Table of Contents

Sura Ya 53: Vita Vya Tabuk

Ile ngome ya kifahari na imara iliyojengwa kandoni mwa chemchemu kwenye barabara itokayo Hijr kwenda Damascus kwenye eneo la mpakani mwa nchi ya Shamu, iliitwa Tabuk. Katika siku zile Shamu ilikuwa moja ya makoloni ya Dola ya Rumi Mashariki (Ugiriki). Mji mkuu wa Dola ya Urumi ya Mashariki ulikuwa ni Constantinople.

Watu wa mipakani mwake walikuwa ni wafuasi wa dini ya Ukristo na machifu wa wilaya walikuwa vibaraka wa mtawala wa Shamu ambaye yeye mwenyewe alikuwa akipokea amri moja kwa moja kutoka kwa mfalme wa Urumi.

Kupenya na kuenea upesi upesi kwa Uislamu kwenye Rasi ya Uarabuni na utekaji wa haraka haraka uliokuwa ukifanywa na Waislamu nchini Hijaz kulikuwa kukionekana kwenye maeneo ya nje ya Hijaz na kulikuwa kukiwatetemesha maadui wao na kuwafanya wafikirie njia na jinsi ya kulikomesha wimbi hili.

Kuanguka kwa Serikali ya Makka, kusilimu kwa machifu wakuu wa Hijaz, ushujaa na kujitoa mhanga kwa wapiganaji wa Kiislamu kulimfanya mtawala wa Urumi kuamua kufanya mashambulio ya kushitukiza dhidi ya Uislamu kwa msaada wa jeshi lenye silaha za kutosha, kwa sababu alihisi kwamba dola yake ilikuwa kwenye hatari kuu kutokana na ushawishi usio kifani na kutanuka kwa Uislamu. Alikuwa akihofia mno kuongezeka kwa nguvu za kijeshi na kisiasa kwa Waislamu.

Katika siku zile, Urumi ilikuwa adui pekee wa Iran na alikuwa anayo nguvu kubwa zaidi ya kisiasa na kijeshi. Ilikuwa ikijivuna sana kutokana na ushindi wa mara kwa mara iliokuwa ikiupata dhidi ya Iran na kushindwa ambako ilikusababisha katika jeshi la Iran.

Jeshi la Urumi lililokuwa na askari 4000 wapanda wanyama na watembeao kwa miguu na walikuwa na silaha za muundo mpya kabisa zilizopatikana kwenye zama zile, walipiga kambi kwenye ukanda wa mpakani mwa Shamu. Makabila yaliyokuwa yakiishi kwenye maeneo ya mpakani (kama vile makabila ya Lakham, Aamilah, Ghassan na Jazaam) nayo yalijiunga nao, na watangulizi wa jeshi lile wakaenda hadi Balqaa.1

Taarifa za kupiga kambi kwa kundi la askari wa Kirumi kwenye ukanda wa mpakani mwa Shamu zilimfikia Mtume (s.a.w.w.) kupitia misafara iliyokuwa ikisafiri baina ya Hijaz na Shamu kuhusiana na biashara. Hakupata njia yoyote nyingine ila kuwajibu washambuliaji kwa jeshi kubwa na kuihami dhidi ya shambulio la kuotea, ile dini iliyokwisha kuenea kwa gharama ya uhai wa watu wapenzi katika Uislamu, na kujitoa mhanga kwake binafsi, na sasa imeshaimarisha mizizi yake, nayo ilikuwa karibuni ienee ulimwenguni kote.

Taarifa hizi zisizopendeza zilimfikia Mtume wakati watu wa Madina walipokuwa bado hawajayavuna mavuno yao yote, na tende zilikuwa karibu kuiva, na Madina na viungani mwake kusema kweli, ilikuwa kwenye makucha ya namna ya njaa. Hata hivyo, kwa watu wachamungu, maisha ya kiroho na ulinzi wa maadili matukufu na Jihad katika njia ya Allah yana kipaupembele zaidi kuliko kitu chochote kingine.

Kuwaita Mashujaa Na Upatikanaji Wa Gharama Za Vita

Kwa kiasi fulani Mtume (s.a.w.w.) alitambua uwezo na uzoefu wa jeshi la adui na alikuwa na uhakika kwamba ukiachilia mbali kule kuhitajia rasilimali ya kiroho (nayo ni imani juu ya Allah, na kupigana kwa ajili ya Allah) ushindi katika vita hivi pia ulitegemea kuwa na jeshi kubwa. Akilizingatia jambo hili aliwatuma watu kwenda Makka pamoja na maeneo yenye kuuzunguka mji ule wa Madina kwenda kuwaita Waislamu watoke na kupigana katika njia ya Allah na kuwaomba Waislamu wenye uwezo kugharimia gharama za vita kwa kutoa Zaka.

Mara tu baada ya tangazo la Mtume (s.a.w.w.) watu 30,000 walitangaza kuwa tayari kwao kushiriki katika vita na kujikusanya kwenye kiwanja cha kupigia kambi cha mji wa Madina (Thaniyyatul Widaa). Gharama za vita zilitolewa kwa kukusanya Zaka. Kati ya hawa watu 30,000, watu 10,000 walikuwa ni askari wapanda wanyama, na wale askari 20,000 waliobakia walikuwa askari waendao kwa miguu. Baadae Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha kwamba kila kabila lijichagulie bendera yake.2

Watu Waliokataa Kushiriki Kwenye Vita

Vita vya Tabuk vilikuwa fursa nzuri zaidi ambamo ndani yake watu wenye kujitoa mhanga na watu wadanganyifu wanaojionyesha tu na wanafiki waliweza kutambulika, kwa sababu kuondoka kwa askari wote kuliamrishwa wakati wa hali ya hewa ilipokuwa na joto sana, na jamii ya kibiashara ya mji wa Madina ilikuwa tayari kuanza kuvuna tende.

Kukataa kwa baadhi yao kushiriki kwenye vita vile kwa kutoa nyudhuru mbalimbali kunalitoa pazia kutoka kwenye nyuso zao halisi, na aya za Qur’ani Tukufu zilifunuliwa zikikilaumu kitendo chao kile. Aya zote hizi zimo kwenye Surat al-Tawbah. Baadhi ya watu walikataa kushiriki kwenye hii Jihad takatifu kwa sababu zifuatazo:

Mtume (s.a.w.w.) alipompendekeza Jadd bin Qays, aliyekuwa mtu mwenye mvuto kwa watu ajiunge na jeshi dhidi ya Warumi, alijibu akisema: “Mimi nina upendo wa kishabiki mkali sana kwa wanawake. Hivyo basi mimi ninachelea kwamba ninaweza nikawaona wanawake wa Kirumi na nikashindwa kujitawala.” Mtume (s.a.w.w.) alipousikia udhuru wake huu wa kitoto, aliamua kumwacha na kuwasiliana na watu wengine juu ya jambo hili. Jadd alilaumiwa na Allah kwenye Aya hii:

وَمِنْهُمْ مَنْ يَقُولُ ائْذَنْ لِي وَلَا تَفْتِنِّي ۚ أَلَا فِي الْفِتْنَةِ سَقَطُوا ۗ وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمُحِيطَةٌ بِالْكَافِرِينَ {49}

“Na miongoni mwao wapo wanaosema: Niruhusu wala usinitie katika fitina. Kwa yakini wao hivyo wamekwisha tumbukia katika fitina. Na hakika Jahannamu imewazunguka.”
(Sura al-Tawbah, 9:49)

Wanafiki: Wale watu waliowatishia Waislamu katika kushiriki kwenye vita vile, na wakasema: “Waarabu hawana uwezo wa kupigana na Warumi na matokeo yake yatakuwa kwamba wale wote watakaoshiriki kwenye vita vile watafungwa kamba na kuuzwa masokoni.3

Kugunduliwa Kwa Kituo Cha Wapanga Makri Mjini Madina:

Yule kiongozi mkuu wa Uislamu (s.a.w.w.) alizipa umuhimu mkubwa taarifa za kijasusi, na nusu ya ushindi wake ulikuwa ni matokeo ya taarifa alizozipata kabla juu ya hali ya maadui na waeneza fitna. Kwa njia hii aliweza kuyakomesha mengi ya matendo yao ya kishetani na mipango iliyo dhidi ya Uislamu tangu mwanzoni kabisa.

