read

Sura Ya Kumi Na Tano

Kuwalingania Watu Wote

Ilikuwa imekwishapita miaka mitatu tangu kuanza kwa kazi ya Utume. Baada ya kuwaitia jamaa zake wa karibu zaidi kwenye Uislamu, Mtume (s.a.w.w.) aliamua kufanya mwito kwa watu wote.

Kwenye hiki kipindi cha miaka mitatu, amewaongoza baadhi ya watu kwenye Uislamu kwa mawasiliano maalum, lakini wakati huu aliwaita watu wote kwenye dini ya kumwabudu Allah, Aliye Mmoja wa Pekee. Siku moja alisimama kwenye mwamba mrefu na akasema kwa sauti kuu: “Yaa Sabah’aah!”1

Mwito wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ulipata mazingatio. Baadhi ya watu waliotokana na familia tofauti za Waquraishi walimkimbilia. Kisha aliwageukia wale waliokusanyika pale na kusema:

“Enyi watu! Je, mtaniamini kama nikikuambieni ya kwamba maadui zenu wako kwenye upande wa pili wa kilima hiki (safa) na wanadhamiria kuyashambulia maisha na mali zenu?” Wote wakamjibu wakasema: “Katu hatujasikia jambo lolote la uongo kutoka kwako maishani mwetu mwote.” Kisha Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Enyi Waquraishi! Jiepusheni kutokana na Moto. Sina chochote niwezacho kukutendeeni mbele ya Allah. Ninakuonyeni dhidi ya mateso makali!” Kisha akaongeza kusema: “Nafasi yangu ni kama ile ya mlinzi, amwonaye adui kwa mbali na upesi upesi akawakimbilia watu wake kwa ajili ya usalama wao na kuwaonya dhidi ya hatari inayowakabilia kwa kusema: “Yaa Sabah’aah kwa njia fulani malumu.”
Sentensi hizi zanaashiria msingi wa mwito wake na dini. Kwa kadiri fulani Waquraishi walikuwa wakiitambua dini yake hii, lakini maneno haya yalijenga hofu nyoyoni mwao kiasi kwamba mmoja wa viongozi wa ukafiri (Abu Lahabi) alikivunja kimya cha watu wale na akasema: “Ole wako! Hivi umetuita kwa ajili ya jambo hili?” Kisha wale watu wakatawanyika.

Wajibu Wa Imani Na Uvumilivu

Siri ya ushindi wa kila mtu imelalia kwenye mambo mawili: La kwanza, ni imani juu ya lengo lake mtu, na la pili, ni umadhubuti na juhudi kwenye njia ya kulifikia kwake lengo hili. Imani ni kichocheo cha ndani ambacho mchana na usiku hakina budi kumsukumiza mtu kwenye kuyafikia malengo yake, kwa sababu anaamini kwa dhati kwamba ustawi wake, ubora, kuneemeka kwake na mwisho mwema vinashirikiana nayo.

Na kuhusiana na shauku ambayo mwanaadamu anakuwa nayo mwenyewe, kila anapoikuza imani na matumaini yake, basi kwa utaratibu ule ule nguvu ya imani yake humwongoza na kumshauri kuyashinda magumu yote na kumweka mbali na shaka yoyote ile, ingawa ukweli uliopo ni kwamba, ustawi wake waweza kutegemeana na kulifikia lengo maalumu. Kwa mfano, mgonjwa ajuaye kwamba tiba yake na ustawi wake vinategemea kunywa dawa iwashayo, atainywa kwa urahisi, na mzamiaji aaminiye kwamba kuna lulu chini ya wimbi la bahari, basi hujitupa ndani ya kinywa cha wimbi bila ya kujali; na kuibuka baada ya kulifikia lengo lake.

Hata hivyo, iwapo yule mgonjwa au mzamiaji wana mashaka juu ya kuyafikia malengo yao, au hawaamini hata kidogo faida ya kazi yao, hawatachukua hatua yoyote kwenye mwelekeo ule, au japo wafanye, watakabiliwa na matatizo na machungu. Hivyo basi, ni ile nguvu ya imani hasana mategemeo vinavyotatua matatizo yote.

Hata hivyo, hakuna shaka yoyote juu ya ukweli uliopo kwamba mtu kuyafikia malengo yake kunaandamana na matatizo na vikwazo. Hivyo basi, ni muhimu kwetu kupambana dhidi ya vizuizi na kwa nguvu zetu zote kufanya juhudi ihitajikayo juu ya jambo lile, ili kwamba vikwazo vyote viweze kuondoka. Tangu kale imekuwa ikisemekana kwamba popote pale liwapo ua (lengo lenye tunzo) vile vile pana mwiba (tatizo) pamoja nalo. Hivyo basi, ua lile ni lazima lichumwe katika hali ambayo ule mwiba hautaichoma mikono au miguu ya mchumaji.

Qur’ani tukufu imelitaja jambo hili (kwamba siri ya ushindi imo mwenye imani juu ya lengo na uvumilivu wa mtu katika kulifikia lengo lile) katika sentensi fupi na imesema; “Hakika wale wanaosema: ‘Mola wetu ni Allah’ kisha wakaendelea kuushika unyofu…..(Surah al-Fussilat, 41:30).

Yaani wale wamwaminio Allah na kuliamini lengo maalumu na kisha wakaonyesha uimara, na uhodari, bila shaka watalifikia lengo lao na watasaidiwa na Malaika.

Uthabiti Na Ustahimilivu Wa Mtukufu Mtume (S.A.W.W.)

Kama matokeo ya mawasiliano maalumu ya Mtume (s.a.w.w.) kabla ya ‘kuhubiri Uislamu kwa watu wote’ na juhudi zake zisizolegea baada ya hapo, timu iliyoteuliwa na aminifu iliundwa dhidi ya nguvu za ukafiri na ibada ya masanamu. Waislamu waliosilimu kwa siri kabla ya ‘ulingano kwa watu wote’ walipata uzoefu na wale walioitika mwito wa Mtume (s.a.w.w.) baada ya kulingania huko, na ikagonga kengele ya hatari kwenye mikusanyiko yote ya ukafiri na ushirikina.
Hakuna shaka kwamba ilikuwa rahisi kwa Waquraishi waliokuwa na nguvu na silaha za kutosha kukisagasaga chama hiki kinachoanza, lakini sababu ya hofu yao ilikuwa kwam- ba wanachama wa chama hiki kipya hawakuwa wa familia moja, bali watu wa familia mbali mbali nao wamesilimu. Hivyo, haikuwa rahisi kwa Waquraishi kuchukua hatua za uamuzi.

Machifu wa Kikuraishi, baada ya kushauriana waliamua kuubomoa msingi wa imani hii na yule mwanzilishi wa hii dini mpya kwa njia mbali mbali. Waliamua kulifikia lengo hili kwa kumwendea kwenye nyakati mbali mbali na vitu vya kuvutia na wakati mwingine kumwendea na kumpa ahadi mbali mbali na mara kwa mara kutumia vitisho na kumtesa. Kwa kipindi cha miaka kumi Waquraishi walifanya hivyo na hatimaye waliamua kumwua Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Hivyo basi, ili kumwokoa, Allah alimwamrisha Mtume (s.a.w.w.) kuutoka mji wa Makkah.

