read

Mlango Wa Nne

Je Ahlul-Bayt Ni Nani?

Utafiti huu ni miongoni mwa tafiti za wazi mno, kwa kuwa mtu hawezi kujifanya hawajui Ahlul-Bayt, ila yule mkaidi ambaye hajapata upenyo wa kuzikimbia dalili za kata shauri za kuwajibika kuwafuata. Hivyo basi mtu kama huyu huwa anageukia kwenye mbinu za kuwatilia shaka. Na hili ni ambalo nimelishuhudia mimi mwenyewe nilipokuwa nikijadiliana na baadhi ya ndugu na jamaa, basi pindi mmoja wao anapokosa upenyo wa kuikwepa lazima ya kuwafuata Ahlul-Bayt utamkuta moja kwa moja analeta maswali yasiyofahamika: Ahlul-Bayt ni nani? Je wake zake sio ahali zake?! Je Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) hajasema: Salman ni miongoni mwetu Ahlul-Bayt?! Bali je Abu Jahli pia sio miongoni mwa ahali wake (s.a.w.w)?!

Wala hakusudii lolote kwa maswali yote haya isipokuwa kukanusha ukweli wa Hadithi ya Vizito Viwili kuwa ni miongoni mwa hadithi zinazojulisha uimamu wa Ahlul-Bayt, akidhania kwa maswali haya ya kuduwaza yasiyo wazi anaweza kuinyamazisha akili yake na wito wa dhamiri yake, lakini umbali ulioje hoja ipo hadhiri sawa akanushe au asikanushe.

Nilikuwa ninasema kwa baadhi yao mtu anapouliza maswali kama haya: Kwa nini ninyi mnataka kila kitu kiwe kimekwisha andaliwa mkipate bila ya taabu wala kutafiti?! Kwa kweli fikra zilizowekwa kwenye mkebe hazifai.

Mimi naweza kujibu na ninyi mwaweza kupinga majibu yangu na mkayakanusha na mkayapinga kwa kuwa ninyi hamjaonja uchungu wa utafiti na wala hamjavumilia mashaka ya kujibu.

Halafu je hivi mimi ni peke yangu ndiye nilazimikae kujibu? Je Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ameniamuru kushikamana na Ahlul-Bayt mimi tu khususan?! Sisi sote ni mukalafu na ni wajibu juu yangu na juu yenu kujibu, kwa sababu hoja imethibiti kwetu kuwa ni wajibu kuwafuata Ahlul-Bayt, na kuichukuwa dini kutoka kwao, kwa hiyo yalazimu kuwatambua na halafu kuwaiga wao?!

Na mimi pia hapa, sitoi dalili na uthibitisho kwa upana, ila tu natosheka na baadhi ya ishara za wazi, na mwenye kutaka ziyada ni juu yake kujipanua.

Ahlul-Bayt Katika Aya Ya Tohara:

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنْكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا {33}

“Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba, na kukutakaseni kabisa.” (Sura Ahzab: 33).

Kwa kweli kuteremka kwa Aya hii iliyobarikiwa kuwahusu Ali, Fatima, Hasan na Husein, ni miongoni mwa mambo yaliyo wazi mno kwa mwenye kufuatilia vitabu vya hadithi na tafsiri.

Ibnu Hajar anasema kwa lengo hili: “Kwa kweli wafasiri wengi wanasema kuwa hii Aya ilishuka kuwahusu Ali, Fatima, Hasan na Husein.”1

Na Aya hii kwa dalili yake iliy wazi juu ya umaasumu wa Ahlul-Bayt haina uwiano ila na wao, kwa lile ambalo tumeliwadhihisha hapo kabla, kwa sababu wao ni thamani ya umma huu. Na ni maimamu waongozi baada ya Mtume (s.a.w.w), na kwa sababu hiyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) aliamuru kuwafuata.

Na ufidishaji wa umaasumu kutokana na Aya hii ni wa wazi kwa mwenye moyo wa kuelewa au akapewa usikivu akiwa hadhiri. Hiyo ni kwa sababu ni muhali kulikosa kusudio ikiwa mkusudiaji ni Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Na zana ya kifungo ya kilugha iliyotumika ni shahidi juu ya hilo. La muhimu kwetu hapa ni kuthibitisha kuwa Aya hii khususan iliteremka kwa ajili ya Ali, Fatma Hasan na Husein (a.s.).

