read

Utangulizi Wa Chapa Ya Pili

Haja Ya Kuweko Mkutano Wa Kiislamu Wa Ulimwengu Ili Kuidurusu Tauhidi Na Shirki

Bila shaka Al-Kaaba ndiyo nyumba ya mwanzo iliyojengwa kwa ajili ya ibada ya Mwenyezi Mungu na humo apwekeshwe yeye Mwenyezi Mungu, na kwa hakika misingi yake ilidhoofika kabla ya zama za Nabii Nuh [a], na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu inatueleza juu ya jambo hilo.

"Kwa yakini nyumba ya mwanzo iliyowekwa kwa ajili ya watu (kufanya Ibada) ni ile iliyoko katika jangwa takatifu (Makka) lenye kubarikiwa na muna uongofu kwa walimwengu." Qur'an, 3:96.

Na kwa kweli Al-Kaaba (baada ya kujengwa) ilichakaa kwa sababu ya tufani (zilizokuwa zikitokea), jambo ambalo lilipelekea kubomoka jengo lake na kuvunjika kuta zake, na alipokuja Nabii Ibrahim [a] akalijenga jengo lake kama anavyotufahamisha Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema:
"Na kumbukeni Ibrahim alipoinua kuta katika nyumba (Al-Kaaba) yeye na Ismail."
Qur'an, 2:127
Na baada ya Ibrahim [a] kuisimamisha misingi yake na kuijenga Al-Kaaba alielekeza mwito maalum kwa amri ya Mwenyezi Mungu na Wahyi wake kwa kila mwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu ili aizuru nyumba hii na akahiji.

Mwenyezi Mungu anasema: "Watangazie watu habari ya Hijja." Qur'an, 22:27.

Na Mwenyezi Mungu ameifanya nyumba yake hiyo tukufu, kuwa ni kituo cha mkusanyiko wa waumini na ni nyumba ya amani kwa wenye kumpwekesha, basi inapasa mtu yeyote asihisi hofu awapo hapo wala asiogope hatari yoyote wala dhulma, kama kauli ya Mwenyezi Mungu inavyojulisha.

"Na kumbukeni tulipoifanya nyumba (Al-Kaaba) pawe ni mahala panapoendewa na watu na pawe pa amani." Qur'an, 2:125 Pia 28:57.

Hiyo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameifanya ziyara ya kuzuru nyumba yake iwe ni dhamana ya kuendelea kwa maisha ya waumini, na imekuwa kusimamisha maadhimisho ya Hijja ni jambo linaloleta amani kwa maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii, pia kwa maisha ya kimaada na ya kiroho kwa waumini.

"Mwenyezi Mungu ameifanya Al-Kaaba (ambayo ni) nyumba takatifu kuwa tengenezo la (maisha ya) watu…" Qur'an, 5:97.

Kwa mujibu wa aya hii Tukufu Imam As-Sadiq [a] anasema: "Dini itaendelea kuwa imara muda wote Al-Kaaba itapokuwa imesimama."1

Kwa hakika ubora wa kuizuru nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu ni mwingi mno kuliko tunavyoweza kuuzungumzia ndani ya utangulizi huu, lakini kitu tunachopenda kukiashiria ni yale mazingira iliyonayo Al-Kaaba leo hii, mazingira ambayo yameifanya iwe mikononi mwa watu ambao wao wanajiona kuwa ni watumishi wa miji miwili mitakatifu, na wanajifakharisha kwa jambo hilo.

Nasi kufuatana na ubora ambao Mwenyezi Mungu ameihusisha nao Al-Kaaba, tunajiuliza mambo mawili muhimu.

Kwanza: Je, hivi leo hii maadhimisho ya Hijja yanazingatiwa kuwa ni tengenezo la (litakalowarekebisha) watu sasa hivi?

Je, kuizuru Al-Kaaba na kukusanyika pembezoni mwake Waislamu zaidi ya milioni mbili kumeleta amani kwenye maisha ya kimaada na ya kiroho kwa Waislamu na kuwadhaminia kuendelea kwa amani hiyo maishani mwao?

