read

Sura Ya Kumi Na Nne:Kukoma Kwa Ufunuo

Roho ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) iliangazwa na nuru ya wahyi na aliendelea kutafakari na kuwaza juu ya jukumu lisilo kifani ambalo Mola Mwenyezi amempa akisema:

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ {1}

قُمْ فَأَنْذِرْ {2}

وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ {3}

“Ewe uliyejitanda shuka yako! Simama na uonye (watu). Na Mola wako umtukuze.”
(Surat al-Muddath’thir 74:1-3).

Vile vile alitegemea kuupata ujumbe mwingine kutoka kwa Mola wake, ili kwamba kwa kuzisikia aya hizi na maneno ya Allah, akili yake iweze kuangazwa zaidi na maamuzi na dhamira yake viweze kuwa thabiti zaidi. Hata hivyo zilipita siku na miezi, lakini yule Malaika wa Allah aliyekutana naye mle kwenye pango la Hira hakutokea tena na ile sauti isiyonekana iliyoifunulia roho yake haikusikika tena! Hatuifahamu sababu yake.

Yawezekana kwamba sababu ya kukoma kwa ule ufunuo ilikuwa kumpumzisha Mtume (s.a.w.w.), kwa sababu historia inasema kwamba daima ufunuo huandamani na shinikizo la kiroho lisilo la kawaida, hasa katika siku za awali za uteuzi wa Mtume kuishika kazi ya Utume, kwa sababu hadi katika muda ule, bado roho yake haijauzoea uoni wa kisiri wa kiasi kile. Tarehe ya kukoma kwa ule ufunuo pia nayo haifahamiki vizuri, lakini baada ya kuvisoma vitabu vya historian na Ahadithi tunaweza kuamua kwamba huu ufunuo ulikatwa kabla ya ubalighisho wa watu wote na hasa kule kuwabaghilishia ndugu wa karibu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Ilikuwa ni katika muda ambao Mtume (s.a.w.w.) bado Hajayapanua mahubiri yake hadi kuwafikia watu wote na kule kuwasiliana na watu binafsi kulikuwa bado hakujadumishwa. Hata hivyo, kama ilivyonukuliwa na marehemu Allamah Majlis1 kutoka kwenye kitabu ‘Manaaqib’ cha Ibn Shahr Aarhub, muda wa kukoma kwa ufunuo kulikuwa ni baada ya kuyapanua mahubiri yake hadi Mtume (s.a.w.w.) kuwahubiria Uislamu nduguze wa karibu. Hivyo basi, tunaweza kusema kwamba tukio hili lilitokea kati- ka mwaka wa nne tangu Mtume (s.a.w.w.) kuteuliwa kuishika kazi ya Utume, kwa kuwa kule kuwahubiria Uislamu nduguze kulifanyika baada ya miaka mitatu tangu kuanza kwa Utume wake.

Wako baadhi ya wanahistoria wenye maoni tofauti2 kuhusiana na jambo hili, ambayo hayakubaliani na ukweli uliothibiti wa waandishi wa wasifu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na mkewe mpenzi wanasema: “Pale ulipokatwa mkondo wa ufunuo, mchafuko wa akili na shaka iliyomkumba Mtume (s.a.w.w.) wakati wa kuanza kwa kazi ya utume ulifufuka upya, mkewe nae akapatwa na mshtuko na akamwambia: “Nadhania kwamba Allah amekata mawasiliano yake na wewe.”
Baada ya kuyasikia maneno hayo alirejea kule kwenye sehemu yake ya siku zote (Mlima Hira). Wakati ule ule ufunuo wa mbinguni ulikuja mara mbili na kuzungumza naye kwa maneno ya aya zifuatazo:

