read

Sura Ya Saba: Kujiunga Tena Na Familia Yake

Allah kamwekea kila mtu kazi maalum. Kama mtu kaumbwa ili aitafute elimu na hekima, mwingine atakuwa kabarikiwa uwezo wa kugundua vitu na wa tatu atakuwa kabarikiwa uwezo wa kazi na juhudi. Kama watu fulani wamejaaliwa uwezo wa kuzifanya kazi za serikali na siasa, wengine wamepewa kazi ya kufundisha na kuwafunza wenzao na kadhalika.

Viongozi wenye huruma, wenye shauku ya kuwapo kwa utaratibu mzuri na jamala katika mazingira yao, na wenye kupenda maendeleo ya mtu mmoja mmoja pamoja na ya jamii nzima, huutahini ujuzi na akili za mtu kabla ya kumpa kazi, na humpa tu ile kazi ilandanayo na welekevu wake.
Kama halikufanyika hili, jamii hupatwa na hasara mbili. Kwanza kabisa yule mtu ahusikaye hafanyi kile awezacho na huthibitika kuwa bure. Inasemekana kwamba: “Kila kwenye kichwa mna welekevu. Yu mwenye bahati yule autambuaye welekevu wake.”

Mwalimu fulani alikuwa akimshauri mwanafunzi mvivu. Alikuwa akimweleza kuhusu uovu wa uvivu na hatima ya wale wasiojifunza, lakini wakayatumia maisha yao katika kuyatafuta mambo ya uvivu. Ghafla akaona kwamba yule mwanafunzi, alipokuwa akiyasikiliza yale maneno yake, alikuwa pia akichora picha mchangani kwa kipande cha mkaa na mawe.

Mara moja akatambua ya kwamba kijana yule hakuumbwa kwa ajili ya kusoma na kwamba mkono wa maumbile umemdhamiria kuwa mchoraji. Hivyo akawaita wazazi wa kijana yule na akawaambia; “Ingawa mtoto wenu yu mzembe na mzito katika masomo, anao welekevu mzuri katika uchoraji. Hivyo basi, itakuwa vema kama mtamtayarishia mafunzo ya uchoraji. Wazazi wa kijana yule waliukubali ushauri wa mwalimu yule. Hivyo yule mwanafunzi akaanza kujifunza sanaa ile na hatimaye akawa mchoraji mkuu wa zama zake.

Kipindi cha awali cha maisha ya mtoto huitoa nafasi nzuri zaidi kwa wazazi na walezi wao kuutahini mwelekeo wepesi na kupata ujuzi juu ya akili zao kutokana na matendo, tabia, fikara na uwezo. Jambo hili huwa hivyo kwa sababu fikra, matendo na maneno mazuri na ya upole ya mtoto na kioo cha hali ya baadae ya maisha yake na kama akipewa mwongozo bora kwa akili zake, ndivyo atakavyoweza kupata faida kubwa kutokana na wepesi wake wa kuyaelewa mambo.

Kujifunza jinsi na tabia za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) tangu utotoni mwake hadi pale ilipoanza kazi ya Utume huisawiri machoni mwetu picha ya msingi wa maisha yake na fikara zake tukufu, na uchunguzi wa historia ya utotoni mwake hutuonyesha uzuri wa maisha yake ya baadae. Zaidi ya hapo, historia fupi ya maisha yake, tangu awali hadi pale alipoteuliwa kuishika kazi ya Utume, alipojitangaza kuwa yu kiongozi wa jamii, hutupa taarifa za maisha yake ya baadae na hulidhihirisha lengo la kuumbwa kwake, na vile vile hutuarifu kama dai lake la utume na uongozi liliafikiana na matukio ya maisha yake au la.

