read

Sura Ya Tano: Kuzaliwa Kwa Mtukufu Mtume (S.A.W.W)

Wingu jeusi la ujinga lilifunika kabisa Rasi ya Uarabu. Matendo yachuk- izayo na haramu, kama vile kampeni ya umwagaji wa damu unyang’anyi ulioenea kote kote na uuaji wa watoto wachanga vimeyaharibu maadili mema yote, na kuiweka jamii ya kiarabu kwenye mwinamo. Umbali baina ya uhai na vifo vyao umekuwa mfupi mno. Katika wakati huu huu nyota ya alfajiri ya ustawi ikajitokeza na ile hali ya hewa ya giza iliangazwa kwa kheri ya kuzaliwa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Hivyo basi, hatua ya awali ya kuelekea kwenye msingi wa ustaarabu na maendeleo na ustawi wa taifa lililokuwa nyuma ulifikiwa. Mara miali ya nuru hii iliangaza ulimwengu mzima na msingi wa elimu, hekima na ustaarabu ukawekwa.

Kila ukurasa wa maisha ya watu wakubwa unafaa kujifunza na kuchun- guza. Wakati mwingine nafsi ya mtu huwa kubwa na kuu sana kiasi kwam- ba awamu zote za maisha yake, hata uchangani na utotoni mwake huwa siri. Maisha ya watu mastadi, viongozi wa jamii na watangulizi wa msafara wa ustaarabu, kwa kawaida ni yenye kuvutia na yana awamu zilizo nyeti na za kustaajabisha. Tangu kwenye susu hadi kaburini, maisha yao yamejaa siri. Tunasoma juu ya watu wakuu kwamba vipindi vya utotoni na ujanani mwao ni vyenye kuvutia na vya kimiujiza. Na kama tunaikubali alama hii kuhusiana na watu wakuu wa ulimwenguni hapa, kukikubali kitu kifananacho na hivyo kuhusiana na Mitume na mawalii huwa rahisi mno.

Taurat na Qur’ani vimeyaelezea maisha ya utotoni ya Nabii Musa (a.s.) kuwa ni siri kubwa, na kusema: “Mamia ya watoto wasio na hatia walikatwa vichwa kwa lengo la kwamba Nabii Musa (a.s.) asizaliwe. Hata hivyo, kwa kuwa Allah Alipenda kwamba Nabii Musa (a.s.) ajitokeze ulimwenguni, ilitokea kwamba sio tu kwamba maadui zake hawakuweza kumdhuru, lakini hata Firauni, adui yake mkuu, mwenyewe akawa mlezi na msaidizi wake; Qur’ani Tukufu inasema:

إِذْ أَوْحَيْنَا إِلَىٰ أُمِّكَ مَا يُوحَىٰ {38}

أَنِ اقْذِفِيهِ فِي التَّابُوتِ فَاقْذِفِيهِ فِي الْيَمِّ فَلْيُلْقِهِ الْيَمُّ بِالسَّاحِلِ يَأْخُذْهُ عَدُوٌّ لِي وَعَدُوٌّ لَهُ ۚ وَأَلْقَيْتُ عَلَيْكَ مَحَبَّةً مِنِّي وَلِتُصْنَعَ عَلَىٰ عَيْنِي {39}

إِذْ تَمْشِي أُخْتُكَ فَتَقُولُ هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَىٰ مَنْ يَكْفُلُهُ ۖ فَرَجَعْنَاكَ إِلَىٰ أُمِّكَ كَيْ تَقَرَّ عَيْنُهَا وَلَا تَحْزَنَ ۚ وَقَتَلْتَ نَفْسًا فَنَجَّيْنَاكَ مِنَ الْغَمِّ وَفَتَنَّاكَ فُتُونًا ۚ فَلَبِثْتَ سِنِينَ فِي أَهْلِ مَدْيَنَ ثُمَّ جِئْتَ عَلَىٰ قَدَرٍ يَا مُوسَىٰ {40}