وَالضُّحَىٰ {1}

وَاللَّيْلِ إِذَا سَجَىٰ {2}

مَا وَدَّعَكَ رَبُّكَ وَمَا قَلَىٰ {3}

وَلَلْآخِرَةُ خَيْرٌ لَكَ مِنَ الْأُولَىٰ {4}

وَلَسَوْفَ يُعْطِيكَ رَبُّكَ فَتَرْضَىٰ {5}

أَلَمْ يَجِدْكَ يَتِيمًا فَآوَىٰ {6}

وَوَجَدَكَ ضَالًّا فَهَدَىٰ {7}

وَوَجَدَكَ عَائِلًا فَأَغْنَىٰ {8}

فَأَمَّا الْيَتِيمَ فَلَا تَقْهَرْ {9}

وَأَمَّا السَّائِلَ فَلَا تَنْهَرْ {10}

وَأَمَّا بِنِعْمَةِ رَبِّكَ فَحَدِّثْ {11}

“Naapa kwa mng’ao wa mchana na kwa usiku unapotia giza. Hakukuacha Mola wako, wala hakukukasirikia. Bila shaka mwisho ni bora zaidi kwako kuliko mwanzo. Na Mola wako hivi karibuni ataku- pa na utaridhika. Je, hakukuta ukiwa u yatima na akakuhifadhi? Na akakukuta ukihangaika Naye akakuongoza? Na akakukuta (ukiwa) masikini naye akakutajirisha? Basi usimkemee yatima, wala usimkaripie mwenye kuomba. Na neema ya Mola wako itangaze.” (Surat Adh-Dhuha, 93:1-11).

Kufunuliwa kwa aya hizi kulimpa furaha isiyo kifani na akatambua kwam- ba chochote kile kisemwacho na watu juu yake, hakikuwa na msingi wowote.

Maoni Yetu Juu Ya Jambo Hili

Hatuwezi kuyakubali masimulizi haya katika ukamilifu wake. Maisha ya Bibi Khadija na mazungumzo yake na mumewe pamoja na ukumbuko wake bado vimehifadhiwa katika historia. Ni huyu huyu Bibi Khadija aliyefanya kazi kwa juhudi zake zote katika siku za awali za ufunuo katika kuuondoa mshituko wa mumewe. Basi vipi sasa anaweza kuwa chanzo cha mshituko wake, wakati bado angali akiziona tabia na utu wema wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na alijua ya kwamba Allah, anayemwamini, alikuwa mwadilifu na mnyofu. Ndiyo! Tukiyaachilia mbali yoye haya, vipi aweza kujenga akilini mwake, mashaka ya ajabu juu ya Allah na Mtume wake?

Licha ya haya yote wanachuoni wameeleza katika vitabu vyao vya ‘Kalaam’ (theolojia) kwamba: “Baada ya kujipatia nyororo ya tabia njema zaidi zenye kumwainisha aliyenazo kutokana na wengineo, cheo cha Utume anakipewa mtu yule mwenye tabia bora zaidi na sifa maarufu, na kwa kadiri Mtume akosavyo kuwa na idadi fulani ua hizi tabia maarufu, na hazitimizi masharti maalumu, cheo hiki hakipewi kamwe.

Juu ya sifa zote hizi ni utakaso, amani ya kiakili, itikadi, na kumtawakali Allah, na kwa sababu Mtume anakuwanazo sifa hizi, fikara zake haziwezi kupotoka.” Wanachuoni wamesema: “Maendeleo ya polepole ya Mtume huanzia tangu utotoni mwake na pole pole elimu yake huifikia hatua ya ukamilifu. Haipiti akilini mwake shaka juu ya vitu avionavyo au avisikiavyo, japo iliyo ndogo kabisa. Zaidi ya hapo, maelezo ya mtu yeyote yule hayajengi shaka yoyote akilini mwa mtu mwenye cheo hiki.”

Aya za Qur’ani tukufu tulizozinukuu hapo juu, na hasa ile aya isemayo: “Hakukuacha Mola wako, wala hakukukasirikia.
Inaonyesha tu kwamba mtu fulani alimwambia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) maneno haya, lakini hayaonyeshi ni nani aliyeyasema na kama yalikuwa na athari gani nafsini mwake. Hata hivyo baadhi ya wafasiri (wa Qur’ani tukufu) wanasema kwamba maneno haya yalitamkwa na washirikina, na kutokana na uwezekano huu, aya zote hizi haziwezi kuhusiana na kuanza kwa ufunuo, kwa sababu hakuna yeyote miongoni mwao aliyeujua mwanzo wa Utume pamoja na kushuka kwa ufunuo ila Khadija na Ali, ili kwamba aweze kutoa lawama zake. Jambo hili lilikuwa hivi kiasi kwamba kama tutakavyoeleza baadae, ukweli wa Utume wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) haukufahamiwa na washirika kwa kipindi fulani cha miaka mitatu kamili na alikuwa Hajaamrishwa kuutangaza Utume wake kwa watu wote, hadi ilipofunuliwa aya isemayo:

فَاصْدَعْ بِمَا تُؤْمَرُ وَأَعْرِضْ عَنِ الْمُشْرِكِينَ {94}

“Basi yatangaze yale uliyoamrishwa,…..” (Surat al-Hijri, 15:94).