Hutuarifu kama maisha yake ya miaka arobaini, na mwenendo, taratibu, kauli na mwongozo wa ushirikiano wake mrefu na watu waunga mkono Utume wake au la. Hivyo basi, tukilizingatia hili tunaweka mbele ya wasomaji wetu, sehemu ya maisha ya awali ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Mama wa kunyonya mwenye huruma, wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.), alimlea kwa muda wa miaka mitano na alifanya kila alichokiweza katika kumlea na kumhifadhi. Katika kipindi hiki Mtume alijifunza ufasaha wa lugha ya kiarabu, katika siku za baadae alijifaharisha mno katika lugha hii. Baadae bibi Halima alimleta Makkah na akakaa na mama yake mpenzi kwa kipindi fulani akiwa chini ya ulezi wa babu yake mwenye huruma. Mtoto huyu ndiye peke yake aliyekuwa ukumbusho wa Bwana Abdillah katika familia yake iliyofiwa.1

Safari Ya Kwenda Yathrib

Tangu siku ile yule mkemwana mpya wa Bwana Abdul-Muttalib (yaani bibi Amina) ampoteze mumewe aliye bado yu kijana na mtukufu, alikuwa akiisubiri nafasi ya kwenda Yathrib kujionea kwa macho yake pale mahali alipolalia mumewe mpenzi na vile vile kuwaona ndugu zake mjini mle.
Mwishowe aliamua kwamba muda ufaao kwa safari hiyo umewadia na mwanawe mpenzi kaishakuwa vya kutosha, kiasi cha kuweza kufuatana naye. Walijitayarisha kwa safari ile na wakaondoka kwenda Yathrib wakifuatana na Ummi Aiman.

Kwa mtoto mdogo wa kiquraishi safari hii ilikuwa ngumu na ilimsababishia maumivu ya kiroho, kwa sababu, kwa mara yake ya kwanza aliiona nyumba aliyofia baba yake mpenzi pamoja na sehemu aliyozikwa, na kwa kawaida, hadi wakati ule, mama yake tayari alikuwa kaishamueleza mambo mengi kumhusu baba yake.

Maumivu ya huzuni yalikuwa bado yamo moyoni mwake ulipotokea msiba mwingine wa kumpiga wimbi jipya la huzuni na masikitiko, kwa sababu, alipokuwa njiani akirejea Makkah, alimpoteza mama yake alipokuwa mahali paitwapo Ab’wa.2

Tukio hili la bahati mbaya lilimfanya kijana Muhammad kuwa mpendwa zaidi machoni mwa watu wa familia, kama waridi pekee lililosalia kwenye bustani hii ya mauaridi na akawa mpenzi zaidi wa Abdul-Muttalib. Alimpenda zaidi kuliko wanawe na akampa upendeleo zaidi kuliko mtu yeyote yule mwingine.

Kandoni mwa Kaabah liliwekwa zulia kwa ajili ya mtawala wa Waquraishi (yaani Abdul-Muttalib). Machifu wa Waquraishi pamoja na wanawe mwenyewe walikuwa wakikaa kwa mzunguko juu ya zulia lile. Hata hivyo, kila macho ya Abdul-Muttalib yalipoangukia kwenye huu ukumbusho wa Abdulah, aliamrisha wampishe ili kwamba apewe nafasi ya kumweka kijana Muhammad (s.a.w.w.) katika zulia lile3. Qur’ani Tukufu inakitaja kipindi cha uyatima wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika Surah al-Dhuha na inasema:

أَلَمْ يَجِدْكَ يَتِيمًا فَآوَىٰ {6}

“Je, Hakukukuta ni yatima na akakupa mahali pa usalama?” (Suratal-Dhuha, 93:6).

Falsafa ya msingi wa hali ya watoto yatima wa Waquraishi haieleweki vizuri kwetu. Tunajua tu kwamba ngurumo ya mafuriko ya matukio huashiria lengo jema.

Kwa kulizingatia jambo hili, tunaweza kukisia ya kwamba Allah alipenda kwamba kabla huyu kiongozi wa wanaadamu kuzishika hatamu za mambo na kuanza uongozi wake, hana budi kulionja pigo na misiba, na kuonja mageuzi ya hali za maisha ili aweze kujijengea uvumilivu mkubwa na moyo wa ushupavu na kwa taabu hizo aweze kujitayarisha kwa ajili ya kupambana na maisha yake ya baadae yenye silsila ya matatizo na kunyimwa, pamoja na kutokuwa na makazi.

Allah alipenda kuwa Mtume (s.a.w.w.) asiwe na elimu ya kufunzwa na mwanadamu na asiwajibike na kumnyenyekea mtu yeyote.

