read

Sura Ya Tatu: Hali Ya Dola Za Kirumi Na Ki-Iran

Ni muhimu mno kujifunza mazingira mawili yafuatayo ili kuweza kutath- mini harakati takatifu za kiislamu: Mazingira ya kuteremshwa kwa Qur’ani Tukufu – yaani ile sehemu ambayo kwayo Uislamu ulianzia na kupiga hatua ya maendeleo.

Jinsi ya fikara za watu walioishi kwenye sehemu zilizostaarabika kwenye zama zile, na ambao fikara zao na tabia zao ziliaminiwa kuwa ndizo zilizoendelea na zilizokuwa bora zaidi. Historia yatueleza kwamba sehemu zilizoelimika zaidi kwenye zama zile, zilikuwa falme za Urumi na Iran.

Ili kuukamilisha mjadala huu ni muhimu kwamba hatuna budi kujifunza hali ya hizi falme mbili, kila moja peke yake, ili kwamba iwezekane kukadiria thamani ya ustaarabu ulioletwa na Uislamu.

Katika siku hizo Urumi haikuwa na hali njema ikilinganishwa na mpinzani wake, yaani Iran. Upinzani wa ndani na vita vilivyokuwa vikiendelea kutoka nje, vilivyopiganwa na Iran juu ya Armenia, n.k. vimewaweka watu wake kwenye hali ya kuyakubali mapinduzi. Zaidi ya jambo jingine lolote lile, kutofautiana katika maoni ya kidini kumezifanya tofatuti hizi kuwa pana zaidi.Ugomvi baina ya Wakristo na wenye kuabudu masanamu haukukoma. Wakuu wa kanisa walipozitwaa hatamu za serikali, mikononi mwao, waliwakandamiza mno wapinzani wao, na jambo hili lenyewe, lilitengeneza njia ya ujenzi wa kikundi cha raia wachache wasioridhika; jambo ambalo laweza kuhesabiwa kuwa kipengele kikubwa cha kusilimu kwa taifa la Kirumi na ukaribisho wa furaha waliotoa kwenye harakati hii lilikuwa ni kunyimwa haki walikokuhisi watu wa makundi mbalimbali kwa sababu ya ukali na utesaji wa wakuu wa Kanisa.

Siku baada ya siku, hofu na nguvu ya dola ya Kirumi ilikuwa ikipungua kutokana na tofauti zilizokuwapo miongoni mwa makasisi katika upande mmoja na kuwako kwa madhehebu nyingi za kidini, kwa upande mwingine.

Zaidi ya hapo, mataifa meupe ya kaskazini na ya njano ya mashariki yalitamani sana kulitwaa eneo lenye rutuba la Ulaya, na kwenye wakati fulani walileteana madhara makubwa wao kwa wao kwa vita baina yao.

Jambo hili, lenyewe likawa sababu ya kugawanyika kwa Dola ya Kirumi na kuwa na pande mbili ambazo ni upande wa Mashariki (wa Kigiriki) na upande wa Magharibi wa (Urumi –Kilatini au Utaliani wa kale). Wanahistoria wanaamini ya kwamba hali za kisiasa, kijamii na kiuchumi za Urumi kwenye karne ya sita Masihiya zilivurugwa mno. Kiasi kwamba hawakuweza kuifikiria hata ile nguvu ya Urumi juu ya Iran kuwa ni ushuhuda wa uwezo wake wa kijeshi. Na hivyo walikuhusisha kushindwa kwa Iran na utawala mbaya wa serikali ya Iran. Hizi Dola mbili zilizokuwa viongozi na watawala wa ulimwengu, zilikuwa kwenye hali ya ghasia na utovu wa serikali wakati wa kuanza kwa Uislamu. Dalili zake zilizaa nyoyoni mwa watu shauku na tamaa kubwa ya sheria maalum zitaka- zoweza kuwathibitishia ustawi wao.

Majadiliano Ya Msimu Nchini Urumi

Kwenye baadhi ya nchi watu wazembe na wenye tamaa za kimwili wali- toa mijadala kadhaa juu ya matatizo yasiyo na maana na yaliyo duni kwa lengo la kuwarudisha nyuma watu kutokana na aina zote za maendeleo ya kisayansi na kiviwanda na hivyo kuyafanya maisha ya watu wa hali ya juu kuwa yasiyo na maana yoyote.

Kuhusiana na jambo hili tunayo idadi kubwa ya mifano na matukioa ya kale yafananayo na haya ya sasa kwenye nchi nyingi za kiislamu ambayo hayawezekani kuyataja hivi sasa. Ilitukia kwamba Urumi ya siku hizo ilikuwa zaidi ya mambo yote, ikitatanishwa na matatizo ya aina hii. Kwa mfano, mfalme na watu wa baraza lake, chini ya ushawishi wa baaadhi ya taasisi za kidini, waliamini ya kwamba Nabii ‘Isa (a.s.) alikuwa na asili mbili na utashi namna mbili, ambapo baadhi ya Wakristo wa Kiya’qubi walikuwa wakiitakidi ya kwamba alikuwa na hali moja tu na utashi mmoja tu.

Jambo hili lisilo na msingi liliushambulia uhuru na amani ya Urumi, na likajenga mfarakano mkubwa miongoni mwa watu hao, kwa kuwa serikali ililazimika kuzihami itikadi zake, na hivyo basi, ikawatia wapinzani wake kwenye mateso makali. Kwa matokeo ya shinikizo na chuki kubwa, baadhi yao walikimbilia Iran.

