read

Mlango Wa Tatu

Hadithi: “Kitabu Cha Mwenyezi Mungu Na Kizazi Changu” Katika Rejea Za Kisunni

Kuthibitisha hadithi: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu”:

Imekuwia wazi katika uchambuzi uliotangulia, ule udhaifu wa hadithi ya kushikamana na Sunna, ambayo yazingatiwa kuwa ni nguzo ya msingi ya kusimama jengo la Usunni, na kutikisika kwa msingi huu latikisika jengo lote la Usunni.

Na hii ndio tafsiri ya ile pupa ya wanachuoni wao ya kuificha riwaya ya: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu,” kiasi kwamba imefunika mawazo ya watu walio wengi kufikia daraja mimi niitajapo Hadiithi ya kizazi kwenye kikundi chochote kile, hali ya kuduwaa hujichora kwenye nyuso zao.

Kwa ajili hiyo ili hoja itimie nilipenda kuthibitisha ‘Hadithi ya kizazi’ katika mlango huu kutoka katika vitabu vya Ahlu Sunna, kwa njia zake zote, na ufuatao ni ufafanuzi wake:

Kwanza: Sanad Ya Hadith:

Idadi ya wapokezi katika maswahaba:

Kwa kweli Hadithi hii imekuja mfululizo (mutawatir) kutoka kundi la maswahaba, na yafuatayo ni baadhi ya majina yao:

1. Zayd bin Arqam
2. Abu Said al Khudry
3. Jabir bin Abdullah
4. Hudhayfa bin Asid
5. Khuzaymah bin Thabit
6. Zayd bin Thabit
7. Suhayl bin Saad
8. Dhumiratul al-Asadiy
9. Amiru bin Abi Layla (al-Ghafariy)
10 Abdur Rahman bin Aufi
11. Abdullah bin Abbas
12. Abdullah bin Umar
13. Uddiy bin Hatim
14. Uqba bin Amir
15. Ali bin Abi Talib
16. Abu Dharr alGhafariy
17. Abu Raafi’i
18. Abu Shariih al-Khuzaiy
19. Abu Qudama al Ansariy
20. Abu Huraira
21. Abul Haythami bin Tihani
22. Umu Salmah
23. Umu Hani’i bint Abi Talib
24. Warjalu min Quraysh

Idadi Ya Wapokezi Katika Tabiina:

Na kunakili huku kumekuwa mfululizo pia katika zama za Tabiina na wafuatao ni baadhi ya walionakili hadithi: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu”:

1. Abu Tufail Aamir bin Wathilah
2. Atyatu bin Said al Aufiy
3. Hunshu bin Al-Muutamar
4. Al-Harithu Al-Hamdaniy
5. Hubaybu bin Abi Thabit
6. Ali bin Rabiiah
7. Al-Qasim bin Hasan
8. Huswinu bin Sibra
9. Amru bin Muslim
10. Abu Dhwahiy Muslim bin Swabiih
11. Yahya bin Juudah
12. Al-Asbagh bin Nabata
13. Abdullah bin Abi Rafi’i
14. Al-Muttalib bin Abdillah bin Hantab
15. Abdur Rahman bin Abi Said
16. Umar bin Ali bin Abu Talib
17. Fatumah bint Ali bin Abu Talib
18. Al-Hasan bin Al-Hasan bin Ali bin Abi Talib
19. Zaynul-Abidiin Ali bin Al-Husein..... na wengineo

Idadi Ya Wapokezi Katika Karne Kadhaa:

Ama kuhusu walioieleza baada ya Swahaba na Tabiina miongoni mwa walio mashuhuri katika umma huu, na mahafidhu wa Hadithi na walio mashuhuri miongoni mwa maimamu, karne na karne ni kundi kubwa, nafasi haituruhusu kutaja majina yao na riwaya zao. Na baadhi ya watafiti na wanavyuoni wameorodhesha idadi yao, hivyo ukitaka kupata ufafanuzi zaidi rejea kitabu Abaqatul-An’war, juzuu ya kwanza na ya pili.

