read

Sura Ya 2: Uarabuni Kabla Ya Uislamu

Ili kuielewa hali iliyokuwapo Bara Arabu kabla ya Uislamu vyanzo vifuatavyo vinaweza kututosha: Agano la Kale (licha ya kuwa na mabadiliko yote ambayo yaliyofanywa humo).

Maandishi ya Wagiriki na Warumi kwenye Zama za Kati.

Historia ya kiislamu iliyoandikwa na wanachuoni wa kiislamu, na Masalio ya zamani, yaliyopatikana kutokana na ufukuaji uliofanywa na mustashirik, ambao ulidhihirisha habari kwa kiasi fulani.

Licha ya vyanzo tulivyovitaja hapo juu, mambo mbalimbali yahusianayo na historia ya Uarabuni bado hayajaeleweka kwa ukamilifu, na yanasalia kuwa fumbo lisilofumbuka.

Hata hivyo, kwa vile kujifunza hali ya Uarabuni ya kabla ya Uislamu ni utangulizi tu wa mazungumzo yetu; lakini azma yetu hasa ni mchanganuo wa maisha ya Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) hivyo basi, tunatoa hapa chini mukhtasari wa taarifa za baadhi ya watu na hali za mambo zilizo maarufu za Waarabu wa kabla ya Uislamu.

Ni ukweli ukubalikao kwamba tangu kwenye siku za kale, Rasi ya Bara Arabu ilikuwa ikikaliwa na makabila mengi, ambayo baadhi yao yamekwisha kupotea kutokana na kupita muda mrefu. Hata hivyo, kwenye historia ya nchi hii, makabila matatu yafuatayo, ambayo baadae yaligawanyika na kuwa koo nyingi tofauti, yalipata sifa kuu kuliko mengineyo:

Waba’idah: Neno ‘Ba’idah’ lina maana ya iliyokufa, isiyokuwepo tena, na watu hawa waliitwa hivyo kwa sababu, kutokana na uasi wao uliodumu, walifutiliwa mbali kutoka usoni mwa ardhi, ikiwa ni matokeo ya misiba ya mbinguni na ya duniani. Inawezekana kwamba watu hawa ndio waliokuwa makabila ya Waadi na Wathamudi waliokuwa wakitajwa mara kwa mara kwenye Qur’ani Tukufu.

Waqahtani: Hawa walikuwa ni vizazi vya Ya’rab bin Qahtani. Watu hawa waliishi nchini Yemen na sehemu nyingine za Bara Arabu ya Kusini na waliitwa Waarabu wa damu kamili. Wayemeni wa siku hizi na makabila ya Aws na Khazraj, ambao waliyajumlisha makabila mawili makuu ya Madina, kwenye siku za awali za Uislamu ni wa kizazi cha Waqahtani. Walifanya juhudi za nguvu kwa ajili ya maendeleo ya Yemen na wameacha idadi kadhaa ya ustaarabu ukiwa ni kumbukumbu yao. Sasa watu wanajifunza maandishi yao, kwa mujibu wa njia za kisayansi, historia ya Waqahtani imegundua hivyo kwa kiwango fulani. Lolote lile lisemwalo kuhusu utamaduni wa kabla ya Uislamu na ustaarabu wa Bara Arabu linahusiana kabisa na kundi hili la Waarabu na linauhusu mkoa wa Yemen.

Waadnani: Hawa ni dhuria wa Nabii Isma’il (a.s.). Maelezo marefu ya nasaba ya kabila hili yatatolewa kwenye hatua itakayofuatia baadae, lakini tukizungumzia kwa kifupi tu, hali ni hii: Nabii Ibrahimu (as) aliamrishwa na Allah kumloweza mwanawe Isma’il (a.s.) na mamie Haajar (a.s.) kwenye nchi ya Makkahh. Hivyo basi akawasafirisha kutoka Palestina na kuwapeleka kwenye bonde lenye kina kirefu (Makkahh) lililokuwa kame kabisa. Allah Aliwahurumia na akawajaalia chemchemi ya Zamzam. Nabii Isma’il (a.s.) alioa kwenye kabila lililoitwa Jarham, lililokita mahema yao kwenye sehemu iliyokuwa karibu na Makkahh. Dhuria wake (Nabii Isma’il a.s.) walikuwa wengi. Mmoja wao alikuwa ni Adnan ambae alisogezwa mbele kwa vizazi vichache kutoka kwa Nabii Isma’il (a.s.).

Dhuria wa Adnan waligawanyika katika makabila mengi. Kabila lililojipatia sifa kutoka miongoni mwao lilikuwa ni lile la Quraysh, na Bani Hashim walikuwa sehemu ya kabila hili.

Maadili Ya Waarabu Kwa Ujumla

Tunaposema hivi tuna maana ya maadili na tabia za kijamii zilizokuwapo miongoni mwa Waarabu kabla ya Uislamu. Baadhi ya desturi zikifuatwa na Waarabu wote. Sifa za Waarabu wote na zenye kustahili kusifiwa kwa ujumla zingaliweza kuelezwa kwa ufupi hivi, katika sentensi chache:

“Waarabu wa Zama za Ujinga (zama za kabla ya Uislamu) na hasa vile vizazi vya Adnan walikuwa wakarimu na wenye tabia ya ukaribishaji. Walivunja ahadi kwa shida mno. Waliamini kuwa kuvunja ahadi ni dham- bi isiyosameheka. Walikuwa wakiishika dini yao na walijaaliwa sifa kamili ya ufasaha wa lugha. Walikuwa na akili zenye uwezo mkubwa wa kukum- buka mambo. Kwa urahisi sana waliweza kujifunza beti (za mashairi) na hotuba kwa kukariri. Kwenye sanaa ya utunzi wa mashairi, waliwazidi wengineo wote.

Ushujaa wao ulikuwa ukifahamika kote. Walikuwa na ustadi mkuu kwenye mbio za farasi, na upigaji mishale. Waliamini kuwa kumkimbia adui ni jambo lenye kuchukiza na lisilopendeza kabisa.

Na pengine tungaliweza kuzitaja hapa sifa zao zilizokuwa njema zaidi. Hata hivyo, kinyume na hivi, silsila ya utovu wao wa maadili mema na tabia zao mbaya, ambazo kwa kiasi fulani, zimewafanya waichukue tabia ya pili, hufutilia mbali utukufu wa mafanikio, na kama wasingalifunguliwa dirisha kutoka kwenye yasiyoonekana, msokoto (scroll) wa maandishi wa maisha yao ya kibinaadamu ungekunjwa, nao wangeliangukia kwenye shimo lenye kina kirefu na lenye kutisha la kutokuwapo. Kwa kauli nyingine ni kwamba, kama jina la Uislamu lilishalo nafsi lisingaliziangaza nyoyo zao katikati ya karne ya sita Masihiya, siku hizi usingaliziona dalili zozote za Waarabu na hadithi ya Waarabu wa Baaidah ingalirudiwa.

Kutokana na kukosekana kwa mwongozo na maelekezo sahihi, na kuwepo kwa utovu wa maadili mema, na imani za kishirikina, Waarabu walikuwa wakiishi maisha yaliyo sawa na yale ya wanyama. Historia imetuwekea kumbukumbu za hadithi za vita vya miaka hamsini na vita vya miaka mia, na hizo pia ni kwa sababu ndogo ndogo na zisizo na maana.

Huu utawala huria, ukosefu wa sheria na taratibu na kukosekana kwa serikali yenye mamlaka ambayo ingeliweza kuitawala hali ya mambo na kuwashughulikia waasi vipasikavyo, vilikuwa sababu ya Waarabu kuishi maisha ya kibedui na ya kuhama hama kwao kwa kila mwaka pamoja na wanyama wao wakiziendea sehemu za majangwa ambako maji na malisho viliweza kupatikana. Kila walipopata maji na majani mabichi mahali popote pale walikita mahema yao karibu na hapo. Hata hivyo, mara tu wapatapo mahali pafaapo zaidi, waliendelea na kuhamahama kwao kwenye jangwa.

Kuhamahama na hali ya kutokuwa na maskani maalum kulitokana na mambo mawili; kwanza ni ile hali mbaya ya jiografia ya eneo hili, na jingine ni kujitia kwao kwenye umwagaji wa damu uliokithiri, jambo lililowawajibisha kufanya misafara ya mara kwa mara na uhamiaji.

Je, Waarabu Wa Kabla Ya Uislamu Walistaarabika

Kama matokeo ya mafunzo yake juu ya hali ya Waarabu wa Zama za Ujinga, mwandishi wa kitabu kiitwacho Tama-ddun-i- Islam wa Arab’ amemalizia kwa kusema kwamba Waarabu hao walikuwa wamestaarabika kwa karne nyingi.

Kwa mujibu wa maoni yake, majengo matukufu na marefu waliyoyajenga kwenye sehemu mbalimbali za Uarabuni na uhusiano wao na mambo ya kibiashara na mataifa mbalimbali yaliyoendelea, kunathibitisha kustaarabika kwao, kwa kuwa, watu walioweza kujenga majumba makubwa kama hayo hata kwenye kipindi cha kabla ya kuja kwa Warumi, na wakawa na uhusiano wa kibiashara na mataifa makuu ya ulimwengu, wasingeliweza kuitwa washenzi.

