read

Sura Ya Kumi Na Mbili:Wahyi Wa Kwanza

Tarehe Ya Kwanza Kwa Kazi Ya Utume

Kama vile ilivyo tarehe ya kuzaliwa na kufa kwake Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), tarehe ya kuanza kwake kazi ya utume nayo haifahamiki kwa mtazamo wa kihistoria, karibuni wanachuoni wote wa Kishi’ah wanasema kwamba alipokea ujumbe wake wa kwanza mnamo tarehe 27 Rajab na alianza kazi yake ya Utume katika siku hiyo hiyo. Hata hivyo, wanachuoni wa Kissuni kwa kawaida hudai kwamba aliteuliwa kuishika kazi hii katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kwa vile Mashi’a wanadai kuwa ni wafuasi wa dhuria wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) huzichukulia taarifa zao kuwa ni za kweli, na zenye kukata shauri. Kutokana na ‘Hadithi Thaqalayn’ wamezikubali taarifa za kizazi cha dhuria wa Mtukufu Mtume kuhusiana na tarehe ya uteuzi huu wa kazi ya Utume na kuwa ndiyo sahihi.

Dhuria wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) wamesema: “Chifu wa familia (yetu) aliteuliwa kuishika kazi ya utume tarehe 27 ya mwezi wa Rajab.”Kufuatana na jambo hili, Mashi’a hawatilii shaka yoyote kuhusiana na usahihi wa tarehe hii.

Kitu kiwezacho kuchukuliwa kuwa ndio msingi wa maoni mengine ni ile kauli ya Qur’ani tukufu, ambayo ndani yake imeelezwa kwamba aya za Qur’ani zilifunuliwa katika mwezi wa Ramadhani.

Na kwa vile siku ya kuanza kwa kazi ya Utume ni ile siku ya kuanza kufunuliwa Qur’ani tukufu, tunaweza kusema kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliteuliwa kuianza kazi ya Utume katika mwezi ule ule wa Ramadhani. Aya za Qur’ani tukufu zitajazo kwamba ilifunuliwa katika mwezi wa Ramadhani ni hizi:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنْزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ{185}

“Mwezi wa Ramadhani ndio (mwezi) ambao ilifunuliwa Qur’ani…….” (Suratul-Baqarah 2:185).

وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ {2}

إِنَّا أَنْزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنْذِرِينَ {3}

“Naapa kwa Kitabu kitukufu kwamba tumeifunua (hii Qur’ani ) kati- ka usiku uliobarikiwa…..(Surah al-Dukhaan, 44:2-3).

Na huu ni ule usiku wa Qadr (utukufu) uliotajwa katika Surat al-Qadr (aya ya 1) ambayo ndani yake mmesemwa ya kwamba: Tumeifunua Qur’anim katika usiku wa cheo.”

Jibu La Wanachuoni Wa Kishi’ah

Wanahadithi wa Kishi’ah na wafasiri wa Qur’ani tukufu wametoa majibu na maelezo mbali mbali kuhusiana na hoja hii; baadhi ya hoja hizo tunazitaja hapa chini.

Jibu La Kwanza

Aya tulizozitaja hapo juu zaonyesha kwamba Qur’ani tukufu ilifunuliwa katika usiku mmoja uliobarikiwa wa mwezi mtukufu wa Ramadhani unaoitwa ‘Usiku wa Cheo’ lakini hapatajwi mahala pa kufunuliwa kwake na vile vile hawaashirii kwamba zilifunuliwa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika usiku huo huo.

Inawezekana kwamba zilikuwepo funuo mbali mbali za Qur’ani, na masimulizi mengi ya Kishi’ah na Kisunni yanauthibitisha uwezekano huu. Mmoja wa funuo hizi ni ufunuo wa pole-pole wa Qur’ani tukufu kwa Mtume (s.a.w.w.), na mwingine ni ufunuzi wake wa visehemu sehemu kutoka kwenye ‘Lauhul Mahfudh1 kwenda ‘Baytul Ma’amur2 hivyo basi, hakuna kosa lolote kwa aya chache za Surat al-Alaq kufunuliwa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika tarehe 27 ya Rajab na Qur’ani yote katika hali ya kitu chote kizima, ikafunuliwa katika mwezi wa Ramadhani kutoka mahali palipotajwa na Qur’ani tukufu kuwa ni ‘Lauhul Mahfudh’ kwenda kwenye sehemu nyingine iitwayo ‘Baytul Ma’amur’.