Natosheka na kutaja idadi yao katika kila tabaka la wakati fulani, kutokea karne ya pili mpaka karne ya kumi na nne:
• Karne ya pili: Idadi ya wapokezi ni 36

• Karne ya tatu: Idadi ya wapokezi ni 69

• Karne ya tatu: Idadi ya wapokezi ni 69

• Karne ya nne: Idadi ya wapokezi ni 38

• Karne ya tano: Idadi ya wapokezi ni 21

• Karne ya sita: Idadi ya wapokezi ni 27

• Karne ya saba: Idadi ya wapokezi ni 21

• Karne ya nane: Idadi ya wapokezi ni 24

• Karne ya tisa: Idadi ya wapokezi ni 13

• Karne ya kumi: Idadi ya wapokezi ni 20

• Karne ya kumi na moja: Idadi ya wapokezi ni 11

• Karne ya kumi na mbili: Idadi ya wapokezi ni 18

• Karne ya kumi na moja: Idadi ya wapokezi ni 11

• Karne ya kumi nambili: Idadi ya wapokezi ni 18

• Karne ya kumi na tatu: Idadi ya wapokezi ni 12

• Karne ya kumi na nne: Idadi ya wapokezi ni 13

Kwa hiyo inakuwa jumla ya wapokezi wa hadithi katika karne ya tatu mpaka karne ya kumi na nne ni 323.

Hadithi ya ‘Kitabu na Kizazi’ ndani ya vitabu vya Hadithi:

Ama kuhusu vitabu vilivyoeleza Hadithi hii ni vingi, tunataja miongoni mwavyo:

Sahih Muslim: Juz. 4 Uk. 123, chapa ya Darul-Maarif, Beirut, Lebanon. Muslim ameeleza ndani ya Sahih yake kuwa: “Ametusimulia Muhammad bin Bakar bin al-Tiryan:

Ametusimulia Hasan (yaani Ibnu Ibrahim), kutoka kwa Said (na yeye ni Ibnu Masruq), kutoka kwa Yazid bin Hayyan, kutoka kwa Zayd bin Arqam. Alisema: Tuliingia kwake na tulimwambia: ‘Kwa kweli umeyaona mengi na ulikwa swahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na uliswali nyuma yake.

Ewe Zayd kwa kweli umekutana na mengi mengi. Tusimulie ewe Zayd uliyoyasikia kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).’

“Alisema: ‘Ewe mwana wa ndugu yangu! Wallahi umri wangu umekuwa mkubwa na ahadi yangu imewadia na nimesahau baadhi niliyokuwa nayaelewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), hivyo basi nitakayowasimulia yakubalini na ambayo nitashindwa msinikalifishe nayo.’

“Halafu akasema: ‘Alisimama Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kati yetu akitoa hotuba mahali kwenye maji paitwapo Khum, kati ya Makka na Madina, alimhimidi Allah (s.w.t.) na kumsifu, aliwaidhi na kukumbusha hatimaye akasema: ‘Ama baad, enyi watu! Kwa kweli mimi ni mtu yakaribia mjumbe wa Mola wangu akaja na nitamjibu.

Na mimi nimeacha kwenu vizito viwili, cha kwanza ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mwenye enzi na utukufu, nayo ni kamba ya Mwenyezi Mungu mwenye kuifuata atakuwa katika uongofu na mwenye kuiacha atakuwa katika upotovu.’

Hatimaye akasema: ‘Na Ahlul-Bayt wangu, ninakukumbusheni Mwenyezi Mungu kuwahusu Ahlul-Bayt wangu. Nakukumbusheni Mwenyezi Mungu kuwahusu Ahlul-Bayt wangu. Nakukumbusheni Mwenyezi Mungu kuwahusu Ahlul-Bayt wangu.’’
“Tuliuliza: Ahlul-Bayt wake ni wakeze? Akasema: ‘Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwa kweli mwanamke huwa pamoja na mwanaume muda katika zama, kisha humtaliki naye hurejea kwa baba yake na watu wa kaumu yake. Ahlul-Bayt wake ni asili yake na nasaba yake. wale walioharamishi- wa swadaka baada yake.”’

Pia Muslim ameieleza kutoka kwa Zahir bin Harbi na Shujai bin Mukhalid, wote kutoka kwa Ibnu Ulyata. Zahiru akasema: “Ametusimulia Isma’ili bin Ibrahim: Amenisimulia Abu Hayyan: Amenisimulia Yazid bin Hayyan akasema: Alisema: Nilitoka…..” Hatimaye aliieleza Hadithi.

Na Muslim aliieleza kutoka kwa Abu Bakr bin Abi Shayba: Ametusimulia Muhammad bin Fudhwail na alitusimulia Is’haqa bin Ibrahim: Ametupa habari Jarir wote wawili kutoka kwa Abu Hayyan kuwa….....Kisha akaitaja Hadithi.