Tena, kwenye sehemu nyingine, ameitaja fasihi ya Waarabu na kuwa kwao na lugha kamili kuwa ni ushahidi wa kuliunga mkono dai lake hilo la kwamba walikuwa na ustaarabu uliokuwa na mizizi ya kina. Anasema: “Kwa mfano, tusikijue cho chote kile kihusianacho na historia ya Waarabu wa kale, vivyo, tungaliweza kuikataa dhana ya kuwa kwao watu wasiostaarabika, kwa sababu, chochote kile kihusianacho na lugha ya taifa, vilevile chahusiana na kustaarabika na utamaduni wa taifa hilo. Haiwezekani kwamba lugha nzuri mno yenye kuhusiana na uandishi wake, ijitokeze bila ya chanzo chochote. Zaidi ya hapo, udumishaji wa uhusiano na mataifa yaliyoendelea daima huwa ni njia ya maendeleo kwa watu wenye uwerevu.”

Mwandishi tuliyemtaja hapo juu amezitumia kurasa kadhaa za kitabu chake kuthibitisha kuwapo kwa ustaarabu wa hali ya juu miongoni mwa Waarabu wa zama za kabla ya Uislamu na akaliweka tumaini lake kuhusiana na jambo hili kwenye mambo matatu, ambayo ni:

(1). Kuwa kwao na lugha nzuri zaidi.
(2). Kudumisha kwao uhusiano na mataifa yaliyoendelea
(3). Majengo mazuri mno ya Yemen yaliyotajwa na Herodote na Artemidor, wanahistoria mashuhuri walioishi mwenye zama za kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (a.s.) pamoja na Mas’udi na waandishi wengine wa historia ya kiislamu.1

Hakuna shaka kuhusiana na ukweli uliopo kwamba, zilikuwapo staarabu za nyakati fupifupi kwenye sehemu mbalimbali za Uarabuni, lakini hoja alizozitoa mwandishi huyu hazitoshelezi kuthibitisha ya kwamba ulikuwapo ustaraabu na utamaduni kwenye sehemu zote za nchi hii.

Kwanza, kukamilika kwa lugha kunaandamana na dalili nyingine za ustaarabu, lakini kimsingi, kiarabu hakiwezi kudhaniwa kuwa ni lugha yenye kujitegemea, isiyohusika na Kiebrania, Kishamu, Kiassiria, Kikaldayo, kwa sababu, kama ilivyothibitishwa na wanafalsafa, lugha zote hizi zilihusiana kwenye wakati fulani na zote zilitokana na lugha moja. Katika hali hiyo, uwezekano uliopo ni kwamba, kiarabu kiliufikia ukamilifu wake pamoja na Kiebrania, na Kiassiria na ilijitokeza katika hali ya lugha binafsi baada tu ya kuufikia ukamilifu huo. Kuwa na uhusiano wa kibiashara na mataifa ya ulimwenguni yaliyoendelea bila shaka ni ushahidi wa maendeleo na ustaarabu wa Waarabu.

Hata hivyo, swali liibukalo hapa ni kama sehemu zote za Bara Arabu zilikuwa na uhusiano huo na mataifa mengine, au yawezekana kwamba Hijaz haikuwa nao? Zaidi ya hapo, uhusiano na Iran, na Wagiriki wa majimbo mawili ya ‘Hira’ na ‘Ghassan’ yaliyoko kwenye jimbo la Hijaz vile vile hauwi ushahidi wa kustaarabika kwao, kwa kuwa hali yao iliweza kuwa kama ile ya ‘setalaiti’, ambayo kwa kweli twaweza kuiita makoloni. Hata katika zama zetu hizi ziko nchi nyingi barani Afrika, zilizo sehemu ya makoloni ya nchi za magharibi, lakini hazina dalili zozote za ustaarabu na utamaduni wa kizungu.

Hata hivyo, haiwezekani kukana kwamba ulikuwako ustaarabu mzuri zaidi huko Saba na huko Ma’arib kwenye jimbo la Yemen. Kwa kuwa, tukiyaachilia mbali yale tuliyokwisha kuyasema kuhusiana na jambo hili, kwenye Agano la Kale, na yule mwanahistoria Herodote na wengineo, mwanahistoria mashuhuri, Mas’udi anasema hivi kuhusu mji wa Ma’arib: “Ulizungukwa na majengo mazuri, miti ya kivuli na vijito vitiririkavyo kwenye pande zote.

Eneo la jimbo hili lilikuwa pana mno kiasi kwamba hata mpandafarasi mwepesi wa mwendo asingaliweza kuumaliza urefu na upana wake kwenye muda wa mwezi mzima; na msafiri, awe anampanda mnyama au anasafiri kwa miguu, haweza kuliona jua anapoikata nchi kutoka mwishilizio mmoja hadi mwingine, kwa kuwa barabara zilifunikwa na miti ya kivuli kwenye pande zote mbili. Nchi hii iliendelea kustawi na maji yalipatikana kwa wingi. Na serikali yake iliyokuwa imara, ilikuwa maarufu duniani kote.2

Hata hivyo, iwekwe akilini kwamba habari hizi hazituongozi kwenye ustaarabu uliopasika kuwako mwenye majimbo yote ya Bara Arabu na hasa kule Hijaz, ambako kwa hakika hakukuwa na dalili zozote za ustaarabu huu, kiasi kwamba hata Bwana Gustave Le Bon, kuhusiana na jambo hili, anasema hivi: “Ukiiachilia mbali mipaka yake ya Kaskazini, Bara Arabu ilisalia kuwa huru kutokana na mashambulizi ya wageni na hakuna yeyote aliyeweza kuikalia. Washindi Wakuu wa Iran, Urumi na Ugiriki waliouteka ulimwengu mzima hawakuijali Bara Arabu hata kidogo.”3

Na hata kama tukichukulia kwamba hadithi hizi ni za kweli kuhusiana na majimbo yote ya Rasi ya Bara Arabu, yale yote tuwezayo kuyasema kwa uhakika ni kwamba, kwenye wakati wa kuingia kwa Uislamu haikuonekana dalili yoyote ya ustaarabu huo, kwa kuwa Qur’ani Tukufu inalitaja jambo hili na inasema:

وَكُنْتُمْ عَلَىٰ شَفَا حُفْرَةٍ مِنَ النَّارِ فَأَنْقَذَكُمْ مِنْهَا ۗ {103}

“…; Na (enyi Waarabu! Kabla ya kusilimu kwenu) mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto wa Jahanamu Naye (Allah) Akawaokoeni nalo (kwa Uislamu)…” (Al- Imran 03: 103)

Kurasa za Nahjul Balagha zilipokuwa zikiisimulia hali ya Waarabu wa kabla ya Uislamu, zina ushuhuda ulio hai kwamba, ukiliangalia jambo hili la mtindo wa maisha, akili, uchafu na kuharibika kwa maadili, waarabu walikuwa katika hali ya kuhuzunisha. Hapa tunanukuu maneno yaangazayo ya Sayyidna Ali, Amirul Muuminiina (a.s.). Kwenye moja ya hotuba zake anaielezea hali ya mambo ya Bara Arabu kwenye siku za kabla ya Uislamu hivi: “Mola Alimteua Muhammad kuwaonya watu wa ulimwenguni na kuwa mdhamini wa Ufunuo Wake na Kitabu chake.

Nanyi waarabu mlikuwa mkizitumia siku zenu kwa dini iliyokuwa mbaya zaidi ya zote na kwenye sehemu mbaya zaidi. Mlikuwa mkiishi kwenye sehe- mu za mawe na miongoni mwa nyoka walio vipofu (wasiosogea kwa sababu ya sauti yoyote ile). Mlikunywa maji ya tope na kula chakula duni (kama vile guruguja, na unga wa mbegu za tende). Mlimwaga damu yenu wenyewe na mkajitia kwenye kukata udugu. Mmewaweka masanamu miongoni mwenu. Hamkuziambaa dhambi.”

(Nahjul Balagha, Hotuba ya 26).

Hapa, mifano ya hali ya kishenzi ya Waarabu wa Zama za Ujinga imenukuliwa. Ikiwa kama mfano, tunanukuu hapa chini hadithi ya As’ad bin Zurarah inayotupa mwanga kwenye tabia mbalimbali za watu wa Hijaz:

As’ad Bin Zurarah Akutana Na Mtukufu Mtume (S.A.W.W)

Kwa muda mrefu vita kali ilipiganwa baina ya makabila mawili (ya mjini Yathrib) Aws na Khazraj. Katika wakati huo, As’ad bin Zurarah, mmoja wa machifu wa Khazraj alifunga safari kwenda Makkahh kwa ajili ya kuimarisha nguvu ya kabila lake. Lengo lake lilikuwa kwenda kutafuta msaada wa kijeshi na kiuchumi kutoka kwa Waquraishi ili kumshinda adui yake mwenye umri wa miaka mia moja (yaani kabila la Aws). Kutokana na uhusiano wake wa tangu kale na ‘Atbah bin Rabiyyah, alifikia kwake. Alimweleza shabaha ya safari yake ile na akamwomba msaada. Hata hivyo, huyu rafiki yake wa tangu kale (‘Atbah), alimjibu kwa maneno haya:

“Hivi sasa hatuwezi kuridhia ombi lenu kwa sababu sisi wenyewe tumo mwenye mashaka ya ajabu. Ameamka mtu kutoka miongoni mwetu. Anawatusi miungu wetu, anaamini kuwa jadi zetu walikuwa wapuuzi na wajinga. Kwa maneno yake matamu amewavutia baadhi ya vijana wetu na hivyo amejenga mfarakano mkubwa baina yetu. Anatumia muda wake mwingi kwenye ‘Sha’ab (Njia ya Mlimani) ya Abu Twalib ila kipindi cha wakati wa Hajj. Hata hivyo, katika wakati huo wa Hajj, hujitokeza kutoka huko na kukaa kwenye Hajjar Isma’il. Hapo huwaitia watu kwenye dini yake.”

