read

Sura Ya Kumi Na Moja:Udhihiriko Wa Kwanza Wa Ukweli

Kwa kweli, kimsingi historia ya Uislamu huanzia kwenye ile siku ambayo Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipewa amri ya kuianza kazi ya Utume na kuleta mfululizo wa matukio katika mkondo wake. Siku ambayo Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipewa amri ya kulianza jukumu la kuwaongoza watu na maneno: “Wewe ni mjimbe wa Allah” yalikuwa yakigonga masikioni mwake, alilibeba jukumu lililo kuu lililobebwa na Mitume wote wa awali (a.s.). katika siku ile, sera ya yule ‘mtu mkweli’ wa Waquraishi ilifahamika vizuri na lengo lake likajidhihirisha zaidi. Kabla ya kulisikia tukio la kwanza la Utume wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ni muhimu kwamba tuyaeleze mambo muhimu mawili:

1. Umuhimu wa kuteuliwa kwa Mitume.

2. Mvuto wa Mitume katika kuitengeneza jamii.

Umuhimu Wa Kuteuliwa Kwa Mitume

Allah Mwenyezi Amedukiza njia za maendeleo na ukamilifu katika maum- bile ya kila kiumbe na amekishehenesha na nyenzo mbalimbali za msaada kwa ajili ya kupita katika njia iendayo kwenye ukamilifu. Hebu utupie jicho mche mdogo. Idadi kubwa ya visababisho hufanya kazi kwa ajili ya ukamilifu wake. Mizizi ya mche huu hufanya kazi kwa kadiri ya uwezo wake wote kuupatia chakula chake na kuupatia mahitaji yake yote na mishipa yake mbalimbali hutawanywa kwa kadiri ihitajikayo majimaji ya chakula miongoni mwa matawi na majani yake.

Hebu litizame umbo lake ni lenye kushangaza zaidi ya lile la miti mingine. Bakuli la ua huifanya kazi ya kuufunika uso wa chipukizi na kuyahami majani ya ua (petals) na rangi yake. Kadhalika sehemu nyingine za ua lile, ambazo zote zimeteuliwa kwa ajili ya kukilisha kiumbe chenye uhai na zinayatekeleza majukumu yao kwa njia iliyo bora zaidi kwa kadiri ya uwezo wao. Na kama ukienda hatua moja na kulitupia jicho umbo lishangazalo la ulimwengu wa wanyama utaona kwamba visababisho viwezeshavyo kuifikia mipaka ya ukamilifu viko pamoja nao.

Kama tukitaka kuelezea jambo hili kisayansi, tutasema kwamba ujuzi wa uhai, ambao ni baraka ya utendaji kazi wa maumbile, wamepewa viumbe wote. Qur’ani Tukufu imeueleza muongozo huu wa kweli kwa maneno haya:

Yeye (Allah) Ameumba kila kiumbe na akakifunza jinsi ya kuishi”

Viumbe vyote, tangu kwenye chembe ndogo ya uhai (atom) hadi makundi makubwa ya nyota ya ulimwengu, vina fungu lao katika baraka hii. Allah baada ya kuchukua kipimo kamili ameionyesha njia ya ukamilifu na maendeleo yake ya polepole na ameainisha vipengele kwa ajili ya mafunzo na mabadiliko (evolution) ya kila kiumbe. Na huu ndio haswa ‘mwongozo kwa ajili ya uwepo’ ambao hutawala viumbe wote wa ulimwengu bila tofauti yoyote.

Hata hivyo, swali huibuka hapa kuhusu kama huu msukumo wa kimaum- bile juu ya kuwepo hutosheleza pia kwa kiumbe kile, ambao ndio bora kuliko vyote. Bila shaka sivyo hata kidogo. Sababu yake ni kwamba, ukiachilia mbali yale maisha ya kimaada, vile vile mwanadamu anayo maisha mengine ambayo ndio hasa msingi wa kuwepo kwake. Kama mwanadamu ataishi maisha ya kimaada tu na yasiyo na akili, kama jamii ya wanyama na ya miti, basi vile vipengele vya kimaada vingalitosha kwa mwendo wake, maendeleo na ukamilifu. Hata hivyo, kwa vile ametokea kuwa na maisha aina mbili, siri ya ustawi wake na utukufu umo katika ukamilifu wa maisha yote hayo.

Mtu wa kwanza wa kawaida ambaye aliishi kwenye mapango na kuwa na hali ya asili halisi, na ambaye katika silika yake ya kimaumbile hakuna upotovu hata kidogo uliotokea, mtu huyu hakuhitaji mafunzo makubwa kama yale ayahitajiyo mtu aliye staarabika.

Hata hivyo, mwanadamu anapoichukua hatua ya kwenda mbele na akayabadilisha maisha yake na kuwa ya mkusanyiko mmoja, pia wazo la ushirikiano likajikita imara vizuri maishani mwake na kulitawala, basi kukengeuka ambako ni matokeo ya mgongano wa kijamii na mawasiliano hutokea katika nafsi yake, na tabia mbaya na fikara zisizo sahihi huichukua nafasi ya kiini cha fikara za asili na kuvuruga awiano na usawa wa jamii.

Mikengeuko hii humfanya Muumba wa huu ulimwengu alete waelimishaji wairekebishe jamii na kuyapunguza maovu ambayo ni matokeo ya wanadamu wanapoishi pamoja, ili kwamba, kutokana na taa ziangazazo na sheria za uadilifu, waweze kuongoza jamii kwenye njia iliyonyooka, ambayo huhakikisha ustawi wa watu wote wenye ustadi katika kila fani.

