read

Sura Ya Nane:Kipindi Cha Ujana

Ni lazima kiongozi wa jamii awe mvumilivu, mwenye subira, afya timam na nguvu, shujaa na jasiri, asiye na woga na shupavu, na ni lazima awe na moyo mkuu.

Je, yawezekanaje kwa watu waoga, wanyonge wenye fikara dhaifu na wavivu kuiongoza jamii katika kuzipitia njia zenye mambo mengi? Je, watawezaje kuuchukua msimamo maalum mbele ya maadui na kuuhami utu na ukuu wao kutokana na mashambulizi ya watu kwa ujumla?

Ukuu na utukufu wa moyo wa kiongozi na nguvu na uwezo wake wa kimwili na kiroho vina athari ya ajabu kwa wafuasi wake. Wakati Sayyidna Ali, Amirul Muuminina, alipomteuwa mmoja wa wafuasi wake waaminifu kwa ajili ya ugavana wa Misri, aliwaandikia barua wale watu wa Misri walioathiriwa na wengi wao kutolewa nje ya nchi hiyo kutokana na udhalimu wa serikali iliyokuwa ikitawala nchini mle.

Katika barua ile alimsifu gavana wake mteuliwa kwa ushujaa wake na usafi wa moyo wake. Hapa chini tunanukuu mateuzi fulani – fulani kutoka kwenye barua ile ambayo ndani yake sifa halisi za mtawala zimeelezwa: “Ninakuleteeni mja wa Allah asiyelala katika siku za hofu na asiyeonyesha woga anapomkabili adui mwenye hatari. Kwa wale walio waovu yu mkali mno zaidi ya moto uunguzao. Yeye ni Maliki bin Harithi atokanaye na ukoo wa Mazhaj. Yasikilizeni maneno yake, kwa kuwa yeye ni mmoja wa panga za Allah usiokuwa butu na ambao dharuba yake haikosi kuitenda kazi yake barabara.”1

Nguvu Ya Kiroho Ya Mtukufu Mtume (S.A.W.W)

Mtukufu Mtume (s.a.w.w katika kipindi cha utoto na ujana wake dalili za nguvu, ushujaa, umadhubuti na uhodari zilionekana katika paji la uso wa kipenzi cha Waquraishi. Alipokuwa na umri wa miaka kumi na mitano alishiriki katika vita vilivyopiganwa na Waquraishi dhidi ya kabila la Hawaazan na ambavyo viliitwa ‘vita vya Fujjar’ katika vita vile, kazi yake ilikuwa ni kuikinga mishale iliyolengwa ami zake.
Katika Siirah-i-Ibn Hisham2 mwandishi anainukuu sentensi ifuatayo kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Niliikinga mishale mbali na ami zangu.”

Kushiriki kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika vita hivi na vile vile katika umri mdogo kiasi hiki kunatujulisha juu ya ushujaa usio kifani wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na sasa tunaelewa ni kwa nini Imam Ali (a.s.), yule shujaa mkuu zaidi wa mashujaa Amirul Muuminina anasema: “Kila mambo yalipotuwia magumu (sisi askari wa kiislamu) katika mstari wa mbele wa vita tulikimbilia kwa Mtukufu Mtume wa Allah (s.a.w.w.) na hakuna yeyote miongoni mwetu aliyekuwa karibu zaidi na adui kuliko Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe.”3

Tutaitaja misingi ya mafunzo ya kijeshi ya kiislamu katika sura ihusianayo na vita vya Waislamu dhidi ya washirikina, na tutajifunza jinsi ya kupigana kwao, ambako daima kuliichukua sura yake kufuatana na maagizo ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Na jambo hili lenyewe ni moja ya mijadala ivutiayo ya historia ya Uislam.

Vita Vya Fujjaar (Vya Kidhalimu)

Maelezo kamili ya mambo haya yako nje ya lengo la kitabu hiki. Hata hivyo, hapa chini tunaeleza kwa kifupi tu sababu na matukio ya vita hivi ambavyo moja miongoni mwao alishiriki Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ili kwamba wasomaji wangu wapenzi msisalie msiojua lolote juu yake.

