read

Sura Ya Kumi Na Sita: Uamuzi Wa Waquraishi Juu Ya Qur’ani Tukufu

Mjadala ambao hasa ni juu ya kiini cha mujiza, na hali ya kimuujiza ya Qur’ani tukufu uko nje ya nafasi ya kitabu hiki. Hata hivyo mijadala ya kihistoria inatuambia kwamba hiki Kitabu cha mbinguni kilikuwa silaha kuu na kali zaidi ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Ilikuwa hivyo kiasi kwamba washairi mahiri na duru za kuarudhi na kutunga na kuhutubia zilikanganywa na kushangazwa na ufasaha, utamu wa sauti na mvuto wa maneno yake, sentensi na mistari ya tenzi zake, na wote walikiri kwamba Qur’ani tukufu ya Muhammad iko kwenye kiwango cha juu zaidi cha ufasaha wa lugha na uwazi na ustadi wake juu ya maneno na jinsi yake ya kuelezea mambo haikuwa na kifani.

Kuchoma kwake moyoni, kupenya kwake, upeo wa furaha na mvuto wa Qur’ani tukufu vilikuwa kwenye hali ya kwamba hata wale maadui wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) walio wakali zaidi walitetemeka nafsini mwao walipozisikia baadhi ya aya zake zikisomwa, na wakati mwingine walikuwa wakifurahishwa mno kiasi kwamba kwa kiasi cha muda hivi hawakuweza kusogea kutoka pale walipokuwa kutokana na kubutwaa. Hapa chini tunatoa mifano juu ya jambo hili.

Uamuzi Wa Walid

Walid alikuwa mmoja wa mahakimu wa Uarabuni. Matatizo mengi ya Waarabu yalitatuliwa kupitia kwake. Alikuwa na utajiri mwingi mno. Kikundi cha Waquraishi kilimwendea ili wapate ufambuzi wa tatizo la kupenya kwa Uislamu kwenye nyumba zote na wakamweleza jambo hili na wakamwomba awape maoni yake juu ya Qur’ani ya Muhammad. Walimwuliza: “Je, Qur’ani ya Muhammad ni uchawi au kupiga bao au ni hotuba au ni ufasaha wa kusema alioutayarisha?” Yule mtaalamu wa Uarabuni aliomba apewe muda ili kwamba aweze kuyaeleza maoni yake baada ya kuisikiliza Qur’ani tukufu. Kisha aliamka kutoka kwenye maskani yake akaenda kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Alikaa pamoja nae kwenye Hajar-i Isma’il na akasema: “Hebu nisomee chochote kile kutokana na ushairi wako.”

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimjibu akisema: “Ninachokisema mimi si ushairi. Sivyo, bali ni neno la Allah alilo- literemsha kwa ajili ya mwongozo wenu.” Kisha Walid akasisitiza kwam- ba Mtume (s.a.w.w.) amsomee Qur’ani. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akam- somea aya kumi na tatu za kwanza za Surah al-Fussilat na alipoifikia Aya hii: “Na kama wakikengeuka, sema: ‘Nakuhadharisheni na adhabu iliyowakamata Waadi na Wathamudi.”(Surah al-Fussilat, 41:13).

Walid alitetemeka vikali mwilini mwake. Nywele zake zote zikasimama mwilini mwake na akaamka akiwa mwenye hali ya kushangaa na akarudi nyumbani kwake. Hakutoka nje ya nyumba yake kwa siku nyingi, kiasi kwamba Waquraishi wakaanza kumdhihaki na kusema: “Walid ameiacha dini ya jadi zake na kuichukua dini ya Muhammad.1

Tabari anasema: “Ilipofunuliwa Surah al-Ghaafir kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), aliisoma kwa sauti ya kuvutia mno ili kuzifikisha aya za Allah kwa watu. Kwa bahati wakati ule Walid alikuwa ameketi karibu naye na alizisikia aya hizi lakini hakuzingatia.