Tulimfunulia mama yake Musa mapenzi yetu, ya kwamba: ‘Mtie sandukuni mtoto wako kisha litie mtoni na mto (utamchukua na) utamtupa ufukoni kwa usalama, ili amchukue (yule aliye) adui Yangu na adui yake. Na ninakupa huba itokayo kwangu na ili ulelewe machoni pangu.’ Dada yake Musa alikwenda nyumbani kwa Firauni na akasema: “Je, nikuletee (mtu) atakaye mlea?” Basi mama yake Musa aliajiriwa kumlea mtoto yule na hivyo mwanawe akarejeshwa kwake!” (Surah Twaahaa, 20:38-40)

Kipindi cha ujauzito, kuzaliwa na kulelewa kwa Nabii Isa (a.s.) kilikuwa chenye kustaajabisha zaidi ya kile cha Nabii Musa (a.s.).
Qur’ani Tukufu inakisimulia kipindi cha kukua kwa Nabii Isa, hivi:

فَاتَّخَذَتْ مِنْ دُونِهِمْ حِجَابًا فَأَرْسَلْنَا إِلَيْهَا رُوحَنَا فَتَمَثَّلَ لَهَا بَشَرًا سَوِيًّا {17}

قَالَتْ إِنِّي أَعُوذُ بِالرَّحْمَٰنِ مِنْكَ إِنْ كُنْتَ تَقِيًّا {18}

قَالَ إِنَّمَا أَنَا رَسُولُ رَبِّكِ لِأَهَبَ لَكِ غُلَامًا زَكِيًّا {19}

قَالَتْ أَنَّىٰ يَكُونُ لِي غُلَامٌ وَلَمْ يَمْسَسْنِي بَشَرٌ وَلَمْ أَكُ بَغِيًّا {20}

قَالَ كَذَٰلِكِ قَالَ رَبُّكِ هُوَ عَلَيَّ هَيِّنٌ ۖ وَلِنَجْعَلَهُ آيَةً لِلنَّاسِ وَرَحْمَةً مِنَّا ۚ وَكَانَ أَمْرًا مَقْضِيًّا {21}

فَحَمَلَتْهُ فَانْتَبَذَتْ بِهِ مَكَانًا قَصِيًّا {22}

فَأَجَاءَهَا الْمَخَاضُ إِلَىٰ جِذْعِ النَّخْلَةِ قَالَتْ يَا لَيْتَنِي مِتُّ قَبْلَ هَٰذَا وَكُنْتُ نَسْيًا مَنْسِيًّا {23}

فَنَادَاهَا مِنْ تَحْتِهَا أَلَّا تَحْزَنِي قَدْ جَعَلَ رَبُّكِ تَحْتَكِ سَرِيًّا {24}

وَهُزِّي إِلَيْكِ بِجِذْعِ النَّخْلَةِ تُسَاقِطْ عَلَيْكِ رُطَبًا جَنِيًّا {25}

فَكُلِي وَاشْرَبِي وَقَرِّي عَيْنًا ۖ فَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ الْبَشَرِ أَحَدًا فَقُولِي إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنْسِيًّا {26}

فَأَتَتْ بِهِ قَوْمَهَا تَحْمِلُهُ ۖ قَالُوا يَا مَرْيَمُ لَقَدْ جِئْتِ شَيْئًا فَرِيًّا {27}

يَا أُخْتَ هَارُونَ مَا كَانَ أَبُوكِ امْرَأَ سَوْءٍ وَمَا كَانَتْ أُمُّكِ بَغِيًّا {28}

فَأَشَارَتْ إِلَيْهِ ۖ قَالُوا كَيْفَ نُكَلِّمُ مَنْ كَانَ فِي الْمَهْدِ صَبِيًّا {29}