Haipingiki kwamba, kuishi kwa pamoja, licha ya kuwa kwake na faida, vile vile kunabeba maovu fulani na kunaleta mikengeuko mingi. Kwa sababu hii, Allah Mwenyezi, ameleta waalimu ili kwamba waweze kuipunguza mikengeuko na ukaidi, kwa kadiri iwezekanavyo, na kuliweka gurudumu la jamii katika njia sahihi kwa kuweka sheria za dhahiri.1

Jukumu La Mitume Katika Kuitengeneza Jamii

Kwa kawaida inadhaniwa kwamba Mitume ni waalimu wa ki-Mungu ambao wanateuliwa ili kuwaelimisha watu. Watu hujifunzia kwenye shule za Mitume na njia zao za kijamii na tabia zao zimeelekezwa kwenye ukamilifu wa polepole kuelekea kwenye mwelekeo ulio sambamba na mafunzo ya wale viumbe waliobora zaidi. Ni kama kijana wa kiume aji- funzaye mambo mengi kwenye shule ya msingi, ya kati, chuo na chuo kikuu na anasogea siku hadi siku, ingawa katika siku ya kwanza hakuwa hata na picha japo ndogo ya mafunzo haya akilini mwake.

Hali kadhalika watu huipata elimu kutoka kwenye shule za Mitume, na sambamba na kuelimika kwao kutoka kwa Mitume, tabia zao na maisha yao ya kijamii hujipatia ukamilifu. Hata hivyo, tunaona kwamba Mitume ni waelekezaji wa watu. Kazi na jukumu lao ni kuwapa mazoezi na wala si kuwaelimisha, na kwamba msingi wa dini na sheria zao mkabala na mtazamo wao wa kimaumbile si kitu kipya au zawadi mpya. Na kama maumbile hayakukengeuka, na kama ujinga na tamaa ya mali haukuyakumba, yangetambua asili ya Sheria ya Mungu.

Hakika, yale tuliyoyasema hapo juu yametegemeana na kauli za viongozi wakuu wa Uislamu. Imam Ali, Amiri wa waumini (a.s.) amesema katika Nahjul Balaghah kuhusu lengo la Mitume hivi:“Yeye (Allah) amewateuwa Mitume kutoka miongoni mwa kizazi cha Adamu na akachukua ahadi kutoka kwao ya kuupeleka ufunuo kwa watu na kueneza ujumbe ambao wameaminishwa nao.

Amewapeleka ili wawaambie watu watimize ahadi yao ya kimaumbile na kukumbuka baraka walizozisahau. Aidha, kwa mafundisho yao, wao (Mitume) wawape watu onyo na kuwataka wazichimbue johari za hekima zao, kitu kilichosalia kwenye hali ya kufichikana katika hazina ya maumbile yao.”2

Mfano Wa Dhahir

Tunapodai kwamba kazi iliyofanywa na Mitume katika kuwafunza na kuwatengeneza watu ni sawa sawa na ile inayofanywa na mkulima wa bustani anayeulea mti, au tunaposema kwamba, kutokana na kuwaongoza watu na kufungua mtazamo wao wa kimaumbile, Mitume ni kama wataala- mu wa madini wanaochimba madini yenye thamani kutoka kwenye kiini cha milima, wala hatulisemi jambo lenye kupita kiasi (au kutia chumvi).

Jambo hili laweza kuelezwa hivi: Tangu katika hatua ya kwanza ya matengenezo ya kiini cha mmea, utakuwa na kila aina ya uwezo wa maendeleo ya kukua na kupevuka. Mara tu baada ya mmea huu kuanza kufanya kazi ya kuimarisha mizizi yake, kila aina ya utendaji wa mitambo ya madawa hewani na upatikanaji wa nuru na mabadiliko hutokea katika mmea mzima. Katika hatua hii, yule mkulima wa bustani anatakiwa afanye mambo mawili. Kwanza lazima afanye mambo muhimu yapatikane kwa ajili ya kuimarisha mizizi ili kwamba nguvu ya fichu ya mmea iweze kukua.

Pili, hana budi kuizuia mikengeuko, ili kwamba, kama nguvu ya ndani ya mmea ule ikichukua hatua inayozuia ustawi wake, hana budi kuikata. Hivyo basi, si kazi ya yule mkulima wa bustani kuufanya mmea ule ukue. Kinyume na hivyo, kazi yake ni kutoa na kuthibitisha kwamba zinapatikana hali zilizo muhimu ili kwamba ule mmea uweze kuufunua ukamilifu wake wa fichu.

Muumba wa huu ulimwengu alimuumba mwanadamu na akamjaalia nguvu nyingi na utashi wa kimaumbile. Ameurekebisha utashi wake (mwanadamu) wa kimaumbile kwa nuru ya upweke, na ibada ya Allah, pamoja na hisia za uadilifu, haki na upole na silika za kazi na juhudi. Mbegu hizi huanza kuota kwa kujiendesha zenyewe moyoni mwa mwanadamu. Hata hivyo, maisha yake ya kijamii huleta mkengeuko moyoni mwake. Silika ya kazi na juhudi hulitwalia umbo la choyo na tamaa ya mali, huba ya ustawi na maisha hujitokeza katika umbo la choyo na tamaa ya kuikuza hali yake, na ile nuru ya upweke wa Allah na ibada yake hujit- walia vazi la ibada ya miungu wa uongo.
Katika hali hii, Wajumbe wa Allah humpatia mwanadamu nuru ya ufunuo na mpango wenye hali sahihi za ukuaji na maendeleo, na kuurekebisha uasi wa silika.

Kama ulivyoona, Amiri wa Waumini (a.s.) amesema: “Mwanzoni mwa uumbaji (wa huu ulimwengu) Muumba alichukua ahadi inayoitwa ‘ahadi ya viumbe’ au ‘Angano la viumbe na maumbile.’ Ni nini lengo la ahadi hii ya viumbe? Lengo lake ni kwamba Allah Mwenyezi, baada ya kuwapa wanadamu mamia ya silika zenye faida na kwa kuchanganya na utashi wao, korija za tabia njema ziliichukua ahadi ya kimaumbile kutoka kwao kwamba watazifuata silika na tabia njema. Kwa mfano, kumpa kwake mwanadamu macho, kuna maana ya aina fulani ya kuichukua ahadi yake kwamba hatatumbukia kisimani.