Hawa ndio wale watu ambao, katika kulikabili jeshi la Waislamu, waliyakimbia mahandaki yao na kuwapokea Waislamu kwa mikono miwili. Urumi ya siku hizo ilikuwa kama Ulaya ya Zama za Kati. Mnajimu maarufu wa Kifaransa aliyeitwa Camile Flammarion anaisimulia hadithi ifuatayo kuhusu kiwango cha elimu huko Ulaya katika Zama za Kati:

“Kitabu kiitwacho Majmu’a-i Lahutiah (Kitabu cha Elimu ya tabia na sifa za Mungu – mkusanyo wa kitheolojia) kilikuwa ni mdhihiriko kamili wa falsafa ya kiuwanachuoni katika Zama za Kati na kilifundishwa barani Ulaya kwa muda wa miaka mia nne kikiwa ndicho kitabu cha mafundisho. Sehemu ya kitabu hiki inajadili kama inawezekana kwa malaika wachache hivi kuishi kwenye ncha ya sindano au ni umbali wa ‘league’ (maili) ngapi kutoka mtoto wa jicho la kulia hadi yule wa jicho la kushoto la Baba wa Mbinguni?”

Imekuwa na bahati mbaya kiasi gani Urumi! Katika wakati ule ule ilipokuwa imetatizwa na vita kutoka nje yake, mfuriko wa tofauti za ndani, ambazo nyingi kati yao zilijidhihirisha kwenye vazi la dini, zilikuwa zikiikokota, siku hadi siku, karibu zaidi na genge. Wakati Wayahudi, ambao walikuwa watu waovu na wenye makri walipoona kuwa shinikizo la Mfalme wa Kikristo wa Urumi limeivuka mipaka waliyoiweka, wakapanga kuiangusha serikali ya Kirumi na hata kuukalia mji wa Antakia katika wakati fulani na kuyakata masikio, pua na midomo ya Askofu Mkuu.

Baada ya muda fulani Serikali ya Urumi ililipiza kisasi kwa kuwachinja Wayahudi wa Antakia.Mauaji ya kikatili ya aina hii yalirudiwa mjini Roma kwa mara kadhaa baina ya Wayahudi na Wakristo na kwenye nyakati fulani, hizi hisia za kulipiza kisasi zilikuwa na matokeo hasi yake hata nje ya mipaka ya Dola hiyo. Kwa mfano, safari moja Wayahudi wal- inunua Wakristo elfu themanini kutoka kwa Wairani na wakawachinja kama kondoo kwa lengo la kulipiza kisasi kwenye jamii ya Kikristo.

Hapa ndipo mahali ambapo msomaji mwenye ujuzi anaweza kuuona msingi wa giza na ghasia wa ulimwengu unaoendana na zama za kuja kwa Uislamu na kukubali kwamba haya mafundisho yaliyo bora zaidi yaliyothibitisha wokovu wa mwanaadamu kutokana na hali ya hewa ile ya giza, hayatokani na akili za mwanaadamu, na huu upepo wa kusisimua na wenye kuburudisha wa umoja na makubaliano ya pamoja, na huu ujumbe wa amani na uaminifu, ambao ndio lengo la dini ya kiislamu, hauna chanzo kingine badala ya kile cha ghaibu.

Yawezekanaje kusemwa kwamba Uislamu, uliotoa haki ya kuishi hata kwa wanyama, ni mtoto wa mazingira kama haya ya umwagaji wa damu?! Uislamu uliweka kando mijadala yote hii isiyo na msingi na ya kipuuzi kuhusu utashi na Nabii ‘Isa (a.s.) na ukamtambulisha kwa maneno yafuatayo:

مَا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ ۖ كَانَا يَأْكُلَانِ الطَّعَامَ ۗ {75}

“Masihi mwana wa Mariamu (si chochote kingine) ila ni mtume (tu); bila shaka mitume (wengi) wamekwishapita kabla yake; na mama yake ni mwanamke mkweli; wote wawili walikuwa wakila chakula (kama watu wengine)…” (Al-Ma’idah, 5:75).

Kwa Aya hii, Uislamu uliikomesha idadi kubwa ya mijadala ya kipuuzi ya wakuu wa Kanisa juu ya roho, damu, na upekee wa Nabii Isa (a.s.). Wakati huo huo, ulimshawishi mwanaadamu kuachana na ugomvi na umwagaji wa damu kwa kumfunza mafundisho yaliyo bora zaidi na kuzihuisha sifa zake bora za kibinadamu.

Iran Au Chanzo Cha Ustaarabu Wa Zama Zile

Wanachuoni wa elimu ya jamii wanaona kwamba ubovu wa serikali ya Iran katika zama zile ulitokana na hali yake ya kidhalimu na utawala wa mtu mmoja juu ya watu wengi.

Waarabu wajinga, pamoja na ushenzi wao, walikuwa na aina fulani ya serikali ya kidemokrasia. Kwa kuwa kwao na ‘Darul Nadwah’ iliyokuwa na cheo cha Baraza la Mashauriano la Kitaifa, kwa kadiri fulani walikuwa wameiondoa hitilafu ya utawala wa Kiimla. Ingawa serikali, iwe ya kikatiba au ya kiimla, haiwezi kutatua matatizo bila ya utawala wa kidini, na imani na ulinzi wa askari kanzu, na vile vile haiwezi kuidumisha sheria na utaratibu mwema, kitu ambacho ndio hasa lengo la serikali yoyote ile, lakini ni ukweli ukubalikao kwamba hekima na busara za mtu mmoja haziwezi kuwa sawa na utambuzi wa kundi la watu.

Makri na ugomvi ni kidogo mno katika serikali ya kidemokrasia. Ni kwa sababu hii kwamba utukufu na uwezo au unyonge na fedheha ya Wairani umehusika mno na udhaifu au nguvu ya serikali yao ya mtu mmoja. Uchunguzi wa kipindi cha serikali ya Wasasani uliotokea katika kipindi kile unaudhihirisha usemi huu kwa ukamilifu kabisa.