Katika kipindi hicho kilichokwisha elezewa, chifu wa Bani Hashimu alikuwa ni Bwana Abu Twalib. Alikuwa ni mtu aliyekuwa na tabia ya kiungwana na moyo wa ukarimu, na nyumba yake ilikuwa kimbilio la masikini na yatima. Mbali na kuwa chifu wa Makkah na kuzishika kazi fulani fulani zihusianazo na Ka’aba tukufu, pia alikuwa na cheo kikuu kwenye jamii ya Waarabu na kwa kuwa alikuwa mlezi wa Mtume (s.a.w.w.) baada ya kufariki dunia kwa Bwana Abdul-Muttalib, hivyo machifu wengine wa Waquraishi walimwendea kwa kikundi2 na kumwambia hivi:

“Ewe Abu Twalib! Mpwa wako anawatukana miungu wetu, anaisema vibaya dini yetu, anazicheka fikara na itikadi zetu na anawachukulia jadi zetu kuwa walipotoka. Mwambie aachane nasi au umweke mikononi mwetu na ujizuie kumpa msaada.”3

Mzee wa Waquraishi na kiongozi wa ukoo wa Bani Hashim aliwajibu kwa namna ya busara na kwa sauti laini, na matokeo yake waliyaacha matendo yao hayo. Hata hivyo, Uislamu ulikuwa ukipenya na kuenea siku hadi siku na upeo wa hisia za kiroho za dini ya Mtume (s.a.w.w.) na maneno ya kuvutia na ya ufasaha ya kile Kitabu cha Mbinguni (Qur’ani tukufu) vilikuwa vikuipa msaada. Mtume (s.a.w) aliiwasilisha dini yake mbele ya watu hasa miezi ambayo vita iliharimishwa, wakati idadi kubwa ya mahu- jaji walipokusanyika mjini Makkah. Hotuba zake zenye ufasaha wa lugha na utamu na itikadi zake zenye kuvutia viliwavutia watu wengi.

Wakati huo huo, yule Firauni nae alitambua ya kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amepata umaarufu miongoni mwa makabila yote na amejipatia wafuasi wengi miongoni mwa makabila ya kiarabu yaishiyo mijini na mabedui. Hivyo mara moja wakaamua kumwendea kwa mara nyingine tena yule msaidizi pekee wa Mtume (Abu Talib) kumfanya atambue zile hatari ambazo zimeukumba uhuru wa watu wa Makkah na dini yao kutokana na ulinganiaji na kupanuka kwa Uislam. Hivyo wakamwendea tena kwa pamoja, na wakiyarejea maombi yao ya awali, walimwambia:

“Ewe Abu Twalib! Wewe ni mtu bora zaidi miongoni mwetu katika utukufu na umri, hata hivyo tulikujia hapo kabla na kukuomba umzuie mpwa wako asihubiri hii dini yake mpya, lakini hukuyasikiliza maneno yetu. Sasa hali imekuwa isiyovumilika kwa upande wetu. Hatuwezi kuvumilia zaidi kwamba mtu fulani awatusi miungu wetu na atudhanie kuwa tu wapumbavu na wajinga. Ni muhimu kwako kumzuia kutokana na matendo yote haya, na ambapo ikishindikana tutapigana dhidi yake pamoja na dhidi yako wewe, ambaye ndio msaidizi wake, ili kwamba wajibu wa kila kundi uweze kuwa dhahiri na moja ya makundi haya mawili liangamizwe.”
Bwana Abu Twalib, msaidizi na mlinzi mkuu wa Mtume (s.a.w.w.), kutokana na utambuzi wake na hekima zake kamilifu, alitambua kwamba ilikuwa inafaa kuonyesha uvumilivu kwa watu wale ambao heshima yao yote ya uhai wao ilikuwa ikikabiliwa na hatari.

Hivyo akatwaa msimamo wa amani na akawaahidi kwamba atazifikisha hisia zao machifu wale kwa mpwa wake. Bila shaka jibu hili kimsingi lilitolewa kwa lengo la kuuzima moto wa hasira zao ili kwamba hapo baadae njia ifaayo ya kulitatua tatizo hili iweze kufuatwa. Hivyo basi, baada ya kuondoka kwa machifu wale aliwasiliana na mpwa wake na kumfikishia ujumbe wao, na kwa bahati, ili kuitahini itikadi yake katika lengo lake, alitaka jibu kutoka kwake.

Hata hivyo, alipokuwa akijibu, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliitamka sentensi moja inayofikiriwa kuwa moja ya mistari ya historia ivutiayo na ya thamani mno. Haya ndio maelezo ya jibu lake: “Ami yangu mpenzi! Ninaapa kwa jina la Allah kwamba japo waniwekee jua kwenye mkono wangu wa kulia na mwezi kwenye mkono wangu wa kushoto (yaani japo wanipe utawala wa ulimwengu mzima) sitaacha kuitangaza dini yangu na kulitafuta lengo langu, na nitaziendeleza juhudi zangu hadi nizishinde taabu hizi na kulifikia lengo langu la mwisho au niutoe uhai wangu kwa ajili yake”.

Bada ya kusema hivyo macho ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) yalijiwa na machozi kutokana na huba na shauku ya kulifikia lengo lake na akasimama akaenda zake. Kauli yake yenye kupenya na kuvutia ilitoa hisia za ajabu moyoni mwa yule chifu wa Makkah kiasi kwamba, ingawa zilikuwapo hatari zote zile zilizomwelekea, alimwita yule mpwa wake arudi na alipofika alimwambia: “Ninaapa kwa jina la Allah! Sitaacha kukusaidia na unaweza kuendelea vizuri katika kulifikia lengo lako hadi mwis- honi mwake.”4

Waquraishi Wamwendea Bwana Abu Twalib Kwa Mara Ya Tatu

Kule kuendelea kwa Uislamu kwa kila siku kuliwasumbua mno Waquraishi na walikuwa na juhudi za kupata ufumbuzi wa tatizo hili. Wakakusanyika na wakawa na maoni ya kwamba msaada wa Bwana Abu Twalib unawezekana kwamba ni kutokana na ukweli kwamba alimtwaa Mtume (s.a.w.w.) kama mwanawe na kama ilikuwa ndio hivyo, ingewezekana kwamba wangeweza kumpelekea kijana mwenye sura nzuri na kumtaka amtwae kama mwanawe.

Hivyo basi walimwendea na kijana aliyeitwa ‘Ammaarah bin Walid bin Mughayrah’ aliyependeza mno miongoni mwa vijana wa Makkah, na wakimwendea Bwana Abu Twalib kwa mara ya tatu, walianza kulalamika na kumhofisha kwa maneno haya: “Ewe Abu Twalib! Mwana wa Walid ni kijana mshairi na vile vile yu mwenye sura ya kupendeza mno na mwenye akili. Tuko tayari kukupa kijana huyu ili umtwae kama mwanao na uache kumsaidia mpwa wako!” Abu Twalib aliposikia hivyo alichomwa sana moyoni, na akawakemea kwa sauti kuu na uso wenye hasira, akisema: “Mnanifanyia udhalimu mkubwa sana! Mnanitaka nikuleleeni mwana wenu nami nikupeni mwanangu kipenzi ili mkamwuue. Ninaapa kwa jina la Allah kwamba haitakuwa hivyo.” Hapo akasimama Mut’am bin Adi na akasema: “Pendekezo walilotoa Waquraishi ni la sawasawa kabisa, lakini wewe hutaikubali.” Bwana Abu Twalib akajibu akasema: “Hamjakuwa waadilifu na nina uhakika kwamba mnataka kunifidhehesha na kuwachochea Waquraishi wapigane dhidi yangu. Hata hivyo, mko huru kutenda lile mlitakalo!”

