read

Mazingatio Kwa Mfanya Mjadala Ambayo Hapana Budi Kwake

Kabla ya kuanza kusajili baadhi ya tafiti zangu katika kitabu hiki, napenda niashirie baadhi ya mambo ambayo yapasa kuzingatiwa, niliyofaidika nayo kutokana na uzoefu wangu wa hapo mwanzo kuhusu taratibu za mjadala.

1. Kujiamini na kumtegemea Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Na hiyo ndio nukta ya kuanzia katika mjadala. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa mwanadam nuru ya akili na elimu, na amejaalia suala la kufaidika navyo mkononi mwa binadamu mwenyewe, kwa hiyo mwenye kuzembea kwa kutofaidika na nuru hii wala asiing’arishe ili kufichua ukweli, ataendelea kuishi kwenye rundo za ujahilia na imani za kuwazika tu na potovu.

Kinyume na anayefaidika na akili yake na kuikuza.

Na tofauti kati ya mawili hayo yarejea kwenye sababu moja, nayo ni kujiamini na kutojiamini. Hivyo basi anayehisi udhaifu na kushindwa hawezi kufaidika na akili yake, ama mwenye kuwa na matumaini na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na kwa alichomtunukia miongoni mwa nuru ya akili, hufikia kilele cha maarifa na maendeleo. Kwa ajili hiyo wengi waliokuwa wanapinga njia yangu katika kufanya utafiti walikuwa wanatumia utaratibu huu ili kuangusha matumaini yangu, alikuwa (mtu) anasema: “Una uwezo gani wewe wa kufanya utafiti wa mambo haya?! Kwa kweli wanavyuoni wetu wakubwa hawakufikia ulipofikia, nini thamani yako mbele ya miamba ya wanavyuoni wenye maarifa makubwa?!” Na yasiyokuwa hayo miongoni mwa njia za kuharibu uwezo. Hawakuwa wananitaka zaidi ya kuwa niwe naingia waingiapo, na nipige kelele kama wapigavyo, amesema (s.w.t.) Yatutosha tuliyowakuta nayo baba zetu.” (Maida: 104).

2. Kujiepusha na hadaa ya utu uliyonayo, kwa maana ya kupuuzuia ukweli usipenye kwenye akili. Hilo laweza kuwa kwa kuzifunga penyo za nafsi chunguzi kuutambua ukweli wa nje. Hivyo (mtu) hujipendelea na hujizuia asisikilize maneno ya maarifa na fikra zingine na kusoma vitabu, na mengine yasiyo kuwa hayo. Hivyo basi kila aina ya wito unaoamrisha kujifungia na kutofanya utafiti na kujipatia maarifa, ni wito unaokusudia kuimarisha ujinga na kuwaweka watu mbali na ukweli. Kwa hakika yafanywayo na uwahabi, kule kujizatiti kwenye ngome ya kutotaka kujua yaliyomo ndani ya vitabu vya Shia na kutokaa na kuketi na yeyote miongoni mwa Shia na kujadiliana naye, ni njia ya mwenye kuhemewa na ni mantiki isiyo salama. Qur’ani tukufu imepinga fikra hii kwa kauli yake (s.w.t.): “Sema: Leteni dalili yenu kama nyinyi ni wakweli.” (Baqarah: 111).

3. Kuukuza utashi mbele ya mawimbi ya matamanio na mistari ya mbinyo wa kijamii, ambapo kwa kawaida jamii humchukia kila anayekwenda kinyume na inavyoona, au kuiasi, kwa hiyo hapana budi kuikabili mibinyo hii kwa subira na azma, kwa kuwa ukweli hauwi kwa kuendeleza hali ya kijamii na yatokanayo na tabia ya mwanadamu. Historia ya manabii wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni hiyo, wamekumbana na aina kali mno za adhabu kutoka kwa jamii zao. Waisraeli walikuwa wanawauwa kwa siku manabii sabiini wa Mwenyezi Mungu. Allah (s.w.t.) anasema: “Na hakuwafikia Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli.” (Sura Zukhruf: 7).