تَنْزِيلُ الْكِتَابِ مِنَ اللَّهِ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ {2}

غَافِرِ الذَّنْبِ وَقَابِلِ التَّوْبِ شَدِيدِ الْعِقَابِ ذِي الطَّوْلِ ۖ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ إِلَيْهِ الْمَصِيرُ {3}

مَا يُجَادِلُ فِي آيَاتِ اللَّهِ إِلَّا الَّذِينَ كَفَرُوا فَلَا يَغْرُرْكَ تَقَلُّبُهُمْ فِي الْبِلَادِ {4}

“Hiki Kitabu kimefunuliwa na Allah, Mwenye nguvu. Mjuzi Mwenye kuzighufiria dhambi na mwenye kuzikubalia toba, mkali wa kuad- hibu, Mola wa ukarimu. Hakuna apasaye kuabudiwa ila yeye (tu); vyote vitarejeshwa kwake. Hakuna abishanaye juu ya ufunuo wa Allah ila wale waliokufuru. Yasikughuri matendo yao nchini……….”
(Surah al-Ghaafir, 40:2-4).

Aya hizi zilimvutia mno yule mtaalamu wa Uarabuni. Bani Makhzumi walipomkusanyikia alitoa uamuzi wake juu ya Qur’ani tukufu kwa maneno haya: “Leo nimesikia kutoka kwa Muhammad maneno yasiyotokana na aina ya maneno ya mwanaadamu na jinni. Ni yenye sauti tamu na yana uzuri maalumu. Matawi yake yamejaa matunda na mizizi yake imejaa mibaraka tele. Ni maneno yaliyojitokeza kwa dhahiri na hakuna maneno yoyote mengine yaliyojitokeza zaidi ya haya.”

Alizitamka sentensi hizi na kisha akaenda zake na Waquraishi walifikiri kwamba ameanza kuiamini dini ya Muhammad.2

Kutegemeana na kauli ya mwanachuoni mkuu3 huu ulikuwa ndio utuku- zo na usifiwaji wa awali kabisa wa Qur’ani uliotolewa na mwanadamu, na uchunguzi makini wa maneno haya; huifanya hali ya kimuujiza ya Qur’ani tukufu mkabala na ujinga wa kiarabu kuwa dhahiri kabisa. Na inadhihirika kwamba sababu ya Qur’ani kuwa muujiza machoni pao ilikuwa ni ule mzamo wake usio na kifani, mvuto, uzuri na utamu wa sauti, kwa sababu hawakupata utamu na uzuri kwenye kitu chochote kingine ila Qur’ani tukufu.

Mfano Mwingine

Utbah bin Rabiyyah alikuwa mmoja wa wazee wa Kiquraishi. Wakati ule Bwana Hamza aliposilimu baraza lote la Quraishi liliingiwa na huzuni na masikitiko na machifu wao walihofia kwamba dini ya kiislamu itazidi kuenea zaidi. Katika hatua hiyo Utbah akasema: “Nitamwendea Muhammad na kuweka ahadi kadhaa kwake. Inawezekana akaikubali mojawapo ya hizo na kuiacha dini hii mpya.” Wale machifu walikubaliana na maoni yake. Hivyo akaamka na akaishika njia kumwendea Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ambaye wakati ule alikuwa amekaa kule Masjid. Alimpa ahadi za utajiri, utawala, na matibabu kwa maneno ya upole. Alipokoma kuzungumza, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akamwambia: “Je, hayo ndiyo yote yale uliyotaka kusema?” akajibu “Ndio!” hapo Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Hebu zisikilize aya hizi, kwani hili ndilo jibu la hayo yote uliyoyasema”:

حم {1}

تَنْزِيلٌ مِنَ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ {2}

كِتَابٌ فُصِّلَتْ آيَاتُهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ {3}

بَشِيرًا وَنَذِيرًا فَأَعْرَضَ أَكْثَرُهُمْ فَهُمْ لَا يَسْمَعُونَ {4}

“Haa Miim. (Huu ni) Uteremsho utokao kwa Mwingi wa rehema, Rahimu. Ni Kitabu ambacho aya zake zimefafanuliwa wazi wazi, ni Qur’ani yenye uwazi kwa watu wanaojua. Itoayo habari njema na ionyayo, lakini wengi wao wamekengeuka hivyo hawasikii.” (Surah Haa Miin, 41:1-4).