Tangu katika siku za awali za uhai wake awe huru na mwenye kujitosheleza na ajipatie uwezo wa kuendelea na utukufu kama mtu aliyejiumba ili watu waweze kutambua ya kwamba, kwa upande wake ufunuo si ufunuo wa kibinaadamu na kwamba wazazi wake hawakuwa na lolote walilolifanya katika kuzirekebisha tabia zake, fikara zake na uangavu wa maisha yake ya baadae na ukuu wake na ubora wake vimetokana na msingi wa utukufu wake.

Kufariki Dunia Kwa Bwana Abdul-Muttalib

Matukio ya kiulimwengu ya kuhuzunisha sana hujitokeza katika kipindi cha uhai wa mwanadamu, moja baada ya nyingine, kama mawimbi makubwa ya bahari na kuumiza nafsi ya mwanadamu.

Mawimbi ya huzuni kubwa yalikuwa bado yangali yakiukumba moyo wa Mtume wa Allah pale ilipombidi kupambana pia na msiba mwingine. Alikuwa bado hajaufikia umri wa miaka minane pale alipompoteza babu yake. Kifo cha Bwana Abdul-Muttalib kilikuwa na athari kubwa mno kwa Mtume (s.a.w.w.) kiasi kwamba aliendelea kulia hadi ukingoni mwa kaburi lake na katu hakupata kumsahau.

Ulezi Wa Bwana Abu Twalib

Tutazungumzia juu ya sifa na ukuu wa Bwana Abu Twalib katika sura maalum ya kitabu hiki na kuuthibitisha Uislamu wake na itikadi yake juu ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa thibitisho zikubaliwazo na wanachuoni wa kiislamu. Hata hivyo, kwa sasa itafaa tu kwamba tusimulie matukio yanayohusiana na malezi ya Mtume (s.a.w.w.) aliyoyapata kwa Bwana Abu Twalib.

Zilikuwepo sababu kadhaa zilizomfanya Bwana Abu Twalib alichukue jukumu na heshima ya kumlea Mtume (s.a.w.w.). Yeye na Bwana Abdullah, baba yake Mtume Muhammad (s.a.w.w.) walitokana na mama mmoja.4

Na vile vile Bwana Abu Twalib alifahamika mno kwa ukarimu na wema wake, kwa sababu hiyo Bwana Abdul-Muttalib alimteuwa kuushika ulezi wa mjukuu wake mpenzi. Huduma aliyoitoa kwa uwezo wake wote imehifadhiwa katika vitabu vya historia kwa maneno mazuri mno na hapo baadae itasimuliwa.

Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa na umri wa miaka kumi na mitano, alishiriki katika vita pamoja na ami yake. Kwa vile vita hivi vilipiganwa mnamo miezi ambayo vita vilipigwa marufuku, vita vile viliitwa ‘Vita vya Fujjaar.’ Maelezo marefu juu ya ‘Vita vya Fujjaar’ yametolewa katika vitabu vya Historia.

Safari Ya Kwenda Sham

Ilikuwa ni desturi ya Waquraishi waliojishughulisha na biashara kwenda Sham mara moja kwa mwaka. Bwana Abu Twalib alidhamiria kushiriki katika safari ya Waquraishi mwaka ule. Ama kuhusu yule mpwa wake (yaani Mtume s.a.w.w) ambaye kwa kawaida hakumwacha japo kwa kita- mbo kidogo tu, aliamua kumwacha mjini

Makkahh na kuwateuwa watu wengine kumwangalia. Hata hivyo, msafara ulipokuwa tayari kuondoka, Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alitiririkwa na machozi na kuuhisi mtengano ule na mlezi wake. Uso wa Muhammad (s.a.w.w.) uliojawa na huzuni ulizipandisha mno hisia za Bwana Abu Twalib kiasi kwamba alijua kuwa yu alazimika kuzikabili taabu kuwa naye Muhammad mwenyewe katika safari ile.

Safari hii aliyoichukua Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili inachukuliwa kuwa ni moja ya safari zenye kupendwa mno alizozichukua kwa sababu katika safari hii alipitia Madian Bonde la Qura nchi ya Wathamudi na kuyaona mandhari yenye kupendeza ya sura ya nchi ya Sham.

