read

Sura Ya Sita: Utotoni Mwa Mtukufu Mtume (S.A.W.W)

Historia inatuambia kwamba maisha ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) yule kiongozi mtukufu wa waislamu yalijaa wingi wa matukio ya ajabu tangu utotoni mwake hadi kwenye kipindi cha kupewa kazi ya Utume, na matendo yote haya yalikuwa na hali ya ukuu. Kwa ujumla matukio haya yalithibitisha ya kwamba maisha ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) hayakuwa ya kawaida.

Ama kuhusu maelezo ya matukio haya, waandishi wamegawanyika makundi mawili, watu wa kimaada na idadi ya mustashirik.

Wanachuo wakimaada (materialist) ambao huuangalia ulimwengu kwa mtazamo wa kimaada na huufikiria utaratibu wa maisha kuwa umo ndani ya kuta nne za maada na wanaoitakidi kwamba mambo yote ni ya kimaada na hutegemea visababisho vya kimaada, nao hawayapi matukio haya muhimu wowote na hata matukio haya yaungwe mkono na ushahidi wenye nguvu zaidi, hawayasikilizi. Sababu ya msimamo wao huu ni kwamba, kwa mujibu wa kanuni za maada kutokea kwa matukio ya aina hii ni jambo lisilowezekana.

Hivyo basi, wanapoyaona matukio hayo yakiwa yamehifadhiwa kwenye historia, wanayahukumu kwamba ni kizazi cha dhana, huba na kuabudu kwa wafuasi wa dini maalum.

Vile vile liko kundi la mustashirik (orientalists), ambao kwa dhahiri hujionyesha kuwa wao ni wenye kumwamini Mungu na wachamungu na huidhihirisha itikadi yao juu ya nguvu kuu, lakini kutokana na unyonge wa itikadi yao, kiburi chao juu ya elimu yao na shinikizo la maada katika mawazo yao, wanapoyachambua matukio, huzifuata kanuni za maada. Katika mazunumzo yao mara kwa mara huikuta sentensi hii: “Utume ni hali ya kuwa mwanaadamu mwenye kipaji. Mtume ni mwenye kipaji cha kijamii aiangazaye njia ya maisha ya wanadamu kwa fikra zake nzuri n.k…”

Mazungumzo ya aina hii hutokana na fikra za kimaada zenye kuchukulia kwamba dini zote ni matokeo ya fikara za mwanaadamu, ingawa wanachuoni wa mafundisho ya dini, wanapozungumzia utume wa ujumla, wamethibitisha kwamba utume ni zawadi itokayo kwa Mungu ambayo ni chanzo cha mfumo wa kiroho na uhusiano, na haipatikani faida japo iliyo ndogo mno kwa upande huu (yaani wa mitume) ila pale tu uwapo uenezaji (wa taarifa ) kutoka upande wa Mwenyezi Mungu.

Hata hivyo, mustashirik wa Kikiristo kwa huyaangalia mambo haya kwa mtazamo wa kiulimwengu, na wanataka kuyapima matukio yote kulingana na misingi ya kisayansi, iliyogundulika kwa kuzipitia njia za majaribio, huyalaumu matukio yote yenye hali ya kiroho na huukana ukweli wake.

Wenye Kumuabudu Allah

Hawa ni wale watu walioamini kwamba sifa na muundo wa ulimwengu huu wa kidunia viko chini ya utawala wa ulimwengu mwingineo na nguvu nyingine (ulimwengu wa faragha na asili ya uhai), na kwamba ulimwengu huo ndio wenye madaraka ya utaratibu huu ulioko kwenye huu ulimwengu wa kimaada (kidunia) ambao si huru na si wenye kujitegemea, na kwamba hizi taratibu zake zilizomo humu na kanuni zake za kimaumbile na za kisayansi zinaendeshwa na ulimwengu mwingine ambao ni mapenzi ya Muumba yanayozunguka vitu vyote vilivyoko. Yeye (Muumba) ndiye aliyeumba maada (matter) na kuweka kanuni madhubuti miongoni mwa michanganyiko yake na akaisimamisha kwenye msingi wa nyororo ya misingi ya kimaumbile na kisayansi.

Pamoja na kuziamini kanuni za kisayansi, na kuyakubali maneno ya wanachuoni kwa moyo wote juu ya uhusiano wa kimaumbile wa kimaada kwa kiasi ambacho zimethibitishwa na sayansi. Vile vile watu wa kundi hili wanaamini ya kwamba hizi kanuni na misingi ya kisayansi na utarati- bu upendezao mno wa ulimwengu huu wa kimaada vimeungana na mpan- go mwingine, ambao sehemu zake zote huzunguka kutegemeana na mapenzi ya Asili kuu. Aidha, hawazichukulii hizi kanuni za kisayansi kuwa ni za kudumu na zisizoweza kubadilishwa na wanaamini kwamba nguvu iliyo hadhiri daima inaweza kuzibadili wakati wowote ule inapopenda, ili kuweza kulifikia lengo maalum. Inao uweza wa kufanya hivyo na (wala sio tu kwamba inao uwezo, bali) kwa hakika ishafanya hivyo kwenye nyakati nyingi kwa ajili ya kuyafikia malengo ya aina hiyo kwa kadri ilivyotaka.