Kama kweli ndivyo, basi hebu tuulizaneni, ni msimu upi miongoni mwa misimu ya hija za kila mwaka Makhatibu wa Makka na Madina walipata kuzungumzia masuala ya maisha ya Waislamu?

Na je, mambo ya Waislamu na matatizo yao yalipata kuwasilishwa katika uwanja wa majadiliano na kuyatafutia ufumbuzi katika mikusanyiko hii mikubwa?
Basi ni lini watumishi hao wa Haramain (Makka na Madina) na Makhatibu wao walipata kuyasuluhisha mambo ya Waislamu na matatizo yao?

Na ili iwe kama mfano kuhusu mazingira ya kuhuzunisha ambayo Al-Kaaba inakabiliana nayo, ninaeleza kisa kifuatacho.

Mwaka 1396 A.H. nilibahatika kuizuru nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu na nikafanya umra pamoja na kundi la watu waliohifadhi Qur'an, ili kushiriki mashindano ya kuhifadhi Qur'an.

Na katika siku hizo (tulipokuwa Makka) idhaa mbali mbali na vyombo vya habari vilikuwa vikitangaza uvamizi wa Israel huko kusini mwa Lebanon na vitendo vyake vya kishenzi ilivyokuwa ikivifanya dhidi ya Wapalestina na wengineo.

Na katika siku ya Ijumaa tulifika kwenye kituo cha kuhifadhisha Qur'an kilichopo ubavuni mwa msikiti mtukufu wa Makka, na baada ya kumalizika kikao cha mashindano ya Qur'an ­paliadhiniwa na hivyo wakati wa Sala ukawa umeingia, na Khatibu akapanda kwenye mimbari ili kutoa khutba.

Mimi nilikuwa nikidhnai kwamba, Khatibu huyu huenda atahutubia kuhusu tukio lililotawala katika kipindi hicho (nalo ni lile la uvamizi kusini mwa Lebanon na wajibu wa Waislamu kusimama dhidi ya vita hivi vya Kizayoni vya kupanua mipaka yake) lakini mara dhana yangu nzuri ilibadilika na kuwa yakini mbaya, kwani Khatibu huyu alianza kuzungumzia unadhifu na namna ulivyosisitizwa na athari zake nzuri na (alizungumzia) adabu zinazohusu msikiti na Sala ya Ijumaa na mengine kama hayo na wala hakutamka japokuwa neno moja kuhusu tukio lilokuwepo katika kipindi hicho.

Kuna mtu fulani alikuwa amekaa pembeni yangu ambaye alikuwa Mmisri miongoni mwa "Ikh-wanil-Muslimina" waliokimbia kutoka Misri na kwenda Hijaz, basi mimi nikamwambia, hivi kweli khutba hii ilikuwa inaafikiana na mazingira wanayoishi Waislamu leo hii? Na kwa kuwa mtu huyu alikuwa mtu wa haki alishirikiana nami katika masikitiko na huzuni.

Inaonyesha wazi kwamba khutba za sala ya Ijumaa zote huwa zinafanyiwa sensa na uchunguzi kabla ya kusomwa, na serikali ya Saudia ndiyo inayowaelekeza Makhatibu kile watakiwacho kukisema ili wasije wakayavuka maelekezo hayo. Basi hukuti katika khutba hizo maelezo yoyote juu ya ukoloni na vitimbi vyake dhidi ya Uislamu wala maneno yanayohusu maadui wa Uislamu na hali za Waislamu.

Amma kuwazungumzia Mashia na "Majusi" hilo linazungumzwa kwa mapana yote kwa kiwango cha kumridhisha shetani.

