read

Sura Ya Kumi Na Tatu :Ni Nani Waliokuwa Watu Wa Kwanza Kusilimu?

Maendeleo Ya Uislamu

Maendeleo ya Uislam na kupenyeza kwake ndani ya watu tofauti tofauti kulifanyika polepole. Kwa mujibu wa maneno ya Qur’ani tukufu watu hao waliowatangulia wengine wote katika kusilimu na kuuhubiri Uislamu wanaitwa ‘As-Saabiqun’ (watangulizi) na katika siku za mwanzoni mwa Uislamu heshima hii ya ziada ilikuwa kipimo cha usafi na ubora na hata miongoni mwa watu hawa, mtu amtanguliaye mwingine alipewa cheo cha heshima. Hivyo basi, hatuna budi kuzirejea taarifa zikubalikazo na kuamua, bila ya upendeleo kuhusu ni nani waliokuwa wa kwanza miongoni mwa wanaume na wanawake waliosilimu.

Wa Kwanza Miongoni Mwa Mwanamke Kusilimu Alikuwa Ni Bibi Khadijah

Ni ukweli wa kihistoria ukubalikao kwamba miongoni mwa wanawake Bibi Khadija alikuwa wa kwanza kusilimu na hakuna riwaya zipinganazo juu ya jambo hili. Hapa tunataja muhtasaroi wa maandishi ya kihistotia yaliyo muhimu na yenye nguvu yaliyonukuliwa na wanahistoria kutoka kwa mmoja wa wakeze Mtume (s.a.w.w.)

Bibi Aisha asema hivi: “Kila mara nilikuwa nikisikitishwa na kutokiona kipindi cha Khadija, nilishangazwa na huruma na huba aliyoionyesha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwake, kwa sababu mumewe mpenzi alikuwa akimkumbuka zaidi kuliko mtu yeyoye mwingine na kama akimchinja kondoo aliwatafuta marafiki wa Khadija na kuwapelekea fungu la nyama ile. Siku moja Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa akitoka nje ya nyumba, alimkumbuka Khadija na kumsifu. Hatimaye nilishindwa kujizuia na nikasema kwa ujasiri kabisa: “Yeye hakuwa chochote zaidi ya kuwa bibi kizee na Allah amekupa mwanawake aliye bora.”

“…. Maneno yangu yalikuwa na athari mbaya kwa Mtukufu Mtume wa Allah(s.a.w.w.). Dalili za kuchukia na ghadhabu zilitokea katika paji la uso wake, na akasema: Si hivyo hata kidogo ….. sijajipatia mwanamke bora. Aliuamini Utume wangu wakati watu wote walipokuwa wamezama katika ukafiri na ibada ya miungu mingi.

Aliuweka utajiri wake mikononi mwan- gu wakati wa kwenye mazingira tahinifu. Kutokana na naye, Allah ameni- pa kizazi, ambacho sikukipata kutoka kwa yeyote yule mwingine”.1

Ushahidi mwingine juu ya Bibi Khadija kuwa mwanamke wa kwanza hapa ulimwenguni kusilimu ni lile tukio la kuanza kufunuliwa Qur’ani tukufu, kwa sababu Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliposhuka kutoka kule pango la Hira na kumsimulia mkewe tukio hili, mara moja aliyathibitisha maneno ya mumewe na akamfariji. Zaidi ya hapo, alikuwa amesikia kutoka kwa watabiri na wapiga ramli wa Uarabuni juu ya Utume wa mumewe na ilikuwa ni kutokana na uaminifu na unyoofu wa huyu kijana wa Kibani Hashim kwamba alikubali kuolewa naye.

Wa Kwanza Kusilimu Miongoni Mwa Wanaume Alikuwa Ni Ali (A.S)

Karibuni wanahistoria wote wa Kishi’ah na Kisunni wanakubaliana kwamba mwanaume wa kwanza kusilimu alikuwa ni Sayyidna Ali (a.s.). Na dhidi ya kauli hii maarufu vile vile inawezekana kupata kauli za nadra katika historia. Wasimuliaji wao wamechagua kuzungumza kinyume na hivyo. Kwa mfano, inasemekana kwamba mwanaume wa kwanza kusilimu alikuwa ni bwana Zay’d bin Harith au bwana Abu Bakr. Hata hivyo, nyingi ya hoja zinatoa ushahidi dhidi ya kauli hizi mbili. Baadhi ya hoja hizo ni hizi.