Msafara ule ulikuwa bado haujawasili Sham pale lilipotokea tukio fulani ulipokuwa njiani, mahali paitwapo Basra, ambalo lilivuruga mpango wa safari ya Bwana Abu Twalib kwa kiasi fulani. Maelezo ya tukio hili ni haya yafuatayo:

Kwa miaka mingi mtawa mmoja aliyekuwa akiitwa Bahira alikuwa akijishughulisha katika kufanya ibada zake katika nyumba yake maalum ya utawa iliyokuwa pale Basra. Mtawa huyu alikuwa na elimu nyingi juu ya Ukristo, na Wakristo wa sehemu ile walimtukuza mno. Wakati mwingine misafara ya kibiashara ilitua mahali pale na wasafiri fulani walimtembelea mtawa yule ili kuzipata baraka zake.

Kwa bahati Bahira alipata kukutana na ule msafara wa Waquraishi. Macho yake yalimwangalia yule mpwa wake Bwana Abu Twalib aliyemvutia mno. Mtazamo wake wa siri na wa makini ulidhihirisha siri iliyojificha moyoni mwake. Alimkodolea macho kwa kitambo fulani, na ghafla tu akakivunja kimya kile na kuuliza:

“Ni nani anayehusiana na kijana huyu miongoni mwenu?” Baadhi ya wale waliokuwepo pale walimtazama ami yake. Bwana Abu Twalib, akasema: “Huyo ni mpwa wangu.” Hapo Bahira akasema: “Kijana huyu ana maisha ya baadaye yaliyo matukufu. Huyu ndiye yule Mtume aliyeahidiwa, ambaye Utume, ushindi na utawala wake wa ulimwengu mzima vimetabiriwa katika vitabu vya Mbinguni na dalili nilizozisoma vitabuni zinamhusu yeye.

Ndiye yule Mtume ambaye jina lake na jina la baba yake na kuhusu familia yake nimevisoma katika vitabu vya kidini na ninaelewa atatokea wapi na vipi dini yake itakavyoenea hapa ulimwenguni. Hata hivyo, itakubidi kumficha kutoka machoni pa Wayahudi, kwa kuwa, kama wakiyajua mambo yahusianayo naye, watamuua”.5

Wengi wa wanahistoria wanasema kwamba yule mpwa wake Bwana Abu Twalib hakuendelea zaidi ya sehemu ile (Basra). Hata hivyo, haifahamiki wazi kama yule ami yake Muhammad alimrudisha Makkah pamoja na mtu mwingine (jambo hili laonekana kuwa lisilowezekana hata kidogo baada ya Bwana Abu Twalib kusikia kutoka kwa mtawa yule kwamba asijitenge hata kidogo na yule mpwa wake) au yeye mwenyewe alirejea naye mjini Makkah na kutoendelea na ile safari. Na wakati mwingine inasemekana kwamba alikwenda pamoja na Muhammad kule Sham huku akimlinda mno.

Uongo Wa Mustashirik

Katika sura moja ya kitabu hiki tutaelezea makosa na mara kwa mara uongo na masingizio ya uonevu wa mustashirik hawa ili kwamba msingi wa taarifa zao ueleweke na vile vile iwe dhahiri kwa kiasi fulani wanavyojaribu kwa makusudi kuzichanganya akili za watu wepesi wa kuamini kila kitu. Mkutano wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na yule mtawa ni jambo la kawaida kabisa.

Hata hivyo, hivi sasa ni miaka mingi ishapita tangu kutokee tukio hilo. Mustashirik wamelifanya kuwa hoja na wanasisitiza kuthibitisha kwamba Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.) katika safari yake hii alijifunza kutoka kwa Bahira yale mafundisho yake matukufu ambayo aliwafunza watu miaka ishirini na nne badaye, na ambayo yalichangamsha upya, kama kioevu cha maisha kwenye mwili uliokufa wa jamii ya mwanadamu wa zama zile.

