read

Sura Ya Kumi: Kuanzia Ndoa Hadi Utume

Kipindi cha maisha ya mwanadamu kilicho nyeti zaidi huanza pale anapopata makamu kiasi. Huwa hivyo kwa sababu hisia za kijinsia huufiikia ukamilifu wake, kila wakati tamaa za mwili huishawishi juhudi ya moyo kichwani mwake mtu, dhoruba ya ashki huitia giza hali ya hewa ya akili za mwanadamu, msingi wa kanuni za hisia za kimwili huwa thabiti zaidi na matokeo ya yote haya ni kwamba ile taa ya hekima hufifia. Katika kipindi cha mchana na usiku na mara kwa mara, kasiri kubwa la tamaa hujitwalia umbo thabiti machoni pa watu wazima.

Kama ikitokea kwa mtu fulani kuwa na utajiri pia katika kipindi kile, maisha huwa kitu cha hatari mno kwake. Wakati hisia za kinyama na afya njema na bahati za kimaada na utajiri mwingi mno wa mtu vinapoungana, matokeo yake ni kwamba huujaza mpangilio wa maisha yake wingi wa matendo ya kiashki na amejawa na tamaa nyingi za kiashki bila ya kujali maisha ya baadae.

Kipindi hiki huitwa mpaka baina ya ustawi na upotovu, na mtu hufaulu kwa shida sana katika kujiamulia njia nyingine kwa ajili yake na katika kuchagua, kwa matumaini ya kujipatia tabia njema na fikara halisi, njia iwezayo kumsalimisha mtu kutokana na hatari zote.

Katika hali kama hiyo, huwa ni kazi ngumu mno kwa mtu kujihadharisha, na endapo mtu huyu hakulelewa na kuelimishwa vizuri katika mazingira ya kifamilia, basi mtu huyo hana budi kusubiri maanguko ya muundo wa maisha yake.

Utu Uzima Wa Mtukufu Mtume (S.A.W.W)

Hakuna shaka yoyote ile kuhusu ukweli uliopo kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikuwa shujaa, mwenye nguvu na afya njema, kwa sababu alilelewa kati- ka mazingira yasiyo na waa lolote, na wanafamilia wote wa ile familia alimozaliwa walikuwa na asili ya uhodari na ushujaa. Utajiri mkubwa wa Bibi Khadija alikuwa akiumiliki yeye vile vile na uwezo wote wa maisha mazuri ulikuwa mikononi mwake. Hata hivyo, lazima ifahamike ni kwa vipi alitumia mali hii ya kiulimwengu. Je, alijichagulia maisha ya anasa na je, alielekea kwenye kujitoshelezea matamanio yake, kama wafanyavyo vijana wengine? Au kwamba, ingawa alikuwa na njia na uwezo wote wa mali, alichagua mpangilio mwingine wa maisha yake ambao uliudhihirisha kikamilifu msingi wa maisha yake hisia halisi? Historia inashuhudia ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliyaongoza maisha yake kama watu mwenye busara na uzoefu walivyoishi. Daima alikuwa akiambaa ufisadi wa mali na uzembe na dalili za busara na tafakuri zilikuwa siku zote dhahiri usoni kwake. Ili kukaa mbali na ufisadi wa jamii aliutumia muda wake mwingi katika pango lililoko chini ya milima na kujifunza alama za uwezo wa Allah na kutafakari juu ya kuumbwa kwa ulimwengu.

Hisia Za Utu Uzima Wake

Tukio moja lililotokea katika soko la Makkahh lilizijeruhi hisia za kiutu za Mtume (s.a.w.w.). Alimwona mtu akicheza kamari; kwa bahati mbaya mtu yule alimpoteza ngamia wake pamoja na nyumba yake kwa mchezo ule. Na si hayo tu, bali pia alijihatarisha na kuipoteza miaka kumi ya maishani mwake. Mtume (s.a.w.w.) alihuzunishwa mno na tukio hili kiasi kwamba hakukaa mjini Makkah siku ile. Hivyo basi, aliviendea vilima vya karibuni na hapo na kurudi mjini baada ya kupita sehemu ya usiku. Alihuzunishwa sana na kukiona kioja hiki cha kusikitisha na akafikiria sana na akashangazwa na utovu wa busara na hekima za watu hawa waliopotoka.
Kabla Bibi Khadija hajaolewa na Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.) nyumba yake ilikuwa kitovu cha matimaini ya maskini. Na hata baada ya kuolewa kwake na Mtume (s.a.w.w.) hakuruhusu litokee japo badiliko lililo dogo mno katika hali ya nyumba yake au katika ukarimu wa utu wema wa mumewe.