Hivyo basi, hadithi ya kukoma kwa ufunuo ina ushuhuda wa kihistoria na haina ushuhuda wa Qur’ani, na huo nao hauna sura ya kupinga bali una tabia tulioieleza mwanzoni mwa sura hii.

Mtukufu Mtume (S.A.W.W) Aliyaanza Mageuzi Kuanzia Kwenye

Mzunguko Mdogo

Watu wenye hekima na viongozi wa jamii huzungumzia juu ya mipango mikubwa mikubwa, lakini huzianza kazi zao kwenye eneo dogo, na mara tu baada ya kupata ushindi mara moja hufanya juhudi ya kuzipanua kazi zao na hulipanua eneo la kutendea kazi kulingana na ushindi wao, na kujitahidi katika maendeleo ya pole pole.

Mwenye hekima mmoja3 alimuuliza mmoja wa viongozi wa moja ya Mataifa makubwa ya siku hizi: “Ni ipi siri ya mafanikio yako kwenye mambo ya jamii?” Kiongozi yule alijibu akisema: “Njia ya fikara za watu wa Magharibi kama sie ni tofauti na zile zenu za watu wa Mashariki.

Daima tunaianza kazi kwa mpango mpana na uliofikiriwa vizuri lakini tunaianza kutoka kwenye sehemu ndogo na tunajaribu kuipanua baada ya kupata ushindi.

Na kama kwenye wakati ule tutagundua kuwa mpango ule si sahihi huiacha mara moja na kuanza kazi nyingine. Kwa upande mwingine, ninyi watu wa Mashariki hujitia kwenye kazi kwa mpango mpana na kuianza kazi hiyo kwenye sehemu kubwa na kuuweka mpango mzima kwenye vitendo, wote mara moja.

Na wakati wa kuitenda mkipatwa na tatizo, hamna njia yoyote ya kugeukia kulia ila kupata hasara kubwa. Zaidi ya hapo, ari yenu imekuwa katika hali ya kwamba daima mnafanya haraka na papara na daima mnataka kuyavuna mazao yenu siku ile ile ya kwanza. Mnatamani kuyapata matokeo ya mwisho katika siku za awali, na jambo hili lenyewe ni njia ya hatari sana ya fikara za kijamii ambayo hum- fanya mwanaadamu kuishia kwenye mvutano wa ajabu.

Tunafikiria kwamba njia hii ya fikara haihusiani ama na Mashariki au Magharibi. Daima watu wazima na wenye hekima na elimu huyafikia malengo yao kwa njia hii.
Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) vilevile aliyatenda mambo kwa mujibu wa kanuni hii ikubalikayo na aliibaghilisha dini yake kwa kipindi cha miaka mitatu kamili bila ya kufanya papara. Aliwafikishia dini wale aliowaona kuwa wanastahili na walioko tayari kwa mujibu wa mtazamo wa fikara na uwezo.

Ingawa lengo lake lilikuwa kuijenga jamii kubwa na iliyoenea kote duniani ili kwamba aweze kuwaleta watu wote chini ya athari ya bendera moja (bendera ya Upweke wa Allah) lakini kwenye kipindi hiki cha miaka mitatu, katu hakukimbilia kwenye ubalighisho kwa watu wote.

Alifanya mawasiliano maalumu tu na watu fulani fulani na kuwalingania kwenye dini yake watu wale aliowaona kuwa wanastahili, wanafaa na walio tayari kuipokea dini yake. Hatimae ni kwamba, kwenye kipindi hiki cha miaka mitatu alifaulu kuwaongoza watu wachache tu.

Katika kipindi hiki cha miaka mitatu machifu wa Waquraishi walikuwa wameleweshwa na utunzaji wa Ka’aba. Wakati Firauni wa Makkah (Abu Sufyani) na genge lake walipopata kuitambua asili ya wito na dai lake, walionyesha tabasamu la dhihaka midomoni mwao na wakaambiana: “Mwale wa mwito wake nao utakufa kama mwito wa Waraqah na Umayyah (waliouingia Ukristo kama matokeo ya kujifunza kwao Taurati na Injili na wakajifanya kuuhubiri Ukristo kwenye mikusanyiko ya Waarabu) na hautapita muda mrefu kabla yeye naye kujiunga na msafara wa wale waliosahaulika.”