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alizisoma aya fulani fulani za Sura hii. Alipoifikia aya ya thelathini na saba ya Sura hii akafanya ‘Sajdah.’ Baada ya hapo alimgeukia ‘Utbah na kumwambia: “Ewe Abu Walid! Je, umeusikia Ujumbe wa Allah?” Kwa kiasi fulani ‘Utbah alikuwa amebumbuazwa na lile Neno la Allah. Alikuwa ameweka mikono yake nyuma ya kichwa chake, kikawa kimeegea hapo, aliendelea kuukodolea macho uso wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa kipindi kirefu, kana kwamba alikuwa amenyang’anywa uwezo wake wa kunena.

Kisha aliamka na kwenda kwenye sehemu waliokusanyika Waquraishi. Kutokana na hali yake na uso wake machifu wa Waquraishi walitambua kwamba alikuwa amevutiwa na maneno ya Muhammad na amerudi katika hali ya fedheha iliyoandamana na mhangaiko wa akilini. Wote walikuwa wakitazama kwa shauku kamili wauone uso wa ‘Utbah.

Wote wakamwuuliza: “Kumetokea nini?” akajibu: “Ninaapa kwa jina la Allah nimesikia kutoka kwa Muhammad nisiyopata kuyasikia kutoka kwa mtu yeyote. Ninaapa kwa jina la Allah! Maneno hayo si ushairi wala uchawi wala upiga ramli. Ninafikiria kwamba ingalifaa tumwache aendelee kuihubiri dini yake miongoni mwa makabila mbali mbali. Kama akifaulu na kujipatia nchi na milki, tutalichukulia jambo hilo kuwa ni fahari kwa ajili yenu na ninyi nanyi mtanufaika kutokana na nayo. Na kama akishindwa, watu wengine watamwua na ninyi vile vile mtapata sahala.”

Waquraishi wakamdhihaki ‘Utbah kwa kauli na maoni yake yale na wakasema kwamba amepumbazwa na maneno ya Muhammad.4

Hii ni mifano miwili ya maoni ya wazungumzaji wakuu wenye ufasaha wa lugha wa Zama za Ujinga na mifano mingine vile vile inapatikana.

Makri Ya Ajabu Ya Waqurishi

Siku moja baada ya jua kuzama, machifu wa Waquraishi kama vile ‘Utbah, Shaybah, Abu Sufyan, Nazar bin Harith, Abul Bakhtari, Walid bin Mughayrah, Abu Jahal, Aas bin Waai’l n.k. walikusanyika kandoni mwa Ka’bah na wakaamua kumwita Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na kujadiliana nae moja kwa moja kuhusu jambo lile. Hivyo basi, wakamtuma mtu mmoja kwenda kumtaka Mtume ashiriki kwenye mkutano ule. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipoarifiwa jambo lile alitoka upesi upesi na kujiunga na mkutano wao, akitegemea kuwaongoza kwenye njia iliyonyooka.

Yalianza mazungumzo kutoka pande zote na Waquraishi wakarudia kuzieleza huzuni zao. Wakalalamika kwamba mfarakano na ugomvi vimejitokeza miongoni mwa Quraishi, na wakonyesha kuwa kwao tayari kwa kafara lolote lile. Mwishoni walimwomba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ombi lililoelezwa kwenye aya zifuatazo:-

وَقَالُوا لَنْ نُؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ تَفْجُرَ لَنَا مِنَ الْأَرْضِ يَنْبُوعًا {90}

أَوْ تَكُونَ لَكَ جَنَّةٌ مِنْ نَخِيلٍ وَعِنَبٍ فَتُفَجِّرَ الْأَنْهَارَ خِلَالَهَا تَفْجِيرًا {91}

أَوْ تُسْقِطَ السَّمَاءَ كَمَا زَعَمْتَ عَلَيْنَا كِسَفًا أَوْ تَأْتِيَ بِاللَّهِ وَالْمَلَائِكَةِ قَبِيلًا {92}