As’ad aliamua kurudi nyumbani bila ya kukutana na machifu wengine wa Kiquraishi. Hata hivyo, ili kuitimiza desturi ya Waarabu ya tangu kale, aliamua kufanya ibada kwenye Nyumba ya Allah (Al-Ka’ba) kabla ya kuondoka kwake. Lakini ‘Atbah alimwonya asije akayasikia maneno yenye kuroga ya yule Nabii mpya wakati atakapokuwa akifanya tawafu, na akavutika naye. Ili kulitatua tatizo hili, ‘Atbah alimshauri As’ad kushindil- ia pamba masikioni mwake ili kwamba asiweze kumsikia yule Nabii.

Pole pole As’ada alishuka na kuingia kwenye Masjidul Haraam na akaan- za kufanya tawafu kwenye ile Ka’abah. Kwenye mzunguko wa kwanza alimtupia jicho Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na akamwona ameketi kwenye Hajjar Isma’il wakati Bani Hashim kadhaa walikuwa wakimhami. Akiuchelea uchawi wa maneno ya Mtume (s.a.w.w), yeye (As’ad) hakumwendea.

Hata hivyo, hatimaye, alipokuwa akiizunguuka Al-Ka’ba (kwenye ile ibada ya tawafu) aliwaza akilini mwake na akajihisi kwamba alikuwa akitenda jambo la kijinga kwa kumwepuka Mtume (s.a.w.w) kwa sababu, inawezekana kwamba watu wanaweza wakamwuliza kuhusu jambo hili atakaporudi Yathrib na itakuwa ni lazima kwake yeye kuwapa jibu litoshelezalo. Hivyo basi, aliamua kupata taarifa za awali kuhusu hiyo dini mpya, bila ya kuchelewa zaidi.

Alijitokeza mbele na akamsalimu Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kwa maneno: Awam Sabahan” (Habari za asubuhi), kwa mujibu wa desturi zilizokuwako kwenye zama za ujinga. Hata hivyo, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alimjibu; akamwambia kwamba Allah Ameamrisha aina iliyo bora zaidi ya kusalimiana. Alisema kwamba watakapokutana watu wawili, hawana budi kusema: “Salaamun ‘Alaykum.” Kisha As’ad alimwomba amfafanulie lengo na madhumuni ya dini yake. Ili kumjibu A’sad, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alimsomea Aya mbili zifuatazo:

قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۖ وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُمْ مِنْ إِمْلَاقٍ ۖ نَحْنُ نَرْزُقُكُمْ وَإِيَّاهُمْ ۖ وَلَا تَقْرَبُوا الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ ۖ وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلَّا بِالْحَقِّ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُمْ بِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ {151}

وَلَا تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ حَتَّىٰ يَبْلُغَ أَشُدَّهُ ۖ وَأَوْفُوا الْكَيْلَ وَالْمِيزَانَ بِالْقِسْطِ ۖ لَا نُكَلِّفُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۖ وَإِذَا قُلْتُمْ فَاعْدِلُوا وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۖ وَبِعَهْدِ اللَّهِ أَوْفُوا ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُمْ بِهِ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ {152}

“Sema (ewe Rasuli Wetu Muhammad): ‘Njooni nikusoneeni Aliyokuharimishieni Mola wenu; ya kwamba msimshirikishe na kitu chochote na kuwatendea hisani wazazi (wenu), wala msiwauwe watoto kwa (kuchelea) umaskini; Sisi Tutakupeni riziki na wao pia; wala msiyakaribie manbo maovu, ya dhahiri na ya siri, wala msiiue nafsi Aliyoharamisha Allah ila kwa haki; hayo Anakuusieni kwayo ili mzingatie. Wala msiikaribie mali ya yatima ila kwa njia iliyo bora mpaka abalehe; na kamilisheni vipimo na uzani kwa uadilifu, Hatuikalifishi nafsi ila (kuipa majukumu) kwa kadiri ya uwezo wake, na mnaposema, basi fanyeni uadilifu japo iwe ni dhidi ya jamaa (yako); na itimizeni ahadi ya Allah; hayo Anakuusieni kwayo ili mpate kukumbuka.”(Al-An’am 06:151-152).

Aya hizi hutoa taaswira ya kweli ya fikara na mtindo wa maisha wa Waarabu wa zama za ujinga. Hizi Aya mbili zinazotaja maradhi pamoja na tiba ya watu waliokuwa wakigombana wao kwa wao kwa miaka mingi mno kiasi cha kufikia mia moja na ishirini, zilimwibua As’ad mawazo ya ndani zaidi. Alisilimu mara moja na akamwomba Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kumpeleka mtu huko Yathrib akawe mbalighishaji wa Uislamu.

Tunaona kwamba kama tukienda ndani zaidi ya hizi aya mbili itatosha kuondoa majadiliano na mafunzo (marefu zaidi) kuihusu hali ya Waarabu wa Zama za Ujinga, kwa kuwa aya hizi zatosheleza kuifafanua kadiri ya maradhi ya siku nyingi ya kimaadili yaliyokuwa yakitishia kuwako kwa watu hawa. Hapa chini tunayatoa mambo yaliyomo kwenye Aya hizo pamoja na mukhtasari wa maelezo yake:

Nimetumwa kwenye huu ujumbe wangu wa Kiutume kuuondoa ushirikina na ibada ya masanamu.

Kuwatendea wema wazazi huichukua nafasi ya juu zaidi kwenye Ujumbe wangu.

Kwa mujibu wa sheria takatifu kuwaua watoto kwa kuchelea umaskini ni tendo baya zaidi awezalo kulitenda mtu.

Nimeteuliwa ili kuwazuia watu wasitende matendo maovu na kuwaon- dolea uchafu wa kila aina, uwe wa dhahiri au wa siri.

Sheria yangu inasema kwamba kuua mtu na kumwaga damu bila ya sababu ya haki, vimeharimishwa kabisa.

Kuitwaa mali ya yatima pasi na haki, kumeharimishwa.

Sheria yangu imesimama kwenye msingi wa uadilifu, hivyo basi, kwa mujibu wa sheria hii, kuuza vitu kwa uzani pungufu ni haramu. Simpi mtu jukumu zaidi ya lile awezalo kulibeba.

Ulimi na kauli ya mtu, vitu ambavyo ni kioo chenye kung’aa, chenye kuzieleza fikara zake, havina budi kutumika katika kuunga mkono ukweli na uhakika, na mtu asikiseme cho chote kile ila ukweli japo umsababishie hasara.
Uwe mkweli katika ahadi umwahidizo Allah. Hayo yameamrishwa na Mola wako na ni lazima juu yako kuyafuata.4

Kutokana na mambo yaliyomo kwenye hizi aya mbili na jinsi Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alivyozungumza na As’ad, inaweza kufahamika vizuri mno kwamba, Waarabu walikuwa walishajijengea sifa zote hizi zilizo mbaya na kwa sababu hiyo, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) akamsomea As’ad aya hizi mbili mwanzoni kabisa zikiwa ndio shabaha ya Ujumbe wake.

Kwenye hali hiyo, je, yawezekana kukubaliana na dai la watu wale wasemao kwamba ulikuwako ustaarabu wa hali ya juu zaidi kwenye sehemu zote za Bara Arabu kwa karne nyingi?

Dini Bara-Arabuni

Nabii Ibrahimu alipoitweka bendera ya ibada ya Allah na akainua misingi ya Al-Ka’ba tukufu, akisaidiwa na mwanawe Nabii Isma’il (a.s.) baadhi ya watu walimkusanyikia, na miali ya utukufu wake iliyomulika kama jua iliziangaza nyoyo zao. Hata hivyo, kiasi ambacho hii roho tukufu iliweza kupambana na ibada ya masanamu na kuunda safu imara za wenye kumwambudu Allah hakifahamiki kwa uhakika.