Katika kipindi hiki cha miaka mitatu machifu wa Waquraishi hawakuchukua fursa yoyote na Mtukufu Mtume japo iliyo ndogo kabisa lakini daima walimheshimu. Yeye nae hakuwalaumu masanamu na miungu wao wazi wazi kwenye kipindi hiki bali akajishughulisha na kudumisha mawasiliano maalumu na watu wenye uoni wa dhahiri.

Hata hivyo, Waquraishi nao waliamka tangu mwenye ile hatua ya awali wakati ulipofanywa ule mwito maalumu kwa ndugu wa karibu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na ule mwito wa jumla kwa watu wote, na shutuma zake kwa masanamu na vitendo visivyo vya kiutu na tabia za Waquraishi vilianza kuzungumziwa.

Katika siku ile walitambua kwamba ilikuwako tofauti kubwa sana baina ya mwito wake na ile ya Waraqah na Umayyah. Hivyo basi ulianza upinzani na ushindani wa siri na wa dhahiri. Mwanzoni kabisa alivunja kimya chake mbele ya nduguze na baada ya hapo akautoa mwito wake kwa watu wote.

Hakuna shaka yoyote juu ya ukweli uliopo kwamba matengenezo yenye mizizi iliyozama ndani zaidi, yenye kuathiri maneno yote ya maisha ya mwanaadamu na kumbadili mwelekeo wa jamii, hasa huhitaji nguvu mbili imara – nguvu ya kauli na nguvu ya ulinzi.

Nguvu ya kauli ili kwamba mzungumzaji aweze kuelezea kweli fulani fulani kwa jinsi ivutiayo na aweze kuwavutia watu wote na aweze kuwafikishia watu mawazo yake mwenyewe au zile fikara apokeazo kutoka kwenye ulimwengu wa ufunuo.

Nguvu ya ulinzi ili kwamba itokeapo hatari aweze kuandaa safu ya ulinzi dhidi ya maadui wavamiao. Unapokosekana uwezo huu, mwali wa mwito wake, huzimika pale mwanzoni kabisa.

Nguvu ya kauli ya Mtume (s.a.w.w.) ilikuwa kamilifu ajabu na hakuna ukanusho wa ukweli kwamba alikuwa mzungumzaji mwenye mvuto aliyeweza kuieleza dini yake kwa ufasaha mkubwa.
Hata hivyo, kwenye siku za awali za mwito wake, hakuwa na ile nguvu ya pili, kwa sababu, kwenye hiki kipindi cha miaka mitatu, aliweza kuwasilimisha kiasi cha watu arobaini tu na ni dhahiri kwamba kipindi kidogo kiasi hiki kisingeweza kuchukua kazi ya ulinzi wake.

Hivyo basi, ili kuweza kujipatia safu ya ulinzi na ili kutayarisha kiini cha msingi, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliwalingania nduguze wa karibu zaidi kwenye dini yake kabla ya kufanya ulinganiaji wa jumla.

Kwa njia hii aliuondoa unyonge wa ile nguvu ya pili na aliweza kujenga ngome muhimu dhidi ya hatari yoyote ile iliyoweza kutokea. Kwa uchechefu mwito huu ulikuwa wenye faida kwa maana ya kwamba japo nduguze wasingalivutika na dini yake wangalisimama kumlinda kutokana na athari za kidugu na kikabila, hadi ulipowadia wakati ambapo mwito wake ulipowavutia baadhi ya machifu wa taifa hili na kulifanya kundi jingine kumwelekea.

Vile vile aliamini kwamba ule msingi wa mageuzi umesimamia kwenye mageuzi ya mwilini mwa mtu binafsi. Mpaka mtu aweze kuwazuia watoto na ndugu zake kutokana na matendo maovu, vinginevyo mwito aufik- ishao mtu huyu kwa watu wengine hauwezi kuwa na athari zozote, kwa sababu kwenye tukio kama hilo, wapinzani wanaojitumbukiza kwenye lawama, watamuonyesha tabia ya nguduze mwenyewe.