أَوْ يَكُونَ لَكَ بَيْتٌ مِنْ زُخْرُفٍ أَوْ تَرْقَىٰ فِي السَّمَاءِ وَلَنْ نُؤْمِنَ لِرُقِيِّكَ حَتَّىٰ تُنَزِّلَ عَلَيْنَا كِتَابًا{93}

“Na wanasema: ‘Katu hatutakuamini mpaka utububujishie chemche- mi kutoka ardhini mbele ya macho yetu, au ububujishe mito kwenye mabustani ya mitende na mizabibu; au utuangushie mbingu ikatike vipande vipande kama ulivyodai, au utuletee Allah na Malaika katikati yetu; au ujenge nyumba ya dhahabu, au upae mbinguni; wala hatutakuamini kupaa kwako mpaka ututeremshie Kitabu tukisome (na chenye kuthibitisha utume wako)….” (Surah Bani Isra’il, 17: 90-93).

Ni dhahiri kwamba yale yote waliyoyasema yalikuwa udanganyifu mtupu, kwa sababu mitende na mizabibu haina chochote kihusianacho na Utume wa mtu na kuzifanya mbingu zipasuke vipande vipande na kuanguka mchangani ni jambo haliendani na ujumbe wa Utume ambao lengo lake ni kuwaongoza watu. Miongoni mwa matakwa yao kuna jambo moja tu lenye hali ya kimiujiza, nalo ni kupaa mbinguni kwa Mtume! Na japo Mtume (s.a.w.w.) angaliufanya mujiza huu wasingalimwamini, kwa sababu, walishasema wazi kwamba ni lazima ateremshe Kitabu kitakachouthibitisha utume wake!

Kama Waquraishi wangalipenda kweli kweli kuuthibitisha ukweli wa madai ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), basi kule kupaa kwake kwenda mbinguni kungalitosha kuwa uthibitisho wake.

Hata hivyo, walisema kwamba hawatatosheka nako. Matakwa yao yote yalikuwa na malengo maalumu. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliwajibu akisema: “Hakika mimi si chochote ila ni Mjumbe na siwezi kufanya mujiza wowote bila ya ruhusa ya Allah.”5

Kichocheo Cha Ukaidi Wa Machifu Wa Kiquraishi

Sehemu hii ya historia ya kiislamu ni moja ya mambo yahitajiayo majadiliano, kwa sababu mtu hufikiria ni kwa nini Waquraishi waligombana na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kiasi hiki, ingawa wote walimtambua kuwa yu mkweli na mwaminifu na kwamba hadi kufikia wakati ule hawajaona kosa lolote kwake japo lililo dogo zaidi, na kila mara wamekuwa wakisikia maneno ya kusisimua na fasaha kutoka kwake, na wakimwona akitenda matendo yasiyo ya kawaida na yaliyokuwa nje ya epeo la kanuni za maumbile. Mambo machache yangaliweza kufikiriwa kuwa ndio chanzo au vyanzo vya kichocheo cha ukaidi huu.

Waquraishi Walikuwa Wanamwonea Kijicho Mtukufu Mtume (S.A.W.W.).

Baadhi yao walikataa kumfuata Mtume (s.a.w.w.) kwa sababu walimwonea kijicho na walitamani kwamba wao wenyewe ndio wangaliishika kazi hii tukufu. Qur’ani tukufu inasema:

وَقَالُوا لَوْلَا نُزِّلَ هَٰذَا الْقُرْآنُ عَلَىٰ رَجُلٍ مِنَ الْقَرْيَتَيْنِ عَظِيمٍ {31}

Na wanasema: ‘Kwa nini hii Qur’ani hakuiteremshiwa mtu mwenye uwezo mkubwa kutoka katika miji miwili hii?’ (Surah al-Zukharuf, 43:31).

Wafasiri wa Qur’ani tukufu wanapoieleza sababu ya kufunuliwa kwa aya hii (yaani hoja ya Makafiri kuhusu ni kwa nini Qur’ani haikufunuliwa Makkah au Taifu) wanandika hivi.