Hadithi Ya Kishamia Ni Kiainishi Cha Utambulisho Wa Ahlul-Bayt:

Dalili zilizo karibu mno na za wazi mno ni yale yaliyokuja katika tafsiri ya Aya hii miongoni mwa riwaya, khususan ile iliyojulikana kwa wanahadithi kuwa ni Hadithi ya Kishamia, usahihi wake na kufululiza kwake sio kuchache kwa kuilinganisha na Hadithi ya Vizito Viwili.
A) Al-Hakim ameeleza ndani ya kitabu chake cha Al-Mustadrak Alas- Swahihayni Filhadithi: “Kutoka kwa Abdullah bin Ja’far bin Abu Talib kuwa yeye amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alipoangalia rehema inashuka alisema: ‘Niitieni, niitieni.’ Safiyya akasema: ‘Nani ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?’ Akasema: ‘Ahlul-Bayt wangu, Ali, Fatima Hasan na Husein.’ Hatimaye wakaletwa. Nabii (s.a.w.w) aliwafunika shuka yake, halafu alinyanyua mikono yake na akasema: ‘Ewe Allah hawa ni ahali wangu. Mtakie rehema Muhammad na Aali Muhammad.’ Mwenyezi Mungu mwenye enzi na utukufu akateremsha:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنْكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا {33}

“Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba, na kukutakaseni kabisa.” (Sura Ahzab: 33).”2

Al-Hakim amesema: “Hadithi hii sanad yake ni sahihi.”

B) Na Al-Hakim ameeleza riwaya nyingine mfano wa hii, kutoka kwa Ummu Salamah akasema: “Nyumbani mwangu iliteremka: “Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba” ndipo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) akatuma waitwe Ali, Fatima, Hasan na Husein, akasema: ‘Ewe Allah! Hawa ndio Ahlul-Bayt wangu.”3

Halafu al-Hakim akasema: “Hii ni sahihi kwa sharti ya Bukhari.” Na ameieleza mahali pengine kutoka kwa Wathilah akasema: “Ni sahihi kwa sharti ya wawili, Bukhari na Muslim.”

C) Muslim ameieleza ndani ya Sahih yake kutoka kwa Aisha akasema: “Alitoka Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) asubuhi akiwa na shuka ya manyoya meusi, punde alikuja Hasan bin Ali akamwingiza halafu alikuja Husein akamwingiza halafu alikuja Fatima akamwingiza halafu alikuja Ali akamwingiza halafu akasema:

‘Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba, na kukutakaseni kabisa.”4

Na habari hizi zimekuja ndani ya riwaya nyingi katika vitabu Sahihi na vitabu vya Hadithi na Tafsiri.5 Nazo ni katika habari zilizo sahihi zilizofululiza, hakuna yeyote aliyezidhaifisha miongoni mwa wa mwanzo na wa mwisho. Tukizitaja riwaya hizi zote nafasi itatuwia ndefu, hivyo mimi nimezihesabu miongoni mwazo riwaya ishirini na saba, zote ni sahihi.

Na miongoni mwa riwaya zilizo wazi mno ndani ya mlango huu katika kuwaainisha Ahlul-Bayt mbali na wengine miongoni mwa wake wa Nabii (s.a.w.w), ni riwaya aliyonakili Suyuti iliyomo ndani ya Durul-Manthur kutoka kwa Ibnu Mardawayhi kutoka kwa Ummu Salama akasema:

“Iliteremka Aya hii chumbani mwangu: “Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba, na kukutakaseni kabisa,” hali ndani ya chumba mkiwa waheshimiwa saba:
Jibril, Mikail, Ali, Fatima, Hasan, na Husein, hali mimi nikiwa kwenye mlango wa chumba. Nilisema: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi si katika Ahlul-Bayt?!’ Alisema: ‘Kwa hakika wewe uko katika kheri, kwa hakika wewe ni miongoni mwa wake wa Nabii.”6

Na katika riwaya ya Al-Hakim katika Mustadrak yake ni kuwa Ummu Salamah alisema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mimi si katika Ahlul-Bayt?!” Akasema (s.a.w.w): “Kwa hakika wewe uko katika kheri kwa hakika wewe ni miongoni mwa wake wa Nabii. Ewe Mwenyezi Mungu wangu Ahlul-Bayt wangu ni wenye haki zaidi.’’7

Na ilivyo katika riwaya ya Ahmad ni: “Nikainua Kishamia ili niingie akakivuta toka mkononi mwangu na akasema: ‘Kwa hakika wewe u kati- ka kheri.”8

Katika hayo inatosha kuthibitisha kuwa Ahlul-Bayt wao ndio watu wa kishamia kwa ibara za wazi mno na matamshi safi sana. Kwa hiyo wao wanakuwa kizito ambacho ni pacha wa Qur’ani ambacho Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ametuamrisha katika Hadithi ya Vizito Viwili kushikamana nacho.

