read

Sura Ya Kumi Na Saba:Kuhama Kwa Mwanzo

Kuhama kwa kikundi cha Waislamu kwenda Ethiopia ni uthibitisho wa dhahiri wa imani na uaminifu wao wa kina zaidi. Wakiwa na lengo la kuyaambaa madhara na maovu ya Waquraishi na kupata mazingira yenye amani itakayoruhusu kuzitekeleza ibada za dini yao na kumwabudu Allah aliye Mmoja tu, waliamua kuutoka mji wa Makkah na kuuacha utajiri wao, biashara zao, watoto wao na ndugu zao.

Hata hivyo, hawakujua wafanye nini na waende wapi, kwa kuwa waliona kwamba ibada ya masanamu ilikuwapo kila mahali katika Penisula ya Uarabuni yote na hapakuwapo mahali popote ambapo jina la Allah lingaliweza kutamkwa kwa sauti kuu au sheria za kiislamu kutumiwa. Hivyo, wakaamua kuyapeleka maoni yao yale kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), ambaye msingi wa dini yake umesi- mama juu ya: “….. kwa hakika ardhi yangu ina wasaa, niabuduni Mimi tu.” (kwa kuchagua maskani yatakayokuruhusuni kumwabudu Allah Pekee)” (Surah al-Ankabut, 29:56).

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alitambua vizuri hali mbaya ya kuhuzunisha ya Waislamu. Ingawa yeye mwenyewe alipata msaada wa Bani Hashimu nao walimhami kutokana na kila aina ya madhara, wafuasi wake sana sana wao walitokana ni vijana wajakazi na watumwa na baadhi ya waungwana wasiokuwa na msaada wowote wa ulinzi. Wakuu wa Quraishi waliwatesa hawa watu wasiokuwa na msaada bila ya kukoma, na ili kuzuia vita za kik- abila, machifu wenye nguvu wa makabila mbali mbali waliwatesa watu wa makabila yao waliosilimu. Maelezo ya mateso na maonevu ambayo Waquraishi wamewatendea watu, tayari yameshaelezwa kwenye kurasa zilizotangulia.

Ni kwa sababu hii kwamba wale wafuasi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) walipomwomba ushauri kuhusiana na kuhama, aliwajibu akisema: “Kama mkisafiri kwenda Ethiopia, mtapata faida zaidi, kwa sababu ya kutokana na kuwapo mtawala mwenye nguvu na mwadilifu kule, hakuna yeyote ateswaye kule na ardhi ya nchi ile ni nzuri na safi na mnaweza kuishi pale hadi Allah Mwenyezi atakapokupeni auni.”1

Bila shaka mazingira yaliyo safi, ambapo mtu mwenye kufaa na mwadili- fu yu katika usukani wa mambo, ni mfano wa Pepo, na lengo pekee la wafuasi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika kuiendea nchi ile ni kwamba waweze kuzitekeleza ibada zao kwa usalama kamilifu na utulivu wa akili.

Kikundi Cha Kwanza Kwenda Ethiopia

Maneno ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) yenye kupenya yalikuwa na athari njema mno kiasi kwamba mara tu baada ya ushauri ule, wale waliokuwa tayari wamekwisha kujiandaa kabisa, waliifungasha mizigo yao na wakaenda Jiddah wakati wa usiku, imam wakiwa kwenye wanyama au wakienda kwa miguu bila ya maadui wao (waabudu masanamu) kutambua kule kuondoka kwao. Idadi kamili ya wale waliohama wakati huu ilikuwa kumi na walikuwamo pia wanawake wa kiislamu wanne.

Hapa inafaa kujua ni kwa nini Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) hakuzitaja sehe- mu nyingine. Hata hivyo, mtu akizichunguza zile hali zilizokuwapo Uarabuni na kwenye sehemu nyinginezo wakati ule, basi siri ya kuichagua Ethiopia itadhihirika kabisa. Sababu yake ilikuwa kwamba kuhamia kwenye sehemu zilizokuwa zikikaliwa na Waarabu, ambao kwa kawaida walikuwa wakiabudu masanamu ilikuwa ni hatari.
Wenye kuyaabudu masanamu hawakupenda kuwapokea Waislamu, imma kwa sababu walitaka kuwaridhisha Waquraishi au kwa sababu waliipenda mno dini ya jadi zao.