Hali kadhalika, kule kumpa hisia za kumtambua Allah, na ile ya kutenda uadilifu n.k ina maana ya kupata ahadi yake ya kwamba atakuwa mchamungu na mwaminifu. Kazi ya Mitume ni kwamba wawashauri wanadamu wayatende mambo yao kwa mujibu wa ushuhuda wa uhai na kulipasua pazia la bahati mbaya liwekwalo juu ya maumbile yake. Ni kutokana na sababu hii kwamba inasemekana ya kuwa msingi wa dini za kimbinguni unaundwa na mambo ya kimaumbile.

Unaweza kusema kwamba mwanadamu yu kama mlima wenye mawe ya thamani na chembe za dhahabu zilizojificha humo kama vile ambavyo wema, ujuzi, na maadili yamefichwa ndani ya maumbile ya mwadamu katika sura mbali mbali. Wakati Mitume na waaminio mizimu wanapouchunguza mlima wa moyo wetu kwa uangalifu sana wanaona kwamba umeungwa na idadi fulani ya sifa njema na fikara na hisia safi. Kisha wanaugeuza kwenye dharura ya maumbile kwa mafundisho na mipango yao. Wanaukumbusha maamrisho ya maumbile na dhamiri. Wanaulingania usikivu wa mwanadamu kwenye sifa njema za utu ulioji- ficha ndani mwake.

‘Mwaminifu’ Wa Waquraishi Akiwa Katika Mlima Hira

Mlima Hira uko Kaskazini mwa mji wa Makkahh na mtu anaweza kuki- fikia kilele chake katika muda wa nusu saa. Uso wa mlima huu una mabamba ya jiwe jeusi na hakuna dalili zozote za uhai zionekanazo mlimani humo. Katika sehemu yake ya kaskazini kuna pango liwezalo kufiki- wa na mwanadamu baada ya kuyapita mawe. Kimo chake ni kama kimo cha mwanadamu. Mwanga wa jua hupenya hadi kuifikia sehemu ya pango hili na sehemu yake iliyosalia daima huwa yenye giza.

Hata hivyo, pango hili lenyewe ni ushahidi wa matukio kama hayo ya kuhusu rafiki yake wa karibu kwamba hata katika siku hizi, watu huharak- isha kwenda huko kwa shauku kuu ili kuyasikia matukio haya kutokana na lugha yake ya kimya kimya na kukifikia kizingiti chake baada ya kuzipata taabu nyingi, na ili kuchunguza kutoka pango hili kuhusu taarifa za tukio la ufunuo, pamoja na kuhusu sehemu ya maisha ya yule mfadhili mkuu wa wanadamu. Na lile pango nalo linajibu kwa ile lugha yake ya kimya kimya; “Hii ndiyo maabadi (sehemu ya kuabudia) ya yule mheshimiwa wa Waquraishi.

Kabla ya kuianza kazi ya Utume alizitumia humu siku na mikesha mingi. Ameichagua sehemu hii iliyokuwa mbali na makelele, kwa ajili ya sala na ibada. Aliutumia mwezi mzima wa Ramadhani humu na kwenye nyakati nyinginezo alikimbilia katika sehemu hii kila mara.

Alifanya hivi mno kiasi kwamba mkewe mpenzi alijua kwamba asiporudi nyumbani atakuwa akijishughulisha na ibada kwenye mlima Hira. Na alipowatuma watu huko kwenda kumtazama walimkuta akitafakari na kusali kwenye sehemu hii.”
Kabla ya kuianza kazi ya Utume alikuwa na kawaida ya kutafakari sana juu ya mambo mawili:

1. Alichunguza kwa makini mfumo wa maumbile na sayari zenye kung’aa, uwezo na usanii wa Allah katika maumbile ya kila kiumbe chenye uhai.

2. Kwa kufanya uchunguzi wa kina zaidi juu ya anga na nyota na kuvifikiria kwa busara viumbe vyote vya duniani, basi kila siku alikuwa akilikaribia karibu zaidi lile lengo lake.

Alitafakari juu ya jukumu zito ambalo alijua kwamba atalibeba. Pamoja na ubovu na uoza wa jamii ya binadamu ya zama zile, hakuyafikiria mageuzi yake kuwa ni jambo lisilowezekana. Hata hivyo, utiliaji nguvu wa mpango wa kuitengeneza jamii nako hakukukosa matatizo na magumu yake. Hivyo basi, aliyatazama maisha yaliyochafuka ya watu wa Makkah na anasa za Waquraishi na akatafakari juu ya njia na jinsi ya ubadilishwaji wao.

Alishangazwa na watu kuabuduo masanamu yasiyo na uhai wala uwezo, na kuonyesha unyonge wao mbele yao na hapo dalili za kutokuwa na raha zilijidhihirisha usoni mwake. Hata hivyo, kwa vile alikuwa bado Hajaamrishwa kuielezea hali halisi, alijizuia kuielezea kwa watu wale.

Kuanza Kwa Ufunuo

Malaika mmoja aliteuliwa na Allah kumsomea ‘yule mwaminifu’ wa Waquraishi aya chache ikiwa ni mwanzo na utangulizi wa kitabu cha mwongozo na ustawi, hivyo basi, ili kumpa ‘mwaminifu’ heshima kwa kumpa vazi la Utume. Malaika Mkuu Jibril mwenyewe na ile siku yenyewe ilikuwa ni ile siku ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kuteuliwa kuishika kazi ya Utume. Tutazungumzia juu ya lengo la siku ile hapo baadae.

Hakuna shaka juu ya ukweli uliopo kwamba kumkabili malaika kunahitaji matayarisho maalum. Mpaka pale tu moyo wa mtu uwapo mkuu na wenye nguvu hataweza kuvumilia kukutana na Malaika.

