read

Mlango Wa Kwanza

Dondoo Kutoka Katika Maisha Yangu

أَفَمَنْ شَرَحَ اللَّهُ صَدْرَهُ لِلْإِسْلَامِ فَهُوَ عَلَىٰ نُورٍ مِنْ رَبِّهِ ۚ فَوَيْلٌ لِلْقَاسِيَةِ قُلُوبُهُمْ مِنْ ذِكْرِ اللَّهِ ۚ أُولَٰئِكَ فِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {22}

“Ambaye Mwenyezi Mungu amemfungulia kifua chake kuukubali uislamu, naye yuko katika nuru itokayo kwa Mola wake. Basi adhabu kali kwa wale wenye nyoyo ngumu kumkumbuka Mwenyezi Mungu, hao wako katika upotovu ulio bayana.” (Sura Az-Zumar: 22).

“Mwenyezi Mungu akimtakia kheri mja wake hufanya nukta nyeupe moyoni mwake, hivyo moyo huzunguka ukitafuta ukweli kisha anakuwa mwepesi mno kuielekea amri yenu kuliko ndege kuelekea kiota chake.”1 (Imam Jafar Swadiq (a.s).

Siku Za Utoto:

Upendo ulikuwa unaniandama toka utoto wangu. Na hali ya kimaumbile ilikuwa inanifunga kuelekea kushikamana na dini, na sura iliyokuwa ikizunguka akilini mwangu na kupitia humo ikiuangalia mustakbali wangu haikutoka nje ya wigo wa kuwa mwanadini. Hivyo nilikuwa najiona binafsi kupitia njozi kuwa ni mtu niliye macho, shujaa, na askari wa kiislam mpambanaji, nairudishia dini heshima yake na Uislamu nguvu zake. Hapo nilikuwa sijaivuka daraja ya kwanza katika masomo yangu ya akademia. Kwa minajili hiyo fikra zangu zilikuwa fupi, na uelewa wangu kuhusu historia ya waislam na maendeleo yao ni haba. Nilikuwa sijui isipokuwa baadhi ya visa kumuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na vita vyake na makafiri, na ushujaa wa Imam Ali (a.s.) na uhodari wake.

Na baada ya kusoma kwetu historia ya dola ya Al-Mahdi katika nchi ya Sudan, nilivutiwa na shakhsia ya Uthman Deqnah, naye alikuwa mmoja miongoni mwa wakuu wa kijeshi wa jeshi la Al-Mahdi walioasi Mashariki ya Sudan. Mapambano yake yalikuwa yananivuta wakati ustadhi wetu wa somo la historia alipokuwa anatufanyia taswira ya ukakamavu wake na adhama ya shaksia, naye akiwa mpiganaji katika milima na mabonde. Kama hivyo moyo wangu uliungana naye, na nilijenga matarajio yangu niwe kama yeye.

Hapo nilianza kufikiri kulingana na akili yangu ya udogo, njia ya kulifikia lengo hili.

Hivyo basi njia yangu pekee ambayo ilikuwa ninaifanyia taswira ni niwe mtu aliyehitimu chuo kikuu cha kijeshi, ili nipate kujifundisha fani za kivita na matumizi ya silaha, niliishi katika upendaji wa ukichaa kama huu miaka kadhaa katika umri wangu, mpaka nilipofikia sekondari hapo nilifunguka kifikra, na maarifa yangu yalizidi.

Hapo niliwajua viongozi wa ukombozi katika ulimwengu wa kiislam, mfano wa Abdur Rahman Al-Kawakibiy, na As-Sanusiy, na Umar Mukhtar…na Jamalu din Afghaniy, naye ni mwanamageuzi stadi wa kivita, mwanafikra aliyechomoza kutokea Afghanistan na kuingia katika miji mikuu ya dola za kiislam na zisizo za kiislam akieneza fikra hai ambayo inagusa umbali wa kuchelewa katika ulimwengu wa kiislam na jinsi ya kuutibu.

Na kilichotilia nguvu mzinduko wangu ni zile mbinu zake alizokuwa akizifanya katika shughuli zake za kimapambano, miongoni mwa hekima na busara na kueneza taaluma na kutoa mwongozo kifikra kwa umma wa kiislam, bila ya kushika silaha…!

Nilikuwa naamini kuwa kila atakaye kufanya mapambano na kuwalinda waislam, hapana budi anyanyue upanga na aingie vitani na apigane, lakini mbinu zake zilikuwa kinyume kabisa na nilivyokuwa nafanya taswira. Hivyo mbinu ya neno na taaluma ya uelewa ni kitu kipya kilichojitokeza katika fikra zangu za kidini, lakini mimi sikuweza kuachia kwa urahisi ambalo nililokuwa nimezijengea fikra zangu na utashi wangu, japokuwa niligundua kuwa tatizo la umma ni tatizo la elimu ya kiujumbe iliyoiva. Kwa kuwa taaluma ndio iwezayo kumbebesha kila mmoja jukumu lake.

Huyu ndie Jamaludin, amezunguka ulimwengu akieneza nuru yake na baraka zake, na anayeeneza fikra na elimu ambayo waislamu waliipokea kwa shangwe na taathira, kwa sababu ilikuwa inatatua matatizo yao na ilikuwa inaendana na hali yao halisi, hilo likazitisha nguvu za kikoloni zenye hikdi, na Al-Urwatul’wuthqa2 pekee ndilo lilikuwa linawainulia sauti, ndio maana walifanya juhudi kuliwekea vikwazo na kulizuia kabisa lisitoke.

Hivyo kujiuliza ambako kulikuwa kunanishawishi ni: Vipi huyu mtu mmoja pekee aliweza kubadilisha ule uwiano wa uzito, na vipi alizitisha nguvu hizi zenye kiburi?!