Hali Ya Ujumla Ya Iran Pamoja Na Mapambazuko Ya Uislamu

Kuja kwa Uislamu na uteuzi kwenye ujumbe wa kiutume wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) katika mwaka wa 611 Masihiya ulikwenda pamoja na utawala wa Khusro Pervez (mwaka 590 hadi 628 Masihiya). Kuhajiri kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kutoka Makkahh kwenda Madinah pia kulitokea kwenye kipindi cha utawala wake (mnamo siku ya Ijumaa. Tarehe 16 Julai, 622 Masihiya) na tukio hili likawa mwanzo wa historia ya Waislamu.

Katika siku hizo, dola mbili zilizokuwa kubwa na zenye nguvu (Ugiriki na Usasani) Iran ilitawala sehemu kubwa ya ulimwengu uliostaarabika wa zama zile. Walikuwa wakigombana na kupigana wao kwa wao kwa kipindi kirefu kila moja ikitaka kumiliki na kuutawala ulimwengu.1

Vita virefu walivyopigana Wairani dhidi ya Warumi vilianza katika zama za utawala wa Anushirwan (aliyetawala tangu 531 hadi 589 Masihiya) na ikaendelea kwa kipindi cha miaka ishirini na minne yaani hadi kwenye zama za utawala wa Khusro Pervez.

Hasara kubwa na matumizi makubwa mno ambayo yalibebwa na dola hizi mbili, Iran na Urumi kutokana na vita hivi yalizipiga nchi hizi mbili zilizokuwa kubwa pigo kali mno na hakuna chochote kilichoachwa kwenye nchi hizi ila umbo tu, bila ya kiini hasa.

Ili tuweze kuielewa hali ya Iran vizuri mno, kutoka kwenye kila pembe, itatulazimu kujifunza kwa mukhatasari hali ya serikali mbalimbali tangu mwishoni mwa utawala wa Anushirwan kwenda mbele hadi kwenye wakati Waislamu walipojitokeza.

Huba Ya Anasa Katika Kipindi Cha Wasasani

Kwa kawaida Wafalme wa Kisasania walipenda mno anasa na raha. Fahari na mapambo ya baraza la Kisasania viliyastaajabisha macho.

Katika kipindi cha utawala wa Wasasani, Wairani walikuwa na bendera iliyoitwa ‘Dirafshi Kaavyaani’. Wasasani waliitweka bendera hiyo kwenye uwanja wa vita au waliiweka juu ya paa la Ikulu wakati wa sherehe. Bendera hiyo ilinakshiwa kwa kila aina ya vito. Kwa mujibu wa mwandishi mmoja, bendera hii isiyo na kifani ilinakshiwa kwa njumu za vito na vitu vingine vyenye thamani, ambavyo gharama yake ilikasimiwa kuwa dirhamu 1, 200, 000 (au pauni 30,000).2

Kwenye Ikulu za kustaajabisha za Wasasani kulikuwa na vito vingi na vitu vingine vya thamani, na yamekusanywa masanamu ya ajabu na michoro mingi mno kiasi kwamba macho ya watazamaji yalishangazwa mno.

Kama tukitaka kuyajua maajabu ya ikulu hizi itatutosha kama tukilitazama zulia jeupe kubwa walilolitandaza mwenye ukumbi wa moja ya ikulu hizi. Zulia hili, lililoitwa ‘Sabaristan-i Kisra’ lilitengenezwa na watawala wa Kisasania kwa lengo la kwamba, katika nyakati za furaha waweze kuwa kwenye mielekeo mizuri na ili daima waweze kuwa na mandhari nzuri na za uchangamfu za majira ya kuchipua machoni mwao.3

Imesemekana kwamba zulia hili lilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja na hamsini na upana wa dhiraa sabini. Pindo lake lote pamoja na nyuzi za pindo hilo zimesukwa kwa dhahabu, na vito vilitomewa humo.4

Miongoni mwa wafalme wa Kisasania aliyekuwa akipenda mno anasa alikuwa ni Khusro Pervez. Kwenye Ikulu yake alikuwa na maelfu ya wake, wajakazi, malenga na wanamuziki. Kwenye kitabu chake kiitwacho ‘Sanii Mulukul Ardh’ (wafalme wakuu wa duniani) Hamza Isfahani anayaelezea maisha ya anasa ya mfalme huyu kwa maneno haya:

“Khusro Pervez alikuwa na wake elfu tatu na wajakazi elfu kumi na mbili waliokuwa wacheza muziki. Alikuwa na wanaume elfu sita waliokuwa wakifanya kazi ya ulinzi. Farasi wapatao 8,500 walikuwa wamewekwa alama za masikioni kuwaainisha kwamba ni kwa ajili ya yeye kupanda. Alikuwa na tembo (ndovu) 960 na nyumbu 12,000 kwa ajili ya kubeba mizigo yake. Vile vile alikuwa na ngamia elfu moja.”5
Kisha Tabari anaongezea juu ya hayo kwa kusema kwamba: “Mfalme huyu alipenda sana vito na vyombo vya thamani n.k. zaidi ya mtu ye yote mwingine.”6

Hali Za Kijamii Nchini Iran

Kwa vyovyote vile hali za kijamii ya Iran katika zama za Wasasani hazikuwa nzuri zaidi ya hali ya kisiasa iliyokuwako mwenye baraza la Mfalme. Utawala wa kitabaka uliokuwako nchini Iran tangu zamani, ulilichukua umbo lake kali zaidi kwenye zama za utawala wa Wasasani. Watu wa koo zilizo bora na wakuu wa dini walikuwa bora zaidi kuliko watu wa matabaka mengine. Ofisi zote za umma na kazi zilizo muhimu ziliwekwa kwa ajili yao.

Mafundi na wakulima walinyimwa haki na upen- deleo wote wa kijamii. Ukiachilia mbali kule kulipa kodi na kushiriki kwenye vita, hawakuwa na kazi yoyote nyingine ya kutenda.

