read

Hoja Dhidi Ya Hadithi Ya “Vizito Viwili”

Ibnu Al-Jawziy ameitia dosari katika kitabu chake Al-Ilalul-Mutanaahiya Fil-Hadithil-Waahiyah. Alipoitaja Hadithi ya kushikamana na vizito viwili: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu” Amesema: “Hadthi hii haisihi. Ama kuhusu Atiya, ni kuwa Ahmad, Yahya na wengine wamemfanya kuwa yu dhaifu. Ama Ibnu Abdul-Qudus, Yahya amesema: ‘Si chochote yeye ni Rafidhi khabithi.’ Ama Abdullahi bin Daahir, Ahmad na Yahya wamesema: ‘Si kitu, haandiki toka kwa mtu aliye na kheri.’”

Kujibu Hoja Husika:

Hadithi ya vizito viwili haiishii kwenye sanad hii, kwa kweli imeelezwa kwa sanad nyingi kama ilivyotangulia.

Kwa hakika Muslim ameieleza katika Sahihi yake, kwa njia nyingi, ni wazi kuwa kuieleza Muslim riwaya hii japo kwa njia moja yatosha kuithibitishia ukweli wake, hili halina tofauti kati ya waislamu masunni.

Kama alivyoieleza At-Tirmidhiy ndani ya Sahihi yake kwa njia nyingi. Kutoka kwa Jabir, na Zayd bin Arqam, Abu Dharr, Abu Said na Hudhayfa.

Maneno ya Ibnu Al-Jawziy mwenyewe ndani ya kitabu chake Al- Mawdhuuati Juz.1, Uk. 99 tamko lake ni kama ifuatavyo: “Ukiona Hadithi imetoka nje ya usajili wa kiislam (Al-Muwatau, Musnad ya Ahmad, Sahihayni, Sunan Abi Daud, Tirmidhiy na mfano wa hizo) basi ichunguze, ikiwa kuna mfano wake katika vitabu Sahih (Sahih-Sita) na vizuri basi jambo lake lipo karibu mno…” Na yeye kwa usemi huu anajipinga mwenyewe kwani imeelezwa Hadithi hii katika vitabu ambavyo ameviita usajili wa kiislam, kama ilivyokwisha kupitia!

Kwa kweli maneno ya Ibnu Al-Jawziy kumhusu Atiyah hayakubaliki, kwa kuwa Ibnu Saad amemhesabu kuwa ni mwaminifu wa hadithi, kwani Ibnu Hajar Al-Asqalani amesema: “Ibnu Saad amesema: ‘Atiyyah alitoka pamoja na Ibnu Al-Ash’ath, ndipo al-Hajjaj alipomwandikia Muhammad bin al-Qasim amwambie amtukane Ali, na endapo hatofanya hivyo mpige mijeledi mia nne na nyoa ndevu zake. Alimwita, na alikataa kumtukana Ali, hivyo alitekeleza hukumu ya al-Hajjaj kwake.

Hatimaye alikwenda Khurasani alibakia huko mpaka Umar bin Habiir alipokuwa liwali wa Iraq, akaenda Iraq na alibaki huko mpaka alipokufa mwaka wa mia na kumi, alikuwa mwaminifu inshaallah na alikuwa na Hadithi njema.”1

Yajulikana kuwa Ibnu Saad ni miongoni mwa Nawasibu2 ambao wanawafanyia uadui Ahlul-Bayt kiasi cha kumfanya Imam Jafar bin Muhammad Swadiq (a.s.) kuwa ni dhaifu. Hivyo kule kumfanya kwake Atiyah kuwa ni mwaminifu kunamtosha hasimu.