Katika kipindi cha njaa na ukame, mama mlezi wa Mtume (s.a.w.w.), Bibi Halima alikuwa nyakati nyingine akija kumsalimia mwanawe. Hapo, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na kawaida ya kutanda joho lake miguuni pa mama huyu akizikumbuka huruma zake na maisha ya kawaida aliyokuwa akiishi na Bibi huyu na kusikiliza yale aliyokuwa akisema. Wakati wa kuondoka kwake alimsaidia kwa kadiri ya uwezo wake.1

Watoto Wake Watokanao Na Bibi Khadija

Kuzaliwa kwa mtoto huimarisha zaidi fungamano la ndoa na huyafanya maisha kuwa angavu na yenye kung’aa. Mkewe Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimzalia watoto sita. Wawili miongoni mwao walikuwa ni wanaume–mkubwa wao akiwa ni Qasim na mdogo ni Abdillah. Vile vile alizaa mabinti wanne, mwanahistoria ibn Hisham anaandika hivi:

“Binti wao mkubwa alikuwa ni Ruqayyah na wale watatu wengineo walikuwa ni Zainab, Ummi Kuluthum na Fatimah.”2 Wale watoto wa kiume walifari- ki dunia kabla ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kuanza kazi ya utume, lakini wale mabinti waliendelea kuishi.”3

Kujizuia kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika matukio ya misiba kulikuwa kukijulikana sana. Hata hivyo, wakati wa vifo vya watoto wake wakati mwingine hisia za huzuni za moyoni mwake zilijidhihirisha machoni pake kwa njia ya kutiririkwa na machozi kwenye mashavu yake na jambo hili lilidhihirika mno wakati wa kifo cha Ibrahim ambaye mamake alikuwa ni Maria.

Wakati ule, moyo wake ulipokumbwa na huzuni, Mtume alikuwa akijishughulisha na kumhimidi Allah kwa ulimi wake. Alifanya hivyo sana kiasi kwamba mwarabu mmoja, kutokanana ujinga wake na utovu wa elimu juu ya misingi ya kanuni za Uislam, alipinga kulia kwa Mtume (s.a.w.w.). hata hivyo Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Kulia kwa aina hii ni neema.”4

Dhana Isiyo Na Msingi

Dakta Haikal ameandika hivi: “Hakuna ukanusho juu ya ukweli uliopo kwamba wakati wa kifo cha kila mmoja wa watoto wake Khadija aliiendea miungu (ya masanamu) na kuiuliza ni kwa nini miungu hiyo hikufurahishwa na kumbariki.”

Kauli tuliyoinukuu hapo juu haiungwi mkono japo na ushahidi wa kihistoria ulio mdogo mno na si chochote ila ni dhana tupu.

Lengo lake ni kutoa dhana ya kwamba, kwa vile katika zama za Bibi huyu watu wote walikuwa wakiyaabudu masanamu, bila shaka Bibi Khadija naye alikuwa kama wao.

Hata hivyo, itikadi ya Kishi’ah ni kinyume na kauli hii na, kwa hivyo hali halisi nayo ni lazima iwe kama ile iaminiwayo na Mashi’ah. Sababu yake ni kwamba, bila shaka Mtume (s.a.w.w.) aliichukia ibada ya masanamu tangu utotoni mwake na hali hii aliidhihirisha wazi wazi katika msafara wake wa kwenda Sham. Kwa kuwa, alipopata kutofautiana na mfanyibiashara mmoja, kuhusiana na hesabu, na lile kundi la pili likaapa kwa ‘Laat’ na ‘Uzza’. Mtume (s.a.w.w) alisema: “Hivyo ndivyo vitu vibaya zaidi machoni mwangu!”

Katika hali hiyo, yawezaje kusemwa kwamba mwanamke kama Bibi Khadija, ambaye heshima na huba yake kwa mumewe haikuwa jambo la kutiliwa shaka, akimbilie kwenye masanamu (yaliyokuwa kitu kibaya zaidi machoni pa mumewe) wakati wa vifo vya wanawe. Aidha, sababu ya kuvutiwa kwake na Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na kule kujingiza kwake katika ndoa naye ni kuvutiwa kwake na tabia yake na mambo yake ya kiroho, kwa kuwa alisikia kwamba alikuwa ni Mtume wa mwisho. Katika hali hii, yawezekanaje kwamba aende na kuyalalamikia masanamu katika jambo hilo?” Tayari tulishawasimulia wasomaji wetu baadhi ya mazungumzo yake na Waraqa bin Nawfal (mnajimu wa kiarabu) pamoja na wanachuoni wengineo wa zama zile.

