read

Sura Ya Nne: Jadi Wa Mtukufu Mtume (S.A.W.W)

Nabii Ibrahm (A.S.), Bingwa Wa Imani Ya Mungu Mmoja.

Lengo la kutoa taarifa za maisha ya Nabii Ibrahim (a.s.) ni kuwajulisha wasomaji jadi zake Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) kwa kuwa yeye Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alikuwa ni kizazi cha Nabii Isma’il (a.s.) aliyekuwa mwana wa Nabii Ibrahim (a.s.). Na kwa vile watu hawa waw- ili watukufu pamoja na halikadhalika na jadi wengine wengi watukufu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) wengi wana fungu kubwa katika hisoria ya Bara Arabu na Uislamu, ni bora kwamba taarifa fupi ya maisha yao itolewe hapa, kwa sababu matokeo ya historia ya Uislamu, kama zilivyo pete za mnyororo, yana uhusiano kamili na yale matukio yaliyotukia kwenye wakati ule ule wa kuanza kwa Uislamu pamoja na yale ambayo kwa kadiri fulani yalikuwa yakitokea kwenye sehemu za mbali kutoka yalipo.

Kwa mfano, ulinzi na msaada alioupata Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kutoka kwa Abdul-Muttalib, upendeleo alioupata na taabu alizozipata Abu Twalib (as) kwa ajili yake, ukuu wa familia ya Hashim na chanzo cha uhasama wa Bani Umayyah (dhidi ya familia ya Hashim) vinafikiriwa kwamba ni matukio muhimu yanayounda msingi wa historia ya Uislamu. Ni kwa sababu hii kwamba sura moja ya historia ya Uislamu iwekwe kwa kuyajadili matukio haya.

Tunayakuta matukio yaliyo mashuhuri na yenye kuonekana dhahiri, ya maisha ya Nabii Ibrahim (a.s.). Ni vigumu kuzisahau juhudi zake katika kuiinua bendera ya Upweke wa Mungu na kuing’oa ibada ya masanamu na watu. Halikadhalika midahalo yake mikuu na ya adabu njema aliyoifanya baina yake na wenye kuziabudu nyota, iliyonukuliwa na Qur’ani Tukufu kwa lengo la kuwaelimisha na kuwaongoza watu, ni mafundisho matukufu zaidi juu ya itikadi ya upweke wa Mungu kwa ajili ya wenye kuutafuta ukweli.

Kwa Nini Kuabudu Viumbe Kulitokea

Sababu iliyomfanya mwanadamu kuviabudu viumbe si yoyote nyingine ila ni ujinga ulioandamana na maamrisho ya maumbile (ambayo, ikiwa ni kanuni ya ujumla, hukiamini kisababisho cha kila tukio).

Kwa upande mmoja, mwanadamu anapokuwa yu mwenye kutawaliwa na maumbile alilazimika kukimbilia kwenye sehemu fulani fulani, kuifikiria mamlaka yenye kushinda na yenye nguvu itoshelezayo katika kuumba utaratibu huu usio kifani na kuzifikiri nakshi zenye kupendeza kwenye maumbo mbalimbali kuwa ni kazi ya kistadi ya mchoraji. Hata hivyo, kwa upande mwingine, kwa kuwa mwanaadamu anataka kuipita njia hii bila ya mwongozo wa Manabii, ambao ndio viongozi wa Mwenyezi Mungu, nao wame- teuliwa ili kuusalimisha ukamilifu wa hii safari ya kiroho ya mwanaadamu, alikimbilia kwenye viumbe visivyo na uhai pamoja na wanyama na wanadamu kabla ya kulifikia lengo lake sahihi (yaani Allah, Mungu wa Pekee) na kuipata njia yake kwa kuzichunguza dalili za maumbile na kukimbilia Kwake.
Hivyo basi, alivifikiria viumbe hivyo kuwa ndivyo yale malengo anayoyatafuta. Kwa sababu hiyo, wanachuoni, baada ya kuvisoma vitabu vya Mwenyezi Mungu na jinsi Mitume walivyowaita watu kwa Mungu na midahalo yao na watu hao, walikiri kwamba lengo la Mitume halikuwa kuwafanya watu waamini kuwako kwa Mwumba wa Ulimwengu. Kwa kweli, kazi yao halisi katika jamii ilikuwa kuwafanya watu kuwa huru kutokana na makucha ya ushirikina na ibada ya masanamu. Kwa usemi mwingine ni kuwa, wamekuja kuwaambia watu, “Enyi watu! Allah, Ambaye kuwako Kwake twakuamini sisi sote Yuko hivi na wala Hayuko vile; Yeye Yu Mmoja tu, wala si wawili. Msiwape viumbe nafasi ya Allah. Mkubalini Allah kuwa Yu Mmoja tu. Msimkubali mshirika yeyote au mwenzi wake.”

Sentensi isemayo: “Hakuna Mungu ila Allah”, hutoa ushuhuda uangazao juu ya yale tuliyoyasema hapo juu. Huo ndio mwanzo wa mahubiri ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w). Maana ya sentensi hii ni kwamba, hakuna apasikaye kuabudiwa ila Allah, na kusema hivyo kwalazimu kwamba kuwako kwa huyo Mwumba ni ukweli ukubalikao, ili kwamba watu waweze kuitwa kwenye kuukubali “Upweke” na “Umoja” wake. Sentensi hii yaonyesha kwamba, machoni mwa mwanadamu wa zama zile, sehemu ya kwanza (yaani kwamba Ulimwengu unaye Allah) si jambo la kupingana. Tukiliachilia mbali jambo hili, kujifunza hadithi za Qur’ani Tukufu na mazungumzo ya Mitume na watu, hulifafanua zaidi jambo hili. 1

Mahali Alipozaliwa Nabii Ibrahim (A.S.)

Mtetezi wa imani ya Mungu Mmoja alizaliwa katika mazingira yaliyozagaa giza la ibada ya masamu na ya wanadamu. Mwanadamu alionyesha unyenyekevu mbele ya masanamu aliyoyatengeneza kwa mikono yake mwenyewe na vilevile mbele ya nyota. Katika hali hizi, jambo lililoliinua daraja la Nabii Ibrahim (a.s.) na kuzivika taji juhudi zake kwa ushindi lilikuwa ni uvumilivu na ustahimilivu wake.

Mahali alipozaliwa yule mshika bendera wa imani ya Mungu Mmoja palikuwa ni Babeli (Babylon). Wanahistoria wamekuwa wakiifikiria sehemu hii kuwa ni moja ya maajabu saba ya ulimwengu na wameyarekodi masimulizi mengi kuhusu utukufu na ukuu wa ustaarabu wa nchi hii.

Mwanahistoria maarufu wa Kigiriki Herodote (aliyeishi kati ya mwake 484 – 425 kabla ya Masihi) aliandika hivi: “Babeli ilijengwa kwa umbo la pembemraba. Kila upande wake ulikuwa na urefu wa ‘league’ 120 (‘league’ moja ni kiasi cha kilometa tano hivi) na kizingo chake kilikuwa ‘league’ 480”.2 Vyovyote vile iwavyo maelezo haya yawezavyo kutiwa chumvi zaidi, yanaudihirisha ukweli usiokatalika (yanaposomwa pamoja na maandishi mengine).

Hata hivyo, siku hizi, miongoni mwa hayo mandhari na majengo marefu yenye kuvutia hakuna chochote kiwezacho kuonekana ila kichunguu cha udongo baina ya Mito Tigrisi na Furati, kilichofunikwa na kimya cha kifo. Wakati mwingine kimya hiki huvunjwa na wataalamu wa elimu ya nchi za mashariki (mustashirik) kupitia uchimbaji wanaoufanya ili kupata taarifa za ustaarabu wa Wababeli.
Nabii Ibrahim (a.s.) msanifu wa itikadi ya upweke wa Mungu, alizaliwa katika zama za utawala wa Namrud mwana wa Kan’an. Ingawa Namrud alikuwa mwenye kuabudu masanamu, vile vile alidai kuwa yu Mungu na akijinufaisha kutokana na ujinga wa umma wenye wepesi wa kuamini bila ya kuhitaji ushuhuda, alizitia itikadi zake akilini mwao. Yaweza kuonekana kwamba ni jambo lenye kushangaza kuwa mtu anaweza akawa mwenye kuabudu masanamu na pia adai kuwa yu mungu. Hata hivyo, Qur’ani Tukufu inatupa mfano wa itikadi hii. Nabii Musa (a.s.), mwana wa Imran alipoyatingisha madaraka ya Firauni kwa mantiki yake yenye nguvu na akaukanusha uongo wake kwenye mkutano wa hadhara, wale waliomwunga mkono Firauni walimwambia Firauni:

وَقَالَ الْمَلَأُ مِنْ قَوْمِ فِرْعَوْنَ أَتَذَرُ مُوسَىٰ وَقَوْمَهُ لِيُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَيَذَرَكَ وَآلِهَتَكَ ۚ {127}

“Kundi toka kaumu ya Firaun likasema: Je, utamwacha Musa na kaumu yake walete uharibifu katika nchi na kukuacha wewe na miungu yako…” (Al-Araaf, 7:127).

Inafahamika wazi kwamba Firauni alikuwa akidai kuwa yu mungu na alikuwa na kawaida ya kutangaza akisema: “Mimi ndimi mola wenu mkuu.” Hata hivyo, aya hii yaonyesha kwamba, ijapokuwa Namrud alikuwa na itikadi na dai hilo, vile vile alikuwa akiyaabudu masanamu.

Ulinzi mkubwa zaidi aliojipatia Namrud ulikuwa ni kujipatia msaada wa wanajimu na wapiga ramli, watu waliokuwa wakifikiriwa kuwa ndio wenye hekima wa zama zile. Haitakuwa kosa kusema kwamba, unyenyekevu wao mbele ya Namrud uliimarisha njia ya Namrud kuyanyonya matabaka ya watu wenye kukandamizwa na wajinga. Zaidi ya hapo, baadhi ya jamaa zake Nabii Ibrahim (a.s). – kwa mfano Azar aliyeyatengeneza masanamu na ambaye pia alikuwa mjuzi wa unajimu) walikuwa miongoni mwa wafuasi wa Namrud. Jambo hili lenyewe lilikuwa kizuizi kwa Nabii Ibrahim (a.s.) kwa kuwa, zaidi ya kupambana na itikadi za ujumla, vile vile aliwajibika kuukabili upinzani wa ndugu zake mwenyewe.

Namrud alikuwa kazama kwenye bahari ya itikadi za kishirikina. Alikuwa amelitandaza zulia la kufanyia tafrija na kunywa pale wanajimu walipoipiga kengele ya kwanza ya hali ya hatari na kusema: “Serikali yako itaan- guka kupitia kwa mtu ambaye yu mwana wa ardhi hii.” Hofu ya ndani ya Namrud iliamshwa na akasema: “Je, mtu huyo tayari kaishazaliwa au bado?” Wanajimu walimjibu ya kwamba alikuwa bado Hajazaliwa. Hapo Namrud akaamrisha wanawake watengwe na wanaume (kwenye usiku ambao, kutegemeana na matabiri na maamuzi ya wanajimu mimba ya mtu huyu aliye adui itabebwa). Hata hivyo ingawa lilitendeka hilo, wauaji wake waliwaua watoto wa kiume. Wakunga waliamrishwa kupeleka taarifa juu ya watoto waliozaliwa kwenye ofisi maalum.

Katika usiku huo huo mimba ya Nabii Ibrahim (a.s.) ilitunga. Mama yake akawa mjamzito na kama vile alivyokuwa mama wa Nabii Musa (a.s.), mwana wa Imran, aliificha habari ya ujauzito wake hadi mwishoni. Baada ya kujifungua alilikimbilia pango lililokuwa karibu na mji wake, ili kuyahami maisha ya mwanawe mpenzi. Alimwacha mwanawe yule pembeni mwa pango lile na kulitembelea katika nyakati za mchana au usiku, kwa kadiri hali ilivyomruhusu. Matokeo ya udhalimu huu ni kwamba, kwa kadiri muda ulivyopita, Namrud alijipatia amani ya kifikra, na akaamini ya kwamba amemchinja adui wa kiti chake cha enzi na utawala wake.

Nabii Ibrahim (a.s.) aliitumia miaka kumi na mitatu ya uhai wake kwenye pango lile lililokuwa na njia nyembamba ya kupitia na kisha mama yake akamtoa. Alipotokea mbele ya watu, wale waliomuunga mkono Namrud walidhania kwamba alikuwa mgeni nchini mle.

Hivyo mama yake akasema: “Huyu ni mwanangu. Alizaliwa kabla ya utabiri waliotabiri wanajimu.”3

Nabii Ibrahim (a.s.) alipotoka mle pangoni aliimarisha itikadi yake asilia katika upweke wa Mungu kwa kuichunguza dunia na mbingu, kumetameta kwa nyota na ubichi wa miti. Aliishuhudia jamii ngeni ya ajabu na kushangaza.

Aliliona kundi la watu waliokuwa na tabia ya kipuuzi ya kuzielekeza nyuso zao kwenye nyota zimetametazo. Vile vile aliwaona baadhi ya watu ambao kiwango chao cha akili kilikuwa chini kuliko kile cha wengine. Walitengeneza masanamu kwa mikono yao na kisha wakayaabudu.

Kitu kilichokuwa kibaya zaidi miongoni mwa vitu hivi ni kwamba, mwanadamu, akijichukulia faida isiyo ya haki kutokana na ujinga na upuuzi wa watu, alidai kuwa yu mungu wao na akajitangaza kuwa yeye ndiye yule aliyevihuisha viumbe vyote na kuyaamuru matukio yote. Nabii Ibrahim (a.s.) alilazimika kujitayarisha kupambana katika mistari ya mbele wa mapambano hayo matatu. Qur’ani Tukufu imeisimulia hadithi ya kampeni zake kwenye hii mistari ya mbele mitatu.

Kampeni Ya Nabii Ibrahim Dhidi Ya Ibada Ya Masanamu

Giza la ibada ya masanamu limeenea katika nchi nzima ya Babel, na mahali alipozaliwa Nabii Ibrahim (a.s.): Miungu mingi ya kidunia na ya kimbinguni imeyanyima matabaka mbali mbali ya jamii uwezo wao wa kufikiri na ujuzi. Baadhi ya watu hawa waliifikiria miungu hiyo kuwa yenyewe inayo nguvu, ambapo wengine waliwafikiria kuwa ni wasila (njia) wa kuipatia radhi ya Mwenyezi Mungu.

Siri Ya Ushirikina

Waarabu wa kabla ya Uislamu waliamini kwamba kila kiumbe na kila tukio halina budi kuwa na kisababisho maalum na kwamba Allah Aliye Mmoja tu hana nguvu za kuviumba vyote hivyo.

Hii ilitokana na ukweli wa kwamba kwenye zama zile, sayansi ilikuwa bado kugundua uhusiano uliopo baina ya viumbe na matukio mbali mbali. Matokeo yake ni kwamba watu wale walidhania kwamba viumbe vyote na matukio ya kimaumbile ni vitu tofauti na visivyohusiana. Kwa sababu hii walilazimika kumfikiria Mungu mwenye kujitegemea kwa kila tukio kama vile mvua na theluji, tetemeko la ardhi na kifo, njaa na upungufu, amani na utulivu, ukatili na umwagaji wa damu n.k. Hawakuuwazia ukweli uliopo kwamba ulimwengu mzima ni mmoja na sehemu zake zote zinafungama, na kila moja miongoni mwazo inayo athari kwa zile nyingine.

Akili isiyoelimika ya mwanadamu wa siku zile ilikuwa bado haijaitambua siri ya kumwabudu Allah Aliye Mmoja tu na haikutambua kwamba Allah, Anayeutawala ulimwengu wote Yu Mola mwenye nguvu zote na Mjuzi wa yote. Yeye Yu Muumba Aliye huru kutokana na kila aina ya unyonge na upungufu, Uwezo Wake, ukamilifu Wake, elimu Yake na hekima Yake havina kikomo.
Yu juu ya kila kitu kiwezacho kufikiriwa kuwa ndio Yeye. Hakuna ukamilifu Asiokuwa nao. Hakuna kitu kiwezekanacho Asichoweza kukiumba. Yeye ndiye Allah Aliye Mmoja tu, Mwenye uwezo wa kuviumba viumbe na matukio yote bila ya msaada na kuungwa mkono na mtu yeyote. Anaweza kuviumba viumbe na matukio mengine kwa jinsi ile ile Aliyoviumba hivi vilivyoko hivi sasa. Hivyo basi, kutegemeana na akili, kuwako kwa wasila wa mamlaka yawezayo kuwa kando na uhuru wa mapenzi ya Allah Asiye kifani ni jambo lisilokubalika.

Itikadi ya kwamba ulimwengu una waumba wawili, mmoja wao akiwa yu asili ya mema na nuru, na mwingine yu asili ya uovu na giza vile vile haikubaliki. Na itikadi kwamba kuna wasila wa watu fulani kama vile Mariamu na Isa kuhusiana na mambo ya uumbaji wa Ulimwengu, au kwamba utawala wa ulimwengu wa kimaada (huu uonekanao) umewekwa mwenye mamlaka ya mwanaadamu, ni udhihiriaho wa ushirikina na kuongezea chumvi. Mwenye kuuamini Upweke wa Allah ni yule ambaye, ukiwaachilia mbali Mitume na Mawalii, hukihifadhi cheo cha Mwumba wa huu ulimwengu na haihusishi kazi ya mmoja wao na mwingine.

Njia waliyoitumia Mitume katika kuwafunza na kuwaongoza watu ni ile ya mantiki, (kutumia hoja) na akili, kwa kuwa walihusika na akili za wanaadamu. Walitamani kuijenga serikali ipasikayo kujengwa chini ya msingi wa imani, elimu na uadilifu, na serikali ya namna hiyo haiwezi kujengwa kwa kutumia ugomvi, vita, na umwagaji wa damu. Hivyo basi, hatuna budi kutofautisha baina ya serikali ya Mitume na serikali ya Firaun na Namrud. Lengo la kundi la pili ni usalama wa utawala na serikali zao kwa kuzitumia njia zote ziwezekanazo, japo nchi zao zianguke baada ya kufariki kwao dunia.

Kwa upande mwingine, watu wa kimungu hupenda kuunda serikali itakayokuwa na njia katika maisha ya mtu sirini na katika hadhara, awe mtawala huyo yu mwenye nguvu au dhaifu katika wakati wowote ule maalum, au awe yu hai, au kaisha kufa. Hakika lengo hili haliwezi kufikiwa kwa kutumia nguvu au shinikizo.

Mwanzoni kabisa Nabii Ibrahim (a.s.) alifanya kampeni dhidi ya itikadi ya nduguze (yaani wenye kuabudu masanamu), ambao miongoni mwao ni Azar aliyekuwa na cheo kikuu zaidi. Alikuwa bado Hajapata ushindi kamili kwenye jambo hili alipolazimika tena kupigana kwenye nyanja nyingine ya mapambano. Kiwango cha fikara za hili kundi la pili kilikuwa juu kidogo na kilichoeleweka kuliko kile cha kundi la kwanza, kwa kuwa, kinyume na dini ya jamaa zake Nabii Ibrahim (a.s.), watu hawa wamevitupilia mbali viumbe duni na visivyo na faida vya kidunia na wakawa wanaziabudu nyota za mbinguni.

Nabii Ibrahm (a.s.) alipokuwa akifanya kampeni dhidi ya ibada ya nyota, alianza kwa maneno mepesi, ukweli mchache wa kifalsafia na kisayansi uliokuwa bado haujazingatiwa akilini mwa watu wa zama zile na hata siku hizi, hoja zake hizi zinawabumbuaza wanachuoni wenye utaalamu wa mantiki na midahalo. Zaidi ya hayo yote, vile vile Qur’ani Tukufu imezinukuu hoja za Nabii Ibrahim (a.s.) na mwandishi wa kitabu hiki anayo heshima kuziingiza tena hoja hizo kwenye kurasa hizi pamoja na maelezo mafupi.