Kwa kweli Atiyah ni katika wapokezi wa Ahmad bin Hanbali, na Ahmad haielezei riwaya ila kutoka kwa waaminifu, kama ijulikanavyo, hivyo Ahmad alieleza riwaya nyingi mbalimbali kutoka kwake. Hivyo basi kunasibisha kuwa Ahmad alimuona Atiya kuwa ni dhaifu ni uwongo wa dhahiri. Kwani Taqiyu al-Sabakiy amesema: “Ahmad - Mwenyezi Mungu amrehemu - alikuwa haelezi riwaya ila kutoka kwa mwaminifu. Hasimu amesema wazi (anamkusudia Ibnu Taymiyya) hilo katika kitabu alichokitunga kumpinga al-Bakriy baada ya kurasa kumi za kitabu hicho, amesema: ‘Kwa hakika wazungumziao Jarhu na Taadiil miongoni mwa wanavyuoni wa Hadith wako aina mbili: Miongoni mwao kuna ambaye haelezei hadithi ila kutoka kwa aliye mwaminifu kwake, kama vile Malik, na Ahmad bin Hambal.....’

Hivyo basi kwa usemi huu hasimu ametutosheleza kazi ya kubainisha kuwa Ahmad huwa hapokei ila toka kwa mwaminifu, hapo basi hatobaki wa kumkebehi katika Hadithi.”3

Sibtu Ibnu Al-Jawziy anathibitisha uaminifu wa Atiya: Kwa kweli amebainisha uaminifu wa Atiyyah na amekanusha kumfanya kuwa yeye ni dhaifu, pale aliposema baada ya kuleta kauli ya Nabii (s.a.w.w) kumhusu Ali (a.s.): “Si halali kwa yeyote asiye kuwa mimi au wewe awe na janaba ndani ya msikiti huu.” “Kama itasemwa Atiyyah ni dhaifu, watasema na dalili ya udhaifu wa Hadithi ni kuwa Tirmidhiy amesema: ‘Na nimeisimulia Hadithi hii au ameisikia kutoka kwangu Muhammad bin Ismail – yaani Bukhari – naye akajitenga nayo.’

“Najibu: Kwa kweli Atiyyah al-Aufiy amekuwa mpokezi kutoka kwa Ibnu Abbas na kwa Swahaba na alikuwa mwaminifu. Ama kauli ya Tirmidhiy kutoka kwa Bukhariy alijitenga nayo kwa sababu ya kauli yake (s.a.w.w): “Simhalalishii ila aliye tohara, si mwenye hedhi wala mwenye janaba.” Na imepatikana kutoka kwa Shaafiy: ‘Ni halali kwa mwenye janaba kuvuka msikitini.’ Na kutoka kwa Abu Hanifa: ‘Si halali mpaka aoge, kwa sababu ya kuwepo kwa tamko linaloharamisha. Na Hadithi ya Ali huchukuliwa kuwa yeye ilikwa ni mahsusi kwake hilo, kama ilivyokuwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), kwani vitu kadhaa vilikuwa mahsusi kwake.”4

Nasibisho la Ibnu Al-Jawziy kuwa Yahya bin Muiyn kamdhaifisha Atiyyah halikubaliki, kwa sababu ya nukuu ya Dawriy kutoka kwa Ibnu Muiyn kuwa yeye (Atiyyah) ni mtu mwema. Bila shaka al-Hafidh Ibn Hajar amesema katika wasifu wa Atiyyah usemi ambao tamko lake ni: “Dawriy amesema kutoka kwa Ibnu Muiyn: ‘Ni mwema.”’ Hivyo basi kikaporomoka alichokinasibisha Ibn al-Jawziy kwa Yahya bin Muiyn.5 Zingatia.

Na linalojulisha kutoijua kwa Ibnul Jawziy Hadithi ya Vizito Viwili ni dhana yake kuwa kwa kumdhaifisha Atiyyah peke yake ni hoja tosha ya kuidhaifisha Hadithi ya Vizito Viwili.

Hali yajulikana kuwa kuthibiti kwa uaminifu wa Atiyyah au kuthibiti kwa udhaifu wake hakuitii dosari Hadithi ya Vizito Viwili. Kwa kuwa hadithi ya Atiyya aliyoieleza kutoka kwa Abu Said pia Abu Tufail ameieleza kutoka kwa Abu Said, naye Abu Tufail yuahesabika katika tabaka la Swahaba.