Yule ‘Mwaminifu wa Waquraishi’ amejipatia matayarisho kama hayo kwa njia ya sala ndefu, kutafakari sana na baraka za Allah, kama ilivyoelezwa na waandishi wengi wa Sirah, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), hata kabla ya kuteuliwa kuianza kazi ya Utume, aliota ndoto zilizokuwa za dhahiri kabisa kama mwanga wa mchana. Baada ya muda fulani masaa yaliyokuwa ya kupendeza sana kwake yalikuwa yale ambayo ndani yake alisali akiwa katika hali ya kujitenga.

Alizipitisha siku zake katika hali hiyo hadi katika siku maalumu, Malaika alimwekea ubao wa maandishi karibu naye na kusema: “Soma” Na Mtume (s.a.w.w.) kutokana na ukweli kwamba hakujua kusoma na kuandika, na hakujifunza kusoma na kuandika, alijibu ya kwamba hajui kusoma. yule malaika Mkuu akambana kwa nguvu3 na kisha akamtaka asome. Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) alilirudisha jibu lilelile. Yule Malaika akambana tena kwa nguvu.
Kitendo hiki kilirudiwa mara tatu kwa ghafla alijihisi mwilini mwake kwamba anayaweza kuyasoma yale maandishi yake yaliyoko katika ule ubao ulioshikwa na yule Malaika. Hapo akazisoma aya zifuatazo ambazo kwa hakika huhesabiwa kuwa ni utangulizi wa kitabu cha ustawi wa mwanadamu.

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ {1}

خَلَقَ الْإِنْسَانَ مِنْ عَلَقٍ {2}

اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ {3}

الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ {4}

عَلَّمَ الْإِنْسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ {5}

“Soma kwa jina la Mola wako Aliyeumba (kila kitu). Alimuumba mwanadamu kutokana na tone la damu! Soma na Mola wako ni Mkarimu. Ambaye Alimfunza mwanadanmu kuandika kwa kalamu yale asiyoyajua.” (Surah al-Alaq, 96:1-5).

Malaika Mkuu Jibril akaimaliza kazi yake na baada ya ule ufunuo, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) naye akashuka kwenye mlima ule wa Hira na akaenda akiielekea nyumba ya Bibi Khadija.4

Aya tulizozinukuu hapo juu zaonyesha waziwazi mpango wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa maneno machache, na kusema kwa dhahiri kwamba msingi wa dini yake unapatikana kwa kusoma na kujifunza na hekima na matumizi ya kalamu.

Ulimwengu Kama Unavyoonekana Kwa Myakinifu

Maendeleo yanayoongezeka daima ya sayansi ya kawaida yamechukua kutoka kwa wanachuoni wengi ile nguvu ya kuingia ndani zaidi katika mambo ya kiroho yaliyo nje ya mipaka ya kalamu na sayansi ya kawaida na wamezizuia nuru zao. Wanadhania kwamba huu ulimwengu wa kimaada ndio ulimwengu pekee na chochote kile kisicho maada hakina faida yoyote. Kufuatana na maoni yao, chochote kile kisichoungana na kanuni za maada ni dhana tu na uongo.

Haina kupinga hapa kwamba wanasayansi hawa hawana ushahidi wowote juu ya kutokuwepo kwa ule ulimwengu mwingine ambao ndiko unakotoka ufunuo na msukumo. Yale wayasemayo tu ni haya: “Majaribio, maono na sayansi ya maumbile havituongozi kwenye jambo hili (yaani ule ulimwengu mwingine) na havitupi taarifa juu ya kuwako kwake. Kwa mfano, wanapokana kuwapo kwa roho itokayo, wanasema: “Kitu hicho hakionekani chini ya kisu cha uchambuzi wetu, na dalili za viumbe vya aina hii hazipatikani katika maabara yetu chini ya darubini na hivyo basi, kwa vile zana zetu za siku hizi hazituongozi kwenye vitu hivi si lazima kwamba viwe na uhai wa nje (ya huu wa duniani).”

Aina hii ya kufikiria ni pungufu, yenye ila na iliyochanganyika na upuuzi, ambayo ‘kutokuwepo’ kumeamuliwa au kuhesabiwa kuwa ni ‘kutokuwa na ufahamu’ na kwa vile zana walizonazo walimwengu hazifikishi kwenye hali halisi wanazoamini wale wanachuoni wamwaminio Allah, wao (wayakinifu) wanadhani kwamba zote hazina msingi.

Hakuna shaka juu ya ukweli kwamba wayakinifu hawajafaulu kuutambua ukweli wa yale wayasemayo wanachuoni wa kidini kuhusu kuwako kwa Muumba, achilia mbali vitu vingine vya kimetafizikia.

Na inajitokeza kwamba kama hayo makundi makuu mawili (wanasayansi na wanadini) yakifanya midahalo katika hali ifaaayo, iliyo huru kutokana na chuki na kiburi, umbali baina ya uyakinifu na Dini utatoweka upesi sana na zile tofauti zilizowagawa wanachuoni katika makundi mawili zitatoweka.

Wale wamwabuduo Allah wametoa sababu kadhaa kuhusu kuwako kwa Allah Mwenyezi na wamethibitisha ya kwamba hizi hizi sayansi za kimaumbile zimewaongoza kwa yule Aliye mjuzi wa yote na huu utarati- bu wa ajabu unaozitawala sehemu za ndani na za nje za viumbe vyote, ndani yake mna uthibitisho wa kuwapo kwa Muumba. Vitu vyote hapa ulimwenguni, tangu lile kundi la nyota liitwalo ‘Milky Way’ hadi chembehai (atom), vinasogea kwa kufuatana na nyororo ya sheria zenye utaratibu maalum na katu haiwezekani maumbile yasiyoona wala kusikia yawe ndio chanzo na kidumisho cha utaratibu wa ajabu kiasi hiki. Na ni haja hii ya ‘utaratibu mzuri wa ulimwengu’ iliyo msingi wa korija za vitabu na majarida yachapishwayo na wanachuoni wa kiislamu.