Sehemu za Uarabuni zilizokuwa zikikaliwa na Wakristo na Wayahudi hazikufaa hata kidogo kwa kuhamia, kwa sababu walikuwa wakipigana na kugombona wenyewe kwa wenyewe kwa ajili ya kupenyeza kwao kiroho, na haikuwapo nafasi kwa mshindani wa tatu. Zaidi ya hapo, vikundi hivi viwili viliwachukulia watu wenye asili ya kiarabu kuwa ni duni na waliotezwa.

Yemen ilikuwa chini ya maongozi ya Mfalme wa Iran na watawala wa Iran hawakuwa tayari hata kidogo kuwaweka Waislamu nchini mle, kiasi kwamba Khusro Pervez alipoipokea barua itokayo kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), mara moja alimwandikia barua Gavana wa Yemen kumkamata yule Nabii mpya na kumpeleka Iran. Hira, nayo ilikuwa chini ya utawala wa Iran kama vile ilivyokuwa Yemen; Sham ilikuwa mbali kutoka Makkah. Zaidi ya hapo, Yemen na Sham zilikuwa masoko ya Waquraishi na zilikuwa na uhusiano wa karibu zaidi na watu wa sehemu hizi.

Kama Waislamu wangalikimbilia huko, watu wale wangaliwafukuza kutokana na ombi la Waquraishi, waliokukwa wametoa ombi la aina hiyo hiyo kwa Mfalme wa Ethiopia ambaye alikataa kulitimiza.

Katika siku hizo, safari ya baharini, hasusan na wanawake na watoto ilikuwa ni kazi ngumu isiyo kifani. Kuichukua safari kama hii na kuzitelekeza njia za kupatia mahitaji ya maisha ilikuwa ni dalili ya utii kwa Allah na imani halisi. Jiddah (na kwa mujibu wa kauli ya Jurji Zaydaan’ bandari ya Shuaibiyah ya siku hizo) ilikuwa ni bandari ya kibiashara iliyoendelea, na kwa bahati, meli mbili za kibiashara zilikuwa tayari kung’oa nanga kutoka pale kwenda Ethiopia.

Wale Waislamu, wakichelea kufuatwa na Waquraishi, walilidhihirisha lengo lao na kuichukulia safari ile na waliipanda meli hiyo kwa haraka mno, kwa malipo ya nusu dinar. Taarifa inay- ohusu kule kuondoka kwa Waislamu vile vile iliyafikia masikio ya machi- fu wa Makkah na wakawatuma watu kwenda kuwarudisha, lakini walipofika kule bandarini, ile meli ilikuwa tayari ishaondoka pwani ya Jiddah nayo haikuweza kuonekana.

Kuwafuata wale waliochukua hifadhi kwenye nchi ya kigeni kwa ajili tu ya usalama wa imani yao, ni uthibitisho wa dhahiri wa uovu wa Waquraishi. Wahamaji hawa wamezitelekeza mali zao, watoto wao, makazi yao, na kazi zao lakini machifu wa Makkah hawakuwa tayari kuwaacha. Wazee wa ‘Dar-un Nadwah’ waliyachelea matokeo ya safari ile na wakalijadili jambo hili miongoni mwao, na majadiliano haya tutayaeleza baadae.

Watu wa kikundi hiki hawakuwa wa familia moja, na kwa mujibu wa kauli ya Ibn Hishamu2 kila mmoja wa hawa watu kumi alikuwa wa familia tofauti.

Kikundi Cha Pili Kwenda Ethiopia

Uhamaji mwingine ulifanyika baada ya huu wa kwanza na kiongozi wa msafara wa wahamaji wa kikundi cha pili alikuwa ni Bwana Ja’far bin Abu Twalib. Uhamaji huu ulitayarishwa kwa uhuru kamili na hivyo basi, baadhi ya wahamaji walifaulu kuwachukua wanawake wao na watoto pamoja nao.
Matokeo yake yakawa kwamba idadi ya Waislamu nchini Ethiopiua ilifikia themanini na watatu, na kama tukiwahesabu watoto waliochukuli- wa kule au waliozaliwa nchini mle, idadi yao itazidi hii.

