read

Mlango Wa Pili

Upotovu Umefichuka

Upotovu ulifichuka
Kwa kweli Hadithi mbili:

“Ni juu yenu kuishika Sunna yangu na Sunna ya makhalifa baada yangu. Shikamaneni nazo na ziumeni kwa magego.”

“Mimi ni mwenye kuacha kile ambacho endapo mtakishika hamtopotea: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu.”

Kwangu mimi zilikuwa ni dalili zenye nguvu mno ambazo nilikuwa nazitolea hoja nilipokuwa naelemea kwenye fikra ya kiwahabi. Na nilipohifadhi hadithi mbili ambazo wanazuoni wao wanazirudiarudia sana katika vitabu na mihadhara, wala siku moja nafsi yangu haikupata kunisemesha nifanye rejea kwenye chimbuko lake la asili katika vitabu vya hadithi. Na nilikuwa nazitendea kazi utendeaji kazi wa hadithi zilizokubalika na zilizo dhahiri. Na hiki sio kitu cha ajabu, kwani hizo kwa kweli ni msingi wa kwanza ambao juu yake fikra ya kisunni hujengeka, na hasa fikra ya kiwahabi ambayo hujengwa na hadithi mbili hizi kwa uthabiti.

Akilini mwangu hamkuwa na shaka ya kutosihi kwa hadithi hizo, kwa kuwa ni kituo ambacho natokea humo katika kujihusisha kwangu na madhehebu ya Sunni, kwani kuzishakia Hadithi mbili hizo maana yake ni kujishakia mwenyewe kuhusu ujihusishaji wangu na madhehebu hayo.

Na fikra hii ambayo kwayo nilihadaika nayo haikuwa baada ya kuhakiki, na wala haikuwa ni matokeo ya zama au matokeo ya fikra ya kisunni, bali ni matokeo ya mpango uliodurusiwa, ulipangwa toka zamani ili kuifunika haki na kuikabili safu ya Ahlul-Bayt, ambayo inawakilisha Uislam kwa sura zake zilizo nzuri mno, na yasikitisha sana kuwa madarasa nyingi za kifikra, zimesimama juu ya mpango ule mbaya, zikajengea fikra zake juu yake kana kwamba wenyewe umeteremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.), na wameueneza na kuuhami kwa njia na sababu zote.

Na uwahabi si kitu kingine ila ni mfano wa wazi wa kujitoa muhanga kwa mpango huo ambao umeutumbukiza umma wa kiislam kwenye bonde lenye kina kirefu la kugawanyika na kufarikiana na mtawanyiko.

Tutajaribu kufichua kiasi kidogo cha vitimbi vyake katika kila mlango miongoni mwa milango ya kitabu hiki. La muhimu kwetu kuhusiana na mpango huo katika uwanja huu ni Hadithi mbili ambazo zilikuwa ndio hatua ya kwanza ya kuipotosha dini na kubadilisha mwelekeo wa Risala hii (Risala ya Uislam), na kuwaweka waislamu mbali na Hadithi hii ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w):

“Kwa hakika mimi nimeacha katika ninyi ambacho endapo mtashikamana nacho hamtopotea baada yangu kamwe: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu.”

Hadithi hii ni mutawatir, ambayo imeelezwa na vitabu vya hadithi na rejea zake zimefikia idadi nyingi kwa Sunni na Shia, lakini mkono mdanganyifu na wenye khiyana ulifanya juhudi kuificha mbali na maono na badala yake uliitawanya Hadithi:
“Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu.” Na Hadithi: “Ni juu yenu kuishika suna yangu…” ambazo udhaifu uliomo ndani ya Hadithi hizo utafichuka punde tu.

Nilishtukizwa kwa mara ya kwanza niliposikia Hadithi: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu.” Hofu ilinishika, na nilitamani isingekuwa sahihi, kwa kuwa itabomoa kila nililokuwa nimejijengea katika fikra za kidini, bali itabomoa ngome ya madhehebu ya Sunni. Lakini pepo zimevuma kusiko elekea jahazi. Ilitokea kinyume kabisa nilipoziangalia Hadithi mbili hizi kwenye rejea zake za asili.

Nilikuta Hadithi: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu,” ina usahihi na uthibitisho kwa kiwango ambacho mtu yoyote hawezi kuwa na shaka nayo, kinyume na hadithi: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu.” ambayo si zaidi ya kuwa ni khabari ya a’ahadi marfuan au mursala ikiwa tupu na dhaifu, jambo ambalo lilifanya moyo wangu uvunjike.

Kutokea hapa ilikuwa ndio mwanzo wangu wa kufanya utafiti nilipohisi uchungu wa kushindwa, baada ya hapo muktadha na ishara zikaanza kujikusanya kwangu moja baada ya nyingine mpaka ukweli ulinifichukia kwa sura zake za wazi mno. Na tutathibitisha hapa udhaifu wa hadithi mbili: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu.” Na “Ni juu yenu kuishika suna yangu…” Na pia usahihi wa Hadithi ya kizazi ambayo ni risasi ya kwanza ambayo huusibu moyo wa fikra ya kisunni.