Na kwa hakika baada ya mapinduzi (ya Kiislamu) nchini Iran, kilitolewa kitabu kiitwacho, "Wajaa Daurul-Majus" yaani umefika wakati wa majusi.2

Baada ya maelezo yaliyotangulia, je, inafaa kusemwa kwamba, watawala wa Najdi na Hijazi ni watumishi wa ‘Haram ya Mwenyezi Mungu’ na walinzi wa ‘Nyumba ya Mwenyezi Mungu’?!
Na je, Hivi katika zama zao (Watawala hawa) Al-Kaaba imekuwa ni tengenezo kwa ulimwengu wa Kiislamu?

Ya Pili: Je, Haram ya Mwenyezi Mungu ni nyumba ya utulivu na amani siku hizi?

Kwa hakika Qur'an Tukufu inaizingatia Al-Kaaba na viunga vyake kuwa ni Haram ambavyo ni mahala pa Mwenyezi Mungu penye amani.

Mwenyezi Mungu Anasema: "Na yeyote atakayeingia Makka atakuwa katika amani."Qur'an, 3:97.

Bila shaka Nabii Ibrahim ambaye ndiye baba wa Waislamu wote, alimuomba Mola wake aifanye Haram (ya Makka) kuwa hi mahali pa salama na amani. Mwenyezi Mungu amesema Akimnukuu Ibrahim:
"Ewe Mola wangu ufanye mji huu kuwa mahali pa amani." Qur'an, 14:35.

Na sasa hebu tujiulize: Je, Watumishi hao wa Haramaini hivi wao kweli ndiyo walinzi wa sheria hii ya Mwenyezi Mungu?

Je, Waislamu pamoja na khitilafu zao za Madh-hebu wanao uhuru wa kutatua mambo yao ya kisiasa na kubadilishana mitazamo yao hapo kwenye Al-Kaaba Tukufu?

Hivi Waislamu waliokusanyika kwenye Al-Kaaba wanaweza kutangaza matatizo yao na kujulishana wao kwa wao hali zao na mambo yanayowakabili?

Je, Mambo ndivyo yalivyo, au ni kwamba uhuru wa kusema na kutoa maoni unatolewa kwa madh-hebu ya Hanbal peke yake tu miongoni mwa Madhehebu ya Kiislamu?! Na wala hakuna ruhusa ya kutoa fikira na maarifa ya juu katika Uislamu isipokuwa zile fikra dhaifu za Ibn Taymiyyah na Ibn Al-Qayyim na zaidi ya hapo ni fikra za Muhammad Ibn Abdil-Wahhab!!

Na wala hakuna kizungumzwacho katika khutba za Ijumaa na nyinginezo kuhusu maudhui yoyote ya Uislamu isipokuwa ni kuzuru makaburi na kuharamisha hafla za maulidi ya Mtume [s] na kuharamisha kuwaheshimu Mawalii wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, eti kama kwamba Uislamu umedhibitiwa katika maudhui hizi peke yake!!

Na yeyote mwenye kuzikhalifu fikra zao hizo batili, basi malipo yake ni kumhukumu kuwa ni kafiri na ni mshirikina, na kwamba inajuzu kumshutumu na kumpiga na kumlaani, hivyo basi ni kafiri tena mshirikina na mengineyo.

Je, hii ndiyo maana ya "Haraman Aminan" (Yaani Nyumba Tukufu ya Amani) na je, hivi tutakuwa tuko kinyume cha ukweli ulivyo iwapo tutasema kwamba leo hii Al-Kaaba inakanyagwa na nyayo za Mawahabi?

Bila shaka fikra Kiwahabi imesimama juu ya msingi wa kuyakufurisha Madh-hebu na vikundi vya Kiislamu na kupanda mbegu ya utengano miongoni mwa Waislamu na kuharibu heshima ya Uislamu na mafunzo yake bora na kuondosha athari za Utume; na (pia Uwahabi umesimama juu ya msingi wa) kufanya mapatano na kujipendekeza kwa kila waovu na watawala wachafu na waovu mpaka hata (wanajipendekeza) kwa Yazid bin Muawiyah!!
Nao Makhatibu na waandishi ambao wanatumiwa na Masultani wa Kiwahabi, hao siyo Makhatibu (Safi) isipokuwa ni waajiriwa wa Pilato na wawaidhi wa Masultani, hawasemi wala hawaandiki ila kile wanachokitamani mabwana zao wa Kiwahabi wasiyoijuwa Dini.