Na ili kujibu swali hili, mbele yangu kulifunguka mlango mkuu wa maswali, baadhi yalikuwa rahisi na baadhi hayakuwa na jibu katika hali halisi ya Sudan, ni miongoni mwa ambayo yalinifanya mimi nijaribu kujikomboa mbali na hali hii halisi, na nifungue kila vifundo na vifungo ambavyo vilikuwa vinaniita nisalimu amri na niwe mnyenyekevu kwenye hali hii halisi ya kidini, ili niweze kwenda katika maisha haya kama walivyokuwa baba zangu na babu zangu, lakini kutambua kwangu jukumu na kumpenda kwangu Jamaludin ilikuwa ni kengele yagongwa kwenye kamba ya maumbile yangu. Nilikuwa najiuliza:

Vipi nitaweza kuwa mfano wa Jamaludin?! Na je dini ambayo nimeirithi itaweza kunibeba mimi kuifikia daraja ile? Kisha nasema: Kwa nini isiwe hivyo? Hivi Jamaludin alikuwa na dini isiyokuwa hii dini yetu? Na ni Uislamu wa aina nyingine sio huu wetu?

Ili kujibu niliduwaa miaka mingi na lote nililofikia ni kubadilisha uelewa wangu wa dini kabisa, hivyo nilifikia kumuona Jamaludin ni uongozi na ni mfano ikiwa hapo kabla alikuwa Uthman Deqnah, na nilibadilika kwa njia hiyo, hivyo badala ya kuwa chuo cha kijeshi ndiyo tumaini langu, ikawa tumaini langu ni njia iliyo salama itakayo nitambulisha mimi fikra na taaluma asili ya kiislam ambayo kupitia hiyo mwamko wa kiislamu utakuwa.

Mwanzo Ulikuwaje:

Ilikuwa kutafuta utaratibu na fikra iliyowiva na taaluma itakiwayo ni vigumu, na daraja hii ilikuwa chungu, japokuwa utafiti wangu ulikuwa kwa sura ya msamaha na wa kimaumbile. Katika maisha yangu ya kawaida nilikuwa nauliza na kujadili na vinginevyo, wala hapakuwa na utayarifu wa kutafiti na kuhimili. Na baada ya uvamizi mkali wa mawahabi kuiv- amia Sudan, na kushika kasi malumbano na mijadala na kukithiri kwa harakati za kidini, ukweli mwingi ulifichuka, na zikajitokeza tofauti na mifarakano mingi ya kihistoria, kiitikadi na kifiq’hi.

Na tendo la kuvikufurisha baadhi ya vikundi na kuvitoa nje ya tanzi la uislamu ilianza, ni miongoni mwa mambo ambayo yalisababisha mfarakano wa kimadhehebu na safu kutengana. Pamoja na uchungu wa yaliyotokea, nilipata utashi wangu na udadisi wangu ulizidi, na nilikuwa naona uhalisi wa yale maswali yaliyokuwa yanaishawishi akili yangu.

Hapo basi hima yangu ya kuutilia maanani uwahabi ilizidi, nilikuwa nafuatilia mijadala yao na mikusanyiko yao ambayo ilikuwa inanifunga mimi. Na ambalo ni la muhimu nililojifunza kutoka kwao katika ngazi ile, ni ujasiri na kuukabili ukweli na kuukinza, nami nilikuwa naamini kuwa ukweli ni kitu kitakatifu na ni mwiko kuuhujumu au kuupinga, japokuwa uangalizi wangu ulikuwa mwingi kuuhusu, ambapo aghlabu nilikuwa siangalii kupitia dhati yangu na umbile langu, hivyo basi nilikuwa najizuia sana matendo na zoezi za jamii ya kidini.

Niliendelea nao, na ilijiri kati yangu na wao mijadala mingi, ambayo ukweli wake ulikuwa yale maswali ambayo yalikanganya akili yangu, baadhi yake nilipata majibu yaliyoniridhisha katika ngazi ile, na kulikuwa na maswali sikupata majibu yake kutoka kwao, hilo lilikuwa dhamana tosha kwangu kuwaelemea na niwaunge mkono, japokuwa kulibaki baadhi ya mazingatio ambayo yalikuwa kizuizi kati yangu na kujihusisha moja kwa moja na mwendo wa kiwahabi. La kwanza na la muhimu ni kuwa mimi sikupata kwao nitoshekalo nalo, ambalo laweza kuwa jibu la matamanio yangu ya kiujumbe. Na wakati mwingine wasiwasi ulikuwa unanichukua kwa kauli yake:

Kwa kweli unalolifikiria na kulitafiti ni kitu cha mfano tu hakina ukweli, na uwahabi ni sampuli bora ya uislamu na hapana kitu badala yake….

Nilikuwa nasukumwa na wasiwasi huu na kuusadiki kwa kutokuwa kwangu na maarifa na fikra za vyuo vingine, lakini haraka nilikuwa na’ngamua kuwa ambalo Jamaludin amelifanya haiwezekani liwe ndio hii fikra ya kiwahabi. Kwa hiyo nilikuwa nasema waziwazi: Kwa kweli Uwahabi ni njia ilio karibu mno kuelekea Uislam, kwa sababu yale wayafanyayo kuonyesha dalili, na matamko rasmi ya kisheria ili kuthibitisha ukweli wa madhehebu yao, ni jambo ambalo sijaliona katika vikundi vingine humu (nchini) Sudan.

Lakini tatizo lao ni kuwa madhehebu hii waliojijengea yashabihiana mno na kanuni za hisabati, kwani yenyewe ni desturi na kanuni iliyoganda, hutekelezwa bila ya kuwa na akisi ya kimaendeleo iliyo wazi katika maisha ya mwanadamu. Na katika fani ya kuamiliana na dunia hii katika nyanja tofauti za mtu mmoja au za kijamii au ya kiuchumi au kisiasa… na hata jinsi ya uhusiano na Mwenyezi Mungu (s.w.t).

