read

Hadithi Hii Ni Dalili Ya Uimamu Wa Ahlul-Bayt

Hadithi kujulisha ustahiki wa uimamu kwa Ahlul-Bayt ni katika mambo yaliyo wazi na dhahiri mno kwa kila mwenye insafu, kwa kuwa inafidisha wajibu wa kuwafuata katika itikadi na hukumu na rai na kutofanya kinyume nao, kwa kauli au kitendo, kwa sababu kazi yoyote itakayotoka nje ya wigo wao itazingatiwa kuwa imetoka nje ya Qur’ani, na kwa hilo inakuwa iko nje ya dini.

Na wao kwa hilo wanakuwa ndio kipimo thabiti ambacho kwacho hujulikana njia iliyonyooka na njia iliyo sawa, kiasi kwamba uongofu hauwi ila kwa njia yao na upotovu hauwi isipokuwa kwa kufanya kinyume na wao: “Mkishikamana na viwili hivi hamtopotea: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu.”

Kwa kuwa kujiambatanisha na Qur’ani maana yake ni kufanya kwa mujibu wa yaliyo ndani yake, yaani kuamrika na amri zake na kujikataza makatazo yake, na ni hivyo hivyo inakuwa katika kushikamana na Kizazi. Hiyo ni kulingana na kanuni ya: Kipatikanacho kwa sharti hakitopatikana ila kwa kutimia sharti.

Kama ambavyo nomino katika (viwili) inarejea kwenye Kitabu na Kizazi. Sidhani mwarabu mwenye kupewa ufahamu wa lugha ya kiarabu japo kidogo atakuwa kinyume na hilo.

Kwa mujibu huo inakuwa kuwafuata Ahlul-Bayt baada ya Mtume (s.a.w.w) ni wajibu kama ilivyo kuifuata Qur’ani ni wajibu, na hilo liko mbali na maudhui ya ‘Je Ahlul-Bayt ni nani?’ kwa kuwa huu ni udadisi wa baadaye, la muhimu hapa ni kuthibitisha kuwa amri, katazo, kufuatwa, na kuigwa ni haki ya Ahlul-Bayt, na wao ni mfano wa kuigwa. Ama kuainisha utambulishi wao kwenyewe kupo nje ya wigo wa mazungumzo haya, kama wasemavyo wanavyuoni wa misingi ya sheria: “Hakika kadhia haithibitishi maudhui yake.” Kwa hiyo kwa dharura tija inakuwa Ahlul- Bayt wao ndio makhalifa baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).
Na kauli yake (s.a.w.w): “Hakika mimi nawaachieni kati yenu” ni tamko linalobainisha wazi kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) amewafanya makhalifa na ameusia umma uwafuate, na amesisitiza hilo kwa kauli yake (s.a.w.w): “Angalieni jinsi mtakavyonifuata katika viwili hivi.” Hivyo ukhalifa wa Qur’ani uko wazi, na ukhalifa wa Ahlul-Bayt hauwi ila kwa uimamu wao. Na kwa hivyo Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi cha Mtume wake (s.a.w.w) ndio sababu inayofikisha kwenye radhi za Mwenyezi Mungu, kwa sababu wao ni kamba ya Mwenyezi Mungu ambayo Mwenyezi Mungu ametuamuru kushikamana nayo: “Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu.....” (Sura Ali Imran: 103)

Na Aya hapa ni jumuishi haijaainisha na kuiwekea mpaka kamba ya Mwenyezi Mungu, au lolote liwezalo kubainika kutoka humo ambalo ni wajibu kushikamana nalo. Ndipo Sunna ikaja na Hadithi ya Vizito Viwili na hadithi zingine, kubainisha kuwa kamba ambayo ni wajibu tushikamane nayo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu pamwe na kizazi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).

Na hilo limesemwa na kundi la wafasiri: Ibnu Hajar amewataja katika kitabu chake Swawaiqul-Muhriqah katika mlango wa yale yaliyoteremshwa kuwahusu Ahlul-Bayt. Rejea huko.

Na Al-Qunduziy ameitaja katika kitabu chake Yanabiul-Mawaddah amesema katika kauli ya Mwenyezi Mungu (s.w.t): “Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu.....”: “Tha’alabiy ameandika kutoka kwa Aaban bin Taghlabi kutoka kwa Jafar Swadiq (a.s.) akasema: ‘Sisi ndio Kamba ya Mwenyezi Mungu ambayo Mwenyezi Mungu Mwenye enzi na utukufu amesema: “Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu wote na wala msifarakane.” (Surat Aali Imran: 103)