قَالَ إِنِّي عَبْدُ اللَّهِ آتَانِيَ الْكِتَابَ وَجَعَلَنِي نَبِيًّا {30}

“……., Kisha Tukampelekea (Mariamu) Roho wetu (yaani Malaika Mkuu Jibrili) aliyejimithilisha kwake (na) mwanaume kamili (katika maumbile). Na (Mariamu) akasema: “Hakika mimi ninajikinga kwa Allah Mwingi wa rehema kutokana nawe (basi niondokee) ikiwa unamuogopa Mwenyezi Mungu” (Yule Malaika) akasema: “Hakika mimi ni mjumbe wa Mola wako (niliyetumwa) ili nikupe (bishara ya) mwana mtakatifu.Mariamu akasema: “Ninawezaje kumpata mwana hali (Mimi ni Bikira) hajanigusa mwanaume yeyote (yule) wala mimi si mwasherati?” Yule malaika akasema: “Itakuwa hivyo, anasema Mola Wako: “Haya ni rahisi Kwangu, na ili kwamba Tumfanye Ishara kwa wanadamu na rehema itokayo Kwetu na hilo ni jambo lililokwisha hukumiwa.”

“Pale pale akatunga mimba na akajitenga na watu, akaenda kukaa kwenye sehemu ya mbali. Na alipopata uchungu wa kuzaa, alilala kwenye shina la mtende; akasema kwa sauti kuu: “Laiti ningalikufa kabla ya haya na nikawa kitu kilichosahauliwa kabisa.” Mara (sauti ya mtoto ) ikamwita kutoka chini yake ikisema: “Usihuzunike, hakika Mola Wako amejaalia (kutiririka) kijito chini yako, na kama ukitikisa hili shina la mtende, litakudondoshea tende zilizo nzuri (na) mbivu.

Hivyo basi, ufurahi, ule na unywe na uburudishe macho, na kama ukimwona mtu yeyote umwambie: “Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa (Allah) Mwingi wa rehema ya kufunga saumu hivyo katu leo sitazungumza na mtu yeyote.”

“Kisha akamleta (mtoto Isa) kwenye kaumu yake akimpakata; wakasema: “Ewe Maryam, hakika umeleta kioja! Ewe dada yake Harun! Baba yako hakuwa mtu mbaya, wala mama yako hakuwa mwasherati. Lakini (Maryam) akaashiria kwake (mtoto Isa); wakasema: “Tuzungumze na aliye (bado yu) mtoto wa kwenye mahdi (susu)? (Isa) akasema: “Hakika Mimi ni mja wa Allah; Amenipa kitabu (Injili) na Amenifanya Nabii.”
(Surah Maryam, 19:17-30)

Waumini wa Qur’ani Tukufu na Torati na wafuasi wa Nabii Isa (a.s.) watakapouthibitisha ukweli tulioutaja hapo juu unaohusu kuzaliwa kwa Mitume hao wawili, hawatakuwa na haja ya kuyastaajabia matukio yasiyo kifani yaliyofuatia kwenye heri za kuzaliwa kwa Mtukufu wa Uislamu (s.a.w.w.) na hawana hoja ya kuyachukulia kuwa ni jambo la kupurukusha.
Tumejifunza kutokana na vitabu vya historia na Hadithi kwamba wakati wa kuzaliwa kwake Mtume (s.a.w.w) kuta za Ikulu ya Makhosro zilikatika na baadhi ya minara ikaanguka. Moto wa hekalu la moto wa Uajemi ulizimika. Ziwa la Sawah lilikauka. Masanamu yaliyokuwamo mwenye Haramu ya Makkahh yaligeuka chini juu.

Nuru ilishuka kutoka mwilini mwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) ikielekea mbinguni na ikauangaza umbali wa ligi (au kilometa) nyingi kwenye njia yake. Anushirwan na Makasisi wa Kimajusi waliota ndoto itishayo mno.

Alipozaliwa Mtume (s.a.w.w) alikuwa tayari kaishatahiriwa na kitovu kilishakatwa. Alipofika hapa ulimwenguni alisema: “Allah Yu Mkubwa na sifa zote njema zamstahiki Yeye tu, Naye Yu mwenye kusifiwa mchana na usiku.”