Bali ni kinyume kabisa mara nyingi humfanya mtu awe mkiwa mwenye kujitenga mbali na jamii, kwa aliyonayo miongoni mwa ufinyu wa fikra katika kila mikato yake. Mtu miongoni mwao hawezi kuishi na jamii bali

huwa ni mwenye kujipambanua mbali nao kwa vazi lake na mwenendo wake na katika kila sehemu ya maisha yake, na hata jinsi ya uongeaji wake, hazoeani ila na watu wa aina yake.
Nilikuwa nahisi kuwa wameghurika na wenye kiburi na dharau kwa kuwa wao huwaangalia watu wengine wakijiona wao wako juu, hawana maingiliano nao wala hawashirikiani nao katika maisha yao.

Vipi watashirikiana nao?! Hali kila lifanywalo na jamii – ya kiislamu - kwao ni bidaa na upotovu. Mimi nakumbuka vyema ulipoingia mvuto wa kiwahabi kijijini petu katika muda mfupi na bila ya darasa lolote wala uelewa, kundi kubwa la vijana walijiunga kwenye uwahabi, hawakuendelea muda mwingi wote walijitoa, na hili lilikuwa ndio tazamio langu, kwa sababu madhehebu mpya imewazuia kuchanganyika na jamii na iliwaharamishia kawaida nyingi ambazo walilelewa nazo, hali zikiwa haziendi kinyume na dini.

Na jipya nikumbukalo ni kuwa, miongoni mwa vitu ambavyo vijana waliojiunga na uwahabi walikuwa wanataabika navyo, ni kwamba ilikuwa ni kawaida kijijini petu vijana zama za usiku wa mbaramwezi hujumuika na kuketi kwenye mchanga ulio safi wanapitisha wakati wao huko, nao ni wakati pekee wa kuonana vijana wa kijijini ambao wanafanya kazi mchana kutwa katika mashamba yao na katika shughuli zao walizozizoea, basi Sheikh wao alikuwa anawazuia kufanya hivyo na kuwaharamishia tendo hilo kwa hoja ya kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ameharamisha kukaa njiani, japokuwa sehemu hizi hazizingatiwi kuwa ni njia.

Na la pili, nalo ni tatizo la kila wahabi, kuwa mmoja miongoni mwao kwa muda mdogo wa kuwa mwanadini na kwa elimu ndogo aliyonayo, mara anakuwa mufti anayo haki ya kutoa fatwa kuihusu mas’ala yoyote iwayo. Nakumbuka siku moja mmoja wao alikuwa ameketi na mimi nikijadiliana naye katika mambo mengi, katikati ya mjadala aliinuka aliposikia sauti ya adhana ya magharibi kutoka msikiti wao, nilimwambia: Tulia hebu tukamilishe mazungumzo yetu.

Akasema: Hapana maongezi, umeingia wakati wa swala, haya twende tuswali msikitini. Nilimwambia: Mimi nitaswali nyumbani mwangu. Japokuwa nilikuwa nadumisha kuswali nao, lakini akasema kwa sauti ya juu kabisa: Swala yako ni baatili.

Nilisitushwa na kauli hii, na kabla sijapata tafsiri aligeuza mgongo wake aondoke, nilimwambia: Ngoja kidogo, nini sababu ya kubatilika kwa swala yangu nyumbani? Alisema (kwa fahari kabisa na kujisikia): Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) amesema: “Hapana swala kwa aliye jirani na msikiti ila ndani ya msikiti.”

Nilimwambia: Hapana tofauti juu ya ubora wa swala ya jamaa msikitini, lakini hilo halimaanishi kuondoa usahihi wa Swala mahali pengine, na Hadith inalenga kutilia nguvu ubora huu, hailengi kubainisha hukumu ya swala nyumbani, na dalili juu ya hilo ni kwamba hatujaona katika fiq’hi kuwa miongoni mwa yabatilishayo swala ni kuswali nyumbani, wala mwanachuoni yeyote hajatoa fatwa katika mas’ala hii.

Pili ni kwa haki gani uliyonayo inayokufanya utoe hukumu kama hizi?! Je hivi wewe ni mwanachuoni?! Na ni vigumu sana mtu atoe fatwa na abainishe hukumu ya maudhui maalum, mwanachuoni huzifanyia darasa nususu zote mfano wa mahali hapa, na apaswa atambue dalili ya amri na katazo katika nassu, je amri hii yajulisha wajibu au istih’babu, na katazo je lajulisha uharamu au ni makuruhu, dini hii ina kina kirefu basi ingia humo polepole.

Alianza kutetereka usoni kwake, alikunja uso na alifura kisha akasema: Wewe unaifanyia tafsiri Hadith na tafsiri ni haram.” Na alikwenda.

Jambo langu niliacha hesabu yake kwa Mwenyezi Mungu kutokana na mpumbavu huyu ambaye hafahamu kitu.
Akili hii ngumu kama jiwe, ilikuwa sababu ya pili ambayo ilinizuia nisiwe wahabi, japokuwa niliathirika sana na fikra zao, kwa hiyo nilikuwa ninashikamana nazo na kuzihami.

Nilibaki katika hali hii kwa muda nikiyumba sina kituo wala mwelekeo, nakuwa karibu na uwahabi wakati mwingine na najiweka mbali nao wakati mwingine, na niliona kuwa ufumbuzi pekee mbele yangu badala ya chuo cha mafunzo ya kijeshi, nisome katika chuo au chuo kikuu cha kiislam ili niendelee na utafiti wangu kwa njia ya undani na mazingatio zaidi.

Na baada ya mtihani wangu wa kujiunga na chuo kikuu, kulikuwa na mapendekezo sita kutoka vyuo vikuu na taasisi ambazo mwanafunzi angependa kusoma. Sikuchagua isipokuwa vyuo vikuu, na vyuo vya kiislam. Na nilikubaliwa katika kitivo miongoni mwa vitivo vya kiislam, (nacho ni kitivo cha masomo ya kiislam na kiarabu katika chuo kikuu cha Wadi Nnil Sudan).