Na pia ameandika mwandishi wa kitabu Al-Manaqib kutoka kwa Said bin Jubair kutoka kwa Ibnu Abbas kutoka kwa wawili hawa, amesema: ‘Tulikuwa kwa Mtume (s.a.w.w.), punde si punde alikuja bedui na akasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nimekusikia unasema: Shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu, hivyo kamba ya Mwenyezi Mungu ni ipi, ambayo tushikamane nayo?” Hapo Nabii (s.a.w.w) aliupiga mkono wake juu ya mkono wa Ali na akasema: ‘Shikamaneni na huyu, ndiyo kamba madhubuti ya Mwenyezi Mungu.”1

Ama usemi wake (s.a.w.w): “Hawatofarakana mpaka wanijie kwenye bwawa.” Yajulisha sababu kadhaa:

Kwanza: Kuthibiti umaasumu kwao wao, kwa kuwa kuambatana kwao na Kitabu ambacho hakiwezijiwa na batili mbele yake wala nyuma yake, ni dalili ya elimu yao ya yaliyomo ndani ya Kitabu na kuwa wao hawafanyi kinyume na Kitabu kwa kauli wala kitendo. Kwani ni wazi kuwa kutokea lolote kwao kinyume na Kitabu sawa iwe kwa makusudi au kusahau ni kuthibitisha kufarakana kwao na Qur’ani, na hali Hadithi yaeleza wazi kutofarakana kwa wawili hawa mpaka wafike kwenye bwawa wakiwa pamoja, vinginevyo itakuwa ni kumkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), kama ambavyo ufahamu huu unaungwa mkono na dalili kutoka katika Qur’ani na Sunna. Tuahirishe utafiti katika hilo mpaka mahali pengine.

Pili: Kwa kweli (Lan) inafidisha: “Abadan”, hivyo inakuwa kushikamana na wao wawili – Kitabu na Kizazi – ni kizuizi cha upotovu daima na abadan, na hilo halitimii ila kwa kushikamana na wote wawili pamoja, sio kushikamana na mmoja wao peke yake kama ilivyotangulia, na usemi wa Mtume (s.a.w.w) katika riwaya ya Tabaraniy:
“Msiwatangulie mkaja mkaangamia na wala msiwaelimishe kwa kuwa wao wana elimu zaidi yenu.” unasisitizia maana hii.

Tatu: Kubakia kwa kizazi pembeni ya Kitabu mpaka Siku ya Kiyama, hivyo hapana zama itakuwa bila ya wao. Na maana hii ameileta karibu Ibnu Hajar ndani ya Swawa’iq yake: “Na katika hadithi za himizo la kushikamana na Ahlul-Bayt kuna ishara ya kutokatika kwa mwenye kustahiki miongoni mwao kushikamana naye mpaka Siku ya Kiyama, kama ambavyo Kitabu kitukufu nacho ni hivyo hivyo. Kwa ajili hiyo wao ni amani kwa watu wa ardhini, kama itakavyokuja, na hilo linashuhudiwa na habari zilizotangulia: ‘Katika kila kizazi cha umma wangu kina waadilifu miongoni mwa Ahlul-Bayt wangu.’ Kisha mwenye haki zaidi ya kushikamana naye miongoni mwao ni imamu wao, na mwanachuoni wao Ali bin Abu Talib, kutokana na tuliyotanguliza miongoni mwa kuzidi elimu yake na fatwa zake za kina.”2

Nne: Kama ambavyo yajulisha kupambanuka kwao na elimu yao ya ufafanuzi wa sheria, na hivyo ni kwa sababu ya kuambatana kwao na Kitabu ambacho hakiachi dogo wala kubwa, kama alivyosema (s.a.w.w): “Wala msiwafundishe kwani wao ni wajuzi mno kuliko ninyi.”

Muhtasari: Hapana budi apatikane lau mmoja kutoka Ahlul-Bayt katika kila zama mpaka Kiyama kitakapowadia, kauli yake na kitendo chake hakihitilafiani na Qur’ani, ili asiwe mbali nayo, na maana ya hatofautiani na Qur’ani kwa kauli na kitendo ni kuwa yeye ni maasumu kikauli na kivitendo, na ni wajibu kumfuata kwa kuwa yeye ni dhamana ya kutoingia kwenye upotovu. Na maana hii haisemwi isipokuwa na Shia, kwa sababu wao wanasema kuwepo Imam kutoka miongoni mwa Ahlul-Bayt, ambaye ni maasumu dhidi ya kukosea na kuteleza, ambaye ni wajibu kumtawalisha na kumtambua, hiyo ni kulingana na maana hii ya kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu: “Ambaye atafariki dunia bila ya kumjua Imamu wa zama zake atakuwa amekufa kifo cha kijahili (yaani muda kabla ya Uislamu). Na imejulisha maana hii kauli yake (s.w.t): “Siku ambayo tutawaita kila watu kupitia Imamu wao.”

  • 1. Al-Yanaabiul-Mawaddah, Uk.118. Manshuratu muasasatul’a’alamiy. Beirut- Lebanon.
  • 2. Swawaiq Uk. 151.