read

Sura Ya Tisa: Kutoka Kwenye Uchungaji Hadi Kwenye Biashara

Viongozi wa ki-Mungu hupewa majukumu muhimu na makubwa. Hilo ni jukumu liandamanalo na mashaka na ufukara, mateso na misiba, mauaji na kifo, n.k, kwa kifupi ni kwamba huandamana na kila aina ya mateso. Na kadiri lengo lao liwavyo kuu na tukufu zaidi ndivyo magumu yaandamanayo nalo yatakavyokuwa makali na mabaya zaidi.

Kuhusiana na jambo hili, ushujaa na uvumilivu, yaani kuwa na subira katika matatizo yote, masuto, kujeruhiwa na mateso, yote hayo ni masharti kwa ajili ya mafanikio ya kiongozi wa ki-Mungu, kwa sababu uvumilivu na subra ni sharti halisi katika hatua ya kampeni ya kulifikia lengo lao.

Katika historia na masimulizi yahusianayo na Mitume, tunayaona mambo yaliyo magumu kwetu (sisi watu wa kawaida) japo kwa kuweza kuyafikiria tu. Tunasoma habari za Nabii Nuhu (a.s.) kwamba alihubiri dini kwa kipin- di cha miaka 950! Na matokeo ya kampeni yake hiyo, na juhudi zilizoen- delezwa kiasi hicho, ni watu themanini na moja tu waliomwamini. Kwa maneno mengine ni kwamba kila kwenye kipindi cha miaka kumi na miwili aliweza kumleta mtu mmoja tu kwenye njia iliyonyooka.

Ubora wa uvumilivu na subira hukua mwilini mwa mwanadamu pole pole. Ni muhimu kwamba ayakabili matukio yasiyopendeza ili kwamba roho yake iyazoee matatizo na mateso kwa ukamilifu.

Kabla ya Mitume hawajalifikia daraja la Utume walikuwa wakiitumia sehemu ya maisha yao wakiwa ni wachungaji wa wanyama ili kwamba wautumie wakati fulani wa maisha yao wakiwa nyikani wakiyalisha makundi ya wanyama, na hivyo waweze kuwa na subira na wavumilivu kwa ajili ya elimu ya wanadamu na ili waweze kuichukulia hali ya kuyavu- milia magumu na matatizo yote kuwa ni jambo la kawaida tu.
Huwa hivyo kwa sababu mtu awezapo kuyavumilia magumu kuhusiana na mnyama ambaye kwa upande wa akili na busara, hawezi kulinganishwa na mwanaadamu, hana budi kulikubali jukumu la mwongozo wa watu waliopotea, wanao wawajibikia na kutayarishwa kwa ajili ya kumwitakidi Allah. Tuliyoyazungumzia hapo juu ni kwa mujibu wa Hadithi inayosema: “Allah Hakumtuma Mtume yeyote asiyefanywa kuwa mchungaji wa wanyama, ili kwamba aweze kujifunza jinsi ya kuwaongoza watu.1

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) naye alikitumia kipindi fulani cha maishani mwake katika kazi hii na karibuni waandishi wengi wa siirah (wasifu) wameinukuu sentensi ifuatayo kutoka kwake: “Mitume wote walikuwa wachungaji kwa kipindi fulani kabla ya kukifikia cheo cha Utume.” Watu wakamwuliza Mtume (s.a.w.w.); “Je, wewe nawe umepata kuwa mchungaji?” akajibu: “Ndio, kwa kipindi fulani niliwachunga kondoo wa watu wa Makkahh kwenye eneo liitwalo Qarariit.”

Hakuna shaka kwamba ilikuwa muhimu kwa mtu yule aliyelazimika kupi- gana na akina Abu Jahl na akina Abu Lahab na aliyetaka kuwatengeneza watu, kutoka kwenye hali ya kuwa watu waliofedheheshwa, ambao akili zao na hekima zao vilikuwa katika kiwango cha kulipigia goti kila jiwe na fimbo, (kuwatengeneza ili) kuwa kundi la wale wasiokubali kulifuata penzi la yeyote yule ila penzi la Allah tu, kwamba mtu huyu ajizoeze somo la uvumilivu na subira, kwa njia mbali mbali na kwa kipindi fulani kitoshelezacho.

