read

Maongezi Na Mwanahadithi Wa Damascus, Abdul-Qadir Al-Arnutiy

Ilinitokea nilipokuwa naishi Sham, kukutana na Sheikh Abdul Qadir Arnutiy, naye ni katika wanazuoni wa Sham (Syria) naye ana ijaza1 katika elimu ya Hadith.

Mkutano huu ulifanyika bila ya maandalizi yangu, bali ulikuwa kwa tukio la bahati.

Nilikuwa na mmoja wa marafiki zangu wa Sudan jina lake Adil, nilifahamiana naye katika kitongoji cha As-Sayyidatu Zaynab (a.s.), na Mwenyezi Mungu alikuwa ameung’arisha moyo wake kwa nuru ya Ahlil- Bayt (a.s.), na amekuwa mfuasi wao, na alikuwa kijana huyu apambanuka kwa sifa njema, ni haba uweze kuzipata kwa mtu mwingine.

Alikuwa mwenye tabia nzuri, mwanadini na mnyenyekevu. Hali duni ya maisha ilimlazimu afanye kazi kwenye shamba mojawapo katika kitongoji kiitwacho Al’Adiliyah karibu kilomita tisa Kusini mwa Sayyidat Zaynab (a.s.). Karibu na shamba alilokuwa akifanya kazi kulikuwa na shamba lingine la mtu wa makamu, mwanadini alikuwa akijulikana kwa jina la Abu Sulayman. Huyu jirani alipojua kuwa Msudani afanyaye kazi jirani yake ni Shia, alikuja kwake na kuzungumza naye, akasema: ‘Ewe ndugu yangu! Wasudani ni masunni wazuri, wewe huu Ushia unatoka nao wapi?! Je katika familia yako kuna Shia yeyote?’

Adil alijibu: ‘Hapana, lakini dini na kukinai havijengeki juu ya kuiiga jamii na familia.’
Akasema: ‘Kwa kweli Shia wanadanganya na wanawahadaa watu wa kawaida.’
Adil akasema: ‘Mimi sijaliona hilo kwao.’
Akasema: ‘Ndio sisi tunawajua vizuri.’
Adil akasema: ‘Ewe alhaji, je waiamini Bukhari, Muslim, na vitabu sahihi vya kisunni?’
Akasema: ‘Ndio. ‘
Adil akasema: ‘Kwa kweli Shia huitolea dalili itikadi yeyote wanayoiamini kutoka vyanzo hivi, sembuse vyanzo vyao.’
Akasema: ‘Kwa kweli wao wanadanganya wanazo Bukhari na Muslim zilizopotoshwa.’
Adil akasema: ‘Wao hawakunilazimisha mimi kitabu mahsusi, bali waliniomba nitafute kutoka maktaba yoyote katika ulimwengu wa Kiarabu.’
Akasema: ‘Huu ni uwongo, na ni wajibu wangu nikurudishe mara nyingine kwenye Usunni.

“Mwenyezi Mungu akimwongoza mtu mmoja kupitia wewe ni bora kwako kuliko vyote vinavyochomozewa Jua.”’
Adil akasema: ‘Sisi ni watafutao haki na mwongozo, tunaelemea ielemeako dalili.’
Akasema: ‘Mimi nitakuletea mwanachuoni mkubwa wa Damascus, ni Allama Abdul-Qadir Arnutiy, ni mwanachuoni mtukufu, msimulizi na muhifadhi wa Hadithi. Shia walijaribu kumrubuni kwa mamilioni ili awe pamoja nao, lakini yeye alikataa.’

Ndugu Adil aliafiki wazo hili, na Abu Sulayman akamwambia: “Ahadi yetu ya kukutana ni siku ya Jumatatu, wewe na Wasudani wote ambao wameathiriwa na fikra za kishia.”

Adil alikuja kwangu, na alinipa habari ya yaliyojiri, na aliniomba niende pamoja naye. Kwa furaha kubwa nilikubali pendekezo hili na niliahidiana naye tukutane saa sita adhuhuri, siku ya Jumatatu 8 Swafar 1417 A.H.

Siku hiyo ilikuwa ya joto kali, tulikutana kwenye ahadi na tulikwenda kule kondeni tukiwa na Wasudani watatu, na tulipofika ndugu Adil alikuwa mpokezi wetu kwenye konde janibichi inayozungukwa na miti ya matunda mbalimbali ambayo mengi hayapo kwetu Sudan.