Mwandishi mmoja, Bwana Nafisi anaandika hivi kuhusu utofautishaji wa matabaka ya watu kwenye zama za utawala wa Wasasani: “Jambo lililokuwa sababu hasa ya kupandikiza ugomvi miongoni mwa Wairani ilikuwa ni utofautishaji wa kitabaka uliokuwa mkali zaidi na uliodumish- wa na Wasasani nchini Iran. Mizizi ya jambo hili ilitokana na ustaarabu wa kale, lakini ilikazwa mno kwenye kipindi cha utawala wa Wasasani.”

Hapo awali familia saba za ukoo bora na baada ya hizo, tabaka nyingine tano zilifaidi upendeleo na mtu wa kawaida alinyimwa upendelea huo. Karibuni ‘umilikaji’ wote ulipewa zile familia saba. Idadi ya watu wa Iran katika zama za Wasasani ilikuwa karibuni watu milioni 140. Kama tukichukulia kwamba idadi ya watu wa kila moja ya familia hizi ni laki moja, idadi ya watu wa familia zote itakuwa ni laki saba.

Na kama tukichukulia ya kwamba maafisa mabwana wa mipakani na ambao nao walifaidi haki ya kumiliki kwa kiasi fulani, nao walikuwa laki saba, hali itakuwa kwamba, kati ya watu milioni 140, ni watu milioni moja na nusu tu waliokuwa na haki ya kumiliki na wale wote wengine walinyimwa hii haki ya kimaumbile ambayo Allah Amempa mwanaadamu.7

Mafundi na wakulima, walinyimwa haki na upendeleo wote lakini walipasika kubeba mabegani mwao mzigo mzito wa gharama za zile koo bora, hawakuona kuwa ni jambo lenye thamani kuzihifadhi hali hizi. Hivyo basi, wengi wa wakulima na watu wa tabaka la chini walizikana kazi zao na wakakimbila kwenye majumba ya watawa ili kuepuka ulipaji wa kodi nzito.8

Baada ya kutoa maelezo ya misiba ya mafundi na wakulima wa Iran, mwandishi wa kitabu kiitwacho ‘Iran-dar Zaman-i- Sasaniyan’ ananukuu maelezo haya ya mwanahistoria mmoja wa kizungu aliyeitwa Amyan Marcilinos: “Mafundi na wakulima waliishi maisha ya kimaskini na fedheha katika zama za utawala wa Wasasani. Ilipotokea vita walitembea kwa miguu na ndio waliounda mstari wa nyuma wa jeshi na wasio na faida yoyote, kana kwamba wameamriwa utumwa wa daima, na hawakuweza kupewa mishahara au zawadi kwa kazi waliyoifanya.”9

Haki Ya Kupata Elimu Ilihifadhiwa Kwa Ajili Ya Watu Wa Matabaka Ya Juu Tu

Katika zama za Wasasani ni watoto wa matajiri na wa koo bora tu waliopasika kupata elimu, na umma na matabaka ya katikati walinyimwa kupata elimu na heshima.

Hii dosari mbaya mno katika utamaduni wa Iran ya kale ilikuwa bayana mno kiasi kwamba hata waandishi wa tenzi (Khudainamah na Shahnamah) wameitaja kwa maneno ya dhahiri, ingawa mada yao hasa ilikuwa ni maelezo ya mafanikio ya mashujaa.

Bwana Firdausi, mwandishi maarufu wa tenzi nchini Iran, ameitaja hadithi moja kwenye Shahnamah yenye ushuhuda wa dhahiri juu ya jambo hili. Hadithi hii ni ya wakati wa Anushirwan yaani katika muda ule ule ambao utawala wa Kisasania ulikuwa ukipita katika zama zake zilizo bora zaidi. Na hadithi hii yaonyesha kwamba watu wengi ukiwamo umma wote hawakuwa na haki ya kuelimika na hata yule mpenzi wa hekima na uadil- ifu, Anushirwan hakuwa tayari kuwapa haki ya elimu watu wa matabaka mengine ya umma ule!

Firdausi anasema: “Fundi viatu mmoja akajitokeza na kujitolea kutoa kiasi kikubwa cha dhahabu na fedha ili kuzilipia gharama za vita baina ya Iran na Urumi. Wakati ule Anushirwan alikuwa mhitaji mno wa msaada wa fedha, kwa kuwa kiasi cha askari elfu thelathini wa Iran walikabiliwa na upungufu wa chakula na silaha. Kulikuwa na makelele miongoni mwa askari walioidhihirisha huzuni yao mbele ya mfalme mwenyewe.

Anushirwan aliudhishwa na hali hii ya mambo na akatahadharika kuhusu mwishilizio wake. Mara moja akamwita waziri wake mwenye hekima aliyeitwa Buzurg Mehr atafute dawa ya hali ile na akamwamrisha aende upesi Mazandran akatafute fedha za kugharimia vita ile.

Hata hivyo, Buzurg Mehr akasema: “Hatari iko karibu sana, hivyo basi ni lazima kufanya jambo fulani liwezalo kutoa dawa ya hatari hii.” Hapo ndipo Buzurg Mehr akapendekeza mkopo wa kitaifa. Ushauri huu ulipendwa na Anushirwan aliyeamrisha ya kwamba zichukuliwe hatua kuhusiana na jambo hili bila ya kuchelewa. Buzurg Mehr akawapeleka maafisa kwenye majiji na miji ya karibuni na wakawafahamisha matajiri wa sehemu hizo hali ile.

Fundi viatu akajitolea kutoa gharama zote za vita ile. Malipo aliyoyataka kutokana na huduma hii yalikuwa kwamba mwanawe wa pekee aliyependa sana elimu aruhusiwe kuipata. Buzurg Mehr alilifikiria ombi hili kuwa ni dogo sana likilinganishwa na zile fedha alizozitoa.