Ushahidi Wa Kwanza

Tangu katika siku za utotoni Sayyidna Ali (a.s.) alilelewa nyumbani kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) naye Mtume alijitahidi kwa nguvu zake zote kumwelimisha kama vile afanyavyo baba mwenye huruma. Wengi wa waandishi wa wasifu husema kwa kukubaliana kwamba: “Kabla ya uteuzi wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kushika kazi ya Utume ulitokea ukame mkali sana mjini Makkah.
Bwana Abu Twalib, ami yake Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na familia kubwa ya kutunza, alikuwa chifu wa Waquraishi, na kipato chake hakikuweza kulandana na matumizi yake naye hakuwa tajiri kama alivyokuwa nduguye Abbas. Hali ya kifedha ya Bwana Abu Twalib ilimhimiza Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kulijadili jambo hili na bwana Abbas na wakaamua kuwachukua baadhi ya watoto wa Abu Twalib majumbani mwao ili waweze kuupunguza mzigo wake na kumsaidia katika kupata mahitajio yake. Matokeo ya mashauriano haya ni kwamba Mtume (s.a.w.w.) alimchukua Sayyidna Ali (a.s.) na bwana Abbas alimchukua Bwana Ja’far chini ya ulezi wake.”2

Katika hali hiyo, tunaweza kusema kwamba, Sayyidna Ali (a.s.) alipokwenda nyumbani kwa Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na umri usiopungua miaka minane au kumi. Sababu ya kudhania hivyo ni kwamba, shabaha ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kumchukua Sayyidna Ali (a.s.) nyumbani kwake na kumweka chini ya utunzaji wake ilikuwa ni kupunguza mzigo wa chifu wa Makkah (Bwana Abu Twalib), na zaidi ya ukweli uliopo ni kwamba kutengana na wazazi wake mtoto aliye chini ya umri wa miaka nane au kumi ni jambo gumu; vile vile isingaliweza kutoa athari zipendezazo katika hali ya maisha ya Bwana Abu Twalib.

Hivyo basi, ni muhimu kwetu sisi kudhani kwamba umri wa Sayyidna Ali (a.s.) wakati ule ulikuwa katika hali ya kutoa athari zipendezazo kwa maisha yake anapochukuliwa kutoka kwa baba yake Bwana Abu Twalib. Katika hali hii, mtu awezaje kusema kwamba watu wasio wa nyumba ile, kama vile Bwana Zayd bin Harith na wegineo walijifungamanisha na siri za wahyi, ambapo binamu yake Mtume (s.a.w.w.), aliyekuwa karibu zaidi naye kuliko watu wote na daima alikuwa pamoja naye, akasalia katika hali ya kutozifahamu?

Lengo la Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kumlea Sayyidna Ali (a.s.) lilikuwa kumfidia Bwana Abu Twalib kwa kadri fulani kwa huduma alizozitoa na kwa kadiri Mtume alivyopasika, hakikuapo chochote kilicho kuwa bora zaidi kwake kuliko kumwongoza mwanaadamu.

Kwa kuyazingatia mambo yote haya, mtu awezaje kusema kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alim- nyima binamu yake baraka hizi ingawa ukweli uliopo ni kwamba, yeye (Sayyidna Ali (a.s.) alikuwa mtu mwenye ujuzi mwingi na mwenye akili yenye elimu nyingi? Ingalikuwa bora kama tunajifunza juu ya jambo hili kutoka midomoni mwa Sayyidna Ali mwenyewe.

Katika hotuba yake iitwayo ‘Qasi’ah’ alikieleza cheo na heshima yake mbele ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Mnaifahamu heshima aliyonipa Mtume (s.a.w.w.) kuhusiana na ujamaa wetu na itibari (nilivyokuwa nayo mbele yake).

Wakati wa utoto wangu alinilea chini ya malezi yake na kunikumbatia. Alinikumbatia kitandani mwake na nilikuwa na kawaida ya kuinusa harufu yake nzuri. Nilimfuata kama vile ndama wa ngamia amfuatavyo mama yake.

Kila siku aliinua (alionyesha ) dalili ya utu wema na kuniamrisha niifuate. Alikuwa akisali huko Hira kila mwaka (kabla ya uteuzi wake wa kushika kazi ya Utume) nami nilikuwa nikienda kumwangalia huko, ambapo hakuna yeyote aliyemwona.