Na riwaya zote za Muslim zarejea kwa Abu Hayyan bin Said Tamimiy, na Dhahabi alikwishasema kumuhusu: “Yahya bin Said bin Hayyan Abu Hayyan Tamimiy. Thauriy alikuwa anamtukuza na kusema kuwa yu mwaminifu. Ahmad bin Abdullahi Al-Ujaliy amesema: Ni mwaminifu, mwema, mwenye kujitokeza mshika Sunna.”1

Na Dhahabi pia amesema katika Al-Ibar, Juz.1, Uk. 205: “Na humo mna Yahya bin Said Tamimiy, ni huria wa Taymu Rubab al-Kufiy, na alikuwa mwaminifu imam mshika Sunna. Shaabiy na aliye mfano wake wameeleza hadithi kutoka kwake.”

Na Al-Yafii amesema: “Ndani yake kuna Yahya bin Said Tamimiy Al- Kufiy, alikuwa mwaminifu na imam mshika Sunna.”2

Na Asqalaniy amesema: “Abu Hayyan Tamimiy Al-Kufiy ni mwaminifu mchapa ibada….amekufa mwaka wa arobaini na tano.”3

Na wengine miongoni mwa wanavyuoni wa jarhu na taadiil. Kama ambavyo ni wazi kuwa Hadithi ikiwa imeelezwa katika Sahih Muslim ni mwamuzi tosha wa kusihi kwake, kwa ijmai ya waislam (masunni) inayozizingatia riwaya zake zote kuwa ni sahihi.

Na Muslim mwenyewe amebainisha kuwa zote zilizomo katika Sahihi yake kuna ijmai ya kusihi kwake, achia mbali ule usahihi wake kwa mtizamo wake (Muslim), kama alivyosema Al-Hafidh Suyutiy: “Muslim amesema: ‘Sio kila kitu sahihi kwa mtizamo wangu tu ndio nimeweka humu, bali nimeweka humu kile kilichokuwa na ijmai ya usahihi wake.”’ Kama ilivyo katika Tadribur-Rawiy.

Na amesema Nawawiy katika kitabu wasifu wa Muslim: “Muslim ametunga vitabu vingi katika elimu ya hadiith, miongoni mwavyo ni kitabu hiki Sahih Muslim ambacho Mwenyezi Mungu Mtukufu kwacho amewafanyia hisani waislam, na imfike yeye shukrani, neema, fadhila na ihsani.”4

Na wengine…nafasi haitoshi kutoa maelezo yao, na kwa sababu ya uwazi wa madai haya.
Al-Mustadrak: Riwaya ya hadithi kwa Imam Al-Hafidh Abu Abdillahi Al- Haakim Nisaburiy katika Mustadrak yake ya Bukhari na Muslim, Jalada 3, Uk. 27, kitabu maarifatus-Swahaba, chapa ya Darul-Maarifa, Beirut – Lebanon.
Abu Awanati ameieleza Hadith kutoka kwa Aamash: Ametusimulia Habib bin Abi Thabit kutoka kwa Abi Tufaili kutoka kwa Zaydu bin Arqam, ame- sema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alipokuwa anarudi kutoka Hijja ya kuaga, na alisimama Ghadir Khum, alitoa amri ya kutengenezwa minbari ya dharura kwa seti za wanyama, nazo zilisimamishwa, akasema: ‘Kana kwamba nimekwishaitwa na nimeitika.

Kwa hakika mimi ni mwenye kuwaachieni vizito viwili, kimoja ni kikubwa zaidi kuliko kingine, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu, basi angalieni jinsi mtakavyonifuata kuhusu viwili hivi, kwa kuwa hivyo havitotengana mpaka vitakaponijia kwenye hodhi.’

Hatimaye akasema: ‘Kwa hakika Allah mwenye nguvu na utukufu ni walii wangu na mimi ni walii wa kila muumini.’ Kisha akaushika mkono wa Ali na akasema: ‘Ambaye mimi ni walii wake basi huyu ni walii wake.’ Kwa hiyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) anasisitiza kuwa wa kwanza na ni mkuu katika Ahlul- Bayt wake ambaye amewajibisha afuatwe ni Ali (a.s.).”

Kama alivyoeleza pia kutoka kwa Hisan bin Ibrahim Al-Kirmaniy. Ametusimulia Muhammad bin Salma bin Kahiil kutoka kwa baba yake kutoka kwa Abu Tufail kutoka kwa Ibnu Wathilah kuwa yeye alimsikia Zayd bin Arqam akisema…

Aliisimulia hadithi kwa mfano uliopita isipokuwa yeye amezidisha: “Mnajua kuwa mimi ni bora kwa waumini kuliko nafsi zao?” mara tatu. Wakasema: “Ndio.” Akasema: “Ambaye mimi ni walii wake Ali ni walii wake.”