Aliharakisha kumwendea mfalme na kumfahamisha lile ombi la fundi viatu. Anushirwan alichukizwa, akamkemea waziri wake na akasema: “Unaniomba jambo la ajabu kiasi gani! Hili ni jambo lisilofaa hata kidogo, kwa sababu, atakapotoka nje ya mpango wa matabaka, mila ya mpango wa matabaka nchini humu itatetereka na madhara yatakayotokana na hali hiyo, yatakuwa makubwa mno kuliko ile dhahabu na fedha anayotaka kuitoa.”

Firdausi anaielezea falsafa ya kidanganyifu ya Anushirwan kwa maneno ya yeye mfalme mwenyewe: “Mwana wa mfanyibiashara atakapokuwa katibu na vile vile akajipatia ustadi, hekima na ujuzi.

Basi, mwana wetu atakapokitwaa kiti cha enzi, atamhitaji katibu aliyejaaliwa bahati njema.
Kama mwana wa mtu ajishughulishaye na viatu atajipatia ustadi, utamwazima macho yenye uwezo wa kuona vizuri, pamoja na masikio.

Katika tukio hilo, hakuna kitakachomsalia mtu mwenye busara wa ukoo bora ila majuto na majonzi.”

Hivyo pesa za fundi viatu yule zilirudishwa kwa amri ya “Mfalme Mwadilifu.” Jambo hili lilimfanya yule fundi viatu asiyekuwa na msaada wowote kutokuwa na furaha hata kidogo na; kama ilivyo kawaida kwa watu wanaokandamizwa, alimlalamikia Allah Mwenye nguvu zote wakati wa usiku na akaifanya “kengele ya uadilifu wa Mungu ilie.”

Kwa kauli ya Firdausi: “Yule mjumbe alirudi na pesa zile na yule fundi viatu akahuzunika sana kuhusiana na fedha zile.

Alihuzunishwa sana na maneno ya Mfalme na ulipoingia usiku aliipiga “kengele ya Mungu.”10

Alipokuwa akizungumzia juu ya sababu za kuanguka, utovu wa utulivu na mvurugiko wa kipindi cha utawala wa Wasasani, mwandishi wa kitabu kiitwacho Tarikh-i-Ijtima’i-Iran; ambaye yeye mwenyewe yu mmoja wa watangulizi wa wazalendo, anatupa picha ya haki ya elimu kuwa kitu kilichotengwa kwa ajili ya watu wa matabaka ya juu, kwa maneno haya: “Katika kipindi hiki elimu na mafunzo ya matawi ya kawaida ya elimu yalikuwa yakimilikiwa na watoto wa watu wa koo bora na viongozi wa dini, na karibuni watoto wote wengine wa Iran waliinyimwa.” 11

Kwa hakika mila hii ya kuuweka umma katika hali ya ujinga ilikuwa muhimu mno kwamba hawakupenda kuiacha kwa gharama yoyote ile. Hivyo basi, wengi wa Wairani walinyimwa haki ya elimu pamoja na haki nyingine, ili kwamba tamaa za kiusumbufu na zisizofaa za hawa watu wachache walioongozwa vibaya ziweze kutimizwa.

Ushuhuda Wa Historia Juu Ya Wafalme Wa Kisasania

Wengi wa wafalme wa Kisasania walijitwalia sera ya ukali ya serikali na walitaka kuwatiisha watu kwa nguvu. Waliwatoza watu kodi kubwa mno na zenye kutaabisha.

Hivyo basi, watu wa Iran kwa kawaida hawakuridhika, lakini kwa kuchelea uhai wao hawakuthubutu kulitamka neno lolote lile la malalamiko. Halikuwezekana hilo, kiasi kwamba hata wasomi na watu wenye uzoefu hawakupewa utambuzi wo wote ule na baraza la Kisasania.

Watawala wa Kisasania walikuwa madikteta na waliozingatia mno matakwa yao kiasi kwamba hakuna mtu yeyote aliyeweza kutoa maoni yake juu ya jambo lo lote lile.

Ingawa mara nyingi historia hugeuzwa kupitia kwa watu washikao madaraka, hadithi zimesimuliwa kuhusu dhuluma na ukatili wa wadhalimu.

Khusro Pervez alikuwa yu mwenye moyo mgumu mno kiasi kwamba Tha’labi anaandika hivi kuhusiana naye: “Khusro aliarifiwa ya kwamba gavana fulani, aliamrishwa kuja kwenye baraza la mfalme lakini alikuwa ametoa udhuru. Mara moja mfalme huyo alitoa amri kwamba: “Kama ni vigumu kwake kuja mbele yetu kwa mwili wake wote, sisi tutatosheka na sehemu tu ya mwili huo, ili kwamba mambo yamuwie mepesi. Mwambie, mtu huyo ahusikaye akilete kichwa chake tu barazani kwangu.”12

Ghasia Katika Zama Za Wasasani

Tunapojifunza sehemu ya mwisho ya zama za Wasasani, jambo lisiloweza kupotea machoni petu ni utawala mbaya wa serikari, na kuwapo kwa utovu wa kanuni na fitina na ghasia kwenye utawala wa Wasasani.

Wana wa wafalme, watu wakuu na machifu wa jeshi walikuwa wakigombana. Kundi moja likimtawaza mwana mfalme mmoja na jingine likimwuzulu na kumchagua mwingine.

Waislamu wa Uarabuni walipoamua kuitwaa Iran, familia ya kifalme ya Wasasani ilikuwa nyonge mno na iliyojitumbukiza mno kwenye ugomvi. Katika kipindi cha miaka minne kilichoanzia kwenye mauaji ya Khusro Pervez na kwenye kupanda kwenye kiti cha enzi kwa Sheroya hadi kwenye kutawazwa kwa mfalme wa Kisasania wa mwisho Yazd Gard, wafalme wengi waliitawala Iran.

