read

Sura Ya Kwanza: Rasi Ya Bara Arabu

Chimbuko La Utamaduni Wa Kiislamu

Arabia ni Rasi kubwa iliyoko Kusini-Magharibi mwa Bara la Asia. Eneo lake ni kilometa za mraba milioni tatu, karibuni maradufu ya eneo la Iran, mara sita ya lile la Utaliani na mara themanini ya lile la Uswisi.

Rasi hii ina umbo la pembe nne zisizo sawa na inapakana na Palestina na jangwa la Sham kwenye upande wa Kaskazini, na Hira, Mto Tigri, Mto Frati na Ghuba ya Uajemi kwenye upande wa Mashariki, na Bahari ya Hindi kwenye upande wa Kusini, na Bahari ya Sham kwenye upande wa Magharibi.

Hivyo, kwenye upande wa Magharibi na Kusini imepakana na bahari, na kwenye upande wa Kaskazini na Mashariki imepakana na jangwa na Ghuba ya Uajemi.

Tangu kwenye Zama za Kale, nchi hii imekuwa ikigawanywa katika mikoa mitatu:

Mkoa wa Kaskazini na Magharibi unaoitwa Hijaz;
Mkoa wa Kati na Mashariki, uitwao Jangwa la Uarabuni; na
Mkoa wa Kusini, uitwao Yemen.

Kwenye Rasi hii, mtu huyaona majangwa mengi yaliyo mapana na maeneo ya mchanga yenye joto kali ambayo karibuni si yenye uwezo wa kukaliwa na watu. Moja ya majangwa haya ni Baadyah Samawah ambalo siku hizi huitwa Nafusi. Vilevile liko jangwa pana jingine linalotanda hadi kwenye Ghuba ya Uajemi na sasa laitwa Rub’ul Khaali. Hapo awali sehemu moja ya majangwa haya iliitwa Ahqaaf na ile nyingine iliitwa Dahna.

Kutokana na kuwapo kwa majangwa haya, karibuni theluthi moja ya eneo la Rasi hii ni kame na isiyofaa kwa makazi ya wanaadamu. Ni katika nyakati fulani-fulani tu kiasi kidogo cha maji chaweza kupatikana kwenye maeneo machache, ikiwa ni matokeo ya mvua kwenye joto la majangwa hayo, na baadhi ya makabila ya kiarabu huwapeleka ngamia na mifugo yao mingine kwenye maeneo hayo kwa ajili ya malisho.

Hali ya hewa ya Rasi hii ni ya joto sana na kavu kwenye majangwa na kwenye maeneo ya kati. Kwenye maeneo ya pwani kuna unyevunyevu na hali ya hewa isiyo ya joto kali wala baridi kali kwenye baadhi ya sehemu. Ni kwa sababu ya hali yake ya hewa isiyofaa kwamba idadi yake ya wakazi haizidi milioni kumi na tano.

Kwenye nchi hii mna safu ya milima inayonyooka tangu Kusini hadi Kaskazini, kilele chake kina urefu wa meta 2470.

Tangu kwenye Zama za Kale, migodi ya dhahabu na fedha na mawe mengine ya thamani imekuwa asili ya utajiri wa Rasi hii. Kutoka miongoni mwa wanyama waliofugwa na Waarabu, wamo ngamia na farasi. Ama kuhusu ndege, njiwa na mbuni walikuwa wengi kuliko ndege wengine. Siku hizi asili kuu zaidi ya mapato ya Uarabuni ni uchimbaji wa mafuta na gesi. Kituo cha akiba ya mafuta cha Rasi hii ni mji wa Dhahraan ambao Wazungu huuita Dahraan. Mji huu umo kwenye wilaya ya Saudia iitwayo Ahsaa jirani na Ghuba ya Uajemi.

Ili kwamba mheshimiwa msomaji aweze kufahamishwa zaidi kuhusu hali ya Uarabuni, sasa tunaendelea kukupa maelezo marefu kidogo ya ile mikoa mitatu tuliyoitaja hapo juu:

Hijaz: Inajumlisha ukanda wa Kaskazini na Magharibi wa Uarabuni nao unatanda tangu Palestina hadi Yemen, unapakana na pwani ya Bahari ya Sham. Hili ni eneo lenye vilima na lenye majangwa mengi yaliyo kame na maeneo ya mawe mawe.

Mkoa huu una sifa njema zaidi kwenye historia kuliko ile mingine. Hata hivyo, ni dhahiri kwamba hizi sifa njema zilitokana na msururu wa mambo ya kiroho na kidini. Kwa mfano hata kwenye huu wakati wa sasa, Al- Ka’ba, Nyumba ya Allah iliyoko kwenye mkoa huu ni Qiblah cha mamia ya mamilioni ya Waislamu wa Ulimwengu mzima.

Eneo linaloizunguka Al-Ka’ba limekuwa likiheshimiwa na Waarabu na wale wasio Waarabu pia kwa karne nyingi za kabla ya Uislamu. Ikiwa ni dalili ya heshima kwa eneo hili, waliamini kuwa kupigana vita ndani ya mipaka ya Al-Ka’ba ni haramu na hata Uislamu umelitambua eneo lizunguukwalo na mipaka hii kuwa ni lenye kustahili heshima.