Mtume (s.a.w.w.) alipokea taarifa kwamba nyumba ya Myahudi mmoja aliyeitwa Suwaylam imekuwa kituo cha matendo yaliyo kinyume na Uislamu na wanafiki wanakusanyika hapo na kupanga mipango miovu ya kuwazuia Waislamu wasishiriki kwenye hii Jihad takatifu. Hivyo basi, Mtume (s.a.w.w.) aliamua kuwatisha wale wapanga makri katika hali ambayo hawatarudia tena kuwa na fikra za kishetani hapo baadae.

Alimwamrisha Talhah bin Ubaydullah kwenda na baadhi ya masahaba shujaa na kuichoma nyumba ya Suwaylam wakati walipokuwa wakiendesha mkutano wao humo. Kama alivyoelekezwa na Mtume (s.a.ww), Talha aliichoma nyumba ile wakati wapanga makri walipokuwa wakijishughulisha na kuujadili mpango uliokuwa kinyume na Uislamu. Wote wakaikimbia miali ya moto na mmoja wao alijeruhiwa mguu wake. Kitendo hiki kilikuwa na athari mno kiasi kwamba kiliweza kutoa funzo kwa wanafiki kwa siku zijazo.4

Kikundi Cha Watu Waliolia Na Kutoa Machozi:

Baadhi ya masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) ambao walikuwa na shauku kubwa ya kushiriki kwenye hii Jihad takatifu walikuja na kumwomba Mtume (s.a.w.w.) awapatie mahitaji ya safari ile ili waweze kutoa huduma ile takatifu ya kidini. Mtume (s.a.w.w.) alipowaambia kwamba hakuwa na mnyama yoyote wa kupanda ambaye angeliweza kuwapa, walilia sana sana na machozi yalitiririka nyusoni mwao.

Kama walikuwako baadhi ya watu miongoni mwa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) waliopanga makri au waliojishughulisha na vizuizi au kutunga nyudhuru, vilevile walikuwepo wengine miongoni mwao waliokuwa na shauku ya kushiriki kwenye Jihad, ambayo wakati mwingine huwa na gharama ya uhai wa mtu, na kutoshiriki ndani yake kunawafanya walie sana. Kwa mujibu wa istilahi za kihistoria watu hawa wanaitwa ‘wenye kulia’ na Qur’ani Tukufu inataja imani yao kwa maneno haya:

وَلَا عَلَى الَّذِينَ إِذَا مَا أَتَوْكَ لِتَحْمِلَهُمْ قُلْتَ لَا أَجِدُ مَا أَحْمِلُكُمْ عَلَيْهِ تَوَلَّوْا وَأَعْيُنُهُمْ تَفِيضُ مِنَ الدَّمْعِ حَزَنًا أَلَّا يَجِدُوا مَا يُنْفِقُونَ {92}

Wala wale waliokujia ili uwachukue ukasema: Sina kipando cha kukuchukueni. Tena wakarudi na macho yao yanamiminika machozi kwa huzuni ya kukosa cha kutoa.”
(Sura al-Tawbah, 9:92).5

Kundi lingine lilikuwa na watu kama vile Ka’ab, Hilal, na Mararah waliokuwa na imani kamili juu ya Uislamu na vilevile walikuwa na shauku kubwa ya kushiriki katika Jihad, lakini kwa kuwa walikuwa bado hawajavuna mazao yao, waliamua kwamba baada ya kuvuna mazao yao watajiunga na mashujaa wa Uislamu. Katika istilahi ya Qur’ani Tukufu (tazama Surat-Tawbah, 9:118) wao ndio wale wenye kuruka mipaka watatu waliokaripiwa vikali mno na Mtume (s.a.ww) aliporejea kutoka Tabuk na lile karipio walilopata, vilevile lilikuwa mfano kwa wengine.

Sayidna Ali (A.S.) Hakushiriki Kwenye Vita Hivi

Moja ya sifa za Amirul-Mu’minin (a.s.) ni kwamba yeye alifuatana na Mtume (s.a.w.w.) na alikuwa mshika bendera wake kwenye vita vyote vya Kiislamu ila kwenye vita vya Tabuk. Yeye alibakia mjini Madina naye hakushiriki kwenye Jihad hii kwa amri ya Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe.

Mtume (s.a.w.w.) aliuchukua uamuzi huu kwa kuwa alitambua vizuri kwamba, wanafiki na baadhi ya watu kutoka miongoni mwa Waquraishi walikuwa wakiitafuta fursa ya kuleta ghasia na kuipindua ile serikali mpya ya Kiislamu pindi Mtume (s.a.w.w.) atakapokuwa hayupo. Tabuk ilikuwa sehemu ya mbali zaidi aliyoifika Mtume (s.a.w.w.) kuhusiana na vile vita alivyoshiriki.

Alitambua kikamilifu kwamba, ingeliwezekana kwamba wakati akiwa hayupo, vikundi vipingavyo Uislamu vingelifanya ghasia na vingeliwaita washirika wao kutoka sehemu mbalimbali na kuwaunga mkono kwa ajili ya kupata ushindi kwenye mpango wao mwovu.

Hivyo basi, ingawa alimteua Muhammad bin Maslamah kuwa mwakilishi wake mjini Madina wakati wa kuondoka kwake, vile vile alimwambia Sayyidna Ali (a.s.): “Wewe ni mlezi wa Ahlul Bayt na ndugu zangu na kundi la Muhajiriin, na hakuna yeyote mwingine afaaye kwa jukumu hili ila mimi mwenyewe na wewe.”

Kubakia kwa Amirul-Mu’minin mle mjini Madina kuliwaudhi mno wale wapanga makri, kwa sababu walitambua kwamba hawataweza kuutekeleza mpango wao mbele ya Sayyidna Ali (a.s.) ambaye daima alikuwa mwangalifu.

Hivyo basi ili kuthibitisha kwamba Sayyidna Ali (a.s.) anaondoka mjini Madina, waliamua kuunda mpango mwingine na wakaeneza uvumi kwamba Mtume (s.a.w.w.) alimtaka Ali ashiriki kwenye Jihad lakini Ali alikataa kushiriki kwenye vita hivi takatifu kutokana na safari ndefu na hali ya hewa yenye joto kali.

Ili kuwapinga watu hawa, Sayyidna Ali (a.s.) alimuona Mtume (s.a.w.w.) (nje ya kidogo ya mji wa Madina ambapo Mtume alipiga kambi ili kusubiri jeshi lote likamilike) na akaliweka suala lile mbele ya Mtume (s.a.w.w.). Wakati ule Mtume (s.a.w.w.) aliitamka ile kauli yake ya kihistoria ambayo ni uthibitisho wa dhahiri wa Uimamu wa Sayyidna Ali (a.s.) na Ukhalifa wake wa mara tu baada ya kufariki dunia Mtume (s.a.w.w.).