Wanasema kwamba matendo ya kiroho na yenye kustaajabisha, ya Mitume, yasiyolandana na kanuni za kimaumbile yameundwa kwa kupitia njia hii. Watu hawa hawajiruhusu pasipo haki kukana au kutilia shaka yale wayaonayo kwenye Qur’ani Tukufu na kwenye Hadith na pia vitabu vya historia vikubaliwavyo na kutegemewa kwa sababu tu kwamba, haiafikiani na kipimo cha maumbile na kanuni za kisayansi. Sasa tunayataja matukio mawili yatokayo katika siri na maajabu ya maisha ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) yakihusuyo kipindi cha utotoni mwake na masimulizi haya yanapozingatiwa, haitakuwapo nafasi yoyote ya kutowezekana au shaka juu yao.

Wanahistoria wamemnukuu Bibi Halima akisema: “Nilipolitwaa jukumu la kumlea mtoto mchanga wa Aminah niliamua kumnyonyesha maziwa yangu kwenye mkutano uleule na mbele ya mama yake. Hivyo nika- muwekea kinywani mwake ziwa langu la kushoto lililokuwa na maziwa, lakini mtoto yuke alilielekea zaidi ziwa langu la kulia. Hata hivyo, sikupa- ta kuwa na maziwa kwenye ziwa langu la kulia tangu nimzae mwanangu wa kwanza. Kufanya kwake vile kulinifanya nimwekee ziwa la kulia lisilo na maziwa kinywani mwake, na mara tu alipoanza kunyonya, lilijaa maziwa na tukio hili liliwashangaza wale wote waliokuwapo pale.1

Vilevile Bibi huyu amesema: “Tangu siku ile nilipomchukua Muhammad na kwenda naye nyumbani kwangu, nilipata ustawi (wa kimaisha) zaidi na utajiri na mifugo yangu ilizidi.”2

Bila shaka kwenye mambo haya hukumu ya watu wenye itikadi ya kimaada na wafuasi wao hutofautiana na ile ya wale wamuabuduo Allah, ingawa hakuna hata mmoja wao aliye yachunguza matukio haya, na ushuhuda pekee walio nao ni kauli ya yaya wake Mtume (s.a.w.w.).
Kwa kuwa wale wafuatao kanuni za kimaada hawawezi kuyaeleza matukio haya kwa njia ya kimaumbile, mara moja husema tu kwamba matukio haya ni sanaa ya dhana. Kama wakiwa na heshima zaidi husema kwamba Mtume wa Uislam hakuwa na haja ya miujiza ya aina hiyo.

Hakuna shaka yoyote juu ya ukweli uliopo kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) hakuwa na haja ya miujiza hii, lakini kutokuhitaji kitu ni jambo lililo tofauti kabisa na hukumu ya ukweli au uongo wake.

Hata hivyo, mtu mcha Mungu, huvichukulia viumbe vya ulimwengu kuwa huzidiwa nguvu na kutiishwa na Mapenzi ya Muumba wa huu ulimwengu, na huamini ya kwamba ulimwengu wote, ikiwa ni pamoja na wale viumbe wadogo (yaani ile chembe ndogo sana atoms) na vitu vikubwa zaidi (yaani Milkyway, au kilimia)3 huzunguka kufuatana na mpango na utawala wake (Muumba).

Baada ya kujifunza matukio haya na dalili zao zinazoyaunga mkono, huyatazama matukio yote haya kwa heshima ipasikayo, na japo asitosheke, hayakatai moja kwa moja.

Katika Qur’ani Tukufu tunaliona tukio lililo mfano wa haya linalomhusu Bibi Maryam (mama wa Nabii Isa (a.s.) ambaye kuhusiana naye, Qur’ani Tukufu inasema:

“Na muda wa Mariamu kumzaa mtoto ulipokaribia, alilala kwenye shina la mtende na (kwa sababu ya uchungu wa kuzaa, upweke na hofu ya kulaumiwa) alimwomba Allah kifo.
Wakati huu alisikia sauti ikisema:

فَأَجَاءَهَا الْمَخَاضُ إِلَىٰ جِذْعِ النَّخْلَةِ قَالَتْ يَا لَيْتَنِي مِتُّ قَبْلَ هَٰذَا وَكُنْتُ نَسْيًا مَنْسِيًّا {23}

فَنَادَاهَا مِنْ تَحْتِهَا أَلَّا تَحْزَنِي قَدْ جَعَلَ رَبُّكِ تَحْتَكِ سَرِيًّا {24}

وَهُزِّي إِلَيْكِ بِجِذْعِ النَّخْلَةِ تُسَاقِطْ عَلَيْكِ رُطَبًا جَنِيًّا {25}

“Usihuzunike. Mola wako amekujaalia kijito kitiririkacho chini ya miguu yako na kama ukilitikisa hili shina la mtende (lililokauka), litakudondoshea nyongani mwako tende nzuri na mbivu. (Sura Maryam 19:23-25).