Miji ya Makkahh, Madinah na Taa’if ndio miji muhimu ya Hijaz. Tangu kale Hijaz imekuwa na bandari mbili. Ya kwanza ni Jiddah inayowahudumia watu wa Makkahh, na nyingine ni Yanbu, ambayo kupitia hapo, watu wa Madinah huingiza baadhi ya mahitaji yao. Hizi bandari mbili zimo kwenye pwani ya Bahari ya Sham.

Makkah:

Ni mmoja miongoni mwa miji maarufu ya ulimwenguni na ni mji wa Hijaz wenye wakazi wengi zaidi, nao uko kiasi cha meta 300 juu ya usawa wa bahari. Kwa vile mji huu uko baina ya safu za milima miwili, hauwezi kuonekana kwa mbali. Idadi ya wakazi wa Makkahh hivi sasa ni watu 200,000.

Historia Fupi Ya Makkah:

Historia ya mji wa Makkahh huanzia kwenye wakati wa Nabii Ibrahim (a.s.). Nabii Ibrahimu (a.s.) alimpeleka mwanawe Nabii Isma’il (a.s.) pamoja na mama yake Haajar (a.s.) kwenye nchi ya Makkah kuishi hapo. Mwanawe alioa kwenye kabila lililokuwa likiishi karibu na hapo. Nabii Ibarahim (a.s.) aliijenga Al-Ka’ba kwa amri ya Allah na baada ya hapo yalianza makazi ya watu hapo Makkahh.

Ardhi ya viungani mwa mji wa Makkahh kidogo ni ya chumvi na hailimiki kabisa. Kwa mujibu wa baadhi ya wataalamu wa elimu ya nchi za Mashariki, hali yake ya kijiografia iliyo mbaya haina kifani hapa duniani.

Madinah:

Madinah ni mji ulioko umbali wa leagues 90 (Kilometa 432) kaskazini mwa mji wa Makkahh.
Una mabustani na mitende kwenye sehemu zote zizungukazo mji huu na ardhi yake ni yenye kufaa kwa mashamba ya miti na kilimo cha nafaka.

Kabla ya Uislamu mji huu uliitwa Yathrib, lakini baada ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kuhamia mjini humu, ukaitwa Madinatur-Rasul (Mji wa Mtume). Hata hivyo, baadae neno la Mwisho liliachwa ili kuweza kulifupisha na hapo ukaitwa Madinah tu. Historia yatueleza ya kwamba watu wa kwanza kuishi mjini hapa walikuwa ni kikundi cha Amaaliqah. Wale ambao waliowafuatia hao ni tapo moja la Wayahudi na makabila ya Aws na Khazraj ambao baadae walifahamika miongoni mwa Waislamu kwa jina la Ansar (Wasaidizi).

Ukiwa tofauti na mikoa mingine ya Uarabuni, Hijaz ulisalia kuwa salama kutokana na mashambulio ya maadui, na dalili za ustaarabu wa Urumi na Uajemi; falme mbili kubwa za ulimengu wa kabla ya Uislamu, haziwezi kuonekana hapa. Ilikuwa hivyo kwa sababu ardhi yake kame na isiyokalika haikuwezesha kuwafaa wageni kufanya safari za kijeshi ili kuichukua na kisha warudi mikono mitupu, baada ya kuyakabili maelfu ya matatizo yaliyotazimiwa katika kuichukua.

Kuhusiana na jambo hili, mtu anaweza kujifunza hadithi ifuatayo kwa makini. Hadithi hii imenukuliwa na mwanahistoria wa kigiriki aliyeitwa Deodre (aliyeishi kwenye miaka ya kabla ya Masih). Aliandika hivi: “Chifu Mkuu wa kigiriki, Demetrius alipofika Patra (mmoja wa miji ya kale ya Hijaz) kwa lengo la kuitwaa Arabia, wakazi wa mji huo walimwambia: ‘Ewe chifu wa Kigiriki! Kwa nini wapigana nasi? Tunaishi kwenye jangwa ambalo umasikini wa kila namna ndio chanzo cha maisha. Tumelichagua hili jangwa kame ili kwamba tusihitaji kuzitii amri za mtu yeyote. Hivyo basi, tafadhali zipokee zawadi na tuzo zetu duni na uache kuikalia nchi yetu.

Na kama ukiendelea kuishikilia azma yako, basi sisi tunatamka dhahiri ya kwamba, hivi karibuni utakabiliwa na maelfu ya matatizo na magumu. Na ufahamu ya kwamba ‘Wanabti’ hawaelekei kuuacha mtindo wa maisha yao.

Hivyo basi, iwapo utawateka kwa nguvu baadhi ya watu wetu, na ukataka kuwachukua nje ya nchi hii, hili halitakusaidia, kwa kuwa watakuwa watumwa waovu na wenye tabia mbaya tu, na hawatakuwa tayari kuubadili mtindo wao wa maisha.”