Maelezo yote haya yameelezwa kwenye taarifa za kihistoria zikubaliwazo na watu wote na kwenye vitabu vya hadith.1 Na tukizirudia habari zihusianazo na Nabii Musa (a.s.) na Nabii Isa (a.s.)’ ambazo tumezitaja hapo juu, hakuna haki ya kusita katika kuyakubali matukio haya.

Mwaka, Mwezi Na Tarehe Ya Kuzaliwa Kwa Mtume Wa Uislamu (S.A.W.W)

Kwa kawaida waandishi wa Siirah/wasifu wa maisha ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) wanakubaliana kwamba Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) alizaliwa mnamo ‘mwaka wa ndovu’ mwaka wa 570 Masihiya. Kwa kuwa ni dhahiri kwamba alifariki dunia mnamo mwaka wa 632 Masihiya, alipokuwa na umri wa miaka 62-63, mwaka wa kuzaliwa kwake hauna budi kwamba ulikuwa ni 570 Masihiya.

Karibuni waandishi wa Hadithi na Historia wote wanakubaliana kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alizaliwa kwenye mwezi wa Rabi’ul Awwal (mfunguo sita) lakini wanatofautiana kuhusiana na tarehe ya kuzaliwa kwake. Inafahamika vema miongoni mwa waandishi wa Hadithi wa Kishi’ah kwamba alizaliwa baada ya kuchomoza kwa jua, mnamo siku ya Ijumaa, tarehe 17 ya Rabi’ul Awwal, ambapo wanachuoni wa Kisunni wanaitakidi kwamba kuzaliwa kwake kulitokea mnamo tarehe 12 ya mwezi ule, siku ya Jumatatu.2

Ni Taarifa Ipi Sahihi Kati Ya Hizi Mbili?

Ni jambo la kusikitisha mno kwamba Waislamu hawana taarifa zikuba- likazo juu ya tarehe ya kuzaliwa na kufa kwa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w), na kusema kweli, juu ya wengi wa viongozi wa kidini, na kuhusiana na shaka hii, nyingi za sherehe za kuzaliwa kwao na kumbukumbu za vifo vyao, hazifanyiki katika mtazamo wa kihistoria.

Ingawa wanachuoni wa kiislamu wameyaandika matukio mbalimbali ya kihitoria ya kiislamu, kwa utaratibu mwema, haifahamiki ni kwa nini tarehe za kuzaliwa na kufa za wengi wa viongozi wa Kidini hazikuandikwa baada ya uchunguzi makini.

Hata hivyo, tatizo hili hutatuka kwa kiasi fulani. Kuhusiana na jambo hili, hebu na tuchukue mfano mmoja.

Kama utataka kuandika maisha ya mwanachuoni wa mji fulani na tufikirie kwamba mwanachuoni huyu ameacha watoto na karaba zake wengine kadhaa, utataka kuulizia juu ya maelezo marefu ya maisha yake kutoka kwa wageni au kutoka kwa marafiki zake na watu wamjuao, ingawa wapo watoto wake na watu wengineo wa familia yake, ambao kwa kawaida wao wanazo taarifa kamili za kina na ujuzi sahihi juu ya maisha yake? Ni dhahiri kwamba dhamira yako haitakuruhusu kufanya hivyo.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w) aliondoka kutoka miongoni mwa watu na akaacha nyuma yake familia na watoto wake. Hawa jamaa zake Mtume (s.a.w.w) wanasema: “Kama Mjumbe wa Allah yu baba yetu mpendwa na sisi tumelelewa nyumbani mwake, na chini ya uongozi wake, tunasema kwamba kiongozi wa familia yetu alikuja ulimwenguni humu katika tare- he hii na aliondoka mnamo tarehe hiii.” Je, katika hali hii, inaruhusiwa kwetu kuyabana maneno ya watoto wake na kuzitegemea taarifa za watu wengine?