Na kwa vile hoja hii ni yenye kueleweka na iwezayo kutumiwa na matabaka mbalimbali, mengi ya maandishi ya maumbile ya vitu vyote yametengenezwa na hoja hii na kila mtu aitegemea katika njia moja au nyngine. Ama kuhusu zile hoja nyinginezo zisizokuwa za maumbile ya vitu vyote, jambo hili limejadiliwa kwa kirefu kwenye vitabu vya Kifalsafa na vya elimu nyingi. Vitabu hivi vina hoja na maelezo juu ya roho yenye kutoka kwa viumbe vyenye uhai. Tungalipenda kuvirejea katika mistari ya maneno ifuatayo:

1. Dhana Ya Roho

Itikadi juu ya ‘roho’ ni moja ya masuala yaliyo magumu na yenye kutatanisha yaliyovutia mazingira ya wanachuoni. Wale wapendao kuliweka kila jambo katika uchambuzi, wamekana kuwako kwa roho na wanaimani ile roho yenye sifa za kimwili na kufanya kazi chini ya utawala wa sheria za umbile.

Kuwako kwa nafsi isiyo na mwili wa dhahiri ni moja ya masuala yaliyochunguzwa kwa makini na wale wamwabuduo Allah Mwenyezi na wanayaamini mambo ya kiroho na wametoa thibitisho nyingi juu ya kuwako kwa viumbe visivyo na miili ya umbo la kuonekana ambavyo kama mtu atajifunza katika hali ya hewa ifaayo, iliyoandamana na maarifa kamili, na misingi ya hoja za Kimungu, husimama katika uthibitisho kamili.

Na yote yale yasemwayo na wanachuoni wa Kimungu juu ya Malaika, roho, ufunuo na Wahyi yanategemea hoja za nguvu na za kusadikika.5

2. Usingizi Wa Kisumaku (Uhiponozi)

Inawezekana kwamba wale wanaotaka kukielewa kila kitu kwa njia ya majaribio ya kivitendo na wanaweza kurejea kwenye maandiko mengi yaliyoandikwa juu ya jambo hili la usingizi wa kisumaku – kuchukuliwa kwa kiinimacho- (hypnotism). Mmoja wa mwanzilishi wa tawi hili la elimu alikuwa ni daktari wa Kijerumani aliyeitwa Mesmer. Ilikuwa ni karne mbili zilizopita alipoianzisha sanaa hii na kadiri muda unavyopita, maoni yake yanathibitishwa na wanachuoni. Aliwafunza baadhi ya watu kama hao kama walivyostahili kutegemeana na tabia na akili zao, wa kufanyiwa kiinimacho (kuwa kwenye hali inayofanana na kulala).

Alifanikiwa kuwabumbuaza, mbele ya wanachuoni wengi, watu walewale alioendeshea majaribio juu yao hapo awali. Alizitoa roho zao kutoka miilini mwao na kwa kuzipitia roho hizo alipata taarifa za matukio yaliyopita na yatakayotendeka baadae. Baada ya kupita karne mbili sanaa hii inapata ukamilifu wa polepole katika njia mbali mbali. Baada ya majaribio mengi, wanachuoni wameamua kama ifuatavyo:

Ukiachilia mbali ule uoni wa nje, mtu mwenye akili anao uoni wa ndani pia, na huu ni uoni ulio mpana zaidi ya ule wa nje.

Mtu awapo katika hali ya usingizi huwa akili zote mbili zaweza kusikia kutoka mbali, kuona kutoka nyuma ya pazia na kutoa taarifa kwa mukhtasari kuhusu matukio yajayo, matukio ambayo hayana dalili ya nje hata iliyo ndogo.

Kwa kutumia kanuni za usingizi huu wa kutengeneza inawezekana kutengeneza roho ya mtu kutoka mwilini mwake hadi kwamba roho hiyo ikaweza kuuona mwili mfu.

Ule utaratibu wa roho huwa na uhuru wa aina maalum.

Roho haikomi kuwako kutokana na kuoza na kutawanyika kwa sehemu mbali mbali za mwili.

Vile vile wanachuoni hawa wametoa uamuzi mwingine ufananao na huo. Hata kama tusiweze kuzikubali thibitisho hizo katika ukamilifu wao, mukhtasari wa majaribio haya yaliyoendeshwa katika kipindi cha karne mbili zilizopita na kushuhudiwa na wengi wa wataalamu wa nchi za Mashariki na za Magharibi; unathibitisha kuwako na ukweli na uhuru wa roho, na hilo ndilo lengo halisi la majadiliano haya. Wale wapendeleao wanaweza kuzisoma taarifa kamili za majadiliano haya katika vitabu vihusikavyo.

3. Msukumo Au Hisia Za Siri

Imani katika msukumo (wa akilini) ni msingi wa utume wa mitume yote na dini za kimbingu na huo (msukumo) umesimamia katika roho iliyotengwa yenye nguvu na uwezo wa kupokea elimu ya ki-Mungu iwe bila ya kuwapo mjumbe au kupitia kwa malaika. Wenye hekima wamesema hivi kuhusu msukumo: Msukumo una maana ya kwamba Allah Mwenyezi anawaonyesha njia halisi kwa mmoja wa aliowachagua na anampa maelekezo katika matawi mbali mbali ya elimu. Hata hivyo, jambo hili hufanyika kwa njia ya kimuujiza na isiyo ya kawaida.

4. Aina Za Wahyi

Kuhusiana na ukomo ulio na roho, inawasiliana na ulimwengu wa kiroho kwa njia mbali mbali. Hapa tunaandika maendeleo ya yale yaliyoelezwa juu ya jambo hili na yule kiongozi wa Uisilamu.6

Wakati mwingine mtu yule ahusikaye anapashwa habari za kweli za mbinguni kwa njia ya wahyi na kila njia ya msukumo na kila linalopendekezwa akilini mwake ni sawa na sayansi inayojishuhudia ambayo ndani yake hakuna shaka au wasiwasi unaoweza kuingizwa.