Waquraishi Wajaribu Kumvutia Mtukufu Mtume (S.A.W.W)

Waquraishi walikuwa na uhakika kwamba isingaliwezekana kumfanya Bwana Abu Twalib aukubali ushauri wao na, ingawa hajaeleza dhahiri kuwa yu mwislamu, bado alikuwa na imani kuu kwa mpwa wake na alimpenda sana. Hivyo wakaamua kujizuia kutoingia kwenye mazungum- zo yeyote naye. Hata hivyo, waliifikiria njia nyingine nayo ilikuwa kwamba wamtamanishe Mtume Muhammad kwa kumpa cheo, utajiri zawadi na mwanamke mrembo, ili kwamba ayaache mahubiri yake. Hivyo, wakaenda nyumbani kwa Bwana Abu Twalib kwa kikundi wakati ambapo yule mpwa wake alikuwa ameketi pamoja nae. Msemaji wa kikundi kile alipokuwa akiyafungua mazungumzo alisema: “Ewe Abu Twalib! Muhammad amezitawanya safu zetu zilizokuwa zimeungana na amesababisha mfarakano baina yetu. Amezicheka akili zetu na ametudhihaki sisi na masanamu yetu. Kama anashawishiwa kafanya hivi na umask- ini na ufukara wake, tuko tayari kumpa utajiri mkubwa sana. Kama anataka cheo, tuko tayari kumkubali awe mtawala wetu na tutamsikiliza. Na kama yu mgonjwa na anahitaji matibabu, tutamleta mganga mzoefu kumtibu….”

Bwana Abu Twalib aliugeuzia uso wake kwa Mtume (s.a.w.w.) na akasema: “Wazee wa kabila lako wamekuja na wanaomba kwamba uache kuwashutumu masanamu ili kwamba wao nao wakuache.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimjibu ami yake akisema: “Sitaki kitu chochote kutoka kwao. Ama kuhusu vitu hivi vinne wanavyovitoa, basi wao nawalipokee neno moja kutoka kwangu ili kwamba, chini ya msaada wake, waweze kuwatawala Waarabu na kuwafanya wasio Waarabu kuwa wafuasi wao.” Alipoifikia hatua hii alisimama Abu Jahal na kusema: “Tuko tayari kukusikiliza mara kumi.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Neno langu pekee ni kwamba muukubali Upweke wa Mola.”

Maneno ya Mtume (s.a.w.w.) yaliyokuwa hayategemewi yalikuwa kama maji baridi yaliyomiminwa kwenye birika la moto. Wote wakazongwa na fadhaha kali iliyoandamana na uchungu na kukata tamaa kiasi kwamba pale pale wote kwa pamoja, bila ya kuhiari wakasema: “Tuiache miungu mia tatu na sitini na tumwabudu Allah, mmoja tu!?”

Waquraishi walitoka nyumbani mle hali nyuso zao na macho yao yakiwa yanaungua kwa ghadhabu na walikuwa wakiifikiria njia ya kulifikia lengo lao. Kwenye aya za Qur’ani tukufu zifuatazo tukio hili hasa limeelezwa:5

وَعَجِبُوا أَنْ جَاءَهُمْ مُنْذِرٌ مِنْهُمْ ۖ وَقَالَ الْكَافِرُونَ هَٰذَا سَاحِرٌ كَذَّابٌ {4}

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ {5}

وَانْطَلَقَ الْمَلَأُ مِنْهُمْ أَنِ امْشُوا وَاصْبِرُوا عَلَىٰ آلِهَتِكُمْ ۖ إِنَّ هَٰذَا لَشَيْءٌ يُرَادُ {6}

مَا سَمِعْنَا بِهَٰذَا فِي الْمِلَّةِ الْآخِرَةِ إِنْ هَٰذَا إِلَّا اخْتِلَاقٌ {7}

“Na makafiri wanastaajabu kwamba amewafikia Mtume kutoka miongoni mwao; makafiri wanasema: ‘Huyu ni mchawi, mwongo.’ Je, anawashutumu miungu wote wengine isipokuwa mmoja tu? Hakika hili ni jambo la ajabu. Kikundi cha machifu wa makafiri wakaondoka kwenye mkutano na Mtume wakiambiana: Twendeni. Dumuni kwenye ibada ya miungu wenu. Mtu huyu anataka kukutawaleni. Sisi hatukuyasikia haya kwenye dini iliyopita. Si chochote haya ila ni uzushi.” (Surah Sad, 38: 4 - 7).

Mfano Wa Mateso Na Maonevu Ya Waquraishi

Moja ya vipindi vya majonzi mengi vya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kilianza siku ile alipoamua kukivunja kimya na wazee wa Waquraishi wakapoteza matumaini yote ya yeye kuvikubali vile vitu walivyotaka kumpa, kutokana na maneno yake maarufu:

“Ninaapa kwa jina la Allah! Japo muniwekee jua kwenye mkono wangu wa kulia na mwezi kwenye mkono wangu wa kushoto ili kwamba niyaache mahubiri yangu, sitapumzika hadi Allah aifanye dini yangu ishinde au niyatoe maisha yangu kwa ajili yake!” Hadi kwenye muda ule Waquraishi walikuwa, wakati wa makabiliano yote naye, waliihifadhi heshima yake, lakini walipoona kwamba zawadi zao za upatanisho zimeshindikana, walilazimika kuibadili njia ya fikara zao na kuuzuia Uislamu kuenea kwa gharama zote na kuzi- tumia njia zote kwa lengo hili. Hivyo basi, baraza la Waquraishi liliamua kwa pamoja kutumia dhihaka, mateso na vitisho ili kumzuia Mtume (s.a.w.w.) kutokana na kulitekeleza lengo lake.

Ni dhahiri kwamba mwana mageuzi, mwenye shauku ya kuwaongoza watu wa ulimwengu wote hana budi kuzingatia subira na uvumilivu mbele ya usumbufu, mateso, mashambulizi ya kiuwoga na mapigo ya kimwili na kiakili, ili kwamba kidogo kidogo aweze kuyashinda matatizo, na hii ndiyo iliyokuwa sera ya wana mageuzi wengine vilevile. Hapa chini tunatoa taarifa za baadhi ya maonevu na mateso ya Waquraishi ili kwamba kiwango cha subira na uvumilivu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) viweze kudhihirika.