Alisema: “Ewe Ndugu yangu! Rejea Madina, kwa kuwa hakuna afaaye zaidi kuuhifadhi utukufu na cheo cha mji wa Madina zaidi yangu mimi mwenyewe na wewe. Wewe ni mwakilishi wangu miongoni mwa Ahlul Bayt na ndugu zangu. Je, wewe hufurahi ninapokwambia kwamba uhusiano wako na mimi ni sawa na ule uliokuwepo baina ya Harun na Musa, ila tu kwamba hatakuja Mtume baada yangu? Kama vile alivyokuwa Harun kwamba alikuwa mrithi wa papo kwa papo wa Nabii Musa, wewe nawe ni mrithi na Khalifa wangu. “6

Jeshi La Uislamu Laelekea Tabuk

Desturi ya Mtume (s.a.w.w.) ilikuwa kwamba anaposafiri kwenda kuwaadhibu watu waliokinza kuendelea kwa Uislamu, au waliodhamiria kuwashambulia Waislamu, au waliokuwa na mipango miovu dhidi yao, hakuidhihirisha nia na madhumuni yake kwa maafisa askari wake na alilifanya jeshi lipitie njia isiyopitiwa mara kwa mara.

Hivyo, hakuwaruhusu maadui wayatambue malengo yake na akawajia maadui wakiwa wao wenyewe hawatambui.7 Hata hivyo, ili kuwafukuzilia mbali majeshi ya kirumi yaliyokusanyika kwenye mpaka wa Shamu kwa lengo la kuzishambulia nchi za Kiislamu, alilifanya lengo lake lieleweke dhahiri kwa wale wote wahusikao, siku ileile ambayo ukusanyaji wa majeshi ulipotangazwa.

Madhumuni ya kufanya hivyo yalikuwa kwamba wale Mujahidiin (mashujaa) watambue umuhimu wa safari ile na taabu zipasazo kukabiliwa mle njiani, na ili waweze kuchukua masurufu yatoshelezayo.
Aidha, ili kuliimarisha jeshi la Uislamu, Mtume (s.a.w.w.) alilazimika kuomba msaada kutoka kwa watu wa makabila ya Tamim, GhatfAn na Tayyi, hawa walikuwa wakiishi kwenye sehemu za mbali kutoka Madina. Kwa sababu hii Mtume (s.a.w.w.) aliandika barua kwa machifu wa makabila haya na vilevile alimwandikia barua ‘Ataab bin Usayd, yule Gavana kijana wa Makka, na kuyaita makabila pamoja na watu wa Makka washiriki kwenye Jihad hii takatifu.8

Kwa kuwa upanuzi wa ule mwito wa watu wote haukuweza kuwa siri. Hivyo ilikuwa muhimu kwamba, aweze kuyafanya mahitaji ya safari kabisa kwa wale machifu wa makabila ili waweze kutayarisha masurufu yatoshelezayo na wanyama wa kupanda kwa ajili ya Mujahidiin wao.

Jeshi Lafanya Gwaride Mbele Ya Mtume (S.A.W.W)

Siku ya kuondoka kwa jeshi la Waislamu ikafika. Siku ile Mtume (s.a.w.w.) alivikagua vikosi kwenye makao makuu ya jeshi ya mjini Madina. Mandhari kubwa mno ya gwaride lile lililokuwa likifanywa na watu waaminifu na wenye kujitoa mhanga ambao ili kuyafikia malengo yao, wamechagua kupata taabu na kifo badala ya starehe na faida za kidunia, kwa shauku na imani iliwavutia waliokuwapo pale.

Wakati wa kuondoka, Mtume (s.a.w.w.) aliwahutubia askari ili kuziimarisha nyoyo zao, na kuwaeleza lengo lake katika kule kuamrisha watu wote kwenda vitani, kisha askari waliendelea wakielekea kwenye njia iliyoainishwa.

Kisa Cha Malik Bin Qays

Baada ya kuondoka kwa jeshi, Maliki bin Qays alirejea Madina kutoka kwenye safari yake. Hali ya hewa ilikuwa ya joto kali mno siku ile. Aliona kwamba upweke ulitawala kila mahali mle mjini Madina na akapata kutambua kuhusu kule kuondoka kwa askari wa Uislamu. Wakati ule ule, aliwasili kwenye bustani yake na akaona kwamba mkewe mzuri amemjengea kibanda.

Aliutupia jicho uso wenye kuvutia wa mkewe na vilevile akakikodolea macho kidogo chakula na maji alichokitayarisha yule mwanamke kwa ajili yake. Baada ya hapo aliyafikiria matatizo machungu ya Mtume (s.a.w.w.) na masahaba wake waliokuwa wakienda kufanya Jihad katika njia ya Allah na kukikabili kifo katika hali ya hewa ya joto kiasi kile.

Kisha akaamua kutokutumia yale maji na kile chakula alichokitayarisha mkewe wala kile kibanda alichokijenga mkewe, bali kumpanda mnyama wake upesi sana, na kwenda kujiunga na jeshi la Uislamu upesi iwezekanavyo. Hivyo, upesi sana alimgeukia mkewe na kumwambia:

“Si sahihi hata kidogo kwamba mimi nipumzike chini ya kivuli cha kibanda hiki pamoja na mke wangu na kula chakula kitamu, na kunywa maji yaliyopoa na matamu, ambapo bwana wangu anakwenda kwenye Jihad katika joto kali kiasi hiki. Hapana jambo hili haliafikiani na uadilifu na kanuni za urafiki, na imani na uaminifu haviniruhusu kufanya hivi.”

Aliyasema maneno haya akaokota masurufu machache hivi kwa ajili ya ile safari na akaenda zake. Alipokuwa njiani alikutana na ‘Umar bin Wahab, ambaye yaonekana alikawia nyuma ya lile jeshi la Uislamu, na wote wawili wakamkuta Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa Tabuk.9

Mtu huyu hakuzipata baraka za kufuatana na Mtume (s.a.w.w.) pale mwanzoni, lakini hatimaye alizitoa huduma zake katika njia hii tukufu kwa njia ya kujitoa mhanga kwake. Kwa upande mwingine, wako watu ambao mlangoni pao bahati njema inabisha hodi, lakini wanakaa mbali nayo kwa kisingizio cha ukosefu wa kufaa na ufanisi na hatimaye wakajitupa wenyewe kwenye uadui na maangamizi. Kwa mfano, Abdullah bin Ubayy, chifu wa wanafiki, alikita hema kwenye sehemu ya kambi ya Mtume (s.a.w.w.) ili kwamba aweze kushiriki kwenye Jihad hii akifuatana na Mtume (s.a.w.w.).

Kwa vile alikuwa adui katili wa Uislam, alibadilisha mawazo wakati jeshi lilipokuwa tayari kuondoka na akarejea Madina pamoja na watu waliokuwa wakimuunga mkono ili aweze kufanya ghasia pale wakati Mtume (s.a.w.w.) akiwa hayupo. Mtume (s.a.w.w.) hakumjali hata kidogo, kwa sababu aliutambua unafiki wake na hakudhania kushiriki kwake kwenye Jihadi ile kuwa na faida yoyote ile.

Tabu Za Njiani

Jeshi la Uislamu lilikabiliwa na matatizo makubwa lilipokuwa njiani kutoka Madina kwenda Shamu na ni kwa sababu hii kwamba lilipewa jina la Jayshul usrah (Jeshi la Tabu). Hata hivyo, imani na juhudi viliyashinda matatizo yote hayo nao waliyakaribisha matatizo yote yaliyo wakabili.