Yule chifu wa kigiriki aliukubali ujumbe wao wa amani na kutakiana heri na akaliacha lile wazo la kuishambulia na kuikalia nchi ya Uarabuni.”1

Mkoa wa Kati Na Mashariki: Unaoitwa ‘Jangwa la Uarabuni’ na unaujumuisha Ukanda wa Najd. Ni uwanda wa juu unaokaliwa hapa na pale.

Baada ya familia ya Saudi kushika madaraka, wilaya ya Riyadh, ambayo ndio mji wao mkuu, imekuwa moja ya vituo muhimu vya Uarabuni.

Urefu wa Yemen: Mkoa wa Kusini-Magharibi wa Rasi hii ni kiasi cha kilometa 750, tangu kaskazini hadi kusini na kiasi cha kilometa 400 tangu magharibi hadi mashariki na eneo lake limekisiwa kuwa ni maili za mraba elfu sitini. Hata hivyo, hapo awali, eneo lake lilikuwa hata zaidi ya hapo na kwenye nusu karne iliyopita, sehemu ya mkoa huu (Aden) ilibakia kuwa kwenye hifadhi ya Kiingereza. Hivyo basi, Najd ikawa mpaka wake wa Kaskazini na Aden ikawa mpaka wake wa Kusini.

Bahari ya Sham iko magharibi kwake, na masharikini kwake inaligusa jangwa la ar-Rub’ul Khaali. Mji maarufu wa Yemen ni mji wa kihistoria wa San’a na bandari yake maarufu zaidi ni Hudaydah, iliyoko kwenye pwani ya Bahari ya Sham.

Nchi ya Yemen ndio tajiri zaidi kwenye Rasi hii. Hapo kale ilikuwa na ustaarabu mzuri na mtukufu. Yemen ilikuwa ndio makao makuu ya serikali ya wafalme wa ki-Tababi’ah, waliotawala kwa kipindi kirefu mno. Kabla ya Uislamu Yemen ilikuwa kituo kikuu cha uchumi na biashara, na kwa kweli ilifikiriwa kuwa ni ‘njia panda’ ya Uarabuni. Ilikuwa na migodi tajiri mno ya vito kama vile dhahabu, fedha, na mawe mengine ya thamani yaliyochimbwa huko. Madini hayo yalisafirishwa kwenda kwenye nchi nyingine.

Dalili na mabaki ya ustaarabu wa Yemen wa siku hizo bado vinapatikana. Kwenye kipindi ambacho mwanaadamu hakuweza kupata zana za kutekelezea kazi zenye udhia, watu mastadi wa Yemen waliweza kujenga majengo yapendezayo na marefu kutokana na kufanya kazi kwao kwa nguvu.

Wafalme wa Yemen, kupitia watawala wa nchi waliokubaliwa na watu wote, hawakusita kuhakikisha ya kwamba katiba iliyoandikwa na iliyothibitishwa na wataalamu wa nchi hiyo inatumika, na wakawazidi watu wengine katika kukikuza kilimo na kilimo cha bustani. Amri ndogondogo zinazohusu kilimo cha mashamba na unywesheaji wa makonde na bustani ziliandikwa na zikafuatwa. Kuhusiana na jambo hili, nchi hii yaaminiwa kuwa moja ya nchi zilizokuwa zikisifika na zilizoendelea kwenye zama hizo.

Mwanahistoria maarufu wa Kifaransa, aliyeitwa Gustave Le Bon, anasema: “Uarabuni kote hakuna mkoa uliostawi na ulio na rutuba zaidi ya Yemen.”

Idrisi, mwanahistoria wa karne ya kumi na mbili aliyesifiwa mno anaandika hivi kulihusu jiji la San’a: “Hapa ndipo ulipo mji mkuu wa Uarabuni na makao makuu ya serikali ya Yemen. Majengo na Ikulu za jiji hili ni maarufu ulimwenguni kote. Hata yale majengo na nyumba zake za kawaida zimejengwa kwa mawe ya kuchonga.”

Hizi kumbukumbu zenye kustaajabisha, zilizogunduliwa zikiwa ni matokeo ya ufukuaji na uchunguzi uliofanywa na mustashirik, zathibitisha kuwako sehemu mbalimbali za Yemen ya siku za kale, ambazo ni Ma’arib, San’a na Bilqis.

Kwenye jiji la Ma’arib (jiji maarufu la Saba) yalikuwako majengo marefu mengi yaliyokuwa na milango na matao yaliyotarizwa kwa dhahabu. Halikadhalika vyombo vya dhahabu na fedha pamoja na vitanda vya samadari vilivyotengenezwa kwa metali vilipatikana kwa wingi huko.”2

Moja ya kumbukumbu za kihistoria za Ma’arib ilikuwa ni bwawa lake maarufu, ambalo dalili zake bado zinapatikana. Bwawa hili liliharibiwa na mafuriko yaliyozungumziwa katika Qur’ani Tukufu kwa jina la ‘Mafuriko ya Iram.’

  • 1. Tamaddhun-i-Islam wa Arab, Uk. 93-94
  • 2. Tamaddun-i- Islam wa Arab, uk. 96.