Sherehe Ya Kumpa Jina Mtukufu Mtume Wa Uislamu (S.A.W.W)

Siku ya saba iliwadia. Abdul-Muttalib alichinja kondoo ili kudhihirisha shukrani yake kwa Allah na watu walialikwa kwenye sherehe ile kuu, iliy- ohudhuriwa na wengi wa Waquraishi, alimpa mjukuu wake jina la ‘Muhammad.’ Alipoulizwa ni kwa nini alimpa mjukuu wake huyo jina hili kwani halikuwa maarufu miongoni mwa Waarabu, alijibu hivi:

“Nilipenda kwamba asifiwe huko mbinguni na hapa duniani.” Mwanachuoni Hassan Thabit, akilizungumzia jambo hili anasema hivi: “Muumba Alilitoa jina la Mtukufu Mtume wake kutokana na jina Lake Mwenyewe. Kwa sababu hiyo, kwa vile Allah ni ‘Mahamud’ (mwenye kustahiki sifa) Mtume Wake naye yu ‘Muhammad’ (mwenye kusifiwa). Maneno yote mawili yame- tokaka na asili moja na yana maana moja.”3

Ni dhahiri kwamba maongezi ya siri yalihusika katika uchaguzi wa jina hili, kwa sababu ingawa jina la ‘Muhammad’ lilifahamika vizuri miongoni mwa Waarabu kabla ya hapo, ni watu wachache mno waliopewa jina hili. Kufuatana na hesabu sahihi, walizozikusanya baadhi ya wanahistoria, ni watu kumi na sita tu waliopewa jina hili kabla ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).4

Si lazima kueleza hapa kwamba jinsi neno litumikavyo kwa uchache ndivyo nafasi ya kutoelewana juu yake itakavyokuwa ndogo. Kwa kuwa Vitabu vya Mbinguni vimetabiri kuja kwa Uislamu na jina, mambo, dalili za kiroho na kimwili za Mtume (s.a.w.w), ililazimu kwamba dalili zake ziwe za dhahiri mno kiasi kwamba suala la kukosea kokote kule lisijitokeze.

Moja ya dalili hizi ilikuwa ni lile jina la Mtume (s.a.w.w.) na ililazimu kwamba jina hili liwe na watu wachache tu kiasi kwamba isiwepo shaka yoyote juu ya kumtambua, hasa pale sifa na dalili zake zitakapoam- batana na jina hilo. Kwa njia hii, yule mtu ambaye kuja kwake kumetabiri- wa na Torati na Injili atambulike kwa urahisi.

Qur’ani imeyataja majina mawili ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w).5 Katika Suratul-Muhammad aya ya 2, Suratul-Fat-ha aya ya 29, na Surah al-Ahzab aya ya 40, ameitwa ‘Muhammad’ na kwenye Surah al-Saff aya ya 6 ameitwa ‘Ahmad’ sababu ya tofauti hii ni kwamba, kama ilivyoelezwa kwenye historia, mama yake Mtume (s.a.w.w) alimwita ‘Ahmad’ kabla ya babu yake kumpa jina la ‘Muhammad’6.

Mtukufu Mtume (S.A.W.W) Wakati Akiwa Mtoto Mchanga

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alinyonyeshwa na mama yake kwa siku tatu tu! Baada ya hapo wanawake wawili walipata heshima ya kuwa mama zake Mtume (s.a.w.w) wa kumnyonyesha.

Suwaybah: Bibi huyu alikuwa mjakazi wa Abu Lahab. Bibi huyu alimnyonyesha Mtume kwa kipindi cha miezi minne na akabakia kuwa kilengwa cha kuthaminiwa na Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe, na vile vile mkewe mwema (bibi Khadija a.s) kwa kipindi chote cha uhai wake.

Hapo kabla, bibi huyu alimnyonyesha Bwama Hamza, ami yake Mtume (s.a.w.w.) pia. Baada ya Mtume (s.a.w.w.) kuianza kazi yake ya utume alidhamiria kumnunua bibi huyu na akamtumia mtu Abu Lahabi, lakini alikataa kumwuza. Hata hivyo, bibi huyu alipata msaada kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) na ali- porejea kutoka kwenye vita ya Khaybar, alipata taarifa za kifo cha bibi huyu na dalili za huzuni zilijidhihirisha usoni mwake. Aliulizia kuhusu mwanawe ili kwamba amfanyie lolote lililo jema kwake, lakini aliambiwa kwamba alifariki dunia mapema kabla ya mama yake.