Mwana Wa Kulea Wa Mtukufu Mtume (S.A.W.W)

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimwita Zayd bin Haarith kuwa ni mwanawe kandoni mwa Jiwe Jeusi. Zayd alikuwa ni mtu aliyetekwa na maharamia wa kiarabu kutoka kwenye mipaka ya Sham na wakamwuza katika soko la Makkah na akanunuliwa na Hakim, jamaa yake Bibi Khadija. Hata hivyo haifahamiki dhahiri jinsi ilivyotokea baadaye hadi akanunuliwa na Bibi Khadija.

Mwandishi wa kitabu ‘Hayaat Muhammd’ anasema: “Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amepatwa mno na vifo vya wanawe, na ili ajiliwaze, alimwomba Khadija amnunue Zayd. Baadae Mtume (s.a.w.w.) alimpa uungwana na akamlea kama mwanawe hasa.”

Hata hivyo, wengi wa waandishi wanasema kwamba wakati wa ndoa ya Bibi Khadija na Mtume Muhammad (s.a.w.w.), Hakim bin Hizaam alimpa shangazi yake (Khadija) huyu zayd. Kwa kuwa Zayd alikuwa kijana mwema na mwenye akili, Mtume alianza kumpenda na Bibi Khadija naye alimpa Mtume (s.a.w.w.) kijana huyu akiwa ni zawadi. Hata hivyo, mwishowe baba yake Zayd alitambua aliko mwanae (Zayd) baada ya kumtafuta kwa muda mrefu. Hapo Mtume (s.a.w.w.) alimruhusu Zayd arudi makwao na baba yake. Hata hivyo, kutokana na huba na upole wa Mtume (s.a.w.w.) juu yake, Zayd alipendelea kubakia na Mtume (s.a.w.w.). hii ndio sababu kwamba Mtume (s.a.w.w.) alimpa uungwana, na kumchukua akiwa kama mwanawe hasa na akamwoza Zaynab, bint Jahsh.5

Mwanzo Wa Tofauti Miongoni Mwa Wenye Kuabudu Masanamu

Kutokana na uteuzi wa Mtume (s.a.w.w.) kuishika kazi ya Utume, kulitokea kutofautiana kwingi miongoni mwa wakuraishi, ingawa msingi wa tofauti hizi ulijengeka zamani sana, na hata kabla ya uteuzi huu wa Mtume (s.a.w.w.), kiasi fulani watu wenye busara waliidhihirisha chuki yao na kutoipenda dini ya Waarabu.
Daima ilikuwako kauli katika kila pembe na ufa juu ya Nabii wa Uarabuni aliyekuwa akisubiriwa, ambaye atazihuisha ibada za Allah Aliye mmoja tu. Wayahudi walikuwa wakisema: “Kwa kuwa msingi wa dini yetu na ile ya yule Nabii wa Uarabuni ni moja, tutamfuata, na kwa msaada wa nguvu zake tutayavunja masanamu na kulivunja jumba la ibada ya masanamu.

Ibn Hisham anasema katika Sirah yake:6 “Wayahudi walikuwa na kawaida ya kuwaogofya Waarabu waliokuwa wakiyaabudu masanamu wakasema kwamba wakati wa kudhihiri kwa Nabii wa Uarabuni ulikuwa ukikaribia upesi sana na atalibomoa jengo la ibada ya masanamu. Mbele ya

Waarabu, maneno haya yalitoa mandhari ya mapinduzi ya zama za ibada ya masanamu. Yalitoa mno picha hii kiasi kwamba kufuatana na mafunzo ya awali ya Wayahudi, baadhi ya makabila yatauitika mwito wa Mtume (s.a.w.w.) na kusilimu. Hivyo, kutokana na sababu fulani fulani tutakazozieleza baadae, Wayahudi waliendelea na ukafiri wao. Aya ifuatayo ya Qur’ani Tukufu inaizungumzia hali hii:

وَلَمَّا جَاءَهُمْ كِتَابٌ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ مُصَدِّقٌ لِمَا مَعَهُمْ وَكَانُوا مِنْ قَبْلُ يَسْتَفْتِحُونَ عَلَى الَّذِينَ كَفَرُوا فَلَمَّا جَاءَهُمْ مَا عَرَفُوا كَفَرُوا بِهِ ۚ فَلَعْنَةُ اللَّهِ عَلَى الْكَافِرِينَ {89}

“Na kilipowajia kitabu (Qur’ani) kutoka kwa Allah kiyasadikishayo yale yaliyo pamoja nao (Torati), na zamani walikuwa wakiomba ushindi dhidi ya makafiri; lakini yalipowafikia yale waliyoyajua waliyakana; basi laana ya Allah iko juu ya makafiri.” (Sura al- Baqarah, 2:89).

Misingi Ya Ibada Ya Masanamu Yatikisika

Katika wakati wa sherehe ya moja ya sikukuu za Waquraishi lilitokea tukio la ajabu ambalo machoni pa watu waonao mbali, liliigonga kengele ya hatari ya kupinduliwa kwa utawala wa wenye kuabudu masanamu. Safari moja wakati wenye kuabudu sanamu walipolikusanyikia sanamu moja na walikuwa wakiyasugua mapaji ya uso ardhini mbele ya sanamu lile, wanne miongoni mwa watu wao maarufu waliokuwa mashuhuri kwa elimu na busara zao, walikikataa kitendo chao hicho na wakaendesha mjadala juu ya jambo hili katika sehemu ya faragha.

Moja ya jambo walilolijadili lilikuwa kwamba taifa lao limepotoka kutoka kwenye njia ya Ibrahim; na mawe waliyoyazunguuka watu hayasikii, wala kuona wala kuwatendea jema lolote wala dhara7 Watu hawa wanne walikuwa ni:

(1) Waraqah bin Nawfal, ambaye baada ya kusoma sana akawa Mkristo na akajipatia elimu pana juu ya Biblia,
(2) Abdallah bin Jahash aliyesilimu baada ya kuanza kwa Uislam na akahamia Ethiopia pamoja na Waislamu wengine,
(3) Uthman bin Huwayris aliyekwenda kwenye mahakama ya Kirumi na kuin- gia Ukristo,
(4) Zayd bin ‘Amri bin Nafil, ambaye baada ya kujipatia elimu ya kutosha, alijichagulia dini ya Ibrahim.

Unyonge Mwingine Wa Waquraishi

Wakati ule Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na umri usiozidi miaka thelathini na mitano, alipolazimika kuuona ugomvi mkubwa miongoni mwa Waquraishi ulioamuliwa kwa mkono wake Mtume (s.a.w.w.) wenye uwezo. Tukio lifuatalo laonesha jinsi Waquraishi walivyokuwa wakimheshimu na kumkubali kuwa yu mwaminifu na mkweli:

Mafuriko yenye kuogofya yalitiririka kutoka kwenye milima mirefu yakiielekea nyumba ya Allah, na kutokana nayo hakuna hata nyumba moja miongoni mwa nyumba za Makkahh hata ile Al-Ka’ba Tukufu Iliyosalimika kutokana na uharibifu ulioletwa na mafuriko hayo. Nyufa nyingi zilitokea katika kuta za Al-Ka’ba. Hivyo Waquraishi wakaamua kuijenga upya ile Al-Ka’ba lakini walichelea kuibomoa. Walid bin Mughayrah alikuwa mtu wa kwanza aliyechukua sululu mkononi mwake na akazibomoa nguzo mbili za Al-Ka’ba. Hapa akajihisi kuwa yu mwenye kuogopa mno na mwenye mashaka.

Watu wa Makkahh walikuwa wakisubiri kupatwa na msiba fulani, lakini walipoona kwamba Walid hakuipata ghadhabu ya masanamu, walipata matumaini ya kwamba kitendo chake kile kilipata kibali cha masanamu. Matokeo yake ni kwamba wote walijitia katika kazi ya kulibomoa lile jengo. Kwa bahati, katika siku ile ile, meli iliyotoka Misri iliyomilikiwa na mfanya biashara mmoja wa Kirumi ilipinduka kwenye bandari iliyopo karibu na Makkahh (Jiddah) kutokana na dhoruba kali. Waquraishi walipata taarifa za tukio hilo. Hivyo basi wakawapeleka watu Jiddah ili wakanunue mbao za meli ile kwa ajili ya ule ujenzi wa Al-Ka’ba. Ama huhusu kazi ya ujenzi walimwajiri mjenzi wa Kimisri aliyekuwa akikaa mle mjini Makkahh.