Baada ya kutoka mle pangoni, Nabii Ibrahim (a.s.), ili aweze kuwaongoza watu aliukodolea macho usiku na kutazama mbinguni wakati wa kuchwa kwa jua na akabakia kuwa macho hadi lilipokuchwa jua tena katika siku ya pili. Katika kipindi hiki cha masaa ishirini na manne alihojiana na kuzungumza na makundi matatu na kuzikanusha itikadi zao kwa hoja zenye nguvu.

Giza la usiku liliingia na kuzificha dalili zote za uhai. Nyota angavu, ‘Zuhura (Venus)’ ilitokea kwenye pembe ya upeo wa macho.
Ili kuwaridhisha wenye kuabudu nyota ya Zuhura, Nabii Ibrahim (a.s.) alikubaliana nao na akajisingizia kuufuata msitari wao na akasema: “Huyu ndiye Mola wangu.” Hata hivyo, ile nyota ilipozama na kutoweka kwenye pembe ya anga, akasema: “Siwezi kumkubali Mungu mwenye kuzama.” Kwa hoja hii yenye nguvu, aliikana itikadi ya wanaoabudu Zuhura na kuuthibitisha uongo wa ibada yao hiyo.

Katika hatua nyingine macho yake yaliuangukia ungo angavu wa mwezi na kwa uangavu wake wenye kuvutia na uzuri. Ili kuwapendeza wenye kuuabudu mwezi, alikubali wazi wazi kuwa ni Mungu, lakini baadae aliipasua vipande vipande itikadi hii nayo kwa hoja zake zenye nguvu. Ilitokea kwamba, mkono wenye nguvu wa Mungu uliufanya ule mwezi nao uzame kutoka kwenye upeo wa macho na mng’ao wake kutoweka nchini. Nabii Ibrahim (a.s.), pasi ya kuzidhuru hisia za wenye kuabudu mwezi, alisema huku akiwa na maono yenye ukweli: “Kama Mola wangu wa kweli hataniongoza, hakika nitapotea, kwa sababu Mungu huyu anazama kama vile zizamavyo nyota, nao wenyewe umo kwenye utaratibu maalum na mpangilio uliotengenezwa na mtu fulani, mwingine.”

Giza la usiku lilikoma na jua likachomoza, na kukipasua kifua cha upeo wa macho na likaanza kuitawanya miali yake ya rangi ya dhahabu kwenye uso wa nchi. Wenye kuliabudu jua walizigeuzia nyuso zao kwa Mungu wao. Ili kuzitimiza kanuni za mdahalo, Nabii Ibrahim (a.s.) nae aliukubali Uungu wake. Hata hivyo, kuzama kwa jua lile kulithibitika utii kwenye utaratibu maalum wa ulimwengu na Nabii Ibrahim (a.s.) alikana waziwazi kupasika kwake kuabudiwa. (Taz. Surah al-An’am, 6:75 –79).

Hakuna shaka kuhusu ukweli uliopo kwamba pale alipokuwa akiishi mle pangoni, Nabii Ibrahim (a.s.), kupitia kwenye upendeleo usio kifani wa Mwenyezi Mungu alijipatia elimu juu ya Upweke wa Allah kutoka chemchemi ya Yule Asiyeonekana (Allah), elimu ambayo ni maalum kwa Mitume. Hata hivyo, baada ya kuzichunguza na kujifunza hizi sayari za angani aliipa elimu ile umbo la hoja. Hivyo basi ukiachilia mbali kule kuwaonyesha njia iliyonyooka wale watu waliopotea na kuwapatia mwongozo, ameacha hazina ya elimu yenye thamani isiyo kifani iwezayo kutumiwa na wale wautafutao ukweli.

Ufafanuzi Wa Mantiki Ya Nabii Ibrahim (A.S.)

Nabii Ibrahim (a.s.) alitambua ya kwamba Allah Anautawala ulimwengu, lakini swali lilikuwa kwamba ni iwapo chanzo kile cha nguvu ni hizi sayari za mbinguni, au ni Yule Mwenye nguvu zote na aliye bora kuliko sayari hizi.

Baada ya kujifunza hali ya sayari hizi zizungukazo huko na huko aligundua ya kwamba sayari hizi zing’aazo na kutoa nuru zinawajibika kuchomoza, kuzama, kupunguka na kutoweka kwa mujibu wa utaratibu maalum na zinazunguka kwenye mihimili yao katika njia isiyo badilika, na jambo hili, lenyewe lathibitisha ya kwamba zinayatii utashi wa mtu fulani mwingine, na nguvu iliyo kuu na yenye uwezo zaidi inazidhibiti na kuzifanya zipite kwenye mzunguko maalum.

Hebu natulielezee jambo hili zaidi: Ulimwengu una “Uwezekano” na “Mahitaji.” Viumbe mbali mbali na matukio ya kimaumbile katu hayako huru kutokana na kumhitaji (Muumba) Mwenye nguvu zote. Yanamhitaji Allah Mjuzi wa yote katika kila sekunde ya mchana na usiku – Allah Ambaye wakati wowote ule, hatakuwa msahaulifu wa mahitaji yao. Sasa, kuzihusu hizo sayari za mbinguni, zinakuwako na ni zenye faida katika wakati fulani na hutoweka na kutokuwa na faida kwenye wakati mwingine. Viumbe vya aina hiyo havina sifa za lazima katika kuwa miungu ya viumbe vingine na kuyatimiza mahitaji yao.

Nadharia hii inaweza kupendekezwa katika namna ya maelezo mbalimbali ya kinadharia na kifalsafia. Kwa mfano tunaweza kusema: Sayari hizi za angani ziko katika mwendo na zinasogea kwenye mihimili yao. Iwapo kama mwendo wao hauna hiari na uko kwenye shurutisho, basi ni lazima uwepo mkono wenye nguvu wenye kuzitawala.

Na kama mwendo wao unategemeana na hiari yao, ni haki ionekane ni nini shabaha ya mwendo huu. Kama zinasogea ili zipate ukamilifu nazo ni kama vile ilivyo mbegu inayoinukia kutoka ardhini na kukua hadi ikawa mti na ukazaa matunda, jambo hili litalazimika kuwa na maana ya kwamba zinahitaji aina ya nguvu yenye huruma, yenye uwezo, yenye akili na iliyo huru itakayoutoa upungufu wao na kuzipa sifa ya ukamilifu.

Lakini, kama mwendo na mizunguko yao yaelekea kwenye unyonge, na kasoro, nazo ni kama mtu aliyeupita ujana wake na kaingia upande wa uzeeni wa umri wake, basi mwendo wao utakuwa ni mwelekeo wa kwenye upungufu na maangamio, na katu hautaafikiana na daraja ya Mungu Apasikaye kuutawala ulimwengu na vile vyote vilivyomo ndani yake.

Mbinu Za Majadiliano Na Midahalo Waliyoitumia Mitume

Historia ya Mitume yaonyesha kwamba waliianza kazi ya kuitengeneza jamii kwanza kwa kuwaita jamaa zao kwenye njia ya kweli na kisha wakauendeleza ‘mwito’ huo hadi kwa watu wengine. Hivi ndivyo hasa alivyofanya Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) mara tu baada ya kuteuliwa kwake kuifanya kazi ya Utume. Kwanza kabisa aliwaita watu wake mwenyewe kwenye Uislamu na akaujenga msingi wa ‘Ujumbe’ wake kwenye mabadiliko yao, kufuatana na amri ya Allah:

وَأَنْذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ {214}

“Na uwaonye jamaa zako wa karibu zaidi.”(Surah al-Shu’araa, 26:214).

Nabii Ibrahim (a.s.) naye aliitumia njia hii na kwanza akayafanya mabadiliko ya watu wake. Azar alikuwa na cheo kikuu sana miongoni mwa ndugu zake, kwa sababu, ukiachilia mbali kwamba alikuwa msomi na msanii, vile vile alikuwa mnajimu mahiri. Katika baraza la mfalme Namrud, neno lake lilichukuliwa kuwa ni lenye nguvu na maamuzi yake ya kinajimu yalikubaliwa na wazee wote wa baraza kuwa ni sahihi.

Nabii Ibrahim (a.s.) alitambua ya kwamba kama angeliweza kumvutia Azar kwenye upande wake, angalikuwa ameikamata ngome yenye nguvu ya wenye kuyaabdudu masanamu. Hivyo basi, alimshauri kwa njia iliyo nzuri mno kwa kadiri alivyoweza, kutoviabudu viumbe visivyo na uhai. Hata hivyo, kutokana na sababu fulani fulani Azar hakuupokea ujumbe na ushauri wa mpwawe, Nabii Ibrahim (a.s.).

Hata hivyo, kwa kadiri tuhusikavyo hapa, jambo lililo muhimu zaidi katika hadithi hii ni ile njia ya kuitia (kwenye ujumbe wa Allah) na jinsi ya kuzungumza alikozungumza Nabii Ibrahim (a.s.) na Azar.

Ukizichunguza kwa undani na kwa uangalifu aya za Qur’ani Tukufu zilizoyanukuu mazungumzo haya huidhihirisha zaidi ile njia ya majadiliano na uitaji (wa kwenye njia ya Allah). Sasa hebu natuone ni njia gani aliyoitumia Nabii Ibrahim (a.s.) kumwitia Azar kwenye njia sahihi:

Alimwambia ami yake:

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنْكَ شَيْئًا {42}

يَا أَبَتِ إِنِّي قَدْ جَاءَنِي مِنَ الْعِلْمِ مَا لَمْ يَأْتِكَ فَاتَّبِعْنِي أَهْدِكَ صِرَاطًا سَوِيًّا {43}

يَا أَبَتِ لَا تَعْبُدِ الشَّيْطَانَ ۖ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلرَّحْمَٰنِ عَصِيًّا {44}

يَا أَبَتِ إِنِّي أَخَافُ أَنْ يَمَسَّكَ عَذَابٌ مِنَ الرَّحْمَٰنِ فَتَكُونَ لِلشَّيْطَانِ وَلِيًّا {45}

قَالَ أَرَاغِبٌ أَنْتَ عَنْ آلِهَتِي يَا إِبْرَاهِيمُ ۖ لَئِنْ لَمْ تَنْتَهِ لَأَرْجُمَنَّكَ ۖ وَاهْجُرْنِي مَلِيًّا {46}

قَالَ سَلَامٌ عَلَيْكَ ۖ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي ۖ إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا {47}

“Alipo mwambia baba yake: Ewe baba yangu! Kwa nini unamwabudu asiyesikia na asiyekufaa chochote? Ewe baba yangu! Bila shaka nimefunuliwa ukweli juu ya siri nyingi; hivyo basi, nifuate, ili nikuongozee kwenye njia iliyo sawa. Ewe baba yangu! Usimwabudu shetani, kwa kuwa yu mwasi kwa (Allah) Mola wa Rehema. Baba yangu! Hakika mimi ninahofia ya kwamba itakugusa adhabu kutoka kwa (Allah) Mwingi wa rehema na kwamba uwe rafiki wa shetani.” Akasema: Je, unaichukia miungu yangu, ewe Ibrahim? kama huachi lazima nitakupiga mawe na uniondokelee mbali kwa muda?(Ibrahim) akasema; Amani iwe juu yako, nitakuombea msamaha kwa Mola wangu, kwani yeye ananihurumia sana. (Surat Maryam; 19:42-47)

Azar akiujibu mwito wa Nabii Ibrahim (a.s.) alisema: “Ewe Ibrahim! Unathubutu kuikanusha miungu yangu? Acha upuuzi (wako) huu, au sivyo utarujumiwa hadi ufe. Toka nyumbani mwangu upesi sana.”

Mnyoofu Ibrahim (a.s.) aliivumilia kauli hii mbaya ya Azar na kwa utulivu kamili, na akajibu: “Amani na iwe juu yako. Nitamwomba Mola wangu Akughufirie.”

Je, yawezekana kuwako jibu lifaalo zaidi na mazungumzo ya upole na yakubalikayo kuliko haya maneno ya Nabii Ibrahim (a.s.)?

Je, Azar Alikuwa Ndiye Baba Yake Nabii Ibrahim (A.S.)?

Aya tulizozinukuu hapo juu pamoja na aya ya kumi na tano ya Surah Tawbah na aya ya kumi na nne ya Surah al-Mumtahinah zinaweza kutoa dhana ya kwamba Azar alihusiana na Nabii Ibrahim (a.s.) katika kiwango cha baba na Ibrahim (a.s.) naye amemwita, ‘baba.’ Hata hivyo wazo la kuwa Azar mwenye kuyaabudu masanamu yu baba yake Nabii Ibrahim (a.s.) haliafikiani na maoni yakubaliwayo na wanachuoni wote wa Kishi’ah, waitakidio kwamba jadi zake Mtukufu Mtume (s.a.w.w) pamoja na wale wa Mitume wengine walikuwa wachamungu walio uitakidi Upweke wa Allah. Mwanachuoni maarufu wa Kishi’ah, Sheikh Mufid katika kitabu chake kizuri sana,4ameichukulia dhana hii kuwa ni yenye kukubaliwa na wanachuoni wote wa Kishi’ah na idadi kubwa ya wanachuoni wa Kisunni pia wameafikiana nao katika kuitakidi hivyo. Hivyo basi, swali huibuka, nini maana halisi ya aya tulizozitaja na suala hili lawezaje kutatuliwa?

Wengi wa wafasiri wa Qur’ani Tukufu wanadai kwamba ingawa kwa kawaida neno “Ab” hutumia mwenye lugha ya kiarabu kwa maana ya ‘baba’, hii si maana pekee ya neno hilo, na katika kamusi ya kiarabu na katika istilahi za Qur’ani mara kwa mara neno hili limetumika kwa maana ya ami vile vile. Kwa mfano, kwenye aya ifuatayo neno ‘Ab’ husimama kwa maana ya ‘ami.’

أَمْ كُنْتُمْ شُهَدَاءَ إِذْ حَضَرَ يَعْقُوبَ الْمَوْتُ إِذْ قَالَ لِبَنِيهِ مَا تَعْبُدُونَ مِنْ بَعْدِي قَالُوا نَعْبُدُ إِلَٰهَكَ وَإِلَٰهَ آبَائِكَ إِبْرَاهِيمَ

وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ إِلَٰهًا وَاحِدًا وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ {133}

“Je, mlikuwapo pale mauti yalipomfikia Ya’qub? Aliwaambia wanawe: “Je, mtamwabudu nani baada yangu?” Wakajibu wakasema: “Tutamwambudu Mola Wako na Mola wa baba (Aba) zako, Ibrahimu, Isma’il na Is’haka; Yeye ni Mola Mmoja tu. Nasi kwake tumenyenyekea.” (Surah al-Baqarah, 2:133)

Hakuna shaka yoyote ile kuhusiana na ukweli uliopo kwamba Nabii Isma’il (a.s.) alikuwa ami yake Nabii Ya’qub (a.s.) na wala hakuwa baba yake, kwa sababu Nabii Ya’qub (a.s.) alikuwa mwana wa Nabii Isihaka (a.s.) aliyekuwa nduguye Nabii Isma’il (a.s.). Hata hivyo, ingawa ilikuwa hivi, wana wa Nabii Ya’qub (a.s.) wamemtaja kuwa yu baba wa Nabii Ya’qub (a.s.) yaani wamemwita ‘Ab’ kama alivyo Nabii Ya’qub (a.s.). Kwa kuwa neno hili lina maana mbili upo uwezekano kwamba kwenye aya zizungumziazo juu ya Azar kuitwa kwenye njia iliyonyoka na Nabii Ibrahim (a.s.), zinaweza zikawa na maana ya ‘ami’, na ni hivyo hasa, kutegemeana na maoni ya pamoja yaliyotajwa na Sheikh Mufid. Na inawezekana kwamba Nabii Ibrahim (a.s.) alimwita mlezi wake kwa muda mrefu sana naye (Nabii Ibrahim a.s.) alimwangalia kana kwamba alikuwa baba yake hasa.

Azar Katika Qur’ani Tukufu

Kwa lengo la kutaka kuona ushahidi wa Qur’ani Tukufu juu ya uhusiano baina ya Nabii Ibrahim (a.s.) na Azar tungalipenda kuukaribisha usikivu wa msomaji kwenye maelezo ya aya mbili:

Yakiwa ni matokeo ya juhudi za nguvu alizozifanya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), Bara Arabu iliangazwa na nuru ya Uislamu. Wengi wa watu wake waliipokea dini hii kwa moyo mmoja na wakatambua ya kwamba ushirikina na uabudu masanamu vitaishilizia Motoni na mateso. Ingawa walifurahia kuwa katika dini ya kweli, walijihisi kuwa ni wenye huzuni kukumbuka kuwa baba zao na mama zao walikuwa wenye kuyaabudu masanamu.

Usikiaji wa aya zenye kuielezea hali mbaya watakayokuwa nayo wenye kuyaabudu masanamu katika Siku ya Kiyama, uliwawia mzito. Ili kuyaondoa mateso haya ya kifikara walimwomba Mtukufu Mtume (s.a.w.w) amwombe Allah maghufira juu ya jadi zao waliofia katika hali ya ukafiri, kama vile Nabii Ibrahim (a.s.) alivyomwombea Azar.

Hatahivyo,ayazifuatazozilifunuliwakulijibuombilaohilo:

مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَنْ يَسْتَغْفِرُوا لِلْمُشْرِكِينَ وَلَوْ كَانُوا أُولِي قُرْبَىٰ مِنْ بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُمْ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ {113}

وَمَا كَانَ اسْتِغْفَارُ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ إِلَّا عَنْ مَوْعِدَةٍ وَعَدَهَا إِيَّاهُ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ أَنَّهُ عَدُوٌّ لِلَّهِ تَبَرَّأَ مِنْهُ ۚ إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَأَوَّاهٌ حَلِيمٌ {114}

“Haimpasi Nabii (Wetu Muhammad) na wale walioamini ya kwamba wawaombee maghfira washirikina, japo wawe ni karaba (zao) baada ya kuwabainikia ya kwamba wao wameichuma adhabu ya Moto (wa Jahanamu) uwakao. Wala haikuwa Ibrahim kumuombea msamaha baba yake kwa ajili tu ya kuitimiza miadi aliyomwahidi; Lakini ilipombainikia ya kwamba yeye alikuwa adui wa Allah alijiepusha naye; Hakika Ibrahim alikuwa mwenye huruma, mvumilivu.” (Surah Tawbah, 9:113-114)

Ingeweza kuonekana kuwa na mwelekeo zaidi kwamba mazungumzo ya Nabii Ibrahim (as) na Azar, na yeye Nabii Ibrahim (a.s.) kumwahidi Azar kumwombea maghfira, jambo lililoishilizia kwenye mkatiko wa uhusiano na kukataana, yalitokea wakati Nabii Ibrahim (a.s.) alipokuwa mtoto – yaani wakati alipokuwa bado anaishi nchini Babeli na alikuwa bado Hajadhamiria kwenda Palestina, Misri na Hijaz.

Baada ya kuichunguza aya hii tunaweza kuamua ya kwamba, Azar alipong’ang’ania kwenye ukafiri na ibada yake ya masanamu, Nabii Ibrahim (a.s.), akiwa bado yu mtoto, alikata uhusiano wake naye na katu hakupata kumfikiria tena baada ya hapo.

Katika kipindi cha baadae cha uhai wake yaani pale alipokuwa mzee, Nabii Ibrahim (a.s.) baada ya kulitimiza jukumu lake kubwa (yaani ujenzi wa Al- Ka’ba) na kumleta mkewe na mwanawe kwenye jangwa kavu la Makkahh, aliwaombea watu kadhaa kutoka ndani ya moyo wake, wakiwemo wazazi wake, na akaomba dua yake itakabaliwe na Allah. Katika wakati ule aliomba hivi:

رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ {41}

“Mola wangu! Unisamehe mimi na wazazi wangu na waumini katika Siku ya Kusimamishwa hesabu.” (Surat Ibrahim, 14:41)

Aya hizi zadhihirisha ya kwamba sherehe ya dua hii ilifanyika baada ya kwisha ujenzi wa Al-Ka’ba wakati Nabii Ibrahim (a.s.) alipokuwa kwenye kipindi cha uzee wake. Kama baba yake aliyeionyesha huba na utii kwake kwenye aya hii na akamwombea ni yule yule Azar, ingalikuwa na maana ya kwamba Nabii Ibrahim (a.s.) hakujitenga naye kwenye kipindi chote cha uhai wake na kwenye nyakati fulani alimwombea, pia ambapo aya iliyofunuliwa kulijibu ombi la kizazi cha washirikina inaonyesha dhahiri kwamba baada ya kipindi fulani, alipokuwa bado yu mtoto, Nabii Ibrahim (a.s.) aliuvunja uhusiano wote na Azar na akajitenga naye, na kujitenga na kukana vina maana ya kukoma kuzungumza, kutokujaliana na kuacha kuombeana dua kwa ajili ya wokovu wa kila mmoja wao.