Waarabu wa zama za ujinga waliutumia mwaka mzima katika vita na utekaji nyara. Vivyo, kuendelea kwa hali hii ya mambo kuliyafuja maisha yao. Kutokana na jambo hili, hawakupigana katika miezi minne ya mwaka (ambao ni Rajab (mfungo kumi), Dhil Qa’ad (mfungo pili), Dhil-Hajj (mfungo tatu) na Muharram (mfungo nne) ili waweze kuyafungua masoko ya biashara zao katika miezi minne na kujishughulisha na kazi na kujichumia na mahitaji ya maisha.4

Kutokana na maamuzi haya, masoko ya Ukaaz, Mujannah na Dhil-Majaaz yalishuhudia mikusanyiko mikubwa ya watu katika miezi hii minne na marafiki pamoja na maadui walijishughulisha bega kwa bega wakiwa pamoja katika kununua na kuuza pamoja na kujitukuza. Malenga wakuu wa Bara Arabu waliziimba tungo zao. Wayahudi, Wakristo na wenye kuabudu masanamu walizielezea itikadi zao za kidini mbele ya ulimwengu wa kiarabu bila ya woga wowote wa kupata madhara kutoka kwa wapinzani wao.

Hata hivyo, katika kipindi cha historia ya Uarabuni mapatano haya yalivunjwa mara nne, wakati baadhi ya makabila ya kiarabu yaliyojitia katika vita baina yao. Na kwa vile vita hivi vilipiganwa katika miezi ambayo mapigano yaliharimishwa, vinaitwa vita za Fujjar. Sasa tunatoa hapa chini mikhtasari wa vita hivi.

FUJJAR YA KWANZA: Makundi mawili yaliyokuwa yakipigana yalikuwa ni makabila ya Kananah na Hawaazan na chanzo cha vita hivi kimetajwa kuwa ni hiki: Mtu mmoja akiitwa Badr bin Ma’shar alijichagu- lia sehemu katika soko la Ukaaz na akawa anasoma beti za shairi la kujitukuza mbele ya watu kila siku.

Siku moja alisimama na upanga wake mkononi, na akasema: “Enyi watu! Mimi ndiye mwenye kuheshimiwa zaidi na kama mtu yeyote yule atapinga dai langu hili, atakatwa upanga.” Wakati ule akasimama mtu mmoja na akampiga Badr dharuba ya upanga mguuni mwake na akaujeruhi. Kutokana na sababu hii haya makundi maw- ili yalikamatana; lakini yaliacha ugomvi kabla ya kuuawa kwa mtu yeyote yule.

FUJJAR YA PILI: Sababu ya vita hivi ilikuwa kwamba mwanamke mmoja wa kabila la Bani Aamir aliyekuwa mzuri sana aliyavutia macho ya kijana mwanaume aliyemwomba mwanamke yule amwonyeshe uso wake. Yule mwanamke alikataa kufanya hivyo, yule kijana aliyejawa na ashiki alikaa nyuma yake na akayafunga kwa kuyashona pamoja mapaja yake marefu kwa miiba ili kwamba atakapoamka, uso wake uweze kuonekana. Katika tukio hili, wote wawili waliyaita makabila yao. Yale makabila maw- ili yaliacha kupigana baada ya baadhi ya watu kuuawa.

FUJJAR YA TATU: Mtu wa kabila la Kananah alidaiwa na mtu mwingine wa kabila la Bani Aamir yule mdeni alikuwa akichelewa kulipa. Watu hawa walianza kugombana kutokana na sababu hii. Vita vya umwagaji damu vilitishia kuzuka baina ya hayo makabila mawili, lakini, kabla ya hali kuchafuka zaidi, jambo hili liliamuliwa kwa amani.

FUJJAR YA NNE: Hivi ndiyo vile vita alivyoshiriki Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe. Kuna maoni tofauti kuhusiana na umri wake wakati ule. Baadhi ya watu wanasema alikuwa na umri wa miaka kumi na minne au kumi na mitano, wakati wengine wameandika kuwa wakati ule alikuwa na umri wa miaka ishirini. Hata hivyo, kwa vile vita hivi viliendelea kwa kipindi cha miaka minne, inawezekana kwamba maelezo yote haya yanaweza kuwa sahihi.5 Asili ya ugomvi huu imeelezwa kuwa ni hii: Mtu mmoja aliyeitwa Nu’maan bin Manzar alikuwa na desturi ya kuandaa misafara, kila mwaka, na kupeleka bidhaa kule Ukaaz, ili kwamba ngozi, kamba na hariri viweze kuuzwa pale kwa kubadilishwa na bidhaa nyinginezo.