Wakati ule Uislamu ulikuwa bado haujaifika nyumba yoyote ila ile ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na Khadija, nami nilikuwa wa tatu wao. Nilikuwa nikiiona nuru ya wahyi na utume na kuinusa harufu nzuri ya Utume.”3

Ushahidi Wa Pili

Alipokuwa akiyasimulia maisha ya Afif Kandi, wanachuoni Ibn Hajjar (katika kitabu chake ‘Al-Isabah Ibn Abdul Bir (katika Isti’ab) na wanachuoni wengine wengi wa historia wamemnukuu (Afif Kandi) akisema kwamba: “Safari moja katika zama za ujinga nilikwenda Makkah. Mwenyeji wangu alikuwa ni Abbas mwana wa Abdul Mutwalib na sote tulifika kwenye mipaka ya Al-Ka’ba Tukufu.

Mara kwa ghafla nilimwona mtu mmoja akiwa kasimama kandoni mwa Al-Ka’ba. Kisha akaja kijana mwamaume na akasimama kuliani mwake. Mara baada ya hapo nilimwona mwanamke akija na kusimama nyuma yao. Nilimwona yule kijana na yule mwanamke wakifanya Rukuu na Sijida wakimwiga yule mwanaume. Mandhari hii isiyo na kifani ilinifanya nimwulize Abbas kuhusiana nayo.

Alisema: “Yule mwanaume ni Muhammad mwana wa Adullah na yule kijana ni binamu yake na yule mwanamke aliyesimama nyuma yao ni mkewe Muhammad.” Kisha akaendelea kusema: “Yule mpwa wangu anasema kwamba ipo siku atakapozitawala hazina za ‘Kisra’ na ‘Kaisari.’ Ninaapa kuwa jina la Allah, hakuna mfuasi wa dini hii katika uso wa hii ardhi ila hawa watu watatu tu.” Kisha yule msimuliaji anasema: “Ningalipenda kwamba ningalikuwa wanne wao!”

Kwa vile masimulizi haya hayamhusu Sayyidna Ali (a.s.) moja kwa moja hata watu hao washindwao kusimulia wema wake wameyanukuu. Miongoni mwa wana hadithi ni Bukhari pekee aliyefikiria kuihesabu kuwa ni ‘dhaifu’, lakini msimamo wake juu ya kizazi cha Mtume (s.a.w.w.) unafahamika vizuri mno. Msomaji anaweza kuyasoma masimulizi tuliyoy- ataja hapo juu kwa kirefu katika vitabu tulivyovitaja hapa chini.4

Ushahidi Wa Tatu

Katika hotuba na maelezo ya Sayyidna Ali (a.s.) mara nyingi tunaziona sentensi zifuatazo na nyingine zifananazo na hizi:

“Mimi ni mja wa Allah na nduguye Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na ni mkweli aliye mkuu zaidi, na hakuna yeyote awezaye kuitamka sentensi hii baada yangu ila yule mtu aliye mwongo. Nilisali pamoja na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa kipindi cha miaka saba5kabla ya mtu yeyote mwingine kufanya hivyo.”

Mwandishi wa Al-Ghadir (Juzuu 3, uk. 222) amewanukuu waandishi wa masimulizi haya kutoka kwenye vitabu vya Ahadith na historia nasi twahitaji kuyanukuu masimulizi haya japo kwa mukhtasari tu.

Ushahidi Wa Nne

Ahadithi za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na mfuatano wa mashahidi wa maelezo mbali mbali yamenukuliwa kuhusiana na jambo hili.

“Mtu wa kwanza atakayekutana nami kwenye chemchemi ya ‘Kauthar’ na mtu wa kwanza kusilimu ni Ali mwana wa Abu Twalib.”

Vile vile unaweza kusoma kuhusu wanachuoni walioziandika Ahadithi hizi katika juzuu ya tatu ya Al-Ghadir, ukurasa wa 320. ushahidi wa sehemu zote mbili umefikia hatua ya mfululizo na mtu anapojifunza Ahadithi hizi bila ya upendeleo wowote anakuwa na uhakika juu ya Sayyidna Ali (a.s.) kuwa wa mbele zaidi miongoni mwa waumini.

Hivyo basi, mtu huyo hat- apendelea zile kauli nyingine mbili ambazo ni chache kuhusiana na kusimuliwa kwao. Idadi ya wenye kuiunga mkono kauli ya awali (yaani ile isemayo kwamba Sayyidna Ali (a.s.) alikuwa wa awali kusilimu) yenye masahaba wakuu wa Mtume (s.a.w.w.) na wanafunzi wa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) ni zaidi ya sitini.