Kwenye nyakati nyingi, na hasa miongoni mwa Waarabu, mara nyingi itikadi ya ibada ya Mungu iliandamana na ushirikina na itikadi ya kwamba masanamu yalikuwa udhihirisho wa Mungu. Kutokana na itikadi zao mbalimbali, Qur’ani Tukufu imeitaja itikadi moja ya aina hiyo, ikisema:

وَلَئِنْ سَأَلْتَهُمْ مَنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ خَلَقَهُنَّ الْعَزِيزُ الْعَلِيمُ {9}

“Na kama ukiwauliza (makafikri wa kiarabu): ‘Ni nani aliyeziumba mbingu na ardhi?
‘bila shaka watasema: ‘Ameziumba Mwenye nguvu, NMwenye kkujua” (Az-Zukhruf 43:9)

أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّهِ {3}

“… Sisi hatuwaabudu hawa (masanamu), ila wapate kutufikisha karibu zaidi na Allah;
(Az-Zumar, 39:3)

Sayyidna Ali, Amirul Muuminin (a.s.) anaielezea hali ya kidini ya Waarabu kwa maneno haya: “Watu wa zama hizo walikuwa na itikadi mbalimbali na uzushi wa aina mbalimbali na walikuwa wamegawanyika kwenye madhehebu nyingi. Kundi moja lilimfananisha Allah na viumbe Wake (na liliamini kwamba Alikuwa na viungo). Wengine walileta mabadiliko kwenye Majina Yake (kwa mfano wenye kuabudu masanamu walijichukulia jina la ‘Lat’ kutokana na Allah na Uzza kutokana na Jina Aziz). Pia lilikuwako kundi lililowaelekea wengine ghairi Yake. Baadae Allah Aliwaongoza kupitia kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na Akawafanya kuwa wajuzi wa elimu ya Allah.”5

Watu wenye elimu miongoni mwa Waarabu waliabudu jua na mwezi. Mwanahistoria mashuhuri wa kiarabu, aliyeitwa Kalbi aliyefariki dunia kwenye mwaka wa 206 Hijiriya, anaandika hivi:

“Kabila lililoitwa Bani Malih liliabudu majini, kabila la Tamim liliabudu Dabaran (moja ya nyota zilizomo kwenye mafungu kumi na mawili ya nyota iitwayo Taurus), kabila la Lakhan liliabudu sayari ya Jupita (Sumbula), kabila la Ta’i liliabudu nyota Shiraa, na kabila la Asad liliabudu sayari Zebaki. Hata hivyo, sehemu iliyotwezwa ya jamii iliyo na wengi wa wakazi wa Bara Arabu, zaidi ya kuabudu masanamu ya familia na makabila yao, vilevile waliyaabudu masanamu 360 na wakayahusisha matukio ya kila siku na moja yao.”

Sababu ya kuasisiwa kwa ibada ya masanamu kwenye eneo la Makkahh baada ya kufariki dunia kwa Mtukufu Nabii Ibrahim (a.s.) itajadiliwa baadae. Hata hivyo, ni ukweli ukubalikao kwamba, kwenye siku za mwan- zoni tendo hili halikukamilika kabisa. Hapo awali Waarabu waliyafikiria masanamu kuwa ni waombezi tu na polepole wakaanza kuyadhania kwamba yanao uwezo. Masanamu yaliyopangwa kwa kuizunguka Ka’bah yaliheshimiwa na makabila yote, lakini masanamu ya makabila yaliabudiwa na kundi maalum tu. Kila kabila liliweka sehemu maalum kwa ajili ya masanamu yake, ili kuuthibitisha usalama wao. Wadhifa wa utunzaji wa funguo za hekalu yalimowekwa masanamu hayo ulishikwa kwa urithi na ulishikwa tangu mtu mmoja hadi mwingine.

Masanamu ya familia yaliabudiwa na watu wa familia ile mchana na usiku. Walipokwenda safarini waliyasugua na miili yao. Walipokuwa safirini waliyaabudu mawe ya jangwani. Walipofika kwenye kituo fulani, walichagua mawe manne. Miongoni mwa mawe hayo, waliliabudu lile lililokuwa zuri zaidi na wakayatumia yale matatu yaliyosalia kuwa mafiga ya jiko la kupikia chakula.

Watu wa Makkahh walikuwa na huba nyingi kwa Al-Ka’ba. Walipokuwa wakisafiri waliokota mawe kutoka karibu nayo na kuyaweka na kuyaabudu kila walipotua. Yawezekana kwamba watu hawa ndio waliokuwa ‘ansaab’ (mawe yaliyowekwa) ambayo yalifasiriwa kuwa ni mawe meroro na yasiyo na umbo wala sura maalum. Kinyume na mawe haya, yalikuwapo yale yaliyoitwa ‘awthaan’, neno lenye maana ya masanamu yenye umbo na yaliyonakshiwa yaliyotengenezwa kutokana na mawe ya kuchonga. Ama kuhusu ‘asnaam’, haya yalikuwa ni masanamu, yaliyotengenezwa kwa dhahabu au fedha ya kusubu au yaliyochongwa kutokana na mti.

Kwa kweli, unyenyekevu wa Waarabu mbele ya masanamu ulishangaza mno. Waliamini kwamba kwa kutoa kafara watapata upendeleo wao. Na baada ya kutoa kafara ya mnyama waliipaka damu ya mnyama yule kichwani na usoni mwa lile sanamu. Vilevile walitaka ushauri wa masanamu kwenye mambo yao makuu na yaliyo muhimu. Ushauri huu ulipatikana kwa vijiti ambavyo kimoja walikiandika “fanya” na kingine wakakiandika

‘Usifanye’. Kisha walinyosha mkono na kuokota kimojawapo na kutenda kama kilivyosema kile kijiti.

Fikara Za Waarabu Kumhusu Mwanadamu Baada Ya Kifo

Waarabu walilifafanua suala hili la kifalsafa na lililo gumu hivi: Baada ya kifo cha mwanaadamu, roho yake huutoka mwili wake kwa umbo la ndege aitwaye ‘Hamah wa Sada’ afananaye na bundi na ndege huyo huomboleza kandoni mwa maiti yule bila ya kukoma. Maombolezo yake huwa yenye kuogofya na kutisha. Yule maiti atakapozikwa, roho yake hutwaa makazi kwenye hali tuliyoitaja, karibu na kaburi lake na hukaa hapo daima.

Wakati mwingine ndege huyu huenda na kukaa juu ya paa la nyumba ya watoto wake na kuwa na mazoea na hali zao.

Kama mtu akifa kifo kisicho cha kawaida (kwa mfano akauawa), ndege yule hulia bila ya kukoma: “Asquni Asquni…” (Yaani nizimeni kiu yangu kwa damu ya muuaji wangu) na hanyamazi hadi alipiziwe kisasi kwa muuaji wake.

Hapa ndipo mahali ambapo hali halisi yaeleweka dhahiri kwa mheshimiwa msomaji na anafahamu ya kwamba historia ya Bara Arabu kabla ya Uislamu na ile ya baada ya kuja Uislamu hazifanani. Inapokuwa kwamba ile ya awali ni hadithi ya mauaji, na mazishi ya mabinti walio hai, utekaji nyara, msiba na shida na kuabudu masanamu, ile ya pili inatueleza kuhusu upole kwa yatima, ukarimu na huruma kwa binadamu na ibada ya Mungu Mmoja.

Kwa kweli kikundi cha Wayahudi na Wakristo vilevile waliishi kwenye jamii hii hii lakini waliidhihirisha chuki yao dhidi ya ibada ya masanamu. Makao makuu ya Wayahudi yalikuwa ni mji wa Yathrib, ambapo Wakristo waliishi Najran. Kwa bahati mbaya jamii hizi mbili pia zilihusika na upotovu kuhusiana na upweke wa Allah.

Fasihi Au Stirioskopu (Kinasa Picha Mbili Kwa Pamoja) Ya Fikra Za Taifa

Njia iliyo bora zaidi ya uchambuzi wa mtazamo na weledi wa taifa ni zile kazi za uandishi na hadithi zilizorithiwa na taifa hilo. Fasihi, ushairi na hadithi za kila jumuiya huwakilisha itikadi yake, huwa kama ndio kipimo cha utamaduni wake, na huidhihirisha namna ya fikira zake. Fasihi ya kila taifa ni kama picha ya rangi ya watu waliojipanga tayari, ambayo hutufanya tupate taswira akilini juu ya maisha ya familia pamoja na nyororo ya matukio ya kawaida na wingi wa machafuko au mandhari ya vita na uteka- ji nyara.

Ushairi wa Waarabu na methali zitumiwazo hivi sasa miongoni mwao zaweza zaidi ya kitu cho chote kingine, kuionyesha tabia halisi ya historia yao. Mwanahistoria mwenye kutaka kuujua mtazamo halisi wa taifa fulani, anapaswa kwa kadiri iwezekanavyo asizipuuze alama za ukumbusho mbalimbali za kisomi za taifa hilo, kama vile ushairi, semi, methali, hadithi n.k. Bahati nzuri, wanachuoni wa kiislamu wameandika na kuweka katika kumbu kumbu kwa kadiri ya uwezo wao, fasihi ya Waarabu ihusianayo na Zama za Ujinga.

Abu Tamaam Habib bin Aws (aliyefariki dunia katika mwaka wa 231 Hijiriya) anayehesabiwa kuwa mmoja wa waandishi wa Kishi’ah, na aliyesifiwa kwa mashairi yanayowasifu viongozi wa kidini wa Kishi’ah, amekusanya idadi kubwa ya mashairi yaliyotungwa katika Zama za Ujinga na ameyapanga katika sehemu kumi ambazo ni Mashairi ya kitenzi – Fasihi ya kimaombolezo – Mashairi yenye hisia yahusianayo na kipindi cha ujana. Tashtiti za watu binafsi na za kabila – Mashairi yaliyolengwa upole na ukarimu – wasifu – sifa za kimaumbile, tabia – ujuaji na ucheshi – na kuwazulia wanawake.

Wanachuoni na waaandishi wa kiislamu wameandika tafsiri ya Kitabu hiki ili kuieleza maana ya maneno na kusudio la mashairi. Kitabu hiki kimetafsiriwa mwenye lugha nyingi za kigeni, baadhi yao zimetajwa mwenye kitabu kiitwacho “Mu’jamul Matbu’aat” (Uk. 297).