Mtu mmoja aliyeitwa Urwatur Rijaal, aliyetokana na kabila la Hawaazan alichukua jukumu la kuiongoza na kuuhami msafara ule. Hata hivyo mtu mmoja aliyeitwa Baraaz bin Qays, wa kabila la Kanana alipatwa sana mawazo kuhusiana na mtu wa kabila la Hawaazan kutokana na kumzidi. Alimwendea Nu’man bin Manzar na akamlalamikia kuhusu mpango ule lakini alikataliwa. Baraaz alichukizwa na akawa mwenye kijicho na kila mara alikuwa akisubiri apate nafasi ya kumshughulikia Urwatur Rijaal watakapokuwa njiani. Hatimaye alimuua mwenyewe nchi ya Bani Marrah na hivyo akaipaka mikono yake damu ya mtu wa kabila la Bani Hawaazir.

Katika siku hizo, kabila la Waquraishi na Kanaanah yalikuwa washirika na tukio hili lilitukia wakati Waarabu walipokuwa wakijishughulisha na biashara zao katika soko la Ukaaz, mtu mmoja aliwaarifu Waquraishi kuhusu yale yaliyotukia. Hivyo, makabila ya Waquraishi na Kinanah wakazikusanya bidhaa zao mara moja na wakakimbilia kwenye eneo lenye Haram (eneo lililo umbali wa ligi nne au kilometa kumi na tisa hivi, kuzunguuka mji wa Makkah linaitwa Haram. Na kupigana katika eneo hili kuliharimishwa miongoni mwa Waarabu). Makabila haya mawili yaliharakisha hivyo ili wawahi kabla Bani Hawaazin hawajalifahamu tukio lile. Hivyo, mtu mmoja wa kabila la Hawaazin aliwafuatia, kabla ya kuifikia mipaka ya Haramu yalianza mapigano baina ya hizo pande mbili. Hatimaye waliacha mapigano baada ya kuingia usiku.

Makabila ya Waquraishi na Kanaanah waliitumia nafasi hii kwa kutorokea kwenye Haram wakati wa giza, na hivyo wakasalimika kutokana na mashambulio ya maadui. Baada ya siku ile Waquraishi na washirikina wao walitoka kule kwenye Haramu na kati- ka nyakati fulani fulani walipigana na maadui. Katika siku fulani Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) nae alishiriki katika vita hivi pamoja na ami zake kama tulivyoeleza hapo juu. Hali hii ya mambo iliendelea kwa kipindi cha miaka minne. Hatimaye vita vilimalizika kwa kabila la Hawaazin kulipwa fidia ambao wamepoteza watu wengi, ikilinganishwa na lile la Waquraishi.6

Mapatano Ya Vijana

Hapo kale yalikuwapo mapatano yaliyoitwa ‘mapatano ya Fuzul’ miongo- ni mwa watu wa kabila la Jarhami, na kazi ya mapatano haya ilikuwa kuzilinda haki za waliokandamizwa. Kwa mujibu wa mwana historia maarufu aliyeitwa Imaduddin Ibn Kathir, wanachama wa mapatano haya walikuwa Fazal bin Fazalah, Fazal bin Harith na Fazal bin Wadaa’ah.7

Yalikuwa ni kama yale mapatano yaliyofanyika miongoni mwa Waquraishi kadhaa baadae, yalikuwa tofauti na Hilful Fuzul, kutokana na malengo yake (ambayo ni kuzilinda haki za waliokandamizwa), vile vile mapatano haya yaliitwa ‘mapatano ya Fuzul’