Kutokana na wazo hili, Allah anamwambia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuhusu kuwaita nduguze kwa maneno haya: “Na uwaonye jamaa zako wa karibu zaidi.” (Surah al-Shua’raa, 26:214) ambapo kuhusu ule mwito wa watu wote, Anasema: “Basi yatangaze yale uliyoamrishwa na ujitenge na washirikina, Nasi tutakuhami dhidi ya maadui.” (Surah al- Hijr, 15:94)

Jinsi Ya Kuwalingania Jamaa Wa Karibu

Njia aliyoitumia Mtukufu Mtume (s.a.w) katika kuwalingania jamaa zake wa karibu ilikuwa yenye kuvutia sana, na siri ya njia hii ya mwaliko huwa wazi kabisa baadae pale hali halisi inapodhihirika.

Karibuni wafasiri na wanahistoria wote, wakiitafsiri aya isemayo: “Na uwaonye jamaa zako wa karibuni zaidi” Wanaandika kwamba Allah Mwenyezi alimwamrisha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) awaite jamaa zake wa karibu kabisa kwenye dini yake. Baada ya kuchukua tahadhari muhimu Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimuagiza Ali bin Abi Twalib, ambaye wakati ule umri wake haukuzidi miaka kumi na mitano, kutayarisha mlo na kutayarisha maziwa pia kwenye mlo huo. Baada ya matayarisho hayo kukamilika, alialika wazee arobaini na watano kutoka miongoni mwa Bani Hashimu na vile vile aliamua kwenye tukio lile kuifichua ile siri iliyofichika.

Hata hivyo, kwa bahati mbaya ule mlo ulipomalizika, mmoja wa ami zake (Abu Lahabi), kabla Mtume (s.a.w.w.) Hajazungumza, alimtangulia kwa kusema mambo yasiyo na msingi na kuifanya hali ya hewa kutofaa kwa kubalighisha kazi ya utume.

Hivyo basi, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliona kuwa inafaa kuliahirisha jambo hilo hadi siku ijayo. Siku iliyofuatia alian- daa tena karamu. Baada ya mlo kwisha aliwageukia wazee wa familia yake na akayaanza mazungumzo yake kwa kumhimidi Allah na kuuhubiri Upweke Wake. Baada ya hapo alisema: “Hakika, kiongozo wa jamii katu hawadanganyi watu wake.
Ninaapa kwa jina la Allah, ambaye hakuna Mungu badala Yake, kwamba nimetumwa na Yeye kama Mjumbe Wake, hususan kwenu ninyi na kwa jumla kwa watu wote wa ulimwenguni humu.

‘Ndio! Enyi ndugu zangu! Mtafariki dunia kana kwamba mnalala na baada ya hapo mtarudishwa kwenye uhai tena na mtapokea malipo kufuatana na matendo yenu. Malipo haya ni pepo ya Allah ya milele (kwa wale waliokuwa wema) na Moto wake wa milele (kwa wale waovu).”

Kisha aliongezea kusema: “Hakuna mwanaadamu aliyepata kuwaletea watu wake kilicho chema zaidi ya kile nilichokuleteeni. Nimekuleteeni mibaraka ya ulimwengu huu na ule wa Akhera. Mola wangu ameniamrisha nikuitieni Kwake. Ni nani miongoni mwenu atakayeniunga mkono ili kwamba awe ndugu yangu?” Hotuba ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ilipofi- ka hapa, kilitawala kimya kamili juu ya mkutano wote na kila mmoja wa wale waliokuwapo pale alikuwa akifikiria juu ya ukuu wa lengo lile na hatima yake mwenyewe hapo baadae.

Mara kwa ghafla, Sayyidna Ali (a.s.) ambaye wakati ule alikuwa kijana wa umri wa miaka kumi na mitano, alivunja kimya kilichokuwa kimetawala mkutanoni pale. Alisimama na kusema kwa sauti ya nguvu: “Ewe Mtume wa Allah! Mimi niko tayari kukuunga mkono!” Mtume (s.a.w.w.) alimwamrisha akae. Akarudia maneneo tuliyoyetaja hapo juu mara tatu lakini hakuna yeyote aliyejibu ila yule kijana wa umri wa miaka kumi na mitano, ambaye alikuwa akitoa jibu lilelile.