Mbali na kipengele cha kiakili na kiroho (imani, uthabiti na uvumilivu) kilichomsaidia Mtume (s.a.w.w.) kwa ndani, vile vile alikuwa na kipengele cha nje kilichomhakikishia usalama na msaada kwa ajili yake, na hicho kilikuwa kule kuungwa mkono na Bani Hashim na Bwana Abu Twalib akiwa kiongozi wao, kwa sababu Bwana Abu Twalib alipotambua kwamba Waquraishi wamechukua uamuzi wa mwisho na usiobadilika wa kumtesa mpwa wake, aliwakusanya watu wote wa ukoo wa Bani Hashim na kuwaomba wamlinde Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Baadhi yao walijitolea kumsaidia na kumlinda kwa ajili ya imani yao na wengine walikubali kufanya hivyo kwa sababu ya ujamaa.

Kutokana nao ni watu watatu tu (Abu Lahabi na wengine wawili ambao majina yao tutayataja hapo baadae), pamoja na maadui wengine wa Mtume (s.a.w.w.) waliojizuia kuyakubali maamuzi yake. Hata hivyo, ingawa yalikuwapo hayo, hizi hatua za kiulinzi hazikuweza kumhami dhidi ya baadhi ya matokeo yasiy- opendeza na kila maadui walipomwona akiwa peke yake, hawakuacha kumtendea kila aina ya madhara. Huu ni mfano wa maonevu aliyopatiwa Mtume (s.a.w.w.) na Waquraushi.

Siku moja Abu Jahl alimwona Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwenye kilima cha Safa na akamtusi na kumhuzunisha. Mtume (s.a.w.w.) hakuzungumza naye hata kidogo na akaenda nyumbani kwake. Vile vile Abu Jahl alik- wenda kujiunga na Waquraishi waliokuwa wamekusanyika kandoni mwa Ka’aba. Bwana Hamza aliyekuwa ami na ndugu wa kunyonya wa Mtume (s.a.w.w.), nae alirudi siku ile ile kutoka kwenye uwindaji na alikuwa amechukua upinde wake begani mwake. Ilikuwa ni desturi yake kwamba baada ya kurudi mjini Makkah na kabla ya kuwaona watoto na ndugu zake, alikwenda kwenye Ka’aba na kufanya Tawafu na kisha ndipo ayaendee makundi mbali mbali ya Waquraishi waliokusanyika kandoni mwa Ka’aba na kusalimiana nao.

Katika siku ile baada ya kuzifanya ibada hizi, alikwenda nyumbani kwake. Kwa bahati mjakazi wa Abdullah Jad’aan, aliyelishuhudia tukio tulilolita- ja hapo juu, alimjia na kumwambia: “Ewe Abu Ammarah (jina la kiukoo la Hamzah)!
Natamani kwamba ungekuwapo hapa dakika chache kabla na ukawa umeliona tukio nililoliona! Hapo ungalifahamu jinsi Abu Jahl alivy- omtusi na kumwonea mpwa wako.” Maneno ya yule mjakazi yalijenga hisia ngeni akilini mwa Bwana Hamza na akaamua kulipiza kisasi cha kutusiwa kwa mpwa wake kwa Abu Jahl, kabla Hajafanya jambo lolote lile. Hivyo basi, alirudi na akamwona Abu Jahl akiwa amekaa miongoni mwa kundi la Waquraishi.

Bila ya kuzungumza na yeyote yule, aliuinua upinde wake wa kuwindia na kuupiga kichwani mwa Abu Lahab na fuvu lake la kichwa likajeruhiwa. Kisha akamwambia: “Unamtusi yeye (Mtume s.a.w.w) na hali mimi nimeipokea dini yake nami ninaipita njia ile ile anayoifuata. Kama una nguvu yoyote ile, basi toka tupigane!”

Hapo kikundi cha watu wa ukoo wa Bani Makhzuni wakasimama ili kumwunga mkono Abu Jahl, hata hivyo, kwa kuwa yeye alikuwa mtu mjanja na mwana diplomasia, aliepusha kila aina ya ugomvi na kujihami na akasema: “Nilimkosea Muhammad, nae Hamza anayo haki ya kutokuwa na raha juu ya jambo hili.”6

Ukweli huu wa kihistoria uliokubalika unaonyesha kwamba Bwana Hamza, ambaye baadaye alikuwa mmoja wa maamiri jeshi wa Uislamu wakuu, alikuwa mtu mwenye ushawishi na shujaa. Alifanya kila aliloliweza katika kumhami na kumlinda Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na kukiimarisha kikundi cha Waislamu. Kama asemavyo Ibn Athir, 7

Waquraishi waliuona Uislamu wa Hamza kuwa ni moja ya vipengele vikubwa zaidi kwa maendeleo na nguvu ya Waislamu na hivyo basi, walikimbilia mipango mingineyo tutakayoieleza baadae.

Wanahistoria wa Kisunni, kama vile Ibn Kathir Shaami wanasisitiza kwamba: “Athari za Uislamu wa Abu Bakr na Ummar hazikuwa ndogo zinapolinganishwa na athari za kusilimu kwa Hamza, na Uislamu wa hawa makhalifa wawili wakuu ulikujakuwa njia ya utukufu, nguvu na uhuru wa Waislamu.8

Hakika hakuna shaka yoyote juu ya ukweli kwamba kila mtu alichangia katika nguvu na kuenea kwa Uislamu, lakini, licha ya hilo, katu haiwezi kusemwa kwamba athari za Uislamu wa hawa makhalifa wawili zilikuwa sawa na athari za Uislamu wa Hamza.

Sababu ya uamuzi huu ni kwamba, Bwana Hamza alikuwa mtu ambaye aliposikia kwamba mzee wa Waquraishi amemtusi Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikwenda kumuuliza yule mkosefu bila ya kumtaarifu mtu yeyote juu ya azma yake ile na akalipiza kisasi vikali mno dhidi yake. Na hakuna aliyethubutu kusimama na kumpinga au kupigana naye.

Kwa upande mwingine, Ibn Hisham, mwandishi mkuu wa wasifu wa Mtume wa Uislamu, alisimulia tukio moja lihusianalo na Bwana Abu Bakr lionyeshalo kwamba alipojiunga na kundi la Waislamu hakuwa na nguvu iliyohitajika katika kujihami yeye mwenyewe au Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).9 Maelezo kamili juu ya tukio hilo tunayatoa hapa chini:

“Siku moja Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipita karibu na kundi la Waquraishi. Mara watu wale walimzingira na kila mmoja wao akaanza kuyarudia, kwa njia ya dhihaka, yale maneno yake aliyokuwa akiyasema juu ya masanamu na Siku ya Hukumu na kusema: “Je, unasema hivi?” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliwajibu akisema: ‘Ndio, mimi ndimi nisemaye hivi.’

Kwa kuwa Waquraishi waliona kwamba hayuko mtu yeyote wa kumhami Mtume (s.a.w.w.) waliamua kumuua. Hivyo, mtu mmoja alijitokeza na kuyakamata mapindo ya vazi lake. Ilitokea kwamba Bwana Abu Bakr ali- tokea kuwapo pale ubavuni pa Mtume (s.a.w.w.). Akiwa kajawa na machozi machoni, alisimama ili amsaidie Mtume (s.a.w.w.), na akasema: “Je, ni sahihi kwamba mumuue mtu auaminiye Upweke wa Allah?” Baadae (kwa sababu fulani fulani) watu wale waliacha kumtendea maovu Mtume (s.a.w.w.) na akaondoka akaenda zake, na Bwana Abu Bakr akaen- da nyumbani kwake akiwa kajeruhiwa kichwani.”