Lau tukiachana na hilo ni kuwa kwa kweli usahihi wa Hadithi ya Vizito Viwili hautegemei riwaya ya Abu Said sawa iwe kwa njia ya Atiyya au Abu Tufail.

Na hata tukikubali tu kimjadala kuwa riwaya ya Abu Said ni dhaifu katika njia zake zote, hilo haliidhuru kitu Hadithi hii, kwa sababu ya riwaya zake na njia zake kuwa nyingi na mbalimbali.

Kumkanusha Ibnu Al-Jawziy Kule Kumdhaifisha Kwake Ibnu Abdul- Qudus:

1. Ama kumtia dosari kwake Abdullah bin Abdul-Qudus hakukubaliki, kwa sababu al-Hafidh Muhammad bin Isa amemthibitisha kuwa ni mwaminifu. Al-Hafidh Al-Muqdisiy amesema katika wasifu wa Abdullah aliyetajwa: “Ibnu Udiyi amenena kutoka kwa Muhammad bin Isa kuwa yeye amesema: ‘Yeye ni mwaminifu.”6

Na al-Hafidh Ibn Hajar al-Asqalaniy amesema: “Na imeelezwa kutoka kwa Muhammad bin Isa kuwa yeye amesema: ‘Ni mwaminifu.”’7

Na Muhammad bin Isa yeye ni kama alivyosema al-Hafidh Dhahabi katika wasifu wake: “Abu Hatim amesema: ‘Ni mwaminifu mwenye kuaminika. Sijamuona katika wasimulizi wa hadithi mwenye kuhifadhi zaidi milango kuliko yeye. Na Abu Daud amesesma: Ni mwaminifu.”’

2. Muhammad bin Hayyan amemuweka miongoni mwa waaminifu, na akasema Ibnu Hajar kwenye wasifu wake: “Ibnu Hayyan amesema yu katika waaminifu.”8

3. Haythamiy amenakili kwenye Majmauz-zawaaid, amesema: “Bukhari na Ibnu Hayyan wamemzingatia kuwa ni mwaminifu.”

4. Asqalaniy amesema kwenye wasifu wake: “Bukhari amesema: ‘Yeye katika asili ni mkweli ila tu ni kwamba ni mpokezi kutoka kwa kaumu ya watu dhaifu.’”

Kwa hiyo Bukhari kumshakia Ibnu Abdul-Qudus baada ya kumthibitisha kuwa ni mpokezi wa madhaifu, shaka hiyo haielekezwi kwenye hadithi hii, kwa sababu Ibnu Abdul’Qudus ameieleza Hadithi ya Vizito Viwili ambayo ameileta Ibnu Al-Jawziy kutoka kwa Aamash, naye ni mwaminifu.

5. Abdullah bin Abdul-Qudus ni miongoni mwa wapokezi wa Bukhari katika Sahihi yake katika maelezo ya ziada, kama ilivyo katika Tahdhib, Juz. 5, Uk. 303, na Taqribut-Tahdhib, Juz. 1, Uk. 430. Na kitendo cha Bukhari kumweka Bwana huyu – Abdullahi bin Abdul’Qudus - japo iwe amemuweka katika maelezo ya ziada, ni dalili ya kuthibitisha uaminifu wake.

Ibnu Hajar al-Asqalaniy amesema katika utangulizi wa Fat’hul-Bariy Fii Sharhi Sahih Al-Bukhariy, pale anapojibu kule kukebehiwa kwa wapokezi wa wa Bukhari:
Na kabla ya kuingia humo inambidi kila mwenye insafu ajue kuwa kumuweka mpokezi yeyote yule ndani ya Sahihi – yaani Al-Bukhari – yalazimu uadilifu wake kwake, udhibiti wake na kutokuwa kwake na mghafala. Na khaswa hilo laongezewa na kule kuafikiana kwa jamhuri ya maimamu kuviita vitabu viwili hivi kuwa ni Sahih mbili. Na maana hii haipatikani kwa asiyetoka katika Sahih mbili.”