4. Kuna vizuizi vingi vinavyoweza kuzuia kuufichua ukweli, hivyo basi hapana budi kutanabahi na kuangalia ili ukweli uwe wazi zaidi na wenye mwanga zaidi, na miongoni mwa vizuizi hivi ni:

Kujipendelea mtu dhati yake, na huo ni ugonjwa mbaya mno unaomsibu kila mtu, na kutokana nao hupatikana akisi ya kila sifa mbaya mfano wa husuda, hikdi, ukaidi, pindi mtu anapozifanya fikra zake na itikadi yake kuwa sehemu ya dhati yake na utu wake. Japo ziwe potovu hatoweza kukubali zikosolewe imani na fikra zake hizo, kwa kuwa yeye anaamini kuzikosoa ni kuitangua dhati yake na utu wake.

Hivyo kwa silika ya mtu kujilinda nafsi yake na kuipenda, anakuwa jasiri kuilinda bila uelewa au ufahamu, na pengine anajijengea upendeleo wa fikra fulani kwa kuwa yamletea manufaa au kumhami dhidi ya madhara, kwa hiyo hujibadilisha rangi na kuihami, kwa minajili hiyo huikataa kila fikra japo ukweli wake uwe dhahiri kwenye macho.

Pia anaweza kuipenda fikra si kwa jingine ila tu kwa kuwa yalingana na utashi wa nafsi yake au wa jamii yake, kwa hiyo haepukani nayo.

Kuwapenda wazazi, hilo humfanya mtu kuwafuata bila kufikiri wala kuzingatia, hivyo basi chini ya dai la kuheshimu na kuogopa, ukiongezea kurithi na malezi, mtu husalimu amri mbele ya fikra zao na itikadi zao moja kwa moja. Na hiki ni kizuizi miongoni mwa vizuizi vikubwa mno ambavyo humzuia mtu kuugundua ukweli.

Kuwapenda waliopita. Kwa kweli mtizamo wa utakatifu kuwaelekea wanavyuoni waliopita na watu watukufu kunampelekea mwanadamu kuwafuata moja kwa moja na kuzitegemea fikra zao na itikadi zao. Hivyo basi kusalimu amri mbele ya ufuataji kama huu ni sababu miongoni mwa sababu za kupotoka mbali na ukweli.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuzijaalia akili zao kuwa hoja juu yetu, bali akili ya kila mtu ni hoja juu yake, hivyo basi heshima zetu kwao zisituzuie kuhoji na kuzipembua fikra zao, ili tusiingie katika hukumu ya kauli yake (s.w.t.):

وَقَالُوا رَبَّنَا إِنَّا أَطَعْنَا سَادَتَنَا وَكُبَرَاءَنَا فَأَضَلُّونَا السَّبِيلَا {67}

“Na watasema: Mola wetu hakika tumewafuata mabwana wetu na wakubwa wetu, basi wao wametupoteza njia.” (Sura Ahzab: 67).

Na pia miongoni mwa sababu za makosa ni kufanya haraka. Na hiyo ni tija ya kupenda raha, hivyo mtu bila ya kujitaabisha binafsi, kutafiti na kuchimbua, hupenda kuharakia kutoa hukumu yake kwenye mtazamo wa kwanza.

Kutokana na hali hiyo wanafikra wamekuwa wadogo ulimwenguni kwa sababu ya ugumu wa kufikiri na kutafiti. Hivyo basi, kwa autakaye ukweli hapana budi afanye juhudi mwenyewe katika kuutafiti.

Na yasio hayo miongoni mwa maono ya kielimu ambayo hapana budi mtafiti ayaweke kwenye mkazo wa macho yake kabla hajaanza utafiti. Hii iwe pamwe na kujiepusha na hayo kikamilifu, na kusalimu amri moja kwa moja endapo ukweli utadhihiri. Ukiongezea kuomba auni na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ili aung’arishe moyo wako kwa nuru ya haki: “Ewe Allah, tuonyeshe ukweli kama ulivyo na turuzuku kuufuata, na tuonyeshe batili kama ilivyo na uturuzuku kujiepusha mbali nayo.” (Hadith tukufu.)