Aya hizi mbili zinaposomwa kwa pamoja, inadhihirika ya kwamba yule mtu ambaye Nabii Ibrahim (a.s.) alimchukia katika ujana wake na ambaye alikata mafungamano yote ya usikivu na kupendana alikuwa ni mtu mwingine kuliko yule aliyemkumbuka hadi kwenye kipindi cha uzee wake na akamwombea maghfira na wokovu.5

Nabii Ibrahim (A.S.) Mvunja Masanamu

Muda wa sikukuu ulikaribia na watu wa Babeli walio wazembe wakautoka mji kwenda porini ili kuondoa na uchomvu wao na kuitia nguvu milango yao ya fahamu na kuzifanya kawaida za sikukuu hiyo. Hivyo mji ukawa hauna watu. Matendo yaliyotangulia ya Nabii Ibrahim (a.s.) na makemeo yake na lawama zake vimewafanya watu wa Babeli kuwa na hofu. Hivyo basi, walisisitiza kwamba Nabii Ibrahim (a.s.) aende pamoja nao na ashiriki kwenye sherehe za sikukuu hiyo.

Hata hivyo, azimio lao hilo liliangukia kwenye kipindi cha ugonjwa wa Nabii Ibrahim (a.s.). Hivyo basi, katika kulijibu wazo lao, alisema kwamba alikuwa mgonjwa na asingaliweza kushiriki kwenye sherehe za sikukuu hiyo.

Hakika hiyo ilikuwa siku ya furaha kwa mtu aitakidiye upweke wa Allah, pamoja na washirikina pia.

Kwa washirikina ilikuwa na maana ya kuisherehekea sikukuu ya zamani sana na walikwenda chini ya mlima na kwenye nchi yenye majani mabichi kuziendesha sherehe za sikukuu ile na kuzihuisha desturi za jadi zao. Na kwa upande wa yule mtetezi wa Upweke wa Allah, vile vile ilikuwa ni siku adhimu ya sikukuu isiyo na kifani ambayo kwa muda mrefu alikuwa akitamani kuipata ili kwamba mji ule wautoke wapinzani na auvunjevunje mdhihiriko wa ukafiri na ushirikina.

Kundi la mwisho la watu likatoka mjini mle, na Nabii Ibrahim (a.s.) akau- fikiria wakati huu kuwa ndio ile fursa aliyokuwa akiitafuta, na akiwa moyoni kajawa na matumaini na imani kwa Allah aliliingia hekalu la masanamu.

Kwa mbali hivi aliviona vipande vya magogo vilivyochongwa na masanamu yasiyo na uhai. Akakifikiria kiasi kikubwa cha chakula ambacho wenye kuyaabudu masanamu hayo walikuwa wakikileta kwenye hekalu lao kikiwa ni sadaka ya kuitafutia baraka, na akaingia kukitafuta chakula kile. Alimega tonge la mkate, akalishika mkononi mwake na kuliashiria kwenye yale masanamu na kusema kwa dhihaka: “Kwa nini hamzili aina zote hizi za vyakula?” Ni dhahiri kwamba hawa miungu wa kubuniwa wa washirikina hawakuwa na uwezo wa kusogea japo kidogo tu, ukiachilia mbali kula kitu chochote kile.

Kimya cha mauti kilijaa kwenye ule ukumbi mkubwa wa hekalu la masanamu, kimya ambacho kiliweza kuvunjwa tu na mapigo makubwa ambayo Nabii Ibrahim (a.s.) alikuwa akiipa mikono, miguu na miili ya masanamu. Aliyavunja masanamu yote, hadi kikapatikana kichuguu kikubwa cha vipande vya miti na madini vilivyovunjika-vunjika na kupondwapondwa katikati ya hekalu lile. Hata hivyo alilisaza lile sanamu kubwa zaidi na akaliweka shoka begani mwake.

Nabii Ibrahim (a.s.) aliyatenda hayo kwa lengo maalum. Alijua kwamba wenye kuyaabudu masanamu watakaporudi kutoka kule porini wataielewa hali halisi na wataitumia hali iliyokuwapo kuwa ni ya kubunia tu na isiyo na ukweli kwa kuwa katu wasingesadiki ya kwamba mapigo hayo yaliyopigwa yale masanamu mengine yalifanywa na lile sanamu kubwa, lisilokuwa na uwezo hata kidogo wa kusogea au kukitenda chochote kile, na kwenye tukio lile, yeye (Nabii Ibrahim a.s.) ataitumia hali ile katika ‘mwito’ wake na kusema kwamba kwa mujibu wa imani yao wenyewe, iwapo lile sanamu halina japo uwezo kidogo tu basi yawezekanaje kwam- ba liwe Mola wa ulimwengu?

Jua liliingia kwenye upeo wa macho na likakoma kuangaza ulimwengu. Katika wakati ule, watu walianza kurudi mjini kwa makundi. Sasa ukaingia muda wa kuzitekeleza ibada za kuyaabudu masanamu, na makundi ya wenye kuyaabudu masanamu yakaanza kuingia hekaluni mle. Mandhari isiyotegemewa, iliyoidhihirisha huzuni na fedheha ya miungu yao, ilizivu- tia shauku zao wote. Kikaingia kimya cha kifo kwenye mazingira ya hekalu na kila mmoja wao akapandwa na ghadhabu. Hata hivyo, mmoja wao alikivunja kimya kile na akasema: “Ni nani aliyeutenda uharibifu huu?” Lawama za Nabii Ibrahimu (a.s.) za tangu kale juu ya masanamu yale na lawama zake za wazi wazi juu ya ibada ya masanamu ziliwafanya waamue kuwa ni yeye tu aliyeyafanya hayo. Hivyo basi lilikaa baraza la hukumu chini ya uongozi wa Namrud na kijana Ibrahim (a.s.) na mama yake waliletwa ili kuhukumiwa.

Mamie (Nabii Ibrahim a.s.) alishitakiwa kwa kosa la kuficha kuzaliwa kwa mtoto wake na kutotoa taarifa kwenye ofisi maalum ya serikali, ili mtoto yule aweze kuuawa.
Maama yule alilijibu shitaka hili hivi: “Niliona kwam- ba matokeo ya maamuzi ya serikali ya wakati ule (yaani kule kuwaua watoto wa kiume) jamii ya wanaadamu nchini humu inamalizika. Sikuiarifu ofisi ya serikali juu ya mwanangu, kwa sababu nilitaka kuona jinsi atakavyoendelea hapo baadae.

Kama ingebidi kuthibitisha kwake kuwa yu mtu yule yule ambaye watabiri (makasisi) wamemtabiri, ingelikuwepo sababu ya mimi kuwaarifu polisi ili waache kuimwaga damu ya watoto wengine. Na kama haijitokezi yeye kuwa ndiye mtu yule, basi nimemwokoa kijana wa nchi hii kutokana na kifo.” Hoja za mama yule ziliwatosheleza kabisa mahakimu.

Sasa Nabii Ibrahim (a.s.) akahojiwa. Akasema: “Hali ya mambo inaonye- sha kwamba lile sanamu kubwa ndilo lililoyapiga mapigo yote hayo na kama masanamu haya yana uwezo wa kusema ni bora mngaliliuliza.” Jibu hili lisiloeleweka vizuri, lililotiiwa madoa na dhihaka na dharau lilidhamiriwa kutumikia lengo jingine, na lengo lile lilikuwa kwamba Nabii Ibrahim alikuwa na uhakika kwamba watu wale watamjibu wakisema: “Ewe Ibrahim! Unatambua vema kwamba masanamu haya hayana uwezo wa kusema. Vile vile hayana hiari wala akili.”

Watakaposema hivyo, Nabii Ibrahim (a.s.) angaliweza kulitanabahisha baraza lile juu ya jambo moja la msingi. Kwa bahati ilitokea kama alivyotazamia Nabii Ibrahim (a.s.). Aliyazungumza yafuatayo kwa kurejea kauli ya watu wale iliyoushuhudia unyonge, fedheha na kutokuwa na uwezo kwa masanamu yale: “Kama masanamu haya yako vile muyaelezavyo, basi kwa nini mwayaabudu na kwa nini mwayaomba kukupeni haja zenu?”

Ujinga, ukaidi na kuiga mambo kwa njia ya upofu kulizitawala nyoyo na akili za mahakimu na mbele ya majibu ya Nabii Ibrahim (a.s.) yasiyokanika hawakupata njia nyingine ila kutoa hukumu itakayopatana na haja ya serikali ya zama zile. Hivyo basi, waliamua kwamba Nabii Ibrahim (a.s.) achomwe moto akiwa hai. Lundo kubwa la kuni lilichomwa na huyu mtetezi wa Upweke wa Allah alitupiliwa kwenye miali ya moto uwakao.

Hata hivyo, Allah Mwenye nguvu zote Alimnyooshea Nabii Ibrahim (a.s.) Mkono Wake wa Huruma na akamfanya sugu kutokana na madhara ya moto ule. Yeye (Allah) Aliigeuza ile hali ya jahannam ya bandia, iliyoten- genezwa na wanaadamu kuwa bustani ya kijani yenye kupendeza 6(Tazama Surah al-Anbiya; 21:51-70).

Nukta Za Simulizi Hii Zenye Mafunzo

Ingawa Mayahudi wanadai kuwa ndio watangulizi wa msafara wa wale waaminio Upweke wa Allah, hadithi hii haikuwa maarufu miongoni mwao na haina nafasi kwenye Taurati yao ya siku hizi. Miongoni wa vitabu vya Mbinguni ni Qur’ani Tukufu tu iliyoisimulia hadithi hii. Hivyo basi, hapa chini tunayataja baadhi ya mafunzo ya hadithi hii ambayo kwa kweli hasa ndio mambo yenyewe hasa ambayo Qur’ani Tukufu inataka kuwafa- hamisha watu kwa kuzisimulia hadithi za Manabii mbali mbali.

Hadithi hii ni ushahidi wa dhahiri wa ujasiri na ushujaa usio kifani wa rafi- ki wa Allah (Nabii Ibrahim a.s.).

Nia yake katika kuyavunja masanamu na kuuvunjavunja mdhihiriko na njia ya ushirikina halikuwa jambo la kubakia kufichikana kwa watu wa Namrud kwa sababu kwa karipio na shutuma zake, tayari kaishadhihirisha kutopenda na chuki yake juu ya ibada ya masanamu wazi kabisa na alikuwa kila mara akisema wazi wazi na bila kificho: “Kama hamtayaacha mwenendo wenu uaibishao nitachukua uamuzi juu yao.” Na siku ile watu walipokwenda porini, alisema waziwazi: “Haki ya Mungu! Bila shaka nitayapindua masanamu yenu mara tu muigeuzapo migongo yenu.” (Surah Anbiya, 21:57).

Allama Majlisi ananakili hivi kutoka kwa Imam Sadiq (a.s.): “Harakati na kampeni ya mtu mmoja dhidi ya safu za makafiri, ambao idadi yao ilikithiri maelfu machache, ni ushahidi ulio hai wa ujasiri na uthabiti wa Nabii Ibrahim (a.s.), ambaye hakuwa na hofu yoyote akilini mwake katika njia ya kutukuza Jina la Allah na kuuimarisha msingi wa ibada ya Allah Aliye Mmoja tu.”7

Wakati ambapo, yale mapigo (ya kuvunja masanamu) yaliyofanywa na Nabii Ibrahim (a.s.) yalikuwa dhahiri ni uasi wa silaha na mkali, lakini kama ionekanavyo kwenye mazungumzo yake na wale mahakimu, hakika harakati hii ilikuwa na hali ya kipropaganda, kwa sababu alifikiria kuwa njia ya mwisho katika kuziibua hekima na fikara za watu wale ni ile ya kuyavunja yale masanamu yote ila lile lililokuwa kubwa zaidi na kuliweka lile shoka begani mwake ili kwamba waweze kufanya uchunguzi zaidi juu ya sababu za tukio hili.

Na kwa kuwa mwishowe wangaliweza kuifikiria mandhari hii kuwa ni mzaha mtupu na katu wasingaliamini kwamba mapigo yale yalipigwa na lile sanamu kubwa, angalilitumia jambo hili katika kuyabalighisha maoni yake na kusema: “Kutokana na itikadi yenu wenyewe, hili sanamu kubwa halina uwezo hata kidogo, basi ni kwa nini mwaliabudu?”

Hii yaonyesha kwamba tangu mwanzoni kabisa Mitume wamekuwa wakizitumia hoja tu na midahalo ikiwa ndio silaha zao kali, ambazo daima zimekuwa zikitoa matokeo mema. Laa sivyo, basi ni nini faida ya kuyavunja masanamu machache ukilinganisha na hatari kwa maisha ambayo Nabii Ibrahim (a.s.) iliyomkabili? Ni muhimu kwamba tendo hili liwe na huduma kuu kwa kazi yake katika hoja zake kiasi cha kuweza kuyatoa mhanga maisha yake kwa ajili yake.

Nabii Ibrahim (a.s.) alitambua kwamba matokeo ya tendo hili ni kwisha kwa uhai wake. Hivyo basi, kama desturi angekuwa na wasiwasi au angejificha mahali fulani au kwa uchache kabisa angejilinda na mzaha na ubishi. Lakini hata hivyo, alikuwa na udhibiti kamili ya moyo wake na mishipa ya fahamu zake. Kwa mfano alipoliingia lile hekalu la masanamu aliliendea kila sanamu na kwa mzaha akalitaka lile chakula. Baada ya kukata tamaa alilivunjavunja na kulifanya kuwa kichuguu cha vipande vya mti vilivyovunjwavunjwa na akayachukulia yote hayo kuwa ni jambo la kawaida kabisa, kana kwamba hayatafuatiwa na kifo chake mwenyewe au kuhukumiwa.

Alipofika mbele ya baraza la hukumu alilijibu swali lao hivi: “Hakika (mtendaji) amelitenda hili, mkuu wao ni huyu, basi waulizeni kama wanaweza kusema.” Ubishi wa aina hii mbele ya baraza lile uliweza kutegemewa tu kutoka kwa mtu aliyejitayarisha kwa hatima zozote zile ziwezazo kutokea na asiyeihisi hofu yoyote ile au kuchelea heshima na cheo cha wakuu wa baraza, moyoni mwake.

Na lenye kustaajabisha zaidi ni kule kuchunguza hali ya fikara za Nabii Ibrahim (a.s.) pale alipowekwa kwenye kombeo na akatambua kwa uhakika ya kwamba karibuni tu atajikuta katikati ya miali ya moto – moto ambao kuni zake zilikusanywa na watu wa Babeli ili kuitenda ibada takatifu ya dini, na ambao miali yake ilikuwa iki- waka kwa kupaa juu kwa nguvu mno kiasi kwamba hata kipanga hakithubutu kuruka kandokando au juu yake. Katika wakati ule ule, Malaika Jibrili a.s. alishuka kutoka mbinguni akidhihirisha kuwako tayari kwake kumpa (yeye Nabii Ibrahim a.s.) kila msaada, na akasema: “Hebu niambie kuhusu matamanio ya moyo wako.” Nabii Ibrahim (a.s.) alimjibu akisema: “Mimi ninayo tamaa. Hata hivyo, wewe hutaweza kuitambua tamaa yangu ila hutambuliwa na Mola wangu tu.8 Jibu hili lauonyesha waziwazi utukufu na ukuu wa kiroho wa Nabii Ibrahim (a.s.).

Kwenye jumba kuu la kifalme lililokuwako maili chache kutoka ulipokuwapo ule moto, Namrud alingojea kwa shauku kuu na pasi na subira kuona kisasi kikilipizwa juu ya Nabii Ibrahim (a.s.) na alitaka kuiona jinsi miali ya moto ikimla. Ile kombeo ilitupwa kwa mrusho mmoja tu, mwili wa yule mtetezi wa Upweke wa Allah uliangukia kwenye moto. Hata hivyo, mapenzi ya Mola wa Nabii Ibrahim (a.s.) yanayopenya ndani yaliubadili ule moto wa bandia uliotengenezwa na watu na kuwa bustani katika hali iliyowashangaza mno watu kiasi kwamba Nimrud alimgeukia Azar kwa ghafla na pasi ya kujijua, na akasema: “Mola wa Ibrahim Anamchukulia kuwa ni kipenzi chake mno. 9

Licha ya matukio yote haya, Nabii Ibrahim (a.s.) hakuweza kuihubiri itikadi yake kwa uhuru kamili. Hatimaye serikali ya zama zile, baada ya kushauriana iliamua kumfukuza nchini humo Nabii Ibrahim (a.s.). Kitendo hiki kiliifungua sura mpya maishani mwake na kikawa mwanzo wa safari yake ya kwenda Sham, Palestina, Misri na Hijaz.

Ukurasa Mpya Katika Maisha Ya Nabii Ibrahim (A.S.)

Mahakama ya mjini Babeli ilimpiga marufuku Nabii Ibrahim (a.s.) kuishi nchini mle na akalazimishwa kuitoka sehemu ile aliyozaliwa na kwenda Misri na Palestina. Mfalme Amaliqa aliyekuwa akizitawala sehemu hizi alimpokea kwa mikono miwili na akampa zawadi nyingi, moja kati ya zawadi hizo ilikuwa ni mjakazi aliyekuwa akiitwa Hajjar.

Hadi wakati ule, mkewe Nabii Ibrahim (a.s.) Bibi ‘Sarah’ alikuwa Hajajaaliwa mwana na maendeleo hayo tuliyotaja hapo juu yaliziamsha hisia zake kwa upande wa mumewe mtukufu. Hivyo akamshauri Nabii Ibrahim (a.s.) amwoe Hajjar kwa kuwa yawezekana kwamba akajaaliwa mwana atakayekuwa chanzo cha faraja na furaha yao. Ndoa ile ilifanyika na baada ya muda, Bibi Hajjar alijifungua mwana aliyeitwa Isma’il. Haikuchukua muda mrefu, Bibi Sarah nae akashika ujauzito na akazaa mwana aliyepewa jina la Isihaka.10

Baada ya muda fulani kupita, akifanya kama alivyoamrishwa na Allah, alimchukua (Nabii) Isma’il (a.s.) na mama yake, Bibi Hajjar (a.s.) na akaelekea kusini (Makkah) na akawaweka mwenye bonde lisilofahamika. Bonde hili halikuwa likiishi watu na ni misafara ya watu tu iliyokuwa ikisafiri kutoka Sham kwenda Yemen au ikitoka Yemen kwenda Sham iliweza kukita mahema yao pale. Siku zote za mwaka zilizobakia sehemu hii ilibakia kuwa tupu na ilikuwa jangwa lenye joto kali tu, kama vile zilivyo sehemu nyingine za Uarabuni.

Makazi katika sehemu yenye kuogofya kama hii yalikuwa mtihani mkuu kwa mwanamke ambaye alikuwa amezitumia siku zake katika nchi ya Mfalme Amaliqa.