Niliruka kwa furaha, na nilijiandaa kwa ajili ya daraja hii mpya maishani mwangu. Na baada ya mazoezi ya kijeshi (Ulinzi wa raia) ambao haiwezekani kujiunga na chuo kikuu ila baada ya kumaliza mazoezi hayo, misafara ya wawakilishi ilianza kutoka pande tofauti za Sudan ikija chuo kikuu na mimi nilikuwa wa kwanza wao, na wakati wa mahojiano, mkuu wa chuo aliniuliza mtu ambaye nimevutiwa naye mno maishani mwangu? Nilimwambia: Jamaludin Afghaniy, na nilimfafanulia siri ya kuvutiwa kwangu naye… alionyesha kufurahiwa kwake na maneno yangu. Na baada ya maswali mengi nilikubaliwa rasmi chuoni. Na baada ya hapo niliingia maktaba ambayo ilikuwa na vitabu vingi na vitabu vya rejea vikubwa, kwa hiyo nikawa nimejiambatanisha nayo, lakini tatizo ambalo lilinikabili ni nianzie wapi? Na kitu gani nisome?!

Nilibaki na hali hii, natoka kitabu hadi kitabu, kabla sijajiwekea utaratibu, mmoja katika watu wa ukoo wangu alinifungulia mlango mpana na muhimu wa kutafiti na kuchimba. Nao ni somo la historia na kufuatilia madhehebu za kiislam ili kuitambua iliyo ya kweli kati ya hizo madhehebu. Na ufunguzi huu ulikuwa ni taufiki ya kiungu ambayo haikuwa katika hesabu yangu, nilipokutana na ndugu yangu wa ukoo wa Abdul Mun’imu, ambaye ni mhitimu wa chuo kikuu cha sharia, nyumbani kwa mtoto wa ammi yangu katika mji wa Atibarah.

Na kabla ya kuzama jua, nilimuona katika ukumbi wa nyumba akijadiliana na mtu mmoja miongoni mwa Ikh’wanul’muslimina ambaye alikuwa mgeni nyumbani, nilisikiliza ili nione wanachojadiliana, niliharakia kuwaendea, hivyo nilipojua hali ya mjadala kuwa ni katika mambo ya dini. Niliketi karibu yao nikiangalia maendeleo ya mazungumzo ambayo Abdul’mun’im alitambulika kwa utulivu kabisa licha ya kuwepo kwa ghasia na hujuma upande wa pili, sikuwa najua aina ya mjadala kiukamilifu mpaka aliposema ndugu mwislamu: “Shia ni makafiri mazandiki!!”

Hapo nilitanabahi na niliangalia kwa makini, lilizunguka akilini mwangu swali la kushangaza: Shia ni akina nani? Na kwa nini wao wazingatiwe kuwa makafiri? Hivi Abdul Mun’im ni Shia? Na asemayo si usemi wa kawaida, je huo ndio usemi wa Shia?!.

Kwa ajili ya kuchunga insaafu kwa kweli Abdul’mun’imu alimkwamisha hasimu wake katika kila mas’ala iliyoletwa kwenye mjadala, achia mbali busara ya maneno yake na nguvu za hoja yake.

Na baada ya kumalizika mazungumzo, na kutekelezwa kwa swala ya magharibi nilijitenga na mwenzangu Abdul’mun’im, nilimuuliza kwa heshima zote: Hivi wewe ni Shia? Shia ni akina nani? Wapi ulijuana nao?

Akasema: Polepole..... swali baada ya swali.

Nilimwambia: Samahani, mimi ningali nimeshangazwa na niliyosikia toka kwako.

Akasema: Huu ni utafiti wa muda mrefu, na ni juhudi ya miaka minne kwa taabu na mashaka, na yasikitisha kuwa tija haijatumainiwa.

Nilimkatisha: Ni tija gani hii?

Akasema: Rundo za ujinga na kufanywa wajinga, tumeishi na hali hiyo maisha yetu yote tukikimbia nyuma ya jamii zetu bila ya kuuliza, je dini tuliyonayo ndiyo iliyokusudiwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t.), nayo ndio Uislam? Na baada ya mjadala ilibainika kuwa haki ilikuwa upande wa njia ya mbali zaidi kwa kufanya taswira kwa mtizamo wangu, nao ni Shia.

Nilimwambia: Labda wewe umefanya haraka..... au umechanganya mambo..!

Alitabasamu huku akisema: Kwa nini wewe haufanyi utafiti kwa kuzingatia na kuvuta subira? Na hasa ikizingatiwa kuwa ninyi mnayo maktaba hapo chuoni, itakusaidia sana kwa jambo hili. Nilisema katika hali ya (kustaajabishwa): Maktaba yetu ni ya kisunni, vipi niutafiti Ushia?!

Akasema: Miongoni mwa dalili za ukweli wa Shia wanatoa dalili ya kuwa kwake sahihi kutoka vitabu vya riwaya za wanavyuoni wa kisunni, humo ndio ukweli wao wadhihiri kwa sura ya wazi zaidi.

Nilisema: Hivi vyanzo vya Shia ni vilevile vyanzo vya Ahli Sunnah?!

Alijibu: Hapana, Shia wana vyanzo mahsusi vinavyovizidi mara kadhaa vyanzo vya Ahli Sunnah, riwaya zake zote zimeelezwa na Ahlul-Bayt (a.s.) kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), lakini wao hawatolei hoja kwa Ahli Sunnah kupitia riwaya zitokazo kwenye vyanzo vyao, kwa kuwa wao masunni hawana ulazima nazo, hivyo basi hapana budi watoe hoja dhidi yao kwa dalili wanazozikubali, yaani (kulingana na usemi mashuhuri): Walazimisheni kwa ambalo wamejilazimisha nalo wao wenyewe.