Ingawa tukio hili laweza kuwa ushahidi wa huba na shauku ya Khalifa huyu kwa Mtume (s.a.w.w.), kwanza kabisani ushahidi madhubuti wa udhaifu na woga wake. Linaonyesha kwamba wakati ule hakuwa na nguvu au cheo cha kijamii kitambulikanacho. Na kwa vile hatua ya kivitendo ya Waquraishi dhidi ya Mtume (s.a.w.w.) ingaliweza kufuatiwa na matokeo maovu dhidi yake, walimwacha yeye na wakayaelekeza makali ya kitendo chao kwa yule mfuasi wake na wakamvunja kichwa chake.

Kama ukiliweka lile tukio la Bwana Hamza lidhihirishalo ujasiri na ushujaa wake sam- bamba na tukio hili mojawapo kati ya matukio, unaweza kuamua vizuri sana kwamba ni Uislamu wa yupi uliokuwa na athari kubwa zaidi kwenye siku za awali za Uislamu juu ya heshima, nguvu na hofu ya makafiri.

Hivi karibuni utasoma habari za Uislamu wa Umar. Uislamu wake nao, ukiwa ni kama ule wa rafiki yake wa tangu kale, haukuimarisha nguvu ya ulinzi wa Waislamu. Lakini kwa Aas bin Waai’l, iliwezekana kwamba damu ya khalifa (Umar) ingeliweza kumwagwa kwenye ile ile siku aliyosilimu, kwa kuwa yeye (Aas bin Waai’l ) alikuja na kulihutubia lile kundi lililotaka kumuua Umar kwa maneno haya: “Mwataka nini kwa mtu aliyejitwalia itikadi kwa ajili yake mwenyewe? Je, mwadhania kwamba ukoo wa Adi utamtoa kwa urahisi? Sentensi hii yaonyesha kwamba ni hofu juu ya ukoo wake iliyowafanya watu wengine kumbakisha hai na ulinzi kutoka kwenye koo za wale watokanao nazo ilikuwa jambo la kawaida na la desturi na haikuwako tofauti yoyote kuhusiana na jambo hili, baina ya wa hali ya juu na wa hali ya chini.

Ndio, Kituo cha ulinzi wa Waislamu kilikuwa ni nyumba ya Bani Hashim na mzigo mzito wa jukumu hili, ulikalia bega la Bwana Abu Twalib na familia yake, kwa sababu, kuhusiana na watu wengine waliojiunga na Waislamu hawakuwa na nguvu iliyohitajika japo kwa kujihami wao wenyewe, na hivyo basi, suala la Uislamu wao kuwa chanzo cha heshima na utukufu wa Waislamu halikuibuka.

Abu Jahl Amvizia Mtume (S.A.W.W)

Kuendelea kwa Uislamu kulikozidi daima kulikuwa kumewafanya Waquraishi wahangaike. Kila siku walifikiwa na taarifa ihusuyo mwelekeo (wa kwenye Uislamu) wa mtu mmoja au mwingine wa kabila lao. Hivyo basi, kutokana na hali hiyo, hasira yao ilikuwa inawaka moto! Siku moja, yule Firauni wa Makkah, Abu Jahl, alisema kwenye mkutano wa Waquraishi: “Enyi Waquraishi! Mnaweza kuona jinsi Muhammad anavyoifikiria dini yetu kuwa ni haina thamani na anaikashifu dini ya jadi zetu na miungu yao, na anatuita wajinga.
Ninaapa kwa jina la Allah kwamba kesho nitamvizia na nitaliweka jiwe kando yangu; na Muhammad atakaposujudu nitamtwanga na jiwe lile kichwani mwake.” Siku iliyofuata, alifika Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwenye Masjidul Haraam ili asali, na akasimama baina ya ‘Rukni Yamaani’ na Hajjarul-Aswad (Jiwe Jeusi). Kikundi cha Waquraishi waliokuwa wakiitambua ile nia ya Abu Jahl walikuwa wakisubiri kuona kama atafaulu kwenye kampeni yake au la. Mtume (s.a.w.w.) akaenda sijida na yule adui yake mzee akajitokeza kutoka kwenye maoteo yake na akamwendea.

Hata hivyo, haikuchukua muda mrefu kabla Hajapigwa na hofu na akarejea kwa wale Waquraishi wenzie huku akitetemeka na kufadhaika na uso wake ukiwa umejaa wasi wasi. Wote wakakimbilia mbele na kuuliza: “Ewe Abu Hakim! Ni kitu gani kilichotokea?” akajibu kwa sauti dhaifu mno iliyoisaliti hofu yake na mchafuko wa akili: “Machoni mwangu yalitokea mandhari nisiyowahi kuyaona kabla yake maishani mwangu. Ilikuwa ni kwa sababu hii ambapo kwamba niliuacha mpango wangu.”

Hivyo basi, bila shaka nguvu isiyoonekana ilitokea kwa amri ya Allah na kujenga kitisho kilichomhami Mtumufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) kutokana na madhara ya maadui kwa mujibu wa ahadi ya Allah isemayo: “Sisi Tutakuhami kutokana na madhara ya wale wafanyao dhihaka.”

Matukio mengi ya mateso ya Waquraishi dhidi ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) yameandikwa kwenye kurasa za historia. Ibn Athar amekusanya sura nzima juu ya somo hili na ameyataja majina ya maadui wakatili wa Mtume (s.a.w.w.) walioishi mjini Makkah na ukatili walioutenda.10

Lolote lile tulilolisema hapo juu ni mfano tu. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alijiona kuwa kila siku alikuwa akikabiliwa na mateso mapya. Kwa mfano, siku moja Uqbah bin Abi Mu’it alimona Mtume (s.a.w.w.) akifanya

‘Tawaf’ na akamtusi. Alimfunga kilemba chake shingoni mwake na akamkokotea nje ya Masjid. Watu fulani wakamwokoa Mtume (s.a.w.w.) kutoka mikononi mwa Uqbah kwa kuwaogopa Bani Hashim.11

Mateso na maonevu aliyopatishwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na ami yake Abu Lahab na mkewe Ummi Jamil hayakuwa na kifani. Alitokea kuwa jirani wao wa mlango wa pili. Hawakujizuia kumtupia kila aina ya uchafu, na siku moja walimtupia matumbo ya kondoo kichwani mwake. Hatimaye Bwana Hamza, akiwa na lengo la kulipiza kisasi akambandika Abu Lahab matumbo yale kichwani.

Mateso Ya Waquraishi Dhidi Ya Waislamu

Katika siku za mwanzoni za kazi ya utume, kuendelea kwa Uislamu kulikuwa na matokeo ya visababisho kadhaa, kimoja miongoni mwao kilikuwa ni uthabiti wa Mtume (s.a.w.w.) na masahaba na wafuasi wake. Mifano ya subira na ustahimilivu wa huyu kiongozi wa Waislamu umeelezwa, ambapo uvumilivu na ustahimilivu wa Waislamu waliokuwa wakiishi mjini Makkah (makao makuu ya ushirikina na ibada ya masanamu) unastahili kuzingatiwa. Maelezo ya kujitoa muhanga na uthabiti wao yatatolewa kwenye sura ihusuyo matukio ya baada ya Hijrah (kuhamia madina).