Joto la jangwa lenye kuunguza na pepo zenye joto lake kali mno viliiwakilisha mandhari ya kifo mbele ya macho yake. Nabii Ibrahim (a.s.) yeye mwenyewe pia alihuzunishwa na matukio haya. Alipokuwa akiishika hatamu ya mnyama wa kupanda kwa nia ya kumwabia kwa heri mkewe na mwanawe, rundo la machozi lilianza kumtiririka machoni mwake na akamwambia Hajjar: “Ewe Hajjar! Yote haya yametendeka kwa mujibu wa amri ya Allah Mwenye nguvu zote na amri Yake haiwezi kukaidiwa. Zitegemee baraka za Allah na uwe na uhakika ya kwamba hatatufedhehesha.” Kisha alimwomba Allah kwa maneno yafuatayo na kwa dhamira halisi:

رَبِّ اجْعَلْ هَٰذَا بَلَدًا آمِنًا وَارْزُقْ أَهْلَهُ مِنَ الثَّمَرَاتِ مَنْ آمَنَ مِنْهُمْ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ {126}

“Ewe Mola wangu! Ufanye mji huu (wa Makkahh) uwe na usalama na uwaruzuku watu wake matunda, wale miongoni mwao wanaomwamini Allah na Siku ya Mwisho…”
(Al-Baqarah, 2:126).

Alipokuwa akikishuka kilima (cha Makkahh akienda zake) aligeuka na kutazama nyuma na akamwomba Allah kuwamiminia baraka Yake.

Ingawa, kwa kadiri ionekanavyo, safari hii ilikuwa ngumu mno na yenye usumbufu, lakini baadae ilidhihirika ya kwamba ilibeba matukio ya maana sana katika hatima yake, miongoni mwao ukiwamo ujenzi wa Al-Ka’ba tukufu iliyotoa msingi mkuu kwa ajili ya itikadi ya Upweke wa Allah, ukiipeperusha bendera ya ibada ya Allah Aliye Mmoja tu katika Bara Arabu na kuuweka msingi wa chama kikuu cha kidini ambacho baadae kitachukua sura yake halisi, yaani kile chama kikuu ambacho baadae kilifanya kazi nchini humu kupitia kwa mwishilizio wa Mitume (s.a.w.w.)

Jinsi Chemchem Ya Zamzam Ilivyopatikana

Nabii Ibrahim (a.s.) aliichukua hatamu ya mnyama wake wa kupanda na akitokwa na machozi machoni mwake, aliiaga nchi ya Makkahh pamoja na Bibi Hajjar na mwanawe. Hata hivyo, baada ya muda mfupi chakula na maji alivyokuwanavyo yule mtoto na mamie vilimwishia na kifua cha Hajjar kilikauka. Hali ya mwanawe nayo ilianza kudhoofika. Mafuriko ya machozi yalitiririka machoni mwa yule mama aliyehamishiwa mbali na yakayalowesha mapaja yake.

Katika hali hiyo ya kutojua afanye nini, aliamsha miguu, yake na akaenda hadi akakifika kilima cha Safa. Kutoka kilimani pale alikiona kioja cha mazigazi karibu na kilima cha Marwa na akayakimbilia. Hata hivyo, uchungu wa sura ya nchi yenye kuhadaa ulikatisha tamaa mno. Maombolezo na wasiwasi wa mwanawe mpenzi ulimfanya akimbie kwa ushupavu zaidi katika mielekeo yote. Hivyo alikimbia mara saba baina ya vilima vya Safa na Marwa ili kuyatafuta maji, lakini hatimaye aliyapoteza mategemeo yote na akamrudia mwanae.

Bila shaka katika wakati ule, mwanawe atakuwa kaishaifika hatua ya pumzi yake ya mwisho na atakuwa kaishaupoteza uwezo wa machozi au kulia zaidi. Hata hivyo, katika muda ule dua ya Nabii Ibrahim (a.s.) ilitakabaliwa. Mama yule mwenye taabu na aliyechoka aliyaona yale maji yaliyo safi yakiwa yameanza kububujika kutoka chini ya miguu ya Nabii Isma’il (a.s.).
Mama yule aliyekuwa akizitazama pumzi za mwisho za mwanawe na aliamini ya kwamba atafariki dunia baada ya muda mfupi tu, alijihisi kuwa yu mwenye furaha mno alipoyaona maji haya. Wote wawili, mama na mwana walikunywa hadi wakatosheka na mawingu ya kukata tamaa na kutokuwa na matumaini ambayo yaliweka kivuli kwenye maisha yao yaliondolewa na upepo mwanana wa baraka za Allah. 11

Kupatikana kwa chemchem hii inayoitwa ‘Zamzam’, tangu siku ile, kuli- wafanya ndege wa angani kurukaruka juu yake na wakazitanda mbawa zao pana kama kifuniko juu ya vichwa vya mama mwenye huzuni na yule mwana. Watu wa kabila la ‘Jarhani’ waliokuwa wakiishi mbali kidogo kutoka kwenye bonde hili waliwaona wale ndege wakienda huko na huko na wakaamua ya kwamba yamepatikana maji katika eneo hilo. Waliwatuma watu wawili miongoni mwa watu wao kuithibitisha hali hiyo.

Baada ya kutembea huko na huko watu wale walikifikia kitovu kile cha baraka za Allah. Walipokaribia, walimwona mwanamke na mtoto mchanga wakiwa wamekaa kandoni mwa bwawa la maji. Walirudi kwa haraka na kuwataarifu machifu wao juu ya jambo hilo. Upesi sana watu wa kabila hili walikita mahema yao kuizunguka chemchem hii iliyobarikiwa na hivyo, Bibi Hajjar (a.s.) aliondolewa taabu na uchungu wa upweke uliokuwa ukimsumbua. Kukua na uchangamfu kamili wa Nabii Isma’il (a.s.) vilikuwa chanzo cha kufanya kwake maingiliano ya kindoa na kabila ya ‘Jarhani’ na hivyo akafaidika na msaada na jamii yao. Mara moja Nabii Isma’il (a.s.) alimwoa msichana wa kabila lile. Hivyo basi, kutokana na upande wa mama yao, kizazi chake kilihusiana na kabila lile.

Wakutana Tena

Baada ya kumwacha mpenzi mwanawe na mkewe nchini Makkahh, chini ya amri ya Allah Mwenye nguvu zote, wakati fulani Nabii Ibrahim (a.s.) alifikiria kwenda kule kumwona mwanawe. Katika moja ya safari zake, ambayo labda ilikuwa ndiyo safari yake ya awali, alifika Makkahh na akaona ya kwamba mwanawe hakuwamo nyumbani mwake. Wakati ule Nabii Isma’il (a.s.) alikuwa kaishakua na kuwa mtu mzima na amemwoa msichana wa kabila la Jarham. Nabii Ibrahim (a.s.) alimwuliza mkewe Nabii Isma’il (a.s.): “Yu wapi mumeo?” Akamjibu akisema: “Amekwenda kuwinda.” Hapo alimuuliza kama anacho kitu chohote cha kula. Alimjibu kwamba hakuna kitu chochote.

Nabii Ibrahim (a.s.) alihuzunika mno kuuona utovu wa adabu na huruma wa mkaza mwanawe na akamwambia: “Isma’il atakaporudi nyumbani mpe salaam zangu na umwambie akibadili kizingiti cha nyumba yake.” Baada ya hapo Nabii Ibrahim (a.s.) alirudi maskanini kwake.

Nabii Isma’il (a.s.) aliporudi aliisikia harufu ya baba yake na kutokana na maelezo ya mkewe alitambua ya kwamba yule mtu aliyeitembelea nyumba yake alikuwa ni baba yake, Nabii Ibrahim (a.s.), mwenyewe. Vile vile kutokana na ule ujumbe ulioachwa na baba yake alitambua ya kwamba alimtaka amtaliki mkewe wa wakati ule na amchague mwingine, kwa kuwa hakumfikiria yule mke wa wakati ule kuwa mwenzi afaaye maishani mwake.12

Pengine mtu anaweza akauliza ni kwa nini kwamba Nabii Ibrahim (a.s.) baada ya kuifanya safari ndefu kiasi kile asisubiri hadi mwanawe akarudi kutoka kule mawindoni na kwa nini alirudi Palestina bila ya kuonana naye?

Wanahistoria wanaelezea kwamba alirudi haraka kwa sababu alifunga ahadi na Bibi Sarah (Mkewe mkuu) kwamba asikae kule kwa muda mrefu na kurudi kwake upesi kulitokana na kuitunza ahadi ile. Vile vile baada ya safari hii aliamrishwa na Allah, Mwenye nguvu zote kufanya safari nyingine ya kwenda Makkahh, kwenda kuijenga Al-Ka’ba, pale na kuzivu- tia hapo nyoyo za wale wote wauaminio Upweke wa Allah.

Qur’ani Tukufu inathibitisha ya kwamba katika siku za mwishoni za uhai wa Nabii Ibrahim (a.s.) mji wa Makkahh ulikwishakua na kuwa jiji, kwa sababu, baada ya kulitimiza jukumu lake alimwamba Allah kwa maneno yafuatayo:

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ اجْعَلْ هَٰذَا الْبَلَدَ آمِنًا وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَنْ نَعْبُدَ الْأَصْنَامَ {35}

“…. Mola wangu! Ujaalie mji huu (wa Makkah) uwe wa amani na uniepushe mimi na kizazi changu kutokana na kuyaabudu masanamu…” (Sura Ibrahim 14:35).

Na wakati wa kuwasili kwake kwenye jangwa la Makkahh, aliomba akisema:

رَبِّ اجْعَلْ هَٰذَا بَلَدًا آمِنًا وَارْزُقْ أَهْلَهُ مِنَ الثَّمَرَاتِ مَنْ آمَنَ {126}

“Mola wangu! Ufanye mji huu uwe wa usalama ...(Al-Baqarah, 2:126).

Ili kuyamaliza majadiliano haya, inafaa kuzielezea hali za wakati wa ujenzi wa Al-Ka’ba na pia kuitoa historia yake fupi. Hata hivyo, ili tuweze kulifupisha lengo letu, hatuna budi kutoa hapa chini taarifa za baadhi ya jadi zake Mtukufu Mtume (s.a.w.w) walio watukufu na walio maarufu katika historia.

Qusayy Mwana Wa Kilaab

Yafuatayo hapa chini ni majina ya baba na jadi zake Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kwa utaratibu wa mwelekeo wa juu: Abdallah, Abdul-Muttalib, Hashim Abd-i-Manaaf, Qusayy, Kilaab, Marra, Ka’ab, Luayyi, Ghalib, Fahr, Malik, Nizar, Kinanah, Khuzaimah, Mudrikah, Ilyaas, Mudhar, Nazaar, Ma’ad na A’dnaan.13

Kizazi cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w) hadi kwa Ma’ad mwana wa Adnaan ni kama ilivyoelezwa hapo juu. Hata hivyo kuna kutoafikiana kuhusu idadi na majina ya nasaba zake tangu kwa Adnaan hadi kwa Nabii Isma’il (a.s.) na kwa mujibu wa taarifa zilizonukuliwa na Ibn Abbas, kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) wakati nasaba yake ifikapo kwa Adnaan mtu na asiendeleze, kwa kuwa yeye Mtukufu Mtume (s.a.w.w) mwenyewe, kila alipoyataja majina ya jadi zake hakuendelea baada ya kufika kwa Adnaan, na akaamrisha kwamba watu wengine nao wasiyataje majina ya jadi zake wengine tangu hapo hadi kwa Nabii Isma’il (a.s.). Vile vile alisema kwamba kile kilichokuwa kikifahamika mno miongoni mwa Waarabu kuihusu sehemu ile ya jadi zake haikuwa sahihi.

Hivyo basi sisi nasi tumeitaja ile sehemu ya nasaba yake ambayo usahihi wake unakubalika, na maelezo marefu ya baadhi ya watu wahusikao. Watu tuliowataja hapo juu ni maarufu katika historia ya Uarabuni na historia ya Uhusiano na baadhi yao.

Hivyo basi, tunatoa hapa chini taarifa za maisha yao tangu kwa Qusayy hadi kwa baba mtukufu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w), Bwana Abdallah, na tutajizuia kuyataja matukio ya maishani mwa wale wengine wasio husika na mambo tunayoyazungumzia.14

Qusayy alikuwa jadi wa nne wa Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w), mama yake Bibi Fatimah aliolewa na Bwana Kilaab na akazaa wana wawili, Zuhrah na Qusayy. Yule wa pili alikuwa bado yu mtoto mdogo pale mumewe Bibi Fatimah alipofariki dunia. Baada ya hapo aliolewa na mume mwingine aliyeitwa Rabi’a na akafuatana naye kwenda Sham.

Qusayy alipata matunzo ya kiubaba kutoka kwa Bwana Rabi’a hadi kulipoibuka kutoafikiana baina yake na kabila la Bwana Rabia na matokeo yake yakawa kwamba wakamfukuza na kumtoa nje ya mipaka ya nchi yao. Mama yake alichukizwa na matendo aliyotendewa na akaamua kumrudisha Makkahh.

Mkono wa kudra ulimvutia Makkahh. Sifa zake njema zilizojificha zilimwezesha kuudumisha ukuu wake juu ya watu wa Makkah na hasa miongoni mwa watu wa kabila la Quraysh. Katika kitambo kifupi tu alijipatia ofisi kuu za serikali mle mjini Makkahh, na vilevile akawa mdhamini wa funguo za Al-Ka’ba na mtawala wa mji ule aliyekubalika. Matukio mengi makuu yanahusika na jina lake.

Miongoni mwao ilikuwa kwamba aliwahamasisha watu kujenga nyumba iitwayo ‘Darun–Nadwah’ pembezoni mwa Al-Ka’ba na hivyo akaasisi ukumbi wa Halmashauri kwa ajili ya Waarabu ili kwamba wakuu na machifu wao waweze kukaa pamoja kwenye jumba hili na kutatua matatizo yao. Bwana Qusayy alifariki dunia kwenye karne ya 5 Masihiya, na aliacha wana wawili, Abdur Daar na Abd Manaaf.

Abd Manaaf

Alikuwa jadi wa tatu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w). Jina lake hasa lilikuwa Muahirah na jina lake la heshima lilikuwa Qamar al-Bat’ha (mwezi wa Bat’ha). Alikuwa mdogo kuliko Abdur Daar, lakini alijipatia heshima kuu miongoni mwa watu. Alikuwa mchamungu mno. Aliwaitia watu kwenye amali njema, akawatendea mema na alidumisha uhusiano mwema zaidi na karaba zake.

Ingawa alikwa na cheo cha juu zaidi kwenye jamii yake, katu hakupata kuwa mpinzani wa kaka yake Abdur Daar kuhusiana na suala la kuzishika ofisi kuu zihusianazo na Al-Ka’ba. Kufuatana na usia wa Qusay, utawala ulibakia mikononi mwa Abdur Daar, lakini ndugu hao walipofariki dunia wana wao walianza kugombea ofisi mbalimbali.

Baada ya ugomvi na kutoafikiana kwingi, hatimaye walipatanishwa na wakavigawa vyeo miongini mwao. Iliamuliwa kwamba udhamini wa Al-Ka’ba tukufu na uwenyekiti wa ‘Darun Nadwah’ vibakie mikononi mwa wana wa Abdur Daar na kazi ya kuwapatia mahujaji maji na kuwabu- rudisha ifanywe na wana wa Abd Manaaf. Mgawo huu wa ofisi ulikuwa ukitumika mwenye siku za kuanza kwa Uislamu. 15

Hashim

Alikuwa baba mkuu (au baba yake babu) wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w). Jina lake hasa ni Amr na jina lake la heshima lilikuwa ‘Ala’. Yeye na Abd Shams walikuwa mapacha na ndugu zoa wawili wengine walikuwa ni Muttalib na Nawfal. Wanahistoria wamehadithia ya kwamba wakati wa kuzaliwa kwa Bwana Hashim na Abd Shams, kidole cha Hashim kiliun- gana na paji la uso la Abd Shams. Damu ilitoka mno pale walipotengan- ishwa na watu wakalichukulia jambo hili kuwa ni ndege mbaya.16

Mwanahistoria Bwana Halabi mwenye kitabu chake ‘Siirah’ ameandika kwamba hii ndege mbaya ilijitokeza baadae, kwa sababu, baada ya kuanza kwa Uislamu, vita kali mno zilipiganwa baina ya Bani Abbas na Bani Umayyah waliodai kuwa kizazi chao kinatokana na Abd Shams.17 Jambo hili laonyesha kwamba mwandishi wa Siirah hii ameyapuuza kabisa matukio ya kimsiba yaliyohusiana na kizazi cha Sayyidna Ali (as.) ingawa mchezo wa umwagaji wa damu walioutengeneza Bani Umayyah kwa kuimwaga damu takatifu ya dhuria wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) ni wenye ushahidi ung’aao wa kuwako kwa uadui baina ya hizi familia mbili. Hata hivyo, haijulikani ni kwanini mwandishi aliyetajwa alishindwa kuyataja matukio haya.

Moja ya mambo makhususi kuhusu dhuria wa Abd Manaaf ambayo yanaakisi kwenye makelele ya vita na kwenye maandishi ya Uarabuni ni kwamba walifia sehemu tofauti, yaani Hashim alifia nchini Ghaza, Abd Shams alifia Makkah, Nawfal alifia nchini Iraq na Muttalib alifia Yemen. Ili kuunakili mfano wa utu wema wa Hashim tunaweza kusema kwamba kila ulipoandama mwezi wa Dhul-Hajj (Mfungo tatu) alikuwa akija kwenye Ka’aba tukufu akauegemea ukuta wake na kuhutubia kwa maneno yafuatayo:

“Enyi Waquraishi! Ninyi ni watu wenye busara na watukufu zaidi miongoni mwa Waarabu. Taifa lenu ni bora zaidi miongoni mwa mataifa yote, Mwenyezi Mungu amekupeni makazi kandoni mwa Nyumba Yake na amekupeni ubora kwa niaba yake juu ya dhuria wote wa Isma’il. Enyi ndugu zangu! Jihadharini! Mahujaji wa Nyumba ya Allah wanakujieni kwenye mwezi huu pamoja na wema mwingi mno. Wao ni wageni wa Allah na ni juu yenu kuwapokea. Wako watu wengi waliofukara miongoni mwao, watakaokuja kutoka sehemu za mbali. Ninaapa kwa Jina la Mola wa Nyumba hii kwamba kama ningalikuwa tajiri nitoshelezaye katika kuwaburudisha wageni wote wa Allah, nisingalikusisitizeni kutoa chakula.

Hata hivyo, hivi sasa mtatumia kila muwezacho kukitoa, na mlichochuma kwa njia ya halali. Ninakuapieni kwa jina la heshima la Nyumba hii kwamba hamtatumia kitu chochote kwa lengo hili, kile mlichokinyang’anya, au kutoa kwa njia ya kiunafiki au kwa kushurutishwa. Kama mtu yeyote yule havutiki kwenye kusaidia, yuko huru kutokukitu-mia kitu chochote kile.” 18

Kwa ajili ya nia na malengo, uongozi wa Hashim ulikuwa ni kwa ajili ya ustawi wa watu wa Makkahh nao ulikuwa na athari kubwa kwenye mategemeo ya hali za maisha yao. Kila ilipotokea njaa, wema wake haukuruhusu kwamba watu wapate taabu yoyote ile kwa tatizo hili. Moja ya hatua zake zilizojitokeza zaidi, alizozichukua kwa ajili ya maendeleo ya biashara ya watu wa Makkahh, ilikuwa ni kukamilishwa kwa mapatano na mtawala wa Ghassan.
Ni kutokana na mapatano haya kwamba mapatano mengine ya aina hiyo yalifanywa na kaka yake Abd Shams na Mfalme wa Ethiopia, na ndugu zake wengine wawili, Muttalib alifanya mapatano mengine na Mtawala wa Yemen, na Nawfal akafanya mapatano mengine na Mfalme wa Iran. Bidhaa ziliweza kubadilishwa kwa uhuru kabisa na nchi mbalimbali. Mapatano haya yalitatua matatizo mengi na yakaleta kuwako kwa idadi mjini Makkahh ambavyo vile vile vilikuwako kwenye zama za kuanza kwa Uislamu. Zaidi ya hapo, moja ya matendo yenye faida ya Hashim lilikuwa ni kuasisiwa kwa misafara ya Waquraishi kwen- da Sham kwenye nyakati za kiangazi na kwenda Yemen wakati wa kipup- we. Tendo liliendelea kwa muda mrefu hata baada ya kuanza kwa Uislamu.