Mtukufu Mtume (S.A.W.W) Alishiriki Katika Mapatano Haya

Miaka ishirini kabla ya kuanza kwa kazi ya Utume, mtu mmoja aliwasili Mjini Makkah katika mwezi wa Dhil Qaadah (mfunguo pili) akiwa na bidha kadhaa. Bidhaa hizi zilinunuliwa na Aas bin Waa’il, lakini akashindwa kuzilipia bei waliyo kubaliana. Yule mtu alimwona Mquraishi mmoja aliyekuwa ameketi karibu na Ka’aba. Alianza kulalamika kwa sauti kuu na vile vile akazisoma beti kadhaa zilizoibua watu wenye fikra za heshima. Bwana Zubayr bin Abdul-Muttalib alisimama na watu wengine nao walimwunga mkono. Walifanya mkutano nyumbani mwa Abdullah bin Jad’aan na wakafanya mapatano na wakala kiapo ya kwamba wataungana, na kwa kadiri ya uwezo wao, na katika hali yoyote iwayo, watamfanya mdhalimu aisalimishe haki ya mdhulumiwa kwao. Ulipomalizika utaratibu wa mapatano haya waliamka na kumwendea Aas bin Waa’il. Walizichukua zile bidhaa alizozinunua na akashindwa kuzilipia kisha wakazirudisha kwa mwenyewe.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alishiriki katika mapatano haya yaliyodumisha ustawi wa waliokandamizwa. Mtume (s.a.w.w.) amezungumzia juu ya ukuu wa mapatano haya na simulizi mbili juu ya jambo hili tunazinukuu hapa chini:

“Nyumbani mwa Abdullah bin Jad’aan niliyashuhudia mapatano hayo. Hata hivi sasa (yaani baada ya kuanza kwa kazi ya Utume), kama nikiitwa kwenye mapatano ya aina hiyo nitayakubali (yaani bado ningali mwaminifu juu ya mapatano yale niliyoyafanya)”

Ibn Hisham ananukuu ya kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akizungumzia hivi, kuhusu mapatano hayo: “Siko tayari kuyavunja map- atano yangu, japo nipewe zawadi yenye thawabu mno.”

Mapatano ya Fuzul’ yalikuwa imara mno na yalithibitishwa kwamba hata vizazi vya baadae vilijiona kwamba ni vyenye kuwajibika nayo.
Mfano wake ni tukio lililotokea katika Ugavana wa Walid bin ‘Utbah bin Sufyani, mpwawe (mtoto wa ndugu yake) Muawiya ambaye aliteuliwa na yeye kama gavana wa Madina. Bwana wa Mashahidi, Imam, Husein bin Ali (a.s.) ambaye katu maishani mwake hakupata kuisalimu amri ya udhalimu aliwahi kutofautiana na Gavana huyu wa Madina kuhusu mambo ya fedha. Gavana huyu, daima aliitegemea nguvu ya jimboni mle na ile ya serikali kuu (ya Sham), na alikuwa na kawaida ya kuwatoza raia zake kodi kubwa zaidi ya ilivyostahili.

Ili kuuvunjilia mbali msingi wa madhalimu na kuwafahamisha watu haki zao za kupata utawala wa haki, Imam Huseni (a.s.) alimgeukia Gavana yule na kumwambia: “Naapa kwa jina la Allah, kila utakaponitoza kodi kubwa kuliko vile inavyostahiki, nitauweka mkono wangu katika upanga na nitasimama katika Masjidun-Nabi na nitawaitia watu katika mapatano yaliyofanywa na jadi zao.”

Miongoni mwa wale waliokuwepo pale ni, Bwana Abdallah bin Zubair aliamka na kuirudia sentensi ile ya Imam (a.s.) na akaongeza kusema: “Sisi sote tutaamka na kuichukua haki yake au tuuawe katika njia hii.” Pole pole mwito wa Imam Husein bin Ali uliyafikia masikio ya watu wenye fikara tukufu kama vile Mansur bin Mukhramah na Abdur Rahman bin Uthman na wote wakauen- dea upesu upesi mlango mtakatifu wa Imam, wakisema: “Tuko hapa!” Matokeo yake yalikuwa kwamba yule Gavana, akichelea maasi ya watu aliacha kuwatoza watu kodi kubwa kuliko ilivyostahili.8

  • 1. Nahju Balaghah, Juzuu 3, uk. 92.
  • 2. Juzuu 1, uk. 186. anaitafsiri kwa namna ile ile tuliyoieleza.
  • 3. Nahjul Balaghah, Juzuu 3, uk. 314.
  • 4. Kutokana na aya ya 36 ya Surah al-Tawbah tunaweza kuona kwamba kuharimishwa kwa vita katika miezi hii minne kuna asili ya kidini na Waarabu hawakuyachupa maharamisho haya.
  • 5. Tarikh-i-Kamil, Juzuu 1, uk. 358-359 na Siirah-i-Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 184.
  • 6. Siirah’i-Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 184-187.
  • 7. Al-Budaayah Wal-Nihaayah , Juzuu ya 2, uk. 292.
  • 8. Siirah-i-Halabi, Juzuu 1, uk. 155-157.