Tunafikiria vilevile kwamba ilikuwepo sababu nyingine iliyomfanya Mtume (s.a.w.w.) aichague kazi ya uchungaji. Ilikuwa kwamba kule kuziona njia za maisha za kipumbavu za wale waliokuwa na mamlaka miongoni mwa Waqureishi na kule kuyadhihirisha kwao maovu, kulikuwa na uzito mkubwa akilini mwa mtu huyu aliye shujaa na muungwana, na aliye na hisia kuu za utukufu wa utu wema. Mbali na hili, kushindwa kwa jamii ya watu wa Makkah kumuabudu Mwenyezi Mungu na kule kuyazunguka kwao masanamu yasiyo na uhai kulikuwa jambo lenye kuchukiza kwa mtu mwenye hekima. Kwa sababu hizi, Mtume (s.a.w.w.) alijitenga na jamii ile na akaitumia sehemu ya maisha yake akiwa porini na katika miteremko ya milima iliyokuwa mbali na ile jamii iliyonajisika, ili kwam- ba, japo kwa kipindi fulani tu, aweze kutokuwa na mateso ya kiakili yaliyosababishwa na hali ya kuhuzunisha iliyokuwepo katika zama zile.

Kwa kulichunguza anga lipendezalo na mpangilio na maumbile ya nyota na kuifikiria miche ya porini, mtu mwenye fikra zilizoongezeka ataweza kujipatia mamia ya dalili za utaratibu wa Mwenyezi Mungu na kuimarisha itikadi ya kawaida juu ya upweke wa Allah kwa nguvu ya dalili za kisayansi. Ingawa kuna ukweli ya kwamba tangu wakati ule wa kuwepo kwao, nyoyo zao ziliangazwa na mwanga wa kurunzi ya upweke wa Alllah, na hawakujifikiria kuwa wako huru kutokana na haja ya kujifunza juu ya viumbe na Ulimwengu, na kwa njia hii waliweza kufikia daraja la juu zaidi la yakini na itikadi.

Pendekezo La Bwana Abu Twalib

Hali mbaya ya kiuchumi ya mpwawe ilimlazimisha Bwana Abu Twalib, ambaye alikuwa mmoja wa machifu wa Makkahh na watu watukufu wa Waquraishi na alikuwa maarufu kwa ukarimu wake, ushujaa wake, na daraja kuu la unyoofu wake, alipanga safari ya kikazi kwa ajili yake. Hivyo basi, alimwambia mpwa wake: “Khadija binti Khuwaylad yu mmoja wa matajiri wa Waquraidhi na shughuli zake za kibiashara zimeenea hadi Misri na Ethiopia. Bibi huyu anamtafuta mtu mwaminifu atakayelibeba jukumu la biashara yake, amfanyie kazi katika msafara wa biashara wa Waquraishi na kuzipeleka bidhaa zake Sham ili akaziuze huko. Ewe Muhammad! Itakuwa bora kiasi gani kama utakwenda kujitambulisha kwake!”2

Unyoofu na ubora wa kiroho wa Mtume (s.a.w.w.) havikumruhusu kumwendea Khadija moja kwa moja bila ya kufahamisha lolote, na bila ombi kutoka kwa Bibi huyu, na kutoa pendekezo kama hilo. Hivyo, alimjibu ami yake akasema: “Inawezekana kwamba yeye mwenyewe Bibi Khadija atanitumia mtu” Mtume (s.a.w.w.) aliyasema hayo kwa sababu alijua kwamba alikuwa maarufu miongoni mwa watu kama mtu mwaminifu. Na ilitokea hivyo.