Maoni haya yanathibitishwa na aya hiyo hiyo ya Surah al-Dukhaan isemayo: Tunaapa kwa Kitabu kitukufu kwamba Tumeifunua (hii Qur’ani) katika usiku uliobarikiwa…..” kutokana na aya hii ni dhahiri kwamba (kutegemeana na uzito wa vijina (pronoun) virudivyo kwenye neno ‘Kitabu’ ) vilifunuliwa katika hali ya ukamilifu wake kwenye usiku mtukufu (ulioangukia katika mwezi wa Ramadhani) na ni sahihi tu kwamba ufunuo huu kuwa ni mwingine ghairi ya ule ufunuo uliofanyika katika wakati wa kuteuliwa kwake Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuishika kazi ya Utume kwa sababu, wakati ule ni aya chache tu zilizofunuliwa.

Kifupi ni kwamba Qur’ani ilifunuliwa katika mwezi wa Ramadhani katika ‘usiku wa cheo’ haiwezi kuwa uthibitisho wa ukweli kwamba ndio siku ya uteuzi wa Mtume (s.a.w.w.) kuishika kazi ya Utume ambayo katika siku hiyo aya chache tu zilifunuliwa, nako kulitokea katika mwezi ule ule, kwa sababu aya tulizozitaja hapo juu zaonyesha kwamba Kitabu kizima (Qur’ani Tukufu) kilifunuliwa katika mwezi ule ule ambapo, katika siku za uteuzi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuishika kazi ya utume ni aya tano au sita tu zilizofunuliwa. Hivyo basi, hizo madhehebu mbili, wanapozieleza maana za aya tulizozitaja hapo juu katika masimulizi yao, wanasema kwamba Qur’ani nzima iliteremshwa kutoka ‘Lauhul Mahfudh’ kwenda ‘Baytul Ma’amur’ katika usiku ule. Wanachuoni wa Kishi’ah na Kisunni wameyanukuu maelezo tuliyoyataja na hasa Profesa Muhamad Abdul Azim Zarqaani wa chuo kikuu cha Al-Azhr’ amezitaja kwa kirefu ndani ya kitabu chake.3

Jibu La Pili

Jibu lililokamili zaidi, lililopata kutolewa na wanachuoni, ni hili la pili. Mwanachuoni Mkuu Tabatabai ameeleza kwa kirefu katika kitabu chake chenye thamani4 na kiini chake tunakitoa hapa chini. Shabaha halisi na ya hakika ya Qur’ani tukufu kusema kwamba:

‘Tumeifunua (hii Qur’ani ) katika mwezi wa Ramadhani’ ni kwamba ili- funuliwa katika mwezi ule kwa sababu, zaidi ya kufunuliwa kidogo kidogo hii Qur’ani ina ukweli ambao ndani yake Allah Mwenyezi Alimwarifu Mtume (s.a.w.w.) katika usiku maalumu wa mwezi wa Ramadhani.

Kwa kuwa Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na elimu ya kitabu kitakatifu chote alielekezwa kutoharakisha katika kuyabalighisha yaliyokuwa humo na kwamba asubiri hadi aipokee amri juu ya ubalighisho wake kwa watu kwa pole pole. Qur’ani tukufu inasema: “Usiharakishe kuzibalighisha habari za Qur’ani hadi upate amri kuhusiana na jambo hili kwa njia ya Wahyi.”

Jibu hili laonyesha kwamba Qur’ani tukufu ilikuwako katika hali ya ujumla wake uliofunuliwa katika ukamilifu wake katika wakati mmoja wa mwezi wa Ramadhani na vile vile ina kuwako kwake kwa utaratibu wa polepole kulikoanzia tangu katika siku ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuteuliwa kuishika kazi ya Utume hadi mwishoni mwa uhai wake.