Lile jeshi la Uislamu lilipoifikia nchi ya Wathamud Mtume (s.a.w.w.) aliufunika uso wake kwa nguo kwa sababu ya upepo wenye joto lichomalo na uvumao sana na akaipita sehemu ile kwa haraka sana na akawaambia masahaba zake: “Utazameni mwishilizo wa uhai wa Wathamud waliopasika na ghadhabu ya Allah kutokana na ukaidi na uasi wao; na kumbukeni kwamba hakuna muumini wa kweli ambaye angelifikiria kwamba mwishilizio wa uhai wake hautakuwa kama wa watu wale. Utulivu mzito kama wa kifo wa sehemu hii, na magofu ya nyumba zilizoharibiwa ambayo yameangukiwa na kimya kizito ni funzo kwa umati nyingine.”

Baada ya hapo Mtume (s.a.w.w.) aliwaamrisha askari wale wasinywe maji ya sehemu ile au kutayarisha chakula au mkate kutokana nayo, na kwamba wasijaribu hata kufanya udhuu nayo, na kama kwa bahati mbaya walishatayarisha chakula au kukanda unga kwa maji yale basi wawape wanyama wale chakula hicho.

Kisha lile jeshi la Uislamu liliendelea na safari likiwa chini ya uongozi wa Mtume (s.a.w.w.) na ilipopita sehemu ya usiku, walikifikia kisima ambacho Ngamia wa Nabii Swaleh alinywea maji. Walipoifikia sehemu ile, Mtume (s.a.w.w.) alitoa amri ya kwamba watu wote wapige kambi pale na kupumzika.

Amri Za Tahadhari

Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akiitambua vizuri sumu ya upepo uvumao kwa nguvu na kimbunga kikali cha eneo lile, ambacho wakati mwingine huwazidi watu na ngamia na kuwafukia chini. Hivyo basi, aliamrisha kwamba magoti ya ngamia yafungwe na mtu yeyote yule asitoke eneo la kambi wakati wa usiku akiwa yu peke yake.

Uzoefu ulithibitisha kwamba ile amri ya tahadhari aliyoitoa Mtume (s.a.w.w.) ilikuwa na faida kubwa, kwa sababu watu wawili wa kabila la Bani Saidah waliikiuka amri hii na wakalitoka eneo la kambi wakiwa peke yao wakati wa usiku, na matokeo yake yakawa kwamba ile dhoruba kali ilimkosesha hewa mmoja wao na kumvurumisha mwingine kwenye kilima. Mtume (s.a.w.w.) alipata habari za matukio haya, naye aliwahuzunikia sana wale watu waliopoteza maisha yao kutokana na utovu wa nidhamu. Hivyo basi, aliwaomba tena wale askari kudumisha nidhamu. 10

Abbad bin Bishr, aliyekiongoza kikosi kilichohusika na usalama na ulinzi wa jeshi la Uislamu, alimwarifu Mtume (s.a.w.w.) kwamba askari wa Uislamu wameingia kwenye matatizo kutokana na upungufu wa maji, na hifadhi yote ya maji yaelekea kumalizika hivi karibuni. Hivyo baadhi yao waliwachinja ngamia wao wa thamani mno ili kuweza kuyatumia maji yaliyokuwamo matumboni mwao, na wengine walijiweka kwenye mapenzi ya Allah, nao walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa rehma za Allah.

Allah Mwenye nguvu zote ambaye amemwahidi ushindi Mtume Wake, alimsaidia tena yeye na masahaba wake waaminifu. Mvua kubwa ilinyesha na wote wakapata maji ya kunywa yenye kuwatosheleza. Zaidi ya hapo, wale walioteuliwa kuhifadhi vyakula, pamoja na jeshi zima waliweza kuhifadhi maji kiasi walichohitaji.

Habari Za Ghaibu Za Mtume (S.A.W.W)

Haukaniki ukweli uliopo kwamba, kama inavyoelezwa dhahiri kwenye Qur’ani Tukufu,11 Mtume (s.a.w.w.) aliweza kutoa taarifa juu ya mambo ya ghaibu ambayo watu wengine hawakuwa wakijua chochote. Hata hivyo, elimu ya Mtume (s.a.w.w.) ilikuwa na kikomo, na ilitegemea kile alichofunzwa na Allah. Hivyo basi, iliwezekana kwamba asitambue mambo fulani fulani. Kwa mfano, aliweza kupoteza pesa au kupoteza funguo ya nyumba na akashindwa kuiona. Hata hivyo, wakati fulani aliweza kutoa taarifa za ghaifu juu ya mambo yaliyokuwa ya siri zaidi na yaliyotatanisha zaidi na kuwaacha watu wakiwa wanashangaa. Sababu ya kupanda na kushuka huku ni ile tuliyoitaja hapo juu. Yaani kila Allah alipopenda alimpa Mtume taarifa za mambo yahusianayo na ulimwengu wa ghaibu.

Wakati jeshi lilipokuwa njiani ngamia wa Mtume (s.a.w.w.) alipotea na baadhi ya masahaba walikwenda kumtafuta. Wakati huo huo mmoja wa wanafiki aliamka na kusema: “Anasema kwamba yu Mtume wa Allah na anatoa taarifa juu ya mbingu, lakini inashangaza kwamba hajui aliko ngamia wake!” Mtume (s.a.w.w.) akapata kulitambua jambo hili na akaifafanua hali ile kwa njia ya kauli fasaha. Alisema: “Ninajua tu yale aniambiayo Allah. Hivi karibuni tu Allah ameniarifu aliko ngamia wangu. Yuko jangwani kwenye bonde hili na hili. Hatamu yake imejifunga kwenye mti na kumzuia kutembea. Nendeni mkamlete.”

Watu fulani walikwenda upesi upesi kwenye sehemu ile na wakamwona yule ngamia akiwa kwenye hali ile aliyoieleza Mtume (s.a.w.w.).12

Taarifa Nyingine Ya Siri

Ngamia wa Abu Dharr alishindwa kutembea na hivyo Abu Dharr aliachwa nyuma na lile jeshi la Kiislamu. Alisubiri kwa muda fulani lakini hakupata matokeo yoyote. Hatimaye alimwacha yule ngamia na akakibeba chakula mgongoni mwake na akaanza kutembea ili aende akajiunge na lile jeshi la Uislamu mapema iwezekanavyo. Wale askari wa Uislamu walikuwa wamepiga kambi mahali fulani kama walivyoamrishwa na Mtume (s.a.w.w.) nao walikuwa wakipumzika.

Mara kwa ghafla waliliona kwa mbali umbo la mtu aliyekuwa akipita njia ile na mzigo mzito mgongoni mwake. Sahaba mmoja alimwarifu Mtume (s.a.w.w.) hali ile. Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Huyo ni Abu Dharr. Allah amsamehe Abu Dhar! Anatembea peke yake, atakufa peke yake na atafufuliwa peke yake.”13
Matukio ya baadae yalithibitisha kwamba alivyotabiri Mtume (s.a.w.w.) vilikuwa sahihi kabisa; kwa sababu Abu Dharr alifariki katika hali ya kuhuzunisha, mbali kutoka kwenye makazi ya watu, kwenye jangwa la Rabzah akiwa peke yake na binti yake tu akiwa karibu naye.14

Jeshi La Uislamu Lawasili Kwenye Eneo La Tabuk

Jeshi la Uislamu lilifika kwenye eneo la Tabuk mwanzoni mwa mwezi wa Sha’aban, mwaka wa 9 Hijiriya. Hata hivyo, hakuna dalili ya jeshi la Kirumi iliyoweza kuonekana pale. Inaonekana kwamba wale makamanda wa jeshi la Warumi waliutambua ukubwa wa jeshi la Waislamu na ujasiri wao na kujitoa mhanga kwao kusiko na kifani, ambako mfano wake mdogo tayari wameshauona kwa karibu zaidi katika Vita vya Muuta, hivyo waliona kwamba inafaa kulirudisha tena jeshi lao katika mipaka ya nchi yao wenyewe. Kwa kufanya hivyo, walitaka kukana kivitendo kwamba walipeleka majeshi dhidi ya Waislamu, na walitaka kutoa dhana ya kwamba katu hawakupata kufikiria kuanzisha mashambulizi, na taarifa zozote za aina hiyo ni dhana tu, na kwa kufanya hivyo walitaka kuthibitisha kutopendelea kwao matukio yaliyokuwa yakitokea Uarabuni.