Bibi Khadija alipata habari za mazungumzo yao, mara moja alimtuma mtu kwa Mtume (s.a.w.w.) akisema: “Jambo lililonivutia kwako ni ukweli wako, uaminifu wako na utu wema. Niko tayari kukupa maradufu ya kile niwapacho watu wengine na nitakupa watumwa wawili wafuatane nawe na ambao watakutii kwa hali yoyote ile iwayo.3

Mtume (s.a.w.w.) alimweleza ami yake habari hii, na yeye akasema: “Kazi hii uliyopewa ni chanzo cha mahitaji ya maisha yako aliyokuruzuku Allah.” Msafara wa Waquraishi uliokuwa na bidhaa za Bibi Khadija ukawa tayari kuondoka. Bibi Khadija alimpa huyu wakala wake ngamia mwenye hatua za taratibu, kiasi fulani cha chakula cha gharama na watumwa wawili, na kuwaamrisha watumwa wale kuwa wenye heshima mno kwa Mtume (s.a.w.w.) katika sehemu zote katu wasilikatae alitendalo, na kumtii kwa hali zote zile.

Hatimaye msafara ule ukafika kule ulikokuwa ukienda na wanamsafara wote walipata faida. Hata hivyo, faida aliyoipata Mtume, ilikuwa kubwa mno ukilinganisha na ile waliyoipata wale wengine na vile vile alinunua vitu kadhaa kwa ajili ya kuviuza katika Soko la Tahaamah.

Baada ya msafara ule kufanya safari iliyofanikiwa kule Sham ulirudi Makkahh. Katika safari hii Mtume (s.a.w.w.), alipitia tena katika nchi ya

Waadi na Wathamudi. Kimya cha kifo kilichokuwepo kwenye mazingira ya taifa lile asi kiliyaibua mazingatio yake zaidi na zaidi juu ya dunia nyinginezo. Zaidi ya hapo kumbukumbu za safari iliyotangulia pia zilihusishwa. Alizikumbuka siku alipoyapita majangwa hayo hayo akiwa pamoja na ami yake. Ule msafara wa Waquraishi ulifika karibu na Makkahh. Akizungumza na Mtume, Mtumwa mmoja kati ya wale wawili aliyeitwa Maysarah alisema: “Ingekuwa bora kama ungeliingia Makkahh kabla yetu na kumwarifu bibi Khadija juu ya mambo ya biashara na faida kubwa mno tuliyoipata mwaka huu.” Mtume (s.a.w.w.) aliingia Makkah wakati bibi Khadija alipokuwa ameketi kwenye chumba chake cha juu. Alishuka chini upesi upesi kumpokea na akaenda naye kule chumbani. Mtukufu mtume (s.a.w.w.) alimhadithia, kwa njia bora zaidi, mambo yaliyohusiana na bidhaa zile. Wakati huo Maysara naye aliwasili.4

Yule mtumwa wa bibi Khadija (Maysara) alimsimulia yale yote aliyoyaona katika ule msafara bila ya kuongeza wala kupunguza na yale yote yaliy- outhibitisha ukuu na imani ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) mwaminifu, pia alimweleza Bibi huyu kwamba katika safari ile yule ‘mwaminifu’ alito- fautiana na mfanya biashara mmoja juu ya jambo fulani.

Yule mtu alimwambia kwamba atayakubali maneno yake iwapo ataapa kwa ‘Lat’ na ‘Uzza’, lakini yule ‘mwaminifu’ alimjibu akisema: “Nawachukulia Lat na Uzza, mnaowaabudu kuwa ni vitu vidogo zaidi na vyenye kutwezwa zaidi usoni pa nchi.”5

Vile vile Maisara aliongeza kusema kwamba kule Basrah, yule ‘mwaminifu’ alikaa chini ya mti akipumzika. Wakati ule mtawa mmoja aliyekuwa katika nyumba yake ya utawa alibahatika kumwona. Alikuja na kumwuliza jina lake na kisha akasema: “Huyu mtu aliyekaa katika kivuli cha mti ndiye yule Nabii niliyesoma bishara nyingi katika Tawrati na Injili.”6

Bibi Khadija Mwanamke Wa Kwanza Wa Uislam

Hadi wakati ule, hali ya kifedha na kuichumi ya Mtume (s.a.w.w.) ilikuwa bado haijawa nzuri na bado alikuwa akihitaji msaada wa kifedha kutoka kwa ami yake Abu Twalib. Mambo yake ya kibiashara yalionekana dhahiri kutokuwa imara kiasi cha kumwezesha kumchagua mke na kujenga familia.