Daraja Ya Wanawake Miongoni Mwa Waarabu

Sehemu ya kumi ya kitabu tulichokitaja hapo juu inaonyesha wazi vya kutosha kwamba wanawake waliwekwa chini ya fedheha ya kipekee mion- goni mwa watu hawa na waliishi maisha ya kuhuzunisha sana. Katika Qur’ani Tukufu pia zimeteremshwa aya zinazolaumu kitendo cha Waarabu, na kutoa mwanga juu ya kushusha kwao maadili. Inakitaja kitendo chao kichukizacho cha kuwaua wasichana, na inasema:

وَإِذَا الْمَوْءُودَةُ سُئِلَتْ {8}

بِأَيِّ ذَنْبٍ قُتِلَتْ {9}

“Na mtoto mwanamke aliyezikwa hai atakapoulizwa, ni kwa kosa gani aliuawa?”
(At-Takwir, 81:8-9).

Yaani wasichana waliozikwa wakiwa hai wataulizwa swali hili katika Siku ya Hukumu. Ni dhahiri kabisa huu ni uvunjaji wa hali ya juu wa maadili kwamba mtoto wake mtu aishapo kukua au ndio kwanza kuwasili ulimwenguni, mtu amzike chini ya tani za udogo na asihuzunishwe hata kidogo na kilio na maombolezo yake.

Watu wa kwanza kukitenda kitendo hiki walikuwa ni watu wa kabila la Bani Tamim. Nu’man bin Munzir, mtawala wa Iraq aliwashambulia maadui wake (ikiwa ni pamoja na hawa Bani Tamim) akiliongoza jeshi kubwa na akawashinda. Alizinyakuwa mali zao na akawachukua mateka wasichana wao.

Wawakilishi wa Bani Tamim walimwendea mtawala huyu na kumwomba awarudishie wasichana wao. Hata hivyo, kwa kuwa baadhi yao walikuwa tayari walishafunga uhusiano wa ndoa katika kipindi cha kutekwa kwao, Nu’man aliwapa uchaguzi wa kukata uhusiano na wazazi wao ili wabakie na waume zao au wapate talaka na warudi majumbani kwao. Mmoja wa wawakilishi wa Bani Tamim alikuwa mzee aliyeitwa Qays bin ‘Aasim.

Binti wake alichagua kubakia na mumewe. Tusi hili lilimchoma moyo mzee yule na akaamua kwamba hapo baadae atawamalizia mbali mabinti zake mara tu wazaliwapo. Pole pole kitendo hiki kiliingia kwenye makabila mengine pia. Qays bin ‘Aasm alipoipata heshima ya kufika mbele ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w) mmoja wa Maansar alimuuliza kuhusu mabinti zake. Qays alijibu akisema: “Nimewazika mabinti zangu wote wakiwa hai na sikuhuzunishwa hata kidogo nilipokuwa nikifanya hivyo (ila safari moja tu). Safari moja nilikuwa nikisafiri na wakati wa mke wangu kujifungua ulikaribia.

Kwa bahati safari yangu ilikuwa ndefu. Niliporudi nyumbani nilimwuliza mke wangu kuhusu jambo hilo. Akajibu kwamba kutokana na maradhi alizaa mtoto asiyetimiza siku zake. Hata hivyo, ukweli ni kwamba alizaa mtoto wa kike, na kwa kuniogopa alimweka mtoto huyo chini ya ulinzi wa dada yake. Miaka mingi ilipita na yule msichana akaufikia ujana wake. Sikupata taarifa hata kidogo, juu yake. Hata hivyo, siku moja nilipokuwa nimeketi nyumbani mwangu, aliingia msichana kwa ghafla na akamulizia mama yake. Alikuwa msichana mzuri na alivaa kidani shingoni mwake. Nilimwuuliza mke wangu ni nani msichana yule apendezaye kiasi kile. Mke wangu akiwa anatiririkwa na machozi machoni mwake alinijubu akisema: “Huyu ni binti yako. Ndie yule msichana aliyezaliwa ulipokuwa safarini.

Kwa kukuogopa, nilimficha.” Kimya changu kilichukuliwa na mke wangu kuwa ni dalili ya kuridhika kwangu na akafikiria kwamba sitaipaka mikono yangu damu ya msichana yule. Hivyo basi, siku moja alitoka nyumbani mle na uhakika wa kwamba sitamdhuru. Kisha, kufuatana na ile ahadi na nadhiri yangu nzito, niliushika mkono wa binti yangu na kumpeleka kwenye sehemu ya mbali. Huko nikaanza kuchimba shimo. Nilipokuwa nikijishughulisha na kazi hiyo binti yangu aliniuliza kwa kurudia rudia ni kwa nini nilikuwa niki- ichimba ardhi? Baada ya kwisha kuchimba niliushika mkono wa binti yangu, nikamtumbukiza shimoni, na nikaanza kumtupia udongo kichwani na usoni mwake bila ya kuvisikiliza vilio vyake vyenye kuupasua moyo.

Aliendelea kupiga kite na kusema: “Baba yangu mpenzi! Unanizika ardhini? Je, utarudi kwa mama yangu baada ya kuniacha hapa peke yangu?” Lakini mimi niliendelea kumimina udongo hadi ukamfunika kabisa. Ni kwenye tukio hili tu kwamba nilipatwa na kiasi kidogo mno cha fahamu.”

Masimulizi ya Qays yalipokoma, machozi yalibubujika machoni mwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na akasema: “Hili ni tendo la ugumu wa moyo na taifa lisilo na hisia za huruma na upole halitapata rehema za Allah.” 6

Nafasi Ya Kijamii Ya Wanawake Miongoni Mwa Waarabu

Miongoni mwa Waarabu, mwanamke alikuwa kama bidhaa ya kibiashara iliyoweza kununuliwa na kuuzwa na hakuwa na haki ya kibinafsi wala kijamii hata ile haki ya kurithi. Watu wenye elimu miongoni mwao waliwaweka wanawake chini ya jamii ya wanyama na kwa sababu hii alichukuliwa kuwa kimoja miongoni mwa vyombo vya nyumbani na mahitaji muhimu ya maisha. Kutokana na itikadi hii, methali isemayo: “Akina mama ni wazuri tu kama vile vilivyo vyombo, nao wameumbwa ili wawe vyombo vya kuwekea manii” ilikuwa ikitumika mno miongoni mwao.

Kwa kawaida kuhusiana na hofu ya njaa na fadhaa yenye kuogofya, mara kwa mara waliwakata vichwa mabinti zao katika siku ya mwanzoni mwa kuzaliwa kwao au kuwasukumizia chini kutoka kwenye mlima mrefu na kuwatupia kwenye bonde lenye kina kirefu au wakati mwingine kuwafisha maji.

Qur’ani, Kitabu kikuu cha dini, ambacho chakubaliwa hata na mustashirik wasio Waislamu kwamba kwa uchache ni maandiko ya kihistoria na yenye mafunzo yasiyoharibiwa, kina maandiko ya ajabu juu ya jambo hili. Inasema:

وَإِذَا بُشِّرَ أَحَدُهُمْ بِالْأُنْثَىٰ ظَلَّ وَجْهُهُ مُسْوَدًّا وَهُوَ كَظِيمٌ {58}

يَتَوَارَىٰ مِنَ الْقَوْمِ مِنْ سُوءِ مَا بُشِّرَ بِهِ ۚ أَيُمْسِكُهُ عَلَىٰ هُونٍ أَمْ يَدُسُّهُ فِي التُّرَابِ ۗ أَلَا سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ {59}

“Na mmoja wao anapopewa habari ya (kuzaliwa) binti, uso wake huwa mweusi, naye kajaa chuki. Hujificha kutokana na kaumu (yake) kwa sababu ya habarimbaya aliyoambiwa (anafikiria) je, amweke kwa fedheha au amzike udongoni (akiwa hai)? Tazama! Ni uovu (kiasi gani) wa wanavyohukumu.” (Al-Nahl, 16:58-59).

Jambo lenye kusikitisha zaidi lilikuwa ni utaratibu wa ndoa zao ambao haukusimamia kwenye msingi wowote wa sheria yenye mtindo utumikao ulimwenguni mwa zama zile. Kwa mfano, hawakuamini kuwapo kwa mipaka yoyote ile katika idadi ya wake. Ili kuepuka kulipa mahari, waliwatesa wanawake na kama mwanamke atakoma kuwa msafi wa tabia, aliikosa mahari yake kabisa.

Wakati mwingine walijinufaisha visivyo haki kutokana na sheria hii na wakawasingizia wake zao kiasi cha kuweza kukataa malipo ya mahari. Kitokeapo kifo cha mtu au kumtaliki mkewe, ilihesabiwa kuwa ni halali kwa mwanawe kumwoa mke yule, na hadithi ya Ummayyah bin Shams kuhusiana na jambo hili imehifadhiwa kwenye vitabu vya historia.
Mwanamke anapojipatia talaka kutoka kwa mumewe, haki yake ya ndoa ya pili ilitegemea ruhusa ya mume wa awali na kwa kawaida ruhusa hiyo ilitolewa kwa yeye kuiachilia mahari yake. Kinapotokea kifo cha mtu, warithi wake waliwatwaa wanawake kama vilivyo kwa vyombo vyote vya nyumbani mle, na kujitangaza kuwa ndio wamiliki kwa kuwatupia nguo ya kichwa juu ya kichwa chake.