Katika hali hii, Mtume (s.a.w.w.) aliwakusanya maafisa wake watukufu na akiutekeleza msingi uliodumishwa wa Uislamu, ule wa kushauriana, aliwataka ushauri kama waendelee na kuingia kwenye nchi ya adui au warejee Madina. Matokeo ya ule ushauriano wa kijeshi ni kwamba, iliamuliwa kwamba lile jeshi la Uislamu lilipata taabu nyingi sana lilipokuwa likisafiri kuja pale Tabuk, hivyo lirudi Madina kwenda kuihuisha nguvu yake. Aidha, kwa kuifanya safari ile, Waislamu watakuwa wamekwisha kulifikia lengo lao kuu ambalo lilikuwa ni kulitawanya jeshi la kirumi.

Warumi walitishwa mno na kuogopa, kiasi kwamba kwa kipindi kirefu sana hawakufikiria kuwashambulia Waislamu, na hivyo basi kwenye kipindi kile usalama wa Uarabuni kutoka kwenye upande wa Kaskazini ulipatikana.

Ili kukilinda salama cheo cha Mtume (s.a.w.w.) na kudhihirisha kwamba maoni yao yangeliweza kukataliwa au kuondolewa; wanakamati wa halmashauri ya ushauriano wa kijeshi, vile vile waliongezea sentensi ifuatayo: “Kama umeamrishwa na Allah Mwenye nguvu zote kuendelea, basi tuamrishe, sisi nasi tutakufuata.”15

Mtume (s.a.w) akasema: “Hakuna amri yoyote iliyofunuliwa kutoka kwa Allah, na kama amri ingelipokelewa kutoka Kwake, nisengelikutakeni ushauri. Hivyo basi, kutokana na heshima ya halmashauri ya ushauri, nimeamua kurejea Madina kutoka mahali hapa.”

Watawala walioyakalia maeneo ya mipakani mwa Shamu na Hijaz na ushawishi ulioungana miongoni mwa watu wao, wote walikuwa Wakristo na ulikuweko uwezekano kwamba siku moja jeshi la Warumi lingeliweza kuwatumia hawa watawala wa kienyeji na kuishambulia Hijaz kwa msaada wao. Hivyo basi, ilikuwa muhimu kwa Mtume (s.a.w.w.) kufanya mikataba ya kutoshambuliana na watawala hawa ili aweze kujipatia usalama mzuri zaidi.

Yeye mwenyewe aliwasiliana na watawala hawa wa mipakani waliokuwa wakiishi kwenye maeneo ya jirani na Tabuk, na kufanya nao mikataba ya kutoshambuliana kwa masharti fulani fulani. Ama kuhusu maeneo yaliyoko mbali kutoka Tabuk alipeleka wawakilishi wake kwa watawala wahusika ili usalama ulio bora zaidi uweze kupatikana kwa ajili ya Uislamu.

Vilevile aliwasiliana na mtawala wa Aylah, Azri’aat na Jarbaa’ na mapatano ya kutoshambuliana yalifanyika baina ya vikundi hivi. Aylah ni mji wa pwani uliokuwako kwenye pwani ya Bahari ya Shamu na uko umbali fulani kutoka Shamu.
Mtawala wake aliitwa Yohana mwana wa Rawbah, alikuja kutoka kwenye mji wake mkuu hadi pale Tabuk akiwa amevaa msalaba wa dhahabu shingoni mwake. Alimpa Mtume (s.a.w.w.) zawadi ya nyumbu mweupe na akadhihirisha utii wake kwake. Mtume (s.a.w.w.) alipendezewa na ishara yake ya urafiki na vilevile yeye naye alimpa zawadi.

Yule mtawala aliamua kubakia kwenye dini ya Ukristo na kulipa Jizayh (kodi) ya dinari elfu tatu kila mwaka na vilevile kumpokea kila Mwislamu apitaye kwenye eneo lile la Aylah. Ulifanyika mkataba wenye masharti yafuatayo na ukasainiwa na pande zote mbili: “Huu ni mkataba wa kutoshambuliana kutoka kwenye upande wa Allah na Mtume Wake, Muhammad kwa ajili ya Yohana na wakazi wa Aylah. Kufuatana na mkataba huu njia zao zote za usafiri, iwe ni kwa bahari au kwa nchi kavu, na watu wote wa Shamu, Yaman na visiwa, yeyote yule awaye pamoja nao atakuwa kwenye hifadhi ya Allah na Mtume Wake. Hata hivyo, kama yeyote miongoni mwao atazikiuka sheria, basi utajiri wake hautamwokoa kutokana na adhabu. Njia zote za bahari na za nchi kavu zitakuwa wazi kwa ajili yao nao wanayo haki ya kuzipita.”16

Mkataba huu waonyesha kwamba kama taifa fulani lilishirikiana na Waislamu kwa njia ya amani, lilipewa njia za kulifanikisha jambo hilo, na vilevile lilithibitishiwa usalama wake.

Vile vile Mtume (s.a.w.w.) alifanya mikataba na watu wa mipakani kama vile watu wa Azri’aat, na Jarbaa’ ambao nchi zao zilikuwa na umuhimu mkubwa wa kimikakati, na hivyo kuthibitisha kuwapo kwa usalama wa nchi za Kiislamu kutoka kwenye ule upande wa Kaskazini.

Khalid Bin Walid Apelekwa Duwmatul Jandal

Ukanda wenye watu wengi na miti ya kijani, maji yatiririkayo na ngome madhubuti iliyokuwa kiasi cha ligi 50 (kilometa 240) kutoka Shamu ulikuwa ukiitwa Duwmatul Jandal.17 Katika siku zile Mkristo mmoja aliyeitwa Okaydar bin Abdil Malik Kindi alitawala hapo. Mtume (s.a.w.w.) alichelea kwamba katika hali ya jeshi la Kirumi kuanzisha tena mashambulizi, yule mtawala wa Duwmatul Jandal angeliweza kuwasaidia na hivyo kuuhatarisha usalama wa Uarabuni.

Kwa sababu hii aliona kwamba ni muhimu kupata faida kiasi iwezekanavyo kutokana na jeshi alilonalo, na kukipeleka kikosi chini ya uamiri jeshi wa Khalid bin Walid kwenda kutisha watu wa ukanda huo tulioitaja. Khalid alifika karibu na Duwmatul Jandal akifuatana na askari wapanda wanyama na akaiotea ile ngome.

Katika usiku wa mbalamwezi Okaydar alitoka nje ya ngome ile akifuatana na nduguye aliyeitwa Hassan wakienda kuwinda. Walikuwa bado hawajakwenda mbali sana kutoka kwenye ile ngome pale walipokutana uso kwa uso na wale askari wa Khalid. Katika mapambano madogo tu yaliyotokea baina ya hivyo vikundi viwili, nduguye Okaydar aliuwawa, na watu wake wakakimbilia mle ngomeni na wakalifunga lango la ile ngome, na Okaydar akakamatwa.

Khalid alimwahidi kwamba kama wale wakazi wa ile ngome wakilifungua lango lake kwa amri yake na kuzisalimisha silaha zao kwenye jeshi la Uislamu atamsamehe na atampeleka kwa Mtume (s.a.w.w.).

