya hayo kuna riwaya nyingi Mutawatiri (zimekuja) katika matumizi ya "Sayyid" kwa Mtume na kwa Hasan na Husein 23 [a] kiasi kwamba hapana yeyote mwenye kutia shaka katika kusihi kwake. Na kwa hakika Abubakr alimuomboleza Mtume Mtukufu kwa beti ambazo mwanzoni mwake (alisema:).

"Ewe Jicho lia wala usichoke na haki ya kumlilia iko juu ya Sayyid; Mlilieni yule ambaye alikuwa mlinzi wetu kwenye mabalaa, na sasa amezikwa kaburini."

Naam, Suyuti ameleta (masimulizi) ndani ya Al-Jamius-Saghir toka kwa Daylami ndani ya Musnad ya Al-Fir-Dausi toka kwa Ali [a] kwamba: "As-Sayyid ni Mwenyezi Mungu."

Kama alivyoleta (masimulizi) AI-Azizi ndani ya Sharhul-Jamii As-Saghir kutoka Musnad ya Abi Dawood kwamba, ulikuja ujumbe wa Bani Amir kwa Mtume [s] wakasema: "Wewe ni Sayyid wetu", Mtume akasema, "Sayyid ni Mwenyezi Mungu."

Basi lau hadithi hizi mbili zitasihi itabidi zichukuliwe kwenye maana ya hakika ya "As-Sayyid" yaani "Mwenye kumiliki na muumba" kwani As-Sayyid kwa maana hii inamuhusu Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kwa nini isi-sihi wakati Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alilitumia neno Sayyid kwa Saad Ibn Maadh r.a. Tabari amesimulia kama ifuatavyo: "Alipotokea Saad, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] alisema: "Simameni kwa ajili ya Sayyid Yenu."24

Makatazo haya yaliyokuja hapa kuhusu neno Sayyid yatachukuliwa kwa makusudio ya maana inayokanusha Tauhidi ya Mwenyezi Mungu pindi ikitumika kwa maana ya mwenye kumiliki na kuumba.

Naapa kwamba, ukweli uko wazi hauhitaji maelezo marefu, itakuwaje hali hii wakati ambapo maneno ya Waarabu na Mtume na Masahaba na Tabi'ina na Maimamu wa nyumba ya Mtume na Mafaqihi wa umma, yamejaa kwa matumizi ya maneno haya kuhusu asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na hapana yeyote aliyeona ubaya wa kayatumia kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na waliyachunguza mas-ala haya kwa upana na mtazamo wa undani na hawakuwatia Waislamu katika dhiki na shida na walifahamu kwamba sheria ya Kiislamu ni nyepesi inafuata makusudio na malengo siyo dhahiri (yake) na matamko (yalivyo).

Basi Mawahabi ni kama Makhawariji, waliyadhiki mambo juu ya nafsi zao na juu ya Waislamu kwa vitu ambavyo Mwenyezi Mungu hakuviwekea vikwazo na makundi mawili haya yanaafikiana katika Mas-ala mengi bega kwa bega.

 • 1. Abu Dawood, Juz. 3, uk. 58, Sunan Ibn Majah, Juz 1, uk. 482
 • 2. Siratul-Halabiya, Juz. 3, uk. 348.
 • 3. Maj-Mauz-Zawaid ya Al-Haithami, Juz. 3, uk. 8.
 • 4. Imtau ya Al-Maqrizi, uk. 154.
 • 5. Majmauz-Zawaid, Juz. 6, uk. 120.
 • 6. Sahih Bukhar, Kitabul-Manaqib Fii Alaamatin-Nubuwwah Al- Islam. (2) Sunan Al-Bayhqi, Juz. 4, uk. 70.
 • 7. Sunan Abi Dawood, Juz. 2, uk. 63, Suna Ibn Majah, Juz. 1, uk. 445.
 • 8. Sunan Abi Dawood, Juz. 2, uk. 58, Sunan Ibn Majah, Juz. 1, uk. 481.
 • 9. Sahih Bukhar, Babu Maradhin-Nabi Wawafatih Musnad Abi Dawood, Juz. 2, uk. 197. "Sunan An-Nasai, Juz. 4, uk. 13, Mustadrak Al-Hakim, Juz. 3, uk. 163, Tarikh Al-Khatib, Juz. 6, uk. 262.
 • 10. Al-Ghadir, Juz. 5, uk. 147.
 • 11. Al-Istiab: Tarjuma ya Abdallah, Juz. 1, uk. 368, Al-Ghadir, Juz. 3, uk. 165-167.
 • 12. Al-Istiab katika Tarjuma ya Nuuman, Juz. 1, uk. 297, Al-Iqd Al-Farid cha Ibn Abdi Rabih Al- Undulus, Juz. 3, uk. 235.
 • 13. Tarikh Tabari, Juz. 2, Uk. 253.
 • 14. Iq-dul-Far, Juz. 3, uk. 235.
 • 15. Ikhtilaful-Hadithi katika Hashiya ya kitabu Al-ummu cha Shafii, Juz. 7, uk. 267.
 • 16. Sahih Bukhar mlango wa 32 katika milango ya Jeneza, Juz. 2, uk. 80, Ikhtilaful-Hadith cha Shafii, Juz. 7, uk. 266, Al-Muwatta cha Malik, Juz. 1, uk. 96, Sahih Muslim Juz. 1, uk. 344, Sunan Nasai, Juz. 4, uk. 17, Sunan Bayhaqi, Juz. 4, uk. 72.
 • 17. Sunan Abi Dawood, Juz. 2, uk. 59, Sunan Nasai, Juz. 2, uk. 17.
 • 18. Musnad Ahmad, Juz. 1, uk. 235-237. Mustadrak ya Al-Hakim, Juz. 1, uk. 191. Na amesema Adhahabi ndani ya Tal-Khisul-Mustadrak: Sanad yake ni nzuri.
 • 19. As-Sunan Al-Kubra, Juz. 4, uk. 70.
 • 20. Umdatul-Qarii, Juz. 4, uk. 87.
 • 21. An-Nihayah cha Ibnul-Athir, Juz. 3, uk. 170.
 • 22. Kashful-Irtiyabi cha Sayyid Muhsin al-Amin: Amenakili toka katika Khul-Satul-Kalam.
 • 23. Kinachokusudiwa ni ile hadithi isemayo Hasan na Husain ni Masayyid wa vijana wa peponi.
 • 24. Tabari, Juz. 2, uk. 249.