Kwa wakati huu tutalieleza matukio mabaya yahusianayo na maisha ya baadhi ya wafuasi wa mwanzoni kabisa wa Mtume (s.a.w.w.) waliokuwa wakiishi kwenye mazigira ya Makkah yasiyokuwa na hifadhi.

Bilal Mu-Ethiopia:

Wazazi wa Bwana Bilal walikuwa miongoni mwa watu walioletwa Bara Arabuni kutoka Ethiopia wakiwa ni mateka. Yeye mwenyewe (ambaye baadaye alikuwa muadhini wa Mtukufu Mtume s.a.w.w.) alikuwa mtumwa wa Umayyah bin Khalaf. Umayyah alikuwa mmoja wa maadui wa kuu wa yule kiongozi mkuu wa Waislamu. Kwa vile nduguze Mtume (s.a.w.w.) walilishika jukumu la ulinzi wake, Umayya kwa lengo la kulipiza kisasi, alikuwa akimtesa hadharani yule mtumwa wake ambaye alisilimu karibuni tu. Akimlaza uchi kwenye mchanga ulio na joto kwenye siku za joto kali zaidi, akimwekea jiwe kubwa na lililo na joto kali kifuani mwake na kumsemesha kwa maneno haya:

“Sitakuachia mpaka ufe kwenye hali hii au uikane dini ya Muhammad, na uwaabudu ‘Laat’ na ‘Uzza!”

Licha ya mateso yote hayo, Bwana Bilal alimjibu Umayyah kwa maneno mawili tu yatokanayo na itikadi yake thabiti; alimwambia: “Ahad! Ahad! (yaani Allah yu Mmoja tu nami katu sitarejea kwenye dini ya ushirikina na masanamu).

Watu waliushangaa sana uthabiti wa huyu mtumwa mweusi aliyekuwa mateka wa mikononi mwa mtu aliyekuwa na moyo mgumu. Watu hawa walishangazwa mno kiasi kwamba Waraqah bin Nawfal yule mwanachuoni mkristo wa kiarabu, alilizwa mno na hali ya Bilal na akamwambia Umayyah: “Ninaapa kwa jina la Allah! Kama ukimwua kwa njia hii, nitalifanya kaburi lake kuwa sehemu takatifu lipasalo kutembele- wa na mahujaji!” 12

Wakati mwingine Umayyah alimtendea Bwana Bilal mambo makali zaidi. Aliifunga kamba shingoni mwa Bwana Bilal na kuwapa watoto kamba ile wamkokote mitaani! 13

Umayyah na mwanawe walitekwa kwenye vita vya Badr, vita vya kwanza vya Uislam. Baadhi ya Waislamu hawakupendelea kuuawa kwa Umayyah, lakini Bwana Bilal akasema: “Huyu ni kiongozi wa ukafiri na hivyo ni laz- ima auawe!” Kwa kushikilia kwake, baba na mwana walilipwa kwa ajili ya maovu na wakauawa.

Kujitoa Muhanga Kwa Ammar Na Wazazi Wake

Ammar na wazazi wake walikuwa miongoni mwa Waislamu wa awali kabisa. Walisilimu wakati Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipoichagua nyumba ya Arqam bin Abil Arqam kuwa makao ya kulingania Uislam. Wakati wenye kuyaabudu masanamu walipotambua kusilimu kwa Ammar na wazazi wake hawakuacha kuwatesa na kuwaonea. Ibn Athir14 anasema: “Wenye kuyaabudu masanamu waliwalazimisha watu hawa watatu kuzitoka nyumba zao kwenye mazingira ya joto kali na kuutumia muda wao kwenye upepo mkali na wenye joto kali wa jangwani. Mateso haya yalirudiwa kwa mara nyingi mno kiasi kwamba, Yaasir alifariki dunia kutokana na taabu alizozipata. Siku moja Sumayyah; mjane wa Yaasir aligombana na Abu Jahl kutokana na jambo hili. Mtu huyu mwenye moyo mgumu na katili alimchoma mkuki moyoni mwake na akamwua na yeye pia.
Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikasirishwa mno na maonevu waliyoten- dewa watu hawa. Siku moja aliwaona wakiteswa. Aliwageuzia uso huku akilia na machozi yakimbubujika machoni mwake, na akasema: “Enyi familia ya Yaasir! Kuweni na subira, kwa kuwa nafasi yenu iko Peponi.”

Baada ya kifo cha Yaasir na mkewe, wenye kuabudu masanamu walimwadhibu na kumtesa Ammar kama walivyomwadhibu Bilal. Ili kuyaokoa maisha yake, hakuwa na njia yoyote nyingine iliyomsalia ila kuukana Uislamu, lakini upesi sana akatubia na akakimbilia kwa Mtukufu

Mtume (s.a.w.w.) kwa moyo uliokuwa ukimdunda. Akamsimulia Mtume (s.a.w.w.) tukio lile, na Mtume (s.a.w.w.) akamwuliza: “Je, kulitokea kule- galega kokote katika imani yako ya ndani?” akajibu; “Moyo wangu umuejaa imani tele.” Hapo Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Usihofu hata kidogo akilini mwako na endelea kuificha itikadi yako ili uweze kujiokoa kutokana na madhara yao.” Aya ifuatayo ya Qur’ani tukufu ilifunuliwa kuhusiana na itikadi ya Ammar:15

مَنْ كَفَرَ بِاللَّهِ مِنْ بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَان{106}ِ

“(Atapata adhabu kali mno yule) anayemkataa Allah baada ya imani yake, ila yule aliyeshurutishwa hali moyo wake ni imara katika imani yake,…...’ (Surah Nahl, 16:106).

Inasemekana kwamba Abu Jahl aliamua kuibana familia ya Yaasir aliyetokana na tabaka la watu wasiokuwa na hifadhi hata kidogo wa mjini Makkah.

Hivyo basi akaamrisha kwamba ukokwe moto na utayarishwe mjeledi wa ngozi. Baada ya hapo Yaasir, Sumayyah na Ammaar walikokotewa kwenye sehemu iliyochaguliwa na wakaadhibiwa kwa kuchomwa na ncha ya upanga na miali ya moto na kutandikwa kwa mjeledi. Maonevu haya yalirudiwa mara nyingi kiasi kwamba Yaasir na Summayah wakafariki dunia, lakini hawakuweza kuiacha sifa ya Mtume (s.a.w.w.) hadi muda wao wa mwisho.

Waquraishi walioishuhudia mandhari hii ya kimsiba na la kuhunisha, ingawa walikuwa na umoja katika kuushinda Uislamu, walimsaidia Ammar ambaye wakati ule alikuwa kakumbwa na majeraha na huzuni mpaka akaachiliwa kutoka makuchani mwa Abu Jahl ili apate nafasi ya kuwazika wazazi wake.