Safari yake ya mwisho kwenda Sham, na safari hii nayo akiwa yu wakala na mwakilishi wa yule mwanamke tajiri na maarufu wa Waquraishi (Khadija) iliimarisha hali yake ya kifedha na kiuchumi kwa kadiri fulani. Ushujaa na uzoefu wake viliyavutia mapenzi ya Khadija na akadhihirisha kuwako kwake tayari kumlipa kitu fulani zaidi na juu ya ujira waliopatana.

Hata hivyo, Mtukufu Mtume alikubali kupokea ule ujira waliopatana hapo awali. Kisha alikwenda nyumbani kwa Abu Twalib na kumpa kiasi chote alichokipata. Ili aweze kumpatia ami yake msaada fulani.

Abu Twalib alikuwa akimsubiri kwa shauku mpwawe aliyekuwa ukumbusho wa baba yake (Abdul-Mutwalib) na nduguye Abdullah. Machozi yalimtiririka machoni mwake mara tu alipomwona. Hata hivyo, alifurahi mno kusikia juu ya shughuli zake za kibiashara na faida zake na alidhihirisha kuwako kwake tayari kumpa farasi wawili na ngamia wawili ili aweze kuendelea na biashara yake. Ama kuhusu ile fedha aliyoichuma katika ile safari na aliyompa ami yake, (Abu Twalib) aliamua kuitumia katika kuchagua mke kwa ajili ya mpwa wake.

Katika hali hii, Mtume (s.a.w.w.) aliamua kumchagua mchumba. Hata hivyo, swala lililoibuka ni vipi uchaguzi ule ulivyomwangukia Bibi Khadija ambaye hapo kabla yake alikataa posa za wanaume wa kiquraishi waliokuwa matajiri zaidi na wenye akili kama vile ‘Uqbah bin Abi Mu’it Abu Jahl na Abu Sufyan.

Ni sababu zipi zilizowaleta hawa watu wawili waliokuwa tofauti kabisa kimaisha, na zilizojenga uhusiano huu mzuri huba na mvuto wa kiroho baina yao kiasi kwamba Bibi Khadija alimpa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) utajiri wake wote, naye akautumia utajiri wa Bibi huyu wote alioupata kutokana na biashara zake zilizoenea hadi Misri na Ethiopia, katika njia ya upweke wa Allah na katika kuutukuza ukweli.

Na ilikuwaje kwamba ile nyumba iliyojaa vitu vilivyotiwa njumu za pembe za ndovu na lulu na kupambwa kwa hariri ya Bara Hindi na mazulia ya nyuzi za dhahabu za Uajemi (Iran) hatimaye ikawa kimbilio la Waislamu?

Sababu za matukio haya hazina budi kuthibitishwa kutoka kwenye historia ya maisha ya Bibi Khadija. Hata hivyo, jambo lisilokamilika hapo ni kwamba huduma, kujitia na kujitolea kwa aina hii bila shaka kusingaliweza kuwa kwenye kudumu ila tu pale kuwapo na chanzo kilichothabiti, safi na cha kiroho.

Kurasa za historia zathibitisha ya kwamba ndoa hii ilikuwa ni matokeo ya itikadi ya Bibi Khadija mwenye ucha mungu, usafi, na wema, pia uamimifu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), kipenzi cha Waquraishi, na historia ya maisha ya Bibi Khadija na masimulizi juu map- ato yake yaliudhihirisha ukweli huu.

Kwa vile Bibi Khadija alikuwa mwanamke mnyofu na mchamungu alita- ka ampate mume mchamungu na mwema na ni kwa sababu hii kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema juu ya Bibi huyu hivi: “Khadija yu miongoni mwa wanawake wa peponi wenye kuheshimiwa” Na mwanamke wa kwanza kumwamini Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alikuwa ni bibi Khadija (a.s.).

Imam Ali (a.s.), Amiri wa waumini, katika moja ya khutba zake, alipokuwa akieleza hali ya Uislam ya siku za mwanzoni za Utume wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) iliyokuwa ikisikitisha alisema: “Wakati huo haikuwako familia ya kiislamu ila familia aliyokuwamo Muhammad na mkewe Khadija, nami nilikuwa wa tatu wao.”