Ingawa kuna tofauti kubwa baina ya Maryam na Halima kuhusiana na vyeo na uchamungu wao, lakini vile vile ipo tofauti baina ya watoto hao wawili (Mtume s.a.w.w. na Nabii Isa a.s). Na kama sifa na fadhila za kibinafsi za Bibi Mariam zilimfanya azistahili baraka za Allah, basi vile vile inawezekana kwamba cheo na daraja ambalo mtoto huyu (yaani Muhammad) atalipata hapo baadae vitamfanya yaya wake astahiki baraka za Allah.

Vile vile tunajifunza jambo jingine zaidi kuhusiana na Bibi Mariam kutoka kwenye Qur’ani Tukufu: “Utakatifu na uchamungu wake (Mariam) vimemkweza mno daraja kiasi kwamba kila Zakaria alipoingia sehemu yake ya ibada alikikuta chakula kitokacho mbinguni, na kila alipomuuliza kinakotoka chakula kile, alikuwa akijibu kwamba kinatoka kwa Allah.” (Surah Aali Imran, 3:35).

Chini ya msingi huu hatuna haja ya kutia shaka kuhusu usahihi wa miujiza hii au kuifikiria kwamba ni mambo yasiyowezekana.

Miaka Mitano Ya Jangwani

Mtukufu Mtume (s.a.w.w) aliitumia miaka mitano akiwa miongoni mwa watu wa kabila la Banu Sa’ad na akawa mtu wa makamo yatoshelezayo. Mnamo kipindi hiki Bibi Halimah alimpeleka Mtume (s.a.w.w), kwa mama yake mara mbili au tatu hivi na mwishowe akamrudisha kabisa.

Mara ya kwanza Bibi Halima alimrudisha kwa mama yake kilipomalizika kipindi cha kunyonyeshwa. Hata hivyo, bibi Halima alisisitiza kwamba apewe tena mtoto yule. Sababu ya msisitizo wake ule ilikuwa kwamba mtoto huyu amekuwa chanzo cha baraka alizozipata, na sababu za mama mtoto (Bibi Amina) kulikubalia ombi la bibi Halima ilikuwa wakati ule maradhi ya kipindupindu yaliukumba mji wa Makkah.

Mara ya pili ilikuwa wakati kikundi cha makasisi wa Kihabeshi walipokuja Hijaz na kumwona Mtume Muhammad miongoni mwa watu wa kabila la Banu Sa’ad. Viongozi wale waliona kwamba ishara zote za Mtume atakayekuja baada ya Nabiii Isa (a.s.), kama zilivyotabiriwa kwenye vitabu vya mbinguni alikuwa nazo mtoto huyu. Hivyo basi, waliamua kumkama- ta kwa njia yoyote ile watakayoiweza, na kumpeleka Ethiopia, ili kwamba ile heshima ya kuwa naye Mtume yule iangukie nchini mwao.4

Jambo hili si lenye kutokuwezekana hata kidogo, kwa sababu kama ilivy- oelezwa kwa dhahiri katika Qur’ani Tukufu, ishara za Mtume wa Waislamu (s.a.w.w.) zimeelezwa katika Injili. Hivyo basi, ilikuwa sahihi kabisa kwamba wataalamu wa zama zile waliweza kumtambua mtu aliye na ishara zile. Kuhusiana na jambo hili, Qur’ani Tukufu inasema:

وَإِذْ قَالَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ إِنِّي رَسُولُ اللَّهِ إِلَيْكُمْ مُصَدِّقًا لِمَا بَيْنَ يَدَيَّ مِنَ التَّوْرَاةِ وَمُبَشِّرًا بِرَسُولٍ يَأْتِي مِنْ بَعْدِي اسْمُهُ أَحْمَدُ ۖ فَلَمَّا جَاءَهُمْ بِالْبَيِّنَاتِ قَالُوا هَٰذَا سِحْرٌ مُبِينٌ {6}

“Na aliposema Isa bin Mariam: ‘Enyi wana wa Israeli! Hakika mimi ni Rasuli wa Allah kwenu, nisadikishaye yaliyo mbele yangu katika Taurati na kumbashiria Mtume atakayekuja baada yangu jina lake ni Ahmad,’ lakini alipowafikia (yule Mtume aliyebashiriwa na Isa) na bayana, wakasema: ‘huu ni uchawi wa dhahiri’” (Sura al-Saff, 61:6)

Vile vile ziko aya zionyeshazo kwamba ishara za Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) zilielezwa katika vitabu vya mbinguni na watu wa kale walikuwa wanatambua kuhusiana na ishara hizo.5

  • 1. Biharul Anwar, Juzuu 15, uk. 345 kama kilivyonukuliwa kutoka ‘Fazaa’ili Waaqidi’
  • 2. Manaaqib-i-Ibn Shehr Ashub, Juzuu 1, uk. 24.
  • 3. Milkway au kwa Kiswahili; kilimia ni nyota ndogo nyingi sana zilizo jikusanya pamoja kama wingu jeupe angani wakati wa usiku.
  • 4. Siirah-i-Ibn Hashim, Juzuu 1, uk. 167.
  • 5. Tazama Sura al-‘Araaf, 7:157.