Yalinifurahisha maneno yake na mwitikio wangu kuuelekea mjadala ulizidi. Nilimwambia: Nitaanzaje? Akauliza je katika maktaba yenu kuna Sahih Bukhari na Sahih Muslim, Musnad Ahmad, Tirmidhiy na Nasaiy? Nilisema: Ndio, tuna kiwango kikubwa cha vyanzo vya Hadith.

Akasema: Anza na hivi, kisha baada ya hapo njoo kwenye tafsiri, na vitabu vya historia, kwa kuwa katika vitabu hivi kuna Hadithi zinazojulisha wajibu wa kuifuata madrasa ya Ahlul-Bayt. Alianza kuniorodheshea mifano, pamoja na kutaja chanzo na namba ya jalada na ukurasa.

Nilisimama nimeduwaa, nikizisikiliza Hadithi hizi ambazo sijapata kuzisikia hapo kabla, ilinifanya niingie shaka kuwepo kwake katika vitabu vya kisunni, lakini haraka sana aliikata shaka hii kwa kauli yake: Zisajili Hadithi hizi, kisha zitafute katika maktaba na tukutane siku ya Alhamisi ijayo kwa idhini yake Allah.

Chuoni:

Baada ya kuzifuatilia zile Hadithi katika Bukhari, Muslim, na Tirmidhiy huko maktaba ya chuo chetu, ulinithibitikia ukweli wa usemi wake, na nilisitushwa na Hadithi zingine zilizo zaidi ya hizi kwa dalili za wajibu wa kuwafuata Ahlu-Bayt, jambo lililonifanya niishi katika hali ya mshtuko. Kwa nini hatujasikia Hadithi hizi hapo kabla.
Nilizionyesha kwa baadhi ya wenzangu chuoni ili washirikiane na mimi katika wakati huu muhimu, baadhi waliathirika na baadhi hawakujali, lakini mimi niliazimia kuendelea na uchunguzi hata kama kufanya hivyo kutanigharimu umri wangu wote. Ilipowadia siku ya Alhamisi, nilikwenda kwa Abdul’mun’imu, alinipokea kwa mapokezi mema kwa utulivu na akasema: “Ni wajibu juu yako usiharakie na uendelee na utafiti kwa ufahamu wote.”

Kisha tulianza uchambuzi wa mambo mengine mbalimbali, uliendelea mpaka jioni ya siku ya Ijumaa, nilifaidika na mengi na nilivijua vitu vingi ambavyo nilikuwa sivijui, na kabla ya kurejea kwangu chuoni aliniomba vitu vingi nivitafute.

Iliendelea hali kama hii kwa muda, na hali ya mjadala kati yangu na yeye ilikuwa ikibadilika kati ya muda na muda, kwani wakati mwingine nakuwa mkali wa maneno kwake, na pengine nafanya inadi kwenye ukweli uliowazi. Kwa mfano nilikuwa ninaporejea baadhi ya Hadithi katika vyanzo na ninakuwa na uhakika kuwa ipo, huwa namwambia: “Kwa kweli Hadithi hizi hazipo.” Mpaka sasa sijui ni kitu gani kilikuwa kinanisukuma nifanye hivyo ila ni kutambua kushindwa na utashi wa ushindi.

Kwa sura kama hii na kwa uchambuzi wa ziada mbele yangu ukweli mwingi ulifichuka mbele yangu ambao ilikuwa sikuutazamia, na nilikuwa katika muda wote huu nafanya mjadala sana na wanafunzi wenzangu, na wenzangu walipoona nawakera waliniomba nijadiliane na Dkt. aliyekuwa akitufundisha Fiq’hi, nikasema: Hapana kizuizi kwangu, lakini tu kuna vizuizi kati yangu na yeye ambavyo vinanizuia kuwa na uhuru wa kuongea. Hawakukinaika na hili, na wakasema: Kati yetu na wewe kuna Ustadh, ukimtosheleza sisi tu pamoja na wewe.

Nikasema: Mas’ala sio kutosheka, bali ni dalili na uthibitisho, na kutafuta ukweli. Na katika somo la kwanza la fiq’hi nilianza mjadala naye kwa sura ya maswali mengi, nilimuona hanipingi sana bali ni kinyume alikuwa anatilia mkazo kuwapenda Ahlul-Bayt (a.s.) na kuwa kuwafuata na kuzitaja fadhila zao ni lazima.

Na baada ya siku nyingi aliniomba niende kwenye maktaba yake kwenye makao ya chuo na baada ya kwenda kwake alinipa kitabu chenye juzuu kadha nacho ni (Sahihul-Kaafiy), ambacho ni miongoni mwa vyanzo vya Hadithi vinavyoaminika mno kwa Shia. Aliniomba nisikipuuze kitabu hiki kwa kuwa ni turatha ya Ahlu-Bayt. Sikusema kitu kwa situkizo kama hili, nilichukua kitabu na nilimshukuru kwa hilo.

Nilikuwa nakisikia kitabu hiki na sikupata kukiona, ni jambo ambalo lilinifanya nimshuku kuwa ni Shia Dr. huyu, pamoja na kuwa namtambua kuwa ni mfuasi wa Malik, na baada ya swali na kutaka tafsiri yake ilinibainikia kuwa yeye ni Sufiy, ni mwenye kujihusisha na kuwapenda Ahlul-Bayt (a.s.).

Na wenzangu walipotambua maafikiano haya kati yangu na huyu ustadh, waliniomba nifanye mjadala na ustadhi mwingine aliyekuwa akitusomesha mada ya Hadith, na alikuwa mtu wa dini sana mnyenyekevu mwenye tabia njema. Na nilikuwa nampenda sana, nilikubali ombi lao, na ilianza kati yetu mijadala mingi, na nilikuwa namuuliza usahihi wa baadhi ya hadithi, alikuwa anatilia mkazo kuwa ziko sahihi, na baada ya muda nilihisi kutopenda kwake na kutoridhika kwake na mjadala wangu, pia wenzangu walihisi hivyo, hapo niliwaza njia bora ya kuendelea na mjadala ni maandishi.