Abdullah Bin Mas’ud

Waislamu waliosilimu kwa siri walikuwa wakiambiana kwamba bado Waquraishi hawajaisoma Qur’ani tukufu na ingefaa kama mmoja wao angalikwenda kwenye Masjidul-Haraam na kuzisoma baadhi ya baadhi ya aya za Kitabu Kitakatifu kwa sauti kuu. Abdullah bin Mas’ud alionyesha kuwa alikuwa tayari kufanya vile. Alikwenda Masjid wakati Waquraishi walipokuwa wamesimama kando kando mwa Al-Ka’ba na akazisoma aya zifuatazo kwa sauti kuu na tamu:

الرَّحْمَٰنُ {1}

عَلَّمَ الْقُرْآنَ {2}

“Mwingi wa rehema. Amefundisha Qur’ani ……….” ( Surah al- Rahman, 55:1-2)
Aya zenye utamu za Sura hii ziliwagonga Waquraishi kwa hofu ya ajabu. Na ili kuzizuia athari za huu mwito wa mbinguni, uliokuwa ukiyafikia masikio yao kupitia kwa mtu yule asiyekuwa na ulinzi, wakasimama wote na kumpiga hadi damu ikaanza kutiririka kutoka mwilini mwake mwote na akarejea kwa wale wafuasi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika hali ya kuhuzunisha. Hata hivyo, walifurahi kwamba hatimaye ile sauti yenye kuhuisha imeyafikia masikio ya maadui.16

Yale tuliyoyazungumza hapo juu yalikuwa ni kwa njia ya mfano, vinginevyo, idadi ya wafuasi wa dhati wa Uislamu waliojitoa mhanga waliovumilia shida kali kupita kiasi kwenye siku za awali za Ujumbe wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na wakaonyesha uthabiti wao katika njia ya kulifikia lengo lao ni kubwa sana. Hata hivyo tutaacha kuyataja majina yao na matukio ya maishani mwao kwa sababu za ufupisho wa mambo.

Maadui Wakali Mno Wa Mtukufu Mtume (S.A.W.W)

Utambuzi wa baadhi ya maadui wa Mtume (s.a.w.w.) ni jambo muhimu kuhusiana na baadhi ya matukio ya Uislamu ya baada ya kuhajiria Madina, na hapa chini tunatoa majina na maelezo yao kwa ufupi:

Abu Lahab: Yeye alikuwa jirani wa Mtume (s.a.w.w.). Hakuiachilia nafasi hata moja katika kumpinga na kumtesa yeye na Waislamu.

As’wad bin Abd Yaghus: Alikuwa mchekeshaji. Alipowaona Waislamu wasio na msaada na maskini aliwadhihaki na kusema: “Hawa watu waliokumbwa na umasikini wanajifikiria kuwa wao ni wafalme wa ulimwengu na wanadhani kwamba hivi karibuni watapata kiti cha enzi na taji la Mfalme wa Iran.” Hata hivyo kifo hakikumruhusu kuona kwa macho yake jinsi Waislamu walivyojipatia nchi, viti vya enzi na mataji ya Kaisari na Kisra.

Walid bin Mughayrah: Alikuwa mzee wa Kikuraishi aliyekuwa na utajiri mwingi. Tutayasimulia mazungumzo yake na Mtume (s.a.w.w.) kwenye sura ifuatayo.

Umayyah na Ubay wana wa Khalaf: Siku moja Ubay alimletea Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) mifupa ya watu waliokufa na kumwuliza: “Je, huyo Allah wako anaweza kuihuisha mifupa hii?” Pale pale lilikuja jibu kutoka kwenye chanzo cha ufunuo:

قُلْ يُحْيِيهَا الَّذِي أَنْشَأَهَا أَوَّلَ مَرَّةٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ خَلْقٍ عَلِيمٌ {79}

“Sema: “Ataihuisha huyohuyo Aliyeiumba hapo awali. Na Yeye ni Mjuzi wa kila (namna ya)kuumba.”(Surat Yaasin: 36:79)

Abul Hakam bin Hisham: Waislamu walikuwa wakimwita Abu Jahl (baba wa ujinga) kutokana na uadui na ukaidi wake dhidi ya Uislamu. Yeye nae aliuawa kwenye vita vya Badr.

Aas bin Waa’il: Alikuwa ni baba yake Amr bin Al-Aas. Yeye ndiye aliyempa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) jina la utani la ‘Abtar(asiye na kizazi).

Uqbah bin Abi Mu’it:17Alikuwa mmoja wa maadui wa Uislamu waliokuwa wakiogofya sana na katu hakuipoteza nafasi ya kumtendea madhara Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na Waislamu.
Vile vile lilikuwapo kundi jingine la maadui wa Uislamu ikiwa ni pamoja na Abu Sufyani na wengineo. Wanahistoria wameandika taarifa zao kwa kirefu na kwa ajili ya kufupisha mambo, tutaacha kuwanukuu hapa.

Umar Ibn Khattab Asilimu

Kusilimu kwa kila mtu miongoni mwa Waislamu wa awali kulikuwa ni athari ya kisababisho kimoja au kingine na wakati mwingine tukio dogo sana liliwezakuwa sababu ya kusilimu kwa mtu au kikundi. Kishawishi cha kusilimu kwa khalifa wa pili ni chenye kuvutia. Ingawa kwa msimamo wa utaratibu wa yalivyotokea matukio ingalikuwa bora kuliandika tukio hili baada ya kuelezea tukio la Waislamu kuhamia huko Ethiopia, lakini, tunaona kwamba inafaa kulieleza hapa, kama tulivyowaeleza baadhi ya wafuasi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Ibn Hisham18 anasema: “Kutoka kwenye familia ya Khattab (baba yake Umar) ni binti yake Fatimah na mumewe Sa’id bin Zayd tu waliosilimu. Kwa kuwa katika siku za awali za Uislamu, uhusiano wa Umar na Waislamu ulikuwa wa uadui mkubwa na alifikiriwa kwamba yu mmoja wa maadui wakaidi zaidi wa Mtume (s.a.w.w.), hivyo dada yake na mumewe siku zote waliificha itikadi yao asiifahamu. Licha ya hivyo, Khubaab bin Art alikuwa akija nyumbani kwao kwenye masaa waliyoafikiana na kuwafundisha Qur’ani tukufu.

Hali ya kuchanganyikiwa ya watu wa Makkah ilimfanya Umar kuwa na hisia kali, kwa kuwa aliona kwamba mifarakano na michafuko ilitawala miongoni mwao na zile siku angavu za Waquraishi zimebadilika na kuwa usiku wa giza.

Hivyo Umar aliamua kwenda kuukatilia mbali mzizi wa fitina na mgawanyiko kwa kumwua Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Ili kulifikia lengo hili, alikuwa akitafuta sehemu anakopatikana Mtume (s.a.w.w.).Aliarifiwa ya kwamba alikuwa kwenye nyumba iliyokuwako kandoni mwa bazaar ya Safa, na watu arobaini kama vile Hamza, Abu Bakr, Ali n.k. wamelichukua jukumu la kumlinda na kumhami.

Na’im Ibn Abdullah aliyekuwa mmoja wa marafiki wa karibu zaidi wa Umar anasema: “Nilimwona Umar akiwa amebeba upanga wake. Nilimwuliza kuhusu lengo alilokuwa akiliendea. Alijibu hivi: “Ninakwenda kumtafuta Muhammad aliyejenga mfarakano miongoni mwa Waquraishi. Ameicheka hekima na akili zao, kuitangaza dini yao kuwa haina thamani na kuwatweza miungu wao. Nakwenda kumuua.”

