Table of Contents

Neno La Mchapishaji

Kitabu kilichoko mikononi mwako ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza kiitwacho, The Message, kilichoandikwa na Sheikh Ja’far Subhani. Sisi tumekiita, Ujumbe. Kwa vile kitabu hiki ni kikubwa, tumekigawa katika juzuu nne ili kuwarahisishia wasomaji wetu kukisoma kwa makini katika kila sehemu. Hii uliyonayo mkononi ni Juzuu ya Kwanza.

Kitabu hiki kilichoandikwa na mwanachuoni mkubwa Sheikh Ja’far Subhani kimekuwa ni miongoni mwa vitabu bora vilivyofanya utafiti wa kina kuhusu historia ya Uislamu na Waislamu. Haya ni matokea ya utafiti wa kielimu pamoja na hoja zenye nguvu na utumiaji sahihi wa akili uliofanywa na mwanachuoni mwandishi wa kitabu hiki juu ya maudhui haya yaliyotaja hapo juu.

Kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote, ambapo uwongo, ngano za kale na upotoshaji wa historia ni mambo ambayo hayana nafasi tena katika akili za watu. Kutokana na ukweli huu, Taasisi yetu ya Al-Itrah Foundation imeamua kuchapisha kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili kwa madhumuni yake yaleyale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili, ili kuongeza ujuzi wao katika masuala ya dini na ya kijamii.

Tunamshukuru ndugu yetu, Maalim Dhikiri Kiondo (Allah ‘Azza wa Jalla amkubalie amali zake na amweke karibu na Maasumina 14 [a.s.] - Amin) kwa kukubali jukumu hili la kukitarjumi kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.
Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam, Tanzania