Umayyah Mwana Wa Abd Shams Aona Kijicho

Umayyah, mwana wa Abd Shams, aliona kijicho juu ya ukuu na heshima ya ami yake, Hashim, na akajitahidi kuwavutia watu kwake kwa kuwapa zawadi. Hata hivyo, ingawa alijitahidi kwa kadiri alivyoweza na akaweka pingamizi zake zote alizoweza, hakuweza kumvua Hashim cheo chake kile. Kinyume na hivyo, matusi yake na kumsingizia Hashim kulimzidishia Hashim heshima zaidi nyoyoni mwa watu.

Moto wa husuda uliendelea kuwaka moyoni mwa Umayyah. Mwishowe alimshinikiza ami yake kwamba wote wawili wamwendee mmoja wa wataalamu (wapiga bao) wa Uarabuni na yule tu atakayethibitishwa na mganga yule kuwa ndiye afaaye kwa utawala, azishike hatamu za utawala mikononi mwake.

Wema wa Hashim hakumruhusu kuingia mwenye mabishano na mwana wa kaka yake. Hata hivyo kwa kuwa Umayyah alikuwa akishinikiza mno, Hashim aliukubali mpango ule kwa masharti mawili:

Kwanza, kwamba yeyote yule atakayeshindwa kwenye jambo hilo atoe kafara ya ngamia mia moja wenye macho meusi wakati wa Hajj, na pili, kwamba akae nje ya mji wa Makkahh kwa kipindi cha miaka kumi.

Sasa ilitokea kwamba, mara tu baada ya mganga yule wa kiarabu (mpiga bao wa Asfaan) alipomwona Hashim, alianza kumsifu na akahukumu kwa kumpa haki. Hivyo basi Umayyah alilazimika kuutoka mji wa Makkahh na akakitumia kipindi cha miaka kumi nchini Sham19

Athari za huu uadui wa kurithi uliendelea kwa kipindi cha miaka 130 baada ya majilio ya Uislamu na ulifuatana na majinai ya mara kwa mara yasiyo na kifani kwenye historia ya mwanadamu. Hadithi tuliyoitaja hapo juu, ukiachilia mbali kule kuudhihirisha ukweli kuhusu jinsi uadui baina ya hizi koo mbili ulivyoanza, vilevile inaielezea sababu ya ushawishi walioufaidi Bani Umayyah mle nchini Sham, na inatambuliwa kwamba uhusiano wao wa tangu kale na watu wa Sham uliujenga msingi wa utawala wao kwenye eneo lile.

Hashim Aoa

Salmah binti wa ‘Amr Khazraji alikuwa mwanamke mchamungu, aliyekuwa katalikiwa na mumewe na hakuwa tayari kuolewa tena.
Hashim alipokuwa akirudi kutoka Sham kwenye mmoja wa misafara yake alitua Yathirib (Madina) kwa siku chache hivi na akamchumbia Salmah. Salmah alivutiwa na utukufu, utajiri na tabia za Hashim, na kwa ushawishi aliokuwa nao miongoni mwa Waquraishi.

Salmah alikubali kuolewa na Hashim kwa masharti kwamba wakati wa kuzaa mtoto yeye Salmah awe miongoni mwa watu wake (yaani ajifungulie kwao). Kufuatana na sharti hili, Salmah aliutumia muda fulani mjini Makkahh pamoja na Hashim na muda wa kujifungua ulipokaribia alirudi Yathrib. Huko alijifungua mwana aliyeitwa Shibah, na baadae alifahamika kwa jina la Abdul-Muttalib. Wanahistoria wamezitaja sababu kadhaa zifuatazo zilizomfanya Shibah ajitwalie jina hili la heshima la Abdul-Muttalib:

Moja inasema kwamba wakati Hashim alipojihisi kuwa kifo chake kinamkaribia, alimwambia nduguye Muttalib: “Ewe ndugu yangu! Mtafute mtumwa wako Shibah.” Na kwa sababu Hashim (baba yake Shibah) amemwita mwanawe, “Mtumwa wa Muttalib” baadae alifahamika kwa jina hili la “Abdul-Muttalib” (yaani Mtumwa wa Muttalib).

Maelezo mengine ni haya: “Siku moja, mkazi mmoja wa Makkahh alipokuwa akipita kwenye mitaa ya mji wa Yathrib, aliwaona watoto wengi wakifanya mazoezi ya kufuma mishale. Mmoja wa watoto wale aliposhinda kwenye mchezo ule, mara moja alisema: “Mimi ni mwana wa chifu wa Bat’ha (Makkahh).” Yule mkazi wa Makkahh alijitokeza na akamuuliza yule kijana. Wewe ni nani?”

Yule kijana akajibu akasema: “Mimi ni Shibah mwana wa Hashim mwana wa Abd Manaaf.”

Yule mtu aliporejea Makkahh alimweleza Muttalib, nduguye Hashim na chifu wa Makkahh, habari zile. Huyu ami alimkumbuka yule mpwa wake na hivyo basi, alikwenda Yathrib. Sura ya yule mwana nduguye ilimkumbusha Muttalib sura ya nduguye na hapo machozi yakamchuruzika mashavuni mwake.

Wakabusiana kwa huba na hisia. Mama yake Shibah hakuwa tayari kutengana na mwanawe na akakataa asichukuliwe na kupelekwa Makkahh lakini kukataa kupinga kwake kuliimarisha zaidi dhamira ya Muttalib.

Hatimaye Muttalib alifaulu kulifikia lengo lake, na baada ya kuipata idhini ya mama yake mtoto, Shibah pamoja na yeye mwenyewe walimpanda mnyama na wakaenda Makkahh. Katika kipindi cha safari ile, joto kali la jua liliugeuza uso wa rangi ya fedha kuwa mweusi na vazi lake nalo lilichakaa na kupasuka.

Hivyo basi, kutokana na sababu hii, walipofika Makkahh, watu walifikiria kwamba yule kijana alikuwa mtumwa wa Muttalib. Walinong’onezana wakisema: “Kijana huyu (Shibah) ni mtumwa wa Muttalib.”Na ingawa Muttalib alisema mara kwa mara kwamba kijana yule alikuwa mpwa wake, ile fikara mbaya iliyokwisha kujenga mizizi akilini mwa watu iliendelea kuling’ang’ania wazo lile. Matokeo yake ni kuwa, yule mpwa wake Muttalib akafahamika kwa jina la Abdul-Muttalib (Mtumwa wa Muttalib).20

Vivyo maelezo mengine ni haya yafuatayo: “Abdul-Muttalib aliitwa hivyo, kwa sababu alilelewa na ami yake na lilikuwa ni jambo la kawaida miongoni mwa Waarabu kwamba kila mtu afugwapo na mtu mwingine aliitwa mtumwa wa mfadhili wake.

Abdul-Muttalib

Abdul-Muttalib mwana wa Hashim, babu yake Mtukufu Mtume (s.a.w.w), alikuwachifu wa Waquraish na mtu maarufu. Maisha yake ya kijamii, yote yalijaa sifa nzuri mno. Kwa vile matukio yote ya zama za uchifu wake vilevile yalihusiana na historia ya Uislamu, tunasimulia hapa chini baadhi ya matukio hayo:

Hakuna shaka yoyote kuhusu ukweli kwamba kwa vyovyote vile mtu awezavyo kuwa thabiti na imara, hatimaye huvutika kwa kiasi fulani na mazingira yake, na tabia na desturi za jamii huziathiri fikara zake. Hata hivyo katika nyakati fulani, baadhi ya watu huwa na utashi wa kimaumbile ya kuyakinza mambo yatawalayo mazingira yao kwa ujasiri na ushupavu, na kujiweka wenyewe na mazingira ya kutoathiriwa na maambukizo maovu.

Shujaa huyu wa mazungumzo yetu alikuwa kielelezo kamili cha wale watu ambao, kwenye maisha yao tunayaona mambo mengi yaliyo mema. Kama mtu ambaye, ingawa alitumia zaidi ya miaka themanini ya uhai wake miongoni mwa watu wenye kawaida ya kuyaabudu masanamu, ulevi, riba, uuaji wa watu, kwenye maisha yake yote asiiruhusu pombe kuigusa midomo yake na kuwazuia watu wasiue, wasinywe pombe, na wasifanye matendo maovu, na kuwazuia kuoa maharimu wao na kufanya tawafu wakiwa uchi, na kuwadhibiti kwenye mambo yahusuyo kiapo na ahadi mpaka kwenye pumzi ya mwisho ya uhai wake, bila shaka mtu huyu atakuwa mmoja wa watu walio vigezo.

Wanaozaliwa mara chache mno kwenye jamii ya wanadamu. Kwa hakika ni muhimu kwamba yule mtu ambaye mwilini mwake imewekwa nuru ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w) (aliye kiongozi mkuu zaidi wa wanadamu) awe msafi halisi na aliyeepukana kabisa na kila aina ya uchafu.

Kutokana na hadithi fupifupi na simulizi zenye mafunzo zisemekanazo kwamba zimesemwa na Abdul-Muttalib tunajifunza ya kwamba hata mle mwenye zile siku za mazingira ya ujinga, Abdul-Muttalib alihesabiwa miongoni mwa wale waliouitakidi upweke wa Allah na Siku ya Hukumu, na kila mara alikuwa akisema: “Mtu aliye mdhalimu huadhibiwa hapa ulimwenguni.

Hata hivyo, kama kwa bahati atakufa kabla ya kuadhibiwa vyakutosha, atapata mapatilizo kutokana na amali zake mwenye Siku ya Hukumu.21

Har’b mwana wa Umayyah alikuwa ndugu wa karibu wa Abdul-Muttalib. Vilevile alikuwa akifahamika kwamba yu mmoja wa watu watukufu mion- goni mwa Waquraishi. Myahudi mmoja alikuwa jirani wa Har’b. Siku moja Myahudi yule aliudhihirisha ukali wake dhidi ya Har’b kwenye moja ya bazaar (maduka) ya Tahamah na wakatoleana maneno makali. Tukio hili liliishilizia kwenye mauaji ya Myahudi yule kutokana na ushawishi wa Har’b.

Abdul-Muttalib alipolifahamu jambo hili alikata uhusiano wake na Har’b. Vilevile alijitahidi kupatikana malipo ya damu kutoka kwake na kuwapa wafiwa wa Myahudi yule. Hadithi hii fupi ni mfano wa shauku ya mtu huyu mnyoofu katika kuwasaidia wanyonge na katika kuutekeleza uadilifu.

Kuchimbwa Upya Kwa Kisima Cha Zamzam

Tangu siku ile kilipopatikana kisima cha Zamzam watu wa kabila la Jarham waliishi kandokando mwake na walinufaika kutokana na maji ya kisima hiki kwenye kipindi kile cha miaka mingi walipokuwa wakiutawala mji wa Makkahh. Hata hivyo, ikiwa ni matokeo ya kuendelea kwa watu wa Makkahh kwenye biashara, utajiri wao, uzembe wao na utovu wa miiko katika matumizi ya maji, polepole kisima kile kilikauka.22

Maelezo mengine (kuhusiana na kisima hiki) yanasema hivi: “Watu wa kabila la Jarham walipotishiwa na kabila la Khaza’ah na wakalazimika kuyaacha makazi yao, chifu wao na mtu aliyekuwa maarufu aliyeitwa Mazaaz mwana wa ‘Amr, alitambua kwamba karibuni atakoma kuwa mshika usukani wa mambo na adui wao ataishambulia nchi na serikali yake na kuiharibu kabisa.

Hivyo akaamrisha kwamba masanamu mawili ya paa yaliyofuliwa kwa dhababu na panga kadhaa za thamani, zilizoletwa kama zawadi kwenye Al-Ka’ba vitumbukizwe kisimani humo, na kisha kifukiwe kabisa ili kwamba maadui watakapokuja wasivitwae, na hapo baadae wao (Bani Jarham) watakapoitwaa tena nchi na utawala wao wenyewe waweze kuja kuutumia utajiri huo. Baada ya muda fulani kabila la Khaza’ah lilianza mashambulizi yao na kabila la Jarham pamoja na idadi kubwa ya dhuria wa Nabii Isma’il (a.s.) walilazimika kuutoka mji wa Makkahh na wakaenda Yemen, na hakuna yeyote miongoni mwao aliyerudi Makkahh baada ya hapo.

Kuanzia muda ule na kuendelea kabila la Khaza’ah liliutawala mji wa Makkahh hadi walipotawala Waquraishi kwa kutawala Qusayy mwana wa Kilaab, baba mkuu wa babu yake Mtukufu Mtume (s.a.w.w)- yaani baba yake babu wa Mtukufu Mtume s.a.w.w).

Baada ya muda fulani Abdul-Muttalib aliushika usukani wa mambo.Aliamua kukichimbua upya kile kisima cha Zamzam, lakini kwa bahati mbaya yeye hakuwa na uhakika wa mahali kilipokuwapo kisima kile. Baada ya kuchimba sana, alifaulu kukipata sehemu yake (halisi) na akaa- mua kuzichukua hatua za awali za kukichimba kisima kile akisaidiwa na mwanawe aliyeitwa Harith.

Kwa kawaida kwenye kila jamii mna kundi la wapinzani waliojaribu kuitafuta sababu moja au nyingine ili kuzuia utendaji wa kila amali ya uhakika. Hivyo basi, wapinzani wa Abdul-Muttalib, wakichelea kwamba heshima hii itamwendea yeye, walianza kumlaumu na wakisema: “Enyi wazee wa Waquraish! Kwa kuwa kisima hiki ni kumbukumbu ya jadi wetu Isma’il, nasi sote twahesabiwa kuwa tu dhuria wake, inafaa kwamba mtu- ruhusu sisi sote tushiriki kwenye kazi hii.”

Kwa sababu fulani fulani Abdul-Muttalib hakukubaliana na wazo lao, kwa kuwa nia yake ilikuwa kukichimba kisima kile peke yake na kisha awaruhusu wote kuyatumia maji yale bila ya malipo. Vilevile alitaka kulichukua tena lile jukumu la kuwapatia maji mahujaji kwenye yale majira maalum ili kwamba kazi hii iweze kutendwa kwa utaratibu mwema chini ya uangalizi wake mwenyewe. Hata hivyo, jambo hili liliweza kuhakikishwa kwa kuishika kazi hii mikononi mwake, akiwa huru kabisa kutokana na wale wengine.

Jambo hili lilizaa mzozo mkali na mwishowe iliamuliwa ya kwamba wamuendee mtaalamu mmoja wa kiarabu (mpiga-bao) na uamuzi wake ufuatwe na watu wote. Hapo Abdul-Muttalib na wapinzani wake wakaianza safari. Walipita kwenye maeneo mengi ya nchi yaliyo kame. Wakiwa njiani mle, walikabiliwa na kiu kali, na ilikaribia kuwa na uhakika kwamba wataangamia.

Hivyo basi wakawa na hofu juu ya kifo na mazishi yao yatakayofuatia. Kwamba kila mtu ajichimbie kaburi, na atakapokufa mmoja wao, wale wengine wamzike. Na kama wataendelea kuyakosa maji na wote wakafa, wote watapata kuzikwa na kuokolewa kutokana na kuliwa na wanyama na ndege, ila yule atakayekuwa wa mwisho kufa.

Ushauri wa Abdul-Muttalib ulikubaliwa na watu wote na kila mmoja wao akaanza kujichimbia kaburi. Sasa wakawa wanakisubiri kifo kwa nyuso za huzuni na zilizopauka. Mara moja Abdul-Muttalib alipiga ukelele akisema: “Enyi watu! hiki kitakuwa kifo chenye kuaibisha na kufedhehesha. Ni bora kwamba sisi sote tutembee kwenye jangwa hili tukitafuta maji. Yumkini kwamba Allah akatuhurumia.23

Wote wakaanza kuwapanda wanyama wao na wakaanza kutwanyika. Hawakuwa na mategemeo sana ya kupata maji na wakaanza kutazamana kwa fadhaa. Hata hivyo, kwa bahati, waliyapata maji safi na hivyo wakaokolewa kutokana na kifo kilichokuwa na uhakika wa kuwakumba. Kutoka hapo walirudi Makkahh na wakakubaliana kwa furaha na maoni ya Abdul-Muttalib kuhusiana na uchimbaji wa kisima kile, wakampa mamlaka kamili ya kuendelea na mradi wake ule.24

Abdul-Muttalib akaanza kukichimba kile kisima na mwanawe wa pekee wa wakati ule aliyeitwa Haarith na kichuguu cha mchanga kikajaa kandokando mwa sehemu ile. Kwa ghafla wakayagusa yale masanamu maw- ili ya paa yaliyofuliwa kwa dhahabu na zile panga kadhaa. Sasa Waquraish wakaamsha mzozo mwingine na wakadai fungu kwenye dafina zile. Hatimaye iliamuliwa kuumaliza mzozo ule kwa kupiga kura, kwa bahati yale masanamu mawili ya paa wa dhahabu yaliangukia kwenye fungu la Al-Ka’ba na zile panga ziliangukia kwenye fugu la Abdul-Muttalib, na Waquraishi wakaambulia patupu. Bwana Abdul-Muttalib mwenye fikara tukufu alizitumia zile panga katika kutengeneza lango la Al-Ka’ba na akawaweka wale paa ndani yake.

Umadhubuti Wake Katika Kutimiza Ahadi

Baadhi ya sifa za Waarabu wa Zama za Jahilia zinastahili kusifiwa. Kwa mfano, walichukulia kuvunja ahadi kuwa ni tendo lenye kuchukiza mno. Kwenye nyakati fulani fulani waliishilizia masuala yao kwa maafikiano mazito na yenye udhia baina ya makabila ya kiarabu na wakayaheshimu maafikiano hayo hadi mwisho. Na kwenye matukio mengine waliweka nadhiri zichoshazo mno na zisizovumilika, lakini wakafanya juhudi zote katika kuzitimiza.

Alipokuwa akichimba Zamzam, Abdul-Muttalib alihisi kwamba kutokana na kutokuwa kwake na watoto wengi cheo chake kilikuwa dhaifu miongoni mwa Waquraishi kwa kiasi fulani. Hivyo basi aliamua kuweka nadhiri kwamba idadi ya wanawe itakapofikia kumi atamdhabihi mmoja wao mbele ya Al-Ka’ba. Hata hivyo, hakumweleza yeyote yule kuhusiana na kule kuiweka nadhiri hii.
Kwa kadiri muda ulivyopita idadi ya wanawe iliongezeka na kufikia kumi, na hivyo ule muda wa kuitimiza nadhiri ile ukafika. Kule kuiwazia tu azma hii kulikuwa mtihani mkubwa kwake. Hata hivyo, alichelea kubakia nyuma katika utekelezaji wa jukumu hili na kwa kufanya hivyo akawa mmoja wa wale walioshindwa katika kuzitimiza ahadi zao hivyo akaamua kuwaeleza wanawe jambo lile, na baada ya kuipata ridhaa yao, amchague mmoja wao kwa ajili ya lengo hilo kwa kupiga kura. 25

Kule kupiga kura kulifanywa na kura ilimwangukia Abdullah (baba yake Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Mara moja Abdul-Muttalib aliukamata mkono wa Abdullah na kumwongozea kwenye madhabahu ya kudhabihia.

Waquraishi wanaume na wanawake walipopata habari za nadhiri ile na kule kupiga kura wakahuzunika mno. Mafuriko ya machozi yalitiririka mashavuni mwa watu. Mmoja wao alisikika akisema: “Oh! Ni bora kwamba wangaliniua mimi badala ya kijana huyu.”

Machifu wa Waquraishi walikuwa wakisema: “Kama uhai wake ungaliweza kufidiwa kwa mali, tuko tayari kuutoa utajiri wetu wote mbele yake.” Abdul-Muttalib hakufahamu afanye nini mbele ya hisia za watu zivumazo.

Alijifikiria asije akawa mkosefu katika kumwasi Allah na kuivunja nadhiri yake. Ingawa aliyafikiria yote hayo, vile vile alikuwa akilifikiria suhulisho la tatizo hili. Mmoja wa wale waliokuwapo pale alisema: “Lipeleke tatizo hili kwa mmoja wa wataalamu wa kiarabu.