Hivyo basi nilimwandikia jumla ya Hadithi na riwaya ambazo kwa wazi zajulisha wajibu wa kufuata madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) na nilimwomba atafiti usahihi wake. Na nilikuwa namuuliza kila siku juu ya majibu, naye hutoa udhuru kuwa hajafanya utafiti. Nilimfuatilia kwa njia hii mpaka alihisi kuwa namdhiki.
Akaniambia zote ni sahihi. Nikasema kwa kweli ziko wazi zikihusu wajibu wa kuwafuata Ahlul-Bayt. Hapo hakujibu na aliondoka haraka kwenda maktaba.

Mwenendo huu ulikuwa ni situsho kwangu na ni jambo lililonifanya nione ukweli wa usemi wa Shia. Lakini nilipenda kwenda polepole na kutoharakia hukumu.

Na miongoni mwa ajabu ya tukio la bahati ni kwamba mkuu wa chuo naye ni ustadhi Ulwan, alikuwa anatusomesha somo la tafsiri, siku moja akasema katika kutafsiri kauli yake (s.w.t): “Kwa kweli Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alipokuwa Ghadiir Khum, alinadi kuwaita watu wakajikusanya, aliushika mkono wa Ali (a.s.) akasema: “Ambaye mimi ni mtawala wake hivyo Ali ni mtawala wake.”

Tukio hili habari zake zilienea nchini na zilimfika Al-Harith bin Nu’man Al-Fahri, huyu bwana alimwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) akiwa juu ya ngamia wake, alimsimamisha ngamia wake na aliteremka na akasema: “Ewe Muhammad, umetuamrisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu tushuhudie kuwa hakuna miungu ila Allah na kuwa wewe ni Mjumbe Wake, hilo tulilikubali kutoka kwako, na ulituamrisha tuswali Swala tano tukakubali, na ulituamrisha kutoa Zaka tulikubali, na ulituamrisha tufunge mwezi wa Ramadhan tukakubali, na ulituamrisha kuhiji tukakubali, halafu haukuridhika na hayo mpaka umenyanyua mabega ya mtoto wa ami yako ukimfadhilisha juu yetu na ukasema: “Ambaye mimi ni mtawala wake hivyo Ali ni mtawala wake.” Je kitu hiki ni kutoka kwako au ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu?

Nabii (s.a.w.w) akasema: “Naapa Mwenyezi Mungu ambaye hakuna miungu ila ni Yeye, kwa kweli hili ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyetukuka.”

Al-Harith aligeuka kumuelekea ngamia wake huku akisema: “Ewe Mwenyezi Mungu ikawa ayasemayo Muhammad ni haki, basi tutiririshie mvua ya mawe toka mbinguni, au tuteremshie adhabu iumizayo.” Hakuwahi kufika kwenye ngamia wake ila Mwenyezi Mungu alimtupia jiwe lililoanguka kichwani kwake na lilitoka kwenye tundu yake ya chini. Hapo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliteremsha Aya:

سَأَلَ سَائِلٌ بِعَذَابٍ وَاقِعٍ {1}

لِلْكَافِرِينَ لَيْسَ لَهُ دَافِعٌ {2}

مِنَ اللَّهِ ذِي الْمَعَارِجِ {3}

“Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayotokea. Juu ya makafiri, hapana awezaye kuizuia. Kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye utukufu mkubwa.” (Sura Maarij: 1 -3).

Na baada ya kumaliza darasa, mmoja katika rafiki zangu alikutana naye, na alimwambia: “Kwa hakika uliyosema ni maneno ya Shia.” Ustadhi alisimama kidogo kisha alimwangalia huyu mpinzani na akamwambia: ‘Niitie Muutaswim aje kwenye ofisi ya idara..! Nilistaajabishwa na wito huu. Niliogopa kukutana na ustadh, lakini nilikata shauri na nilikwenda kwake, na kabla sijakaa akasema: “Wanasema kuwa wewe ni Shia!”

Nikasema: Mimi ni mtafiti tu.

Akasema: Kwa kweli kutafiti ni vizuri na hapana budi.

Ustadh akawa ananitajia mambo yenye utata kuwahusu Shia ambayo mara nyingi yalikuwa yanarudiwarudiwa, Mwenyezi Mungu alinisaidia kujibu kwa dalili na uthibitisho wenye nguvu mno, niliunguruma na Hadithi kwa nguvu zaidi kuliko nilivyokuwa ninategemea, na kabla sijahitimisha mazungumzo yetu aliniusia nisome Al’Muraajaati, na akasema:
“Ni katika vitabu vizuri katika uwanja huu.”

Na baada ya kuwa nimesoma kitabu Murajaati na Maalimul’madrasatayn na baadhi ya vitabu vingine, ukweli uliniwia wazi na batili ilitanzuka, kwa dalili zinazong’ara na uthibitisho utoao mwanga kuthibitisha ukweli wa madhehebu ya Ahlu-Bayt katika vitabu viwili hivi. Nguvu zangu za mjadala na utafiti zilizidi, mpaka Mwenyezi Mungu alinifichulia nuru ya ukweli moyoni mwangu, nikautangaza Ushia wangu!

Baada ya hapo nilianza ngazi mpya ya mapambano, ya wale ambao walishindwa kupata njia kwenye mjadala, ila ni kebehi, matusi, shutma, vitisho na masingizio, na yasio hayo miongoni mwa mbinu za kijinga, lakini nilihesabia hili jambo langu kwa Mwenyezi Mungu na nikafanya subira kwa yaliyojiri, japokuwa mapigo yaliyolengwa kwangu yalikuwa ni kutoka kwa rafiki zangu wapendwa mno ambao walipiga marufuku kula, na kulala chini ya sakafu moja na mimi. Na nilitengwa kikamilifu, isipokuwa na baadhi tu ya ndugu waliokuwa na ufahamu zaidi na wenye kujizuia. Na baada ya muda niliweza kurudisha uhusiano wangu na wote na kwa sura nzuri zaidi kuliko ya kwanza bali nilikuwa naheshimiwa na kuthaminiwa kati yao, na baadhi yao walikuwa wananitaka ushauri kwa dogo na kubwa katika mambo ya maisha yao.