1. Abdullah bin Abdul-Qudus ni katika wapokezi wa Tirmidhiy.

2. Kama ambavyo dosari ya Abdullahi bin Abdil-Qudus haiudhuru usahihi wa Hadithi hii. Hata kwa riwaya ya Al-Aamash kutoka kwa Atiyyah kutoka kwa Abu Said, kwa sababu ya Abdullah bin Abdul-Qudus kutopokea yeye peke yake riwaya hiyo kutoka kwa al’Aamash. Kwani kwa hakika wameielezea kutoka kwa Al-Aamash: Muhammad bin Talha bin al- Misrafu al-Yaamiy, na Muhammad bin Fadhiil bin Ghazawan al-Dhwabiy ndani ya Musnad, na Tirmidhiy, kama ilivyo kupitia. Na hii ni dalili ya ukweli wa riwaya.

Kama ambavyo Al-Aamash hakuipokea yeye pekee riwaya hii kutoka kwa Atiyyah. Al-Aamash ameelezea kutoka kwa Abdul-Malik bin Abu Sulayman Maysariy Azramiy na Abu Israil Ismail bin Khalifa Al-Absiy, kama ilivyo katika Musnad ya Ahmad kama ilivyo kupitia. Na kutoka kwa Harun bin Saad Al-Ajaliy na Kathiyr bin Ismail At-Taymiy, kama ilivyo ndani ya Muujamut-Tabraniy.

Kumdhoofisha Kwake Abdullah Bin Daahir Kwa Sura Ya Jumla:

Kufanya hivyo ni kinyume na asili na kanuni za Jarhu na Taadiil kwa kuwa kumtia dosari isiyo wazi, haikubaliwi kutoka kwa yoyote awaye.

Hapakuwa na sababu yenye maana ya kumtia dosari, ila tu ni kwa ajili ya riwaya yake ya fadhila za Jemedali wa waumini, kama alivyosema Dhahabi: “Ibnu Adiy amesema: ‘Aghlabu riwaya zake huzungumzia fad- hila za Ali, naye ni mwenye kutuhumiwa kwa hilo.’” Na kumfanya dhaifu kwa sababu hiyo hakukubaliki.

Na ni miongoni mwa maajabu na mabaya kumhusu Ibnu al-Jawziy kufanya vitimbi kwa kiwango hiki ili kuidhoofisha Hadithi hii, kwa kumwingiza Abdullah bin Daahir katika sanad ya Hadithi, hali yajulikana kuwa hajapata kuwa katika sanad yoyote miongoni mwa sanad za Hadithi hii kabisa!

Hebu rejea riwaya za mwanzo na ambazo hatukuzitaja, je wamkuta katika sanadi zake Abdullahi bin Daahir?! Wala siipati maana ya kufanya hivyo ila ni uadui wake kwa Ahlul-Bayt na utashi wake wa kuzifukia haki zao. Lakini “Mwenyezi Mungu anakataa ila aitimize nuru yake japo makafiri wachukie.” Zingatia.

Sibtu Ibnu al-Jawziy baada ya kuileta Hadithi ya Vizito Viwili kutoka kwenye Musnad Ahmad bin Hanbal amesema: “Ikisemwa: Babu yako amesema katika kitabu al-Wahiyah…