Anazisikia sentensi na maneno kutoka kwenye kitu chenye umbo la kuonekana (kama vile mlima au mti), kama vile tu Allah alivyozungumza na Nabii Musa (a.s.).

Hali halisi zinafunuliwa kwake wazi wazi katika namna ya ndoto.

Malaika anatumwa na Allah kufikisha amri maalum kwake. Qur’ani Tukufu ilifikishwa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa njia hii, kama vile isemavyo wazi wazi katika Surah al-Shu’ara, 26; 192-195:

“Ameiteremsha Roho (Jibril) mwaminifu juu ya moyo wako ili uwe miongoni mwa waonyaji kwa lugha ya kiarabu iliyo wazi-wazi.”

5 Visasili

Ili kwamba vizazi vijavyo viweze kufahamu mambo ya watu wa ulimwenguni kote, waandishi pamoja na marafiki na washirika wa watu hao wameandika kwa kadri ya uwezo wao matukio ya maishani mwao. Wameandika kwa wingi mno kiasi kwamba ili kuyakamilisha maandishi yao vile vile wanajibebea magumu ya safari. Historia haimjui mtu yeyote ambaye matukio ya maisha yake yangepaswa kuwa yameandikwa kama yale ya Mtukufu Mtume wa Uislam (s.a.w.w.) na ambaye marafiki na wanafunzi wangepaswa kuwa wameandika kila jambo la maisha yake kwa kirefu zaidi.

Hali kadhalika mfungamano wetu umetusaidia katika kuyahifadhi kwa kirefu matukio na maelezo ya maisha ya yule Mtume Mashuhuri wa Uislamu na kumekuwa chanzo cha pambo la kitabu cha maisha yake. Ukiachilia mbali maadui wenye hekima vile vile jambo hili hufanywa na marafiki wajinga. Hivyo basi, ni muhimu kwa mtu aandikaye wasifu wa maisha ya mtu maarufu kwamba achukue tahadhari katika kuyachambua maisha yake na katu asividharau vipimo vikali vya kihistoria katika kuyapima matukio. Sasa tunazijia dalili za tukio la wahyi.

6. Dalili Za Wahyi

Nafsi adhimu ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) iliangazwa na nuru ya wahyi (ufunuo). Alihifadhi moyoni mwake yale aliyoyasikia kutoka kwa Malaika (Jibriil). Baada ya tukio hili Malaika yule yule alizungumza naye hivi: “Ewe Muhammad! Wewe ni mjumbe wa Allah nami ni Jibriil!” Wakati mwingine inasemekana kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliyasikia maneno haya alipokuwa kishashuka kutoka kule mlimani Hira. Haya matukio mawili yalimwogofya na kumshtua kwa kiasi fulani. Sababu za hofu na mshtuko ni kutokana na jukumu kubwa alilopewa siku ile aliyouona ukweli aliokuwa akiutafuta kwa muda mrefu.

Hata hivyo, mshtuko huu wa akili, kwa kiasi fulani ulikuwa ni wa kawaida na haukuwa kinyume na itikadi yake juu ya ukweli aliofikishiwa. Licha ya ukweli kwamba alikuwa na uhakika kwamba yale aliyoyapata yalikuwa ni ujumbe wa Allah na yule aliyeyaleta alikuwa ni Jibriil, mshituko wake wote ulikuwa ni jambo la kawaida kwa kiasi fulani na halikuwa nje ya mpangilio.

Imekuwa hivyo kwa sababu kwa vyovyote vile nafsi ya mtu iwavyo na nguvu na kwa kadiri yoyote atakavyoweza kuhusiana na utaratibu wa ghaibu na ulimwengu wa kiroho, anapokabiliwa na Malaika kwa mara ya kwanza ambaye bado hajawahi kumwona kabla, na vile vile kwamba anamwona Malaika huyo kileleni mwa mlima, anawajibika kushikwa na mshtuko kama huu, na ndio maana mshituko huu ulitoweka baadae.

Mshituko wa akili na uchovu usio wa kawaida ulimfanya aende nyumbani kwa Bibi Khadijah. Alipoingia nyumba ile, mkewe mpenzi aliziona dalili za fikara nyingi na wasi wasi usoni mwake na akamwuliza kulikoni.
Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimsimulia Bibi Khadija yale yaliyotokea na vile vile akaiongezea ile sentensi isemayo “Nilijihisi kujiogopa mwenyewe.”7

Bibi Khadija alimtazama kwa heshima, akamwombea na kumfariji kwa kuzitaja baadhi ya sifa zake njema. Miongoni mwa mambo mengine alisema: “Umpole kwa jamaa zako, unaonyesha ukarimu kwa wageni wako na huogopi kuzikabili taabu katika njia iliyonyooka. Allah Atakusaidia.”

Kwa kuzitaja sifa hizi za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), bila shaka Bibi Khadija alidhamiria kumfanya mwenye matumaini zaidi kuhusu mafanikio yake na kumtia moyo kwa ajili ya kufanikisha lengo lake alilotumwa kulitimiza. Ukweli huu unaweza kuthibitishwa vema kutokana na yale aliyoyasema Bibi huyu.

Kisha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alijihisi kuchoka. Hivyo, alimgeukia Bibi Khadija na akasema: “Nifunike.” Bibi Khadija alimfunika na baada ya hapo upesi sana akapatwa na usingizi.