Siku moja Ibn Mughayrah alikutana na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na akamwambia kwamba yeye (Walid) alifaa sana kuishika kazi ya Utume kwa kuwa yeye anao kipaumbele kuliko yeye (Mtume s.a.w.w) katika umri, utajiri na watoto.6

Umayah bin Abi Salt alikuwa mtu aliyekuwa akimzungumzia juu ya mtume kabla ya kuja kwa Uislamu na yeye mwenyewe alikuwa na shauku ya kuishika kazi hii kuu. Hata hivyo, hakumfuata Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) hadi mwisho wa maisha yake na alikuwa akiwashawishi watu kumwasi Mtume (s.a.w.w.)

Akhnas, aliyekuwa mmoja wa maadui wa Mtume (s.a.w.w.), alimwambia Abu Jahl: “Nini maoni yako kumhusu Muhammad?” Alimjibu akisema: “Sisi na Abdi Munaaf tuligombea utukufu na ukuu na tulikuwa karibu tu sawa nao na tulizitumia njia zote zilizowezekana ili kuwa sawa nao. Sasa ingawa tumekuwa sawa nao, wanasema kwamba ufunuo umemteremkia mtu wa familia yao kutoka mbinguni. Naapa kwa jina la Allah! Katu hatutamwamini.”7

Hii ni mifano inayoonyesha dhahiri kijicho cha machifu wa Kiquraishi. Vile vile iko mifano mingine iwezayo kuonekana kwenye kurasa za historia.

Kuihofia Siku Ya Hukumu

Hiki kilikuwa kisababisho kilichokuwa na athari kuu zaidi cha ukaidi wa Waquraishi, kwa sababu walikuwa watu wakutaanisi, wenye ashki. Mwito wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ulikuwa unapingana na tabia za kale za watu hawa waliokuwa wakiufaidi uhuru kamili kwa karne nyingi zilizopita; na kuziacha tabia mbaya kunafuatiwa na taabu na kazi ngumu zaidi ya hapo, Kuzisikia aya zenye kuyahusu mateso, zenye kuwahofisha watu wanaotaanisi, wadhalimu na wajinga na adhabu kali, kulijenga hofu kuu nyoyoni mwao na kuliwafanya wawe na wasiwasi na wasiokuwa na raha.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipozisoma aya tulizozitaja hapo chini kwenye mikusanyiko ya kawaida ya Waquraishi, kwa sauti ipendezayo, kulitokea ghasia iliyozivuruga furaha zao.

Waarabu waliokuwa na kawaida ya kujiandaa kwa ajili ya kujikinga na aina zote za matukio, walikuwa wakitabiri kwa mishale wakipima ndege kwa mawe ili kupata usalama, na kufikiria kuja na kwenda kwa ndege kuwa ni dalili ya matukio, hawakuwa tayari kutulia mpaka wapate uhakika juu ya adhabu ambazo Mtume Muhammad (s.a.w.w.) aliwaonya juu yao. Hivyo basi, waligombana nae ili kwamba wasizisikie tena bishara na vitisho vyake. Hapa tunanukuu baadhi ya aya zilizozihangaisha mno akili za wale Waarabu wenye kutaanisi na wajinga:

يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ {34}

وَأُمِّهِ وَأَبِيهِ {35}

وَصَاحِبَتِهِ وَبَنِيهِ {36}

لِكُلِّ امْرِئٍ مِنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ {37}

“Itakapokuja siku ya Hukumu mtu atamkimbia nduguye, na mama yake na baba yake, na mkewe na wanawe, Siku hiyo, kila mtu atakuwa na jambo lake mwenyewe”
(Surah Abasa, 80:34-37).

Waquraishi walipokuwa wameketi kandoni mwa Al-Ka’ba wakinywa mvinyo mara kwa ghafla waliyasikia maneno haya:

بِآيَاتِنَا سَوْفَ نُصْلِيهِمْ نَارًا كُلَّمَا نَضِجَتْ جُلُودُهُمْ بَدَّلْنَاهُمْ جُلُودًا غَيْرَهَا لِيَذُوقُوا الْعَذَابَ ۗ{56}

“…. … .., Hivi karibuni tutawatupia Motoni, kila mara ngozi zao zitakapoteketea, tutawapa ngozi (nyingine) badala ya zile, ili waionje adhabu Yetu,….”
(Surah al-Nisa, 4:56).