Kama alivyoeleza Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) Waislamu waliiona nchi ya Ethiopia kuwa ni nchi yenye kustawi na hali ya hewa tulivu na huru. Bibi Ummi Salama, mkewe Abi Salama, ambaye baadaye aliipata heshima ya kuolewa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) anasema hivi kuhusiana na nchi ile: “Tulipokaa Ethiopia tulijiona kuwa tuko chini ya ulinzi wa mlinzi aliye bora zaidi. Hatukupata taabu yoyote ile au kulisikia neno baya lolote kuto- ka kwa yeyote yule.”

Kutoka kwenye beti za mashairi zilizotungwa na baadhi ya wahamaji hawa, inabainika kwamba hali ya hewa ya Ethiopia ilipendeza mno. Maelezo kwa kirefu yanaweza kuonekana kwenye Siirah-i Ibn Hisham.3

Waquraishi Wapeleka Wajumbe Wao Kwenye Baraza La Ethiopia

Machifu wa Makkah walipopata taarifa juu ya uhuru na maisha ya amani ya Waislamu kule Ethiopia, miali ya chuki iliwaka nyoyoni mwao, wali- ingiwa na wasiwasi kutokana na maisha ya furaha waliyokuwa wakiishi huko, kwa kuwa nchi ile ilithibitika kuwa pepo kwa ajili yao. Waliogopa mno isije ikawa kwamba Waislamu wakapata kuwa karibu na Negus (Mtawala wa Ethiopia) na wakaweza kumvutia kwenye ile dini ya Uislamu na hivyo wakatayarisha kuivamia Penisula ya Uarabuni wakiwa na jeshi lililoandaliwa vizuri.

Wazee wa ‘Darun Nadwah’ walikutana tena na wakaamua kwa pamoja kuwapeleka wajumbe kwenye mahakama ya Ethiopia na kutayarisha zawadi zifaazo kwa ajili ya Mfalme na mawaziri wake ili kuipata hisani yao, na kisha kuwashtaki Waislamu wahamiaji hao kwa upumbavu na ujinga na kuzusha dini.

Ili mpango wao huo uweze kupata ushindi wa haraka waliwachagua watu wawili kutoka miongoni mwao wafahamikao kwa hila na vitendo vyao vya kuidanganyifu. Hapo baadae mmoja wao akaja kuwa mzinguaji katika nyanja ya siasa. Kura ziliwaangukia ‘Amr bin Aas na Abdullah bin Rabi’ah. Raisi wa ‘Darun Nadwah’ aliwapa maagizo kwamba kabla ya kukutana na yule Mtawala wa Ethiopia kwanza waanze kuwapa zawadi wale mawaziri na kufanya mazungumzo nao kabla ya kumwona Mfalme na wajaribu kuwavutia kwao, ili kwamba watakapokutana na Mfalme, wao (mawaziri) waweze kuwaunga mkono. Baada ya kupewa maelezo mafupi juu ya jambo hilo, wale watu wawili waliondoka kwenda Ethiopia.

Wale mawaziri wa Ethiopia walikutana na wale wajumbe wa Waquraishi na wale wajumbe baada ya kutoa zile zawadi, walizungumza nao hivi: “Kikundi cha vijana wetu kimeyakana mafundisho ya jadi zao na wameizungusha dini iliyo kinyume na dini yetu na ile yenu. Hivi sasa wanaishi nchini mwenu. Wazee na machifu wa Waquraishi, kwa nia njema wanamwomba Mtukufu Mfalme wa Ethiopia kuwafukuza upesi iwezekanavyo.

Vile vile tunapenda kwamba baraza la mawaziri lituunge mkono mbele ya Mfalme. Na kwa vile tunautambua vizuri upungufu na njia na tabia za watu hawa, ingalifaa kwamba jambo hili lisijadiliwe kabisa pamoja nao, na kiongozi wa nchi hii vile vile asiwape nafasi ya kusikilizwa!”
Wale watu wenye choyo na wasioona mbali (yaani wale mawaziri) wali- wahakikishia uungaji mkono wao kamili. Siku iliyofuata wale wajumbe wa Waquraishi walikaribishwa kwenye Baraza la Kifalme na baada ya kutoa salaam zao na kuwakilisha ujumbe zawadi zao waliwasilisha ujumbe wao kwa yule Mfalme kwa maneno haya: “Ee Jalali Mtawala wa Ethiopia! Baadhi ya vijana wetu walio wapumbavu wamechukua hatua ya kuhubiri dini isiyoafikiana na dini rasmi ya nchi yako wala ile ya jadi zao. Hivi karibuni watu hawa wamekimbilia nchini mwako na wanapata faida visivyostahili kutokana na uhuru ulioko nchini humu. Wazee wa Waquraishi, kwa dhati kabisa, wanakuomba Jalali Mfalme, kwamba itolewe amri ya kuwafukuza ili waweze kurudi nchini mwao. . . .”