Idadi yao imetajwa kuwa ni kuanzia sita hadi kumi na wanne. Hivyo basi, Serikali ya Iran ilipita kutoka mkono huu kwenda mwingine kwa kiasi cha mara kumi na nne katika kipindi cha miaka minne. Inaweza kufikiriwa vizuri, kuwa ni hali gani ya nchi hii iliyokuwa nayo wakati mapinduzi yaliyotokea humo mara kumi na nne katika kipindi cha miaka minne na kila mara mtu mmoja anauawa na mwingine anatawazwa badala yake.

Kila mwenye kuzishika hatamu za Serikali, huwaulia mbali wale wengine waliokitaka kiti cha enzi na alizifanya aina zote za ukatili ili kukipata cheo chake hicho. Baba aliimwua mwanawe, mwana alimwua babie na ndugu aliwamalizilia mbali nduguze.

Sheroya alimua baba yake, Khusro Pervez ili kukitwaa kiti cha enzi 13 na vile vile aliwaua wana arobaini wa Khusro Pervez (yaani nduguze). 14

Shehr Baraz alimua kila mmoja ambaye hakuwa na uhakika naye kwamba labda angalikuwa hatari kwa kiti chake cha enzi au la. Hatimaye, wale wote waliopata kukikalia kiti cha enzi, wakiwa ni wanaume na wanawake, na wakiwa ni wazee au vijana, waliwaua akraba zao (yaani wale wana mfalme wa Kisasania) ili kwamba asiwepo abakiaye hai miongoni mwa wale watakaokitwaa kiti cha enzi.

Kwa kifupi ni kuwa, ghasia na utovu wa serikali vimeitwaa mielekeo hiyo katika zama za Wasasari kiasi kwamba watoto na wanawake walitawazwa kwenye kiti cha enzi, kisha wakauawa baada ya majuma machache, na wengine wakatawazwa badala yao.

Katika hali hii, ufalme wa Kisasania, ingawa ulikuwa na fahari na utukufu wake, ulikuwa ukielekea haraka haraka kwenye uchakavu wake, mgawanyiko na maangamizi.

Hali Ya Mchafuko Ya Iran Ya Wasasani Katika Mtazamo Wa Kidini

Sababu kuu zaidi ya hali ya ghasia nchini Iran katika zama za Wasasani ilikuwa ni tofauti na hitilafu za maoni katika mambo ya dini.

Ardshir Baabkaan, akiwa yu mwasisi wa ukoo wa Kisasania, yeye mwenyewe alikuwa mwana wa Mubid (kasisi wa dini ya Majusi) na alikifikia kiti cha enzi kwa msaada wa watu wa kiroho wa dini ya Majusi, alizitumia njia zote katika kuibalighisha dini ya jadi zake nchini Iran.

Katika siku za Wasasani dini rasmi na maarufu ya Taifa la Wairani ilikuwa ni Umajusi na kwa kuwa Serikali ya Wasasani ilidumishwa kwa msaada wa makasisi, wakuu wa dini ya Kimajusi walipata kila msaada kutoka kwenye baraza la kifalme. Matokeo yake ni kwamba, wakuu wa dini ya Kimajusi walipata nguvu zaidi nchini Iran katika zama za Wasasani, kiasi kwamba waliifaidi nafasi ya tabaka lenye nguvu zaidi nchini humo.

Daima watawala wa Kisasania walikuwa vibaraka tu wa makasisi na, kama ye yote miongoni mwa watawala hawa, hakuwatii watu wa kiroho, alipatwa na upinzani wao mkali na fedheha itokanayo na upinzani huo.

Hivyo basi, wafalme wa Kisasania, waliwazingatia mno wakuu wa dini kuliko watu wengine wote na kutokana na msaada walioupata makasisi hao kutoka kwa Wasasani, idadi yao iliongezeka siku baada ya siku. Wasasani, waliwatumia watu wa kiroho sana katika kuiimarisha dola yao. Walijenga mahekalu mengi ya ibada ya moto kwenye kila pembe na upenyo wa ile dola kuu ya Iran, na kila kwenye hekalu waliiweka humo idadi kubwa ya makasisi.

Inasemekana kwamba Khusro Pervez alijenga hekalu la moto na akawateua makasisi elfu kumi na mbili hekaluni humo kuimba tenzi na kusali. 15

Hivyo, dini ya Kimajusi ilikuwa ndio dini ya baraza la mfalme. Makasisi walijaribu kwa juhudi zao zote kuunyamazisha umma ulionyimwa na ulioteswa na kuijenga hali ya hewa ambayo watu wasiweze kuzihisi taabu zao.

Mwandishi wa kitabu kiitwacho Tarikh-i- Ijtima’i-i-Iran anaandika hivi: “….Wakishinikizwa na nguvu iliyotoka kwao (yaani hao makasisi), Wairani, walifanya juhudi za kujikomboa kutokana na taabu hizi. Kwa sababu hii, ikiwa ni kinyume na itikadi rasmi ya ‘Mazdesti Zartushti’ iliyokuwa dini ya serikali na baraza, na iliyoitwa ‘Behdin’, dini mbili nyinginezo zilitokea miongoni mwa Wamajusi…”16

Hakika hili lilitokana na ukali na matendo makali ya watu wakuu na maka- sisi kwamba katika Iran ya Wasasani dini mbalimbali zilikuwa zikitokea, moja baada ya nyingine. Mazdak na kabla lake Mani, 17 walijaribu kuleta mabadiliko kwenye hali za kiroho na kidini za nchi ile, lakini juhudi zao hazikufaulu.

Ilikuwa katika mwaka wa 497 Masihiya hivi kwamba Mazdak alikuja kwenye umaarufu. Alitangaza kubatilishwa kwa umilikaji wenye mashar- ti, ubatilishaji wa ndoa ya wake wengi na udumishaji wa nyumba za wake na masuria wa mtu kuwa ndio msingi wa mpango huo wa mabadiliko. Mara tu, baada ya matabaka ya walionyimwa kuujua mpango wa Mazdak, walimzunguka na wakayaendesha mapinduzi makuu chini ya uongozi wake.

