read

Ahlul-Bayt Katika Aya Ya Mubahalah

Kwa kweli mapambano kati ya safu mbili, haki na batili kwenye uwanja wa vita ni jambo gumu, lakini ni gumu zaidi ikiwa katika medani ya Mihrabu, pindi kila mmoja anapong’amua mwenyewe binafsi kuwa yupo mbele ya Mjuzi wa ghaibu, na wanamfanya kuwa hakimu na mwamuzi kati yao, kwa hiyo katika hali kama hii hatofanikiwa mwenye shaka au wasiwasi moyoni mwake.
Ndio, inawezekana mtu akawa mpiganaji shupavu katika medani ya mapambano, kwa mantiki hiyo tunaona Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) katika mapambano yake na makafiri alikuwa amuita kwenda kwenye jihadi kila mwenye uwezo wa kubeba silaha japo awe mnafiki. Lakini ilipobadilika aina ya mapambano kutoka yale ya vita na kuwa ya dua na kulaaniana na manaswara, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) hakumwita yoyote kwenye aina hii mpya ya mapambano miongoni mwa maswahaba wake, kwa sababu katika ngazi hii hawezi kuja mbele ya safu ila mwenye moyo uliosalimika, uliotoharika kwa kuwa mbali na uchafu na dhambi, nao ni chaguo lililochujwa. Na mfano wa watu kama hawa hawawi wengi miongoni mwa watu, wao aghlabu huwa wachache, isipokuwa tu wao ni watu bora miongoni mwa walio ardhini.

Basi Ni Nani Hawa Chaguo Lililochujwa?

Pindi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alipofanya mjadala na wanavyuoni wa kinaswara kwa ambalo ni jema, hakupata kutoka kwao ila ukafiri, upinzani na kuasi, na hapakuwa na njia nyingine ila ni kumsihi Mwenyezi Mungu, nako ni kila mmoja kati yao aombe kwa alilokuwa nalo na waijaaliye laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo. Muda huo amri ya Mwenyezi Mungu ilikuja:

فَمَنْ حَاجَّكَ فِيهِ مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ فَقُلْ تَعَالَوْا نَدْعُ أَبْنَاءَنَا وَأَبْنَاءَكُمْ وَنِسَاءَنَا وَنِسَاءَكُمْ وَأَنْفُسَنَا وَأَنْفُسَكُمْ ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَلْ لَعْنَتَ اللَّهِ عَلَى الْكَاذِبِينَ {61}

“Na mwenye kukuhoji katika hilo baada ya kukujia elimu sema: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, wanawake wetu na wanawake wenu, na nafsi zetu na nafsi zenu, halafu tumsihi Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu na tuijaalie laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya waongo.” (Surat Aali Imran: 61).

Hapo makasisi waliitikia pendekezo jipya la Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ili vita viwe vya kuamua hatima kati yao, hivyo basi makasisi walikusanya watu wao walio mahsusi kuiandalia siku hii.

Na siku ya ahadi ilipowadia na umma ulijikusanya, manaswara walitangulia wakiwa na imani kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) naye pia atakuja na kundi la maswahaba wake na wanawake wake, yaani wakeze. Ikajitokeza Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) akija mbele kwa hatua thabiti akiwa na nyota chache katika Ahlul-Bayt, Hasan akiwa kuliani kwake na Husein kushotoni kwake, Ali na Fatima wakiwa nyuma yake.

Pindi manaswara walipoziona nyuso zinazochomoza kwa mwanga wa ucha-Mungu, wao walitetemeka kwa hofu, wote walimgeukia askofu mkubwa wao: “Ewe Abu Haritha waonaje suala hili?” Askofu aliwajibu: “Naziona sura lau kwazo mtu atamwomba Mwenyezi Mungu ili jabali ling’oke kutoka mahali pake angeliondoa.” Mshangao wao ulizidi, na Askofu alipohisi hivyo akasema: ‘’Je hamumwoni Muhammad mwenye kuinua mikono yake akiangalia (mikono) inavyomjibu. Kwa haki ya Masihi akitamka neno hatutarejea kwa ahali wala mali.”1

Hapo basi waliamua kurudi na kutoendelea na dua. Waliridhia udhalili na kulipa jizya2. Kupitia hao watano Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) aliwashinda hao manaswara na aliwarudisha hali wakiwa wamenyongea. Kwa minajili hiyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) akasema:
‘’Naapa kwa Ambaye nafsi yangu ipo mkononi Mwake, kwa hakika adhabu ni yenye kuwakurubia watu wa Najran, lau si msamaha wake wangepatilizwa na kuwa tumbili na nguruwe na wangekolezewa moto katika bonde na Mwenyezi Mungu angeifutilia mbali Najran na watu wake hata ndege mtini, na mwaka haungetimia wangepatilizwa manaswara wote.”