Mara tu baada ya hotuba ya wajumbe wa Waquraishi kuisha, sauti za mawaziri, waliokuwa wamekizunguuka kiti cha enzi cha mfalme, zilipaa. Wote waliwaunga mkono wale wajumbe wa Waquraishi na wakayathibitisha yale waliyoyasema. Hata hivyo, dalili za hasira zilijidhihirisha usoni mwa yule Mtawala mwenye hekima na mwadilifu wa Ethiopia. Akiwapinga wajumbe wa baraza lake aliunguruma, akisema: “Hili haliwezekani! Siwezi kuwakabidhi watu hawa wawili wale watu waliokimbilia nchini mwangu bila ya kufanya uchunguzi ufaao. Ni muhimu kwamba hali na mambo yote ya wakimbizi hawa lazima vitazamwe.

Nami nitawarudisha kwao baada tu ya maelezo ya watu hawa wawili juu yao kuwa yamethibitishwa kutokana na uchunguzi. Kwa upande mwingine, kama yaliyosemwa na hawa watu wawili juu yao hayatokuwa kwenye msingi wa ukweli halisi, basi sitawatelekeza, bali nitawapa msaada zaidi!”

Baada ya hapo mjumbe maalumu wa baraza la mfalme alitumwa kwa hawa Waislamu wahamiaji nae akawaleta mbele ya Mfalme bila ya kuwapa taarifa za kabla. Bwana Ja’far bin Abi Twalib alitambulishwa kuwa ndiye mwakilishi wa Waislamu hawa. Baadhi ya Waislamu walikuwa na wasiwasi kuhusu jinsi atakavyozungumza na yule mtawala wa Kikristo wa Ethiopia. Ili kuwatoa wasiwasi, Bwana Ja’far aliwaeleza ya kwamba atazungumza na Mfalme yule sawa kabisa na vile alivyosikia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akisema.

Mfalme wa Ethiopia alimgeukia Bwana Ja’far akasema: “Kwa nini mmeyakana mafundisho ya jadi zenu na kuifuata dini isiyoafikiana na dini yetu wala ile ya jadi zenu?”
Bwana Jafar akamjibu yule Mfalme, akisema: “Tulikuwa watu wajinga na tulikuwa tukiyaabudu masanamu. Hatukuacha kula mizoga. Daima tulijitia kwenye vitendo viovu. Hatukuwaheshimu jirani zetu. Wale waliokuwa wanyonge na wasiokuwa na msaada miongo- ni mwetu walionewa na waliokuwa na nguvu.

Tuligombana na kupigana na ndugu zetu, tuliutumia muda mrefu sana katika njia hii hadi mtu mmoja kutoka miongoni mwetu, aliyekuwa na maisha ya kabla ya hapo yaliyokuwa angavu mno na safi, aliamka na kutuita, kwa amri ya Allah, kumwabudu Mungu Mmoja na wa Pekee na akatukataza kuwahimidi masanamu kuwa ni jambo baya. Vile vile ametuamrisha kuvirudisha vitu vya watu vilivyowekwa dhamana kwetu, kuyaacha maovu, kuwatendea wema ndugu na majirani zetu, na kuacha umwagaji wa damu, kushughulika na mambo haramu, kutoa ushahidi wa uongo, kunyakua mali ya mayatima na kuwasingizia wanawake mambo mabaya.