Mwanachuoni Ibni Athir anasema kwamba mfanya biashara mmoja aliyeitwa Afif alikuja msikitini Masjidul-Haraam na alishangazwa mno kuuona mkusanyiko mkubwa wa watu na ibada iliyokuwa ikiendeshwa na watu watatu. Aliona ya kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akisali pamoja na Bibi Khadija na Sayyidna Ali (a.s.).

Alipokuwa akirejea kutoka Masjidul-Haraam alikutana na Bwana Abbas, ami yake Mtume (s.a.w.w.). Alimweleza yale aliyoyaona na akauliza kuhusu ukweli wake. Bwana Abas akamwambia: “Kiongozi miongoni mwa watu hao anadai Utume na yule mwanamke yu mkewe Khadija na mtu wa tatu ni Ali, mpwa wangu.” Kisha akaongeza kusema; “Mimi simtambui mtu yeyote katika (huu) uso wa ardhi apasikaye kuwa mfuasi wa dini hii ila hawa watatu.”

Ni nje ya madhumuni ya kitabu hiki kueleza na kunukuu maelezo yaliy- opokelewa juu ya fadhila za Bibi Khadija. Hivyo basi, ingelikuwa bora kama tungelizieleza sababu zilizosabibisha tukio hili la kihistoria (yaani ile ndoa ya Mtume Muhammad s.a.w.w na Bibi Khadija).

Sababu Za Dhati Na Za Siri Za Ndoa Hii

Walimwengu, walichunguza kila jambo kwa mtazamo wa kilimwengu, wanadhania kwamba, kwa vile Bibi Khadija alikuwa tajiri na mfanya biashara, alihitaji mno mtu mwaminifu kuhusiana na mambo yake ya kib- iashara, na hivyo basi, akaolewa na Muhammad.

Na kwa vile Muhammad naye alikitambua cheo chake kikuuu alikubali ombi lake, ingawa ilikuwapo hitilafu katika umri wao. Hata hivyo, historia inatueleza kwamba Bibi Khadija alishawishika kuolewa na Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ‘mtu mwaminifu’ miongoni mwa Waquraishi kutokana na nyororo ya sababu za kiroho, na muungano huu haukuwa na sababu za kidunia. Ushahidi wenye kuunga mkono dai letu hili
ni huu ufuatao: Wakati Bibi Khadija alipomuuliza Maisara kuhusu matukio yaliyotokea katika safari ya Mtume (s.a.w.w.) alimweleza habari za miujiza aliyoiona kwake na vile vile yale aliyoyasikia kwa yule mtawa wa Sham.
Bibi Khadija alipandwa na fikara nyingi, zenye asili ya shauku yake katika mambo ya kiroho ya Mtume na akamwambia Maisara kwa hiari yake mwenyewe: “Maisara! Hiyo inatosha. Umeuzidisha kuvutiwa kwangu na Muhammad mara dufu! Hivyo nakuacha huru wewe na mkeo na pia ninakupa dirham mia mbili, farasi wawili na nguo ya thamani kuu!
Baadae alimweleza Waraqah bin Nawfal yale aliyoyasikia kwa Maisara, Nawfal alikuwa mtaalamu wa Bara Arabuni. Naufal akasema: “Mtu awaye na sifa hizi, atakuwa ndiye yule Nabii wa Uarabuni”.7

Siku moja Bibi Khadija alikuwa ameketi nyumbani mwake akizungukwa na wajakazi na watumwa wake. Pia alikuwapo pale mmoja wa wanachuoni wa Kiyahudi. Kwa bahati Mtume (s.a.w.w.) alipata kupita pale na yule mwanachuoni wa kiyahudi akamwona. Mara moja akamwomba Bibi Khadija amshikilie Mtume Muhammad (s.a.w.w.) aahirishe kazi zake nyingine na ajiunge na kundi hilo lao, kwa kipindi kifupi hivi.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikubali ombi la yule Myahudi mwenye busara ambalo lilitegemezwa juu ya kuziona dalili za Utume kwake. Kisha Bibi Khadija alimgeukia yule Myahudi mwenye busara na kusema: “Ami zake watakapo tambua utafiti wako na uchunguzi wako wataudhihirisha upinzani wao, kwa sababu wanawachelea Wayahudi kuhusiana na mwana wa ndugu yao.” Hapo mtaalamu wa kiyahudi akajibu hivi: “Je, yawezekanaje kwamba mtu yeyote yule amdhuru Muhammad, wakati mkono wa kudra umemlea kwa ajili ya Utume wa mwisho na kwa ajili ya mwongozo wa wanadamu?”