Idadi hii ni kubwa mno kiasi mwanachuoni Tabari6 aliyeliacha jambo hili wazi na akajitosheleza na kuinakili kauli hii tu, anasema kwamba Ibn Sa’id alimwuliza baba yake:

“Je, Abu Bakr alikuwa mtu wa kwanza kusilimu?” baba yake akamjibu akasema: “La! Kabla ya kusilimu kwake zaidi ya watu hamsini walikuwa wamekwisha izunguuka njia ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Hata hivyo, Uislamu wake ulikuwa bora kuliko Uislamu wa wengine.”

Majadiliano Ya Ma’mun Na Is’haaq

Mwanachuoni Ibn Abd Rabbih amelinukuu tukio la kuvutia katika kitabu chake ‘Aqdul Farid’ liwezalo kuelezwa kwa muhtasari hivi: Mamun aliandaa mkutano wa mdahalo, na yule mwanachuoni mashuhuri, Is’haq alichukua nafasi ya mbele zaidi katika mdahalo huo.

Ilipoanzishwa mada ya Sayyidna Ali (a.s.) kuwatangulia wengine katika kusilimu ikasemwa kuwa Ali alikuwa yu mtoto tu lakini Abu Bakr alikuwa mtu mzima (wakati aliposilimu. Hivyo itikadi yake ina bora kuliko ile ya Ali).

Mara moja Ma’mun akaingilia na kusema: “Je, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimwita Ali kwenye Uislamu wakati wa utoto wake, au itikadi yake ilitokana na msukumo wa Mungu? Kamwe mtu hawezi kusema kwamba itikadi yake ilitokana na msukumo, kwa sababu tukimwachilia mbali Ali, hata itikadi ya Mtume haikuwa ya msukumo ila ilikuwa matokeo ya mwongozo na ujumbe ulioletwa na Jibriil kutoka kwa Allah.

Hivyo basi, Mtume (s.a.w.w.) alipomwita kwenye Uislamu, alifanya hivyo kwa hiari yake au aliamrishwa na Allah kulilenda hilo? Hatuwezi kudhania Mtume (s.a.w.w.) ajitie au amtie mtu mwingine kwenye magumu na majukumu bila ya amri ya Allah.

Hivyo basi, hakuna ujira wowote ila kwamba tuseme kuwa mwito wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) unaungwa mkono na amri ya Mungu. Na je, Mola Mjuzi wa yote anaweza kumwamrisha Mtume wake kumwita kijana asiye na welekevu (ambaye ‘kuwa na itikadi’ au ‘kutokuwa na itikadi’ vyote ni mamoja) kusilimu? Hakika kitendo cha aina hiyo hakiwezekani kwa Allah, Mwenye hekima, Mjuzi wa yote.

“Hivyo basi, hatuna budi kulimaliza jambo hili kwa kusema kwamba itikadi ya Ali ilikuwa itikadi ya kweli na thabiti isiyokuwa duni hata kidogo inapolinganishwa na itikadi ya wengineo na ni Ali bin Abi Twalib ambaye aya za Qur’ani tukufu zifuatazo zilimstahili zaidi:

أُولَٰئِكَ الْمُقَرَّبُونَ {11}

فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ {12}

ثُلَّةٌ مِنَ الْأَوَّلِينَ {13}

“Hao ndio watakaokaribishwa. Katika Bustani zenye neema. Fungu kubwa katika wa mwanzo.” (Surat al-Waaqi’a, 56: 11-13)

  • 1. Bihaarul Anwaar, Juzuu 16, uk. 8.
  • 2. Siirah Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 246.
  • 3. Nahju Balaghah, Juzuu 2, uk. 182.
  • 4. Tarikh-i Tabari, Juzuu 2, uk.211; Tarikh-i Kamil, Juzuu 2, uk. 31-38; na Aa’laamul wara, uk. 25.
  • 5. Katika baadhi ya masimulizi kipindi kimetajwa kuwa ni miaka mitano na kwa mujibu wa dalili nyingi inaweza kusemwa kwamba sehemu ya kipindi hiki kiliki- tangulia kipindi cha kazi ya Utume.
  • 6. Tarikh-i Tabari, Juzuu 1, uk. 215. 225