Pia Al-Hakim ameieleza kwa njia mbili zingine, lakini kwa ajili ya kuchunga kutorefusha tumetosheka kwa kuzithibitisha njia mbili.

Na ambalo lajulisha usahihi wa Hadithi hii na kuwa ni katika hadithi mutawatir ni kwa sababu Al-Hakim ameieleza na ameihukumu kuwa ni sahihi kwa sharti ya Bukhari na Muslim.

Musnad Ahmad: Riwaya ya Hadithi kwa mujibu wa Ahmad bin Hanbal: Juz. 3, Uk.17 – 26- 14- 59 – chapa ya Daru Swadir Beirut, Lebanon.

“Ametusimulia Abdullahi: Amenisimulia baba yangu: Ametusimulia Abu Nadhar: Ametusimulia Muhammad, yaani Ibnu Abu Talha, kutoka kwa Al- Aamash kutoka kwa Atiyyah Al-Aufiy, kutoka kwa Abu Said Al-Khudriy, kutoka kwa Nabii (s.a.w.w) amesema:

‘Kwa hakika mimi imekaribia nitaitwa na nitaitika na mimi ni mwenye kuacha kwenu vizito viwili: Kitabu cha Mwenyezi Mungu, ni kamba iliyovutwa toka mbinguni mpaka ardhini, na kizazi changu Ahlul-Bayt wangu, kwa hakika Mwenyezi Mungu ambaye ni Latifu mwenye habari amenipa habari kuwa wao hawatotengana hadi waje kwangu bwawani, hivyo basi angaliyeni jinsi mtakavyonifuata katika viwili hivi!”’

Pia ameeleza: “Ametusimulia Abdullah: Baba yangu alinisimulia: Ametusimulia Ibnu Numayri: Ametusimulia Abdul Malik, yaani Ibnu Abu Sulayman kutoka kwa Atiyyah, kutoka kwa Abu Said Al-Khudriy, akasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) amesema: ‘Kwa hakika mimi nimeacha katika ninyi vizito viwili kimoja ni kikubwa zaidi kuliko kingine, Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mwenye enzi na utukufu, ni kamba iliyovutwa kutoka mbinguni hadi ardhini. Na kizazi changu Ahlul-Bayt wangu, kwa kweli hawatofarikiana hadi watanijia kwenye bwawa.”’

Na ameieleza kwa njia nyingi ambazo sio hizi zilizotangulia.
Sahih Tirmidhiy: Riwaya ya Hadithi kwa mujibu wa Tirmidhiy Juz. 5 Uk. 663 – 662 – chapa ya Daru Ihyau Turathul Arabiy.

“Na ametusimulia Ali bin al-Mundhir al-Kuufiy: Ametusimulia Muhammad bin Fudhwaili, amesema: Ametusimulia al-Aamash kutoka kwa Atiyyah na Abu Said, na pia al-Aamash amesimulia kutoka kwa Habib bin Abu Thabit kutoka kwa Zayd bin Arqam, wamesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w): ‘Kwa hakika mimi nimeacha katika ninyi vizito viwili, kimoja ni kizito zaidi kuliko kingine, Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kamba iliyovutwa kutoka mbinguni hadi ardhini. Na kizazi changu Ahlul-Bayt wangu, kwa kweli havitofarikiana hadi vitakaponijia kwenye bwawa, basi angalieni ni jinsi gani mtakavyobaki navyo baada yangu.”’

Ametusimulia Nasru bin Abdur Rahman al-Kuufiy: Ametusimulia Zayd bin al-Hasan, naye ni al-Anmaatiy kutoka kwa Jafar bin Muhammad kutoka kwa baba yake kutoka kwa Jabir bin Abdillahi akasema: “Nilimwona Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) katika Hijja yake siku ya Arafa akiwa juu ya ngamia wake akihutubu, hivyo nilimsikia akisema:

‘Oh ninyi watu!! Kwa hakika mimi nimeacha katika ninyi ambacho lau mtashikamana nacho hamtapotea: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu Ahlul-Bayt wangu.”’