Na baada ya hapo tuliendelea na safari kwa jirani yake Sunni, alitupokea kwa hamu kubwa. Na baada ya muda kidogo wa kupunga hewa mahali pale pazungukwapo na majani kibichi kila upande, nilikwenda kuswali Dhuhuri na katika hali ile ya Swala msafara ulikuja ukitanguliwa na gari inayombeba Sheikh Arnutiy. Mahali palikuwa pamejaa watu, na walitoka nje waliokuwa ndani ya gari.

Nyuso za swahiba zangu Wasudani zilifunikwa na mshangao kutokana na haiba ya mahali hapo, kwa kuwa walikuwa hawakutazamia kuwa mambo yatakuwa makubwa kwa kiwango hiki. Na baada ya kila mmoja kutuwama nafasi yake, nilichagua mahali karibu na Sheikh.

Na baada ya wote kutambulishana, bwana mwenye konde aliongea na Sheikh akisema: “Hawa ni ndugu zetu kutoka Sudan na wameathirika na fikra ya Kishia huko Sayyidat Zaynab, na kati yao kuna Shia anafanya kazi kwenye konde lililoko jirani yetu.”

Sheikh akasema: “Yuwapi huyu Shia?”

Walimwambia: “Amekwenda kwenye konde lake atarejea baada ya muda tu. “

Akasema: “Basi tungoje, maongezi yaanze baada ya kurejea kwake.” Mmoja kati ya Wasudani alimwendea na alimleta kwenye kikao, na Sheikh aliitumia nafasi hii kwa kusoma Hadithi nyingi anazozihifadhi kwa moyo, na maudhui yake yalikuwa ubora wa baadhi ya nchi kuliko nyingine na hasa Syria na Damascus, na maudhui hii ilichukuwa karibu nusu saa, nayo ni maudhui haikuwa na maana. Nilistaajabishwa naye sana vipi haitumii fursa hii, hali watu wote wamemwazima akili zao ili wapate Hadithi itakayowanufaisha katika dini yao na dunia yao, hatimaye akasema: “Kwa kweli dini ya Mwenyezi Mungu haichukuliwi kwa usharifu, Mwenyezi Mungu amejaalia sheria yake kwa watu wote, hivi ni kwa haki gani tuichukue dini yetu kutoka kwa Ahli’bayt?! Hali Mtume wa Mwenyezi Mungu ametuamuru kushikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna zake, na hii ni Hadithi sahihi hawezi yeyote kuidhaifisha, na hatuna njia nyingine isiyokuwa njia hii.” Na alipiga kwa kiganja chake mgongoni kwa Adil na kumwambia: “Ewe mwanangu, yasikughuri maneno ya Shia.”

Nilimsimamisha nikisema: “Mstahiki Sheikh, sisi twaitafuta haki, na mambo yametuchanganya na tumekuja ili tufaidike kutoka kwako, hasa tulipotambua kuwa wewe ni mwanachuoni mtukufu, mwanahadithi na muhifadhi wake.”

Akasema: “Ndio.”

Nikasema: “Ni miongoni mwa mambo yaliyo wazi, ambayo haghafiliki nayo isipokuwa kipofu, kuwa waislamu wamegawanyika katika makundi na madhehebu yasio na idadi, na kila kikundi kinajigamba kuwa ndicho cha haki na kingine mbali na chao ni batili. Hivyo vipi nitaipata njia, nami nikiwa nakalifishwa na sheria za Mwenyezi Mungu nitambue ukweli kati ya vikundi hivi vyenye kupingana?! Je Mwenyezi Mungu alitutakia tuwe tumefarakana, au alitaka tuwe mila moja tunamfanyia Mwenyezi Mungu ibada kwa sheria moja?!

Na ikiwa ndio, basi ni dhamana gani Mwenyezi Mungu na Mtume wake wametuachia ili umma uhifadhike mbali na upotovu? Kwani yajulikana kuwa tofauti ya kwanza ilitokea kati ya waislam mara tu baada ya kutawafu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) palepale, na sio jaizi kwa majukumu ya Mtume auache umma wake bila ya mwongozo waongokao nao.”