Na hapo akayaleta maneno ya Ibnu Al-Jawziy katika kuidhoofisha Hadithi kama ilivyotangulia. Nitasema: Hadithi tuliyoieleza ameiandika Ahmad katika Al-Fadhail, wala katika sanad yake hakuna yoyote aliyedhoofishwa na babu yangu. Na Abu Daud ameiandika katika Sunan yake na Tirmidhiy pia na wanahadithi wote. Razinu ameitaja ndani ya Al-Jam’u Bayna Swihahi. La ajabu ni vipi yalifichika kwa babu yangu aliyoeleza Muslim ndani ya Sahihi yake miongoni mwa hadithi za Zaydu bin Arqam.”9
Alilosema Sibtu Ibnu Al-Jawziy si chochote ila ni kumtetea Ibnu Al- Jawziy, kwani kama si hivyo basi yeye haghafiliki na Hadithi hii iliyoshuhudiwa na vyanzo vya waislamu pamoja na wingi wa mitizamo yake na uelewa, lakini yeye alitaka kufanya hadaa na vitimbi, na ndipo Mwenyezi Mungu akamfanyia vitimbi na akalifedhehesha jambo lake.

Shaka Ya Ibnu Taymiyah

Ama shaka ya Ibnu Taymiya kuihusu Hadithi ya Vizito Viwili katika kitabu chake Minhajus-Sunnah, ni duni mno si kiasi cha kujadiliwa, lakini tutataja katika njia ya kuzipinga fikra hizi zisizo na maana, ambazo hazijulishi ila ubaya wa uelewa na kuchanganyikiwa na kukithiri kwa dhana zisizo na msingi. Ibnu Taymiyya aliposhindwa kuidhoofisha Hadithi ya Vizito Viwili upande wa sanad kama ilivyo kawaida yake, ya kudhoofisha kila linalokuja na fadhila za Ahlul-Bayt, ndipo kwa makusudi kabisa alielekea kwenye utaratibu mwingine ambao hatujauona kwenye jambo lingine, nao ni usemi wake: “Kwa kweli Hadithi hii haijulishi wajibu wa kushikamana na Ahlul-Bayt, isipokuwa yajulisha wajibu wa kushikamana na Qur’ani tu.”

Je ni nani mwenye akili anayepata maana hii na uelewa kama huu kutoka katika tamko hili la wazi? Na dhahiri ya Hadith yakata shauri na kutilia nguvu ulazima wa kushikamana na viwili vya thamani: Kitabu na Kizazi. Kama si hivyo basi nini maana ya vya thamani viwili? “Hakika mimi ni mwenye kuacha kati yenu vizito viwili”. Na ni nini maana ya kauli yake (s.a.w.w): “Endapo mtashikamana navyo viwili”?! Lakini chuki binafsi inapofusha nyoyo.

Na ametoa dalili – yaani Ibn Taymiyya – kwa hadithi moja katika Sahih Muslim kutoka kwa Jabir, na Hadithi zingine zilizobaki amezipiga ukutani au amejighafilisha mbali nazo japokuwa riwaya zake ni nyingi na zina njia mbali mbali. Nayo ni hadithi inayoonyesha kwa mwenye kuzingatia kuwa ni hadithi iliyokatika sanadi yake kwa kuilinganisha na Hadithi zilizobaki zilizokuja katika mlango huu huu.

Hadithi yenyewe ni: “Nimeacha katika ninyi ambalo hamtopotea baada yake, endapo mtashikamana nalo, Kitabu cha Mwenyezi Mungu...” Na hadithi hii kukatika na kupotoshwa kwake kupo dhahiri, kwani hadithi ya Jaabir mwenyewe imekuja katika riwaya ya Tirmidhiy, na humo mna amri ya wazi ya wajibu wa kushikamana na Ahlul-Bayt. Na tamko la Hadithi kama ilivyotangulia katika riwaya ya Tirmidhiy ni: “Enyi watu! Hakika mimi nawaachieni kati yenu ambalo mkilichukua hamtopotea: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu watu wa nyumba yangu.”