Bibi Khadija akasema: “Unasema kwamba atakishika cheo hiki kwa dalili gani?” Yule Myahudi mwenye busara akajibu: “Nimezisoma dalili za Mtume wa mwisho katika Torati. Dalili zake ni pamoja na mambo matatu; yaani wazazi wake watafariki dunia, babu yake na ami yake watamlea, na atachagua mke kutokana na mwanamke atakayekuwa Sayidati wa Waquraishi.” Kisha akamuonesha kidole Bibi Khadija na akasema “Amebarikiwa (bibi) yule atakayepata heshima kuwa mwenzi wa maishani mwake!”8

Waraqa, ami yake Bibi Khadija, alikuwa mmoja wa watu wenye busara wa Uarabuni. Alikuwa na elimu kamili ya Biblia na kila mara alikuwa akisema: “Allah Atamwinua mtu fulani kutoka miongoni mwa Waquraishi kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu, naye atamwoa mmoja wa wanawake matajiri wa Waquraishi” Na kwa vile Bibi Khadija alikuwa mwanamke tajiri zaidi wa Waquraishi, alikuwa kila mara akimwambia Bibi huyu: “Itawadia siku ambayo utaolewa na mwanaume mtukufu zaidi hapa duniani!”

Usiku mmoja Bibi Khadija aliota kwamba jua lilikuwa likizunguuka juu ya mji wa Makkah na kisha likashuka pole pole na kutua nyumbani mwake. Alimsimulia Waraqah bin Nawfal ndoto yake ile naye Nawfal akaitafsiri ndoto ile hivi: “Utaolewa na mtu mkuu na atakuwa maarufu ulimwenguni kote.”

Haya ndio matukio yaliyonukuliwa na baadhi ya wanahistoria na marehe- mu Allamah Majlis9 na vile vile yameandikwa katika vitabu vingi vya historia. Matukio yote hayo yanapofikiriwa huzidhihirisha wazi wazi sababu za mwelekeo wa Bibi Khadija kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Mwelekeo huu ulikuwa hasa ni kutokana na itikadi ya Bibi huyu katika hali ya kiroho ya Mtume (s.a.w.w.) na kwamba yule ‘mtu mwaminifu’ alifaa zaidi kuliko wengineo, hakuna sababu yoyote nyingine katika kutokea kwa muungano huu.

Mazingara Ya Posa Ya Bibi Khadija

Maelezo haya yanatosha kuthibitisha kwamba uchumba huu ulitoka upande wa Bibi Khadija mwenyewe; kiasi kwamba Ibn Hisham ananukuu10 kwamba Bibi Khadija aliudhihirishia mwelekeo wake kwa hiari yake

na akasema: “Ewe binamu yangu! Kutokana na udugu uliopo baina yetu na ukuu wa heshima uliyonayo miongoni mwa watu wako na unyoofu, tabia njema na ukweli ulionao, ninaelekea kwako kwa moyo (wangu) wote ili unione.” Yule ‘mwaminifu’ wa Waquraishi alijibu akisema: “Sina budi niwaarifu ami zangu jambo hili na jukumu hili halina budi kufanyika kwa ridhaa zao.”