Okaydar alitambua kwamba Waislamu walikuwa wakweli na walizitimiza ahadi zao. Hivyo basi, aliamrisha kwamba lile lango la ngome lifunguliwe na zile silaha zisalimishwe kwa Waislamu. Silaha zilizokuwamo ngomeni mle zilikuwa ni deraya 400, panga 500 na mikuki 400. Khalid aliondoka kwenda Madina pamoja na ngawira zile na Okaydar naye alifuatana naye. Kabla ya kuwasili Madina, Khalid alimpelekea Mtume (s.a.w.w.) mharuma wa Okaydar uliotarizwa kwa zari ambao yeye Okaydar alikuwa akijitandia mabegani mwake kama wafanyavyo wafalme.
Macho ya watu wenye tamaa za kiulimwengu yalipumbazwa katika kuutazama mharuma ule, lakini Mtume (s.a.w.w.) alionyesha kutoupendelea kabisa na akasema: “Mavazi ya watu watakaokwenda Peponi yatakuwa yenye kushangaza zaidi.”

Okaydar alikutana na Mtume (s.a.w.w.). Alikataa kusilimu, lakini alikubali kuwalipa Waislamu Jizyah na ukafanyika mkataba baina yake na Mtume (s.a.w.w.). Baada ya hapo alimpa zawadi zenye thamani na akamteua Abbad bin Bashir kumrejesha Duwmatul Jandal kwa usalama.18

Tathmini Ya Safari Ya Tabuk

Kwa matokeo ya safari hii yenye kuchosha ni kwamba, Mtume (s.a.w.w.) hakukutana uso kwa uso na adui na hakuna mapigano yaliyotokea, lakini faida fulani zilipatikana.19

Kwanza kabisa, safari hii iliharakisha upatikanaji wa heshima ya jeshi la Waislamu na Mtume (s.a.w,w) aliwezeshwa kutia ukuu na nguvu zake nyoyoni mwa watu wa Hijaz na watu wa mpakani mwa Shamu. Matokeo yake ni kwamba, marafiki pamoja na maadui wa Uislamu walipata kutambua kwamba nguvu yake ya kijeshi inakua sana kiasi cha kuweza kuzikabili nguvu na kuzitishia na zikaogopa.

Majinai na uasi vimekuwa sifa ya pili ya makabila ya Kiarabu. Hata hivyo kule kuitambua nguvu ya kijeshi la Kislamu kuliweza kutowapinga Waislamu na kuasi dhidi yao. Hivyo basi, baada ya kurejea kwa Mtume (s.a.w.w.) Madina, wawakilishi wa makabila ambayo hadi pale yalikuwa bado hayajasalimu amri yalianza kuja Madina kwa wingi sana na kutangaza kuhusu utii wao kwa serikali ya Kislamu na kusilimu, kiasi kwamba mwaka wa tisa wa Hijiriya ulianza kuitwa ‘mwaka wa wawakilishi.’

Pili, kwa kufanya mapatano mbalimbali na watu wa mipakani mwa Hijaz na Shamu, Waislamu walithibitishiwa usalama wa ukanda ule, nao walitosheka kwamba machifu wa makabila haya hawatashirikiana na jeshi la kirumi.

Tatu, kwa kuifanya safari hii yenye taabu, Mtume (s.a.w.w.) aliufanya utekaji wa Shamu kuwa wa rahisi zaidi. Aliwafanya makamanda wa jeshi lile kuyazoea matatizo ya ukanda ule na aliwafunza mbinu za kivita dhidi ya madola makubwa ya siku zile.

Hivyo basi, ukanda wa kwanza kutekwa na Waislamu baada ya kufariki dunia kwa Mtume (s.a.w.w.) ulikuwa ni nchi ya Damascus na Shamu. Zaidi ya hapo, kwa kupeleka jeshi kubwa kiasi kile, waumini wa kweli waliweza kuainishwa kutokana na wanafiki, na maelewano mema yalidumishwa miongoni mwa Waislamu.

Wanafiki Waunda Makri Dhidi Ya Mtume (S.A.W.W.)

Mtume (s.a.w.w.) alikaa Tabuk siku kumi20 na akarejea Madina baada ya kumtuma Khalid kwenda Duwmatul Jandal. Wanafiki kumi na wawili ambao nane kati yao walitoka miongoni mwa Waquraishi na wale wanne waliosalia walikuwa wakazi wa Madina, waliamua kumshitua ngamia wa Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa juu ya njia nyembamba ya juu ya mlima iliyokuwako kwenye njia baina ya Madina na Shamu ili kumfanya Mtume (s.a.w.w.) aangukie bondeni.
Jeshi la Uislamu lilipoifikia sehemu ya kwanza ya njia hii, Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Yeyote yule apendaye kulipita jangwa anaweza kupita kwa sababu jangwa ni pana sana.” Hata hivyo, yeye alipanda kwenye ile njia nyembamba wakati Hudhayfah alikuwa akimwendesha ngamia wake kwa nyuma na Ammar alikuwa akizishika hatamu zake kwa mbele.

Alipokigeuzia nyuma kichwa chake aliona kwenye mwanga wa mwezi kwamba watu waliokuwa wamewapanda wanyama walikuwa wakimfuata. Ili kuhakikisha kwamba wasiweze kutambulika walikuwa wamezifunika nyuso zao na walikuwa wakizungumza kwa kunong’onezana. Mtume (s.a.w.w.) alichukia sana na akawapa changamoto na akamwamrisha Hudhayfah awageuze ngamia wao kwa fimbo yake.

Mwito wa Mtume (s.a.w.w.) uliwaogofya mno nao walitambua ya kwamba ameitambua makri yao. Hivyo basi, upesi sana walirudi nyuma na kwenda kujiunga na askari wengine. Hudhayfah anasema: “Mimi niliwatambua kutokana na alama za ngamia wao na nilimwambia Mtume (s.a.w.w.): “Ninaweza kukuambia ni nani hawa ili uwaadhibu.” Lakini Mtume aliniambia kwa sauti ya upole nisiifunue siri yao, kwa kuwa ulikuwapo uwezekano kwamba wakatubia.

Vilevile aliongeza kusema kwamba: “Kama nikiwaadhibu, wale wasio Waislamu watasema kwamba sasa Muhammad amepata mamlaka na amewafanya masahaba wake mwenyewe kuwa mawindo.”21

Vita Baridi

Hakuna mandhari iliyokuwa kuu zaidi ya mandhari ya kurejea kwa jeshi lililoshinda, linaporejea nchini mwake, na hakuna chenye kumfurahisha askari zaidi ya ushindi dhidi ya adui, ushindi unaoihami heshima yake na kuuthibitisha usalama na uhai wake. Ilitokea kwamba mambo yote mawili yalijidhihirisha na yaliweza kuonekana wakati wa kurejea kwa jeshi lililoshinda la Uislamu, kutoka Tabuk.

Baada ya kumaliza ile safiri baina ya Tabuk na Madina, lile jeshi la Uislamu liliwasili Madina kwa utukufu mkubwa. Wale askari wa Uislamu walifurahi sana na fahari ya ubora ilionekana kwenye mwendo na mazungumzo yao. Vilevile sababu ya fahari hii ilikuwa dhahiri, kwa sababu walilifanya taifa kuu lirudi nyuma katika mapambano ya kivita, ambalo ni ile nguvu ambayo hapo mwanzo ilimshinda adui wake aliyekuwa na nguvu zaidi (Iran). Na pia Waislamu wamewatiisha watu wa mipakani mwa Shamu na Hijaz.