Na’im anasema: Nilimwambia “Umedanganyika. Je, wadhania kwamba dhuria wa Abd Munaf wataubakisha uhai wako? Kama wewe ni mtu upendaye amani, basi huna budi kuitengeneza kwanza nyumba yako. Dada yako Fatimah na mumewe wamesilimu na wanaifuata dini ya Muhammad.”

Maneno ya Na’im yalisababisha dhoruba ya ghadhabu akilini mwa Umar. Matokeo yake ni kwamba aliuachilia mbali ule mpango wake wa awali na akaenda nyumbani kwa shemeji yake. Alipofika karibu na nyumba ile, alisikia uvumi wa mtu fulani aliyekuwa akiisoma Qur’ani tukufu kwa sauti ivutiayo. Namna Umar alivyofika kwa nyumbani kwa dada yake ilikuwa kiasi kwamba dada yake yule na mumewe pia walitambua kwamba alikuwa karibuni kuingia.
Hivyo, walimficha yule mwalimu wao wa Qur’ani tukufu nyuma ya nyumba yao ili aweze kubakia kujificha machoni pa Umar. Pia Fatimah alilificha lile karatasi lililoandikwa aya za Qur’ani tukufu.

Bila ya salamu au maamkuzi kwa wenye nyumba wale, Umar akasema: “Uvumi ule niliousikia ulikuwa ni wa nini?’ Wakamjibu; “Hatukusikia kitu chochote.” Umar akasema: “Nimesikia kwamba mumesilimu na kuifuata dini ya Muhammad!” Aliitamka sentensi hii kwa ghadhabu kali na kuanza kumshambulia shemeji yake. Hapo dada yake akasimama ili kumhami mumewe.

Umar akamshambulia yeye pia na akakijeruhi kichwa chake vibaya mno kwa ncha ya upanga wake. Fatimah akiwa hajiwezi pale, akiwa anachuruzika damu kichwani mwake, alisema kwa hamasa kubwa ya imani: “Ndio. Tumesilimu na tunamwamini Allah na Mtukufu Mtume wake. Fanya vyovyote utakavyo.”

Hali ya kuhuzunisha ya dada huyo, aliyekuwa akisimama kandoni mwa kaka yake huku uso na macho yake yakiwa yametapakaa damu na akizungumza naye, vilimfanya Umar atetemeke, na hatimaye alijutia kitendo chake kile. Hivyo basi, akasisitiza kwamba wamwonyeshe lile karatasi ili kwamba ayatafakari maneno ya Muhammad. Dada yake akichelea asije akalipasua, alimtaka aapie kwamba hatafanya hivyo, na yeye aliahidi pia na kuthibitisha kwa kiapo kuwa atalirudisha karatasi lile baada ya kulisoma. Kisha Umar akalishika karatasi lile mkononi mwake. Aya chache za Qur’ani tukufu zilikuwa zimeandikwa mle. Hapa chini tunaiandika tafsiri yake:

طه {1}

مَا أَنْزَلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لِتَشْقَىٰ {2}

إِلَّا تَذْكِرَةً لِمَنْ يَخْشَىٰ {3}

تَنْزِيلًا مِمَّنْ خَلَقَ الْأَرْضَ وَالسَّمَاوَاتِ الْعُلَى {4}

الرَّحْمَٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ {5}

لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا وَمَا تَحْتَ الثَّرَىٰ {6}

وَإِنْ تَجْهَرْ بِالْقَوْلِ فَإِنَّهُ يَعْلَمُ السِّرَّ وَأَخْفَى {7}

Twaa Haa. Hatukukuteremshia Qur’ani ili upate mashaka. Bali iwe mawaidha kwa wenye kunyenyekea. Ni ufunuo utokao kwa Yule Aliyeiumba ardhi na mbingu zilizoinuka juu. Mwingi wa rehema ametawala juu ya Arshi. Ni Vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini na vilivyomo baina yao na vilivyomo chini ya udongo. Na kama ukinena kwa kauli kubwa (au ukinong’ona), basi hakika Yeye anajua yaliyo siri na yaliyofichikana zaidi.” (Surah Twaa Haa, 20:1-7).

Aya hizi zenye ufasaha wa lugha na maneno yaliyowazi na thabiti zilimvutia mno Umar. Yule mtu aliyekuwa adui katili wa Qur’ani tukufu na Uislamu dakika chache zilizopita, aliamua kuzibadili fikira zake. Aliiendea ile nyumba ambayo kabla ya hapo alisikia kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) angaliweza kupatikana humo na akabisha mlangoni. Mmoja wa wafuasi wake Mtume (s.a.w.w.) alichungulia kupitia kwenye tundu la mlango na kumwona Umar akiwa amesimama na upanga mkononi mwake akisubiri mlango ufunguliwe. Mara moja akarudi na kumtaarifu Mtume (s.a.w.w.) hali ile, Bwana Hamza mwana wa Abdul-Muttalib akasema:

“Mwache aingie. Kama kaja kwa nia njema tutamkaribisha, lakini kama malengo yake si mema, tutamwua.” Usimamaji wa Umar mbele ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) uliwahakikishia heri na uso wake mng’avu na kuionyesha kwake huzuni na aibu kuliyashuhudilia malengo yake hasa.
Hatimaye akasilimu mikononi mwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) mbele ya wafuasi wake na hivyo akajiunga na safu za Waislamu.19

 • 1. Badala ya kugonga kengele ya hali ya hatari, Waarabu waliyatumia maneno haya na kwa kawaida wakaanzisha taarifa zenye kutahadharisha pamoja nayo.
 • 2. Ibn Hisham ameyataja majina na maelezo ya watu hawa mwenye ‘Siirah’ yake.
 • 3. Siirah Ibn Hisham, Juzuu 10, uk. 265.
 • 4. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 265-266.
 • 5. Tarikh-i Tabari, Juzuu 2, uk. 66 na 67; Siirah-ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 295 na 296.
 • 6. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 313 na Tarikh-i Tabari, Juzuu 2, uk. 72.
 • 7. Tarikh-i Kamil, Juzuu 2, uk. 59.
 • 8. Al-Bidaayah wan Nihaayah, Juzuu 3, uk. 26.
 • 9. Siirah, Juzuu 1, uk. 311, Tabari amelinukuu tukio zima kwenye Ta’rikh yake, Juzuu 2, uk. 72. isipokuwa kwamba kichwa cha khalifa kilijeruhiwa.
 • 10. Tarikh-i Kamil, Juzuu 2, uk. 47.
 • 11. Bihaarul Anwaar, Juzuu 18, uk. 204.
 • 12. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 328.
 • 13. Tabaqaat-i Ibn Sa’ad, Juzuu 1, uk. 233.
 • 14. Tarikh-i Kamil, Juzuu 2, uk. 45.
 • 15. Siirah-i Hisham, Juzuu 1, uk. 320.
 • 16. Siirahi Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 324.
 • 17. Tarikhi Kamil, Juzuu 2, uk. 47-51; Usudul Ghabah; Al-Asabah; Al-Ist’iaab n.k
 • 18. Siirahi Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 365.
 • 19. Ibn Hisham ametoa masimulizi mengine ya kusilimu kwa Umar (Juzuu 1, uk. 368).