Hadithi: “Ni juu yenu kuishika suna yangu…” ni hadaa potovu:

“Ni juu yenu kuishika Sunna yangu na Sunna ya makhalifa waongofu wenye kuongoza baada yangu. Shikamaneni nazo na ziumeni kwa magego.”

Mtazamaji wa hadithi hii kwa mtazamo wa kwanza atadhani kuwa ndio hoja yenye kuvunja na ni dalili ya wazi ya wajibu wa kufuata madarasa ya makhalifa waongofu, nao ni: Abu Bakr Swidiq, Umar bin al-Khattab, Uthman bin Affan, na Ali bin Abi Talib.

Hatoweza kuichukulia maana nyingine mbali na maana hii, ila kama kutakuwa na aina fulani ya ta’aw- ili na moyo wa kasumba na kupenda mjadala. Kutokana na hali hiyo ndio zinapatikana nguvu za hadaa na werevu wa wapotoshaji, ndani ya hadithi hiyo wajikita usahihi wa madhehebu ya Ahlu Sunnah katika kuikabili madhehebu ya Shia. Kwa mujibu huo tunaweza kuifasiri hali ya kuibuka madrasa zinazoelekea kinyume na madhhebu ya Ahlul-Bayt, kwa sababu hayo madhehebu yamesimama juu ya msingi wa Hadithi hii na zilizo mfano wake.

Lakini kwa mtizamo wa kielimu na kwa juhudi kidogo ili kuchambua ukweli wa kihistoria, na yaliyofunikwa na hadithi hii na zilizo mfano wake, au kuangalia katika nyanja za elimu ya hadithi na fani za jarhu na taadiil1 utadhihiri na kufichuka upotovu wa hadithi hii na ubatili wake.

Ni ujinga kwa Sunni yoyote amtolee hoja Shia kwa hadithi hii, kwa sababu ni Sunni peke yao wanashikamana na hadithi hii, na haitowezekana kuwalazimisha Shia kwa hadithi ambayo hawaielezi ndani ya rejea zao wanazoziamini. Lakini kwa kuwa mimi ni mtafiti wa kisunni hapana budi niwe naanzia katika vitabu na vyanzo vya kisunni, ili iwe lazima kwangu kuzifuata. Na hii ni nukta ya mfumo wa kiutendaji na mazungumzo katika utafiti.

Hapana budi tuangalie katika hoja zetu na mazungumzo yetu kwa sababu hoja haiitwi hoja ila endapo hasimu anashikamana nayo, ili iwe hoja dhidi yake, na hili ndilo ambalo walio wengi katika wanachuoni wa kisunni hawana mwamko nalo, wanapotoa hoja dhidi ya Shia kwa Hadithi hii kuikabili hoja ya Shia, ile ya Hadithi: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu.”

Na tofauti kati ya hoja hizi mbili ni kubwa mno, nayo ni kwamba Hadithi ya ‘Suna yangu’ ni mahsusi kwa Sunni, kinyume na ‘Kizazi changu’ ambayo yakubalika na pande zote mbili.

Vyanzo Vya Hadithi

Ishkali ya kwanza ambayo huelekezwa kwa Hadithi hii: “Ni juu yenu kuishika Sunna yangu” ni kwamba yenyewe ni miongoni mwa Hadithi walizoziacha masheikh wawili – Bukhari na Muslim – wala hawakuitia katika sahihi zao, na hii yamaanisha Hadithi hii ina dosari haikufikia kiwango cha daraja ya Hadithi sahihi.

Hivyo ni kwa sababu Hadithi iliyo sahihi mno ni ile iliyoelezwa na masheikh wawili. Kisha ile aliyoieleza Bukhari peke yake, kisha ile aliyoieleza Muslim peke yake, kisha ile inayotimiza sharti za wawili hawa. Kisha iliyotimiza sharti za Bukhari, kisha iliyotimiza sharti za Muslim. Na sifa hizi teule hazipo katika hadithi hii. Hadithi hii ipo katika Sunan Abi Daud, Sunan Tirmidhiy na Sunan Ibn Majah.

Kwa kweli walioieleza Hadithi hii wote hawaepukani na udhaifu na kubezwa na wanazuoni wa Jar’hu wa Taadiil.2 Na mwenye kufuatilia wasifu wao ataliona hilo vyema kabisa.

Na sina nafasi katika haraka kama hii kuwadodosa waelezaji wa Hadithi hii mmoja baada ya mwingine, kwa njia zake mbalimbali, na kunakili rai za wanavyuoni wa Jar’hu wa Taadiil,3 hivyo nitakomea kuonyesha udhaifu wa mwelezaji mmoja au wawili toka katika kila rejea. Na hiyo inatosha kuidhoofisha riwaya hiyo, kama walivyokubaliana wanazuoni wa elimu ya Jar’hu wa Taadiil4 juu ya hilo, kwani pengine muelezaji huyu dhaifu amejitengenezea riwaya hii!