Lakini kwa nini Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) aliwaleta hawa wanne tu na yeye mwenyewe, wakawa waliohudhuria ni watano, wala hakuwaleta maswahaba wake na wakeze?

Ili kujibu hilo kwa neno moja, ni kuwa: Ahlul-Bayt ni viumbe walio bora mno kwa Mwenyezi Mungu baada ya Mtume, na ni wasafi mno na wako tohara sana, na sifa hizi hawakustahiki nazo watu wengine wasio kuwa wao, sifa ambazo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amezithibitisha kwa Ahlul- Bayt katika Aya ya tohara kama ilivyotangulia.

Kwa minajili hiyo tunamkuta Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) katika kuitekeleza Aya hii ni jinsi gani anavyogeuza mtazamo wa umma ili uielekee daraja ya Ahlul-Bayt. Kwa hiyo anaitafsiri kauli ya Mwenyezi Mungu: ‘Watoto wetu’ kwa maana ya Hasan na Husein (a.s.). Na ‘Wanawake wetu’ kwa maana ya Sayyida Fatima Zahrau (a.s.). Na ‘Nafsi zetu’ kwa maana ya Ali (a.s.). hiyo ni kwa sababu Imam haingii pamwe na wanawake wala pamwe na watoto, kwa hiyo kunabaki kuingia kwake ni katika neno ‘Na nafsi zetu, na ibara ya ‘Nafsi zetu’ ingekuwa mbaya lau tu wito ungekuwa umeelekezwa kwenye dhati yake tu.

Basi ni vipi aiite nafsi yake? Hilo latiliwa nguvu na kauli ya Mtume (s.a.w.w):

“Mimi na Ali ni kutoka mti mmoja na watu wengine waliobaki wanatoka miti mingi tofauti.

Hivyo ikiwa Imam Ali (a.s.) ni nafsi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kwa hiyo yeye ana haki ile aliyonayo Mtume (s.a.w.w) katika uongozi na kuwa walii juu ya waislamu, isipokuwa daraja moja, nayo ni daraja ya unabii kama alivyosema Mtume (s.a.w.w), alivyonakiliwa na Sahih Bukhari na Sahih Muslim: “Ewe Ali nafasi yako kwangu ni sawa na ya Haruna kwa Musa, isipokuwa hakuna Nabii baada yangu.”3

Kwa kweli kuitolea kwetu dalili Aya hii si mahali hapa, ila tu ni katika kubainisha Ahlul-Bayt ni watu gani, na Alhamdulillahi hapajakuwa na tofauti kuwa Aya hii iliteremka kuwahusu watu wa Kishamia. Na kuna habari na Hadithi katika uwanja huu.

Muslim na Tirmidhiy wote wawili wameieleza riwaya hii katika mlango wa fadhila za Ali (a.s.), kutoka kwa Saad bin Abu Waqqas akisema: “Ilipoteremka Aya hii: “Sema: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, wanawake wetu na wanawake wenu” Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alimwita Ali, Fatima, Hasan na Husein, akasema: “Ewe Mwenyezi Mungu hawa ndio Ahlul-Bayt wangu.”4

Na Suyutiy, Al-Hakim na Al-Bayhaki wameitaja. Na kauli yake: “Hawa ndio Ahlul-Bayt wangu.” Yajulisha kuwaainisha Ahlul-Bayt ni hawa wanne.

  • 1. Al-Durul-Manthur cha Suyutiy, Juz. 2, Surat Al Imran: 61.
  • 2. Kodi inayolipwa na makafiri wanaoishi katika nchi za kiislamu.
  • 3. Rejea Bukhari kitabu cha fadhila. Sahih Muslim kitabu cha fadhila za sahaba. Na Musnad Juz.3, riwaya namba 1463.
  • 4. Sahih Muslim, Juz.4, Uk. 360. Chapa ya, Isa al’Halabiy, na Juz.15, chapa ya Misri Uk. 176. Sharhun–Nawawiy. Sahih Tirmidhiy Juz. 4 Uk. 293. Hadithi namba 3085 Juz.5 Uk. 301 Hadith namba 3808. Al-Mustadrak Alas-Swahihayni Juz.3, Uk. 150.