Kanzul-Ummal: Kama alivyoiandika Hadithi hii al-Allama Alaudin Ali al- Mutaqiy bin Hasamud-Din al-Hindiy, aliyefariki mwaka 975 katika kitabu Kanzul-Ummal Fii Sunanil-Aq’wali Wal-Af ’ali, Jalada ya kwanza, mlango wa pili – Katika kichwa cha habari kinachozungumzia: Kushikamana na Kitabu na Sunna – Uk. 172. chapa ya Muasasatu risala – Beirut, chapa ya 5, Mwaka 1985 – nayo ni hadithi namba 810 na 871 na 872 na 873.

Lau tukifuatilia katika mlango huu hali tukitaka kuvileta vitabu ambavyo vimeielezea Hadithi hii, nafasi ingekuwa ndefu na kingehitajika kitabu cha peke yake. Na hapa tutawataja baadhi ya wanahadithi na wanachuoni ambao walioiandika Hadithi hii, ni mfano tu sio kuwataja wote. Na kwa maelezo zaidi rejea kitabu: Ihqaqul-Hhaqi cha Asadullahi Tastariy, Juz. 9, Uk. 311.

Na miongoni mwa ulamaa na wanahadithi hao ni:

Hafidh Tabraniy aliyefariki mwaka 340. Angalia katika kitabu Muujamus- Swaghiir.
Allamah Muhibbu Din Tabariy. Angalia katika kitabu Dhakhairul-Uqba.
Allamah Sheikh Ibrahim bin Muhammad bin Abi Bakr al-Hamuweyniy.
Angalia katika kitabu Faraidus-Samtain.
Miongoni mwao ni Ibnu Saad. Angalia katika kitabu Tabaqatul-Kubra.
Hafidh Nuru-Din al-Haythamiy. Angalia katika kitabu Majmauz-Zawaidi.
Hafidh Suyutiy. Angalia katika kitabu Ihyaul-Mayit.
Hafidh Asqalaniy. Angalia katika kitabu al-mawahibu alladuniyyah.
Allamah Nabhaniy. Angalia katika kitabu Anuwaru Muhammadiyah.
Allamah Daramiy. Angalia katika Sunan yake.
Hafidh Abu Bakr Ahmad bin al-Husein bin Ali al-Bayhakiy. Angalia katika kitabu Sunanul-Kubra.
Allamah al-Baghawiy. Angalia katika kitabu Maswabiihus-Sunnah.
Hafidh Abul Fidai bin Kathiyr al-Damishqiy. Angalia katika kitabu Tafsirul-Qur’ani.
Ibnu Athir. Angalia katika kitabu Jaamiul-Usuul.
Al Muhadithu al-Shahir Ahmad bin Hajar al-Haythamiy al-Makkiy, aliyefariki mwaka 914 A.H. Angalia katika kitabu Swawaiqul-Muhriqah Fii Radi Ala Ahlil-Bidai Wa Zindiqah, chapa ya pili mwaka 1965, chapa ya Maktabatul Qahirah – Shirkatu Taba’a Al-Faniyyah ASl-Mutahidah.
Na baada ya kuileta Hadithi ya Vizito Viwili akasema: “Halafu jua kuwa Hadithi ya kushikamana ina njia nyingi, imeletwa na maswahaba ishirini na kitu, na ina njia za utata kumi na moja zilizotatuliwa, na katika baadhi ya njia hizo ni kuwa aliitamka hiyo akiwa Arafa katika hija ya kuaga. Na katika nyingine ni kuwa aliitamka hiyo katika Ghadir khum. Na katika nyingine ni kuwa yeye alisema hayo alipokuwa amesimama akitoa hotuba mara tu alipotoka Taifu kama ilivyotangulia. Habari hizo hazipingani kwa kuwa yawezekana kuwa yeye (s.a.w.w) alikariri usemi huo kwao katika sehemu hizo na zingine, kwa sababu ya umuhimu wa suala la Kitabu na Kizazi kitakatifu.

“Na katika riwaya kutoka kwa Tabaraniy kutoka kwa Ibnu Umar ni kuwa, la mwisho alilosema Nabii (s.a.w.w) ni: “Nifuateni katika Ahlul-Bayt wangu.” Na katika nyingine kutoka kwa Tabaraniy na Abu Sheikh ni: “Allah Mtukuka ana heshima tatu mwenye kuzihifadhi Mwenyezi Mungu ataihifadhi dini yake na dunia yake, na asiyezihifadhi Mwenyezi Mungu hatoihifadhi dini yake wala akhera yake.” Nikauliza ni nini hizo? Akasema: “Heshima ya uislamu, heshima yangu na heshima ya kizazi changu.”