Halimah: Bibi huyu alikuwa binti wa Abi Zuwayb na alitokana na kabila la Sa’ad bin Bakr bin Hawaazan. Bibi huyu alikuwa na watoto watatu, ambao ni Abdillah, Anisah na Shima. Huyu wa mwisho pia alimhudumia Mtume (s.a.w.w). Ilikuwa ni desturi ya familia tukufu miongoni mwa Waarabu kwamba waliwapeleka watoto wao kwa wanyonyeshaji. Kwa kawaida wanyonyeshaji hawa waliishi kwenye sehemu za nje ya mji ili kwamba watoto hao waweze kulelewa kwenye hewa safi ya jangwani na ili waweze kukaa wakiwa na nguvu na wenye afya.

Kwa bahati, wakati wakiishi huko jangwani, waliweza kuwa na kinga ya magonjwa ya kuambukiza ya mjini Makkah yaliyokuwa hatari kwa watoto wachanga, na vilevile walijifunza lugha ya kiarabu kwenye sehemu isiyoathiriwa na mageuzi mabaya. Wanyonyeshaji waliotokana na kabila la Bani Sa’ad walikuwa maarufu sehemu hii. Walikuja mjini Makkah nyakati maalum za mwaka na kila mmoja wao alichukua mtoto mchanga. Ilipopita miezi minne tangu kuzaliwa kwa Mtume (s.a.w.w) wanyonyeshaji wa kabila la Bani Sa’ad walikuja mjini Makkah. Katika mwaka ule walikuwa na njaa kali na hivyo basi, walihitaji sana msaada kutoka kwa wenye familia tukufu.

Huyu mtoto mchanga wa Kiquraishi (Mtume (s.a.w.w.) hakunyonya ziwa la myonyeshaji yeyote. Mwishowe alikuja Bibi Halima na yule mtoto akakubali. Wakati huu familia ya Abdul-Muttalib ilifurahi sana.7 Abdul- Muttalib alimgeukia Bibi Halima na kumwuliza: “Wewe u wa kabila gani?” Akamjibu ya kwamba alikuwa wa kabila la Bani Sa’ad.

Kisha Abdul-Muttalib alimuliza jina lake na akamuambia kuwa anaitwa Halima. Abdul-Muttalib alifurahi sana alipolisikia jina lake na lile la kabila lake na akamjibu: “Vizuri sana! Tabia njema mbili na sifa njema mbili. Mojawapo ni furaha na ustawi na nyingine ni upole na subra.8

  • 1. Tarikh-i Ya’qubi, Juzuu 2, uk. 5; Bihaarul Anmaar, Juz. 15, sura 3, uk. 231-248; na Siirah-I Halabi, Juz. 1,uk. 64.
  • 2. Mwanachuoni, Bwana Miqrizi amezikusanya taarifa zote zihusuzo siku, mwezi na mwaka wa kuzaliwa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w) kwenye kitabu chake kiitwacho al-Amta’ (Ukurasa wa 3).
  • 3. Siirah-i Halabi, Juzuu 1, uk. 93.
  • 4. Mudrak Pesh, Juzuu 1, uk. 97.
  • 5. Ama kuhusu maneno ‘Twaha’ na ‘Yasin’ baadhi ya wanachuoni wanaamini yakwamba ni ‘Muqatta’ (ufupisho) wa herufi za Qur’ani tukufu wala si majina ya Mtukufu Mtume (s.a.w).
  • 6. Siirah-i-Halabi, Juzuu ya 1, uk. 93.
  • 7. Bihaarul Anwaar, Juzuu 15, uk. 442.
  • 8. Siirah-i-Halabi, Juzuu 1, uk, 106.