Sheikh akasema: “Dhamana ambayo ameiacha Mtume wa Mwenyezi Mungu ili umma uzuilike mbali na kutofautiana ni kauli yake (s.a.w.w):

“Mimi ni mwenye kuacha kile ambacho endapo mtakishika hamtopotea: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu.”

Nilisema: “Kwa kweli ulisema muda mchache uliopita, katika maneno yako huenda ikawa kuna Hadithi haina asili yaani haikutajwa katika vitabu vya Hadithi.”

Akasema: “Ndio.”

Nikamwambia: “Hadithi hii haina asili katika Sahihi Sita, vipi waiongelea na wewe ni bingwa katika taaluma ya Hadithi?”

Hapo moto wake ulilipuka, akawa anakoroma akisema: “Unakusudia nini, wataka kuifanya Hadithi hii ni dhaifu?”

Nilishangazwa na njia yake hii, na sababu ya kuchemka kwake, ingawaje mimi sikusema kitu. Nilisema: “Pole pole, swali langu ni moja na lenye mpaka. Je Hadithi hii ipo ndani ya Sahihi Sita?”

Akasema: “Sahihi sio sita, na vitabu vya Hadithi ni vingi, na Hadithi hii ipo katika kitabu Al-Muwatau cha Imam Malik.”

Nikasema: (nikiwaelekea waliohudhuria): “Vyema, Sheikh amekiri kuwa Hadithi hii haipo katika Sahihi sita, na kuwa ipo katika Al-Muwatau ya Malik.

Alinikata kauli (kwa lahaja ya ukali) akisema: “Nini! Al-Muwatau sio kitabu cha Hadithi?”

Nikasema: “Al-Muwatau ni kitabu cha Hadithi, lakini Hadithi hii: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu” katika Al-Muwatau haina nyororo ya wapokezi, haina sanad, hali hadithi za Al-Muwatau zote zina sanad (ila hii).

Hapo Sheikh alikoroma baada ya hoja yake kuanguka, akawa ananipiga kwa mkono wake na ananitikisa kushoto kulia: “Wewe unataka kuidhoofisha Hadithi hii, wewe ni nani ufikie kuidhoofisha Hadithi hii?!”

Kiasi kwamba alitoka nje ya mipaka ya kiakili. Wote walianza kushangazwa na harakati zake na matendo yake haya.
Nikasema: “Ewe Sheikh! Hapa ni mahali pa mjadala na dalili, na mwenendo huu wa ajabu unaokwenda nao haufai, mimi nimekaa (vikao) na wengi katika wanavyuoni wa Shia, wala sikuona utaratibu kama huu kabisa. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

إِذْ تُصْعِدُونَ وَلَا تَلْوُونَ عَلَىٰ أَحَدٍ وَالرَّسُولُ يَدْعُوكُمْ فِي أُخْرَاكُمْ فَأَثَابَكُمْ غَمًّا بِغَمٍّ لِكَيْلَا تَحْزَنُوا عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا مَا أَصَابَكُمْ ۗ وَاللَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ {153}

“Na lau ungekuwa mkavu na mgumu wa moyo wangetawanyika kukukimbia.”
(Sura al-Imran: 153).

Hapo kidogo ulipoa mhemko wake. Nikasema: “Nakuuliza Sheikh, je riwaya ya Malik katika Hadithi hii “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu” katika Al-Muwatau, ni dhaifu au sahihi?!”

Alisema (kwa masikitiko makubwa): “Ni dhaifu.”

Nikamuuliza: “Kwa nini basi, ulisema Hadithi iko katika Al- Muwatau nawe wajua kuwa ni dhaifu?”

Akasema (kwa sauti ya juu): “Hadithi hii ina njia zingine.”

Nikasema kwa waliohudhuria: “Sheikh ameachana na riwaya ya Al- Muwatau, na amesema kuwa Hadithi hii ina njia zingine, hebu tuzisikilize njia hizo kutoka kwake.”

Hapo Sheikh alihisi kuhemewa na aibu, kwa kuwa Hadithi hii haina njia iliyo sahihi, na wakati huo huo, mmoja kati ya waliohudhuria aliongea, Sheikh alinibonyeza kwa mkono wake, na aliniambia huku akiishiria kwa muongeaji: “Msikilize.”

Na aligeuka akiwa ataka kulikimbia swali linalosumbua nililomuuliza. Nilihisi hali hii kwake lakini nilisisitiza nikasema: “Tusikilize ewe Sheikh njia zingine za Hadithi hii?”