Shabaha pekee ya maasi na vyama hivi ilikuwa kwamba watu waweze kuzipata haki zilizo halali walizozipewa na Allah, Mwenye nguvu zote. Hatimaye ilimbidi Mazdak kupambana na uadui wa watu wa kiroho na upinzani wa jeshi, na matokeo ya jambo hili yalikuwa matatizo na maangamio kwa Iran.

Vile vile dini ya Kimajusi ilikuwa ishaupoteza ukweli wake katika siku za mwishoni za Wasasani. Moto ulikuwa umepewa utakatifu mwingi mno kiasi kwamba ilifikiriwa kuwa haramu kukifua chuma kilichochukua hali ya moto kwa sababu ya kubakia kwenye ujirani wake, na mingi ya msingi na itikadi za Kimajusi zilipewa sura ya ushirikina na visasili.

Katika kipindi hiki, ukweli wa dini hii ulikuwa umetoweka na nafasi yake kuchukuliwa na ibada fulani fulani zilizo duni, zisizo na maana na za kipuuzi. Kawaida zao zilikuwa daima zikikuzwa na makasisi ili kuikuza nguvu yao. Visasili na ushirikina wa kipuuzi vimepenyeza mno kwenye dini hii kiasi kwamba vimewafanya hata wale watu wa kiroho kuwa wagumu. Na hata miongoni mwa makasisi walikuwamo watu walioutambua udanganyifu wa ibada na itikadi za Kimajusi na walikuwa wakijitua mizigo ya ibada na itikadi hizi.

Kuanzia kwenye wakati wa Anushirwan kwenda mbele, njia ya mwangaza ilifunguka nchini Iran, na matokeo ya kupenyeza kwa elimu ya Kigiriki na Kihindi pamoja na kukutana kwa itikadi za Kimajusi na zile za Kikristo na za dini nyinginezo, mwanga ule kila mara ulikuwa ukizaa uangalifu wa watu wa Iran. Hivyo, zaidi ya vile ilivyopata kuwa kwenye wakati wowote ule mwingine, walijihisi kuhuzunishwa na ushirikina na dhana tupu zisizo na msingi za dini ya Kimajusi.

Mwishowe, kuoza kulikotokea kwenye jamii ya kiroho ya Kimajusi na ushirikina na ngano za kipuuzi zilizoivunja dini ya Kimajusi zikawa chanzo cha mwelekeo mwingine na mtawanyiko kwenye dini na maoni ya taifa la Wairani.

Kutokea kwa tofauti hizi, na kuwako kwa dini mbalimbali kulizaa moyo wa mashaka na kutoweza kuamua, kutembea akilini mwa watu wenye busara na kutokana na watu hao, pole pole moyo huo ulipenyeza akilini mwa watu kwamba umma wote uliipoteza kabisa dini na itikadi sahihi waliyokuwanayo hapo mwanzoni.

Hivyo basi, hali ya kutoishika dini na uzembe iliizunguka Iran. Barzuyah, mganga maarufu wa zama za Wasasani ameisawiri picha kamili ya mgeuko wa kiitikadi na hali iliyochafuka ya Iran ya Wasasani kwenye utangulizi wa kitabu chake kiitawacho ‘Kalilah wa Damnah

Vita Baina Ya Iran Na Urumi

Buzurq Mehr, aliyekuwa mtu hodari na aliyekuwa na cheo kikuu zaidi kwenye utawala wa Anushirwan, kwa mara nyingi sana aliiokoa Iran kutokana na hatari kubwa mno kutokana na nguvu ya sera yake ya kibusara na uzoefu. Hata hivyo, kwenye nyakati fulani fulani, watu wenye hila na wachongezi waliutia giza uhusiano wake na Anushirwan na baada ya watu hao kumchochea Mfalme kuchukua hatua dhidi yake, ikatolewa amri ya kufungwa kwake.

Wafitini hao hao waliitia sumu akili ya Anushirwan kuhusu Dola ya Kirumi na ikamchochea kuyakataa mapatano ya amani ya kudumu na kuwahujumu Warumi ili kuipanua mipaka ya nchi na kuyadhoofisha mashindano ya hatari yawezayo kutokea. Hatimaye ilianza vita na katika muda mfupi tu jeshi la Iran liliiteka Sham, likaichoma Antakia na kuiharibu Asia Ndogo.

Baada ya vita na umwagaji damu wa miaka ishirini, majeshi yote mawili yalizipoteza nguvu na nafasi zao za ushindi; na, baada ya kupata hasara kubwa sana, yalifanya mikataba ya amani mara mbili na wakakubaliana kuidumisha mipaka yao ya awali, chini ya masharti ya kwamba serikali ya Kirumi itaitaka Serikali ya Iran kulipa dinari elfu ishirini kila mwaka.

Kadiri ya vita vya muda mrefu, na pia wale waliopigana kwenye maeneo ya mbali kutoka katikati ya nchi, yawezavyo kuleta madhara kwa uchumi na viwanda vya taifa, kunaweza kukisiwa vizuri sana. Tukifikiria uchumi wa zama zile, haikuwazekana kurekebisha upesiupesi athari za vita ndefu kiasi hicho. Vita hivi pamoja na shambulio ilitoa utangulizi wa kuanguka kabisa kwa serikali ya Iran. Madonda ya vita hivi yalikuwa bado hayjapona wakati ilipoanza vita vingine vya miaka saba. Baada ya Mfalme wa Kirumi aliyeitwa Tibrius, kukikalia kiti cha enzi, akiwa na nia ya kulipiza kisasi alifanya mashambulizi makali nchini Iran na akautishia uhuru wa nchi hiyo. Hali ya yale majeshi mawili ilikuwa bado haijaamulika, Anushirwan aliiaga dunia na mwanawe Khusro Pervez akakitwaa kiti cha enzi.