Jibu La Tatu

Kama tulivyoeleza kwa mukhtasari kuhusu aina mbali mbali za ufunuo, kwa hakika una hatua mbali mbali. Hatua ya kwanza ni ile ya ndoto. Hatua ya pili ni ile ya siri na sauti za mbinguni zinazosikika pasi na kumkabili Malaika. Na hatua ya mwisho ni ile ya Mtume kumwona Malaika na kuyasikia maneno ya Allah kutoka kwake na kujifunza kupitia kwake juu ya hali halisi za dunia nyinginezo.

Kwa kuwa roho ya mwanaadamu haina nguvu ihitajikayo kuzihimili hatua mbali mbali za wahyi katika wakati wa kwanza, ni muhimu kwamba uwezo wa kuzihimili ukue polepole, tunaweza kusema kwamba: Katika siku ile ya kuteuliwa kwake kuishika kazi ya utume (tarehe 27 ya Rajab) na kwa kipindi fulani baada ya hapo, alikuwa akizisikia zile sauti za mbin- guni tu zilizomwarifu ya kwamba alikuwa ni Mjumbe na Mtume wa Allah na haikuwapo aya yoyote iliyofunuliwa katika kipindi kile. Na wakati mwingine baadaye polepole ufunuo wa Qur’ani tukufu ulianza katika mwezi wa Ramadhani.

Kwa kauli hii tuna maana ya kwamba kuteuliwa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuishika kazi ya utume katika mwezi wa Rajab hakuhusiani na kufunuliwa kwa Qur’ani tukufu katika mwezi ule. Kutokana na jambo hili, hakuna Haja ya kuwapo hitilafu kati yake na kule kufunuliwa kwa Qur’ani tukufu katika mwezi wa Ramadhani na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuteuliwa kuishika kazi ya Utume katika mwezi wa Rajab.

Ingawa yale tuliyoyasema hapo juu hayaafikiani na maandiko ya vitabu vingi (kwa sababu wengi wa wanahistoria wamesema dhahiri kwamba aya za Surat al-Alaq zilifunuliwa katika siku ile ile ya uteuzi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuishika kazi ya Utume), mpaka tupate masimulizi yanayotueleza kwamba katika siku ile ya uteuzi wa Mtume kuishika kazi aliisikia sauti ya siri na isiyosema lolote kuhusu ufunuzi wa Qur’ani tukufu au aya zake. Wanalieleza jambo hili kwa kusema kwamba katika siku ile

Mtume alimwona Malaika aliyemwambia: “Ewe Muhammad! Wewe ni Mjumbe wa Allah.” Na kwenye baadhi ya masimulizi ni kule kuisikia sauti tu kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) tu kulikotajwa na hakuna lolote lililosemwa kuhusu kumwona kwake Malaika.5

Itikadi Ya Mtukufu Mtume (S.A.W.W) Kabla Ya Kuianza Kazi Ya Utume

Kwa kipindi kirefu suala la dini ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kabla ya kuianza kazi ya Utume limekuwa jambo la kujadiliwa baina ya wanachuoni wa Kishi’ah na Kisunni. Wameibua maswali yafuatayo na kutoa jibu kwa kila moja kati yao:

Je, Mtume (s.a.w.w.) aliifuata dini yoyote ile kabla ya kuteuliwa kuianza kazi ya Utume?

Kuchukulia kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa mfuasi wa dini, je dini hiyo ilikuwa ni dini yake mwenyewe.

Kama alikuwa mfuasi wa dini yoyote ile, je, dini hii ilikuwa dini iliyofunuliwa kwake pekee na alifuata kwa pekee au alihesabiwa kuwa mmoja wa wafuasi wa dini ile?

Kama alitenda kazi katika dini ile peke yake au akiwa yu mfuasi, ni Mtume wa kale yupi aliyekuwa na dini ile?