Ewe msomaji Mtukufu, huenda ukatuona sisi labda tumezidi mno katika kuwaelezea (Mawahabi) na tumejitenga mbali na ukweli na uadilifu katika maelezo tuliyoyaeleza juu ya kundi hili.

Lakini ili usiendelee kuwa na mashaka na wala usitutuhumu kuvuka mipaka katika maelezo, basi sisi tunaweka mbele ya macho yako picha ya Jalada laki moja kati ya vitabu ambavyo vimechapishwa na Serikali ya Saudia na kuvigawa kwa wingi, na kitabu hiki kinahusu kumtukuza na kumheshimu mtu ambaye jeshi lake liliipiga Al-Kaaba kwa mizinga, na kuhalalisha kila kilicho haramu katika mji wa Mtume wa Mwenyezi Mungu [s] kwa jeshi lake kuukalia siku tatu kamili likipora mali na kuwavunjia watu heshima zao na kuwauwa!

Na utaona kwa macho yako pameandikwa juu ya jalada kwamba Wizara ya Elimu katika Serikali ya Kiwahabi ndiyo iliyobeba jukumu la kuchapa na kusambaza kitabu hiki kilicho batili. Baada ya maelezo hayo.... tunasema kwamba: Katika nchi ya Hijazi kuna uhuru usiyo na mpaka na wakati huo huo kuna ukandamizaji usiyo na mpaka.

Ama uhuru usiyo na mpaka ni ule walionao Mawahabi na washirika wao miongoni mwa wanaokula fadhila zao, kwani vitabu na vijitabu vilivyojazwa maandiko yanayowasifia madhalimu na kuwatukuza mafasiki wa Kibanu Umayyah na Bani Abbasi vinachapishwa na kusambazwa bila kikwazo cho chote au Sharti yoyote, bali serikali inachangia kuvichapisha kuvisambaza.

Ama shinikizo na ugandamizaji na unyanyasaji na vizuizi na kupiga marufuku kuko kwenye vitabu vinavyozungumzia Uislamu kama ulivyo shuka toka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na vinavyozungumzia Ahlul-Bait ambao Mwenyezi Mungu amewalinganisha na Qur'an na akaiteremsha Qur'an ndani ya nyumba zao na akawatakasa mno kutokana na uchafu.

Naam... bila shaka kila kitabu kianchoingia Hijazi (Saudi Arabia) ni lazima kichunguzwe na kufanyiwa utafiti na wala hakiruhusiwi kuingia nchini humo mpaka kwanza Wizara ya habari itoe ruhusa!!

Kwa hakika mwaka uliopita, ambao ni mwaka wa 1404 A.H. mimi nilikwenda hija na kuyazuru maziyara matukufu likiwemo la Mtume [s] na kizazi chake kitukufu [a] huko Madina. Basi katika uwanja wa ndege wa Madina nilikuwa na nakala kumi za kitabu kiitwacho "Mas-dar Al-Wujud", ambacho kinachambua dalili za kimaumbile na za kiakili juu ya kuwepo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Na lengo la kuzichukua nakala hizo katika nchi hiyo ilikuwa ni kushirikiana kueneza Tauhid na kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba, mtu anayehusika na mambo ya vitabu katika uwanja wa ndege aliamuru nakala hizo zizuwiwe na zisisambazwe mpaka hapo itakapotolewa hukumu nyingine. Na baada ya yeye kukipitia kitabu hiki kwa haraka haraka aliniambia: "Japokuwa kitabu hiki ni chenye faida na ni kizuri lakini ni lazima kukipeleka kwenye wizara ya habari nawe utakichukua kutoka kwao. Naam hii ndiyo maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Nchi yenye Amani"!!!?

  • 1. Wasailus-Shia, juz. 8 uk 14
  • 2. Watu waliokuwa wakiabudu moto