Na mwenye kusema kuwa al-Itrah (kizazi) maana yake ni karaba ili aigeuze maana, usemi wake huu haukubaliwi, kwa kuwa hilo halijasemwa na yeyote miongoni mwa maimamu wa lugha ya kiarabu. Ibnu Mandhur amenakili katika Lisanul-Arab: “Kwa kweli Al-Itrah wa Mtume ni watoto wa Fatima (r.a).” Hii ni kauli ya Ibnu Sayida.

Na Al-Azhariy amesema: “Na katika hadithi ya Zayd bin Thabit amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w)... - na anaitaja Hadithi ya Vizito Viwili – akajaalia al-Itrah kuwa ni Ahlul-Bayt. Na Abu Ubaida na wengineo wakasema: ‘Al-Itrah wa mtu na familia yake na jamaa zake ni watu wake wa karibu. Ibnu Al-Athir amesema: Itrah wa mtu ni jamaa mahsusi wa karibu mno wa mtu. Na Ibnu Al-Arabiy amesema: Al-Itrah ni mtoto wa mtu na dhuria wake na wajukuze wa kutoka mgongoni mwake.

Kwa hiyo Al-Itrah wa Nabii (a.s.) ni watoto wa Fatima al-Batul (a.s).”9

Kutokana na maana hii inabainika kuwa Ahlul-Bayt sio ndugu wote wa karibu walio kwenye maana ya jumla ya neno Ahlul-Bayt, bali wao ni ndugu wake wa karibu mahsusi. Kwa minajili hiyo Zaid bin Arqam alipoulizwa kulingana na riwaya ya Muslim, wakasema: “Ahlul-Bayt wake ni nani, ni wakeze?” Alisema: “Hapana namuapa Mwenyezi Mungu, kwa hakika mwanamke huwa na mtu muda katika zama halafu anamtaliki na atarejea kwa baba yake na kaumu yake....Ahlul-Bayt wake (s.a.w.w) ni asili yake na ndugu zake wa kiumeni, ambao kwamba wameharamishiwa sadaka baada yake....

Kama ambavyo utukufu wa kunasibika na Ahlul-Bayt hakuudai mtu yoyote miongoni mwa jamaa wa karibu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), wala wakeze. Kama si hivyo historia ingetuhadithia hilo, wala hapana katika historia wala Hadithi kuwa wake wa Nabii (s.a.w.w) walitoa hoja kwa Aya hii na kudai utukufu huu, kinyume na Ahlul-Bayt, kwani huyu hapa Jemedari wa waumini (a.s.) anasema: “Kwa hakika Mwenyezi Mungu Mwenye enzi na utukufu ametufanya bora sisi Ahlul-Bayt. Na vipi isiwe hivyo hali Mwenyezi Mungu mwenye utukufu na enzi anasema kitabuni mwake: “Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba, na kukutakaseni kabisa.

Kwa kweli ametutoharisha Mwenyezi Mungu kwa kutuweka mbali na yasiyopendeza, yaliyo dhahiri miongoni mwayo na yaliyofichika. Hivyo sisi tuko katika njia ya haki.”

Na mwanawe Hasan (a.s.) amesema: “Enyi watu, mwenye kunijua amenijua na asiyenijua basi mimi ni Hasan bin Ali, na mimi ni mtoto wa mbashiri, mwonyaji, mlinganiaji wa Mwenyezi Mungu kwa idhini yake, na ambaye ni taa itoayo nuru. Mimi ni katika Ahlul-Bayt, ni katika jumla ya watu wa nyumba ambayo ndani yake Jibril alikuwa anateremka na anapanda, na mimi ni katika Ahlul-Bayt ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na amewatoharisha kabisa.”