Inawezekana kwamba akaupendekeza ufumbuzi fulani.” Abdul-Muttalib na machifu wa kabila waliliafiki pendekezo lile na wakaondoka kuelekea Yathrib alikokiishi mtaala- mu yule. Yule mtaalamu aliomba aachwe kwa muda wa siku moja ndipo atoe jibu. Siku iliyofuatia watu wote walimwendea. Yule mtaalamu akauliza: “Ni dia gani mliyoiweka kwa mtu mmoja.” Wakamwambia kuwa ilikuwa ni ngamia kumi. Hapo yule mtaalamu akasema: “Hamna budi kupiga kura baina ya ngamia kumi na yule mtu mliyemchagua kudhabihi- wa. Kama kura ikimwangukia mtu yule basi ipandisheni idadi ya ngamia iwe mara dufu (yaani ishirini). Na kama kura ikimwanguka tena mtu yule basi ipandisheni idadi ya ngamia iwe mara tatu (yaani thelathini) na pigeni kura tena, na endaleeni kufanya hivyo hadi kura iwaangukie ngamia.

Ushauri uliotolewa na mtaalamu yule ulizituliza hisia za watu, kwa sababu iliwawia rahisi kuwadhabihi ngamia mia moja ikilinganishwa na kumwona kijana kama vile Abdullah akigaagaa kwenye damu. Alfajiri moja, baada ya kurejea kwao Makkahh, kazi ya kupiga kura ilifanywa kwa mara ya kumi, wakati idadi ya ngamia ilipopanda na kuwa mia moja, ile kura ikawaangukia wale ngamia. Wokovu na usalama wa Abdullah ulizaa kila hisia isiyo na kifani.

Hata hivyo, Abdul-Muttalib akasema: “Ni bora kwamba nipige kura tena ili niwe na uhakika kwamba Allah karidhika na kitendo changu hiki. Hivyo akaipiga kura ile mara tatu na kila mara kura iliwaangukia wale ngamia mia moja. Hivyo alishawishika na radhi ya Allah na akaamrisha kwamba ngamia mia miongoni mwa ngamia wake, wachinjwe kwenye siku ileile mbele ya Al-Ka’ba na asiwepo mwanaadamu wala mnyama atakayezuiwa kula nyama ya ngamia hao.26

Machafuko Ya Mwaka Wa Ndovu

Tukio kuu litukiapo katika taifa, kiini cha sababu zake mara nyingi huwa za kidini, na mara chache huwa za kitaifa na kisiasa. Kwa kawaida huheshimiwa na umma, na kwa sababu hii huchukuliwa kuwa ndio mwanzo wa historia kwa ajili ya matukio ya siku za kale na zijazo. Kwa mfano, kazi ya Nabii Musa (a.s.) na kuhajiri kwa Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) ni mwanzo wa historia kwa Wayahudi, Wakristo na Waislamu na wafuasi wa dini hizi huyahesabu matukio ya maisha yao wakirejea kwenye matukio haya.

Kwenye nyakati fulani fulani, baadhi ya mataifa ingawa wanayo historia ya kimsingi, vilevile huyachukulia baadhi ya matukio kuwa ndio mwanzo wa historia yao. Kama vile tuyaonavyo Mapinduzi Makuu ya Ufaransa na Mapinduzi ya Kikomunisti ya mwezi wa Oktoba 1917 katika Jamhuri ya Muungano ya Kisovieti ni mwanzo wa historia ya matukio mengi kwenye nchi za Magharibi. Mataifa yasiyostaarabika, yaliyonyimwa vyama vya kisiasa na kidini kama hivyo, kwa kawaida huyachukulia matukio yasiyo ya kawaida kuwa ndio msingi wa histoia yao.

Kwa sababu hii, Waarabu wa Zama za ujinga, kutokana na kutokuwa kwao na ustaarabu ufaao, huyachukulia matukio yasiyofaa kama vile vita, matetemeko ya ardhi, njaa, na matukio mengine yasiyofaa kuwa ndio kipimo na asili ya historia yao.

Katika hali hii, tunaona katika kurasa za historia, idadi kadhaa ya vianzio vya historia ya Waarabu, cha mwisho miongoni mwao kilikuwa ni ghasia za Mwaka wa Ndovu, yaani yale mashambulio ya Abraha ili kuibomoa Al- Ka’ba, tukio ambalo baadae likawa mwanzo wa historia ya matukio mengineyo. Hapa chini tunatoa maelezo marefu na mchanganuo wa tukio hili lililo kuu, lililotokea katika mwaka 570 Masihiya, mwaka aliozaliwa Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.)

Asili Ya Tukio Hili:

Tukio la ‘Watu wa Ndovu’ limetajwa kwa ufupi kwenye Qur’ani Tukufu na, baada ya kuisimulia hadithi hii, tutazitaja aya zilizofunuliwa kuhusiana na tukio hili. Wanahistoria wamekitaja chanzo cha tukio hili kama ifuatavyo:

“Baada ya Mfalme Zu Nuwaas wa Yemen kuimarisha mji mkuu wa serikali yake, akiwa kwenye moja ya safari zake alipitia mjini Yathrib (Madina). Wakati ule mji wa Yathrib ulikuwa na hadhi kubwa ya kidini. Kikundi cha Wayahudi kiliishi kwa wingi hapo na kujenga masinagogi kwenye sehemu mbalimbali za mji ule. Wayahudi wenye bahati njema (matajiri) walimkaribisha vizuri mno mfalme yule na wakamtaka awe Myahudi ili kwamba, wakiwa chini ya ulinzi wa serikali yake, wataweza kubakia salama kutokana na mashambulio ya Warumi Wakristo na Waarabu Waabuduo masanamu.

Juhudi zao kwenye jambo hili zilizaa matunda, Zu Nawaas aliifuata dini ya Kiyahudi na akafanya juhudi zote alizoziweza katika kuiendeleza dini ile. Watu wengi walimwelekea kwa kumwogopa. Baadhi yao waliadhibiwa kwa adhabu kali kwa kuwa kwao na maoni tofauti. Hata hivyo, watu wa Najran walioingia kwenye Ukristo muda fulani kabla ya hapo, hawakuwa tayari kwa gharama yoyote ile, kuiacha dini yao na kuyafuata mafundisho ya dini ya Wayahudi. Mfalme wa Yemen alichukizwa mno na uasi na dharau yao na akaja na jeshi kubwa kuwatiisha waasi. Amiri jeshi wa jeshi lile alipiga kambi karibuni na jiji la Najran akachim- ba handaki hapo, akawasha moto mkubwa kwenye handaki lile na kuwaogopesha wapinzani wake kwa kuwachoma.

Hata hivyo, watu mashujaa wa Najran, waliokuwa na itikadi yenye nguvu mno juu ya Ukristo, hawakutishika. Walikipenda kifo na kuchomwa moto kwa mikono miwili na miili yao ililiwa na miali ya moto.” 27

Mwanahistoria mashuhuri wa Kiislam, Ibn Athir Jazari ameandika hivi: “Wakati ule ule mmoja wa wakazi wa Najran aliyeitwa Daws alikwenda upesi–upesi kwa Kaisari, Mtawala wa Kirumi, aliyekuwa mlinzi mkuu wa Ukristo wakati ule, na akamweleza tukio lile. Pia alimwomba yule Mfalme amwadhibu muuaji yule aliyeizima taa ya mwongozi kule Najran na aidumishe kwa marefu zaidi ile nguzo ya Ukristo kwenye eneo lile iliyokuwa ikilegalega.

Yule mtawala wa Kirumi aliidhihirisha huzuni yake na huruma na akasema: “Kwa kuwa mji mkuu wa serikali yangu uko mbali mno kutoka nchini mwenu, ninamwandikia barua Negusi, Mfalme wa Ethiopia, alipize kisasi juu ya katili yule kwa ajili ya kuwaua watu wa Najran. Yule Mnajrani akaichukua ile barua ya Kaisari na akaipeleka Ethiopia upesi kwa kadiri alivyoweza. Alipofika kule alimwelezea Negus hadithi yote. Hisia za heshima za Mfalme wa Ethiopia ziliibuka. Alipeleka nchini Yemen jeshi lililo na zaidi ya askari sabini elfu likiwa chini ya amiri jeshi Mwafrika aliyeitwa Abraha Ashram. Jeshi hili la Waethiopia lenye uongozi mzuri na zana bora na za kutosha likaivuka bahari (ya Sham) na kupi- ga kambi kwenye pwani ya Yemen. Zu Nawaas alikamatwa kwa ghafla. Matendo yote haya yalidhihirisha kwamba hayatoshi na hakuna jibu lolote alilolipokea kuhusiana na barua aliyowaandikia machifu wa kikabila aki- waomba washiriki mwenye vita ile. Shambulio dogo tu lilitosha kuubomoa msingi wa serikali yake (Zu Nawaas) na ile nchi ya Yemen yenye watu wengi ikawa milki ya Serikali ya Ethiopia. Mfalme wa Ethiopia alimteua amiri jeshi wa jeshi lile, Abraha kuwa kaimu katika eneo lile.

Abraha alifurahi sana kwa kuwalipizia kisasi Wakristo wa Najran na kupata ushindi na akaanza kuishi maisha ya kiungwana. Ili ajipatie upendo zaidi mbele ya Mfalme wa Ethiopia alijenga kanisa la fahari mjini San’a lisilokuwa na kifani kwenye zama zile kwa utukufu wake kisha akamwandikia barua Negus akisema hivi: “Kwa kupatana na matakwa yako Jalali Mfalme ujenzi wa kanisa umetimia. Ninategemea kwamba nitaweza kuwafanya watu wa Yemen waache kwenda hija kwenye Al- Ka’ba, na nafasi yake itachukuliwa na kanisa hili.” Mambo yaliyomo kwenye barua ile yalipofahamika, yalitokea mambo yasiyofaa miongoni mwa makabila ya kiarabu. Hali hii ilikithiri mno kiasi kwamba usiku mmoja mwanamke wa kabila la Bani Afqam aliunajisi ua wa kanisa lile.

Kitendo hiki kilichoonyesha dharau kubwa, utwezo na uadui wa Waarabu kwa kanisa la Abraha, kuliishtua Serikali ya wakati ule. Zaidi ya hapo kwa kadiri Abraha alivyozidisha kulinakshi na kulipamba lile kanisa, ndivyo watu walivyozidi kujiambatanisha na Al-Ka’ba.

Matukio haya yalimfanya Abraha aape kwamba ataivunja Al-Ka’ba. Aliandaa jeshi kwa lengo hili, akawaweka ndovu wapiganao kwenye mstari wa mbele na akaamua kwenda kuivunja ile Nyumba ambayo msingi wake ulijengwa na yule mwasisi wa Upweke wa Allah, Nabii Ibrahim (a.s.).

Machifu wa Bara Arabu walitambua ya kwamba hali ile ilikuwa nyeti na ya hatari na wakawa na yakini kwamba uhuru na taifa la kiarabu binafsi ulikuwa unaelekea kwenye kuvunjika. Vile vile ushindi wa Abraha wa siku zilizopita uliwaweka mbali na uchukuaji wa maamuzi yenye maana.

Hata hivyo, machifu wa makabila yenye shauku walimkabili Abraha walipigana kwa ushujaa mkubwa. Kwa mfano, Zu Nafar, aliyekuwa mmoja wa watu wakuu wa Yemen aliwanasihi watu wake, kwa hotuba motomoto, kuihami nyumba takatifu (Al-Ka’ba). Hata hivyo, jeshi kubwa la Abraha lilizikata safu zao zilizoandaliwa upesi sana. Baada ya hapo, Nafil mwana wa Habib alifanya mapigano makubwa, lakini watu wake nao walishindwa. Yeye mwenyewe alikamatwa na akamwomba msamaha Abraha. Abraha alikubali kulitimiza ombi lake kwa sharti la kwamba ayaongoze majeshi yake kuelekea Makkahh. Hivyo Nafil akawa mtumishi wake na akamwongoza hadi alipofika Taif.

Hapo alimpa kazi hiyo mmoja wa marafiki zake aliyeitwa Ayurgha! Huyu kiongozi mpya aliwaongoza hadi Mughmas – sehemu iliyokuwa karibu na Makkahh – na hapo jeshi la Abraha likapiga kambi. Kufuatana na desturi za kale, Abraha alimwamrisha mmoja wa maafisa wake kuwateka ngamia na wanyama wengine wa kufugwa wa Tahamah. Miongoni mwa ngamia waliotekwa, 200 walikuwa mali ya Abdul-Muttalib. Baadae Abraha alimwamrisha afisa wake mwingine aliyeitwa Hanatah kumpelekea chifu wa Waquraishi ujumbe wake.

Alimwambia Hanatah hivi: “Ninaweza kuiona hali halisi ya maangamizo ya Al-Ka’ba. Bila shaka kwenye hatua ya kwanza kabisa Waquraishi watapinga. Hata hivyo, ili kuthibitisha kwamba damu yao haimwagwi, huna budi kwenda Makkahh upesi sana. Huko ukaonane na chifu wa Waquraishi na umwambie kwamba lengo langu ni kuibomoa Al- Ka’ba na kama Waquraishi hawatapinga, watakuwa salama kutokana na usumbufu.” Yule mjumbe aliyetumwa na Abraha alifika Makkahh na akaonana na makundi mbalimbali ya Waquraishi na wakalijadili jambo hilo kwenye sehemu mbalimbali. Alipoulizia juu ya chifu wa Waquraishi alipelekwa nyumbani kwa Abdul-Muttalib. Baada ya Abdul-Muttalib kuusikia ujumbe wa Abraha alisema hivi: “Sisi kamwe hatuelekei kwenye mapigano. Al-Ka’ba ni Nyumba ya Allah. Ni Nyumba aliyoiasisi Nabii Ibrahim (a.s.). Allah atafanya lolote lile Alionalo kuwa linafaa.”

Vile vile yule afisa wa Abraha aliidhihirisha ridhaa yake kwa kuyasikia yale maneno ya chifu wa Waquraishi yaliyo laini na yenye maafikiano na yaliyoiashiria itikadi yake ya kiroho. Hivyo basi, alimwomba Abdul- Muttalib akubali kufuatana naye hadi kambini kwa Abraha.

Abdul-Muttalib Aenda Kambini Kwa Abraha

Abdul-Muttalib alikwenda kambini kwa Abraha akifuatana na wanawe wachache. Busara, utukufu na heshima ya huyu kiongozi wa Waquraishi vilimfanya Abraha ampende na kumheshimu mno kiasi kwamba alishuka kwenye kiti chake cha enzi, akampa mkono Abdul-Muttalib na akamfanya aketi ubavuni kwake. Kisha, kwa heshima kuu akamwuliza Abdul- Muttalib, kupitia kwa mkalimani ni kitu gani kilichomleta pale na alihitaji nini. Akilijibu swali hili alisema: “Wale ngamia wa Tahamah, ambao pia walikuwa na ngamia wangu mia mbili, wametekwa na askari wako. Ningependa kukuomba uamrishe kwamba ngamia hao warejeshwe kwa wenyewe.” Abraha alijibu hivi: “Uangavu wa wajihi wako wenye heshi- ma takatifu ulinifanya nikufikirie kuwa u mtu mkubwa sana. Hata hivyo, ombi uliloliomba kwa ajili ya vitu vidogo mno kumeipunguza thamani yako machoni mwangu. Ukiuzingatia ukweli uliopo kwamba mimi nimekuja kuibomoa na kuiharibu Nyumba takatifu ya jadi zenu nilitege- mea kwamba utazungumzia juu ya Al-Ka’ba na kuniomba niache kulitimiza lengo langu hili ambalo litaupiga pigo kubwa uhuru wenu na maisha yenu ya kisiasa na kidini. Mimi sikutegemea kwamba utazungumzia juu ya vitu vichache vidogo na visivyo na thamani na kuom- ba kwa ajili hiyo.”

Akiyajibu maneno ya Abraha, Abdul-Muttalib aliitam- ka sentensi ambayo, thamani na faida yake bado vimehifadhiwa. Alisema: “Mimi ndiye mwenye ngamia hao. Hii Nyumba nayo inaye Bwana wake mwenye kulikinga kila lenye kujipenyeza juu yake.” Abraha aliposikia hivyo alitikisa kichwa chake na akasema kwa majivuno: “Hakuna yeyote aliye na nguvu zaidi ya kuweza kunizuia nisiitimize azma yangu.” Kisha akaamrisha kwamba ile mali iliyonyakuliwa irudishwe kwa wenyewe.”

Waquraishi Wasubiri Kurejea Kwa Abdul-Muttalib

Waquraishi walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa kurejea kwa Abdul- Muttalib ili wayajue matokeo ya mazungumzo yake na Abraha. Hivyo basi, alipokutana na machifu wa Waquraishi aliwaambia: “Kimbieni upesi kwenye mabonde na kwenye vilima pamoja na wanyama wenu ili kwam- ba muwe salama kutokana na kila aina ya dhara.” Baada ya hapo watu waliziacha nyumba zao upesi upesi na wakakimbilia vilimani. Wakati wa usiku vilima na mabonde yote yalivuma vilio vya watoto, maombolezo ya wanawake na milio ya wanyama.

Katikati ya usiku ule Abdul-Muttalib na Waquraishi wengine walikishuka kilele cha kilima na wakalifikia lango la Kaabah. Yeye (Abdul-Muttalib), huku machozi yakimchuruzika na moyo ukimuungua, aliishika nyororo ya lango la Al-Ka’ba mkononi mwake na akazisoma beti chache za shairi akizunguma na Allah swt. Alisema hivi: “Ee Allah! Sisi hatuitegemezi imani yetu kwa yeyote yule ila Wewe tu, katika kusalia salama kutokana na ufisadi na madhara yao.

Ee Mola! Wazuie dhidi ya Nyumba Yako takatifu. Adui wa Al-Ka’baa ni yeye yule aliye mshindani dhidi Yako.

Ee Mhifadhi! Wakatilie mbali mikono yao ili kwamba wasiinajisi Nyumba Yako.

Mimi ninayo haki juu ya mali yangu, hivyo basi, ninajitahidi kwa ajili ya usalama wake. Hata hivyo, usalama wa Nyumba Yako ni Jukumu Lako. Usiruhusu kuja kwa ile siku ambayo Msalaba utakuwa mshindi juu yake (Nyumba hii), na wakazi wa nchi zao wakajiingiza nchini Mwako na kuiteka.”

Kisha akaiachia ile nyororo ya lango la Al-Ka’ba na akakimbilia kwenye kilele cha mlima ili aone maendeleo ya jambo lile.

Alfajiri na mapema Abraha na majeshi yake wakajitayarisha kuingia mjini Makkahh. Hata hivyo lilijitokeza kundi la ndege kwa ghafla kutoka upande wa baharini, wakivichukua vikokoto vidogo midomoni na mwenye makucha yao kivuli cha hawa ndege weusi kililifanya anga la juu ya kambi kuwa na giza na silaha zao ndogo zionekanazo kutokuwa na thamani zilizaa athari za ajabu. Ndege hawa wenye silaha za vikokoto hivyo walivimimina vikokoto hivyo kwa amri ya Allah juu ya jeshi la Abraha kwa jinsi ambayo vichwa vyao vilivunjikavunjika na nyama ya miili yao ilitolewa miilini mwao.

Kokoto moja ilimpiga Abraha kichwani, na kwa sababu hii hofu ilimshika na akaanza kutetemeka. Alikuwa na uhakika kwamba ghadhabu ya Allah imeshuka. Kisha akawatupia jicho askari wake na akaona kwamba miili yao imeanguka chini kama majani ya miti. Hivyo basi, mara moja akawaamrisha wale waliosalimika kurudi Yemen na kwenda Sa’na kwa kuipitia ile njia waliyoijia. Jeshi lililosalia likaondoka kuelekea Sa’na kwa kuipitia ile njia waliyoijia. Jeshi lililosalia likaondoka kuelekea San’a laki- ni, lilipokuwa njiani, wengi wa askari wake waliangamia kutokana na majereha na hofu.
Hata Abraha mwenyewe alifika Sa’na akiwa kwenye hali mbaya mno kiasi kwamba nyama ya mwili wake ilipasukapasuka na alikufa kifo kibaya mno.