Ulinganisho Mfupi

Kama mtukufu msomaji akiziangalia haki za mwanamke kwenye Uislamu na akapuuza ugomvi na migogoro ambayo hujitokeza ghafla kwenye nyakati fulani, bila shaka atatambua ya kwamba sheria na kanuni na hatua zenye kufaa za kuzitengeneza haki za mwanamke na kuzifanya kuwa za kawaida zilizochukuliwa kupitia kwa Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w), zenyewe ni ushahidi wa dhahiri kabisa wa ukweli wake na mawasiliano yake na ulimwengu wa ufunuo.

Kwani ni huruma gani na kuwatendea mema wanawake kuwezako kuwa bora zaidi ya hapo (ukiyaachilia mbali matangazo ya haki za wanawake kwenye aya mbalim- bali za Qur’ani Tukufu na kwenye Hadithi na pia kutoa mifano ya kivitendo kuhusiana na jambo hili kwa ajili ya wafuasi wake kuweza kufanya hivyo). Kwenye hotuba ya Hija yake ya mwago aliyoifanya, ambapo kwa kuamrishwa na Allah aliurudia rudia ujumbe huo kwa ufupi, akamteua mrithi wake na kwenye wakati huohuo, vilevile aliwakabidhi wanawake kwa wanaume kwa maneno yafuatayo:

“Enyi watu! Mnayo haki juu ya wanawake wenu nao pia wanayo haki juu yenu. Waamrisheni kutenda mema kwa kuwa wanakusaidieni na kukunusuruni. Walisheni vile mvilavyo ninyi wenyewe na wavisheni vile mvivaavyo wenyewe.”

Waarabu Kama Wapiganaji

Hakuna shaka yoyote kuhusu habari kwamba Waarabu walikuwa na moyo wa kupenda vita usiokuwa na kifani na waliyazidi mataifa mengi kwenye sanaa ya vita. Bila shaka moyo huu ulikuwa wa kusifika na kustahili kuthaminiwa mno kiasi kwamba hata Uislamu uliutumia mno mwelekeo wao huu baada ya kuurekebisha. Na ni jambo la heshima kuu kwa Uislamu kwamba baada ya kufanya marekebisho yafaayo kwenye mielekeo ya mataifa mbalimbali, iliitumia katika kuyafikia malengo na shabaha tukufu. Hata hivyo, kabla ya Uislamu, moyo huu wa Waarabu ulikuwa daima ukitekelezwa kivitendo kuyaharibu matengemeo ya maisha ya makabila mbalimbali na haukutoa matokeo yoyote yale ila umwagaji wa damu, mauaji na utekaji nyara.

Waarabu walizidisha mno tabia ya umwagaji wa damu, na utekaji nyara kiasi kwamba wakati wa kujisifu mtu, waliuhesabu utekaji nyara kuwa moja ya heshima zao. Ukweli huu ni wa dhahiri kabisa kutokana na ushairi na maandiko yao.

Mmoja wa washairi wa Zama za Ujinga, alipokuwa akiiangalia hali duni na nyonge ya kabila lake kuhusiana na mauaji na utekaji nyara, alihuzuni- ka mno na akaielezea tamaa yake kwa maneno haya: “O (ningalifurahi mno) kwamba badala ya kuwa wa kabila hili nyonge na lisilo na faida yoyote ningalikuwa mtu wa kabila, ambalo watu wake wamewapanda wanyama au watembeao kwa miguu, daima walijifurahisha kwa utekaji nyara na unyang’anyi, na kuyaishilizia maisha ya watu.”

Hitimisho

Sasa tuishajipatia dokezo la ujumla juu ya ustaarabu wa Waarabu wa Zama za Ujinga. Pia, sasa ishatudhihirikia kwamba hakuna mtu mwadilifu wala mwenye elimu awezaye kuyakubali maoni ya kwamba hali ya kijamii ya Hijaz, iliyojaa machafuko, ukatili na utwezaji wa utu na wema, ingezaa chama kikuu na cha ulimwengu mzima (Uislamu) ambacho kingeliweza kuzitumia nguvu za kiakili zilizo dhahiri kwenye ulimwengu wote wa zama zile na kuirudisha amani na taratibu njema kwenye eneo lile lililosumbuliwa kwa njia ya mpango ulio bora zaidi.

Na vilevile imedhihirika kwamba dai lililotolewa na baadhi ya watu wasioona mbali kwamba Uislamu ni matokeo ya kawaida ya jamii ile, ni lenye kushangaza mno. Bila shaka maoni kama haya yangelikuwa ya haki kama chama hiki kikuu kingelijitokeza kwenye maeneo yaliyostaarabika, lakini itakuwa ni fikara itokanayo na mapenzi ya mtu tu kutoa dai la aina hii kuhusiana na Hijaz.

Sasa, kwa lengo la kuyamalizia mazungumzo yetu juu ya maudhui hii, tunatoa hapa chini taarifa za itikadi na fikara za Waarabu wa Zama za Ujinga kuhusiana na mambo mbalimbali.

Ushirikina Na Ngano Za Waarabu

Qur’ani Tukufu imetaja malengo ya Ujumbe wa Mtukufu Mtume wa Uislamu kwenye sentensi fupifupi. Moja ya sentensi hizi ipasikayo kuchunguzwa vizuri ni hii isemayo:

وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالْأَغْلَالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ ۚ {157}

“…Na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao…” (Al-A’araf, 7:157).

Yaani Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) aliwaondolea matendo magumu na akawaondolea minyororo iliyoifunga mikono na miguu yao. Sasa haina budi kufahamika wazi maana ya minyororo iliyokuwa ikiifunga mikono na miguu ya Waarabu wa Zama za Ujinga wakati wa kuanza kwa Uislamu. Bila shaka hii haina maana ya minyororo na pingu za chuma bali ilikuwa na maana ya itikadi na ushirikina usiokuwa na msingi uliozifunga akili zao kutokana na fikira na maendeleo.

Na ukweli ni kwamba, minyororo na ugwe ulioifunga akili ya mwanaadamu ni vyenye hatari na madhara zaidi kuliko hiyo minyororo ya chuma, kwa kuwa baada ya kupita muda fulani, hiyo minyororo ya chuma huondolewa na mfungwa huibuka tena kwenye maisha na akili yenye afya timam, akiwa huru kutokana na fikara zote za kiufujaji, lakini minyororo ya ushirikina na uduni unaoifunga akili na utumiaji wa akili ya mwanaadamu kama uzi uliojisokota, humweka mwanaadamu kwenye hali ya kufungwa hadi kwenye kifo chake na humzuia kufanya juhudi zozote zile – hata ile juhudi ya kuviondoa vifungo na pingu hizi.

Na kuwa mtu mwenye akili timam anaweza kubuni mbinu ya kuivunjilia mbali minyororo au fito za chuma kwa msaada wa akili na matumizi ya akili hizo, matendo na juhudi za mtu asiye na akili timam na dhana huishilizia patupu na hubakia kuwa ya bure.

Moja ya heshima na sifa kuu za Mtukufu Mtume (s.a.w.w) ni kwamba alipigana dhidi ya ushirikina, itikadi potovu na ngano, na alisafisha bongo za wanadamu na sababu ya imani za kuchukiza za ushirikina.

Alikuwa kila mara akisema: “Nimekuja kuikamilisha nguvu ya akili za mwanaadamu na kuiinua juu, kupiga vita imara dhidi ya aina zote za ushirikina japo ziwe zenye msaada kwa maendeloa ya Ujumbe wangu.”

Wanasiasa wa ulimwenguni wasio na nia wala lengo lolote jingine zaidi ya kuwatawala watu daima hutumia kila tukio kwa faida zao wenyewe kiasi kwamba, kama ngano za kale au itikadi ya ushirikina ya taifa fulani ni zenye faida kwa nchi na serikali zao, hawasiti kuzibalighisha. Na kama ni watu wenye fikara nyingi na hoja, basi huzipa msaada ngano na ushirikina usio na hoja chini ya dhana ya kuziridhia fikara za walio wengi na heshi- ma kwa itikadi ya walio wengi.

Hata hivyo, Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) hakuzikomesha itikadi za kishirikina zilizokuwa na madhara kwake na kwa jamii tu, bali hata ngano ya eneo fulani au wazo lisilo na msingi lililokuwa lenye kutoa msaada kwa ajili ya maendeleo ya ujumbe wake alilifanyia kampeni dhidi yake kwa nguvu zake zote na akajitahidi kwamba watu waufuate ukweli na wala si ngano na ushirikina.

Kijana Ibrahim, mtoto wa kiume wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alifariki dunia. Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alishikwa na masikitiko na akahuzunika kwa sababu ya kifo chake. Na akatiririkwa na machozi kutoka machoni mwake bila kujizuia.