7. Bibi Khadija Aenda Kwa Waraqah Bin Nawfal

Tumekwisha mzungumzia Waraqah kwenye kurasa zilizopita na tumeeleza ya kwamba alikuwa mmoja wa wenye hekima wa Uarabuni. Ulikwishapita muda mrefu tangu auingie Ukristo baada ya kuisoma Injili na alikuwa ni mtu mwenye cheo kikuu katika jambo hilo. Alikuwa ni binamu yake Bibi Khadija. Mke mpenzi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), alimsimulia Waraqah aliyoyasikia kutoka kwa Mheshimiwa mumewe. Baada ya kuyasikiliza hayo, Waraqah alimjibu binamu yake akisema: “Binamu yako (yaani Mtume (s.a.w) yu mtu mkweli, na yale aliyokutana nayo ni mwanzo wa Utume na ameshukiwa na Jibriil……..”8

Matukio tuliyoyataja hapo juu yamenukuliwa kutoka kwenye maelezo ya kihistoria. Haya ndio mambo yaliyosimuliwa na mfululizo wa waandishi na yanapatikana katika vitabu vyote vya historia. Hata hivyo, katika mfululizo wa masimulizi haya, tunayakuta mambo yasiyoafikiana na vile vipimo vihusuvyo Mitume tulivyonavyo. Zaidi ya hayo hayalandani na yale matukio ya maisha ya yule mtu maarufu tuliyokwisha kujifunza kufikia hapa. Na yale tutakayoyaweka mbele yako hivi sasa hayana budi kuchukuliwa kama ni sehemu ya habari za uongo za historia au lazima ifafanuliwe zaidi.

Tunashangazwa mno na maandishi ya Dakta Haikal, mwanachuoni maarufu wa Misri, ambaye ingawa alitoa dibaji ndefu katika utangulizi wa kitabu chake ambacho ndani yake alisema kwamba kikundi cha watu wametia uongo katika mawaidha ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kutokana na uadui au huba, yeye mwenyewe naye ameandika mambo yasiyo sahihi kabisa, ingawa baadhi ya wanachuoni wa Kishi’ah, kama vile marehemu Tabarsi, ametoa tahadhari yenye manufaa juu ya jambo hili.9 Hapa tunazinukuu baadhi ya hizi hadithi za uongo (ingawa isingalikuwa muhimu kuzitaja kama wale marafiki wajinga au maadui wenye hila wasingaliziandika vitabuni mwao):

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipoingia nyumbani mwa Khadija alijifikiria kwamba inawezekana kwamba macho yake yalikosea au kwamba amekuwa mpiga bao!
Hata hivyo Khadija alimwondoshea wasiwasi wake kwa kusema kwamba alikuwa mwenye kuwasaidia yatima na mpole kwa jamaa zake! Hapo Mtukufu Mtume alimwangalia kwa shukurani mno na kumwomba amletee blanketi na amfunike.10

Tabari na wanahistoria wengine wameandika hivi: “Alipoyasikia maneno : “Wewe ni mjumbe wa Allah!” mwili wake mzima ulianza kutetemeka na akaamua kujitupa chini ya mlima. Hata hivyo, wakati ule yule Malaika ali- jidhihirisha na kumzuia asifanye hivyo.11

Baadaye Muhammad alikwenda kufanya ibada ya Tawafu kwenye Al- Ka’ba. Akiwa huko, alikutana na Waraqqah bin Nawfal, na akamsimulia habari zake. Waraqah akasema: “Naapa kwa jina la Allah! Wewe ni Mtume wa watu hawa na yule Malaika Mkuu aliyekuwa akimjia Musa, amekushukia. Baadhi ya watu wako watakataa kulikubali dai lako na watakufanyia madhara. Watakutoa mjini mwako na watakuwa vitani dhidi yako.” Muhammad alijihisi kwamba aliyoyasema Waraqah yalikuwa sahihi12

8. Ukosevu Wa Msingi Wa Kauli Hizi

Tunahisi kwamba hadithi zote hizi ni sehemu ya mpango wa Waisraeli na zimebuniwa na Wayahudi na kuingizwa kwenye historia na Tafsir (maele- zo ya Qur’ani tukufu).

Kwanza, ili kuweza kuzipima kauli hizi, hatuna budi kuzitazama wasifu za mitume walioitangulia. Qur’ani tukufu imezitaja shughuli zao, na maelezo yao marefu yamepokewa juu ya matukio ya maisha yao. Hata hivyo, hatuoni matukio mabaya yafananayo na hayo katika maisha ya yeyote kati yao. Qur’ani tukufu imesimulia kwa ukamilifu habari za mwanzo wa Wahyi kwa Nabii Musa (a.s.) na imeeleza wazi wazi mambo yote ya tukio hili. Hata hivyo, haikutaja jambo kama vile woga, kutetemeka, na mshtuko wa akili yake kwamba, alipoisikia sauti, alijiwa na kutaka kujitupa chini ya mlima. Kwa kuwa amesikia sauti kutoka mtini kwenye jangwa wakati wa usiku wa giza nene na hapo akaarifiwa kuhusu uteuzi wake kuishika ofisi ya Utume.

Kama ilivyoelezwa na Qur’ani tukufu, Nabii Musa (a.s.) alikuwa mtulivu kabisa wakati ule. Na Allah Mwenyezi alimtaka aitupe fimbo yake na ali- fanya hivyo mara moja, hofu yake ilikuwa tu juu ya ile fimbo, iliyogeuka kuwa mnyama wa hatari. Je, yaweza kusemwa kwamba Nabii Musa (a.s.) alikuwa mwenye amani na mtulivu wakati mkuu wa Mitume alikuwa ame- fadhaika sana alipoyasikia maneno ya Malaika, kiasi kwamba alitaka kuji- tupa chini ya kilele cha mlima? Je, lilikuwa ni jambo la hekima kusema hivyo?

Ni ukweli ukubalikao kwamba kwa kadiri nafsi ya mtu asivyokuwa tayari kwa hali yoyote kuzipokea siri za Mbinguni (yaani Utume) Mola, Mwingi wa rehema hamwinui mtu huyo kuishika kazi ya Utume, kwa sababu, lengo la kuwainua Mitume ni kwamba wawaongoze wanaadamu.