Maneno haya yaliwatia wasi wasi na mshtuko mno kiasi kwamba bila ya kujitambua waliviacha vikombe vyao (vya mvinyo) na wakaanza kutetemeka kwa hofu.

Pia zilikuwapo sababu nyinginezo zilizowafanya waache kuutambua ukweli wa Uislamu kwa mfano, siku moja Harith bin Nawfal mwana wa Abd-i Munaaf alikwenda kuonana na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na akamwambia: “Tunajua kwamba kile unachotuogofya nacho ni kweli na sahihi. Hata hivyo, kama tukiidhihirisha imani yetu kwako, Waarabu washirikina watatutoa kwenye nchi yetu.”

Aya zifuatazo zilifunuliwa ili kuwajibu watu hao:

وَقَالُوا إِنْ نَتَّبِعِ الْهُدَىٰ مَعَكَ نُتَخَطَّفْ مِنْ أَرْضِنَا ۚ أَوَلَمْ نُمَكِّنْ لَهُمْ حَرَمًا آمِنًا{57}

“Na wanasema: ‘Kama tukiufuata mwongozo pamoja nawe, tutatole- wa nchini mwetu; je, hatukuwakalisha mahali patakatifu pa amani, . ..” (Surah al-Qasas, 28:57).

Baadhi Ya Mikanusho Ya Washirikina

Wakati mwingine washirikina walisema: ‘Sham ndio nchi inayolea Mitume mapajani mwake na mpaka sasa bado haijawahi kuonekana kwamba mtu awe ameteuliwa kuishika kazi ya Utume kwenye jangwa hili (la Makkahh).” Kwa kuwafuatisha Wayahudi baadhi ya washirikina walisema: “Kwa nini hii Qur’ani iteremshwe kidogo kidogo? Kwa nini haikuteremshwa yote kamili kama Injili na Taurat?” Qur’ani tukufu inanukuu ukanushaji wao huo kwa maneno haya: “Na waliokufuru wanasema: ‘Mbona hii Qur’ani haikuteremshwa kwake yote kwa mara wahyi mmoja tu?”

Kisha inatoa jibu lifuatalo:

كَذَٰلِكَ لِنُثَبِّتَ بِهِ فُؤَادَكَ ۖ{32}

Tumeiteremsha hivyo ili tukuimarishie imani yako . . . .”(Surah al- Furqan, 25:32).

Bila shaka mambo yasiyopendeza na matukio makali yana athari kubwa kwenye moyo wa mwanaadamu na chanzo pekee cha kuridhika kwa upande wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kilikuwa ni maneno mapya aliyoyasikia kutoka kwa Mola wake, ambaye amemwamrisha uvumilivu na ujasiri, na kwa njia hii akajenga moyo mpya muundo wake wote.
Ni kwa lengo hili kwamba Qur’ani tukufu ilifunuliwa kidogo kidogo.

Zaidi ya hapo, kwenye siku za awali za Uislamu, kwa desturi baadhi ya kanuni zilitambulika rasmi, lakini haikufaa kuziacha ziendelee. Hivyo basi, halikuwezekana kwamba Qur’ani tukufu ingaliweza kufunuliwa kwa ufun- uo mmoja tu.

  • 1. Aa’laamul Waraa, uk. 27-28; na Bibaarul Anwaar, Juzuu 17, uk. 211-222.
  • 2. Majma’ul Bayaan, Juzuu 10, uk. 387.
  • 3. Kitabul Mu’jizatil Khaalidah, cha Allamah Shahristaani, uk. 66.
  • 4. Siirah-I Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 293-294
  • 5. Baadhi ya wamishenari wa Kikristo wamehoji juu ya msingi wa aya hii na nyinginezo kwamba, Mtukufu Mtume wa Uislamu hakuwa na muujiza wowote isipokuwa Qur’ani. Hata hivyo, uongo wa hoja hii, umedhihirishwa mwenye kitabu cha Kifursi (Kiirani) kiitwacho ‘Risaalat-i Jahaani-i Pymbaran.’
  • 6. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 361.
  • 7. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 316.