“Ametuamrisha kusali, kufunga, na kulipa kodi kutokana na utajiri wetu (zaka). Tumemwamini na tukajishughulisha na kumhimidi na kumwabudu Allah, Mmoja tu. Tunaamini kuwa kile alichokitangaza kuwa halali, kuwa ni halali kweli. Hata hivyo, Waquraishi wamekuwa wakitutendea ukatili na wametutesa mchana na usiku ili kwamba tuikane dini yetu; na turejee kwenye ibada ya mawe na masanamu na kutenda kila aina za matendo maovu. Tumewapinga kwa muda mrefu hadi nguvu yetu ikamalizika. Tukiwa tumekata tamaa juu ya maisha yetu na mali zetu tumekimbilia Ethiopia ili kuiokoa dini yetu. Sifa njema za uadilifu wa Mtawala wa Ethiopia zimetuvutia kama sumaku, na vile vile, hivi sasa tunayo imani kamili juu ya uadilifu wake.”4

Hotuba ya Bwana Ja’far yenye mvuto na ya kusisimua, ilimvutia mno yule Mfalme, kiasi kwamba yeye Mfalme, akichuruzikwa na machozi machoni mwake, alimwambia Bwana Ja’far: “Hebu soma chochote kile kutoka kwenye Kitabu cha Mbinguni cha Mtume wenu.”

Bwana Ja’far akasoma aya kadhaa kutoka Surat Maryam. Aliendelea kuzisoma aya hizo na akalieleza lengo la Uislamu kwa ukamilifu juu ya usafi wa Bibi Maryam na cheo cha juu cha Nabii Isa (a.s.). Alikuwa bado hajaimalizia Sura ile wakati yule Mfalme na maaskofu walipoanza kulia kwa sauti kuu na ndevu zao pamoja na kurasa za vitabu vilivyofunuliwa mbele yao vikalowa machozi yao!

Baada ya hili, kwa muda fulani hivi kilitawala kimya barazani mle na mvumo ulikoma. Kisha Mfalme akaingilia na kusema: “Maneno ya Mtume wao na yale aliyoyaleta Nabii Isa yametoka kwenye chanzo cha nuru kimoja na kilekile. Nendeni zenu. Sitawakabidhi kwenu katu!”

Kinyume na vile mawaziri na wale wajumbe wa Waquraishi walivyotegemea, mkutano ulimalizika kwa hali ngumu upande wao na haukuwapo mwali wowote wa matumaini uliosalia!

‘Amr bin Aas’ aliyekuwa mjumbe na mtu mwerevu, alifanya mazungumzo na yule mwenzie Abdallah bin Rabi’ah na akamwambia: “Ni bora kesho tuitumie njia nyingine na inawezekana kwamba njia hiyo ikamalizika katika maangamizo ya wahamiaji hawa. Kesho nitamwambia Mfalme wa Ethiopia kwamba kiongozi wa wakimbizi hawa anayo itikadi maalumu juu ya Nabii Isa isiyoafikiana hata kidogo na mafundisho ya Ukristo.”

Abdullah alimkataza asifanye hivyo na akamweleza ya kwamba miongoni mwa wakimbizi wale walikuwapo watu walio ndugu zao. Hata hivyo, ushauri wake haukufaulu. Siku iliyofuata walikwenda kwenye lile baraza la Mfalme pamoja na mawaziri wote. Mara hii walijifanya kwamba ni wenye huruma na kuiunga mkono dini rasmi ya Ethiopia na kuzilaumu itikadi za Waislamu juu ya Nabii Isa na wakasema: “Watu hawa wana itikadi maalumu juu ya Isa zisizoafikiana hata kidogo na mafundisho na itikadi za ulimwengu wa Kikristo na kuwako kwa watu kama hawa ni hatari kwa dini rasmi ya nchi yenu. Ingalifaa kwako wewe Jalali Mfalme, kuulizia jambo hili kutoka kwao.”

Wakati huu yule Mtawala wa Ethiopia mwenye hekima aliamua kulichunguza jambo lile pia na akaamrisha kwamba wale wahamiaji waletwe mbele yake. Wale Waislamu waliifikiria tena sababu ya kuitwa kwao tena. Ilionekana kana kwamba imefunuliwa kwao kwa mzinduo sahihi kwamba lengo la kuitwa kwao lilikuwa kuulizia kuhusu itikadi yao juu ya mwasisi wa Ukristo. Bwana Ja’far akatajwa tena kuwa ndiye mzungumzaji wao.

Ja’far alikuwa tayari kaisha waahidi marafiki zake ya kwamba atazungumza tu yale mambo ya habari ile aliyoisikia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Negus alimgeukia yule mjumbe wa wakimbizi na akasema: “Nini itikadi yenu juu ya Nabii Isa?”