Wanasema: “Kuhusu ukuu wa roho, utakatifu wa akili, akili yenye uwezo wa kushika mambo na fikara za ndani zaidi, ambayo maumbile yamemjaalia Muhammad kwa wingi, alijifunza kutoka kwa mtawa yule hadithi za Mitume na za jamii zilizopita kama vile za Waadi na Wathamudi na vile vile alijipatia mengi ya mafundisho yake muhimu kutoka kwake katika mkutano huo huo.”

Inaonesha wazi kwamba maoni tuliyoyatoa hapo juu si chochote ila ni ubunifu tu na kamwe haifikiani na matukio ya maisha ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Vile vile haiungwi mkono ila inakataliwa kisayansi na vipimo vya kikawaida.

Zifuatazo hapa chini ni thibitisho za yale tuliyoyasema hapo juu: Wanahistoria kwa pamoja wanakubaliana kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w.) hakujua kusoma na kuandika. Aidha, wakati wa ile safari yake umri wake haukuzidi miaka kumi na miwili.

Sasa je, inawezekana kuamini kwamba kijana wa umri usiozidi miaka kumi na miwili, aweze kujifunza habari za Torati na Injili na baadae, akiwa na umri wa miaka arobaini, azipe sura za ufunuo na kuasisi dini mpya? Jambo hili ni kinyume na vipimo vya kawaida na, tukiizingatia kadiri ya uwezo wa binadamu, tunaweza kusema kwamba haiwezekani kiakili.

Kipindi cha safari hii kilikuwa kifupi mno kuweza kumwezesha Mtume Muhammad kujifunza japo sehemu ndogo ya Torati na Injili, kwa sababu msafara ule ulikuwa ni msafara wa kibiashara na haukuchukuwa zaidi ya miezi minne, hii ikiwa ni pamoja na kipindi cha kutua pale Basra. Sababu yake ni kwamba, Waquraishi walisafiri mara mbili katika kipindi cha mwaka mmoja, kwenda Yemen katika majira ya baridi na kwenda Sham katika majira ya kiangazi, na kufuatana na jambo hili haiwezekani kudhania kwamba kipindi cha safari ile tuizungumziayo ulizidi miezi mine.

Na vile vile haiwezekani hata kwa yule mtaalamu mkuu zaidi wa ulimwengu huu kuvijua vitabu hivi viwili vilivyo vikuu katika kipindi kifupi namna hiyo, achilia mbali kijana mdogo asiyejua kusoma na kuandika, hasa tukizingatia ya kwamba hakuwa na mtawa yule kwa kile kipindi chote cha miezi minne na mkutano huu ulifanyika katika kituo wakati wa misafara na haukuendelea zaidi ya masaa machache.

Historia inatupa ushuhuda ya kwamba Bwana Abu Twalib alitaka kumchukua mpwa wake na kwenda naye Sham, hivyo pale Basra hapakuwa lengo la msafara wao. Aidha, Basra palikuwa mahali fulani katika njia na katika nyakati fulani fulani misafara ilitua pale ili kupumzika. Katika tukio lile inawezekanaje kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akae pale na kujishighulisha katika kujifunza Taurati na injili.

Ni mamoja kama tukisema kwamba Abu Twalib alimchukua na kwenda naye Sham au kwamba alikomea hapo (Busra) na kurejea Makkah au alimrudisha mpwa wake Makkah pamoja na mtu fulani, vyovyote vile iwavyo, mwishilizo wa msafara na vile vile ule wa Bwana Abu Twalib haukuwa pale Basra, ili kwamba tukaweza kufikiria msafara ule kwamba uliweza kujishughulisha katika biashara zao na wakati ule ule Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akajishughulisha na masomo.

Kama mpwa wake Bwana Abu Twalib alijipatia mafunzo kutoka kwa mtawa yule, bila shaka jambo hilo lingalipata kutangazwa miongoni mwa Waquraishi na wote wangalilizungumzia wakati wa kurejea kwao.

Zaidi ya hapo, hata Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe asingaliweza kudai mbele ya watu wake kuwa alikuwa asiyejua kusoma na kuandika na kwamba hakupata masomo yeyote, wakati tunapoona kwamba Mtukufu Mtume kwa dai hili hili, na hakuna yeyote aliyemwambia: “Ewe Muhammad! Umejifunza kutoka kwa mtawa wa Basra pale ulipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili na ukajifunza habari hizi zenye kuangaza kutoka kwake.”