Hapo Mtume (s.a.w.w.) aliwageukia jamaa zake na kusema: “Enyi watu! Kijana huyu ni ndugu yangu, wasii wangu na mrithi wangu miongoni mwenu. Yasikilizeni ayase- mayo na mfuateni.” Alipofikia hatua hii mkutano ulimalizika na wale waliokuwapo pale wal- imgeukia Bwana Abu Twalib kwa nyuso za tabasamu na kusema: “Muhammad amekutaka umfuate mwanao na kuzitii amri zake na amemtangaza kuwa mkuu wako.”4

Kilichoandikwa hapo juu ni kiini cha maelezo marefu yaliyonukuliwa na wafasiri na wanahistoria wengi kwa maneno tofauti tofauti ila Ibni Taymiyah mwenye maoni maalumu juu ya watu wa familia ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), hakuna yeyote aliyetia shaka juu ya usahihi wa Hadith hii na wote wameichukulia kuwa ni ukweli wa kihistoria usiokanika.

Uhalifu Na Kuvunja Uaminifu

Upotoshaji na kutafsiri vibaya mambo na kuzificha hali halisi ni jambo la dhahiri la uhalifu na kuvunja uaminifu; na wakati wa mkondo wa historia ya kiislamu limekuwapo kundi la waandishi wenye upendeleo walioifanya njia hii na kupunguza thamani ya maandiko yao kutokana na masingizio. Hata hivyo, mkondo wa historia na maendeleo ya elimu umewafichua. Ufuatao hapa chini ni mfano wa masingizio ya aina hii:

Kama ninyi wasomaji wetu mlivyoona, Muhammad bin Jarir Tabari (aliyefariki mnamo mwaka wa 310 Hijiriya) amelisimulia tukio la mwaliko wa jamaa wa karibu zaidi kwa kirefu kwenye kitabu chake cha historia. Hata hivyo, kwenye tafsiri yake,5 alipokuwa akiitafsiri aya isemayo: “Na uwaonye jamaa zako walio wa karibu zaidi.”

Anataja maneno aliyoyataja kwenye kitabu chake cha historia pamoja na maelezo na wanachuoni waliosimulia tukio hili, lakini anapoifikia sentensi isemayo “Ali yu ndugu yangu, wasii wangu na mrithi wangu.” Anaibadili sentensi hii na kusema “Ali yu ndugu yangu na kadhalika.” Na hakuna shaka na ukweli uliopo kwamba kuyaacha maneno: “wasii wangu na mrithi wangu” na kuweka maneno “na kadhalika” kuwa mbadala wao si chochote ila ni kuvunja uaminifu.

Hakutosheka na hilo tu lakini vile vile ameibadili sentensi ambayo yeye Mtume (s.a.w.w.) aliitamka kumhusu Sayyidna Ali (a.s.) (Huyu ni ndugu yangu na ni wasii wangu na mrithi wangu) na vile vile ameyatumia maneno yale yale “na kadhalika.”

Mwanahistoria hana budi kuwa huru na asiye na upendeleo katika kusimulia mambo na hana budi kuandika kile alichokichunguza na kukiona kuwa ni sahihi, kwa ushujaa usio kifani na uadilifu. Naweza kusema kwamba katu kilichofanya Tabari ayaache maneno haya mawili na kuweka mbadala wa maneno mawili ni ile chuki wake wa Kidini, kwa sababu hakumfikiria Sayyidna Ali (a.s.) kuwa makamu na mrithi wa mara moja wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Na kwa kuwa haya maneno mawili huonyesha dhahiri kwamba Sayyidna Ali (a.s.) alikuwa Wasii na mrithi wa mara moja, Tabari anaona kuwa ni muhimu kuuhami msimamo wake wa kidini pia, alipokuwa akifafanua juu ya tukio la ufunuo wa aya hii.

Ibn Kathir Shaami, aliyefariki dunia kwenye mwaka wa 732 Hijiriya nae ameipita njia hii kwenye kitabu chake cha historia6 aliyoipita Tabari kwenye siku za mwanzoni kwenye Tafsir yake. Hatuwezi kumsamehe Ibn Kathir kwa vyovyote vile, kwa sababu, Tarikh-i Tabari yenyewe ndio msingi wa Kitabu chake cha historia naye wazi wazi ameirejea Tarikh Tabari katika kuipanga sehemu hii ya kitabu chake, lakini ingawa alifanya hivi ameshindwa kulinukuu jambo hili kutoka kwenye kitabu cha historia tulichokitaja hapo, na kinyume na tegemeo letu amelitaja tukio hili kwa mujiubu wa Tafsiri Tabari.