Tukio hili la kimauti na lisilo kifani limepata kutambulika ulimwenguni kote. Qur’ani Tukufu inaisimulia hadithi ya ‘Watu wa Ndovu’ kwa maneno haya:

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ {1}

أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ {2}

وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ {3}

تَرْمِيهِمْ بِحِجَارَةٍ مِنْ سِجِّيلٍ {4}

فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ مَأْكُولٍ {5}

“Je, hukuona jinsi Allah Alivyolitenda jeshi la Ndovu? Je, Hakuiharibu hila yao kwa kuwapeleka makundi ya mbayuwayu waliowavurumishia mawe ya udogo uliookwa, hivyo Akawafanya (kuwa) kama majani makavu (yaliyoliwa na mifugo)” (Suratul-Fiil, 105: 1-5).

Yaliyosimuliwa kwenye kurasa hizi ni kiini cha historia ya Uislamu inay- olihusu jambo hili28 kwenye Qur’ani Tukufu. Sasa tutayasoma maelezo yaliyotolewa na mfafanuzi mkuu wa Kimisri, Muhammad Abduh na wanachuoni maarufu, Dakta Haikal, aliyekuwa Waziri wa Elimu chini Misri.

Mjadala Wa Kiakili Juu Ya Miujiza

Maendeleo ya mwanaadamu yashangazayo na yaliyopatikama hivi karibuni kwenye nyanja mbalimabli za sayansi za kimaumbile na kukoma kwa maisha na nyingi miongoni mwa nadharia tete (hypotheses) za kisayansi, kumeleta ghasia kwenye nchi za Kimagharibi. Ingawa maelezo juu ya mabadiliko haya yamesimamia kwenye mipito ya kisayansi na yalizun- gukia kwenye mhimili wa sayansi ya kimaumbile pekee (kwa mfano, makisio ya Ptolemy yalionekana kuwa si ya kweli) na hayakuwa na uhusiano wowote na itikadi za kidini, yalizaa matazamio mabaya (pessimism) miongoni mwa matabaka mbalimbali kuhusu nadharia na itikadi zilizo salia.

Siri za haya matazamio mabaya imesimama kwenye ukweli uliopo kwamba, wanachuoni walipoona ya kwamba nadharia za zamani zilizokuwa zikitawala fikara za mwanaadamu na vyuo kwa karne nyingi sasa zimesimama kwenye msingi wa uongo, na mkono wa elimu wenye nguvu na uwezo mkuu wa majaribio, na zaidi ya hapo, haikuwapo taarifa yoyote kuzihusu sayari mbalimbali za angani na miendo yao midogomidogo na kuwa katikati kwa dunia, na vilevile kuhusu korija kadhaa za mafafanuzi; walijifikiria kwamba hakuna mtu ajuaye ya kama je, yale mafafanuzi yaliyosalia ya kidini na kisayansi yaweza nayo kuwa kama yale mengineyo? Jinsi hii ya fikara, pole pole ilizipanda mbegu za shaka akilini mwa wengi wa wanachuoni wa sayansi za kimaumbile na kwenye kipindi kifupi tu, shaka hii ilikua na kuenea kwenye maeneo yote ya sayansi za Ulaya za siku zile kama maradhi ya kuambukiza.

Aidha, ‘Baraza Kuu la kuhukumia wazushi wa Dini’ (Idara ya uchunguzi wa itikadi) na ukali wa wakuu wa Kanisa vilikuwa na fungu kamili katika uotaji, na zaidi ukuaji wa hali hii ya kutokuwa na matarajio mema, kwa sababu wanachuoni wa zama zile waliofaulu katika ugunduzi wa nadharia fulanifulani za kisayansi waliangamizwa na Kanisa kwa adhabu kali na mateso.
Na haina hajja kusema kwamba shinikizo na mateso haya hayana budi kwamba yalizaa matokeo mabaya na tangu kwenye siku hizo ilitabiriwa kwamba, kama katika wakati wowote ule wana vyuoni hawa wataipata nguvu na wakayafanya maendeleo yatoshelezayo kwenye uwanja wa kimaumbile, wataipa dini na uchamungu ‘kwa heri’ kutokana na sera mbaya ya Mapapa.”

Kwa bahati mambo yakapata kuwa hivyo. Kwa kuwa elimu kuhusiana na mambo mbalimbali imekua na wanachuoni wamepenya zaidi na zaidi kwenye uhusiano baina ya viumbe, ilizifunua siri zilizofichikana kutoka kwa mwanadamu kwa karne nyingi, na wakapata elimu juu ya sababu za matukio mengi ya kimaumbile kama vile matetemeko ya ardhi na mvua, pamoja na sababu za magonjwa mbalimbali, hawakufaulu sana juu ya mambo ya kimungu. (Asili, ufufunuo, miujiza na matendo yasiyo ya kawaida ya Mtukufu Mtume s.a.w.w na kadhalika) na idadi ya wenye shaka na wenye kukanusha inayoongezeka siku hadi siku.

Majivuno na kiburi juu ya elimu yao waliyokuwa nayo baadhi ya wanachuoni akilini mwao, na shinikizo la mapapa na makasisi vimekuwa chanzo cha baadhi ya wanasayansi kuyatazama mambo yote ya kidini kwa dharau na kutojali. Hawakukubali tena kuwa majina ya Torati au Injili yatajwe. Kwa mujibu wa fikara zao, tukio la fimbo ya Nabii Musa (a.s.) na mkono wake ung’aao havina budi kuchukuliwa kuwa ni hadithi tu, na kupulizia kwa Nabii ‘Isa’ (a.s.) kulikohuisha wafu wengi kwa idhini ya Allah, vile vile kulikuwa hadithi ya kubuniwa tu.

Ilitokea hivyo kwa sababu kiburi juu ya maendeleo ya elimu ya kisayansi na kumbukumbu ya shinikizo waliloshinikizwa nalo hapo kale viliwafanya wajifikirie kwamba: “Yawezekanaje kwamba kinapokosekana kisababisho cha kawaida, kipande cha mti kijitwalie umbo la joka, au wafu waweze kufufuka kwa njia ya dua?” wanachuoni waliolewa na mafanikio katika uwanja wa sayansi walifikiria kwamba walishajipatia funguo ya nyanja zote za elimu na wameuelewa uhusiano baina ya viumbe vyote na matukio.

Ni kwa sababu hii kwamba hawakuona uhusiano, japo ulio mdogo tu, baina ya kipande cha mti kikavu na chatu, au baina ya dua na usikivu wa mtu kwa upande mmoja na kufufuka kwa wafu kwa upande mwingine. Hivyo basi, waliyaangalia mambo haya kwa shaka, na kusita sita au kuyakana kabisa.

Mtindo Wa Fikara Za Baadhi Ya Wanachuoni

Siku hizi mtindo huu wa kufikiria, ukiwa na mabadiliko madogo, umechukuliwa na wanachuoni wa Kimisri. Wanachuoni hawa ambao kwa kweli wao ni kiungo baina ya vyuo vya elimu vya Mashariki na vile vya Magharibi na kwa miaka mingi na mapema kuliko yeyote yule wamekuwa wakihamisha elimu na mitindo ya fikara ya watu wa Magharibi na kuwapelekea wale wa Mashariki, na kwa kweli wanafikiriwa kuwa wao ni daraja ya elimu na uhusiano wa kielimu baina ya pande mbili za nchi hizi, zimekuwa na ushawishi zaidi kuliko mtu yeyote mwingine kwa mtindo huu wa fikara (kwa kweli zikiwa na matengenezo maalum) na wanafuata mtindo huu katika mambo ya kuelezea na uchambuzi wa matatizo ya kihistoria na kisayansi.

Baadhi yao wameichagua njia ambayo kwayo wanataka kuwaridhisha Waislamu waiaminio maana ya dhahiri ya Qur’ani Tukufu na hadith za dhahiri na pia kuzichukua fikara za wanasayansi, au kwa kutolitoa wazo lisiloweza kuelezeka katika mwanga wa kanuni za sayansi za kimaumbile.

Kwa upande mwingine wanaona kwamba Qur’ani Tukufu ina nyororo ya miujiza isiyokanika na Kitabu hiki ni hukumu ya mwisho kwa Waislamu, na chochote kile ikisemacho ni sahihi na ni chenye kuafikiana na ukweli, kwa upande mwingine, wanaona kwamba sayansi za kimaumbile na wenye kuiunga mkono elimu ya kidunia hawayatambui mambo haya ambayo kulingana na fikara zao (zinazong’ang’ania kwenye kisababisho cha asilia kwa kila tukio la kimaumbile) yako kwenye kutoafikiana na kanuni za kisayansi.

Matokeo ya mambo haya mawili, kwa mujibu wa itikadi zao, hakuna hata moja lenye kunyambulika, na sasa wameishika njia nyingine ambayo kwayo wanataka kuyaridhisha makundi yote mawili (lile la dini na lile la sayansi). Yaani wanaihami maana ya dhahiri ya Qur’ani Tukufu na hadithi zenye maana ya dhahiri na vilevile wasikiseme chochote kilicho dhidi ya sheria za kisayansi.

Kufuatana na lengo hili, wanajitahidi kuieleza miujiza na matendo yasiyo ya kawaida ya Mitume (a.s.) kulingana na vigezo vya sayansi ya kisasa na kuzieleza maana za miujiza kwa njia ambayo yaonekana kuwa ni matukio ya kawaida tu. Kwa njia hiyo wameihami heshima istahiliyo ya Qur’ani Tukufu na hadithi zenye maana ya dhahiri na vilevile wamejipa uhuru kutokana na kila aina ya matazamio ya matokeo mabaya na kutokukubalika kwa mafunzo yao. Tukitoa mfano wa jambo hili, tunatoa hapa chini maelezo aliyoyatoa Muhammad Abduh, mwanachuoni maarufu wa Kimisri kuhusu tukio la ‘Watu wa Ndovu’ lililotajwa kwenye Qur’ani Tukufu:

“Ni maradhi ya ndui na homa ya taifodi iliyosababishwa na vumbi lenye kokoto za mawe lililoenea miongoni mwa jeshi la Abraha kupitia wadudu kama vile mbu na inzi. Na maneno “mawe ya udongo uliookwa” yana maana ya “udongo wenye kokoto za mawe” uliotawanyishwa na upepo kila mahali na hivyo basi, ukaganda kwenye miguu ya wadudu wale. Matokeo ya kukutana kwa wadudu wale na miili ya wanadamu, wadudu wa maradhi (germs) waliingia kwenye vinyweleo vya ngozi ya mwili wa mwanaadamu na kufanya madonda yenye maumivu makali na machafu yalitokeza humo. Na wadudu hawa ni askari wa Mwenyezi Mungu walio na nguvu nyingi waitwao ‘Microbes’ katika istilahi za kisayansi.”

Mwandishi mmoja wa kisasa akiyaunga mkono maoni aliyoyatoa mwanachuoni tuliyemtaja hapo kabla, anasema kwamba, neno ‘Tayr’ lililotumika mwenye Qur’ani Tukufu lina maana ya cho chote kile kiruka- cho na ni pamoja na mbu na inzi.

Kabla hatujafikiria kwa makini maneno ya hawa waandishi wawili tuliowataja tunafikiria kwamba ni muhimu kunukuu tena hapa chini zile aya zilizofunuliwa kuhusiana na wale ‘Watu wa Ndovu’. Allah, Mwenye nguvu zote anasema hivi kwenye sura al-Fiil:

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ {1}

أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ {2}

وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ {3}

تَرْمِيهِمْ بِحِجَارَةٍ مِنْ سِجِّيلٍ {4}

فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ مَأْكُولٍ {5}

“Je, hukuona jinsi Allah alivyolitendea Jeshi la Ndovu? Je hakuiharibu hila yao kwa kuwapelekea makundi ya mbayuwayu waliowavurumishia mawe ya udogo uliookwa, hivyo akawafanya (kuwa) kama majani makavu yaliyoliwa na mifugo.” (Suratul-Fiil, 105: 1-5)

Kutokana na maelezo haya aya hizi zinaonyesha kwamba watu wa Abraha walikumbwa na ghadhabu ya Allah na sababu ya kifo chao ilikuwa ni hizi kokoto za udongo wa kuoka ambazo hawa ndege walizichukua na kuzirujumu juu ya vichwa, nyuso na miili yao.

Kujifunza aya hizi kwa undani na moja moja kunatuongoza kwenye kuamini kwamba kifo cha watu hawa kilitokana na silaha hizi zisizo za kawaida zionekanazo kuwa si zenye thamani na dhaifu, za kokoto za udongo uliookwa, lakini kwa kweli zilikuwa zenye nguvu na zenye kuleta madhara makuu. Kwa sababu hii, aya hizi za Allah haziwezi kutafsiriwa kwa maana zozote zile zipewazo, kwa njia ya maelezo yaliyo katika hali ya kutoafikiana na maneno yake ya dhahiri, na pale utolewapo uthibitisho ukubalianao na aya hizo, juu ya usahihi wa maelezo hayo.

Mambo Muhimu Kuhusu Maelezo Tuliyoyatoa Juu

Vilevile maelezo tuliyoyatoa hapo juu hayawezi kulidhihirisha tukio lote kuwa ni la kawaida na vivyo katika hadithi hii, husalia baadhi ya mambo yawezayo tu kuelezwa kwa kutoa sababu zisizo za kawaida. Hivyo basi, japo tuchukulie kuwa vifo na maangamizo ya watu wale yalitokana na ‘microbes’ wa ndui na homa ya taifoidi, swali hubaikia ni kwa vipi na ni kwa njia gani ndege hawa walipata mwongozo na mafunzo hadi wakaelewa kwamba ‘microbes’ wa homa la ndui na taifoidi waishakaa mwenye hizi kokoto za udongo wa kuoka katika ule muda maalum, na badala ya kwenda kuitafuta riziki yao, walijikusanya pamoja wakizielekea zile kokoto za udongo wa kuoka na wakiwa wamezishika kwa midomo yao wakawarujumu watu wa Abraha kama vile jeshi lishambuliavyo adui wake? Katika hali hii je, tunaweza kulichukulia tukio hili lote kuwa ni la kawaida na la kimumbile tu? Kama tuko tayari kukubali kwamba mambo yote haya yalitokea kwa mujibu wa amri ya Allah na kwamba nguvu isiyo ya kawaida ilikuwa ikifanya kazi kwenye tukio hili, basi uko wapi umuhumu wetu wa kuifikiria sehemu tu ya tukio hili kuwa ndiyo ya kawaida na tukimbie kuzieleza sababu zake.

Wadudu wadogo mno waitwao ‘microbes’ walio maadui wa wanaadamu wote, hawana uhusiano na yeyote kutokana na hali hii, jambo hili laweza kuelezekaje kwamba wadudu hawa walishambulia jeshi la Abraha pekee na kuwaacha wakazi wa Makkahh? Vitabu vya historia tulivyonavyo hivi sasa vinakubaliana kwa pamoja kwamba hasara yote waliyoipata ni askari wa Abraha tu, na Waquraishi na Waarabu hawakupata dhara lolote japo lililo dogo tu ingawa homa ile ndui na taifodi ni maradhi yanayoambukiza na vitu mbalimbali vya kimaumbile huvisafirisha kutoka sehemu moja hadi nyingine na wakati mwingine hutokea kwamba huiangamiza nchi nzima. Katika hali hii, je, tukio tunalolizungumzia laweza kuchukuliwa kwamba ni jambo la kawaida?

Tofauti za kimaoni walizonazo wale wanaoyatoa maelezo haya, kuhusu aina hii ya ‘microbes’ yenyewe huidhoofisha dhana yao. Wakati mwingine wanasema kwamba walikuwa wadudu wa kipindupindu na mara kwa mara wanadai kwamba walikwa ni wale wa homa ya ndui na taifoidi, ambapo bado hatujapata taarifa yoyote iliyo sahihi na ya kutegemeka kuhusiana na kutoafikiana huku. Miongoni mwa wasimuliaji wa hadithi ni Akramah pekee, ambaye, yeye mwenyewe yu asili ya kutoafikiana miongoni mwa wanachuoni, ameufikiri uwezekano huu na miongoni mwa wanahistoria Ibn Athri, alipokuwa akiunukuu uwezekano huu kuwa ni kauli dhaifu, amekwenda moja kwa moja kuikanusha.29

Maelezo yastaajabishayo zaidi ni yale aliyoyatoa mwandishi wa kitabu kiitwacho ‘Hayat-i-Muhammad’ (Dakta Haikal, aliyekuwa Waziri wa Elimu wa Misri), alipokuwa akiisimulia hadithi ya ‘Watu wa Ndovu.’ Ingawa jambo lililo machoni mwake ni ile aya isemayo: ‘Tuliwapelekea makundi ya ndege’, yeye, baada ya kuinukuu Sura ya al-Fiil, anasema hivi, kuhusiana na vifo vya jeshi la Abraha: “Pengine wadudu wa kipindupindu walikuja na upepo kutoka kwenye upande wa baharini.” Sasa kama upepo umeleta wadudu wa kipindupindu kwa nini wale ndege walikuwa wakirukaruka vichwani mwao?

Zaidi ya hapo, hao ndege walikuwa waki- wavurumishia hizo kokoto za udogo uliookwa: Sasa kokoto hizi za udon- go uliookwa zilikuwa na kazi gani kwenye vifo vyao? Hivyo basi hatuna budi kuiepuka njia hii ya kufikiria na pasipo haja yoyote tuieleze miujiza mikuu ya Mitume kwa njia hii. Kimsingi, hali ya dini kwenye mambo haya, mbele ya sayansi za kimaumbile, ambazo maeneo yao ni madogo katika uhusiano na mambo ya kimaumbile, ni maradufu. Hivyo basi, hatuna budi kutoiacha misingi ya dini iliyokwisha kudumishwa kwa kutaka kuwaridhisha watu wachache wenye elimu ndogo ya dini na wasio na taarifa juu ya mambo ya aina hii, na hasa pale tusipokuwa na lazima yoyote ya kufanya hivyo.

Mambo Mawili Yaliyo Muhimu

Tungalipenda kuyataja mambo mawili yaliyo muhimu, hapa: Hakutakuwapo kutoafikiana kuhusu ukweli uliopo kwamba kwa maelezo tuliyoyataja hapo juu, hatudhamirii kuyasahihisha na kuyaeleza mambo ambayo watu huyahusisha na Mitume na viongozi wa kidini kwa njia ya uzushi na mambo yasiyoungwa mkono na ushahidi wowote ukubalikao, na ambayo kwa kawaida yana hali ya kiushirikina. Maana yetu ni kwamba, kutegemeana na uthibitisho ukubalikao, tulionao mkononi, Mitume wa Allah waliyatenda matendo yasiyo ya kawaida ili kuuthibitisha uhusiano wao na ulimwengu wa kiroho. Lengo letu ni kuzihami aina hizi za miujiza. Kamwe hatusemi kwamba muujiza hauhitaji kanuni ya kisababisho na matokeo. Tunaiheshimu kanuni hii kikamilifu na tunaamini kwamba matukio yote ya ulimwengu hapa yana visababisho na hakuna jambo lijitokezalo pasi na kisababisho. Hata hivyo, tunalolisema ni kwamba si muhimu kwamba visababisho vya miujiza ni lazima kuwa kwenye mkumbo wa visababisho vya kawaida na vya kimaada. Hivyo basi miujiza na matendo ya Mitume yasiyo ya kawaida yana visababisho ambavyo havikubaliani na visababisho vya kawaida vya kimaumbile na kila mtu si mtambuzi wa siri hizi.