Jua lilipatwa kwenye siku ya kifo cha mtoto huyu. Waarabu wapenda ngano na ushirikina walikuchukulia kupatwa huko kwa jua kuwa ni dalili ya ukuu wa huzuni za Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na wakasema: “Jua limepatwa kwa sababu ya kifo cha mwana wa Mtume.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alipata kuyasikia maneno haya. Aliipanda mimbari na akasema: “Jua na mwezi ni ishara kuu mbili za uwezo wa Allah, navyo huzitii amri Zake. Havishikwi kwa sababu ya kifo au uhai wa mtu yeyote. Kila kutokeapo kupatwa kwa jua au mwezi salini sala ya Ishara.” Baada ya kuyasema hayo alishuka mimbarini na akasali Swala ya Ishara pamoja na wengine.7

Ingawa wazo la kwamba kupatwa kwa jua kulitokea kutokana na kifo cha mwana wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) lingaliweza kuiimarisha itikadi ya watu juu yake, na hivyo ingaliweza kumsaidia katika maendeleoa ya ujumbe wake, katu hakupenda kwamba cheo chake kiimarike nyoyoni mwa watu kwa njia ya ushirikina. Kampeni yake dhidi ya hekaya na ushirikina, ambayo mfano wake ujidhihirishao mno ni vita aliyoipanga dhidi ya ibada ya masanamu na aina zote za dini za uongo, halikuwa jambo lenye kifani kwenye kipindi cha ujumbe wake wa kiutume. Amepigana dhidi ya ushirikina kwenye maisha yake yote hata kwenye siku za utotoni mwake.

Siku moja wakati umri wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) haukuwa zaidi ya miaka minne na alipokuwa akiishi na mlezi wake, Bibi Halima (r.a) aliidhihirisha tamaa ya kufuatana na kaka yake wa kunyonya kwenda naye porini.

Bibi Halima (r.a) anasema: “Siku iliyofuatia nilimwogesha Muhammad, nikazipaka mafuta nywele zake na nikayapaka wanja macho yake. Na vile vile nilimvika ushanga wa Yemen, uliotungwa kwenye kamba shingoni mwake kwa ajili ya usalama wake, ili asidhurike na pepo wabaya. Muhammad aliuvua ushanga ule kutoka shingoni mwake na akaniambia: “Mama yangu mpenzi! Moyo wako na utulie. Mungu wangu aliye nami daima yu Mlinzi na Mhifadhi wangu.” 8

Itikadi Za Kishirikina Za Waarabu Wa Zama Za Ujinga

Wakati wa kuanza kwa Uislamu itikadi za mataifa na jamii zote za wanaadamu wa ulimwenguni kote walikuwa wamefungwa na aina mbalimbali za ushirikina na visaasili na mithiolojia za Kigiriki na Kisasaniaa zilizotawala akili za mataifa yaliyochukuliwa kuwa ndio mataifa yaliyoendelea kwenye siku hizo. Na hata kwenye zama zetu hizi ushirikina mwingi umeenea miongoni mwa mataifa yaliyoendelea ya nchi za mashariki na ustaarabu wa kisasa bado haujafaulu kuufuta kutoka akilini mwao. Hata hivyo, kukua kwa visaasili na ushirikina kuko sambamba na kiwango cha elimu na mafunzo kwenye jamii. Jinsi jamii iwavyo nyuma kwenye mambo ya elimu na mafunzo, ndivyo idadi ya ushirikina itakavyokuwa kubwa humo.

Historia imesajili idadi kubwa ya visasili na ushirikina uhusianao na Waarabu, na Sayyid Mahmud Aalusi, mwandishi wa kitabu kiitwacho Bulughul adab fi ma’rifa ahwaalil Arab9 amekusanya mwingi miongoni mwao kwenye kitabu hicho pamoja na nyororo ya wasimulizi waliozirejea taarifa hizo kwenye maandishi yao. Ukikipitia kitabu hiki na vinginevyo mtu utaweza kuuona ushirikina chungu nzima. Haya mafundisho yasiyo na msingi ya itikadi zisizoeleweka kiakili yalikuwa moja ya sababu zilizolifanya taifa hili kukawia nyuma ya mataifa mengine. Ni jambo la kawaida kwamba, taifa ambalo idadi ya wasomi wake katikati ya mkoa wa Hijaz haikuzidi watu kumi na saba10 liwe ni lenye kukamatwa na ushirikina na visasili.

Visasili hivi vilikuwa kizuizi kikuu kwenye njia ya maendeleo ya Uislamu, na kwa sababu hii, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alijitahidi kwa kadiri alivyoweza kuzifutilia mbali hizi dalili za ‘Ujinga’ zilizokuwa na huu ushirikina na visasili. Alipokuwa akimpeleka Bwana Ma’az bin Jabal huko Yemen, alimpa maelekezo yafuatayo: “Ewe Ma’az! Ondoa kutoka miongoni mwa watu dalili za ujinga na fikara na itikadi za kishirikina na zihuishe hadith za Uislamu ambazo hutulingania kutafakari na kuitumia akili.” 11

Kwa vile ilikuwa kinyume na jamii kubwa ya Waarabu waliotawaliwa kwa miaka mingi na itikadi za kishirikina, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alikuwa akisema: “Dalili zote za ujinga ziko chini ya miguu yangu.” - yaani kwa kuja Uislamu, desturi, itikadi na njia za kupatia vyeo vimeharibiwa kabisa na vimekanyagwakanyagwa chini ya miguu yangu.

Sasa, ili kufafanua uzuri wa mafundisho ya Uislamu, tunatoa hapa chini mukhtasari wa maelezo ya itikadi za Waarabu wa Zama za Ujinga.

1. Kuwasha Moto Kwa Ajili Ya Kuja Kwa Mvua

Maeneo mengi ya Peninsula ya Uarabuni yanakabiliwa na ukame. Ili kuhakikisha upatikanaji wa mvua, watu wa maeneo hayo walikuwa na kawaida ya kujipatia matawi ya miti iitwayo Sala na ‘Ushr ambayo hushika moto upesi. Huyafunga matawi hayo kwenye mkia wa ng’ombe jike na kumpeleka ng’ombe huyo juu ya mlima. Baadae huyachoma matawi hayo.

Kutokana na kuwako kwa vitu vinavyoshika moto kwenye yale matawi ya ‘Ushr miali ilitokea mwenye moto ule na kuuchoma mwili wa yule ng’ombe jike. Kutokana na maumivu yatokanayo na kuungua, ng’ombe yule alianza kukimbia na kulia.

Watu hawa walilitenda jambo hili chafu na kulichukulia kuwa ni ishara ya kufanana na ngurumo na radi ya mbinguni. Waliichukulia ile miali ya moto kuwa inawakilisha radi na mlio wa ng’ombe kuwa unawakilisha ngurumo na kukifikiria kitendo hiki kuwa kinaleta mvua.

2. Kama Ng’ombe Jike Hakunywa Maji Walimpiga Ng’omba Dume

Waarabu waliwapeleka majike na madume ya ng’ombe kwenye kingo za vijito ili wakanywe maji. Wakati mwingine hutokea kwamba madume hunywa maji lakini majike yakaacha kunywa maji. Kutokana na jambo hilo walifikiria ya kwamba, hilo lilitokana na pepo wabaya waliokaa baina ya pembe za madume na ambao hawakuwaruhusu majike yao kunywa maji. Hivyo basi, ili kuwafukuza pepo wabaya hao, walizipiga nyuso za yale madume.

3. Waliwapiga Chapa Ya Moto Ngamia Wenye Afya Njema Ili Wengine Wapone.

Kama kukitokea maradhi miongoni mwa ngamia au kidonda au yakaonekana malengelenge midomoni na makooni mwao, alitafutwa ngamia mwenye afya timam na midomo yake, sehemu ya juu ya mguu wake na nyonga yake vilipigwa chapa ya moto ili kuyazuia maradhi hayo yasienee miongoni mwa wanyama wengine. Hata hivyo sababu ya kufanya hivyo haijulikani. Inaweza ikachuliwa kwamba kitendo hiki kinaweza kikawa na hali ya kuzuia maradhi na kilikuwa aina fulani ya tiba ya kisayansi, lakini tunapouangalia ukweil uliopo kwamba kutokana na ngamia wengi waliokuwapo, ni ngamia mmoja tu aliyechaguliwa katika mateso ya namna hiyo, tunaweza kusema kwamba jambo hili nalo lilikuwa kitendo cha ushirikina na kilisimamia kwenye msingi wa uongo.

4. Ngamia Aliwekwa Pembeni Mwa Kaburi

Mtu mwenye cheo kikuu alipofariki dunia, ngamia aliwekwa kwenye shimo karibu na kaburi lake na alikuwa hapewi maji wala malisho ili kwamba afe, na huyo mtu aliyekufa apate mnyama wa kumpanda katika Siku ya Kiyama na asifufuke akiwa yu atembea kwa miguu.

5. Waliikata Miguu Ya Ngamia Karibu Na Kaburi

Kwa kuzingatia ukweli kwamba mtu alipokuwa hai alikuwa na kawaida ya kuchinja ngamia ili kuwafurahisha ndugu na wageni wake, na kama kuonyesha heshima na malipo kwa marehemu huyo, warithi wake huikata miguu ya ngamia karibu na kaburi lake katika namna ya kumsababishia maumivu makali mnyama huyo.

Uislamu Wapambana Na Ushirikina

Vitendo hivi (tukiachilia mbali ukweli uliopo kwamba hakuna chochote miongoni mwao kinachoafikiana na akili na sababu za kisayansi, kwa sababu mvua hainyeshi kwa kuwasha moto, kumpiga ng’ombe dume hakuna athari zo zote kwa ng’ombe jike, kumpiga chapa ngamia mwenye afya hakuwaponyi ngamia wagonjwa n.k.), ni aina fulani ya ukatili kwa wanyama. Kama tukilinganisha vitendo na itikadi hizi, na sheria thabiti zilizoamrishwa na Uislamu kwa ajili ya hifadhi ya wanyama, bila shaka tutasema kwamba sheria ya dini hii imetangaza vita ya dhahiri dhidi ya fikara za jamii ile.