Katika mwaka 614 Masihiya, yeye naye, akizitegemea nyudhuru fulani fulani alianza upya kuwashambulia Warumi na matokeo ya shambulio la awali kabisa yaliiteka Sham, Palestina, na Afrika; wakaiteka nyara Yerusalemu, yakazichoma sehemu zao takatifu na kuiharibu kabisa miji mbali mbali. Baada ya kuimwaga damu ya Wakristo wapatao elfu tisini, vita hivyo vilikoma kwa faida kuuendea upande wa Iran. Wakati huo ulimwengu uliostaarabika wa siku zile ulipokuwa ukiungua kwenye moto wa vita na ukandamizaji, Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) alipewa dhamana ya ujumbe wa Utume.

Huo ulikuwa ni mwaka 610 Masihiya. Aliwabalighishia watu ujumbe wenye kuhuisha wa Upweke wa Mungu na kuwaitia kwenye amani, ukweli, nidhamu na mibaraka.

Kushindwa kwa Warumi waliokuwa wakimwabudu Mungu mikononi mwa Wairani wenye kuabudu moto kulichukuliwa na watu wa Makkahh wenye kuabudu masanamu kuwa ni ndege njema na walifikiria kwamba, katika wakati wa karibu, wao nao wangaliweza kuwashinda wenye kumwabudu Mungu (yaani Waislamu). Hata hivyo, Waislamu walisikitishwa na taarifa hizi. Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) aliusubiri ufunuo wa Allah na kisha ikafunuliwa aya ifuatayo: “Warumi wameshindwa na Wairani, kwenye nchi iliyo karibu (ya Sham na Palestina), nao baada ya kushindwa kwao, watashinda…”(Al-Ruum, 30:2-3). Utabiri huu uliofanywa na Qurani Tukufu ulitimia katika mwaka wa 627 Masihiya. Hercules alipoishambulia na kuichukua Naynava.

Washindani hawa wawili walikuwa wakipumua pumzi za mwisho maishani mwao na walikuwa wakipanga kupata askari wa kuzidishia nguvu majeshi yao. Hata hivyo, kutokana na mapenzi ya Allah iwe kwamba hizi nchi mbili ziangazwe na ibada ya Allah Aliye pekee, na roho zilizodhoofishwa za Wairani na Warumi ziweze kurudishiwa nguvu na upepo mwanana wenye kuhuisha wa Uislamu, haikuchukua muda mrefu kabla ya kuuawa Khusro Pervez na mwanawe Sheroyah, na huyo mwanawe naye alifariki dunia baada ya miezi nane tangu kufa kwa baba yake.

Katika kipindi hiki Iran ilipitia kwenye ghasia nyingi mno kiasi kwamba, baada ya Sheroyah walikuwapo watawala tisa waliotawala kwenye kipindi cha miaka minne (ambao miongoni mwao wanne walikuwa ni wanawake), hadi mwishowe, jeshi la kiis- lamu likaikomeshezea mbali hali hii ya mambo. Ugomvi huu, ulioenea kwa zaidi ya miaka hamsini, kwa hakika ulikuwa wenye msaada mkubwa wa kutia moyo utekaji wa Waislamu.

 • 1. Tarikh ‘Ulumwa Adabiyat dar Iran Dr. Safa, uk. 3 – 4; Iran dar Zaman-i- Sasaniyan, Christensen, uk. 267.
 • 2. Rejea: Payambar-i- Rehnuma, Juzuu I, uk. 42 – 43.
 • 3. Payambar-i-Rehnuma, Juzuu 1, uk. 42 – 43.
 • 4. Payambar-I-Rehnuma, Juzuu I, uk. 43; Kwenye kitabu kiitwacho ‘Ganj-i- Daanish’ Muhammad Taqi Khan Hakim, Mu ‘tamadus Sultan’, amelielezea zulia hilo ‘Nigaristan’ kwa kirefu zaidi alipokuwa akitafiti kuhusu baraza la Makhosro.
 • 5. Sanii Mulukul Ardh wal Ambiya, uk. 4260.
 • 6. Tarikh-i-Tabari, kama kilivyonukuliwa na Christonson, uk. 327.
 • 7. Tarikh-i-Ijtima’i-i-Iran, Juzuu 2, uk. 24 – 26.
 • 8. Limadha Khasir al-Aalam bi inhi-taatil Muslim, uk. 70-71.
 • 9. Iran fi ahdith Sasani’in, uk. 424.
 • 10. Firdausi ameisimulia hadithi hii mwenye kitabu chake Shahnamah kama tukio la utawala wa Anushirwan kuhusiana na vita baina ya Iran na Urumi (Shahnamah, Juzuu 6, uk. 257-260). Dr Sahib-al-Zamani ameichanganua hadithi hii mwenye kitabu chake kiitwacho ‘Dibacha-i-bar Rehbari’ (uk. 258-262) kwa jinsi ivutiayo mno. Vile vile tazama kitabu kiitwacho ‘Guzarish Nama-i-Iran’, cha bwana Mahali Quli Khan Hidayat. (uk. 232)
 • 11. Tarikh-i- Ijtima’i – i- Iran, Juzuu 2, uk. 26.
 • 12. Al-Uyun, uk. 136, Amali Saduq uk. 274 na Biharul Anwar, uk. 35.
 • 13. Murujuz Zahab, Juzuu 1, uk. 281,
 • 14. Tarikh-i- Ijtima’i-i-Iran, cha Sa’id Nafisi. Juzuu 2, uk. 15 – 19.
 • 15. Tarikh-i-Tamaddun-i-Sasani, Juzuu 1, uk. 1.
 • 16. Tarikh-i-Ijtima’i-i-Iran, Juzuu 2, uk. 20.
 • 17. Dini ya Mani ilikuwa ni muungano wa Uzoroasta na Ukristo. Hivyo, Mani aliasisi dini mpya kwa kuichanganya dini ya kienyeji na ya kigeni.