Haya ndio maswali manne ayaonayo mtu katika vitabu mbali mbali vya Siira (maisha ya Mtukufu Mtume s.a.w.w.), historia, na tafsiri za Qur’ani tukufu.

Hata hivyo, je, ni muhimu kwamba hatuna budi tutoe majibu halisi ya maswali haya? Je, kimsingi ni muhimu tuvisome vitabu mbali mbali vya historia, tafsiri za Qur’ani tukufu na maisha ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na kukusanya majibu yahitajikayo?

Tunaona kwamba mijadala juu ya mambo haya si muhimu hata kidogo.6 Badala yake kilicho muhimu ni kwamba, hatuna budi kuthibitisha kwamba kabla ya uteuzi wake wa kuishika kazi ua Utume, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimwitakidi na kumwabudu Allah Aliye Mmoja tu na alikuwa mchamungu na mnyoofu.

Jambo hili laweza kuthibitishwa kwa njia mbili zifuatazo:

Kwanza, kwa kuchunguza ile miaka yake arobaini ya kabla ya Uteuzi wake wa kuishika kazi ya Utume, na Pili, kwa kuyachunguza kwa makini yale yaliyosemwa na viongozi wa Uislamu kulihusu jambo hili:

Tukitoa mukhtasari wa maisha yake ya miaka arobaini, yalikuwa ni maisha ya wastani na unyoofu, uaminifu na ukweli, haki na uadilifu, wema na huruma kwa waliokandamizwa na masikini na chuki juu ya masanamu na wenye kuyaabudu. Alikuwanazo tabia hizi kwa wingi mno kiasi kwamba, safari moja alipokuwa akienda Sham katika biashara na mtu mmoja aliyekuwa akifanya naye mapatano, aliapa kwa majina ya masanamu, yeye akasema: “Vitu vichukizavyo mno vyenye kupandisha ghadhabu yangu ni hawa ‘Laat’ na ‘Manaat’ anaojiapiza kwao.”

Mbali na hayo alikuwa akisali mfululizo katika pango la Hira katika mwezi wa Ramadhani na kufanya Hijja katika siku za Hajj, na tena kama asemavyo Imam wetu wa sita, yeye (Mtukufu Mtume s.a.w.w) alifanya Hajj kwa siri mara kumi na kwa mujibu wa wasimulizi wengine alifanya hivyo mara ishirini. Na kama tujuavyo ibada zote za Hajj ni utekelezaji wa ibada ambayo Nabii Ibrahim (a.s.) aliwaita watu na akata- ka kwamba kwa njia hii, wale wenye kumwamini Allah wa Pekee, wakusanyike katika sehemu moja maalum katika kipindi maalum.

Hali kadhalika, daima Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akimkumbuka Allah alipokuwa akila chakula na aliacha kula nyama ya wanyama waliochinjwa kwa njia isiyo halali, kwa kila mara alikuwa akishitushwa na kuyaona mandhari machafu, ulevi, na kucheza kamari, alivichukia mno vitu hivi kiasi kwamba wakati mwingine alikuwa akikikimbilia milimani na kurudi nyumbani baada ya kupita sehemu fulani ya usiku. Sasa, linalohitajika na fikara zetu ni hili:

Je, inawezekana kutia shaka juu ya itikadi ya mtu aliyepitisha maisha yake katika hali tuliyoitaja hapo juu na asiyekuwa na udhaifu japo ulio mdogo zaidi tangu mwanzoni mwa maisha yake, na aliyeipitisha sehemu ya maisha yake katika vilima na katika sehemu ya kujitenga ili atafakari juu ya maajabu yapendezayo ya ulimwengu huu. Tunamchukulia mtu wa kawaida kuwa mcha Mungu, mwenye kuwajibika na mwenye haki, kama tukiona moja ya kumi ya sifa hizi kwake, je tuzungumze nini juu ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.)?