Bwana Ja’far akajibu akasema: “Itikadi yetu juu ya Isa ni ile tuliyofundishwa na Mtukufu Mtume wetu. Alikuwa mja na Mtume wa Allah. Alikuwa Roho na Neno la Allah ambalo kwalo Alimbariki Maryam.”

Mfalme wa Ethiopia alifurahi mno kuyasikia maelezo ya Bwana Ja’far, na akasema: “Ninaapa kwa jina la Allah! Isa hakuwa na cheo cha juu zaidi ya hiki!” Wale mawaziri na watu waliopotoka hawakuupenda haya maoni ya Mfalme. Hata hivyo, licha ya maoni yao hayo, Mfalme alizisifu itikadi za Waislamu na akawapatia uhuru kamili! Akazitupilia mbali zile zawadi za Waquraishi mbele ya wajumbe wao na akasema: “Mungu hakuchukua hongo yoyote kutoka kwangu aliponipa mamlaka haya. Hivyo basi, haifai kwamba mimi nilimbikize utajiri kwa njia kama hii!”5

Kurejea Kutoka Ethiopia

Baadhi ya watu waliohamia Ethiopia waliitoka nchi ile na kurudi Hijaz kutokana na taarifa za uongo kwamba Waquraishi wamesilimu. Waliporejea walitambua ya kwamba taarifa walizozipokea zilikuwa za uongo na shinikizo na maonevu juu ya Waislamu yalikuwa bado haya- jakomeshwa. Hivyo basi, wengi wao walirudi Ethiopia na ni wachache wao tu waliouingia mji wa Makkah, imma kwa siri au kwa kuwa chini ya ulinzi wa Quraishi mwenye nguvu.

Uthman bin Maz’un aliingia Makkah chini ya ulinzi wa Walid bin Mughayrah6 na akasalimika kutokana na ukatili wa adui. Hata hivyo, aliweza kuona kwa macho yake mwenyewe kwamba Waislamu wengine walikuwa wakionewa na kuteswa na Waquraishi. Uthman alihuzunika sana kuuona ubaguzi huu. Hivyo basi, alimwomba Walid atangaze hadharani kwamba mwana wa Maz’un hayuko tena chini ya ulinzi wake, ili kwamba yeye nae aweze kuwa mwenye hali ile ile walimo Waislamu wengine, na ashirikiane nao kwenye huzuni na masikitiko yao. Hivyo Walid akatangaza msikitini akisema:

“Kuanzia muda huu Ibn Maz’un na hayuko chini ya ulinzi wangu.” Na Uthman nae akasema kwa sauti kuu: “Nathibitisha hivyo.” Mara tu baada ya hapo, Labid, mshairi wa Uarabuni aliingia msikitini na kuanza kuisoma Qaswida yake maarufu mbele ya ule mkusanyiko mkubwa wa Waquraishi.

Alisema: “Kila kitu si chenye uhakika na ni chenye kuidanganya akili, isipokuwa Allah tu.” Uthman akasema: “Umesema kweli.” Hapo Labid akaisoma sehemu ya pili ya ule mstari wa ubeti. “Baraka zote za Allah ni zenye kugeukageuka.” Uthman akaingiwa na wasiwasi na akasema: “Umekosea. Mibaraka ya Ahera ni yenye kudumu na ya milele.”
Labid aliuchukulia vibaya mkanusho wa Uthman na akasema: “Enyi Waquraishi! Hali yenu imebadilika.

Hapo kale mikutano yenu ilikuwa na mipangilio mizuri na wafuasi wenu hawakuhuzunika. Ni tangu lini hali yenu ikabadilika? Ni nani huyu?” Mmoja wa wale waliokuwapo pale akasema: “Yeye yu mpumbavu aliyeikana dini yetu na kumfuata mtu aliye kama yeye. Usiyasikilize maneno yake.” Kisha yule mtu aliamka na kumpiga Uthman kofi la nguvu usoni mwake hadi ukageuka kuwa mweusi (kwa kuvilia damu).