Ziko kanuni nyingi za kiislamu zenye kuuhusu ulinzi wa wanyama na tunaweza kutaja kuhusiana na jambo hili kwamba, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) amesema: “Mnyama wa kupanda ana haki sita juu ya bwana wake”:
Anapokuwa safarini na akatua (ili kupumzika) ampe malisho mnyama huyo;
Anapopita mahali penye maji amruhusu mnyama yule kunywa maji yale; Asimpige mnyama yule usoni;
Anapokuwa na mazungumzo marefu na mtu, asiendelee kukaa mgongoni mwa mnyama yule;
Asimbembeshe mzigo mzito zaidi ya uwezo wake.
Asimlazimishe mnyama yule kusafiri umbali ulio zaidi ya uwezo wake.12

6. Tiba Ya Wagonjwa:

Kama mtu aliumwa na nyoka au na nge, alivikwa shingoni mapambo ya dhahabu. Waliamini ya kwamba mtu wa aina hiyo akibeba shaba au bati mwilini mwake, angeweza kufa. Kuhusu kichaa cha mbwa (yaani maradhi yasababishwayo na kuumwa na mbwa) waliyatibu kwa kupaka kiasi kidogo cha damu ya chifu wa kabila kwenye kile kidonda.
Na kama mtu akitokewa na dalili za wendawazimu, alikwenda kukaa kwenye matambaa machafu na alivikwa shingoni mifupa ya wafu ili kumfukuza pepo mchafu.

Ili kuthibitisha kwamba mtoto wao hajeruhiwi na pepo wachafu, walifunga jino la mbweha na paka kwenye kamba kisha wakamvika shingoni. Mtoto anapoota majipu au chunusi mwilini mwake, mama yake alimtwisha chungio kichwani mwake na wakaiendea kila nyumba ya mtu wa kabila lao wakikusanya mikate na tende, vitu ambavyo baadae humpa mbwa, ili kwamba majipu na chunusi za mtoto yule ziweze kupona. Wanawake wengine wa kabila lile walijihadhari kwamba watoto wao wasizile tende na mikate ile ili wasije nao wakapatwa na maradhi yale.

Kama mtu alipatwa na ugonjwa wa ngozi (kwa mfano ugonjwa wenye athari za mikwaruzo mwilini) alikuwa akijitibu kwa kukipaka chungu mate yake.

Kama maradhi ya mtu yalichukua muda mrefu kupona, walidhania kwamba mgonjwa yule alimuuwa nyoka au mnyama yeyote mwingine aliyekuwa na uhusiano na pepo wabaya. Hivyo basi, ili kuwaomba radhi hao pepo wabaya walifinyanga masanamu ya ngamia ya udongo na kisha wakayasheheni shayiri, ngano na tende.

Walivipeleka na kuviacha vitu hivi mkabala na tundu kwenye mlima na kisha wakarudi tena kupatembelea hapo siku iliyofuatia.

Kama wakikuta kwamba vitu vile vimeliwa, walilichukulia jambo hilo kuwa ni dalili ya kukubaliwa kwa zawadi zile na hao pepo wabaya na waliamua kwamba yule mgonjwa atapona. Hata hivyo, kama mambo yakienda kinyume na hivyo, walifikiria kwamba zawadi zile, kwa vile zilikuwa ndogo, wale pepo wabaya hawakuzipokea.

Jinsi Uislamu Ulivyofanya Kampeni Dhidi Ya Ushirikina Huu

Uislamu ulifanya kampeni dhidi ya ushirikina huu kwa njia kadhaa. Walikuwako mabedui wa kiarabu waliokuwa wakiwaagua wagonjwa wao kwa viambatisho vya kichawi na mikanda iliyosheheni mawe na mifupa. Walipotokea mbele ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na wakamwuliza kuhusu namna ya kutibu wagonjwa kwa miti shamba na madawa, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema:

“Ni lazima kwa kila mgonjwa kuitafuta dawa, kwa kuwa Allah Aliyeumba ugonjwa pia Ameumba dawa yake.13 Na Sa’ad bin Abi Waqqas alipopatwa na maradhi ya moyo, Mtukufu Mtukume (s.a.w.w.) alimwambia: “Nenda ukamwone Harith Kaldah, mganga maarufu wa Thaqif.” Baadae Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe alimshauri Sa’ad atumie dawa maalum.14

Vilevile kuna simulizi nyingine zinazotangaza viambatanisho vya kiuchawi ili kuondokana na athari zozote ziwazo. Hapa tunanukuu mbili katika hizo:

“Mtu mmoja ambaye mwanawe alikuwa akiugua kutokana na maumivu ya koo alikwenda kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akiwa na viambatanisho vya kiuchawi. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimwambia: “Usiwaogofye watoto wako kwa viambatanisho hivi vya kiuchawi. Huna budi kuyatibu maradhi haya kwa mafuta ya mti wa Aloe (aloe-wood-oil).15

Imam wetu wa sita, As-Sadiq (a.s.) amesema: “Nyingi ya hirizi na viambatanisho vya kichawi huwa sawa na ushirikina.16

Kwa kuwaongozea watu kwenye matumizi ya dawa nyingi (ambazo maelezo yake maalum yote, yamekusanywa na wanavyouni wa kiislamu wakuu wa hadith chini ya kichwa cha habari cha “Tibur Rasul” (Tiba za Rasuli), “Tibur Ridha.” (Tiba za Ar-Ridha), n.k. Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na Warithi wake watakatifu kwa mara nyingine tena walishambulia kwa nguvu ushirikina huu, na kusema kweli, waliwakasirisha Waarabu wa Zama za Ujinga.

Ushirikina Mwingine

Walizitumia njia zifuatazo katika kujikinga na fadhaa na woga: Kila walipofika kwenye kijiji, waliogopa baadhi ya magonjwa ya kuam- bukiza au pepo wabaya. Ili kuiepuka hofu hiyo, walilia kama punda mara kumi kwenye lango la kijiji hicho. Wakati mwingine pia walining’iniza mifupa ya mbweha shingoni mwao. Kama wakipotea njia wakati wa kusafiri jangwani, waliyavaa mashati yao baada ya kugeuza ndaninje. Wakati walipokuwa wakisafiri walihofia vitendo vya kifasiki kwa upande wa wanawake wao.

Kupata uhakika kuhusiana na jambo hili walifunga uzi kwenye vikonyo au matawi ya mti. Kama uzi ule ukibakia kufungika vizuri wakati wa kurejea kwao, waliridhika kwamba wanawake wao hawakutenda makosa ya uasherati. Hata hivyo, kama wakiukuta ule uzi ukiwa umefunguka au haupo, waliwakashifu wanawake wao. Kama meno ya watoto wao yaking’oka waliyakamata kwa vidole viwili na kisha wakayarushia kuelekea kwenye jua wakisema: “Ewe jua! Wape meno yaliyo mazuri kuliko haya.”

Kama watoto wa mwanamke fulani hawakuishi (yaani walikufa kwenye kipindi cha utotoni), waliamini kwamba watoto wake wataishi kama akitembea mara saba juu ya maiti ya mtu mashuhuri aliyeuawa.

Haya ni maelezo mafupi ya ushirikina mwingi mno ulioyatia kiza maisha ya Waarabu wa Zama na Ujinga na umezizuia akili zao kutokana na kuendelea zaidi.

 • 1. “Tamaddun-i- Islamic wa Arab”, uk. 78 -102
 • 2. Murujudh Dhahab, Juzuu ya 3, uk. 373.
 • 3. Kitabu hiki kinatolewa kwa Kiingereza na “Islamic Seminary” kwa kichwa cha habari cha “Peak of Eloquence.”
 • 4. Rejea: A’lamul Wara, Uk. 35 – 40, na Bihaarul Anwaar, Juzuu ya 19, Uk. 8 –11.
 • 5. Nahjul Balaghah, Hotuba ya 1.
 • 6. Mwenye kitabu ‘Usudul-Ghaba’, Ibn Athir anamnukuu Qays akisema kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimuuliza ni mabinti wangapi aliowazika wakiwa hai na akajibu ya kwamba idadi yao ilikuwa ni kumi na wawili.
 • 7. Bihaarul Anwaar, Juzuu ya 22, uk. 155.
 • 8. Bihaarul Anwaar, Juzuu 6, uk. 92.
 • 9. Biharul Anwaar, Juzuu ya 2, uk. 286 – 369.
 • 10. Tazama ‘Futuhul Buldaan,’ Balazari, uk. 458.
 • 11. ‘Tuhaful‘Uqul’, uk. 29
 • 12. Man la Yahzaruhul Faqih, uk. 228
 • 13. At-Taaj. Juzuu 3, uk. 178. Mtukufu Mtume (saw) alikuwa na maana ya kusema kwamba hivyo viambatisho wa kichawi “appendages” havikuwa tiba itoshelezayo
 • 14. At-Taaj, Juzuu ya 3 uk. 179
 • 15. At-Taaj, Juzuu ya 3, uk. 184.
 • 16. Safinatul Bihar, neno la asili ni “raqa.”