Kwa hakika watu hawa wamejipatia heshima kwa kule kuwazidi nguvu adui na ni dhahiri kwamba walikuwa na haki ya kujivuna dhidi ya wale wengine waliobakia mjini Madina bila ya sababu ya haki. Hata hivyo, ulikuwapo uwezekano kwamba namna hii ya fikira, na huku kurejea kwa ushindi vingeliweza kujenga fahari isiyostahili akilini mwa watu wenye akili finyu, na ikawa ni matusi kwa baadhi ya wale watu waliobakia mjini Madina kwa sababu za haki lakini nyoyo zao zilikuwa pamoja na wale askari kule kwenye uwanja wa vita, nao walishirikiana kwa uaminifu kwenye neema na msiba wao.

Hivyo Mtume (s.a.w.w.) alilihutubia lile jeshi la Uislamu lilipokuwa mahali fulani karibu na Madina lilipotua kwa kitambo hivi, kwa maneno haya: “Huko Madina wako baadhi ya watu wanaokuungeni mkono kwenye safari hii na wakawa pamoja nanyi hatua kwa hatua.”

Mtume (s.a.w.w.) aliulizwa ni vipi jambo hili lingaliweza kufikiriwa kwamba wale watu waliobakia mjini Madina nao pia walishiriki kwenye safari ile pamoja na lile jeshi. Mtume (s.a.w.w.) alijibu akisema: “Wao, ingawa walikuwa wakipendelea kushiriki kwenye jukumu hili takatifu (Jihadi), hawakuweza kujiunga kutokana na sababu njema.”22

Kwa njia ya hotuba hii fupi Mtume (s.a.w.w.) alidokezea juu ya mmoja wa mipango elekevu wa Uislamu na akawaongoza watu kwenye ukweli wa kwamba nia njema na fikira nyoofu huchukua nafasi ya amali za uchamungu, na wale watu waliokosa kutenda amali njema kutokana na kukosa kwao nguvu au mali, wanaweza kuwa washirika wa wale wengine katika malipo ya kiroho na kufidiwa kwa ajili ya amali njema. Kama Uislamu unataka matengenezo ya nje, una shauku kuu ya matengenezo ya kiroho na usafi wa fikira, kwa sababu chanzo halisi cha matengenezo ni kuzitengeneza imani na namna ya fikira, na matendo yetu yote hutokana na fikira zetu.

Hivyo Mtume (s.a.w.w.) aliiondoa fahari isiyo ya haki ya wale Mujahidiin na akaihakikisha nafasi ya wale watu wanaosameheka, lakini kuanzia muda uleule alidhamiria kwamba atatoa adhabu ya mfano kwa wale waasi wasiokuwa na sababu ya haki wawezayo kuitoa. Tukio lifuatalo ni mfano wa kitendo cha aina hii.

Siku ambayo jeshi lote lilitangaziwa kuondoka mjini Madina, Waislamu watatu ambao ni Hilal, Ka’ab na Murarah walimjia Mtume (s.a.w.w.) na wakaomba kwamba wasamehewe kushiriki kwenye Jihad ile. Sababu waliyoitaja ilikuwa kwamba mazao yao mashambani na bustani zao yalikuwa bado hayajaiva kabisa. Vilevile walimwahidi Mtume (s.a.w.w.) kwamba watakapomaliza kuvuna baada ya siku chache hivi, watajiunga na jeshi la Waislamu huko Tabuk.

Wale watu wasio tofautisha baina ya faida za kimaada na uhuru wa kisiasa, ni watu wasio na uoni wa mbali wanaozichukulia anasa za huu ulimwengu zenye kupita kuwa sawa na maisha yenye heshima,
awezayo kuyaishi mtu chini ya bendera ya uhuru wa kiakili, kisiasa na kiutamaduni, na wakati mwingine mtu huyapenda zaidi maisha tuliyoyataja kwanza kuliko haya ya pili.

Baada ya kurejea Madina kutoka Tabuk Mtume (s.a.w.w.) alilazimika kuwaadhibu watu hao ili kuyazuia maradhi haya yasiingie kwenye akili za watu wengine. Si hivyo tu kwamba watu hawa hawakushiriki kwenye Jihad lakini vile vile hawakuitimiza ile ahadi waliyomwahidi Mtume (s.a.w.w.). Walikuwa bado wangali wakijishughulisha na biashara zao na katika kujilimbikizia utajiri wakati kwa ghafla taarifa za kurejea kwa Mtume (s.a.w.w.) kwa ushindi zilipoenea mjini Madina.

Watu hawa watatu, ili kufanya masahihisho kwa tabia zao mbaya na kuwahadaa Waislamu wengine, walikwenda kumlaki Mtume (s.a.w.w.) kama walivyofanya wengineo wote na wakatoa heshima zao kwake na kumpongeza; lakini yeye hakuwasikiliza. Alipofika Madina aliwahutubia watu miongoni mwa wale wote waliokuwa wakishereheka na hoi hoi, na jambo la kwanza alilolisema lilikuwa hili: “Enyi watu! Watu hawa watatu walizitweza sheria za Kiislamu pia hawakuitimiza ahadi yao waliyoniahidi. Walizipendelea faida za kidunia badala ya yale maisha ya heshima chini ya bendera ya Uislamu. Hivyo basi hamna budi kukata uhusiano nao.”

Idadi ya waasi ilifikia tisini lakini kwa vile wengi wao walikuwa wa kundi la wanafiki, na haikuweza kutegemewa kutoka kwao kwamba watajiunga kwenye Jihad dhidi ya adui, shinikizo lilielekezwa kwa hawa Waislamu watatu, ambao Murarah na Hilal, walikuwa wameshiriki kwenye Vita vya Badr na waliheshimiwa miongini mwa Waislamu.

Sera yenye hekima ya Mtume (s.a.w.w.) ambayo ni sehemu muhimu yenye kukamilisha Uislamu ilikuwa na athari za ajabu. Biashara na shughuli za waasi zilisimama kabisa. Biashara zao hazikupata wanunuzi kwenye soko. Ndugu zao wa karibu zaidi wakakata uhusiano nao na wakaacha hata kuzungumza nao au kuwatembelea. Mgomo wa kijamii walioufanya watu dhidi yao ulishusha mno moyo na juhudi za watu hawa kiasi kwamba ile ardhi ya Madina iliyokuwa pana haikuweza kuwa chochote zaidi ya kuwa kitundu kwao.23

Hivyo ilikuwa ni bahati njema kwamba watu hawa watatu, kwa akili na uoni wao waliweza kutambua kwamba maisha kwenye mazingira ya Kiislamu hayakuwezekana bila ya kushirikiana na Waislamu kwa moyo wote, na maisha ya watu wachache mno wenye kwenda kinyume na walio wengi yasingeliweza kudumu muda mrefu, hasa pale inapokuwa kwamba lile kundi la walio wachache ni la watu waasi, fitna, wagomvi na wenye mfundo.

Kwa upande mmoja wameitwa watoe maelezo yao na kwa upande mwingine ile nguvu ya kimaumbile na silika inawavutia tena kwenye itikadi sahihi, nao wakatubia kwa Allah kwa kile kitendo chao cha woga. Allah Naye aliwasamehe na akamwarifu Mtume Wake (s.a.w.w.) kule kuwasamehe Kwake. Hivyo basi, amri ihusuyo kufutwa kwa mgomo ule ilitangazwa upesi sana.24

Tukio La Masjid Dhiraar

Kwenye Rasi ya Uarabuni Madina na Najraan zilichukuliwa kuwa ni maeneo mapana na vituo vikuu vya Ahlul-Kitaab (Watu wa Kitabu). Hivyo basi, baadhi ya Waarabu wa makabila ya Aws na Khazraji walikuwa na mwelekeo na dini ya Uyahudi na Ukristo, nao walikuwa wafuasi wa dini hizi.