Kama inavyojulikana waabudu masanamu wa Makkah walimlaumu Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa mambo mbalimbali na wakaisoma Qur’ani Tukufu kwa makini ili wapate sababu ya kumlaumia.

Walifanya hivyo mno kiasi kwamba, safari moja walipoona kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika nyakati fulani fulani alijishirikisha na mtumwa wa kikristo, kule Marmah, waliichukua fursa hiyo na kusema kwamba Muhammad alijifunza yale aliyokuwa akiyasema kutoka kwa yule mtumwa wa kikristo.

Qur’ani Tukufu inaitaja lawama yao hii kwa maneno haya:

وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّهُمْ يَقُولُونَ إِنَّمَا يُعَلِّمُهُ بَشَرٌ ۗ لِسَانُ الَّذِي يُلْحِدُونَ إِلَيْهِ أَعْجَمِيٌّ وَهَٰذَا لِسَانٌ عَرَبِيٌّ مُبِينٌ {103}

“Na bila shaka Tunajua ya kwamba (makafiri) wanasema: ‘Hakika yumo mtu anayemfundisha (Muhammad haya) lakini lugha ya yule wanayemdokeza (yule mtumwa
wa kikristo) ni ya kigeni na hii ni lugha ya kiarabu (fasaha na) cha dhahiri.”
(Sura al-Nahl, 16:103)

hata hivyo, kuhusu lawama hii, (yaani ya kwamba Mtukufu Mtume s.a.w.w alijifunza kwa Bahira) hakikupata kukataliwa na Qur’ani Tukufu wala Waquraishi wagomvi wenye kukanusha hawaifanyi kuwa hoja yao. Na jambo hili, lenyewe ni uthibitisho wa dhahiri wa ukweli uliopo ya kwamba lawama hii ni matokeo ya akili za mustashirik.

Hadithi za Mtume, zilizosimuliwa kwa kirefu katika Qur’ani Tukufu, zinatofautiana mno na zile zilizosimuliwa katika Tourati na Injili. Na mambo yanayohusishwa na Mitume hao yamesimuliwa katika hivi vitabu viwili kwa njia isiyo ya adabu na yenye kuchukiza mno kiasi kwamba hazipatani hata kidogo na vipimo vya kiakili.

Ulinganisho wa vitabu hivi viwili na Qur’ani Tukufu waonyesha kwamba maelezo ya Qur’ani Tukufu hayakuchukuliwa kutoka katika vitabu hivi. Na kama ikidhaminiwa kwamba Mtume Muhammad alizipata taarifa juu ya historia za mataifa kutokana na hizo Injili mbili, ingalilazimu kwamba maelezo yake nayo yachanganyike na maneno ya upotovu na (ngano za watu wa kale).

Kama yule mtawa aliyekuwa akiishi katika njia iendayo Sham alikuwa na elimu pana zaidi ya theolojia na dini kiasi cha kuweza kumwelimisha Mtume kama vile Muhammad (s.a.w.w.) kwa nini mtawa huyu hakujipatia utukufu? Na ni kwa nini hakuweza kumwelimisha yeyote mwingine ghairi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) wakati alipokuwa akitembelewa mara kwa mara na watu wengi?

Kuitupia Jicho Taurati Iliyopo Sasa

Kitabu hiki cha mbinguni! hakifungamani hata kidogo na mambo yahusuyo masimulizi juu ya Mitume. Hapa tutataja kwa kifupi tu baadhi ya matukio yahusianayo na jambo hili ili ieleweke dhahiri kwamba, kama Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) angalipata habari zake hizi za Qur’ani Tukufu ziangazazo, kutoka kwa mtawa yule, kusingalikuwako sababu ya kwa nini lisipatikane humo katika Qur’ani japo jambo lililo dogo mno lenye kuchukiza katika yale aliyoyasema. Kwa mfano: Taurati inasema katika kitabu cha Mwanzo (sura ya 32, aya ya 2-30): “Usiku mmoja Mungu alipigana mieleka na Yakobo hadi alfajiri,”