“Na katika riwaya ya Bukhari kutoka kwa al-Swadiqu kuhusu kauli yake: ‘Enyi watu!! Hivi Muhammad anawapenda watu wa nyumba yake!!?’ yaani muhifadhini kupitia wao, musiwaudhi.

“Na Ibnu Saad na al-Malau katika kitabu chake cha Syra amesema kuwa: “Yeye (s.a.w.w) akasema: ‘Nausia kheri kwa Ahlul-Bayt wangu, kwa hakika mimi nitakuwa hasimu wenu kwa niaba yao kesho, na ambaye nitakuwa hasimu wake nitamgomba na nitakayegombana naye ataingia motoni.”’

“Na kuwa yeye alisema: “Mwenye kunihifadhi mimi katika Ahlul-Bayti wangu amechukua ahadi kwa Mwenyezi Mungu.”

“Na ameandika pia: “Mimi na Ahlul-Bayt wangu ni mti upo ndani ya Jannah na matawi yake yapo duniani, mwenye kutaka na aichukue njia kuelekea kwa Mola wake.”

“Pili ni Hadithi: “Katika kila wanaorithishwa katika umma wangu kuna waadilifu miongoni mwa Ahlul-Bayt wangu, wananiondolea dini hii upotoshaji wa wapotevu na madai ya wabatilifu na tafsiri ya majahili. Tambueni kwa hakika Maimamu wenu ni msafara wenu uelekeao kwa Allah Mtukuka, hivyo basi angalieni mtakayefuatana naye.”

Halafu akasema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) aliiita Qur’ani na watu wa famili yake kuwa ni ‘Vizito Viwili’, nao ni utukuzo wa hali ya juu wa ahali na kizazi na jamaa wa ukoo wa karibu. Kwa kuwa kizito ni kila kilicho na thamani na hatari chenye kuhifadhiwa, na hawa wawili ni hivyo hivyo – Qur’ani na Ahlul-Bayt – kwa kuwa kila kimoja chao ni mahali pa elimu ya dini, siri na hekima ya juu na hukumu za kisheria. Kwa minajili hiyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alihimiza kuwafuata na kushikamana nao na kujielimisha kwao wao na amesema: ‘Alhamdu lillahi ambaye amejaalia hekima katika sisi Ahlul-Bayt.’

“Na kuna kauli isemayo: Wameitwa Vizito Viwili kwa sababu ya uzito wa wajibu wa kuchunga haki zao. Halafu ambao himizo limetuka juu yao ni wenye kukitambua Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake, kwa kuwa wao ndio ambao hawatofarikiana na Kitabu mpaka walifike bwawani. Na wanaungwa mkono na habari iliyotangulia, nayo ni “Wala msiwaelimishe kwa kuwa wao wana elimu zaidi yenu.” Kwa hilo wamepambanuka mbali na wanavyuoni wengine, hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwaondolea uchafu wa kimatendo na kiitikadi na kuwatoharisha safi…”

Ewe Ibnu Hajar je umechunga haya yote na kumhifadhi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) katika Ahlul-Bayt wake na umewafanya mawalii wako na kuchukua dini kwao tu?! Au mwasema kwa midomo yenu ambayo hayapo myoyoni mwenu “Chuki imekuwa kubwa kwa Mwenyezi Mungu mseme ambayo hamyatendi.”

Imam Swadiq (a.s.) amesema kweli aliposema: “Wanajigamba kutupenda hali wanatuasi.” Hivyo Ibnu Hajar na walio mfano wake wanajigamba kuwapenda Ahlul-Bayt hali wanawafanya mawalii na kuichukuwa dini yao kutoka kwa waliowadhulumu Ahlul-Bayt. Huyu Ibnu Hajar mwenyewe anapothibitisha fadhila za Ahlul-Bayt na anatambua ulazima wa kushikamana nao, bado hapo hapo anafanya shambulizi lake dhidi ya Shia katika Swawaiqu yake na kuwaweka safu moja na vikundi vipotovu, na anawamwagia tuhuma mbaya na matusi machafu mno.

Ewe Ibnu Hajar nini dhambi yao?! Je ni kwa sababu wao wamewapenda Ahlul-bayt na kushikamana nao kwa kuchukua dini kwao?!

  • 1. Tahdhibut-Tahdhib Juz. 2, Uk.348.
  • 2. Mir’atul-Janan Jalada.1, Uk. 301.
  • 3. Taqriibut-Tahdhiib Juz. 2, Uk. 348.
  • 4. Tahdhibul-Asmai Wal-Lughati Juz. 2, Uk.91.