Na mahali pengine anasema: “Na ninasema enyi viumbe sikieni, na nyinyi mna nyoyo na masikio, fahamuni kuwa sisi ni Ahlul-Bayt, Mwenyezi Mungu ametupa heshima kwa Uislamu, ametuchagua na kututeua, hivyo akatuondolea uchafu na ametutoharisha kuwa safi kabisa.”

Hoja ya Ibnu Kathiir kuwa kuna ulazima wa kuwaingiza wake wa Nabii (s.a.w.w) katika Aya hii kulingana na muktadha wa muundo wa sentensi, haina nafasi hapa. Kwa kuwa hoja ya udhahiri hutegemea umoja wa maneno, na yajulikana kuwa usemi umebadilika kutoka dhamiri ya kike katika Aya zilizoitangulia Aya hii, na kuwa ya kiume, hivyo basi ikiwa makusudio ya Aya hii ni wakeze usemi utakuwa:

Kwa sababu Aya ziko mahsusi kwa wanawake, kwa ajili hiyo ameanza tena Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kauli yake baada ya Aya hii:

Wala hajapata kusema yoyote kuwa Aya ya tohara iliteremka kuwahusu wake wa Nabii (s.a.w.w) ila Ikrimah na Muqatil. Kwa hiyo Ikrima alikuwa akisema: “Mwenye kutaka nitaombeana naye laana, bila shaka yenyewe iliteremka ikiwahusu wake za Mtume (s.a.w.)”10 Maneno haya ya Ikrima hayakubaliki kwa kupingana kwake na riwaya zilizo sahihi na safi, kama ilivyotangulia kuwa Ahlul-Bayt ndio watu wa Kishamia.

Pili: Ni jambo gani lilimtikisa Ikrima na kuichochea ghadhabu yake kiasi cha kufikia anadi sokoni kutaka kulaaniana? Ni kwa sababu ya kuwapenda wake wa Nabii au ni chuki dhidi ya waliofunikwa na Kishamia? Ni haja ipi inapelekea kulaaniana ikiwa kweli inakubalika kuwa iliteremka kwa ajili ya wake wa Nabii (s.a.w.w.)?! Au rai ya walio wengi na iliyotawala ni kuwa iliteremka kumhusu Ali, Fatima, Hasan na Husein?! Na ndivyo ilivyokuwa, na lijulishalo hivyo ni maana iliyo kwenye usemi wake: “Si hilo mnaloliendea, bali ni wakeze Mtume.” hii inamaanisha kuwa Aya ilikuwa wazi kwa taabiina na wengineo kuwa iliteremka kwa ajili ya Ali, Fatima, Hasan na Husein (a.s.).

Kama ambavyo sisi hatuwezi kumkubali Ikrima kuwa hakimu wala shahidi katika jambo hili kutokana na lile ambalo limekwishajulikana kuhusu yeye, nalo ni uadui wake mkali dhidi ya Jemedari wa waumini (a.s.). Yeye ni miongoni mwa Makhawariju ambao walimpiga vita Ali, kwa hiyo ilikuwa juu yake aseme kuwa iliteremka kwa ajili ya wake za Nabii (s.a.w.w), kwa kuwa lau angekiri kuwa iliteremka kwa ajili ya Ali (a.s.) itakuwa amejitolea hukumu mwenyewe binafsi dhidi ya madhehebu yake na kutikisa misingi ya itikadi yake ambayo imemhalalishia yeye na wenzake kutoka kivita dhidi ya Ali (a.s.), na yasiyo hayo miongoni mwa mambo ambayo ni mashuhuri kwa Ikrima, kama vile kumsemea uwongo Ibnu Abbas mpaka Ibnu Al-Musayib alikuwa anamwambia huria wake aliyeitwa kwa jina la Burdu: “Usinisemee uwongo kama Ikrima alivyomsemea uwongo Ibn Abbas.”
Na katika Mizanul-Itidal ni kuwa Ibnu Umar alisema hilo pia kumwambia mhuria wake Naafiu.