Baada Ya Kushindwa Kwa Abraha

Ghasia za ‘Mwaka wa Ndovu,’ kifo cha Abraha na maangamizi ya maadui wa Al-Ka’ba na Waquraishi, kuliwatukuza mno wakazi wa Makkahh na Al-Ka’ba machoni pa ulimwengu wa kiarabu. Sasa hakuna mtu aliyethubu- tu kufikiria kuwashambulia Waquraishi au kuwafanyia madhara yoyote au kuibomoa Nyumba ya Allah. Mawazo ya watu wote yalikuwa kwamba: “Allah, kwa ajili ya heshima ya Nyumba Yake na kwa ajili ya heshima na umaarufu wa Waquraishi, amemfanya adui yao wa jadi kugaagaa kwenye vumbi na damu. Kutokana na hukmu hii tukufu ya Mwenyezi Mungu, Waquraishi na Al-Ka’ba wamekuwa wenye kuheshimika mbele ya Watu.” ni kwa mara chache mno walifikiria kwamba jambo hili limetokea kwa ajili tu ya ulinzi wa Al-Ka’ba, na kwamba umaarufu au udogo wa Waquraishi hauna lolote lihusianalo nalo. Jambo hili lathibitika na ukweli uliopo kwamba, machifu wa maadui wa zama zile waliwashambulia Waquraishi mara kadhaa lakini katu hawakukabiliwa na hali hii.

Ushindi na mafanikio haya, yaliyopatikana bila ya jasho lolote na bila ya hata tone moja la damu ya Waquraishi kumwagika, yalizaa fikara mpya akilini mwao na majivuno yao, kiburi na kutojali kwao vikazidi. Sasa wakaanza kuamini udhaifu wa watu wengine, kwa sababu walijifikiria kuwa wao ni kundi mashuhuri miongoni mwa Waarabu na wakafikiria kwamba wao peke yao ndio waliopasika na uangalizi wa yale masanamu mia tatu na sitini na kupata msaada wao.

Tangu siku ile walianza kufanya karamu kubwa za furaha zisizo na mwisho na anasa zisizokuwa na kikomo. Waligugumia kikombe baada ya kikombe cha tembo ya mitende na mara kwa mara walijitia kwenye ulevi wa pombe katika eneo la Al-Ka’ba, na kulingana na methali yao, ‘walizitumia siku njema za maishani mwao.’ kwenye ujirani na masanamu yaliyotengenezwa kwa mawe na miti yaliyowahusu makabila ya kiarabu.

Katika mikutano hiyo, kila aliyekuwa amesikia hadithi yoyote ile juu ya Wamanzariya wa Hirah na Waghassaniya wa Sham na makabila ya watu wa Yemeni aliwasimulia wenzie nao waliamini ya kwamba walikuwa wakiyapata maisha yao ya furaha kutokana na uangalizi wa masanamu yaliyowadhoofisha Waarabu wa kawaida wakilinganishwa nao, na wamewapa (wao Waquraishi) fadhila juu ya wengineo wote.

Mipaka Ya Kimawazo Ya Waquraishi

Mungu aepushie mbali kwamba huyu kiumbe mwenye miguu miwili (mwanadamu) siku moja aweze kuja kupata upeo wa maisha ulio wazi na aweze yeye mwenyewe kujidhania kuwa ni wa tabaka la kufikirika kupendelewa zaidi. Ni katika siku hiyo ambapo kwamba atajitengea maisha na uhai kwa ajili yake mwenyewe tu, na atakuwa haamini kwamba viumbe wenzie nao wanayo haki yoyote angalau kidogo ya uhai na thamani.

Ili kuuthibitisha ukuu na ubora wao juu ya wengineo, Waquraishi walia- mua siku ile kwamba hawatawaheshimu hata kidogo watu wa ‘Hil’ (lile eneo linalofikia umbali wa ligi nne – takriban kama maili kumi na mbili hivi – kutoka kwenye Al-Ka’ba kwenye pande zote nne huitwa ‘Haram’ na eneo lililo nje ya umbali huo huitwa ‘Hil’), kwa sababu, kulingana na maoni yao, watu wengine walikuwa wakitegemea Hifadhi yao, na wameona kwa macho yao kwamba wao (Waquraishi) walikuwa ndio walengwa wa upendeleo wa miungu wa Al-Ka’ba.

Tangu wakati ule na kuendelea, Waquraishi walianza kuwa wakali kwa watu wengine. Wakiendesha udikteta kamili, waliamua kwamba kila watu wa ‘Hil’ wajapo kuhiji, wasivitumie vyakula waviletavyo bali wajipatie chakula kutoka kwa watu wa ‘Haram.’ Vile vile waliamua ya kwamba wakati wa kufanya ibada ya Tawafu wasivae nguo yoyote ile ila vazi la kienyeji la watu wa Makkahh lenye sifa za kitaifa.

Kama mtu hakuweza kuikabili gharama ya vazi lile, basi ilimlazimu mtu yule kuhiji bila ya nguo yoyote. Ama kuhusu baadhi ya Waarabu wenye vyeo vikuu ambao hawakuukubali mpango huu iliamuliwa ya kwamba baada ya kufanya Tawafu, itawalazimu kuzivua nguo zao na kuzitupa na hakuna aliyeruhusiwa kuzigusa nguo hizo. Hata hivyo, kuhusu wanawake katika hali zote zile waliwajibika kufanya Tawafu wakiwa uchi. Waliweza kuzifunika pande za vichwa vyao tu kwa kipande cha nguo na walitakiwa wavumishe beti maalum.

Baada ya tukio lihusianalo na Abraha, aliyekuwa Mkristo, hakuna Myahudi wala Mkristo aliyeruhusiwa kuingia mji wa Makkahh, ila pale awapo mfanyakazi wa Makkahh aliyekodiwa. Katika hali hiyo, vilevile ilikuwa wajibu juu yake kutotamka japo neno moja juu ya itikadi na dini yake.

Mambo yalifanyika kwamba Waquraishi wakaziacha baadhi ya ibada za Hajj zilizokuwa zikitekelezwa nje ya Nyumba Takatifu. Kwa mfano hawakuwa tayari kuitekeleza ibada ya kusimama huko Arafah (sehemu iliyo nje ya ‘Haram’ ambako Mahujaji wanatakiwa kukaa hapo hadi kuchwa kwa jua siku ya mwezi tisa Dhul-Hajj (mfunguo tatu).30

Na walifanya hivyo ingawa jadi zao (kizazi cha Nabii Isma’il a.s.) walikufikiria huko kukaa Arafah kuwa ni sehemu ya ibada ya Hajj na ule ubora wao wa dhahiri walionao Waquraishi ulitokana na Al-Ka’ba na hizi ibada, kwa sababu ni kutokana na jambo hilo kuliko wawajibisha watu kuja kwenye sehemu hii iliyo kame, kila mwaka. Na kama si kwa ajili ya hii Nyumba Takatifu tu, hakuna hata mtu mmoja ambaye angalielekea kwenye ziara ya sehemu hii japo mara moja tu maishani mwake mwote.

Kwa mtazamo wa mkokotoo wa kijamii, uovu na ubaguzi huu ni vitu visivyo zuilika. Hivyo basi, ililazimu kwamba mazingira ya Makkahh yajitose kwenye uovu na unajisi ili kwamba ulimwengu uwe tayari kwa mapinduzi ya awali na harakati zenye kupenyeza kila mahali.

Ufukara wote huu, sherehe, ulevi na kutokujizuia vilikuwa vikiyafanya mazingira yale kuwa tayari zaidi na zaidi kwa kuja kwa mtengenezaji mkuu wa ulimwengu huu, na sio kwamba haikuwapo sababu, pale Waraqah bin Nawfal yule mtaalamu wa Uarabuni, aliyeingia kwenye dini ya Ukristo katika siku za mwishoni mwa uhai wake, na akajipatia elimu ya maandiko ya Injili alipozungumzia juu ya Allah na Mitume na aliikabili ghadhabu ya Firauni wa Makkahh kwa jina la Abu Sufyan aliyekuwa akisema: “Sisi watu wa Makkahh si wahitaji wa Allah wala Mitume, kwa kuwa tunaifaidi rehema na upendeleo wa masanamu yetu.”

Bwana Abdallah – Baba Yake Mtukufu Mtume (S.A.W.W)

Wakati ule Abdul-Muttalib alipoununua uhai wa mwanawe kwa kuwadhabihi ngamia mia moja kwa jina la Allah, Bwana Abdullah hakuwa zaidi ya umri wa miaka ishirini na nne. Tukio hili, zaidi ya kuwa sababu iliyomfanya (Abdullah) kuwa maarufu miongoni mwa Waquraishi, vilevile lilimpatia daraja kuu na heshima kwenye familia yake, hasa machoni mwa Abdul-Muttalib.

Sababu yake ilikuwa ni kwamba mtu hupenda hasa kila kitu kithibitishacho kuwa ni chenye gharama kuu kwake, na ambacho amepata taabu kubwa katika kukipata. Kwa sababu hii, Abdallah alipata heshima kubwa mno miongoni mwa marafiki na ndugu zake.

Haihitajiki kusema hapa kwamba pale Abdallah alipokuwa akienda na baba yake kwenye madhabahu ya kudhabihia, alikabiliwa na hisia kali zenye kuipinga azma yake hiyo. Hisia za heshima kwa baba yake na kuzithamini taabu alizozipata kwa ajili yake zikaidhibiti nafsi yake yote, na kwa sababu hiyo, hakuwa na njia yoyote nyingine ila kuitii amri yake. Hata hivyo, kwa upande mwingine kama vile yalivyotaka mamlaka ya takdir kwamba lile ua la majira ya machipuko la maisha yake linyauke kama vile lifanyavyo la majira ya kabla ya baridi, wimbi la ghasia na machafuko liliibuka akilini mwake.

Vilevile Abdul-Muttalib alijikuta akifanya jitihada baina ya nguvu mbili za ‘imani’na ‘upendo’ na bila shaka hali hii ilisababisha mlolongo wa wasiwasi mkali akilini mwao wote.

Hata hivyo, tatizo hili lilipotatuliwa kwa jinsi tuliyoieleza hapo juu, alifikiria kufanya marekebisho kwa ajili ya mihemuko hiyo michungu kwa kumuoza Abdullah kwa Amina haraka sana, na hivyo akayaunga maisha yake, yaliyokwisha kuifikia hatua yake ya kuchoka kabisa kwa uhusiano wa msingi kabisa wa maisha yake mtu.

Hivyo basi, alipokuwa akirudi kutoka kwenye madhabahu ya kudhabihia, Abdul-Muttalib, ambaye bado alikuwa ameushika mkono wa mwanawe, alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa Wahab mwana wa Abd Manaf wa kabila la Zuhrah na akaitimiza ndoa ya Bwana Abdullah na binti yake Wahab, Amina, aliyekuwa maarufu kwa utakatifu na adabu. Kwenye mkutano huo huo, yeye (Abdul-Muttalib) mwenyewe alimuoa Dalalah binamu yake Amina, aliyemzaa Hamza, ami na hirimu lake Mtukufu Mtume (s.a.w.w).31

Mwanahistoria wa zama hizi, Abdul Wahaab (Profesa wa historia wa Chuo Kikuu cha Misri, aliyeandika maelezo yenye faida juu ya historia ya Ibn Athir) ameyachukulia maendeleo tuliyoyataja hapo juu kuwa ni jambo lisilo la kawaida na anaandika hivi: “Kitendo ch Abdul-Muttalib kwenda kule nyumbani kwa Wahab siku ileile, (fikara za watu zilipofikia kikomo cha juu zaidi na machozi ya furaha yalikuwa yakitiririka chini ya mashavu yao) na vile vile kwa lengo la kutaka kuwachumbia wasichana wawili – mmoja kwa ajili yake mwenyewe na mwingine kwa ajili ya mwanawe, Abdullah – hakuafikiani na vipimo vya kawaida. Jambo pekee lenye kuwafaa na kuwa stahili ilikuwa ni kujipumzisha, ili kwamba waweze kujitoa uchovu wa kiakili, na kisha wayashughulikie mambo mengine.”32

Hata hivyo, tunaamini ya kwamba, kama mwanahistoria huyo tuliyemtaja hapo juu angelichunguza suala hili kwa njia tuliyolitazama sisi, ingalikuwa rahisi mno kwake kulithibitisha tendo lao hili. Abdul-Muttalib aliweka muda wa kukamilisha ndoa hii na kulingana na desturi za Waquraishi, muda uleule ulipofika sherehe za harusi zilifanyika nyumbani kwa Amina. Abdullah na Amina walikaa pamoja kwa muda fulani na kisha Abdullah alisafiri kwenda Sham kwa ajili ya kufanya biashara. Hata hivyo, alipokuwa akirejea alifariki dunia kama tutakavyoeleza kwa kirefu hapa chini.

Kufariki Dunia Kwa Abdullah Mjini Yathrib

Kwa kufunga ndoa, Abdullah aliufungua ukurasa mpya maishani mwake na nyumba yake iliangazwa kwa kuwa na mwenzi, ambaye ni Bibi Amina.

Baada ya muda fulani Bwana Abdullah aliondoka kwenda Sham kufanya biashara, akifuatana na msafara uliokuwa ukienda huko kutoka Makkahh. Kengele ya kuondokea iligongwa na ule msafara ukaishika njia yake, ukiyachukua mamia ya nyoyo pamoja nao. Wakati ule Aminah alikuwa mjamzito. Baada miezi michache msafara ule ulirudi Makkahh. Watu kad- haa walitoka nje ya mji kwenda kuwapokea ndugu zao.

Baba mzee wa Bwana Abdullah naye alikuwa pale akimsubiri mwanawe, na macho ya mkewe yenye kudadisi, yalikuwa yakimtafuata miongoni mwa msafara ule, lakini kwa bahati mbaya hakuonekana popote pale. Baada ya kuulizia waligundua ya kwamba Abdullah alipokuwa akirejea kutoka Sham alipatwa na maradhi mjini Yathrib na hivyo basi, alibakia huko akijipumzisha kwa nduguze. Aminah aliposikia hivyo, alihuzunika mno machozi yakamtiririka mashavuni mwake.
Abdul-Muttalib alimtuma mwanawe mkuu, Harith, aende Yathrib akamlete Abdullah. Harith alipofika Yathrib aliambiwa ya kwamba mwezi mmoja tu baada ya kuondoka kwa ule msafara, Abdullah alifariki dunia kutokana na maradhi yale yale ya awali. Harith aliporudi Makkahh, alimpasha habari Abdul-Muttalib pamoja na mjane wa Abdullah yale yaliyotokea. Mali aliyoiacha Bwana Abdullah ilikuwa ni ngamia watano, kundi la kondoo na mjakazi mmoja aliyeitwa Ummi Ayman ambaye baadae alimnyonyesha Mtukufu Mtume (s.a.w.w).

 • 1. Lakini wao walikuwa na wazo lao kuhusu masanamu? Je, waliyafikiria kuwa yanapasika kuabudiwa na kuwa wasila pekee, au walifikiria kwamba wao nao walikuwa na nguvu kama Allah? Jambo hili liko nje ya mazungumzo yetu hivi sasa ingwa maoni ya awali ni thabiti na yenye kuthibitishwa.
 • 2. Lakini wao walikuwa na wazo lao kuhusu masanamu? Je, waliyafikiria kuwa yanapasika kuabudiwa na kuwa wasila pekee, au walifikiria kwamba wao nao walikuwa na nguvu kama Allah? Jambo hili liko nje ya mazungumzo yetu hivi sasa ingwa maoni ya awali ni thabiti na yenye kuthibitishwa.
 • 3. Tafsir-i-Burhan, Juzuu 1, uk. 535.
 • 4. Awa’il al-Maqalat, uk. 12.
 • 5. Majma’ul Bayan, Juzuu 3, uk. 319 na al-Mizan, Juzuu 7, uk. 170.
 • 6. Ama kuhusu maelezo kamili ya sura hii na mambo yahusianayo na kuzaliwa kwa Nabii Ibrahim (a.s.) na kule kuyavunja kwake masanamu, rejea Tarikh-I- Kamil, Uk. 53-62 na Biharul Anwar, Juzuu 12, Uk. 41-55, kwa ajili ya kufupisha maneno hatukuzitaja asili zote za maelezo haya.
 • 7. Biharul Anwar, Juzuu 5, uk. 130, chapa ya ‘Company print.’
 • 8. Al-Uyun, uk. 136, Amali Saduq, uk. 274 na Biharul Anwar, uk, 35.
 • 9. Tafsir-i-Burhan, Juzuu 3, uk. 64.
 • 10. Sa’dus Su’ud, uk. 41-42 na Biharul Anwar, Juzuu 12, uk. 118.
 • 11. Tafsiri-I-Qummi, uk. 52; na Bihaarul Anwaar, Juzuu 12, uk. 100.
 • 12. Biharul Anwar, Juzuu 2, uk. 112 kama kilivyonakiliwa kutoka Qassas-i- Anbiya.
 • 13. Tarikh-i-Kaamil, Juzuu 2, uk. 1 na 21.
 • 14. Maisha yao yamezungumziwa na Ibn Athir mwenye Tarikh-i-Kaamil, Juzuu 2, uk. 15-21.
 • 15. Ni ukweli ukubalikao kwamba ofisi zilizohusiana na Al-Ka’ba hazikuwako ilipojengwa hiyo Al-Ka’ba, na zilianzishwa pole pole, kufuatana na mahitaji ya muda. Hadi ulipokuja Uislamu, ofisi hizi ziligawanywa katika sehemu nne: (1) Udhamini wa Al-Ka’ba na kuzishika funguo zake, (2) Kuwapatia maji mahujaji katika nyakati za Hajj, (3) Kuwapatia mahujaji chakula, (4) Uchifu wa watu wa Makkahh, ushika bendera na uamirijeshi wa jeshi.
 • 16. Tarikh-i-Tabari, Juzuu 2, uk. 13.
 • 17. Siirah-i-Halabi, Juzuu 2, uk. 5.
 • 18. Siirahi-i-Halabi, Juzuu 1, uk. 6-7.
 • 19. Tarikh-i-Kaamil, cha Ibn Athir, Juzuu 2, uk. 10.
 • 20. Tarikh-i-Kaamil, Juzuu 2, uk. 6; Tarikh-i-Tabari, Juzuu, uk. 8-9; na Siirah-i-Halabi, Juzuu 1, uk.8
 • 21. Siirah-i-Halabi, Juzuu 1, uk. 4.
 • 22. Moja ya sababu ziiongozeayo jamii kwenye msiba ni kuweko kwa dhambi na uasherati miongoni mwa watu wake na haiyumkini kwamba vitendo viabishavyo vilete njaa na misiba mingineyo mwenye mkondo wao. Dhana hii, achilia mbali kuafikiana kwake na misingi ya kifalsafa, vile vile imetajwa kwa msisitizo mwenye Qur’ani tukufu na mwenye Ahadithi za kiislamu.
 • 23. Hapa swali huibuka ni kwanini wale wengine hawakuja na wazo hili? Inawezekana kwamba wote walikwisha kuyapoteza matumaini ya kupata maji.
 • 24. Tarikh-i-Ya’qubi, Juzuu 1, uk. 206; na Siirah-i-Ibn Hisham Juzuu 1, uk. 45
 • 25. Tukio tulilolitaja hapo juu limesimuliwa na wanahistoria wengi na waandishi wa Siirah (maandiko ya habari za maisha ya mtu). Hadithi hii yastahili kuthamini- wa kwa sababu hii tu kwamba inauainisha ubora wa tabia na umadhubuti wa Abdul-Muttalib na unaeleza dhahiri jinsi alivyokuwa na shauku katika mambo ya dini yake na katika kuzitimiza ahadi zake.
 • 26. Siirah-i-Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 153; na Bihaar, Juzuu 16, uk. 74 – 79.
 • 27. Tarikh-i-Kaamil, Juzuu 1, uk. 253 na kuendelea.
 • 28. Siirah -i-Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 43-62; Fadhaa’il Shazaan, uk. 52-64; Bihaarul Anwaar, Juzuu 15, uk. 146-155; na Tarikh-i- Kaamil, Juzuu 1, uk. 260-263.
 • 29. Tarikh-i-Kaamil, Juzuu 1, uk. 263.
 • 30. Tarikh-i-Kaamil, cha Ibn Athir, Juzuu 1, uk. 266.
 • 31. Tarikh-i-Tabari, Juzuu 2, uk. 4, na Siirah-i-Halabi, Juzuu 1, uk. 54.
 • 32. Tarikh-i-Ibn Athir, Juzuu 2, uk. 4 – sehemu ya maelezo ya chini ya ukurasa