Njia ya pili ya kuipata hali halisi ni uchunguzi wa nyaraka na masimulizi yaliyotufikia kutoka kwa viongozi wa Uislamu. Moja kati ya hayo ni masimulizi ya Imam Ali (a.s.), chifu wa itikadi ya Upweke wa Allah, katika ‘Khutba-i Qaasi’ah’: “Tangu wakati Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipoacha kunyonya, Allah Mwenyezi alimshirikisha Malaika mtukufu zaidi pamoja naye ili aweze kumwonyesha njia ya unyoofu na wema wakati wa mchana na usiku.7

Ulinganisho Baina Ya Mtume Muhammad (S.A.W.W) Na Nabii Isa (A.S).

Hakuna shaka juu ya ukweli kwamba Mtume wa Uislam (s.a.w.w.) anazo fadhila juu ya Mitume wote wa kabla yake. Na imeelezwa dhahiri katika Qur’ani tukufu juu ya baadhi ya Mitume kwamba waliinuliwa hadi kwenye daraja la Utume tangu utotoni mwao na vile vile walipelekewa vitabu. Kwa mfano, Qur’ani tukufu inasema juu ya Nabii Yahya (a.s.) hivi:

يَا يَحْيَىٰ خُذِ الْكِتَابَ بِقُوَّةٍ ۖ وَآتَيْنَاهُ الْحُكْمَ صَبِيًّا {12}

“Kwa Yahya Tulisema: ‘Kishikilie Kitabu kwa nguvu, na tukampa hekima, rehema na usafi tangu yungali mtoto.” (Surat Mariam, 19:12.)

Wakati Nabii Isa (a.s.) alipokuwa bado yu mtoto mchanga wazee wa Bani Israiil walimshikilia mama yake awajulishe wamjue baba wa mtoto yule.

Bibi Mariam aliashiria kwenye kitanda cha mtoto yule ili kwamba watu wale walipate jibu la swali lao kutoka kwa yule mtoto mwenyewe. Nabii Isa (a.s.) aliwajibu kwa maneno haya kwa ufasaha mkuu na uthabiti:

قَالَ إِنِّي عَبْدُ اللَّهِ آتَانِيَ الْكِتَابَ وَجَعَلَنِي نَبِيًّا {30}

وَجَعَلَنِي مُبَارَكًا أَيْنَ مَا كُنْتُ وَأَوْصَانِي بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ مَا دُمْتُ حَيًّا {31}

“….Hakika mimi ni mja wa Allah; amenipa Injili na amenifanya Nabii, na amenifanya mbarikiwa, popote niwapo, na ameniusia Sala na Zaka maadamu ningali hai.” (Surat Mariam, 19:30-31).

Mwana wa Mariam anatufafanulia juu ya misingi na kanuni za dini yake tangu katika wakati wa utotoni mwake na anatangaza ya kwamba anaifuata kanuni ya ibada ya Allah Aliye Mmoja tu.

Sasa tunazivuta fikara zako kushuhudia na kukuuliza: “Wakati Nabii Yahya (a.s.) na Nabi Isa (a.s.) ni waumini wa kweli na wanazitangaza kweli za maumbile, je, tunaweza kusema kwamba huyu kiongozi wa wanaadamu asiye na kifani na aliye mtukufu zaidi miongoni mwa wanaadamu hakuiona itikadi isiyo kifani hadi alipofikia umri wa miaka arobaini, ingawa hata katika muda wa ufunuo katika lile pango la Hira tayari alikuwa akijishughulisha na kutafakari?”

  • 1. Tazama: “Tafsirul Mizaan” cha Allamah Muhammad Husayn Tabatabai.
  • 2. Tazama: “Tafsirul Mizaan” cha Allamah Muhammad Husayn Tabatabai.
  • 3. Manaahilul ‘Irfaan fi’Ulumil Qur’ani, Juzuu 1, uk. 37.
  • 4. Al-Mizaan, Juzuu 2, uk. 14-16.
  • 5. Bihaarul Anwaar, Juzuu 18, uk. 184, 190 na 103.
  • 6. Bihaarul Anwaar, Juzuu 18, uk. 271- 281.
  • 7. Nahjul Balaghah, Juzuu 2, uk. 182