Wengi wa wanahistoria wanaamini ya kwamba Bibi Nafisa bint Alyah ndiye aliyelipeleka pendekezo la Bibi Khadija kule kwa Mtume (s.a.w.w.) la kutaka kuchumbiwa na Mtume (s.a.w.w.) kwa jinsi hii, Bibi Nafisah alisema:

“Ewe Muhammad! Kwa nini hukiangazi chumba cha usiku cha maishani mwako kwa nuru ya mke? Je, utakubali kama nikikualika kwenye urembo, utajiri, upole na heshima?” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akajibu hivi: “Ni nini maana yako?” Hapo Bibi Nafisah akamtaja Bibi Khadija. Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Je, Khadija yuko tayari kwa jambo hilo wakati inapokuwapo tofauti kubwa baina ya hali ya maisha yangu na yake?” Bibi Nafisah akasema: “Ninayo mamlaka kwa niaba yake nami nitamfanya akubali, weka tarehe ya kulitimiza jambo hili ili kwamba walii wake (Amr bin Asad) akae pamoja nawe na jamaa zako na sherehe ya ndoa na tafrija viweze kufanyika.11

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alilizungumzia jambo hili na ami yake mheshimiwa (Abu Twalib). Ilifanyika tafrija kubwa iliyohudhuriwa na watu maarufu miongoni mwa Waquraishi. Jambo la kwanza kabisa Bwana Abu Talib alitoa hutuba, akiianza kwa kumhimidi Allah. Kuhusu yule mpwa wake, alimtambulisha hivi: “Mpwa wangu Muhamamd bin Abdallah yu bora kuliko mtu yeyote wa kabila la Waquraishi atakayelin- ganishwa naye. Ingawa hana aina yoyote ile ya utajiri, hata hivyo mali ni kivuli kinachopita, na asili na nasaba ni vya kudumu.”12

Kwa kuwa Bwana Abu Twalib aliwataja Waquraishi na familia ya Hashim katika hotuba yake, Waraqah, ami yake Bibi Khadija aliijibu hotuba ile akasema: “Hakuna yeyote miongoni mwa Waquraishi aukanaye ubora wenu. Tunayo shauku ya kutaka kuikamata kamba ya utukufu wenu.” Hivyo sherehe ya ndoa hii ilifanyika na mahari ikaamuliwa kuwa ni dinar mia nne. Baadhi ya watu wanasema kwamba mahari ile ilikuwa ya ngamia ishirini.

Umri wa Bibi Khadija: Kwa kawaida inasemwa kwamba wakati wa kuolewa na Mtume (s.a.w.w.) Bibi Khadija alikuwa na Umri wa miaka arobaini na alizaliwa miaka kumi na mitano kabla ya ‘mwaka wa ndovu’ Hivyo baadhi ya waandishi wamesema kwamba umri wake mwenyewe wakati wa ile ndoa ulikuwa chini ya hapo. Kabla ya hapo aliolewa mara mbili. Majina ya waume zake yalikuwa ni Ais bin Abid na Abu Halah na wote wawili walikuwa wamefariki dunia.

 • 1. Safinatul Bihar, chini ya neno ‘Nabi’
 • 2. Bihaarul Anwaar, Juzuu 16, uk. 22.
 • 3. Siirah Ibn Hisham, Juzuu 2, uk. 24.
 • 4. Al- Kharaa’ij, uk. 186 na Bihaarul Anwaar, Juzuu 16, uk. 4.
 • 5. Tabaaat-i-Kubra, uk..140.
 • 6. Bihaarul Anwaar, Juzuu 15 uk. 18.
 • 7. Siirah-i-Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 26.
 • 8. Bihaarul-Anwaar, Juzuu 16, uk. 19.
 • 9. Biharul-Anwaar, Juzuu 6, uk. 124
 • 10. Siirah-i-Ibn Hisham. Juzuu 1, uk. 204.
 • 11. Inafahamika vema kwamba Khuwaylid aliuawa katika vita vya Fujjar na kwa sababu hii ami yake aliidhinisha ndoa ile kwa niaba ya Bibi huyu. Hivyo basi, maoni yaliyotolewa na baadhi ya wanahistoria kwamba kwanza Khuwaylid hakukubali, lakini baadae alikubali kutokana na mwelekeo mkali wa Khadija, hayana msingi hata kidogo.
 • 12. Manaaqib, Juzuu 1, uk 30 na Bihaarul-Anwaar, Juzuu 15, uk. 6.