Kuta za Al-Ka’ba zilifikia urefu wa mwanadamu. Sasa ukafika wakati wa kuliweka lile Jiwe Jeusi kwenye sehemu yake. Katika hatua hii, ziliibuka tofauto miongoni mwa machifu wa makabila na kabila la Bani Abduddar na Bani Adi walifanya mapatano ya kwamba hawatamruhusu mtu yeyote mwingine kuifaidi heshima hii. Ili kuyaimarisha mapatano yao hayo, walikijaza damu chombo fulani na wakachovya mikono yao humo.

Kutokana na hali hii, ile kazi ya ujenzi ilisimama kwa kipindi cha siku tano. Jambo hili lilifika katika hali mbaya. Makundi mbali mbali ya Waquraishi yalikusanyika kwenye Masjid ul Haraam na likawapo tishio la kuzuka kwa ugomvi wa kumwaga damu.

Hata hivyo, hatimaye mzee mmoja mwenye kuheshimika kutoka miongoni mwa Waquraishi, aliyeitwa Abu Umayyah bin Mughyrah Makhzumi aliwakusanya machifu wa Kikuraishi na kuwaambia: “Mkubalini kuwa mpatanishi yule mtu atakayeingia (humu Masjidul Haraam) kupitia lango la Safa (kufuatana na baadhi ya vitabu vya historia ni Babus Salam).” Machifu wote waliukubali ushauri huu. Mara Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.) akaingia Masjidul Haraam kupitia lango lile. Wote wakasema kwa pamoja: “Ni Muhammad, mtu mwaminifu. Tunakubali awe mpatanishi!”

Mtume (s.a.w.w.), ili kuumaliza ugomvi huu, aliwaomba walete shuka. Aliliweka lile Jiwe Jeusi katika ile shuka kwa mikono yake na kisha akashauri kila mmoja wa wale machifu wanne wa Makkahh ashike pembe moja ya ile shuka. Lile Jiwe Jeusi lilipoletwa karibu na ile nguzo (ya kuwekea), Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akaliweka katika sehemu yake kwa mikono yake ya heri.

Kwa njia hii aliumaliza ugomvi ule wa Waquraishi uliokuwa ukingoni mwa kuzaa tukio la umwagaji wa damu.8

  • 1. Siirah-i-Halabi, Juzuu 1, uk. 123.
  • 2. Kuna tofauti kubwa kuhusu mabinti watatu wa Mtukufu Mtume, yaani Zainab, Ummu Kulthum na Ruqayyah.
  • 3. Manaqib Ibn Shihr Ashub, Juzuu 1, uk. 140; Qurbul Asnad uk. 6-7; al- Khisaa’il, Juzuu 2, uk. 37; Bihaarul-Anwaar, Juzuu 22, uk. 151-152. baadhi ya wanahistoria wanasema kwamba wana wa kiume wa Mtume (s.a.w) walikuwa zaidi ya wawili (Tarikh-i-Tabari, Juzuu 2, uk. 35 na Bihaarul-Anwaar, Juzuu 22; uk. 166.
  • 4. Amaali, Shaykhal-Mufid, uk. 247.
  • 5. Al-Isaba, Juzuu 1, uk. 545; Usudul Ghabah, Juzuu 2, uk. 224.
  • 6. Siirah-i-Ghabah, Juzuu 1, uk. 231
  • 7. Siirah-i-Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 222-223.
  • 8. Mtu mmoja aliyeitwa Habirah bin Wahab Makhzumi ameliandika tukio hili katika hali ya shairi katika wasifu aliouandika. Siirah-i-Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 213; Tarikh-i-Tabari, Juzuu 2; Furu’I Kafi, Juzuu 1, uk. 225; na Bihaar Anwaar, Juzuu 15, uk. 39-41. Inafaa kuona kwamba, wakati wa ujenzi wa Ka’bah, wale wote waliohusika wali- pashwa habari kama ifuatayo: “Katika ujenzi wa Al-Ka’ba tumieni mali mlizoji- patia kwa njia ya halali. Fedha mliyoichuma kwa njia isiyo sahihi au kwa rushwa au kwa dhuluma isitumike kwa lengo hili.” Bila shaka fikara hii ndio hasa masim- bi ya mafundisho ya Mitume yaliyokuwa bado yamesalia miongoni mwa Waquraishi.