Walid bin Mughayrah akasema: “Ewe Uthman! Ungelisalia kwenye ulinzi wangu yasingalikupata yote haya.”
Uthman akamjibu akasema: “Mimi niko chini ya ulinzi wa Allah Mwenyezi!” Walid akasema: “Niko tayari kukupa ulinzi tena.” Uthman akamjibu akasema: “Sitaukubali hata kidogo.”7

Ujumbe Wa Wakristo

Matokeo ya kuhubiri Uislamu kulikofanywa na wahamiaji yalikuwa kwamba, ujumbe wa kuuliza juu ya Uislamu ulitembelea Makkah kwa niaba ya kituo cha kidini cha Wakristo wa nchini Ethiopia. Walikutana na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) msikitini na wakamwuliza maswali fulani. Mtume (s.a.w.w.) alijaribu kujibu maswali yao kisha akawaomba wasilimu na akawasomea baadhi ya aya fulani fulani za Qur’ani tukufu.

Hizi aya za Qur’ani zilizibadili akili zao katika hali ambayo walianza kutiririkwa na machozi kutoka machoni mwao bila ya kukusudia na wakauamini Utume wake mara moja, na wakazithibitisha dalili zote za yule Mtume aliyeahidiwa ambaye bishara zake wamezisoma kwenye Injili.

Abu Jahl aliuchukia mkutano huu wenye shauku na uliomalizika kwa mafanikio. Kwa ukali mwingi, aliwaambia wajumbe wale: “Watu wa Ethiopia wamekutumeni katika ujumbe wa uchunguzi na haikuwa nia ya watu wale kwamba muikane dini ya jadi zenu. Mimi sidhani kwamba wako watu wapumbavu zaidi yenu kwenye uso wa ardhi hii.”

Wale watu waliyatamka maneno ya upatanishi katika kumjibu huyu Firauni wa Makkah, aliyetaka kuificha miali ya jua yenye kutia nguvu, kama vile lifanyavyo wingu jeusi na hivyo wakaukomesha ugomvi ule.8

Ujumbe Wa Waquraishi

Ujumbe wa watu wa Ethiopia ulikuwa njia ya kuwaamshia Waquraishi na wao nao wakaamua kufanya utafiti. Kikundi cha watu wakiwamo Harith bin Nasr na ‘Uqbah bin Abi Mu’it walikwenda Yathrib (Madina) wakiwa ni wajumbe wa waquraishi kwa lengo la kwenda kuuliza maswali juu ya Utume na ‘mwito’ wa Muhammad kwa Wayahudi. Wanachuoni wa Kiyahudi waliwashauri wajumbe wale kwenda kumwuliza Mtume Muhammad (s.a.w.w.) maswali yafuatayo:- Ni nini uhakika wa roho?

Hadith ya watu waliotoweka kwenye siku za kale (watu wa pango). Ujasiri wa yule mtu aliyesafiri upande wa Mashariki na upande wa Magharibi wa ulimwengu (Dhulqarnayn).

Waliwaambia wajumbe hawa kwamba, kama Muhammad ataweza kuyajibu maswali haya, hawana budi kuwa na uhakika kwamba yu mteule wa Allah, lakini kama akishindwa kutoa majibu yaliyohitajika, hawana budi kumchukulia kwamba yu muongo astahiliye kuondoshelewa mbali upesi iwezekanavyo.

Wajumbe wale walirejea Makkah katika hali ya furaha mno na wakawaarifu Waquraishi juu ya maswali yaliyotajwa hapo juu. Hivyo, ukatayarishwa mkutano ambao Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) nae alikaribishwa. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliwaambia kwamba alikuwa akisubiri ufunuo wa Allah kuhusiana na yale maswali matatu.9
Ule ufunuo wa mbinguni ukafika. Jibu la swali la kwanza kuhusiana na roho liko kwenye Surah Bani Israil, 17:85. Na kuhusu yale maswali mengine mawili, yamejibiwa kwa kirefu mwenye Surah al-Kahf, aya ya 9- 28 na 83-98. Majibu ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa kirefu, juu ya maswali haya matatu yanapatikana kwenye vitabu vya tafsiri na hayahitaji kurudiwa hapa.

  • 1. Siirah-i Hisham, Juzuu 1, uk. 321; na Tarikh-i Tabari, Juzuu 2, uk. 70.
  • 2. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 245.
  • 3. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 353.
  • 4. Tarikh-i Kamil. Juzuu 2, uk. 54-55.
  • 5. Siira-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 338.
  • 6. Siira-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 369
  • 7. Siira-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 371.
  • 8. Siira-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 392.
  • 9. Siira-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 300-301.