Riwaya Ya Tirmidhiy:

Tirmidhiy ameieleza Hadithi hii kutoka kwa: Baghyatu bin Al-Walid, na hizi hapa rai za wanavyuoni wa Jarhu wa Taadiilu kumhusu yeye: Ibnu al-Jawziy amesema kumhusu anapozungumzia Hadithi hiyo:

“Tulikwishataja kuwa Baghyatu alikuwa anaelezea Hadithi kutoka kwa wasiojulikana na waelezao Hadithi dhaifu, na pengine anaacha kuwataja wao na hata wale waliomuelezea kutoka kwao.”5

Na Ibn Haban amesema: “Haitolewi hoja kupitia Baghyatu.” Na akasema: “Baghyatu ni mwenye kufanya hadaa katika Hadithi. Anaelezea Hadithi kutoka kwa waeleza Hadithi walio dhaifu, na swahiba zake hawazisawazishi hadithi zake na wanawaondoa walio dhaifu miongoni mwao.”6

Na Abu Is’haaq al-Jawzijaniy amesema: “Mwenyezi Mungu amrehemu Baghyatu, alikuwa hajali aukutapo uzushi kwa ambaye kwake anazichukua Hadithi.”7

Na yasiyo hayo miongoni mwa maneno ya wanahadithi na wanazuoni wa Jarhu wa Taadiilu. Tuliyotaja yanatosha katika mahali hapa.

Sanad Ya Hadithi Kwa Mujibu Wa Abu Daud:

Al-Walid bin Muslim: Ameeleza habari kutoka kwa Thaur An-Naswibiy kulingana na usemi wa Ibn Hajar al-Asqalaniy: “Babu yake aliuawa siku aliochomwa mshale pamoja na Muawiyah, kwa hiyo Thaur alikuwa amtajapo Ali (a.s.) husema:

“Simpendi mtu aliyemuua babu yangu.”8

Ama kumhusu al-Walid, Dhahabi amesema: “Abu Mas’har amesema: al’Walid ni mwenye kufanya hadaa katika Hadithi, na huwenda akahadaa kwa kunukuu toka kwa waongo.”9

Na Abdullahi bin Ahmad bin Hanbal amesema: “Baba yangu aliulizwa kuhusu yeye akasema: ‘Alikuwa mtu anayeirusha Hadithi kwa Mtume bila ya kutaja nyororo ya wapokezi.”’10

Na mengine yasio hayo, na hiyo yatosha kuidhoofisha riwaya yake.

Sanad Ya Hadithi Kwa Mujibu Wa Ibnu Majah:

Imeelezwa kwa njia tatu:

Katika njia ya Hadithi ya kwanza yumo Abdullahi bin Ala’u. Dhahabi amesema kumhusu: “Ibnu Hazmi amesema: ‘Yahya na mwingine wamemdhoofisha’11 Naye ameieleza habari kutoka kwa Yahya naye ni mtu asiyejulikana kwa mujibu wa Ibnu Qattan.12

Ama katika njia ya pili yumo Ismail bin Bashir bin Mansur, alikuwa Qadiriya kama ilivyo katika Tahdhibut-Tahdhib.13

Ama katika njia ya tatu kwa mujibu wa Ibn Majah: Habari amezieleza Abdul Malik bin Swabbahin kutoka kwa Thaur An-Naswibiy, na ilivyo katika Mizanil-Iitidali ni kuwa: “Ni mtuhumiwa wa wizi wa Hadithi.”14

Achilia mbali kuwa Hadithi hii ni habari ya mpokezi mmoja, riwaya zake zote zarejea kwa Swahaba mmoja naye ni Urbadh bin Saariyah. Na habari ya mpokezi mmoja haithibitishi kitu katika kutoa hoja, zaidi ya hapo ni kuwa Urbadh alikuwa miongoni mwa wafuasi wa Muawiyah na ni askari wake.

 • 1. Jarhu na Taadiil humaanisha hali za wapokezi wa hadithi, yaani kukubaliwa na kutokukubaliwa kwao.
 • 2. Jarhu na Taadiil humaanisha hali za wapokezi wa hadithi, yaani kukubaliwa na kutokukubaliwa kwao.
 • 3. Jarhu na Taadiil humaanisha hali za wapokezi wa hadithi, yaani kukubaliwa na kutokukubaliwa kwao.
 • 4. Jarhu na Taadiil humaanisha hali za wapokezi wa hadithi, yaani kukubaliwa na kutokukubaliwa kwao.
 • 5. Maudhuatu ibn Jauziy; Jalada 1, Uk.109.
 • 6. Maudhuatu ibn Jauziy; Jalada 1, Uk. 151
 • 7. Khulaswatu Abakatul’anwar J. 2, Uk. 350.
 • 8. Khulaswatu Abakatul’anwar J. 2, Uk. 344.
 • 9. Mizanul’I’itidal Juz.2. Uk. 347.
 • 10. Tahdhiibut-Tahdhiib Juz. 4 Uk. 154
 • 11. Mizanul’I’itidal, Juz. 2, Uk. 343.
 • 12. Tahdhibut-Tahdhib, Jalada 11, Uk. 280.
 • 13. Tahdhibut-Tahdhibu, Jalada 1, Uk. 284.
 • 14. Mizanul’I’itidal, Juz. 2, Uk. 656.