Na Ali bin Abdullah bin Abbas alijaribu kumzuia Ikrima na kumtoa katika tatizo hilo, na miongoni mwa nyezo alizozitumia ni kumsimamisha chooni ili aache uwongo dhidi ya baba yake. Abdullah bin Abil Harth anasema: “Niliingia kwa Ibnu Abdullah bin Abbas na Ikrima akiwa amedhibitiwa kwenye mlango wa choo. Nikasema: Mwamtendea hivi huria wenu?” Akasema: ‘Kwa kweli huyu anamsemea uwongo baba yangu.’’11

Ama Muqatil, yeye si wa chini kwa uadui wake dhidi ya Amirul- Mu’minina (a.s.) na umashuhuri wake kwa uwongo ukimlinganisha na Ikrima, kiasi kwamba Nasaiy amemhesabu katika jumla ya waongo walio maarufu wa kuzua Hadithi.12 Na amesema Al-Jauzijaniy kama ilivyo katika wasifu wa Muqatil ndani ya Mizanud-Dhahab: “Muqatil alikuwa mwongo shupavu.”13

Muqatil alimwambia Al-Mahdiy Al-Abbasiy: “Ukipenda nitakuwekea Hadithi kumhusu Abbas.” Akasema: ‘’Sina haja nazo.’’14

Na watu kama hao haifai tuchukuwe maneno yao, hiyo ni aina ya ghururi na ujinga, kwa kuwa Hadithi zilizo sahihi zilizofululiza ziko kinyume na hivyo, kama ilivyotangulia. Na hii ni kuachia mbali zile riwaya zisemazo kuwa baada ya kushuka kwa Aya hii, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alidumu miezi tisa akienda mlangoni kwa Ali bin Abu Talib (a.s.) wakati wa kila Swala na anasema: ‘’Amani iwe juu yenu, rehema za Allah na baraka zake, enyi Ahlul-Bayt. Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba, na kukutakaseni kabisa.” Kila siku mara tano.15

Na katika Sahih Tirmidhiy, Musnad Ahmad, Musnad Tayalisiy, Mustadrakul-Hakim Alas-Swahihayni, Usudul-Ghaba, Tafsiru-Tabariy, Ibnu Kathir na Suyutiy:
“Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akipita mlangoni kwa Fatima muda wa miezi sita, kila atokapo kwa ajili ya Swala ya alfajiri, na husema: ‘Swala enyi Ahlul-Bayt. Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba, na kukutakaseni kabisa.”16

Na zisizo hizo miongoni mwa riwaya zinazoshabihiana ambazo zimekuja katika mlango huu. Na kwa mujibu huo imetuwia wazi kuwa Ahlul-Bayt wao ni Ali, Fatima, Hasan na Husein, wala hakuna nafasi kwa mpingaji mwenye vitimbi, kuwa na shaka katika hili, kwani kufanya hivyo ni kama kuwa na shaka juu ya uwepo wa jua katikati ya mchana.

 • 1. Swawaiq Uk. 143.
 • 2. Mustadrakul-Hakim, Juz. 3, Uk. 197 – 198.
 • 3. Mustadrakul-Hakim, Juz. 3, Uk. 197 – 198.
 • 4. Sahih Muslim, mlango wa fadhila za Ahlul-Bayt.
 • 5. Sunanul-Kubra, mlango wa kubainisha Ahlul-Bayt, na ambao ndio ahali zake. Tafsirut Tabariy Juz. 22, Uk. 5. Tafsir Ibni Kathiyr Juz. 3, Uk. 485. Tafsir Durul- Manthur Juz. 5, Uk.198 – 199. Sahih Tirmidhiy, mlango wa fadhila za Fatima. Na Musnad Ahmad Juz. 6, Uk. 292 – 323 na vingine.
 • 6. Ad - Durul-Manthur. Juz 5 Uk. 198.
 • 7. Mustadrakul-Haakim. Juz. 2. Uk. 416. Tafsir ya Aya toka Surat Ahzab.
 • 8. Musnad Ahmad. Juz.3, Uk. 292 – 323.
 • 9. Lisanul-Arab Juz. 9, Uk. 34.
 • 10. Durul-Manthur Juz.5, Uk.198.
 • 11. Wafayatul-Aayan Juz.1, Uk. 320.
 • 12. Dalailus-Swidq Jalada.2, Uk. 95.
 • 13. Kalimatul-Gharai cha Sharafud-Din Uk. 217.
 • 14. Al-Ghadiir Juz. 5, Uk. 266.
 • 15. Tafsiri ya Aya kutoka kwa Ibn Abbas ndani ya kitabu Durul-Manthur Juz. 5, Uk. 199.
 • 16. Mustadrak Swahihayni Juz. 3,Uk.158. Na amesema: Hadithi hii ni sahihi kwa mujibu wa sharti za Muslim, japo hajaiandika.