Kama ambavyo shaka hii hii pia yamrejelea Ibnu Taymiyya, kwa kuwa yeye anasema: “Ni wajibu kushikamana na Kitabu na Sunna.” Ni lazima amri kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) iwe moja, ima inayolazimisha kushikamana na Kitabu tu, au Kitabu na Sunna. Na Ibnu Taymiyya alipochagua wajibu wa kushikamana na Qur’ani tu, hapo wajibu wa kushikamana na Sunna unaanguka kwa mujibu wa maneno yake. Na hiyo ni kinyume na mwendo wa Ibnu Taymiyya, kama ilivyo dhahiri katika madhehebu yake ya Ahlu Sunna, kama ambavyo amekiita kitabu chake ambacho ndani yake ameitaja Hadithi hii Minhajus-Sunnah, wala hakukiita Minhajul-Qur’ani!

Na ikiwa katika itikadi yake ni kuwa Hadithi hii aliyoitaja haibatilishi Hadithi yakushikamana na Kitabu na Sunna, basi pia haibatilishi wajibu wa kushikamana na Kitabu na Kizazi.

Ibnu Taymiyya hakuishia katika kiwango hiki, hivyo basi akasema kuhusu: “....Na kizazi changu, kwa hakika havitoachana mpaka vinifikie katika bwawa”:
“Hii ameieleza al-Tirmidhiy. Ahmad aliulizwa kuhusu hii. Na wameidhoofisha wanavyuoni zaidi ya mmoja, wamesema kwa kweli si sahihi.”

Najibu: Utahisi katika kauli yake kuwa tamko hili la Hadithi halijaelezwa na yoyote ila Tirmidhiy. Na ulikwishajua kama ilivyotangulia kuwa hiyo imeelezwa na zaidi ya mmoja miongoni mwa ulamaa wa kisunni na wanahadithi wao.

Basi nini anakusudia kwa kauli yake: Ameipokea Tirmidhiy?! Je kupokewa na Tirmidhiy ni dalili ya udhaifu wake?! Na nani ambaye alimuuliza Ahmad?! Na alimjibu nini?! Na kauli hii ilikuwa mahali gani?! Au Ahmad mwenyewe hakuieleza na hakuizingatia kuwa ni sahihi?! Na nani alimdhoofisha hata aseme: Si mmoja?! Basi ni kwa nini hakuwataja?!

Na yasiyo hayo miongoni mwa maswali ambayo yaweza yakaelekezwa kwa Ibnu Taymiyya, akiyajibu kwa maneno thabiti tutaikubali shaka yake, wala haiwezekani tuikubali hovyo hovyo tu, nayo iko katika sura ya jumla. Lakini hii ni tabia ya Ibnu Taymiyya akipania kuupotosha umma na kuufunika ukweli.

Hizi ndizo shaka muhimu zilizokuja katika mlango huu na wala sijapata kumuona kulingana na ufuatiliaji wangu ambaye anaiponda Hadithi ya Vizito Viwili iliyothibiti kwa mfululizo na ambayo wamekiri kuwa ni sahihi watu maarufu katika umma miongoni mwa mahafidhu na wanahadithi, na wala hathubutu kuikebehi isipokuwa mwenye moyo muele uliojaa chuki na hasira kuwaelekea Ahlul-Bayt. Na baada ya kuthibiti kwetu kwa wazi kabisa ukweli wa Hadithi hii, ni wajibu sasa juu yetu kuiweka wazi dalili na baada ya hivyo kujiambatanisha nayo.

  • 1. Tahdhibut-Tahdhib Juz. 2, Uk. 226.
  • 2. Nawasibu: Ni watu wanaowafanyia uadui Ahlul-Bayt.
  • 3. Shifaul-Asqam Juz.10, Uk. 11.
  • 4. Khulaswatul- Abaqaatul-Anwar. Juz. 2, Uk. 45.
  • 5. Tahdhibut-Tahdhib Juz. 7, Uk. 225.
  • 6. Khulaswatul- Abaqaatul-Anwar. Juz. 2, Uk. 47. Nukuu kutoka kwenye Al- Kamal Fi Asmair-Rijal.
  • 7. Tahdhibut-Tahdhib, Juz. 5, Uk. 303.
  • 8. Tahdhibut-Tahdhib, Juz. 5, Uk. 303.
  • 9. Tadhkiratu Khawasul-Umma.