Mungu alimdanganya Adamu kwa kumwambia kuwa kama akila tunda la mti fulani atakufa, ambapo ukweli ulikuwa kwamba kama akilila tunda la mti ule atatambua mema na mabaya kama Mungu. Na alipolila, aliupata utambuzi ule.6

Taurati inasimulia kwa jinsi hii kushuka kwa malaika wawili kuja kumtembelea Nabii Ibrahim (a.s.). Mungu alishuka na malaika wawili ili kujua kama taarifa alizokuwa akizipata juu ya watu zilikuwa sahihi au zina uongo, kwa sababu hii, Mungu alimtokea Ibrahim, naye akasema: “Acha nilete maji mkanawe miguu.” Baada ya hapo Mungu na wale malaika wawili waliochoka wakapumzika na wakala chakula (Tazama Mwanzo, sura ya 18, aya ya 1-9).

Mpenzi msomaji! Tafadhali soma pia habari zilizosimuliwa katika Qur’ani Tukufu na kisha uamue kama inawezekana kusema: “Qur’ani Tukufu iliyosimulia kila jambo kwa jinsi iliyo tukufu mno inayatwaa masimulizi yenye kuwahusu Mitume kutoka kwenye Taurati hii?” Na kama imey- achukua kutoka kwenye Taurati kwa nini usiwepo upotovu ulioakisiwa katika masimulizi haya yaliyopigwa chuku ndani yake?

Kuitupia Jicho Injili

Tutayataja hapa matukio matatu ya ukweli wa dhahiri juu ya Injili, ili kuonyesha kama kweli hii Injili ndio asili ya Qur’ani ya Waislamu au la:

Nabii Isa (A.S) Aonyesha Muujiza

Nabii Isa (a.s.) alikwenda harusini pamoja na mama yake na wanafunzi wake. Ilitokea kwamba mvinyo ulimalizika pale harusini. Kwa muujiza aliyabadili mabalasi saba yaliyojaa maji na kuwa mvinyo (Mt. Yohana, Sura ya 2, aya ya 1-11).

Nabii Isa (a.s.) alichukua kikombe cha mvinyo ule, akawapa na akasema: “Kunyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu….” (Mathayo, 26:27).

Ndugu msomaji, hata hivyo mtaiona mantiki ya Qur’ani Tukufu juu ya kule kunywa mvinyo ambao kunapingwa kabisa na maoni tuliyoyaona hapo juu. Qur’ani tukufu inasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنْصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ {90}

“Enyi mlioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na mishale ya kupigia ramli ni uchafu utokanao na kazi ya shetani; basi uam- baeni ili mpate kufaulu.”
(Sura al-Maida, 5:90).

Katika mazingira haya je, tunaweza kusema kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alizipata taarifa za Qur’ani Tukufu kutoka kwa yule mtawa wa Basra?

Injili ya siku hizi inamueleza Nabii Isa (a.s.) kama mtu mkali asiyekuwa na huruma hata kidogo kwa mama yake (tazama Mathayo, sura ya 12; Marko sura ya 13; Luka, sura ya 83) ambapo Qur’ani Tukufu inamweleza kinyume kabisa na hivyo:

وَبَرًّا بِوَالِدَتِي وَلَمْ يَجْعَلْنِي جَبَّارًا شَقِيًّا {32}

“Na (yeye Allah Ameniusia) kumfanyia wema mama yangu, wala hakunifanya niwe jeuri (wala) muovu.” (Surat Mariam, 19:32).

Watu wasio na upendeleo, wanapoyalinganisha masimulizi na maamrisho ya Qur’ani Tukufu na Biblia wanaweza kuelewa ya kwamba Biblia haiwezi kuwa chanzo cha Qur’ani.

  • 1. Siirah-I Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 167.
  • 2. Siirah-i-Ibn Halabi, Juzuu 1, uk. 125
  • 3. Siirah-i-Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 168
  • 4. Siirah-i-Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 179.
  • 5. Tarikh-i-Tabari, Juzuu 1, uk. 33; Siirah-i-Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 180-183.
  • 6. Taurati imeeleza kwa kirefu hadithi ya Adamu na Hawa katika kitabu cha Mwanzo Sura ya 2 aya ya 3.