Lakini hali hii haikuendelea muda mrefu, moto wa fitna ulilipuka upya, baada ya wanafunzi watatu walipotangaza Ushia wao, zaidi ya hapo ni kuwa kundi kubwa la wanafunzi walidhihirisha kuelemea kwangu na kuuunga mkono Ushia, hapo kukaibuka mlolongo mwingine wa mapigo na mifadhaisho, katika yote hayo tulishikamana na tabia njema za kiujumbe na hekima, kwa hiyo tuliweza kuzifyonza ghadhabu haraka iwezekanavyo.

Kijijini Kwetu:

Kijiji chetu ni Nudaa, ni miongoni mwa vijiji vidogo kaskazini mwa Sudan kwenye kingo za mto Nile, wengi katika wakazi wake ni wa kabila ya Rubaataab, kabila hili ni mashuhuri kwa werevu na haraka hudhihirikiwa, wakazi wake wanategemea mitende na kilimo cha mavuno ya msimu.

Mawahabi walifaidika na uzuri wa watu hawa kuieneza fikra ya kiwahabi, waliathiri kwa njia isio ya moja kwa moja akili zao na fahamu zao, kwa sababu ya kukithiri mihadhara na vikao wanavyofanya, mwanzo nilionyesha kujizuia, na wakati wangu niliutumia kwa kusoma na kutaka kujua na kuifanyia daawa madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) kati ya ndugu na watu wa karibu. Na ilijiri kati yangu na kaka yangu mijadala mingi na malumbano kiasi ilifikia akatae kusoma vitabu vya Shia na alinitishia kuwa ataviunguza, na baada ya mjadala niliweza kumwathiri, na alisoma baadhi ya vitabu mfano wa Ahlul-Bayt Qiyadatur-Rabbaniyah, Al’murajaatu, Maalimul’madrasatayni mpaka Mwenyezi Mungu alipomuongoza kwenye nuru ya Ahlul-Bayt (a.s.), hivyo aliutangaza Ushia wake. Ama kuhusu ahali wengine waliobaki, wengi wao wamedhihirisha kuelemea kwao na kuunga kwao mkono.

Kwa hiyo habari zangu zilienea kijijini, na nilianza kuifikisha madhehebu ya Ahlul-Bayt kwa wakazi wake wengi. Hivyo moto wa mawahabi ulikolea na ghadhabu ya wanaousambaza ikatokota, kwa hiyo ikawa kila mhadhara wao katika jambo lolote ni kuwatukana na kuwashutumu Shia na kuwasingizia, na wakati mwingine wananichokoza mimi mwenyewe, na yote hayo nilikabiliana nayo kwa uvumilivu na msamaha mwema.

Mjadala Na Sheikh Wa Kiwahabi:

Kulifanyika mazungumzo kati yangu na Sheikh wao-Ahmad al-Aminiy na nilimuomba kutumia busara na kuacha utashi, batili na hujma bila ya faida, na baada ya kuzidi kipimo na kuzidi ghasia zao na kasumba zao nilikwenda msikitini kwao na niliswali nyuma yake Swala ya dhuhuri, na baada ya kwisha Swala nilimuuliza: “Je kuna siku yoyote nilikuchokoza muda huu wote, ambao wewe unawatukana Shia na unawakufurisha kwa kutumia kipaza sauti?!”

Akasema: Hapana.
Nikasema: Wajua kwa nini?!
Akasema: Sijui.

Nikasema: Kwa hakika maneno yako ni hujuma na ujinga, na uchokozi dhidi yangu, nilihofia kukupinga ingekuwa kujihami nafsi yangu na si kuuhami ukweli, kwa hiyo sasa nakuomba mjadala wa kielimu wenye nidhamu, mbele ya wote ili ukweli ufichuke.

Akasema: Hapana kizuizi kwangu.
Nikasema: Basi ainisha duru husika za mjadala.
Akasema: Kuibadilisha Qur’anii, na uadilifu wa Sahaba.
Nikasema: Vyema, lakini kuna mambo mawili ya dharura hapana budi yajadiliwe, nayo ni sifa za Mwenyezi Mungu, na unabii katika itikadi yenu na riwaya zenu.

Akasema: Hapana.
Nikasema: Kwa nini?
Akasema: Mimi ninaainisha mjadala, mimi nikikuomba mjadala, haki itakuwa yako kuainisha mjadala.
Nikasema: Hatutofautiani (kwa hilo)…lini ahadi yetu?
Akasema: Leo, baada ya Swala ya magharibi. - Akidhania atanitisha kwa muda huu mfupi wa ahadi - basi nilidhihirisha kuafiki kwangu kwa furaha kabisa, nikatoka msikitini.

Na baada ya kutekeleza Swala ya magharibi, mjadala ulianza, sheikh wao Ahmad Amiin alianza mazungumzo kama kawaida yao kwa hujuma na kuwatuhumu Shia kwa kuifanyia Qur’anii mabadiliko (tahriif).

Mkononi mwake alikuwa ameshika kitabu Al-Khututu Al-Ariidhwa cha Muhibudin, na baada ya kumaliza maneno yake nilianza maneno yangu, nilianza kwa ufafanuzi kupinga yote aliyoyazua miongoni mwa tuhuma, na niliwatakasa Shia kwa kuwaweka mbali kabisa na usemi wa kuifanyia Qur’anii mabadiliko (tahriif), na baada ya hivyo, nilimwambia kama alivyosema Isa (a.s.):

“Mwaliona kapi machoni kwa wengine na wala hamulioni gogo machoni kwenu.”