Mtu anawezaje kuwavutia watu wakati hisia za usalama wake na utulivu ni mchache mno kiasi kwamba anakuwa tayari kujiua kwa kuusikia Wahyi au unapokatika au kukoma. Wanachuoni wa ‘Kalaam’ (theolojia) wanakubaliana kwa pamoja kwamba Mtume anapaswa awe huru kutokana na vitu vyote vile viwavyo sababu ya watu kujitenga mbali naye. Katika hali hiyo je, tunaweza kuzikubali kauli hizi ambazo kwa vyovyote vile haziwezi kutumika kwa ajili ya kiongozi mkuu wa wanaadamu?

Pili, ilitokeaje kwamba kwa kuisikia sauti ya Mungu Nabii Musa alitosheka kabisa kwamba sauti ile ilitoka kwa Allah na mara moja alimwomba Allah kwamba ateuliwe Haruni ili awe mfuasi na msaidizi wake, kwa kuwa aliweza kuzungumza kwa ufasaha zaidi, lakini yule sayidi wa Mitume alisalia kuwa mwenye shaka kwa muda fulani hadi Waraqah alipoitoa shaka na kutokuwa na uamuzi huko kutoka akilini mwake?

Tatu, ni ukweli ukubalikao kwamba Waraqah alikuwa mkristo. Hata hivyo, alipotaka kuuondoa mshituko ule wa akili na kusitasita kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alitaja jina la Nabii Musa mwana wa Imrani tu; “Hiyo ndio kazi ile ile aliyoteuliwa Musa mwana wa Imrani kuishika.” 13

Je, jambo hili peke yake halithibitishi kwamba mkono wa wasimulizi wa kiisraeli umekuwa kazini na kwamba wameibuni hadithi hii bila ya kuzingatia dini ya shujaa wake (Waraqah).

Tukiyaachilia mbali yote hayo inaweza kusemwa kwamba mambo hayaafikiani hata kidogo na ukuu na ubora wa Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) tunaoutambua. Mwandishi wa kitabu ‘Hayat-i-Muhammad’ alitambua kwa kadiri fulani kuhusu kuzushwa kwa hadithi hizi. Hivyo basi, kwa sababu hii, wakati mwingine ameyanukuu mambo tuliyoyataja hapo juu kwa kutanguliza maneno: ‘kama isemekanavyo’

Marehemu Allamah Tabarsi, mwanachuoni mkuu wa Kishi’ah amefanya uadilifu katika mambo haya katika Tafsiri yake.14

Kwamaelezozaidi,basirejeayawezakufanywakwenyekitabukile.

 • 1. Jambo hili laweza kueleweka vizuri zaidi kutokana na aya ifuatayo ya Qur’ani tukufu:-“Watu wote walikuwa taifa moja; hivyo Allah akawainulia Manabii ili wawe wabashiri na waonyaji, na pamoja nao akateremsha kitabu na ukweli ili kihukumu baina ya watu katika yale waliyohitilafiana;….(Surah al- Baqarah, 2:213).
 • 2. Nahjul Balaghah, Hotuba 1.
 • 3. Baadhi ya wachambuzi hawaafiki wazo hili la Mtukufu Mtume kubanwa kwa nguvu na Jibril, hivyo wanaona kipengele kama hicho ni chumvi iliy- oongezwa na wanukuu wa historia. Kwani kiakili ni vigumu sana siku ya kwanza ya masomo mwalimu mwenye hekima kumfanyia kitendo kama hicho mwanafun- zi asiyejua kitu, ambaye yeye mwalimu ajua fika kwamba hajui chochote. Ukweli ni kwamba mawazo kama haya yahitaji uchambuzi wa ndani zaidi kimantiki na kihistoria. Na Allah ndiye Ajuaye – Mhariri.
 • 4. Siirah Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 236, na Sahih Bukhari, Juzuu 1, uk. 3.
 • 5. Maelezo kamili juu ya hoja hizi yanaweza kupatikana katika vitabu vya fal- safa chini ya kichwa cha habari cha: ‘Majadiliano juu ya jambo hili kwenye kitabu: A’sfaar’ cha Sadrul Muta’allihin.’
 • 6. Bihaarul Anwaar, Juzuu 18, uk. 193, 194,255 na 256.
 • 7. Tarikh-i-Tabari, Juzuu 2, uk. 205; Tarikh-i-Kamil Ibn Athir Juzuu 2, uk. 31.
 • 8. Inapasa kufahamika kuwa aliyekwenda kwa Waraqah si Mtukufu Mtume bali ni Khadija, na hii hailazimu kuwa naye Mtume alikwenda kuthibitisha utume wake kwake. Pia dhahiri ni kuwa Khadija hakwenda kwa Waraqa ili kutaka kuthibitisha utume wa Mtume (s.a.w.w.), bali alikwenda kwa lengo la kumpa habari juu ya hali halisi iliyompata mumewe – Mhariri.
 • 9. Majma’ul Bayaan, Juzuu 10, uk. 384.
 • 10. Tabaqaat-Ibn Sa’ad, Juzuu ya 1, uk. 289; Hayaati Muhammad, Juzuu 1, uk. 195.
 • 11. Tarikh-i-Tabari, Juzuu 2, uk. 205.
 • 12. Tafsir-i-Tabari, Juzuu 30, uk. 161, tafsiri ya Surah al- Alaq; na Siirah-i-Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 238.
 • 13. Siirah Ibn Hishamu, Juzuu 1, uk. 238. marehemu Allamah Majlis amenukuu katika kitabu Biharul Anwaar, Juzuu 18, uk. 228 na isa kutoka kwenye kitabu Bihaarul Anwaar, Juzuu 18, uk. 228, na Isa kutoka kwenye Sahih Bukhari na Siirah-i- ibn Hisham ambamo majadiliano haya yametegemezwa.
 • 14. Majma’ul Bayaan, Juzuu 1, uk. 384.