Akasema (kwa lahaja ya kunyongea): “Sikuzihifadhi, nitakuandikia.”

Nikasema: “Subhanallah!, wewe wahifadhi hadithi zote hizi kuhusu ubora wa nchi na vitongoji wala hauhifadhi njia ya Hadithi muhimu mno miongoni mwa Hadithi ambayo ndio ngome ya Ahlu Sunna, na ni Hadithi ambayo yauhifadhi umma huu usipotee, kama ulivyosema!”

Alibaki kimya. Na waliohudhuria walipohisi kuwa ameaibika, mmoja wao aliniambia: “Wamtaka nini Sheikh na amekuahidi kuwa atakuandikia?”

Nikasema: “Mimi nakusogezea njia, kuwa Hadithi hii pia ipo katika Siira ya Ibnu Hisham bila ya sanad.”

Sheikh Arnutiy akasema: “Kwa kweli Siira ya Ibnu Hisham, ni kitabu cha siira sio cha Hadithi.”

Nikasema: “Kwa hiyo waiona dhaifu riwaya hii?”

Akasema: “Ndio.”

Nikasema: “Umenitosheleza mzigo wa kuijadili.”

Na niliendelea na maneno yangu nikisema: “Na pia ipo katika kitabu Ilmau cha Kadhi Iyyadh, na katika kitabu Al-Faqiihul-Mutafaqihu cha al-Khatib al-Baghdad. Je wazichukua riwaya hizi?”

Akasema: “Hapana.”

Nikasema: “Hivyo basi Hadithi ya “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu” ni dhaifu kwa ushuhuda wa Sheikh. Mbele yetu hapajabaki dhamana ila moja tu itakayouzuia umma usitofautiane, nayo ni Hadithi mfululizo kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w). Na imeelezwa na vitabu vya Hadithi vya kisunni, na Sahih-Sita isipokuwa Bukhari. Nayo ni kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w):

“Kwa hakika mimi ni mwenye kukuachieni katika ninyi viwili vya thamani, endapo mtashikamana navyo hamtopotea baada yangu kamwe: Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni kamba iliyovutwa kati ya mbingu na ardhi, na kizazi changu watu wa nyumba yangu. Kwa kuwa mjuzi mwenye habari, amenipa habari kuwa hivyo havitotengana hadi vitakaponijia kwenye dimbwi.”

Kama ilivyo katika riwaya ya Ahmad bin Hanbal, wala hapana kimbilio lingine mbali na njia hii kwa muumini autakaye Uislamu ambao Mwenyezi Mungu na Mtume wake wameamrisha. Nayo ni njia ya Ahlul- Bayt (a.s) waliotoharishwa mbali na uchafu na maasi katika Qur’ani tukufu.

Na nilitaja jumla ya fadhila za Ahlul-Bayt (a.s.). Sheikh alikuwa amenyamaa hakutoa neno muda wote huu, na si kawaida yake kwani hapo kabla alikuwa akiyakata mazungumzo yangu kati ya neno na neno. Na wapenzi wake walipoona hali ya kushindwa ya Sheikh wao walifanya ghasia na fujo.

Nikasema: “Watosha udajali, unafiki na hadaa dhidi ya ukweli. Mpaka lini kujingikiwa huku?! Ukweli alama zake ziko wazi, ubainifu wake uko dhahiri, na nimesimamisha hoja kwenu, kuwa hapana dini bila ya Kitabu na kizazi kilichotoharika ambacho ni Aali Muhammad (s.a.w.w).”

Sheikh alibaki kimya wala hakunipinga japo neno moja. Alisimama akijipangusa huku akisema: “Mimi nataka kwenda, nina darasa.” Na hali ikiwa yajulikana kuwa alikuwa amealikwa kwenye chakula cha mchana hapa!!.

Mwenyeji alimuomba abakiye, na baada ya kuletwa chakula cha mchana kikao kilitulia. Sheikh hakusema neno lolote katika maudhui nyingine yoyote muda wote wa chakula cha mchana, na hali hapo kabla alikuwa yeye ndiye mwenye kikao na ndiye msemaji namba moja.

Hali ni kama hii kwa kila ambaye anafanya hadaa na kuuficha ukweli, hapana budi afedheheke mbele ya watu.

  • 1. Hati maalumu ya ruhusa ya kunukuu hadithi.