Na tunauona uasi uliofanywa na Daktari Haykal, aliyekuwa Waziri wa Elimu wa Misri na mwandishi wa kitabu kiitwacho: “Hayaat-i Muhammad” aliyeifungua njia kwa ajili ya kizazi kipya kuuendea upotoshaji wa ukweli. Kidogo inashangaza kwamba inapokuwa kwamba kwenye dibaji ya kitabu chake ameyatumia maneno makali sana kwa wataalamu wa nchi za Mashatiki na kuwalaumu kwa upotoshaji wa mambo na uzushi, yeye mwenyewe analitenda kosa hili hili, kisha anaendelea mbele kidogo kwa sababu:

Kwanza: Kwenye toleo lake la kwanza la kitabu tulichokitaja, analinukuu tukio hili kwa njia ya pande mbili muhimu, yeye anaiandika sentensi moja tu (nayo ni Mtukufu Mtume s.a.w.w aliwageukia wazee na akasema:

Ni nani miongoni mwenu atakayeniunga mkono kwenye kazi hii ili awe ndugu yangu, wasii wangu na mrithi wangu?) lakini akaiacha kabisa ile sentensi nyingine ambayo Mtume (s.a.w.w.) alizungumzia Sayyidna Ali (a.s.) akiueleza uungaji mkono wake, na katu hakutaja kwamba Mtume (s.a.w.w.) alizungumzia akisema: “Enyi watu! Kijana huyu yu ndugu yangu, wasii wangu na mrithi wangu.”

Pili: Kwenye toleo la pili na la tatu aliendelea mbele hatua moja na akaziacha sentensi zote mbili kutoka kwenye zile sentensi mbili na hivyo akapiga pigo lisilo lengeka kwenye msimamo wake yeye mwenyewe pamoja na ule wa kitabu chake.

Utume Na Uimam Vimeungana

Kuutangaza urithi (Imamati) wa Sayyidna Ali (a.s.) siku za awali za utume wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kunaonyesha kwamba nafasi hizi mbili hazikutengana, na wakati Mtume wa Allah alipotangazwa mbele ya watu mrithi wake naye aliteuliwa na kutambulishwa kwa watu siku ile ile, na jambo hili lenyewe laonyesha kwamba Utume na Uimamu vimeungwa na hakuna umbali baina yao.

Kwa dhahiri shahiri kabisa tukio hili lathibitisha uhodari na ushujaa wa kiroho wa Imam Ali (a.s.), Amiri wa Waumini. Hii ni kwa sababu, kwenye mkutano ambao watu wenye uzoefu na wazee walizama kwenye tafakari na mshangao, yeye alitamka uungaji mkono wake na utii kwa uthabiti halisi na akaudhihirisha uadui wake kwa maadui wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) pasi na kuipita njia ya wanasiasa wanaojijali wenyewe. Ingawa wakati ule alikuwa kijana mdoga zaidi miongoni mwa wale waliokuwapo pale, kwa kadiri umri ulivyohusika, lakini ushirikiano wake na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa kipindi kirefu kwenye siku zilizopita, ulikuwa umeitayarisha akili yake kwa kupokea hali halisi ambazo wazee wa taifa lile walisitasita kuzikubali.

Abu Ja’far Askari amezungumza kwa ufasaha zaidi juu ya tukio hili. Wasomaji wanaweza kulirejea jambo hili lenyewe ndani ya Sharh-i Nahjul Balagha.7

  • 1. Bihaarul Anwaar, Juzuu 18, uk. 197.
  • 2. Tarikh-I Tabari, Juzu 1, uk. 48-52.
  • 3. Mmoja wa wafalme wa ukoo wa Qajaar alipotembelea London.
  • 4. Tarikh-i-Tabari, Juzuu 2, uk. 62-63; Tarikh-i Kamili, Juzuu 2, uk. 40-41; Musnad Ahmad bin Hanbal,
    Juzuu 1, uk. 111; na Sharh-i Nahjul Balaghah ya Ibn Abal Hadid, Juzuu 13, uk. 210-22.
  • 5. Tafsir-i Tabari, Juzuu 19, uk. 74.
  • 6. Al-Bidayah wan Nihaya, Juzuu 3, uk. 40.
  • 7. Sharh-i Nahjul Balaghah, cha Ibn Abil Hadid (toleo la Misri) Juzu 13, kuanzia ukurasa 215 na kuendelea.