Kwa kuwa riwaya ambazo zimo katika vitabu vya Hadithi vya masunni ni dhahiri zinaituhumu Qur’anii tukufu kuwa imefanyiwa mabadiliko (tahriif), basi kuinasibisha kauli ya mabadiliko (tahriif) kwa Sunni masafa yake ni ya karibu mno kuliko kuinasibisha kwa Shia. Nilitaja karibu riwaya ishirini pamwe na kutaja chimbuko, na namba ya ukurasa kutoka katika Sahih Bukhari, Muslim, Musnad Ahmad, Itqaan Fii Ulumil’Qur’ani ya Suyuti.

Mfano: Imam Ahmad bin Hanbal ametoa maelezo katika Musnad yake, kutoka kwa Ubayya bin Ka’ab, amesema:

“Mnaisoma Aya ngapi Sura Ahzabi?” Akasema: “Aya sabini na kidogo.”
Akasema: “Bila shaka niliisoma pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) mfano wa Baqarah au zaidi yake, ikiwemo Aya ya kupopoa mawe.”3

Na Bukhari ametoa maelezo katika Sahih yake kwa sanadi yake kutoka kwa Ibnu Abbas kuwa Umar bin Khattab alisema: “Kwa kweli Mwenyezi Mungu alimtuma Muhammad (s.a.w.w) kwa ukweli na alimteremshia kitabu ikawa miongoni mwa aliyoteremsha Mwenyezi Mungu ni Aya ya rajmu na tuliisoma na tuliitia akilini na tuliielewa ndio maana Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alifanya rajmu na tulifanya rajmu baada yake. Kwa hiyo naogopa muda ukiwa mrefu kwa watu asije kusema msemaji: Wallahi hatuikuti Aya ya rajmu katika kitabu cha Mwenyezi Mungu, kwa hivyo watapotea kwa kuacha faradhi aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu….. Kisha sisi tulikuwa tukisoma katika tuyasomayo katika kitabu cha Mwenyezi Mungu:

(Msijitenge na baba zenu, kwani bila shaka ni ukafiri kwenu kujitenga na baba zenu. Na ahakika ni ukafiri kwenu kujitenga na baba zenu.)4

Muslim ameeleza riwaya katika Sahih yake, amesema: Abu Musa alitumwa kwa wasomaji wa Qur’ani wa watu wa Basra, waliingia kwake watu mia tatu waliokuwa wamesoma Qur’ani, akasema: “Ninyi ni watu bora wa Basra, na wasomi wake, hivyo basi isomeni wala jambo lisiwe refu kwenu, nyoyo zenu zitakuwa ngumu kama zilivyokuwa ngumu nyoyo za waliokuwa kabla yenu, kwa kweli sisi tulikuwa tunaisoma Sura ambayo tulikuwa tunaifananisha na Surat al-Baraa kwa urefu na ugumu, na nimeisahau isipokuwa tu nimehifadhi katika hiyo:

“Lau mwanadamu angekuwa anamiliki bonde mbili za mali angependa awe na bonde la tatu wala tumbo la mwana wa Adamu halijai ila kwa udongo.”

Na tulikuwa tunasoma Sura tuliyokuwa tukiifananisha na mojawapo kati ya sura za Musabihati, nimeisahau ila tu nimehifadhi katika hiyo:

“Enyi mlioamini! Kwa nini mwasema msiyoyatenda, itaandikwa shahada katika shingo zenu, na mtakuja kuulizwa kwayo siku ya Kiyama.5

Nilipokuwa nazitaja riwaya hizi niligundua kuwa Sheikh alipepesa macho yake na alifungua kinywa chake na kulidhihiri hali ya kukanganyikiwa na kuduwaa usoni kwake, niliposimama kusema tu akasema: “Mimi sijasikia hivyo na mimi sijaona hilo, nakuomba ulete vyanzo hivi mbele yangu.

Nilisema: Muda mfupi uliopita ulikuwa unawahujumu Shia na ukiwatuhumu kuwa wanafanya mabadiliko (tahriif), kwa nini hukuleta vitabu vyao ambavyo haujaviona maisha yako yote, wewe walazimika kuleta rejea zako na hii ni maktaba yako, kuna Bukhari, Muslim na vitabu vya Hadith, vilete nikutolee riwaya hizi kutoka humo!

Na alipokosa upenyo alirukia maudhui nyingine, nayo ni: Shia wanasema Taqiya, vipi tutasadiki maneno yao?! Alifanya fujo na vurugu mpaka mmoja wao aliposimama kutoa adhana ya Swala ya Isha, na baada ya Swala tuliahidiana tukamilishe mjadala siku zijazo, kwa sharti tuwe tunachagua maudhui tutakayojadili.

Na kesho ilipowadia nilikuwa nimeketi mbele ya nyumba yetu asubuhi punde Sheikh alipita na alinisalimia kwa heshima zote na akasema: “Kwa kweli mijadala kama hii hawawezi kuelewa watu wa kawaida, ni bora tuongee na kujadiliana mimi na wewe tukiwa peke yetu.” Nikasema ninaafiki, lakini kwa sharti uache hujuma dhidi ya Shia, baadae hatukumsikia akiwahujumu Shia.

  • 1. Biharul’anwar. Juz. 5, Uk. 204.
  • 2. Al-U’rwatul’wuthqa ni jarida alikuwa analitoa Jamalu-din na mwanafunzi wake
    Muhammad Abduh huko London.
  • 3. Musnad Ahmad, jalada,5,Uk.131.
  • 4. Sahih Bukhari, Juz.8. Uk. 26, Rajmul’hubla mina zina idha ahswanat.
  • 5. Sahih Muslim, Juz. 3, Uk. 155, mlango wa Lau mwana adamu……