Kwenye Zama za Ujahilia Abu Aamir baba yake Hanzalah, yule shahidi maarufu wa Vita vya Uhud, alikuwa na mwelekeo mkubwa na Ukristo na alikuwa mtawa. Uislamu ulipoanza mjini Madina na kuimeza jamii ndogo ya dini, Abu Aamir alichukizwa sana na akaanza kushirikiana kwa uaminifu na wanafiki wa makabila ya Aws na Khazraji. Mtume (s.a.w.w.) aliyatambua matendo yake yenye uharibifu na akataka kumkamata, lakini alikimbia kutoka Madina akaenda Makka na kisha akaenda
Taa’if, na baada ya kutekwa kwa Taa’if alikwenda Shamu. Kutoka pale alianza kuuongoza mtandao wa ujasusi wa wanafiki.

Kwenye moja ya barua zake, Abu Aamir aliwaandikia marafiki zake hivi: “Jengeni msikiti kwenye kijiji cha Quba’a mkabala na msikiti wa Waislamu. Kusanyikeni hapo nyakati za sala, na kwa kujifanya kana kwamba mnasali, jadilianeni na pangeni mipango dhidi ya Uislamu na Waislamu.”

Kama walivyo wale maadui wa Uislamu wa siku hizi, Abu Aamri naye alitambua kwamba kwenye nchi ambayo dini ilikuwa imeshamiri, njia iliyo bora zaidi ya kuiangamiza ni kulitumia jina la dini ile, na dini inaweza kudhuriwa zaidi kwa kulitumia jina lake kuliko njia yoyote nyingine. Alijua vizuri sana kwamba Mtume (s.a.w.w.) asingeliwaruhusu wanafiki wajijengee kituo kwa hali yoyote ile, isipokuwa pale walipokipa kituo kile rangi ya kidini na wakajenga sehemu ya kukutania kwa ajili yao kwa jina la msikiti.

Mtume (s.a.w.w.) alipodhamiria kwenda Tabuk wawakilishi wa wanafiki walimjia na kumwomba awaruhusu kujenga msikiti kwenye eneo lao, kwa kusema kwamba katika usiku wa giza au inaponyesha mvua wazee na wagonjwa wao hawakuweza kwenda mwendo mrefu tangu kwenye nyumba zao hadi kwenye Masjid Qubaa. Mtume (s.a.w.w.) hakuwapa jibu lolote lile la kukubali au la kukataa, na aliahirisha kutoa uamuzi wa mwisho juu ya jambo hili hadi baada ya kurejea kutoka kwenye ile safari iliyokusudiwa.25

Baada ya Mtume (s.a.w.w.) kutoka, wale wanafiki walichagua mahali na wakakijenga hadi wakakimaliza upesi iwezekanavyo kile kituo chao cha kuundia maovu, kwa kukipa jina la msikiti. Katika siku ambayo Mtume (s.a.w.w.) alirejea Madina walimwomba afanye sherehe ya kuifungua sehemu ile ya ibada kwa kusimamisha rakaa chache za sala mahali hapa.

Wakati huo huo Malaika Mkuu Jibril alishuka na kumweleza Mtume (s.a.w.w.) kuhusu hali ya jambo lile la Masjid Dhiraar kwa kuwa ulijengwa ili kujenga mfarakano miongoni mwa Waislamu.26 Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha Masjid Dhiraar ibomolewe kabisa, boriti zake zichomwe na takataka zake zitupwe hapo kwa muda fulani.27

Kubomolewa kwa Masjid Dhiraar kulikuwa ni pigo kali kwa wanafiki na baada ya hapo kikundi chao kilivunjika na Abdullah bin Ubay, mtu pekee aliyekuwa akiwaunga mkono naye alikufa baada ya miezi miwili tangu kupiganwa kwa Vita vya Tabuk.

Tabuk ilikuwa ni vita vya mwisho vya Uislamu ambavyo Mtume alishiriki. Baada ya vita hivi Mtume hakushiriki kwenye vita nyingine yoyote ile.

 • 1. Tabaqaatil-Kubra, juz. 2, uk. 165.
 • 2. Tabaqaatil-Kubra, Juz. 2, uk. 166.
 • 3. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 3, uk. 1003.
 • 4. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 517.
 • 5. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk 518. Maghaazil-Waaqidi, juz. 3, uk. 992-993.
 • 6. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 520; Bihaarul An’war, Juz. 21, uk. 207.
 • 7. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 3, uk. 990.
 • 8. Bihaarul-Anwaar, Juz. 21, uk. 244.
 • 9. Siiratu Ibh Hisham, Juz. 2, uk. 520. Lakini Waaqidi amelihusisha tukio hili kwa mabadiliko kidogo, na Abdulah bin Khaythamah.
 • 10. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 3, uk. 152.
 • 11. Allah (s.w.t) amesema: “(Yeye ndiye) Mjuzi wa siri, na wala Hamdhihirishii yeyote yule siri Zake ila kwa Mtume Aliyemchagua; na kisha Humwekea mlinzi mbele yake na nyuma yake.” (Sura al Jinn, 72:27)
 • 12. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 523.
 • 13. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 525.
 • 14. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 3, uk. 1000.
 • 15. Siiratu Ibn Halabi, Juz. 3, uk. 161.
 • 16. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 526; Siiratu Ibn Halabi, Juz.3, uk. 160; na Bihaarul-An’waar, Juz. 21, uk. 160.
 • 17. Duwmah ilikuwa umbali wa maili 10 (Kilomita 16) kutoka Madina.
 • 18. Tabaqaatil-Kubra, Juz. 2, uk. 146; Bihaarul-An’waar, Juz. 2, uk 246.
 • 19. Mtume (s.a.w.w.) alikaa Tabuk siku ishirini. Siku moja baada ya kusali sala ya asubuhi alitoa hotuba moja iliyokuwa ndefu, yenye ufasaha wa lugha na yenye mafunzo. Baada ya hapo aliyanukuu maneno ya hotuba ile (Maghaazil-Waaqidi, juz. 3, uk. 1014-1015).
 • 20. Muda wa kukaa kwa Mtume (s.a.w.w.) kule Tabuk umeelezwa kwamba ni siku ishirini. (Siiratu Ibn Hisham, Juz.3, uk. 527; Tabaqaati Ibn Sa’ad, Juz. 2, uk. 168).
 • 21. Maghaazil- Waaqidi, Juz. 3, uk. 1042-1043; Bihaarul-An’waar, juz. 21, uk. 247; Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 162.
 • 22. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 163; Bihaarul-An’waar, juz. 20, uk. 219.
 • 23. Maneno ya sentensi hii ni nukuu itokayo kwenye Qur’ani ambako imesemekana kwamba “Kana kwamba haikuwako nafasi kwenye nchi yote (hii) iliyo pana ya kuweza kuwaficha au kwenye nafsi zao kuweza kuwafariji.” (Surah, al-Tawbah, 9:118).
 • 24. (Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 165 na Bihaarul-Anwaar, Juz. 10, uk. 119). Hii njia ya Mtume (s.a.w.w.) yenye mafunzo ilikuwa mfano kwetu sisi Waislamu, kuhusiana na kikundi cha watu walio wachache kwenye jamii. Upinzani wa aina hiyo ungeliweza kuondolewa tu kwa uaminifu, dhamira na umoja. Waaqidi ametoa maelezo marefu zaidi ya hawa watu watatu. (Tazama Maghaaz, Juz. 3, uk. 1045-1056).
 • 25. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 3, uk. 1046.
 • 26. Aya 107-110 za Surah al-Tawbah zilifunuliwa kuhusiana na Masjid Dhiraar.
 • 27. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 530; Bihaarul-An’waar, juz. 20, uk. 253.